Skip to content

Habari

Habari
Hifadhi

Risala na Barua

Matini
Hifadhi

Kumbukumbu na Simulizi

Kabla ya Mapinduzi
Baada ya Mapinduzi

Sauti na Taswira

Picha
Sauti
Video
Maelezo ya Sayyid Hassan Nasrullah kuhusu Walii Amr wa Waislamu Chapa
06/06/2011

 Kongamano la "Ubunifu na Ijtihadi kwa Mtazamo wa Ayatullah Khamenei" limefanyika mjini Beirut Lebanon. Kongamano hilo limejadili vipengee mbali mbali vya kielimu na ijtihadi vya Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei. Wasomi na wanafikra kutoka nchi tofauti duniani wameshiriki kwenye kongamano hilo. Mtu wa kwanza kabisa kuzungumza kwenye kongamano hilo alikuwa ni Sayyid Hasan Nasrullah Katibu Mkuu wa chama cha Hizbullah cha Lebanon.

Baada ya Bismillahi na utangulizi mfupi, Katibu Mkuu wa chama cha Hizbullah cha Lebanon amesema:
Kongamano hili ni hatua muhimu na ni kongamano la kwanza la kifikra na kielimu ambalo linazungumzia fikra na shakhsia ya Imam Khamenei (daama dhilluh) ambalo linafanyika nje ya Iran likiwa na vipengee vingi tofauti. Kabla ya yote nachukua fursa hii kuwashukuru hadhirina na washiriki wote wa kongamano hili.

Kumtambua kwangu kwa mara ya kwanza
Kumjua na kuonana kwangu ana kwa ana na Imam Khamenei kwa mara ya kwanza ilikuwa ni mwaka 1986 ambapo niliweza kutambua kwa kiasi kikubwa fikra zake, mitazamo yake, misingi yake ya kifikra na mtazamo wake kuhusu matukio mbali mbali na njia za kuongoza mambo na kuchukua maamuzi pamoja na sifa zake nyingine za kiakhlaki na kimaadili.
Kwa jinsi ninavyomjua na kwa kuzingatia welewa nilionao kuhusu shakhsia yake ninathubutu kusema kwamba, Imam Khamenei ni kiongozi mkubwa katika masuala ya uongozi, taqwa, fikihi na ijtihadi, na ni kiongozi ambaye ana misingi thabiti katika kugalia mambo kwa pande zake zote na kwa kina na umakini mkubwa. Anayajua vizuri matatizo na mahitaji ya watu, anajua suhula na uwezo uliopo na anazijua vizuri njia laiki na selehi za utatuzi wa mambo zinazokubaliana na misingi na usuli unaotakiwa. Ni kwa sababu hiyo ndio maana akawa na mtazamo mpana na wa kina kuhusu matukio yote na ana kipaji kikubwa cha kuamiliana na mambo yote hayo kwa kuangalia pande zake zote kwa uketo wa hali ya juu. Katika mikutano na mazungumzo yake yote na watu utamuona Imam Khamenei ana mtazamo wa kina sana kuhusu vipengee mbali mbali vya maudhui inayohusu mkutano huo na maelezo yake anayotoa kwenye mikutano yote ni ya utaalamu wa hali ya juu.
Imam Khamenei ni shaksia adhimu wa kipekee na watu wengi katika umma huu hawajui mengi kuhusu shakhsia yake. Ni watu wachache tu wanaojua vizuri shakhsia yake. Sisi tunajua ni jinsi gani kiongozi huyu hajapewa haki yake katika umma huu na hata ndani ya Iran kiasi kwamba hajapewa haki yake hata katika kipengee cha shakhsia yake yaani kipengee cha uongozi na siasa. Hivi sasa mnaye kiongozi huu ambaye amezingirwa na maadui huku marafiki wake nao hawampi haki yake vile inavyopasa.
Jukumu letu sisi ni kwamba tumtangaze Imam huyu adhimu kwa umma ili tuweze kufaidika na baraka za uwepo wa kiongozi kama huyu mwanachuoni, fakihi na msomi kwa ajili ya zama hizi na zijazo na kwa ajili ya duniani na Akhera. Hususan kwa vile umma huu unakabiliwa na changamoto nyingi kwa karne nyingi na makumi ya miaka. Jukumu la kongamano hili ni nyeti na ni kubwa sana.
Mkutano wa Madrid
Katika mkutano wa Madrid uliofanyika mwaka 1991 yaani wakati ule milingano ya kimataifa ilipoanza kubadilika, eneo hili na ulimwengu kiujumla ulishuhudia mabadiliko makubwa. Serikali ya Marekani ilitangaza kuwa imedhamiria kumaliza mchakato wa mazungumzo ya mapatano. Watu wengi wakati huo walidhani kuwa tunakaribia kushuhudia kufikiwa mapatano ya Mashariki ya Kati na karibu watu wote waliamini kuwa Wamarekani watawabebesha watu mapatano. Lakini Imam Khamenei yeye alikuwa na mtazamo mwingine kabisa uliotofautiana na mtazamo waliokuwa nao watu wengine. Alisema wazi kwamba mkutano huo hautazaa matunda yoyote ya maana na hakuna mapatano ya aina yoyote yatakayofikiwa. Alisema Wamarekani hawana uwezo wa kubebesha watu mapatano. Hivi sasa na baada ya kupita miaka 20 tangu kufanyika kongamano la Madrid tunazisikia pande zilizoshiriki kwenye mkutano huo na baadhi ya shakhsia waliohudhuria mkutano huo wa Madrid wakikiri kwamba kipindi hiki cha miongo miwili cha tangu kufanyika mkutano huo kilikuwa kibaya kabisa kwao kilichowakatisha tamaa na kuwazubaisha kwa kuwaburuza katika mazungumzo ya mapatano yasiyo na maana yoyote.

