Skip to content

Habari

Habari
Hifadhi

Risala na Barua

Matini
Hifadhi

Kumbukumbu na Simulizi

Kabla ya Mapinduzi
Baada ya Mapinduzi

Sauti na Taswira

Picha
Sauti
Video
Tahadhari za hivi karibuni za Walii Amr wa Waislamu kwa Viongozi wa Nchi za Kiarabu Chapa
18/05/2011

Sambamba na kuongezeka wimbi la mwamko wa wananchi wa mataifa ya eneo, Mtandao wa Intaneti wa Ayatullah Udhma Khamenei umeanzisha ukurasa maalumu ulioupa jina la "Mwamko wa Kiislamu" tangu tarehe Mosi Mei, 2011, kwa ajili ya kuakisi mitazamo mbali mbali ya Walii Amri wa Waislamu kuhusu mwamko huo. Hapa chini tunakuleteeni baadhi ya maonyo na tahadhari zilizowahi kutolewa na Walii Amr wa Waislamu Ayatullah Udhma Khamenei kwa viongozi na tawala za nchi za Kiarabu katika miaka ya hivi karibuni.

***

Pateni funzo kutokana na yaliyomfika Saddam Husain
Ulimwengu wa siasa za kimataifa ni ulimwengu usio na taqwa. Kukosekana taqwa katika ulimwengu huo kumepelekea mabeberu wa dunia kuwasaliti hata marafiki zao. Mumeyaona yaliyomfika Saddam? Walimsaidia na kumtia nguvu Saddam pale walipokuwa na haja naye. Katika kipindi cha vita tulivyolazimishwa kupigana, hawa hawa Wamarekani walimsaidia na kumuunga mkono Saddam Husain kwa uwezo wao wote. Walimsaidia kuanzia kwenye mipango na mbinu za angani na taarifa za kijasusi hadi kwa silaha, wakimtia nguvu, wakimuunga mkono kwa kila hali na walifikia hadi kuwachochea vibaraka wao wamsaidie kwa fedha na kwa kila njia kwani walikuwa wana haja naye. Walidhani kwamba kwa kumsaidia Saddam wataweza kutia doa katika sura madhubuti na iliyo na azma thabiti ya taifa la Iran. Lakini walipokata tamaa kwa kuona hawawezi kufikia malengo yao, na wakati walipoona Saddam hana faida tena kwao, wamemfanyia ya kumfanyia kama mlivyoshuhudia wenyewe na waliamua kutumia mbinu nyingine za kufanikishia malengo yao. Jambo hili kwa kweli ni funzo kwa watu ambao wanadhani madola ya kibeberu yanaweza kuwasaidia na kuwalinda.
Sehemu ya hotuba aliyoitoa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika sherehe za pamoja za kijeshi za vikosi vya ulinzi vya mkoa wa Fars 01/05/2008.

Mtakwenda kumwambia nini Mtume wa Mwenyezi Mungu?
Msiba wa tukio hili la kutisha ni mkubwa mno kwa Waislamu bali kwa kila mtu mwenye hisia za kibinaadamu na heshima kote ulimwenguni, lakini msiba mkubwa zaidi ni kimya kinachoonyesha kuridhika na kufurahishwa na tukio hilo kinachooneshwa na baadhi ya tawala za nchi za Kiarabu zinazodai ni za Waislamu. Kuna msiba mkubwa kiasi gani kupita huu wa kuona tawala za Waislamu badala ya kuwasaidia wananchi madhulumu wa ghaza kutokana na jinai wanazofanyiwa na utawala ghasibu, kafiri na adui wa Kizayuni, ndio kwanza tawala hizo zinawarahisishia kazi viongozi watenda jinai wa utawala wa Kizayuni kiasi kwamba watenda jinai hao wanasema kwa jeuri kwamba viongozi wa tawala hizo wanashirikiana nao na wanaafiki maafa makubwa wanayofanyiwa wananchi madhlumu wa Ghaza.
Viongozi wa nchi hizi za Kiarabu watakwenda kumwambia nini Mtume wa Mwenyezi Mungu? Watawaambia nini wananchi wao ambao bila ya shaka yoyote wanaomboleza maafa haya? Kwa hakika leo hii nyoyo za wananchi wa Misri, Jordan na nchi nyinginezo za Kiislamu zinachirizika damu kutokana na mauaji haya wanayofanyiwa wananchi wa Ghaza tena baada ya kuzingirwa kwa muda mrefu wakinyimwa hata chakula na madawa.
Sehemu ya ujumbe wa Kiongozi Muadhamu alioutoa tarehe 8/10/87 kulalamikia mauaji waliyokuwa wanafanyiwa wakati huo wananchi madhlumu wa Ghaza na utawala wa Kizayuni wa Israel katika mashambulizi ya kikatili ya siku 22 yaliyofanywa na wanajeshi katili wa Israel huko Ghaza.

