Skip to content

Habari

Habari
Hifadhi

Risala na Barua

Matini
Hifadhi

Kumbukumbu na Simulizi

Kabla ya Mapinduzi
Baada ya Mapinduzi

Sauti na Taswira

Picha
Sauti
Video
Mtazamo wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kuhusu Mwamko wa Kiislamu Chapa
17/05/2011
Faslu ya Kwanza – Mfumo wa Kiislamu; mwonyesha njia ya wanadamu
Faslu ya Pili – Maana na umuhimu wa mwamko wa Kiislamu
Faslu ya Tatu – Mwamko wa Kiislamu; vitisho na changamoto
Faslu ya Nne – Majukumu ya mataifa kwa mwamko wa Kiislamu
Mtazamo wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kuhusu Mwamko wa Kiislamu
Faslu ya Kwanza – Mfumo wa Kiislamu; mwonyesha njia ya wanadamu
Uislamu; rasilimali adhimu ya umma wa Kiislamu
Rasilimali adhimu ya umma wa Kiislamu ni dini ya Uislamu, mafundisho yake wadhiha na bayana, sheria zake makini na maamrisho yake yaliyojumuisha kila kitu kwa ajili ya maisha ya watu. Uislamu unaonesha mtazamo wa busara na wa kina kuhusu ulimwengu na mwanadamu, tauhidi halisi, muongozo wa hekima wa kivitendo wa akhlaqi na umaanawi na vile vile unatoa na kubainisha taratibu na kanuni imara na kamili za kisiasa na kijamii na kuainisha majukumu ya kiibada kwa wote na kwa mtu binafsi ili kuwalingania na kuwataka wanadamu wote wazisafishe batini zao na mabaya, maovu, udhaifu na uchafu wa kiroho na kuzijaza ndani yake imani, ikhlasi, upendo, unyofu, matumaini na ukunjufu. Aidha waisafishe dunia yao kwa kuondoa ufakiri, ujinga, dhulma, ubaguzi, hali ya kudumaa na kubaki nyuma, uonevu, udunishaji, utezaji, udhalilishaji na uzugaji.
Uislamu umeyafanya maisha na ulimwengu kuwa vitu vyenye maana maalumu na umeonyesha njia sahihi ya maisha ili kumsaidia mwanadamu katika kujitayarishia maisha ya saada ya kweli na kumtambulisha njia iliyonyooka ya Mwenyezi Mungu. Hukumu na maamrisho yote ya Kiislamu, miongozo yote ya asili ya taratibu za kisiasa, kijamii na kiuchumi ya Uislamu na taratibu na ibada zote za Uislamu zinazofanywa na mtu peke yake na kwa umoja, ni majimui ya vifungu vilivyoshikamana pamoja vya muongozo huu wa maisha ya kweli na ya saada. [01]
Kuenea kwa Mfumo wa Kiislamu
Tangu Mfumo wa Kiislamu ulipoanza kuwepo umekabiliwa na changamoto kubwa ulimwenguni. Na sababu yake ni kwamba watumiaji mabavu ulimwenguni ambao walichokuwa na wanachoendelea kukifikiria ni maslahi yao tu, hawakuweza kuvumilia kuwepo na kustawi nguvu nyingine mpya iliyo dhidi ya maslahi yao haramu. Nguvu hiyo mpya ilijitokeza baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu na kuundwa Mfumo wa Kiislamu nchini Iran. Na si huu utawala na Mfumo wenyewe wa Kiislamu tu, bali yamkini lililokuwa muhimu na la hatari zaidi kwa Uistikbari ilikuwa ni kuenea kwa mwamko wa Kiislamu katika Ulimwengu wa Kiislamu; hatari ambayo leo hii pia inautishia Uistikbari na kuufanya uelekeze uadui wake kwa Ulimwengu wa Kiislamu na hasa kwenye kitovu cha mhimili wa Ulimwengu wa Kiislamu, yaani Mfumo wa Kiislamu (wa Iran).
Medani ya pili ni kueneza utamaduni wa Uislamu wa asili na fikra ya kidini na kueneza fikra iliyopelekea kuamka Ulimwengu wa Kiislamu. Jina la Uislamu na hakika ya Uislamu katika sura ya mtu binafsi ilikuwepo katika ulimwengu mzima wa Kiislamu, baadhi yao kwa kiwango cha juu na baadhi yao kwa kiwango cha chini. Ama mtazamo wa Uislamu kwa ulimwengu, kwa mataifa na kwa umma wa Kiislamu katika sura ya mjumuiko adhimu wenye uwezo na vipawa chungu nzima na wenye uwezo wa kuamka na kuanzisha harakati, ni mtazamo ambao chimbuko lake lilianzia na kudhihiri katika Iran ya Kiislamu na kuenea ulimwengu mzima. Kuuangalia Uislamu kwa mtazamo huo na kueneza fikra hii katika Ulimwengu wa Kiislamu – fikra ambayo ilipelekea kupatikana utawala, na ambao kutokana na mafunzo na mafundisho ya Uislamu umeweza kuleta uhuru, mfumo unaotokana na matakwa ya umma na utawala unaotegemea kura za wananchi – si kitu ambacho kimewahi kushuhudiwa katika sehemu yoyote ile ya Ulimwengu wa Kiislamu katika zama zetu au kwa akali katika karne za karibu na zama zetu. [02]
Upepo wa mwamko wa Kiislamu
Baada ya kufifia fikra za kigeni zilizokuja kwa vishindo na makeke kama vile Usoshalisti na Umaksi, na hasa hasa baada ya kuraruka pazia la uzandiki, hila na hadaa lililoifunika demokrasia ya Kiliberali ya Magharibi, sifa ya kutetea uadilifu na kuleta uhuru ya Uislamu imedhihirika zaidi kuliko ilivyokuwa katika wakati wowote ule na kubakia bila mshindani katika nafasi ya juu kabisa ya matarajio ya wapigania uadilifu, watetezi wa uhuru, wanafikra na wenye vipawa. Kwa jina la Uislamu na kwa matarajio na matamanio ya kuwa na utawala wa uadilifu wa Kiislamu, vijana na mashababi wengi katika nchi za Kiislamu wanaendesha jihadi ya kisiasa, kiutamaduni na kijamii na kueneza katika jamii zao hisia ya kuwa na azma thabiti ya kusimama imara katika kukabiliana na ubeberu na utezaji nguvu wa madola ya kigeni ya Kiistikbari. Upepo wa mwamko wa Kiislamu umevuma katika sehemu zote za Ulimwengu wa Kiislamu; na kuutumia Uislamu katika uga wa utekelezaji limekuwa takwa linalopiganiwa mno. Naam, mwamko wa Kiislamu umetibua na kuvuruga mahesabu ya Uistikbari na kuubadilisha mlingano wa kimataifa uliokuwa ukikidhi matilaba ya Waistikbari. Kwa upande mwengine kuchipuka na kukua fikra mpya za Kiislamu katika kalibu ya usuli na misingi ya Uislamu pamoja na ubunifu katika uga wa siasa na elimu vimethibitisha hadhi ya juu kabisa na hali ya kwenda ulingana na zama iliyonao Uislamu na kufungua uwanja mpana kwa wanafikra na wasomi wenye mwamko wa Ulimwengu wa Kiislamu.
Wakoloni wa jana na Waistikbari wa leo, ambao kwa kutumia siasa zao za hila na ujanja walikuwa wanataka kwa upande mmoja kuziweka jamii za Kiislamu katika hali ya kudumu ya kuwa na fikra mgando na kutotaka mabadiliko, na kwa upande mwengine kutangatanga kati ya hali ya uduni na udhaifu na kuhaha huku na kule kwa ajili ya kupata kila zinachohitajia, hivi sasa wanajiona wamekabiliana na fikra hizi za Kiislamu zilizo imara na zinazokwenda na wakati na kukidhi kila mahitaji ya zama.
Hii tabia ya hamaki na ushari wanayoionesha haitokani na kuwa na nguvu na hali ya kujiamini, bali zaidi inasababishwa na hali ya fadhaa na kuchanganyikiwa. Kwani sasa wanauhisi mwamko wa Kiislamu na wanahisi ni hatari kubwa kwao kuenea fikra ya “Uislamu wa Kisiasa” na kuwa na utawala wa Kiislamu. Wanatetemeka na kutaharuki wanapoifikiria siku umma wa Kiislamu utakaposimama ukiwa umeshikamana kitu kimoja, na ukiwa na matumaini kamili.
Siku hiyo ikifika umma wa Kiislamu ambao una utajiri mkubwa wa maliasili, turathi adhimu za kiutamaduni na kihistoria, eneo pana la kijiografia na idadi kubwa ya watu hautoyaruhusu tena madola ya kibeberu ambayo kwa muda wa miaka mia mbili yalikuwa yakiunyonya damu yake na kuuvunjia heshima na hadhi yake, yaendelee kuufanyia ushari na uovu huo. [03]
Faslu ya Pili – Maana na umuhimu wa mwamko wa Kiislamu
Maana ya mwamko wa Kiislamu
Harakati ya Kiislamu na Mapinduzi ya Kiislamu, maana yake ni kuziasi thamani za kijahilia na mifumo ya kitaghuti ambayo - imemfunga minyororo mwanadamu na kusababisha dhulma, upotovu, ubaguzi wa rangi na wa kimatabaka, ufuska katika jamii, hali ya wananchi kuridhia dhulma na masaibu mengineyo yaliyopata mataifa- na ambayo imekifanya mhanga kila kitu kwa ajili ya kuwafanya wenye nguvu wapate faida na maslahi zaidi na wazidi kuendeleza tawala zao za kidhalimu. Kwa hivyo harakati sahihi ya Kiislamu ni kukabiliana kwa mifumo miwili yenye thamani tofauti na mpambano baina ya tamaduni mbili: utamaduni uliomfunga minyororo mwanadamu, na utamaduni wa kumuokoa mwanadamu. Kwa hivyo kila harakati ya Kiislamu inapaswa ijiweke tayari kukabiliana na watumiaji mabavu wote wa ulimwengu na wala isingoje kushtukizwa.
Leo hii ambapo baada ya karne kadhaa za upotevu, udhalili na uzorotaji, mataifa ya Kiislamu katika pembe nne za Ulimwengu wa Kiislamu yameelekea kwenye mwamko na mapambano kwa ajili ya Allah, huku manukato ya uhuru, kujitawala na kurejea kwenye Uislamu na qur’ani yakiwa yamesambaa kwenye anga ya nchi nyingi za Kiislamu, kile ambacho Waislamu wanakihitajia zaidi hivi sasa kuliko ilivyokuwa katika wakati wowote ule ni kufungamana zaidi na historia yao yenye kung’ara na ya kimuujiza ya huko nyuma, ya kipindi cha mapambano kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na mapambano kwa ajili ya Uislamu cha zama za mwanzoni mwa Uislamu. Kumbukumbu za Kiislamu katika ardhi hii kwa kila Muislamu muelewa na mwenye kutadabari ni sawa na dawa yenye kuponya ambayo imemuokoa na kumtoa yeye kwenye hali ya udhaifu, ya kuwa duni, ya kukata tamaa na kukosa matumaini, na kumuonyesha njia ya kuyafikia malengo ya Uislamu, ambayo kwa kila mtu mwenye hekima na mtazamo wa kina, daima limekuwa ndio lengo la maisha na lengo la kufanya idili na jitihada. [04]