Ahadi za Is'haq Rabin
Mwaka 1996, watu wote wanakumbuka hatua kubwa zilizopigwa katika mazungumzo kati ya Israel na Syria na jambo kubwa lililowapa matumaini watu wakati huo ni ahadi za Rabin yaani kutangaza Is'haq Rabin kuwa yuko tayari kurudi nyuma hadi kwenye mstari wa tarehe 4 Juni mwaka 1967 yaani kuondoka kwenye milima ya Golan (ya Syria). Wakati huo katika eneo letu kuliundika mazingira ambayo yaliwafanya watu waamini kwamba sasa bila ya shaka yoyote kutafikiwa makubaliano ya mapatano na matatizo yote yaliyopo yatatatuliwa. Watu walidhani kuwa yatakayobakia ni mambo machache na madogo madogo tu hivyo baadhi ya watu walifikia kutwambia kuwa msijisumbue, mambo yote yameisha.
Watu hao walitutaka tuachane na muqawamah katika hali ambayo muqawamah wakati huo ulikuwa unazidi kuimarika na walitwambia kuwa mambo yote yamemalizika na hakuna haja tena ya kutoa muhanga. Hata baadhi ya watu walifikia kutwambia kuwa pangilieni vingine mambo yenu kwa kuzingatia kuwa makubaliano ya mapatano ni kitu ambacho hakina shaka hata chembe kuwa kitatokea. Hata walitutaka tuangalie upya mambo yetu, si katika muundo wetu wa harakati ya muqawamah tu, bali hata katika jina na muundo wa taasisi zetu na mikakati yetu ya kisiasa.
Lakini wakati watu wakiwa na matumaini makubwa kiasi hicho, Imam Khamenei alitwambia wazi kuwa hadhani kwamba jambo hilo litafikiwa, yaani kufikiwa makubaliano ya mapatano kati y a Israel na Syria na hatimaye kuathiri hali ya Lebanon ni jambo ambalo lisingelitokea. Alitwambia wazi kuwa nakushaurini muendelee na muqawamah na jihadi, si hivyo tu, bali mikakati yenu ya kujiimarisha kwa jihadi na muqawamah itieni nguvu zaidi hadi muweze kupata ushindi wala msidangayike na fikra, mitazamo na madai ya watu hao. Baada ya kurejea nchini Lebanon tulishuhudia wenyewe jinsi Mzayuni mmoja alivyompiga risasi na kumuua Rabin wakati akihutubia, na nafasi yake ikachukuliwa na Shimon Perez.
Wakati huo harakati za HAMAS lakini hasa Jihadul Islami za Palestina zilipata pigo kubwa sana kiasi kwamba baadhi ya watu walidhani kuwa sasa wanamuqawamah wa Palestina hawatakuwa na uwezo tena wa kufanya operesheni zao lakini operesheni za kujitolea kufa shahidi zilizotokea Quds na Tel Aviv zilitoa pigo kubwa kwa utawala wa Kizayuni. Baada ya hapo hali ya kusini mwa Lebanon ikawa mbaya na kupelekea kuitishwa kikao cha Sharm Sheikh (nchni Misri) na viongozi wa nchi nyingi za dunia walikusanyika kwenye kikao hicho ili kuiunga mkono Israel na kulaani kile walichodai ni ugaidi na walitangaza wazi kwamba lengo lao ni kuzilaani harakati za HAMAS, Jihadul Islami na Hizbullah. Viongozi hao katika kikao hicho walikubaliana kuzibana zaidi harakati hizo walizodai eti ni za kigaidi na ni baada ya kikao hicho cha Sharm Sheikh ndipo vilipoanza vita vya "Vishada vyenye hasira" mwezi Aprili 1996 ambapo baada ya vita hivyo, Benjamin Netanyahu alirejea madarakani (huko Israel) na mchakato wa mazungumzo ya amani nao ukakwama na kurudi katika siku yake ya awali kabisa.