Hatima ya watenda jinai wa nchi za Kiarabu
Watenda jinai wa nchi za Kiarabu wajue kuwa hatima yao haitatofautiana na ile iliyowakumba Mayahudi katika Vita vya Ahzab ambapo Mwenyezi Mungu amesema kuhusu vita hivyo kwamba:

" واَنزَلَ الَّذين ظَاهَرُوهُم مِن اَهلِ الكِتَاب وَ مِن صَيَاصِيِهم وَقَذَفَ فِي قُلُوبِهِمُ الرُّعْبَ فَرِيقاً تَقْتُلُونَ وَتَأْسِرُونَ فَرِيقاً"

Na akawateremsha wale waliowasaidia (maadui) katika Watu wa Kitabu kutoka katika ngome zao; na akatia khofu katika nyoyo zao. Baadhi yao mkawa mnawauwa, na wengine mnawateka. Ahzab; 33:26 
Wananchi katika mataifa ya Kiislamu wanawaunga mkono mujahidina na wananchi wa Ghaza. Utawala wowote utakaofanya mambo yake kinyume na matakwa hayo ya wananchi basi wananchi watazidi kuutenga utawala huo na hatima ya tawala kama hizo iko wazi. Kama watawala wa nchi hizo wanajali maisha na heshima zao basi wazingatie maneno ya Amirul Muminin Imam Ali AS aliposema:

"المَوتُ فی حَياتِكُم مَقهورين وَ الحَياةُ فی مَوتِكم قاهِرين"

Ni sawa na mauti kuishi kwenu katika maisha kudhalilishwa; na ni sawa na uhai kufa kwenu katika maisha ya kishujaa (yaani kama mtaishi maisha ya ushindi na kutosalimu amri basi hata kifo kwenu kitakuwa ni sawa na uhai, lakini mkiishi maisha ya kujidhalilisha na kusalimu amri mbele ya maadui, basi maisha yenu yatakuwa ni sawa tu na mauti).
Sehemu ya ujumbe wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa Ismail Hania, Waziri Mkuu wa serikali halali ya Hamas, aliomtumia tarehe 15/01/2009.

Hatima ya tawala dhalili, dhaifu na vibaraka
Mtu yeyote katika ulimwengu wa Kiislamu atakayeichukulia kadhia ya Ghaza kuwa ni kadhia ndogo, ya watu binafsi na inayohusiana na eneo fulani tu, atakuwa amekumbwa na ule usingizi wa sungura ambao hadi leo umeyaletea maafa makubwa mataifa ya dunia. Hapana, suala hili la Ghaza si suala la Ghaza pekee, bali ni suala linalohusu eneo hili zima. Hivi sasa wamechagua eneo hilo ambalo wameliona ni dhaifu zaidi. Naam, mashambulizi yao wameyaanza katika eneo hilo na kama watafanikiwa basi hawataishia hapo, bali shari zao zitaenea katika eneo hili zima. Tawala za nchi za Waislamu ambazo ziko katika eneo hilo na ambazo zinao uwezo wa kusaidia ndugu zao wa Ghaza lakini hazisaidii, zijue kuwa zinafanya kosa kubwa. Kadiri Israel inapopewa fursa zaidi na kadiri udhibiti wa madola ya kibeberu unavyoongezeka katika eneo, ndivyo tawala hizo zinavyozidi kuwa dhaifu na dhalili. Kwa nini tawala hizi hazizinduki? Tawala hizo zinapokuwa dhalili, zinapelekea kudhalilishwa pia mataifa yao. Utawala wa nchi fulani unapokuwa dhalili, dhaifu na kibaraka, hupelekea taifa nalo kuwa dhaifu, dhalili na kibaraka. Ni kwa sababu hii ndio maana tukayataka mataifa hayo yazinduke.
Sehemu ya hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aliyoitoa mbele ya wananchi wa Qum tarehe 08/01/2009.