Kuwepo mwamko wa Kiislamu maana yake si kwamba mataifa yote na wananchi wote waliochangia mwamko huo wameitambua misingi ya kifikra ya mfumo wa Kiislamu kwa sura ya kimantiki na ya ujengaji hoja, bali ni kwa maana ya kwamba hisia za kurejea kwenye utambulisho wa Kiislamu zimejitokeza kwa wananchi Waislamu wa kila mahali. [05]
Mwamko wa Kiislamu, tokea mwanzo wake hadi hii leo.
Uhuru, usawa baina ya watu, uadilifu wa kijamii, kuwa na uelewa watu katika jamii, kupambana na maovu na upotofu, kufadhilisha malengo matukufu ya kiutu kuliko matashi ya kibinafsi, kumuelekea na kumkumbuka Mwenyezi Mungu na kukana matashi ya kishetani, kuzingatia misingi mingine ya kijamii ya mfumo wa Kiislamu na vile vile kuzingatia akhlaqi, mwenendo wa mtu binafsi na taqwa ya kisiasa na katika ufanyaji kazi, yote hayo yamepata ilhamu na yametokana na mtazamo huo juu ya ulimwengu na ufahamu wake jumla juu ya ulimwengu na mwanadamu. Uislamu unaipinga na unaiitakidi kuwa ni batili mifumo iliyojengeka juu ya msingi wa utumiaji mabavu, inayoeneza dhulma, ujinga, ukandamizaji, udikteta, udhalilishaji watu na kuwabagua kwa msingi wa rangi, utaifa, damu na lugha zao. Uislamu unakabiliana vikali na kila mfumo au mtu anayejizatiti kufanya uadui dhidi ya mfumo wa Kiislamu. Lakini ghairi ya hao unaamuru kuamiliana nao kwa upendo na kuwasaidia wanadamu wote, wawe ni Waislamu au wasio Waislamu. Ni juu ya misingi hiyo na kwa ajili ya malengo hayo Mapinduzi ya Kiislamu yalitokea nchini Iran na kuasisi mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu. [06]
Katika karne hii moja iliyopita nchi za Kiislamu zimepata hasara isiyoweza kufidika. Wimbi la ukoloni na uvamizi wa madola ya kigeni ulisababisha madhara mengi kwa mataifa ya Kiislamu ambayo utajiri na maliasili zao zilifanywa mlengwa wa hujuma za kila upande za madola ya kikoloni.
Baada ya kupita miaka mingi mataifa ya Kiislamu yalizinduka na harakati ya mwamko wa Kiislamu na bendera za kupigania haki na uhuru zilitoa mwanga wa matumaini kwao katika ulimwengu mzima wa Kiislamu; na hatimaye ushindi wa Uislamu nchini Iran na kuasisiwa mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ukatangaza kuanza kwa zama mpya kwa Ulimwengu wa Kiislamu. [07]
Leo wimbi la mwamko wa Kiislamu ni ukweli halisi na hakika isiyoweza kukanushika. Leo Waislamu wanahisi kuwa wanaweza kuna na taathira duniani katika maamuzi yanayohusu hali ya wanadamu na juu ya hatima na mustakbali wao. Wakati hisia hii inayojengeka ndani ya mataifa inapofikia nukta maalumu hudhihiri na kubadilika kuwa hali halisi. [08]
Leo hii, kutokana na jamii mbalimbali za wanadamu kukabiliwa na ukosefu wa umaanawi na hali ya kutangatanga kutokana na kutingwa na mazonge na masaibu makubwa ya kijamii na ya mtu binafsi yaliyosababishwa na wababe na watumiaji mabavu wa dunia, zinauhitajia Uislamu, miongozo yake na mafundisho yake adhimu; na wito wa Uislamu hauna faida kwa mataifa yanayohiliki tu kwenye lindi la unyonge na ufakiri, bali unatoa matumaini, mvuto, faida na taathira ya kiwango hicho hicho kwa watu walionasa pia kwenye kinamasi cha pumbao na wanaohaha kwa sababu ya ufukara wa umaanawi ulioko kwenye nchi tajiri na zilizoendelea. Mvuto wa Uislamu unaoongezeka siku hadi siku kwa matabaka ya vijana, na hali ya kukirihishwa na pumbao la ulimwengu wa kimaada katika nchi zilizoendelea za Magharibi ambayo inatihibitishwa na tafiti na takwimu zilizopo, ni ishara mojawapo ya ushawishi na mvuto huo.
Ikiwa Waislamu duniani wataielewa na kuithamini rasilimali hiyo adhimu wataweza kuleta mageuzi ya kweli katika maisha yao na wataweza kuziokoa nchi za Kiislamu na hali ya udhaifu, ya utegemezi, ya kubaki nyuma na ya upotevu inazozikabili nchi hizo leo hii. [09]
Suala jengine ni kuhusu harakati za Kiislamu katika baadhi ya nchi za Kiarabu na za Kiafrika. Hii ni bishara njema zaidi katika matukio ya Ulimwengu wa Kiislamu ambapo taifa na vijana wake, wanafikra wake na wananchi wake wa kawaida wa vichochoroni na mitaani wanataka uundwe utawala wa Kiislamu na kutekelezwa sheria za Kiislamu na wanapiga hatua ili kulifikia lengo hilo. Tangu yalipochomoza Mapinduzi adhimu ya Kiislamu nchini Iran na kuundwa Jamhuri ya Kiislamu marafiki walipata matumaini, na kambi ya Uistikbari ikiongozwa na Marekani iliingiwa na khofu na wasiwasi mkubwa kwamba Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yatageuka kuwa kitovu na ngome kuu kwa ajili ya ushindi wa Waislamu katika pembe nyingine za Ulimwengu wa Kiislamu. [10]
Matukio ambayo yamejiri hivi karibuni katika eneo – matukio ya Misri, Tunisia, Libya na Bahrain – ni matukio muhimu sana. Mageuzi ya msingi yamo katika hali ya kujiri katika eneo hili la Kiislamu na Kiarabu. Hii ni ishara ya mwamko wa umma wa Kiislamu. Suala hili ambalo kwa miaka kadhaa sasa sha'ar yake imekuwa ikitolewa katika Jamhuri ya Kiislamu, leo hii linajionyesha kwenye maisha halisi ya wananchi wa nchi hizo.[11]
Kuna hali mbili zilizojitokeza katika matukio haya: Ya kwanza ni kujitokeza kwa wananchi na nyengine ni mwelekeo wa kidini uliopo katika harakati hizi. Hizi ni nukta mbili za msingi. Kujitokeza wananchi wao wenyewe binafsi; ni sawa kabisa na ilivyotokea katika Mapinduzi ya Kiislamu. Vyama vya siasa, waratibu wa mambo mezani na wachambuzi wa kidhahania wa mambo hawakuweza kufanya chochote. Ustadi mkubwa wa Imam (Khomeini) wetu muadhamu ni kwamba aliweza kuwafanya wananchi wajitokeze uwanjani. Wakati wananchi walipojitokeza uwanjani, walivileta pamoja nao viwiliwili vyao, nyoyo zao, nia zao na hima zao zote; na matokeo yake pale palipokuwa na mafundo yalifunguka na pale palipokuwa na mkwamo ulikwamuka. Hayo hayo ndiyo yanayotokea leo katika nchi nyingine. Nchini Misri au Tunisia wananchi wamejitokeza na kujitosa uwanjani; kama ingekuwa ni wanafikra tu na wapangaji mambo kwenye majengo ya roshani hao wamekuwepo siku zote na kila mara wamekuwa wakizungumza; mara chungu nzima wamekuwa wakitoa miito kwa wananchi, lakini hakuna mtu aliyekuwa akiyajali maneno yao. Hapa wananchi wenyewe wamejitokeza na kujitosa uwanjani na muelekeo wao ni muelekeo wa kidini; yaani sala ya Ijumaa; sala za jamaa, jina la Mwenyezi Mungu, maulamaa wa dini, wafanya tablighi ya dini na waasisi wa fikra mpya za kidini katika baadhi ya nchi. Hao ndio waliojitosa uwanjani na kwa hivyo wananchi nao wakajitokeza uwanjani. Hii ndio hali maalumu ya kadhia hii. Na kwa nini walijitokeza? Ni wazi kabisa kwamba kitu kilichowavuta, ni suala la izza na heshima ya utu. Nchini Misri, nchini Tunisia na vile vile katika nchi nyingine, ghera za wananchi zilikuwa zimechomwa na kuumizwa na watawala hao madhalimu. [12]
Kuupata tena Waislamu utambulisho wao wa Kiislamu
Leo hii kuna matukio kadhaa yanayojiri ulimwenguni ambayo ukweli wake hauwezi kukanushika. Jambo la kwanza ni la mwamko wa Ulimwengu wa Kiislamu; hakuna mtu yeyote mwenye shaka juu ya hili. Leo Waislamu wa kila pembe ya dunia – iwe ni katika nchi za Waislamu wenyewe au katika maeneo ambayo Waislamu ni jamii ya wachache – wanaonyesha muelekeo wa kurejea kwenye Uislamu na kuupata tena utambulisho wao wa Kiislamu. Leo wanafikra wa Ulimwengu wa Kiislamu ambao wamechoshwa na Usoshalisti na nadharia za Kimagharibi wanaonyesha muelekeo wa kuvutiwa na Uislamu na wanatafuta dawa na ufumbuzi wa matatizo ya mwanadamu kutoka katika Uislamu. Leo nyoyo za umma wa Kiislamu zimeonyesha kuvutiwa na Uislamu kwa namna ambayo haijawahi kushuhudiwa kwa muda wa karne kadhaa. Baada ya ubeberu na udhibiti mkubwa na wa uga mpana wa miongo kadhaa, wa kisiasa na kiutamaduni wa Magharibi na Mashariki katika nchi za Kiislamu, leo mtazamo na uoni wa vijana wa Ulimwengu wa Kiislamu umeelekea kwenye Uislamu; huu ni ukweli halisi ambao wanaukiri hata Wamagharibi wenyewe na Waistikbari wa dunia. Wameshakariri mara kadhaa kusema kwamba endapo utafanyika uchaguzi huru katika nchi yoyote ile ya Kiislamu, watakaochaguliwa na wananchi ni wale wenye imani na walioshikamana na Uislamu na ambao wanafanya kazi ya kuueneza Uislamu. Na ni kwa sababu hiyo ndiyo maana leo hii madai ya Magharibi ya kutetea demokrasia yamekuwa na migongano. Kwa upande mmoja wameishika bendera ya demokrasia na ya kutaka tawala zinazotokana na matakwa ya wananchi, lakini kwa upande mwengine hawajusuru na wala hawathubutu kupeperusha bendera hiyo ya demokrasia kwa maana yake halisi katika Ulimwengu wa Kiislamu; kwa sababu wanajua kwamba katika nchi yoyote ile miongoni mwa nchi za Kiislamu, ikiwa kura za wananchi na matakwa yao yatapewa nafasi hakuna shaka yoyote kuwa wanaotaka Uislamu ndio watakaoshika hatamu za madaraka na utawala, na wale walio Waislamu hasa ndio watakaochaguliwa na wananchi.