Suala la Kukimbia Israel
Imam Khamenei alikuwa akizungumzia asili ya ushindi wa Muqawamah na siku zote alikuwa akisema kwamba hana shaka hata kidogo kuwa ushindi huo utapatikana. Baada ya mwaka 1996, alikuwa akisema kuwa Israel imezama kwenye kinamasi cha tope na kwamba sasa haiwezi kwenda mbele kuiteka na kuikalia tena kwa mabavu Lebanon na wala haiwezi kutoka nchini humo kama ambavyo haiwezi pia kukaa ilipo, hivyo lililobakia ni kwa sisi kuupa fursa wakati na tusubiri kuona nini kitatokea, lakini yote yatategemea hatua zitakazochukuliwa na wanamapambano na Muqawamah. Mwishoni mwa mwaka 1999 kulifanyika uchaguzi wa kumchagua Waziri Mkuu huko Israel na mchuano ulikuwa kati ya Netanyahu na Ehud Barak. Barak aliahidi kuwa (akichaguliwa basi) ataondoa wanajeshi wa Israel (kusini mwa) Lebanon mwezi Julai (mwaka huo) na hali ya Syria na Lebanon ilikuwa katika hali ambayo sisi tungeliweza kufika kwenye tarehe aliyoitangaza Ehud Barak na tusingeliona chochote kikifanywa na Barak kuhusiana na kuondoa wanajeshi wake Lebanon. Ehud Barak naye alifanya juhudi kubwa za kupata dhamana za usalama kutoka kwa viongozi wa Lebanon na Hafidh Asad katika mkabala wa kuondoka wanajeshi wa Israel nchini Lebanon lakini hakufanikiwa katika juhudi zake hizo. Matokeo yake ikawa ni kuandaliwa mazingira ya kumfanya yeye asiondoe wanajeshi wa Israel nchini Lebanon na angelisubiri hadi ufike wakati alioahidi na aseme kuwa alifanya juhudi kubwa za kupata dhamana ya usalama kutoka kwa viongozi wa Lebanon na Syria lakini hakupata, hivyo hawezi kuondoa wanajeshi wa Israel nchini Lebanon.
Hata sisi katika Muqawamah tuliamini hivyo hivyo. Tulipokwenda kuonana na Imam Khamenei na kumuelezea jinsi tunavyoliangalia suala hilo, yeye alikuwa na mtazamo mwingine kabisa. Alitwambia kuwa ushindi wenu huko Lebanon uko karibu sana kabisa na uko karibu sana kiasi kwamba hata nyinyi wenyewe hamuwezi kutarajia. Maelezo yake hayo kwa kweli yalikuwa yanatofautiana kikamilifu na taarifa, uchambuzi na mahesabu ya mezani yaliyokuwepo wakati huo. Wakati huo hata hakukuwa na dalili zozote za kujiandaa Israel kuondoa wanajeshi wake lakini Imam Khamenei alitwambia kuwa tujiweke tayari na tujiandae kwa kwa ajili ya tukio hilo na tuangalie tutaamiliana vipi na hali itakayojitokeza baada ya wanajeshi wa Israel kuondoka Lebanon. Ni kwa sababu hiyo ndio maana sisi hatukushituka wakati tulipoona wanajeshi wa Israel wanaondoka Lebanon (mwaka 2000) kwani tulikuwa tumeshajiandaa kikamilifu kwa ajili ya jambo hilo.
Ayatullah Khamenei anaamini kuwa kitu kinachoshuhudiwa katika mchakato wa mazungumzo ya amani au katika matukio mbali mbali ya Muqawamah au harakati za Wapalestina kinathibitisha uhakika huu kwamba leo hii kumejitokeza kizazi kipya cha wananchi wa Palestina ambao wana imani kubwa zaidi na suala la kurejea kwao Palestina kuliko wakati mwingine wowote.
Vita vya Siku 33
Katika vita vya siku 33 ambavyo kwa hakika vilikuwa ni vita vya kimataifa na maamuzi yake yalichukuliwa kimataifa huku baadhi ya pande za Kiarabu zikiunga mkono vita hivyo ambavyo viliendeshwa na Israel huku jina la vita hivyo likiwa ni kuangamiza Muqawamah Lebanon na nyote mliona jinsi Israel ilivyoendesha vita hivyo kwa ukatili mkubwa na kwa kutumia nguvu zake zote hali ambayo iliwafanya watu iwe vigumu kwao hata kufikiria tu ushindi wa Muqawamah na hali ilikuwa tata kiasi kwamba hata kuzungumzia tu kuokoka na kusalimika wanamapambano wa Lebanon kulionekana kama ni wendawazimu vile kwani uwezo uliokuwa nao Muqawamah ulijulikana na Lebanon nayo kama nchi kwa kweli ni nchi ndogo na ilionekana ni vigumu sana kwake kuweza kuhimili mikiki ya vita hivyo vilivyopangwa na kuendeshwa kimataifa na ilikuwa dunia nzima imekaa dhidi yake na kuendesha vita vya kinyama kabisa kama vile.
Lakini wakati hali ilipokuwa iko hivyo, mimi nilipata ujumbe wa maneno wa Imam Khamenei nikiwa kwenye viunga vya kusini mwa Beirut na wakati huo majengo ya eneo hilo yalikuwa yanaporomoka kutokana na kushambuliwa vikali na Israel. Ujumbe huo ulikuwa mrefu lakini mimi nitagusia baadhi tu ya yale yaliyokuwemo kwenye ujumbe huo. Imam Khamenei alisema katika ujumbe huo kwamba ndugu zangu wapendwa, vita hivi vinafanana na vita vya Khandaq (Vita vya Ahzab) ambayo Makureish na Mayahudi wa Madina na makabila mengine yote yaliungana pamoja na kujumuisha nguvu zao zote ili kwenda kummaliza Bwana Mtume Muhammad SAW na kutaka kuuangamiza Uislamu na kundi dogo la waumini. Vita hivi vinafanana na vita hivyo na hali itakuwa nguvu sana lakini tawakalini kwa Allah na mtegemeeni Mwenyezi Mungu na mimi ninakuhakikishieni kuwa bila ya shaka yoyote nyinyi ndio mtakaoshinda bali napenda kukuhakikishieni jambo jengine nalo ni kwamba baada ya kumalizika vita hivi na nyinyi kupata ushindi, mtabadilika na kuwa nguvu ambayo hakuna nguvu yoyote itakayoweza kusimama dhidi yenu.
Kwa kweli katika wakati huo na hasa katika zile siku za mwanzo za vita, ni nani angeliweza kutabiri hali itakayotokea na kuwa na yakini kiasi hiki cha ushindi wa Muqawamah?