Tawala za nchi za Kiarabu zimefeli vibaya sana katika mtihani
Tawala zote zina majukumu mbele ya Palestina iwe ni tawala za Waislamu au zisizo za Waislamu. Utawala wowote unaodai kutetea ubinaadamu, una jukumu; lakini jukumu walilo nalo Waislamu kuhusiana na Palestina ni kubwa zaidi. Tawala za nchi za Kiislamu zina jukumu na zinapaswa kutekeleza majukumu yao na utawala wowote ambao utakataa kutekeleza majukumu yake kuhusiana na Palestina utapata pigo kwani wananchi wa mataifa ya Kiislamu wameamka na wanataraji kuona tawala zao zinatekeleza majukumu yao hivyo tawala hizo hazina njia nyingine isipokuwa kutekeleza matakwa ya wananchi wao...
Tawala nyingi za nchi za Kiarabu zimefeli vibaya sana katika mtihani huu wa kadhia ya Ghaza na masuala ya kabla ya hapo. Kila lilipozungumwa suala la Palestina, tawala hizo zilikuwa zinadai kwamba kadhia ya Palestina inawahusu Waarabu tu! Ilipofika wakati sasa wa kufanyiwa kazi suala la Palestina, kadhia hiyo waliitoa kabisa kwenye ajenda zao na badala ya kuisaidia Palestina na Wapalestina yaani ndugu zao na Waarabu wenzao - kama wanavyodai kuwa suala hilo ni la Waarabu na wala si la ulimwengu wa Kiislamu basi angalau kwa uchache wangelifikiri kuwa ni la Waarabu wenzao - lakini ilipofika wakati wa tawala hizo kuifanyia kazi kadhia ya Palestina zote zilirudi nyuma! Wamefeli vibaya sana katika mtihani huo. Historia imerikodi mambo yote haya. Malipo ya vitendo vyao hivyo hayahusiana na Akhera tu, yatashuhudiwa pia hapa hapa duniani. Hii ni kwa sababu hata nusura ya Mwenyezi Mungu kwenu nyinyi ambao mnaendesha mapambano hivi sasa itapatikana hapa hapa duniani.
Sehemu ya miongozo aliyoitoa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu tarehe 27/02/2010, mbele ya washiriki wa kongamano la Ghaza.

Mtihani uliozikumba tawala za nchi za Kiarabu
Tawala za nchi za Kiarabu zimekumbwa na mtihani mgumu. Wananchi walioamka wa mataifa ya Kiarabu wanazitaka tawala hizo zichukue hatua kali na za maana. Jumuiya ya Nchi za Kiislamu (OIC) na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu (Arab League) hazipaswi kutosheka na hatua yoyote itakayochukuliwa hadi pale zitakapohakikisha zimeondoa kikamilifu kuzingirwa Ghaza na kukomeshwa kikamilifu kuvunjwa nyumba za raia katika ardhi za Palestina na Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na kupandishwa kizimbani watenda jinai wote kama vile Netanyahu na Ehud Barack.
Sehemu ya ujumbe wa Ayatullah Udhma Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu alioutoa tarehe 01/06/2010 kufuatia shambulizi la baharini la utawala wa Kizayuni kwenye ufukwe wa Ghaza.

Marekani itakufungieni milango
Marekani hata imeshindwa kumpa tunzo Husni Mubarak, licha ya Rais huyo wa zamani wa Misri kuwa kibaraka mkubwa wa Marekani. Leo pia hali ni hiyo hiyo, imeshindwa kumpa zawadi yoyote licha ya kuwa yuko katika hali mbaya. Hivi sasa pia, wakati wowote ambapo Mubarak atakimbia nchini Misri - Inshaallah - bila ya shaka yoyote nchi ya kwanza itakayofunga milango yake ili Husni Mubarak asipate njia ya kwenda huko, ni Marekani. Hii ni sawa kabisa na walivyomfanyia Ben Ali (Rais wa zamani wa Tunisia) na kama ambavyo pia walimfanyia Muhammad Reza (Mfalme wa Iran). Hivi ndivyo walivyo mabeberu hawa. Wale watu ambao wana matumaini sana na Marekani, wana urafiki na Marekani, ni watiifu kwa Marekani inabidi wapate funzo katika mifano kama hii. Mabeberu hawa ni sawa na shetani. Katika kitabu cha dua cha Sahifat Sajjadia - tab'an sinukuu neno kwa neno - tunasoma: "Wakati shetani anaponitumbukiza kwenye madhambi na kuniona nimetumbukia humo, yeye hukaa pembeni na kunicheka, wakati huo tena hunikana na hanijali tena." Sasa mabeberu hao wako hivi hivi. Siku zote Marekani inajali tu maslahi yake na inafanikisha maslahi yake hayo kwa kuwatumia watu kama hawa dhaifu na duni.
Sehemu ya hotuba za sala ya Ijumaa alizotoa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu mjini Tehran tarehe 4/2/2011.