Jambo la pili ni kwamba adui nambari moja wa mwamko huu wa kuelekea kwenye Uislamu na kupigania kuwa huru ni madola ya Kiistikbari. Na sababu yake inajulikana wazi; sababu ni kwamba Uislamu unapinga ubeberu; unapinga mataifa kuwa na utegemezi kwa madola ya kigeni; unapinga hali ya kubaki nyuma kielimu na kiutendaji ambayo madola hayo yamezitwisha nchi za Kiislamu kwa miaka na miaka; unapinga mataifa kufuata na kuiga kibubusa kila kitu kwa wengine. Na hayo yote ni mambo yanayokinzana na siasa za kikoloni na kiistikbari ambazo kwa muda wa miaka mia mbili au zaidi zimekuwa zikitekelezwa na Waistikbari na Wamagharibi katika Ulimwengu wa Kiislamu; leo hii pia wana manufaa na maslahi yao waliyojiainishia katika eneo hili. Mwamko wa Kiislamu ni nukta inayokinzana kikamilifu na matakwa yao; na ndiyo maana wanaupiga vita kwa nguvu zao zote na kuupinga kisiasa na kwa propaganda.
Jambo la tatu – ambalo watu wote wanauelewa ukweli wake, japokuwa kuna wengi wanaoukana – ni kwamba dhihirisho la mwamko huu wa Kiislamu si wale watu ambao leo hii wanauonyesha Ulimwengu wa Kiislamu kwa sura ya ugaidi. Wale watu ambao wanatenda jinai hizo huko nchini Iraq; watu ambao katika Ulimwengu wa Kiislamu wanatumia jina la Uislamu kufanya mambo dhidi ya Waislamu; watu ambao kubwa linalowashughulisha wao ni kuanzisha hitilafu baina ya Waislamu – kwa kutumia anuani za Ushia na Usuni, anuani za ukabila – watu hao hawawezi asilani kuwa kielelezo na nembo ya mwamko wa Kiislamu; na hili hata Waistikbari wenyewe wanalijua. Hao watu wanaojaribu kuuonyesha Uislamu katika Ulimwengu wa Magharibi kupitia sura ya makundi yenye mawazo finyu na fikra mgando na za watu waenezaji khofu na vitisho, wanaelewa kwamba ukweli hauko hivyo. Uislamu ambao Ulimwengu wa Kiislamu unahisi mwamko wake leo hii ni Uislamu wa fikra, tafakuri ya kina na wenye hoja mpya; ni Uislamu wenye kutoa njia za ufumbuzi wa maisha kwa ajili ya kutatua matatizo na mazonge yanayoyakabili maisha ya wanadamu; si Uislamu wa fikra yabisi, si Uislamu wa uoni finyu na si Uislamu uliojiweka mbali na kila aina ya uhuru wa kifikra; Waistikbari wanalijua hilo. [13]
Umuhimu wa mwamko wa Kiislamu
Hakuna shaka yoyote kuwa ulimwengu wa Uistikbari unauhesabu mwamko wa Waislamu, Umoja baina ya Waislamu na maendeleo ya mataifa yetu katika medani za elimu, siasa na teknolojia kuwa ni kikwazo na kizuizi kikubwa zaidi kwa ubeberu na udhibiti wao wa ulimwengu, na kwa hivyo wanapambano nayo kwa nguvu zao zote. Tajiriba ya kipindi cha ukoloni na ukoloni mamboleo iko mbele ya macho yetu sisi mataifa ya Waislamu. Leo hii ambapo tuko katika kipindi cha Ukoloni mamboleo wa kisasa inatupasa tujifunze kutokana na tajiriba hizo za huko nyuma na wala tusikubali kwa mara nyingine mustakbali wetu uwe chini ya udhibiti wa adui kwa kipindi kingine kirefu.
Hivi sasa, - ambapo kwa baraka za kujitolea mhanga wanamapambano na kutokana na ushujaa na ukweli wa viongozi katika baadhi ya sehemu za Ulimwengu wa Kiislamu, mwamko wa Kiislamu umeeneza mawimbi yake na kuwaleta uwanjani vijana, wenye vipawa na wananchi wote kwa ujumla katika nchi nyingi za Kiislamu na kuianika hadharani sura ya kihaini ya mabeberu mbele ya wanasiasa na viongozi wengi wa Kiislamu, - kwa mara nyingine tena viongozi na viranja wa Uistikbari wanatafuta mbinu mpya za kuwawezesha kuendeleza na kuimarisha udhibiti wao kwa Ulimwengu wa Kiislamu.
Nukta kuu ya malengo haya ni kulizima wimbi la wanaotaka Uislamu na kuziweka tena katika hali ya kutengwa thamani za Kiislamu. Leo hii nyenzo zote za propaganda na za kisiasa za Marekani na mabeberu wengine zinatumiwa ili kuchelewesha na au kama itawezekana kuikandamiza na kuizima kabisa harakati ya mwamko wa Kiislamu.
Leo ulimwengu na hasa Ulimwengu wa Kiislamu unakipita kipindi nyeti. Kwa upande mmoja mawimbi ya mwamko yameenea ulimwengu mzima wa Kiislamu, na kwa upande mwingine nikabu ya ghilba na unafiki iliyokuwa imefunika sura ya kihaini ya Marekani na Waistikbari wengine imedondoka. Kwa upande mmoja harakati kuelekea kwenye utambulisho, nguvu na izza imeanza katika sehemu mbalimbali za Ulimwengu wa Kiislamu, na katika nchi yenye adhama ya Iran ya Kiislamu, mmea wa elimu na teknolojia ya kujitegemea itokanayo na wataalamu wa ndani umestawi, na hali ya kujiamini iliyobadilisha anga ya kisiasa na kijamii imeenea hadi kwenye anga ya elimu na ujenzi wa nchi. Na katika upande mwingine nyufa na matundu ya udhaifu na mparaganyiko yamejitokeza kwenye safu za kisiasa na kijeshi za maadui. Leo Iraq kwa upande mmoja na Palestina na Lebanon kwa upande mwengine, zimekuwa mahali pa maonyesho ya udhaifu na kuishiwa nguvu za majigambo Marekani na Uzayuni. Siasa za Mashariki ya Kati za Marekani zimekabiliwa na vizuizi vikubwa katika hatua zake za awali; na kugonga mwamba kwa siasa hizo kumekuwa pigo kubwa dhidi ya wapangaji wake. [14]
Kuongezeka mvuto wa Uislamu kwa mataifa
Hasira za vyombo vya Uistikbari na hasa Marekani zinatokana na kuona kwamba mwamko wa Kiislamu unazidi kuenea siku baada ya siku katika ulimwengu mzima wa Kiislamu. Wao walikuwa na matumaini kwamba baada ya muda kupita sha’ar za Jamhuri ya Kiislamu duniani zitakuwa zimechakaa na kutokuwa na taathira tena; lakini wanaona haikuwa hivyo. Tamaa zao zote zilikuwa ni kwamba kutokana na kufariki na kuaga dunia Imam (Khomeini) – ambaye alikuwa mwenge uliowavuta wapenzi wa haki ulimwengu mzima - sha’ar za Kiislamu hazitokuwa na athari na zitasahaulika; lakini wanaona haikuwa hivyo.
Leo hali imekuwa hivi; na hili ndilo linalowakasirisha maadui. Wao walikuwa na tamaa kwamba ndani ya Jamhuri ya Kiislamu mwanga wa nuru hii utaanza kufifia taratibu na hatimaye kuzimika kabisa, seuze kwamba nuru hii ing’are, na siku baada ya siku mwanga wake uongezeke zaidi ulimwenguni. Leo wanaona nuru ya mafundisho ya Kiislamu, jihadi dhidi ya mashetani na Shetani Mkubwa (Marekani) na harakati kuelekea kwenye thamani za kidini na za Kiislamu inazidi kutoa mwanga siku baada ya siku, ndani na nje ya nchi. [15]
Leo kuenea wimbi la mwamko wa Kiislamu ulimwenguni imekuwa ni hakika yenye kutoa bishara njema ya mustakbali mwema kwa umma wa Kiislamu. Mwamko huu wenye nguvu ulianza tangu miongo mitatu nyuma kwa ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu na kuundwa mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu. Umma wetu mkubwa ulipiga hatua mbele bila ya kusita, ukaviondoa vizuizi ulivyokumbana navyo njiani na kupata ushindi katika medani mbalimbali. Kuwa tata zaidi mbinu za uadui wa Uistikbari na kutumia gharama kubwa kufanya kila uwezalo ili kukabiliana na Uislamu kunatokana na maendeleo hayo yaliyopatikana. Propaganda kubwa za adui zenye lengo la kuufanya Uislamu uonekane tishio, hatua za kujaribu kuanzisha hitilafu kati ya madhehebu za Kiislamu, kupalilia taasubi za kimatapo na kimadhehebu, kuchochea uadui bandia wa Shia dhidi ya Suni na Suni dhidi ya Shia, kuzusha mifarakano baina ya nchi za Kiislamu na kufanya kila njia ili kushadidisha hitilafu na kuzibadilisha kuwa uadui na migogoro isiyoweza kutatuka na kuyatumia mashirika ya kiintelijinsia na kijasusi ili kueneza sumu ya uovu na ufuska miongoni mwa vijana, yote hayo ni radiamali za kutapatapa na kupaparika kutokana na harakati makini na hatua thabiti za umma wa Kiislamu kuelekea kwenye mwamko, izza na uhuru. [16]
Taathira ya Mapinduzi ya Kiislamu katika mwamko wa mataifa