Mtazamo wa Ayatullah Khamenei kuhusu Matukio ya baada ya Septemba 11
Baada ya matukio ya Septemba 11 tuliona jinsi gani watu wote duniani walivyotetereka ambapo watu wengi walitabiri kuwa eneo letu limeingia kwenye kipindi cha Umarekani na litadhibitiwa moja kwa moja na Marekani. Walitabiri kuwa udhibiti huo utadumu (kwa uchache) karne moja au mbili katika eneo hili huku wengine wakifananisha vita hivyo vipya vilivyoanzishwa na Marekani katika eneo hili na Vita vya Msalaba. Mimi nilikwenda Iran na nikapata fursa ya kuonana na Imam Khamenei na nikamuuliza mtazamo wake kuhusu hali hiyo. Lakini yeye alisema kitu kingine kabisa tofauti na ule uvumi uliokuwa umeenea katika eneo. Nakumbuka wakati huo serikali nyingi na makundi ya kisiasa ya eneo yalikuwa yanajadili hali na mustakbali wao chini ya kivuli dha dhana ya udhibiti wa Marekani katika eneo na hata baadhi ya viongozi nchini Iran walikuwa wanakuja na kusema kwamba matukio mapya yatakayotokea yatakuwa hivyo hivyo na inabidi tufanye mazungumzo ya mapatano na Marekani. Lakini kutokana na mtazamo wake wa kiistratijia, Imam Khamenei aliniambia kwamba usiwe na wasiwasi wowote kwani Marekani imefikia ukomo wake na kuanzia sasa hakuna tutakachoshuhudia isipokuwa kuporomoka Marekani. Alisema kuwa hivi sasa mkondo wa kuporomoka Marekani umeanza huko Afghanistan na Iraq. Alisema, Wamarekani wanatafuta jabali (la kujiimarishia) lakini huu ni mwanzo wa kumalizika Marekani na malengo yake katika eneo na nyinyi mnapaswa kupangilia mambo yenu kwa kuzingatia uhakika huo.
Alisema kuwa, wakati Marekani inashindwa kulinda manufaa yake katika eneo kupitia tawala za hivi sasa za eneo na licha ya kuwa na majeshi na manuwari zake nyingi kwenye eneo hili kiasi kwamba hata inalazimika kuleta manuwari zake zote katika eneo hili; huu ni ushahidi tosha kwamba Marekani imedhoofika na jambo hilo linaonesha wazi kuwa watawala wa nchi za eneo hili hawawajui wananchi wao ambao wamefungamana na utamaduni wa jihadi na muqawamah hivyo alisema mambo yanayoendelea hivi sasa yasitutie wasiwasi bali tunatakiwa kuwa na matumaini ya mustakbali mzuri.
Ninathubutu kusema kuwa katika kipindi cha miaka 10 iliyopita, umma wetu umekabiliwa na vita vigumu sana katika historia yake huku Marekani na waitifaki wake wakitumia uwezo wao wote ili kujaribu kulidhibiti eneo letu na kujaribu kuiangusha mifumo na tawala za muqawamah na zilizosimama kidete mbele ya maadui. Imam Khamenei naye amekuwa akiongoza vita vigumu mno katika kipindi chote hiki jambo ambalo linahitajia hekima, akili, ushujaa na fikra na umakini wa hali ya juu sana, ambapo hivi sasa kuna masuala mengi sana yanayohusiana na vita hivyo ambayo hatuwezi kuyasema.