Madikteta wanapokosa faida hutupwa mithili ya tambara bovu
Hadi hivi sasa kitu tulichokishuhudia kutoka kwa Marekani na nchi nyingine zenye tabia kama ya Marekani ni kuwaunga mkono madikteta kadiri inavyowezekana. Wamemuunga mkono Husni Mubaraka kwa nguvu zao zote. Wamemlinda na kufanya kila njia kuhakikisha hang'olewi madarakani, lakini wakati walipoona kuwa hawana njia nyingine ya kufanya wamemtupa chini Pwaa!!! Hili ni somo jingine kwa vibaraka wa Marekani, wajue kuwa Marekani itaendelea kuonyesha urafiki kwao hadi pale tu itakapoona wana faida kwake. Wakati inapoona hawana faida tena kwake, huwatupa mithili ya tambara bovu na haiwajali tena!
Sehemu ya hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mainduzi ya Kiislamu aliyoitoa kwenye Haram ya Imam Ridha AS tarehe 21 Machi, 2011.

Matokeo ya kosa la Aal Saud ni hasira za wananchi wa eneo
Tunavyoamini sisi ni kuwa Saudia wamefanya makosa kupeleka wanajeshi wao huko Bahrain. Hawakupaswa kufanya kitu kama hicho kwani jambo hilo linawafanya wananchi wa eneo wazidi kuichukia Saudia. Naam, Marekani iko mbali na eneo hili kwa maelfu ya kilomita na kama wakazi wa eneo hili wataichukia, pengine Wamarekani watajifanya hawajali, lakini kwa upande wa Saudia ni kwamba nchi hiyo iko katika eneo hili hili na kama wakazi na mataifa ya eneo hili yataichukia basi jambo hilo litakuwa baya na lenye hasara kubwa kwa nchi hiyo. Kitendo chao cha kupeleka vikosi vyao huko Bahrain ni kosa. Kama mtu mwingine yoyote naye angelifanya kitu kama hicho, naye angelikuwa amefanya makosa.
Sehemu ya hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aliyoitoa kwenye Haram ya Imam Ridha mjini Mashhad - kaskazini mashariki mwa Iran - tarehe 21/3/2011.

Kuwafanyia vitendo vya kinyama wananchi kutazidisha hasira zao
Sisi tumetangaza hadharani mitazamo yetu. Sisi hatushughulishwi na kufutuka madola yenye nguvu bandia duniani. Hakuna wakati tumejali hamaki za madola hayo na katika siku za usoni pia hatutashughulishwa na hamaki na kufutuka kwao. Tutaendelea kusema maneno ya haki na tutaendelea kutangaza wazi misimamo yetu ya haki. Msimamo wa haki ni kwamba wananchi wa Bahrain wanadhulumiwa na ni haki yao kulalamika. Kama jambo hilo atafafanuliwa mtu yeyote yule mwenye insafu na mtazamo huru duniani bila ya shaka na yeye msimamo wake utakuwa ni huo huo wa kuwaunga mkono wananchi wa Bahrain. Kama mtu huyo atafafanuliwa jinsi serikali inavyowafanyia wananchi madhlumu wa Bahrain na jinsi watawala wa nchi hiyo wanavyowafanyia wananchi wao, bila ya shaka atawapa haki wananchi wa Bahrain. Wanafanya makosa, wanapambana na wananchi, wajue jambo hilo halitawasaidia kitu. Naam, mtu anaweza kuweka mashinikizo, akafanya unyama, akaweza kwa muda fulani kuzima moto, lakini hii haina maana kuwa atakuwa amefanikiwa kuzima moto uliowaka kwani vitendo vyake hivyo vitaongeza tu utata wa suala hilo kadiri siku zinavyokwenda. Kuna wakati itafika mahali hali ya mambo itakuwa haidhibitiki tena na wakati huo watashindwa kufanya lolote. Watawala wa nchi hiyo wanafanya makosa, wao wanafanya kosa na watu waliotoka nje na kupeleka vikosi vyao huko Bahrain nao wanafanya makosa makubwa zaidi. Wanajidanganya kudhani kuwa kwa vitendo vyao hivyo wataweza kuzima harakati ya wananchi.
Sehemu ya hotuba aliyoitoa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu mbele ya wananchi wa mkoa wa Fars, tarehe 23 Aprili, 2011.

 

 
< Nyuma   Mbele >

^