Alhamdulillah leo jamii za Kiislamu zimeelewa umuhimu wa mfumo wa Kiislamu. Kwa muda wote wa kipindi cha miaka mingi waandishi, wazungumzaji wakubwa wakubwa na nyoyo chungu nzima zimepata mvuto wa kuelekea upande huu. Mwamko wa Kiislamu umeanza; jamii za Kiislamu zimeelewa umuhimu wa hazina hii waliyonayo; tab’an ni kwa sababu hiyo pia ndio maana uadui wa maadui wa Uislamu pia umeongezeka. Daima wamo katika kuchochea hitilafu na mifarakano kati ya mataifa ya Waislamu ili kwa kuamsha hisia za ukabila, utaifa, ghera na taasubi kuweza kulivuta na kulielekeza kila kundi upande fulani. Hii inaonesha kuwa adui ametambua kwamba uelewa wa Kiislamu na mwamko wa Kiislamu katika maeneo ya Waislamu ulimwenguni, unaonyesha athari zake. Huo ndio ukweli wa mambo. Kwa hakika hisia hizi ndizo zitakazoyavuta mataifa ya Kiislamu kuelekea kwenye mfumo wa Kiislamu na kuelekea katika ujengaji wa umma mmoja wa Kiislamu; huu ni mustakbali usio na shaka. Na huu uadui wa kila aina hauna athari yoyote. Nguvu ya Uislamu ni kubwa zaidi hata kuweza kuathiriwa na uadui huo; kama ambavyo ndani ya Iran ya Kiislamu kile ambacho hakuna aliyekuwa akikitarajia ni kuona kuwa nguvu adhimu ya Kiislamu imeweza kuwaunganisha wananchi; imeweza kuzikurubisha nyoyo pamoja; ikaifanya imani ya Kiislamu kuwa mwega na kutoa msukumo kwa harakati hii na kupelekea kuundwa hapa mfumo wa Kiislamu. Hili ni jambo ambalo limeweza kutokea. [17]
Leo harakati iliyoanzishwa na Imam wetu muadhamu (Khomeini) imetoa mvukuto mkubwa kwa dunia na kuzitikisa pande zote mbili za mashariki na magharibi. Matukio haya yanayojiri ulimwenguni – baadhi yao moja kwa moja, na baadhi yao kwa njia isiyo ya moja kwa moja – yanahusiana na mapinduzi yetu ya Kiislamu. Hii kwamba leo katika ulimwengu uliokuwa umejengeka kutokana na kambi mbili kambi moja imeshaondolewa kwenye uga wa siasa za ulimwengu na hivyo hakuna tena kitu kinachojulikana kama kambi ya Mashariki na Usoshalisti, na hii kwamba mlingano wa kimataifa katika uhusiano baina ya madola yenye nguvu, madola na nchi ndogo ndogo, na mataifa na tawala mbalimbali umesambaratika kikamilifu, yote haya yanahusiana na ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu na dini nchini Iran na yanahusiana na mwamko wa Waislamu na kupatikana uelewa wa hisia za dini ndani ya nyoyo na dhamiri za watu. [18]
…Adui anajaribu kueneza makelele na kufanya hila za kipropaganda ili mhisi kuwa kuna haja ya kujihadhari na jina la Utawala wa Kiislamu na mfumo wa Kiislamu, na pengine kwa njia hiyo huenda baadhi ya watu wenye nyoyo nyepesi wakajiwa na fikra kwamba ili wasiitie wasiwasi Marekani na madola ya Magharibi ni bora wajiepushe kutumia jina la Utawala wa Kiislamu katika matamshi wanayotoa hadharani. Nasaha zangu ni kwamba jiepusheni kabisa na dhana hii ya ufanyaji mambo kimaslahi unaokinzana na maslahi halisi. Lielezeni bayana, kwa uwazi kabisa, kwa kukariri na katika mazingira yoyote yale lengo la kuunda mfumo wa Kiislamu, utawala wa qur’ani na Uislamu pasina kuwa na hali yoyote ya kulegeza msimamo, na wala msitake kukwepa kulitamka jina tukufu la Uislamu mkamtia tamaa adui na kuligubika lengo hili kwa kiwingu cha utata. [19]
Faslu ya Tatu – Mwamko wa Kiislamu; vitisho na changamoto
Upinzani wa Magharibi na Kukabiliana kwake na mwamko wa Kiislamu
Ukweli mwengine wa mambo ni kwamba ulimwengu wa Magharibi pamoja na uwezo wake wote haujaweza kuushinda na kuuzima mwamko wa Kiislamu. Katika maeneo mbalimbali ya Kiislamu, wamefanya kila aina ya propaganda dhidi ya Uislamu, dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu, dhidi ya viongozi na wafanya islahi wakubwa wa Kiislamu na dhidi ya hukumu za Uislamu. Wameandaa kila aina ya mamluki kwa ajili ya kuusema vibaya Uislamu na kueneza tuhuma dhidi ya Uislamu na hukumu za Kiislamu; wametumia silaha ya nguvu za kijeshi, wametumia silaha ya uchumi na wametumia silaha ya propaganda kubwa za vyombo vya habari kwa namna ya ajabu na ya kushangaza; lakini hadi sasa hawajafika popote. Muelekeo mkubwa zaidi wa vijana Waislamu katika nchi za Kiislamu ni wa kuvutiwa na Uislamu na fikra za Kiislamu. Hamu, shauku na mapenzi hayo yanazidi kuongezeka ndani ya nyoyo za wananchi wa mataifa ya Waislamu siku baada ya siku.
Kile ambacho kinapasa kuwa natija ya ukweli huu ni kwa Ulimwengu wa Kiislamu kuelewa thamani yake. Leo hii njia pekee itakayouwezesha Ulimwengu wa Kiislamu kulinda maslahi ya mataifa ya Kiislamu ni kushikamana na kalima ya umoja katika mhimili wa Uislamu; kusema “hapana” kwa tamaa na malengo ya kikoloni ya maadui na Waistikbari. Lengo la Uistikbari ni kufuta utambulisho wa kitaifa na kidini katika Ulimwengu wa Kiislamu na hasa katika Mashariki ya Kati. Kukabiliana na lengo hili kutawezekana kwa kuwa na umoja zaidi, mshikamano zaidi, kushikamana na Uislamu, kueneza Uislamu na kusimama dhidi ya malengo ya kibeberu ya Marekani na Waistikbari, na si vinginevyo. Leo Marekani imekuwa na sura yenye doa na isiyokubalika popote pale ulimwenguni. Leo Wamarekani wamekanyaga sha’ar zao zote kutokana na vitendo vyao. Leo mashinikizo wanayotoa Wamarekani kwa taifa la Iraq, hali ya machafuko iliyoko Iraq, uungaji mkono wao usio na masharti wala mipaka kwa Wazayuni wauaji na wamwagaji damu, maafa waliyoyaanzisha Afghanistan na mashinikizo wanayotoa kwa nchi za Kiislamu, yote hayo yameifanya Marekani iwe na sura yenye kukirihisha na kuchukiza katika Ulimwengu wa Kiislamu. Leo Ulimwengu wa Kiislamu unaweza kukabiliana na mwenendo huu wa Marekani wa kutaka kuwa na nguvu na mamlaka zaidi; unapaswa kukabiliana nao; na hakuna njia nyingine ghairi ya hiyo. [20]
Leo Uistikbari wa dunia, manduli wa kisiasa wa ulimwengu na madola yenye nguvu za kijeshi na kimaada katika kila pembe ya dunia ambayo yameghiriki kwenye ufisadi na upotofu yana uadui na Uislamu na mfumo wa Kiislamu; na sababu ni kwamba Uislamu na mwamko wa Waislamu ndio tishio kwao na ndio unaofichua maovu yao. [21]
Ukatili na uovu ulioonyeshwa na madola ya Kiistikbari katika miaka hii ya karibuni katika sehemu mbalimbali za dunia ni radiamali kwa mwamko na ushujaa wa mataifa. Wakati mataifa yaliyodhalilishwa yanapoamua kulikumta vumbi la idhilali nguoni mwao na kuziweka kando hisia za kujiona dhalili na hivyo kusimama kidete, madola yanayowadhalilisha hulazimika kujiangalia tena. Bila ya shaka yatapata pigo; yamepata pigo, na mapigo zaidi ya hayo yatafuatia. Katika jamii za Kiislamu wimbi la mvuto kuelekea kwenye Uislamu wa kimapinduzi ni wimbi lililo hai; hakuna chochote wanachoweza kufanya ili kulidhibiti. Bila ya shaka wanafanya ukandamizaji, wanatoa mbinyo, wanazusha tuhuma, wanawapa jina la ugaidi; hata kama watakuwa hawana uhusiano wowote na Jamhuri ya Kiislamu, lakini ili kuweza kuzibana pande zote mbili, wanazusha madai ya kuwepo uhusiano huo. Hizi ni kazi ambazo adui anazifanya; lakini kile ambacho hawezi kukifanya ni kulifuta na kulizima wimbi hili la kuelekea kwenye Uislamu wa kimapinduzi katika mataifa. Hili hawawezi kulifanya, hawajaweza kulifanya na baada ya hapa pia hawatoweza kulifanya. [22]
Hata hivyo vita vya madola ya Kiistikbari dhidi ya Uislamu havijakomea katika yale yaliyofanywa na madola hayo kuhusiana na Iran tu, watu wake na mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu; bali uadui wao dhidi ya Uislamu umepanua wigo wake kwa nguvu kubwa zaidi, kwa kutumia mbinu za kisiasa na kipropaganda na vile vile mbinu za kiutamduni. Mashinikizo na mbinyo unaotolewa na tawala tegemezi na vibaraka wa Marekani dhidi ya wanamapambano, watetezi wa uhuru, maulamaa na wanafikra Waislamu katika nchi za Kiislamu, na pia mbinyo unaotolewa kwa Waislamu ambao ni jamii ya wachache katika nchi zisizokuwa za Kiislamu ni mifano ya wazi ya vita vya kisiasa dhidi ya Uislamu; na uandishi wa makala na vitabu na uandaaji filamu za kuuvunjia heshima Uislamu na kuzionyesha kwenye mazingira ya Kiislamu na yasiyo ya Kiislamu ni mifano ya vita vya kiutamaduni dhidi ya Uislamu. Hivi sasa madola ya Kiislamu kama vile Marekani, Uingereza na mfano wa madola hayo yanatumia pesa chungu nzima kutekelezea hujuma zao za kijinai; na kwa masikitiko ni kwamba wako waandishi na wasanii ambao kwa sababu ya manufaa na maslahi ya kimaada, wanazipa kisogo dhamiri zao za kisanaa na kifasihi na kuzifanyia miamala kalamu, ndimi na sanaa zao ili zitumikie malengo maovu ya madola yenye nguvu. [23]
Mwamko, wenzo wa kudhibitia madola ya kikoloni
Katika kukabiliana na hulka ya kufurutu mpaka uliyonayo Uistkibari, kuna wenzo mmoja tu unaoweza kudhibiti na kuzuia kufurutu mpaka huko; nao ni mwamko na irada ya mataifa. Wakati taifa linapokuwa limeamka hutambua haki zake, humjua adui yake, hulielewa lengo la adui huyo na hivyo huchukua uamuzi wa kukabiliana naye. Inapofikia hatua hiyo, wingi wa Uistikbari, Marekani pamoja na zana zao za kijeshi hukwama na kugonga mwamba. Inapofikia hatua hiyo huwa hawana uwezo tena wa kufanya lolote. Hii ndio nukta kuu na ya msingi ambayo Mapinduzi ya Kiislamu yalishikamana nayo tokea siku ya kwanza na mfumo wa Kiislamu ukaundwa kwa kuzingatia msingi huu imara.[24]