Kuangamia Israel Kumekaribia
Imam Khamenei anaamini kuwa Israel inaelekea kutoweka na anaamini kwamba kuangamia utawala huo hakuko mbali bali anaami kumekaribia. Anaamini kuwa mwenendo huu wa mazungumzo ya mapatano hautafika popote na kwamba haya mafanikio yaliyopatikana hadi hivi sasa huko Palestina na katika eneo iwe ni katika mchakato wa mazungumzo au matukio mengine ya muqawamah na harakati za Wapalestina yanaonyesha uhakika kwamba leo hii kumejitokeza kizazi kipya huko Palestina ambacho kina imani kubwa zaidi na suala la kurejea kwao Palestina kuliko wakati mwingine wowote.
Sisi tunaweza kuyadiriki na kuyaelewa vizuri anayoyasema Imam Khamenei kuhusu Israel kwa kuangalia hali ya Marekani na mafanikio ya muqawamah na uzoefu wa vita vya siku 33 vya Lebanon na vile vya siku 22 vya Ghaza. Tukikusanya yote hayo tutaona kuwa kuangamia kwa Israel na mwisho wa utawala huo Inshaalh uko karibu sana na huu ni mtazamo sahihi uliosimama juu ya misingi ya kuelewa vizuri kiongozi huyu shujaa matukio yanayoendelea duniani.
Mwisho nigusie harakati ya vijana wa Kipalestina katika eneo la mpakani la milima ya Golan ya Syria inayokaliwa kwa mabavu na Israel. Harakati na msimamo thabiti wa vijana hao katika kupambana na adui unatoa ujumbe wa wazi wa kuwa umma wetu sasa umeamua na vijana hawa kwa mara nyingine wamefanikiwa kufichua sura halisi ya serikali ya Marekani ambayo inajaribu kuteka nyara mapinduzi ya wananchi katika nchi za Kiarabu. Matukio ya hivi karibuni ya huko Golan yamethibitisha kwa mara nyingine kuwa, Marekani inaiunga mkono Israel kwa hali yoyote ile. Damu za vijana hao wa Kipalestina wasio na hatia, kwa mara nyingine imemwagwa na Israel huko Golan na kwa mara nyingine umefichuka ukweli wa madai ya uongo ya Marekani ya eti inatetea demokrasia na haki za binaadamu. Jambo hili linaonesha mwamko wa kisiasa na kihistoria ambao misingi yake iliwekwa na Imam Khomeini (quddisa sirruh) na baadaye kuendelezwa na kuimarishwa na Imam Khamenei.

 

 

 
Mbele >

^