Hatari zinazoukabili mwamko wa Kiislamu
Kwa muda wa karne kadhaa madikteta, wakoloni, tawala za kijabari na maadui wa Uislamu waliwaweka Waislamu katika hali ya udhaifu na idhilali. Leo hii ambapo kuna harakati kuelekea kwenye izza na mwamko wa Waislamu hakuna shaka yoyote kwamba maadui watakuwa wanavizia na kunyemelea njiani; kwa hivyo inapasa kujihadhari nao. Mimi nitaitaja moja ya hatari zinazotukabili; nayo ni kuwepo hitilafu baina ya Waislamu, hitilafu baina ya mapote na madhehebu za Kiislamu; na hitilafu baina ya kaumu na makabila ya Kiislamu.
Angalieni wenyewe, ni wapi katika Ulimwengu wa Kiislamu ambako hakuna mikono ya kihaini inayojaribu kuanzisha hitilafu na mifarakano? Na ni wapi ambako bongo chafu za wapangaji mikakati wa Kiistikbari zimefanikiwa kuwapata watu dhaifu na wenye nyoyo rahisi kughilibika ambao hazikuwatumia kwa ajili ya malengo yao? Lengo la karibu na hatua kubwa tunayopaswa kuipiga ni kujenga umoja baina ya matapo na madhehebu za Kiislamu na baina ya makundi ya Waislamu. Kuna baadhi ya watu ambao kazi yao kubwa ni kuanzisha mifarakano ili kuidhuru harakati hii ya kuleta izza ya Kiislamu; watu hao watambueni kisha mkabiliane nao kwa umakini na busara. Ikiwa Waislamu watakuwa macho na makini, na wakajihisi wana izza kutokana na Uislamu na wakajihisi wana nguvu kutokana na Uislamu hakuna shaka yoyote ile harakati hii itaweza kufikia malengo yake. [25]
Kujinyongesha kwa watawala wa Kiislamu
Inasikitisha kuona kwamba aghalabu ya wanasiasa wa nchi za Kiislamu, kwa sababu ya kutoijua thamani ya nguvu kubwa na adhimu waliyonayo ya wananchi wao wameamua kujinyongesha mbele ya madola ya kibeberu, na badala ya kuitumia fursa kubwa na adhimu ambayo ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu umewapatia ili kuangalia upya uhusiano mchafu na wa kiudhalilishaji uliopo baina yao na Marekani na Ulaya, wameamua kuchukua hatua ya ukurupukaji ya kuyafanyia uadui mapinduzi haya ya uokovu na yenye baraka kubwa ambayo wananchi wao wana hamu nayo kubwa; na matokeo yake wamezidi kutopea kwenye lindi la giza la uhasama na wananchi wao na kuselelea kwenye mnaso wa mazonge ya kuburuzwa na kunyongeshwa na madola ya kishetani. Kwani kinyume na maneno ya qur’ani ambayo inasema: فان العزة لله جميعا yaani izza yote iko (inapatikana) kwa Mwenyezi Mungu wameamua kwenda kutafuta izza kwa Marekani. Hakuna jaza na malipo ya ufahamu huu pogo na utendaji huu mbovu ghairi ya kubaki katika hali dhalili ya kukhofu na kuchelea hatima yao na ya tawala zao, pasina kufikia kwenye nukta yoyote ya uhakika; na badala yake kujionea kivitendo na kwa macho yao kwamba wakati wa kukabiliwa na hatari Marekani na viongozi wengine wa madola ya Kiistikbari hawana uwezo wa kuwaokoa; na pia kuelewa bayana kuwa ni uwongo kudhani kwamba Marekani inao uwezo wa kufanya chochote inachotaka.[26]   …Suala muhimu ambalo Waislamu wote wanapaswa kulielewa na kujihisi kuwa wana jukumu la kukabiliana nalo ni kwamba leo hii takribani katika kila mahali duniani kuna vita vikali na vya njama kubwa vinavyoendeshwa na madola ya Kiistikbari dhidi ya Uislamu na Waislamu. Japokuwa asili yake vita hivi havikuanza leo na ishara zake zimeonekana waziwazi katika historia ya ukoloni wa Ulaya, lakini tunaweza kusema kuwa kutumia kwake mbinu za kila aina, kudhihirishwa waziwazi, na kutekelezwa katika baadhi ya hali kwa ukatili mkubwa, hadi sasa hayo yalikuwa hayajawahi kushuhudiwa, na kwa kweli ni mambo yanayohusiana na zama hizi. Kwa kuiangalia hali ya hivi sasa ya Ulimwengu wa Kiislamu ndipo hali hii ya kushadidi na kuendeshwa waziwazi vita dhidi ya Uislamu inapodhihirika zaidi. Na sababu yake haitokani na kitu kingine isipokuwa ni kuongezeka na kuenea kwa mwamko wa Waislamu. Ukweli ni kwamba katika muongo mmoja hadi miwili ya hivi karibuni Waislamu wa pande za mashariki na magharibi ya Ulimwengu wa Kiislamu na hata katika nchi zisizokuwa za Kiislamu wameanzisha harakati ya kina na ya kweli, ambayo inapasa kuitwa harakati ya “kuhuisha Uislamu”. Hivi sasa kizazi cha vijana na ambao ni wasomi na wenye elimu na utaalamu wa taaluma za zama hizi, ambao kinyume na mtarajio ya wakoloni wa jana na waistikbari wa leo, wana uoni mpana na wa kina juu ya mambo hivi sasa wameuelekea Uislamu na kuitafuta ndani yake hakika iliyowapotea. Mapambano ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Iran, uthabiti wake, nguvu zake na uimara wake unaoongezeka siku hadi siku ndio kilele cha harakati hii changa na yenye chimbuko imara; na mapambano hayo ndiyo yaliyotoa mchango mkubwa zaidi katika kuenea kwa mwamko wa Waislamu. Hiki ndicho kile ambacho kambi ya Uistikbari, ambayo siku zote imekuwa ikijifanya kuwa inajiepusha na upigaji vita itikadi na matukufu ya mataifa, sasa kinailazimisha kupambana na Uislamu waziwazi, kwa kutumia kila njia inayowezekana, na baadhi ya wakati kwa ukatili na utumiaji nguvu. Huko Marekani na katika nchi za Ulaya, wameshawahi kushuhudiwa kwa uchache mara moja viongozi na wanasiasa kadhaa ambao wameeleza kinagaubaga katika matamko yao kwamba kukua na kuenea kwa imani ya Kiislamu ni tishio na hatari kubwa ambayo kuna ulazima wa kupambana nayo. Kadiri mvuto na muelekeo wa vijana wa Kiislamu wa kushikamana na Uislamu kiimani na kimatendo unavyoongezeka zaidi ndivyo matamshi hayo yanayotokana na uadui na hali ya kutapatapa yanavyowekwa bayana na wadhiha zaidi. Na hivi sasa hali imefikia hadi hata viongozi na wanasiasa wa baadhi ya nchi za Kiislamu pia, ambao siku zote walikuwa wakiificha inadi na uadui wao dhidi ya Uislamu nyuma ya nikabu ya unafiki, wanawafuata mabwana zao wa Marekani na UIaya, na kutangaza kinagaubaga na hadharani juu ya hatari ya Uislamu! Na kuichukulia imani tukufu ya wananchi wanaotawala kuwa ni tishio kwao. [27]
Vita vya kinafsi vya Uistikbari dhidi ya mwamko wa Kiislamu
Silaha kubwa zaidi aliyonayo mkononi mwake adui Muistikbari ambaye wimbi hili linaloongezeka la mwamko wa umma wa Kiislamu ni tishio kwa tamaa na maslahi yake haramu, ni silaha ya vita vya kinafsi: kujenga hisia za kutokuwa na matumaini, kudunisha utambulisho na kuonyesha makeke kutokana na nguvu na uwezo wake wa kimaada alionao. Leo hii zimetumika, na katika siku za usoni pia zitatumika maelfu ya nyenzo za propaganda ili kuwavunja moyo na kuwakatisha tamaa Waislamu juu ya mustakbali unaong’ara au kuwashajiisha juu ya mustakbali utakaokwenda sambamba na malengo machafu ya maadui. Vita hivi vya kiutamaduni na kinafsi vya tokea mwanzoni mwa kipindi cha ukoloni hadi sasa ndio silaha ambayo imekuwa na ufanisi mkubwa zaidi kwa Magharibi katika kuzidhibiti nchi za Kiislamu. Hujuma za mshale huu wenye sumu zimewalenga kwanza wenye vipawa na wanafikra, na kisha wananchi wa kawaida. Kupambana na mbinu hii hakutowezekana isipokuwa kwa kuupa mgongo utamaduni wa kutwisha na kulazimisha wa Magharibi. Wanafikra na wenye vipawa wa Kiislamu wanapaswa kuuchuja utamaduni wa Magharibi, kwa kuyachukua yale yenye faida, na kuyatupilia mbali kwa kuyaondoa kwenye fikra na utendaji katika jamii za Kiislamu yale yenye madhara, uharibifu na yanayochochea ufisadi na ufuska. Kipimo cha kutumia katika uchujaji huu muhimu ni utamaduni wa Kiislamu na fikra kwasi zenye kutoa mwanga wa uongofu na ufumbuzi wa matatizo zitokazo kwenye qur’ani na suna. Hii ndio nukta ya msingi katika mapambano ya pande zote na yenye mwisho mwema ambayo jukumu lake liko kwenye mabega ya maulamaa wa dini, wanafikra na wanasiasa wenye vipawa katika ulimwengu mzima wa Kiislamu. [28]
Hivi sasa Marekani na Uistikbari wa Magharibi kwa ujumla umefikia natija kwamba kitovu cha mwamko na harakati ya kukabiliana na njama yao ya kutaka kuutawala ulimwengu mzima ni nchi na mataifa ya Waislamu hususan ya eneo la Mashariki ya Kati. Kwa hivyo kama hawatoweza katika kipindi cha miaka michache ijayo kuidhibiti na kuizima harakati ya mwamko wa Kiislamu kwa kutumia wenzo wa kiuchumi, kisiasa, kipropaganda na hatimaye kijeshi basi mipango na mahesabu yao yote –ya kuwa na mamlaka mutlaki ya ulimwengu na kudhibiti maliasili muhimu za mafuta na gesi ambazo ndio nyenzo pekee za kuendeshea sekta yao ya viwanda na kuwawezesha kuwa juu katika uwezo wa kimaada kuliko wanadamu wote – yatavurugika. Na kwa njia hiyo mabepari wakuu wa Magharibi na wa Kizayuni ambao ndio waendeshaji wa nyuma ya pazia wa madola yote ya Kiistikbari wataporomoka na kupoteza nafasi ya juu waliyonayo ya uwezo wa utwishaji na uburuzaji. [29]
Changamoto na upotokaji wa umma wa Kiislamu

Katika kipindi cha karne kadhaa umma mkubwa wa Kiislamu umekabiliwa na changamoto kadhaa na upotokaji wa kukengeuka njia. Tulijiweka mbali na Uislamu na tukashughulishwa na mambo ambayo Uislamu umetutahadharisha nayo. Katika kipindi hiki kirefu cha historia tulishughulishwa na vita vya ndani na madola ya kitaghuti. Matokeo yake ikawa ni kwamba, kwa muda wa karne kadhaa, baada ya kupita karne za mwanzoni mwa Uislamu, umma ukashindwa kufikia ghaya na lengo kuu ambalo Mtume na Uislamu azizi walitutaka sisi tulifikie. Pamoja na kwamba Mwenyezi Mungu mtukufu amezijaalia nchi za Kiislamu kuwa na utajiri mkubwa wa maliasili za kimaada ambazo zingeweza kuwa wenzo wa kutupatia maendeleo lakini tumekuwa miongoni mwa maeneo ya ulimwengu yaliyobaki nyuma kimaendeleo katika elimu, viwanda na vielezo vingine vingi vya maendeleo. Hivi sivyo ulivyotukadiria Uislamu; hii ni hali iliyotokana na utendaji mbaya, mwenendo na mghafala uliotupata sisi Waislamu: ما اصابك من سيئة فمن نفسك Ubaya uliokufikia unatoka nafsini mwako (Mwenyewe umefanya mambo hata yakakufika hayo). Ni sisi wenyewe, ambao kutokana na mghafala uliotupata kwa muda mrefu, ndio tuliojisababishia hali hii iliyotusibu. [30]
Ni sawa kabisa kwamba udhaifu wa ndani ya jamii ndio unaoandaa mazingira ya adui kushambulia; hata hivyo udhaifu huo unatwishwa hata katika jamii safi na adui kwa kutumia nyenzo na suhula zake. Tusilifahamu kimakosa suala hili. Muelekeo wa harakati ya jamii ya Kiislamu, leo hii unapaswa uwe ni dhidi ya Uistikbari na dhidi ya ubeberu wa dunia ambao kwa masikitiko ni kwamba makucha yake yameelekezwa sehemu zote za Ulimwengu wa Kiislamu. Wana uadui na Uislamu; wana uadui na mwamko wa Waislamu, wana uadui na Iran ya Kiislamu kwa sababu ya kuwa kwake nchi ya Kiislamu. Wanafanya kila wanaloweza ili kuhakikisha harakati ya Kiislamu haibakii hai duniani. Bila ya shaka wa mbele kabisa katika uadui huu ni utawala jabari na mchokozi wa Marekani, na nyuma yake yanafuatia madola mengine yote makubwa na madogo ambayo ambayo yana uadui wa muda mrefu na Uislamu, au yana mikwaruzano nao ya kimaslahi au yanauogopa Uislamu. Yana uadui na Iran ya Kiislamu pia kwa sababu hapa ndipo ilipotokea chemchemu ya mwamko wa Kiislamu; na leo hii wananchi wa mataifa ya Kiislamu popote walipo duniani wanajizatiti na kupiga hatua mbele kutokana na matumaini waliyonayo kwa harakati hii na Mapinduzi haya yaliyopata ushindi. Ikiwa (maadui) wataweza – na Mwenyezi Mungu aepushie mbali – kuushinda Uislamu mahala hapa (Iran) watakuwa wamepata ushindi mkubwa zaidi dhidi ya wimbi la Uislamu katika ulimwengu mzima. Hivi ndivyo ilivyo hakika ya mambo leo hii. [31]

Faslu ya Nne – Majukumu ya mataifa kwa mwamko wa Kiislamu
Ulazima wa kukabiliana na njama za kiutamaduni na kisiasa za Magharibi
Kwa muda wa miaka mingi utamaduni potofu wa Magharibi umekuwa ukifanya uharibifu na ufisadi katika nchi za Kiislamu bila kizuizi wala pingamizi. Kwa bahati mbaya tawala mbovu na tegemezi hazikuweza kuweka ngome imara kama ambavyo ingetarajiwa kwa utawala safi ili kukabiliana na njama za kiutamaduni na kisiasa za maadui; kwa sababu hiyo viongozi wa nchi za Magharibi waliweza kuendesha ubeberu wao wa kisiasa na uporaji wa kiuchumi na kueneza utamaduni wao potofu wa udunishaji na udhalilishaji katika nchi za Kiislamu; na hakuna mtu yeyote aliyewazuia na kuwawekea pingamizi.
Madola ya Kiistikbari yanadhani kwamba kwa kututwisha vita vya miaka minane, kutuwekea mzingiro wa kiuchumi na kipropaganda na kueneza uvumi na tuhuma ulimwenguni yataweza kutudhuru na kutoa pigo dhidi yetu; lakini yameghafilika kwamba Uislamu na mwamko wa Waislamu umetikisa mihimili ya nguvu zao, na kadiri siku zinavyopita mawimbi mazito ya mwamko wa Kiislamu yataitikisa na kuiteteresha zaidi mihimili ya nguvu za mafirauni wa dunia. [32]
Kujihisi kuwa na wajibu kwa upepo wa mwamko
Leo umma wa Kiislamu unakipita kipindi cha tajiriba ya mafanikio haya na machungu mbalimbali uliyopata. Serikali za nchi za Kiislamu na wananchi wa mataifa yenyewe, wote wawili wana wajibu na jukumu kubwa kuhusiana na hali hizo kwani Ulimwengu wa Kiislamu unakipita kipindi nyeti katika historia yake. Kuelewa Waislamu wajibu walionao na kuhisi kuwa hilo ni jukumu lililoko mabegani mwao kunaweza kufuta na kuondoa ukurasa wa masaibu na udhaifu katika kitabu cha historia ya Uislamu, na kwa mara nyingine kufungua ukurasa wa izza na adhama kwa Waislamu na kung’ara Ulimwengu wa Kiislamu kimaada na kimaanawi. Leo ulimwengu wa Magharibi ambao ndio uliokuwa ukishadidisha hali ya udhaifu na kubaki nyuma kimaendeleo nchi za Kiislamu umetingwa na mazonge makubwa na yasiyoweza kutatuka. Ufisadi wa mfumo wa kimaada na wa kibepari umeanza taratibu kupenya na kuonyesha waziwazi taathira yake kwenye mihimili ya ustaarabu huo wa kimaada. Aidha magonjwa sugu yaliyokuwa yamejificha chini ya cheche za marembo ya kuvutia ya viwanda na utajiri yanaanza kujitokeza taratibu na kutoa ujumbe wa kukaribia kuzuka kwa janga. Ulimwengu wa Kiislamu unauhisi upepo wa mwamko wa Kiislamu unaovumia kwenye uso wake uliosawijika kwa machungu na mateso, na ishara zake zinaonekana katika pembe mbalimbali za Ulimwengu wa Kiislamu hususan katika Iran ya izza na jihadi na pia huko Palestina na Lebanon. Mwanga wa matumaini umeziangazia nyoyo za vijana katika kila mahali na kuvunjilia mbali dhana ya kuendelea kuridhia kuburuzwa na kudunishwa na Magharibi. [33]
Leo hii Ulimwengu wa Kiislamu unahitajia zaidi umoja, utangamano na kushikamana na qur'ani kuliko wakati mwengine wowote ule. Kwa upande mmoja uwezo wa Ulimwengu wa Kiislamu wa kuwa na ustawi, nguvu na izza umedhihirika zaidi leo hii kuliko ilivyokuwa huko nyuma, na kurejesha heshima na adhama ya umma wa Kiislamu ndio hamu na takwa la vijana na watu weledi katika ulimwengu mzima wa Kiislamu. Sha'ar za kinafiki za Waistikbari zimechujuka na nia zao chafu dhidi ya umma wa Kiislamu zimeanza kudhihrika polepole. Na kwa upande mwengine manduli wa dunia ambao wanafikiria akilini mwao jinsi ya kujipatia faida kwa kuutawala ulimwengu mzima wameingiwa na khofu na kiwewe kutokana na mwamko na umoja wa umma wa Kiislamu. Wanauhisi mwamko na umoja huo kuwa ni pingamizi na kizuizi kikubwa kwa mawimbi angamizi ya njama zao na kwa hivyo wanafanya kila wawezalo ili kuuzuia usitokee. [34]
Kurejea kwenye usuli na misingi ya Kiislamu
Leo hali katika Ulimwengu wa Kiislamu imebadilika; mwamko wa Kiislamu unahisika katika ulimwengu mzima wa Kiislamu; vuguvugu na harakati adhimu iliyofikia kwenye awamu tofauti inashuhudiwa katika kila pembe ya Ulimwengu wa Kiislamu na kunashuhudiwa pia hamu ya kurejea kwenye usuli na misingi ya Kiislamu ambayo ndiyo chachu ya kupatikana izza, ustawi na maendeleo. Wanafikra, maulamaa na wanasiasa wa Ulimwengu wa Kiislamu wanapaswa kuitia nguvu na kuiimarisha harakati hii. Katika Ulimwengu wa Kiislamu, mtu atakuwa amekosea kama atadhani kwamba harakati ya mwamko wa Kiislamu inayoshuhudiwa kwa vijana ina madhara kwa serikali za nchi za Kiislamu; la hasha. Kwa baraka za mwamko wa Kiislamu, serikali za nchi za Kiislamu zitaweza kujirejeshea izza yao ziliyokuwa zimenyang'anywa na madola ya Kiistikbari.[35]
Nguvu za mataifa katika irada na matumaini yao
Ikiwa dunia imeshuhudia baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran hadi hii leo wananchi wa mataifa ya Waislamu katika kila pembe ya dunia wameanzisha harakati zinazotokana na moyo wa kujiamini zenye lengo la kurejea kwenye utambulisho na utamaduni wa Kiislamu, sababu yake ni kwamba mapambano ya kujitolea mhanga ya taifa la Iran yamebatilisha na kuvunja hila ya kikoloni na kiistikbari ya kuonyesha kwamba mataifa ya Mashariki na mataifa ya Waislamu hayana uwezo wa kuyarudisha nyuma madola yenye nguvu ya Ulaya pamoja na Marekani na vile vile kwa sababu yameonyesha nafasi ya nguvu halisi. Nguvu halisi ni wananchi wenye imani; na mbele ya wananchi kama hao hakuna nguvu zozote za kimaada – hata ziwe kubwa na zilizojizatiti kiasi gani – zitakazoweza kulifanyia taifa zitakavyo. [36]
Ni sawa kwamba kutokana na maendeleo ya vyombo vipya, televisheni, redio, propaganda, fedha na suhula za kiviwanda na nyinginezo, ubeberu na udhibiti wa madola ya Kiistikbari juu ya mataifa na mambo yao ya ndani umezidi kuongezeka siku baada ya siku; lakini utaratibu wa takdiri ya Mwenyezi Mungu ni kwamba mataifa yaamke; na leo hii tunajionea mataifa yanaamka siku baada ya siku; na hii imetokana na matumaini yaliyopata mataifa hayo juu ya mustakbali. Matumaini yanayaamsha mataifa. Hakuna shaka kwamba wenzo muhimu zaidi wa matumaini kwa mataifa katika kipindi cha miaka kumi ya hivi karibuni ulikuwa ni ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran, kuundwa utawala wa wananchi, kuasisiwa utawala wenye sha'ar ya "Si Mashariki wala si Magharibi" na kupiga hatua siasa za muqawama wa kukabiliana na madola ya Kiistikbari.Matukio haya yamewapa matumaini na kuwaamsha walimwengu hususan Waislamu. Hii ilitokana na makadirio na uwezo wake Mola. [37]
Kuendeleza njia ya mwamko hadi kufikia malengo matukufu
Leo umetokea mwamko katika Ulimwengu wa Kiislamu na maadui wa Uislamu wamefedheheka; njia hii inapasa iendelezwe. Njia hii ni njia inayoweza kulifikisha taifa hili kwenye malengo yake halisi matukufu; yaani kwenye ile majimui tukufu ya izza, umaanawi, nguvu, hali bora ya maisha na adhama ya kielimu; yaani yale mambo yanayopendwa na yanayotakiwa na kila taifa. Njia sahihi ambayo ilifuatwa na watoto wa mapinduzi haya na watoto wa Imam (Khomeini), itatufikisha huko tulikokusudia; lakini ina sharti lake nalo ni kusimama imara. Kusimama imara maana yake ni kutopotea njia; kutohadaiwa na madhihirisho ya kimaada; kutotekwa na hawaa na matamanio ya nafsi; kutoyaacha maamrisho, adabu na faradhi za kiakhlaqi na kimaanawi za Uislamu na kutokuwa na roho ya kupenda raha na kupenda anasa . Huo ndio msingi wa kila kitu. [38]
Licha ya njama zote walizounganisha pamoja na kuzitekeleza dhidi ya Uislamu na wimbi la mwamko wa Kiislamu – iwe ni katika bara la Asia au la Afrika – wimbi hili la Kiislamu na mwamko huu wa Kiislamu unazidi kuongezeka siku baada ya siku, na wao hawana uwezo tena wa kufanya chochote. Hii imetokana na baraka za Mapinduzi yenu na mapambano yenu ya kiume, ya kiumini na ya kishujaa. [39]
Kuungana umma wa Kiislamu kwa ajili ya kukabiliana na ukoloni
Suala linalopasa kufikiriwa na kutekelezwa hususan katika zama na wakati huu ni suala la kuuunganisha umma wa Kiislamu na historia yake na pia na mustakbali unaopaswa kuwa nao. Historia na rekodi ya umma wa Kiislamu ni kitu ambacho wakati Ukoloni ulipoingia Asia na Afrika ulifanya hima na bidii kubwa ya kuitia doa na kutaka isahaulike. Udhibiti wa rasilimali za kimaada pamoja na rasilimaliwatu katika nchi za Kiislamu na ushikaji hatamu za maamuzi juu ya mustakbali wa mataifa ya Waislamu – ambalo lilikuwa ndio lengo la wakoloni, iwe ni kwa njia ya moja kwa moja au isiyokuwa ya moja kwa moja kuanzia mwishoni mwa karne ya kumi na nane miladia na kujia huku – ndio ulioua hisia za ghera na shakhsia ya mataifa ya Waislamu na kupelekea kukatika kikamilifu mfungamano baina yao na historia yao ya kujivunia. Na kwa njia hiyo wakauacha utamaduni na maadili yao na kuwa tayari kupokea utamaduni wa Magharibi na mafundisho ya kikoloni. Hila hii ikatumika kuandaa mazingira mwafaka ya kuziweka nchi za Kiislamu chini ya tawala mbovu na za kidikteta na kufuatiwa na wimbi la hujuma za utamaduni wa Kimagharibi na kila aina ya fikra ambazoUkoloni ulihisi kuwa kuna ulazima wa kuzisambaza katika mataifa ya Waislamu ili kuweza kuyaweka mataifa hayo chini ya udhibiti wao wa kisiasa na kiuchumi. Matokeo yake ni kwamba ndani ya kipindi cha miaka mia mbili nchi za Kiislamu zikageuzwa mali ya bure kwa waporaji wa Magharibi kuchota kila watakacho bila kizuizi wala pingamizi yoyote. Walijiwekea mamlaka ya kuzitawala nchi hizo moja kwa moja, kumiliki utajiri wao wa maliasili, kubadilisha hati za maandishi na lugha zao na hata kuihodhi kikamilifu nchi ya Kiislamu kama ilivyotokea Palestina; lakini pia kuyadunisha na kuyadhalilisha matukufu ya Kiislamu n.k. na kwa njia hiyo kuwakosesha Waislamu baraka zote za kuwa na uhuru wa kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni; miongoni mwao ikiwa ni kupata ustawi wa kielimu na kiutamaduni. [40]
Nyoyo za umma wote adhimu wa Kiislamu zinapaswa kukurubiana zaidi siku hadi siku. Nyenzo na silaha za kuzusha hitilafu na mifarakano ambazo adui ameyatwisha mataifa ya Waislamu, zisiathiri anga ya mwamko wa Waislamu ulioko hii leo. Licha ya umbali uliopo baina yao wa kieneo na kijiografia pamoja na tofauti za lugha na rangi, Waislamu wanapaswa kuwa kitu kimoja, kuziunganisha pamoja nyoyo zao, fikra, mitazamo na harakati zao na kuelekea kwenye malengo makuu ya Kiislamu. [41]
Leo wananchi wetu wana jihisi kuwa na adhama ndani ya nafsi zao. Hakuna mtu yeyote katika jamii ya Kiislamu – kama ana imani na Uislamu na Mapinduzi – ambaye anajihisi ni mtu duni ndani ya nafsi yake. Hii ni hali yenye adhama kubwa. Na hivi ndivyo jamii ya Kiislamu inavyopasa kuwa. Maadui wametaka Waislamu wajihisi ndani ya nafsi zao kuwa ni watu duni na dhaifu. Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu na mvuto wake kwa ulimwengu hali hii ya kujihisi duni katika mataifa imepungua kwa kiwango kikubwa. Mataifa yaliyokuwa yamebaki nyuma kimaendeleo na yaliyokuwa yakinyongeshwa, ambayo yalikuwa yakijihisi yako duni yalichangamka kwa kiwango kikubwa na kujihisi kuwa nayo yapo baada ya kupatikana ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu; kwa sababu yaliona ni jinsi gani mapinduzi haya na taifa hili liliweza kulifanya dola lenye nguvu kubwa zaidi duniani liwe si lolote si chochote, likaweza kuzima nguvu zake na kulishinda katika medani ya mpambano na makabiliano. Mataifa makubwa ya dunia, mataifa yaliyobaki nyuma kimaendeleo na pia mataifa ya ulimwengu wa tatu yamejionea hilo na limeyapa hamasa na msisimko. [42]

[01] Ujumbe  kwa mahujaji wa nyumba tukufu ya Mwenyezi Mungu 19/3/1999

[02] Hotuba katika mkutano na wajumbe wa Baraza la Wanazuoni Wataalamu wa kumchagua Kiongozi Mkuu 10/9/2003

[03] Ujumbe kwa kongamano adhimu la Hija 28/1/2004

[04] Hotuba katika mkutano na maafisa wa Wizara ya Mambo ya Nje na wakuu wa ofisi za uwakilishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nje ya nchi 15/8/2004

[05] Ujumbe kwa mahujaji wa nyumba tukufu ya Mwenyezi Mungu 16/6/1991

 [06] Hotuba katika kikao cha pili cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, New York 22/9/1987

 [07] Ujumbe kwa mahujaji wa nyumba tukufu ya Mwenyezi Mungu 7/2/2003

 [08] Hotuba katika mkutano na viongozi na wakuu watendaji wa Mfumo 18/3/2002

 [09] Ujumbe kwa mahujaji wa nyumba tukufu ya Mwenyezi Mungu 19/3/1999

 [10] Ujumbe kwa mahujaji wa nyumba tukufu ya Mwenyezi Mungu 16/6/1991

[11] Hotuba katika haram toharifu ya Imam Ridha (AS) wakati wa kuanza mwaka mpya  21/3/2011

[12] Ibid

[13] Hotuba katika mkutano na viongozi na wakuu watendaji wa Mfumo kwa mnasaba wa mab'ath tukufu ya Mtume Mtukufu (SAW) 2/9/2005

[14] Ujumbe kwa mahujaji wa nyumba tukufu ya Mwenyezi Mungu 9/1/2006

[15] Ujumbe wa Walii Mkuu wa Waislamu kwa mahujaji wa nyumba tukufu ya Mwenyezi Mungu 2010

[16] Hotuba mbele ya hadhara kubwa ya askari wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi kwa mnasaba wa siku ya kuzaliwa Imam Hussein (AS) na Siku ya Jeshi la Walinzi 1/3/1990

 [17] Hotuba katika mkutano na viongozi na wakuu watendaji wa Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu kwa mnasaba wa kuzaliwa Mtume mtukufu (SAW) na Imam Jaafar Sadiq (AS) 1/7/1999

 [18] Hotuba mbele ya hadhara kubwa ya maulamaa, mafudhalaa, wahadhiri na wanafunzi wa chuo cha kidini cha Qum na shule za kidini za Tehran 21/2/1990

[19] Ujumbe kwa mahujaji wa nyumba tukufu ya Mwenyezi Mungu 16/6/1991

[20] Hotuba katika mkutano na viongozi na wakuu watendaji wa Mfumo kwa mnasaba wa mab'ath adhimu Mtume mtukufu (SAW) 2/9/2005

[21] Hotuba katika hafla ya utoaji bai'a Waziri wa Elimu na Malezi, walimu na idadi kadhaa ya wanafunzi wa mkoa wa Tehran 16/6/2001

[22] Hotuba katika mkutano na wakuu wa taasisi ya Mashahidi, familia tukufu za mashahidi, waliopotea vitani, mateka wa vita na majeruhi wa vita wa miji ya Rudbar, Manjil, Saveh, Arak, Mahmoudabad, Amol na Feridun pamoja na familia tukufu za mashahidi wa Wizara ya Usalama 3/1/1989

[23] Ujumbe kwa mahujaji wa nyumba tukufu ya Mwenyezi Mungu 5/7/1989

[24] Hotuba katika mkutano na vijana wa Ahwaz 30/7/2003

[25] Hotuba katika mkutano na kundi la pili la wageni kutoka nje ya nchi walioshiriki kwenye maadhimisho ya mwaka wa pili tangu kuaga dunia Imam Khomeini (MA) 5/6/1991

 [26] Ujumbe kwa mnasaba wa Siku ya Taifa ya kupambana na Uistikbari wa dunia 4/11/1990

 [27] Ujumbe kwa mahujaji wa nyumba tukufu ya Mwenyezi Mungu 18/5/1993

 [28] Ujumbe kwa mahujaji wa nyumba tukufu ya Mwenyezi Mungu 2/3/2001

 [29] Ujumbe kwa kongamano adhimu la Hija 18/1/2005

 [30] Hotuba katika mkutano na viongozi na wakuu watendaji wa Mfumo kwa mnasaba wa tarehe 17 Mfunguo Sita (Rabiul Awwal) 19/5/2003

 [31] Hotuba ya Kiongozi Muadhamu katika mkutano na mashekhe na maulamaa 29/7/1992

 [32] Hotuba katika Arubaini ya Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu (Imam Khomeini) mbele ya hadhara ya wananchi wa mji wa Mashhad na makabila ya jadi ya Khuzestan 13/7/1989

 [33] Ujumbe kwa mahujaji wa nyumba tukufu ya Mwenyezi Mungu 2/3/2001

[34] Ujumbe kwa kongamano adhimu la Hija 18/1/2005

[35] Hotuba katika mkutano na viongozi na wakuu watendaji wa Mfumo kwa mnasaba wa tarehe 17 Mfunguo Sita (Rabiul Awwal) 19/5/2003

[36] Ujumbe kwa mnasaba wa Siku ya Taifa ya kupambana na Uistikbari wa dunia 4/11/1990

[37] Hotuba katika mkutano na wakuu na wafanyakazi wa Wizara za Biashara, Kilimo, Usalama, Posta na Simu, wakuu wa taasisi ya mashahidi, taasisi ya wanyonge na majeruhi wa vita, taasisi ya maskani, wakuu wa itikadi, siasa na makamanda wa kanda za jeshi la polisi nchini kote na idadi kadhaa ya familia tukufu za mashahidi na majeruhi wa vita katika maadhimisho ya siku ya kuzaliwa Imam wa Zama (Imam Mahdi ) (Allah aharakishe kudhihiri kwake) 13/3/1990

[38] Hotuba katika mkutano na hadhara kubwa ya askari wa jeshi la walinzi wa Mapinduzi kwa mnasaba wa kuzaliwa Imam Hussein (AS) na Siku ya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi 9/10/2002

[39] Hotuba mbele ya hadhara kubwa ya wananchi wa mji wa Qum 8/1/2001

[40] Ujumbe kwa mahujaji wa nyumba tukufu ya Mwenyezi Mungu 16/6/1991

[41] Hotuba katika Arubaini ya Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu (Imam Khomeini) mbele ya hadhara ya wananchi wa mji wa Mashhad na makabila ya jadi ya Khuzestan 13/7/1989

[42] Hotuba katika mkutano na wakuu wa taasisi ya Mashahidi, familia tukufu za mashahidi, waliopotea vitani, mateka wa vita na majeruhi wa vita wa miji ya Rudbar, Manjil, Saveh, Arak, Mahmoudabad, Amol na Feridun pamoja na familia tukufu za mashahidi wa Wizara ya Usalama 3/1/1989

 
< Nyuma   Mbele >

^