Skip to content

Habari

Habari
Hifadhi

Risala na Barua

Matini
Hifadhi

Kumbukumbu na Simulizi

Kabla ya Mapinduzi
Baada ya Mapinduzi

Sauti na Taswira

Picha
Sauti
Video
Ujumbe wa Hija, ulikuwa ni ubunifu wa Imam Khomeini (quddisa sirruh) Chapa
05/11/2011
Mahojiano na Ayatullah Taskhiri, Katibu Mkuu wa Taasisi ya Kimataifa ya Kukurubisha Pamoja Madhehebu ya Kiislamu kuhusu risala na ujumbe mbali mbali wa Hija uliokuwa ukitolewa na Imam Khomeini (quddisa sirruh), mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pamoja na risala kama hizo za Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei.
Baada ya kusita kwa muda mrefu na baada ya kuanza kutumwa tena mahujaji wa Iran nchini Saudi Arabia, viongozi wa nchi mbili yaani Iran na Saudia waliamua kuwa na mazungumzo na uratibu wa pamoja kuhusu utumaji wa mahujaji hao. Ayatullah Taskhiri alikuwa mmoja wa wajumbe wa tume ya Iran ya mazungumzo na viongozi wa Saudi Arabia. Mahojiano haya yana taarifa mpya na za kuvutia kuhusiana na kazi na kushiriki Katibu Mkuu wa Taasisi ya Kimataifa la Kukurubisha Pamoja Madhehebu ya Kiislamu katika mikutano mbali na jambo hilo linayafanya (mahojiano haya) yazidi kuwa na mvuto na umuhimu mkubwa. Ayatullah Taskhiri ni Mshauri Mkuu wa Masuala ya Kimataifa wa Bi’itha ya Hija ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, vile vile ni mjumbe katika Kamati Kuu ya Mahusiano ya Maulamaa wa Waislamu katika mji mtakatifu wa Makkah kama ambavyo pia ni Katibu Mkuu wa Taasisi ya Kimataifa la Kukurubisha Pamoja Madhehebu ya Kiislamu (kama tulivyosema) na amefanya juhudi kubwa za kuleta umoja na mshikamano katika umma wa Kiislamu.
Swali: Katika kila msimu wa Hija kila mwaka tumekuwa tukiona Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu akitoa ujumbe maalumu kwa ajili ya kongamano hilo kubwa linalowakusanya Waislamu kutoka kona zote za dunia, risala na ujumbe ambao mara zote unakuwa na nukta muhimu na nyeti kwa ajili ya Waislamu duniani. Kwa mtazamo wako, falsafa ya kutolewa ujumbe huo kila mwaka ni nini?
Jawabu: Inabidi nitaje nukta kadhaa ili kujibu swali hili. Kwanza ibada yenyewe ya Hija ambayo chimbuko lake ni sheria za Kiislamu, ina malengo mengi makubwa. Yamkini lengo kubwa zaidi la Hija ni lile tunalolipata katika Qur’ani Tukufu yaani jinsi Waislamu wanavyounganishwa kikamilifu na sira na matendo matukufu ya Mitume waliotangulia. Yaani kama tunavyoona katika Suratul Baqarah, mwanzo wa kuumbwa mwanaadamu, kusujudiwa kwake na malaika, mtihani na uzoefu alioupata Adam alipokuweko peponi na masuala ya baada ya hapo, kuja kwake Adam ardhini na kutumia uzoefu alioupata peponi yaani kuasi na baadaye kutubu na kurejea kwa Mwenyezi Mungu na kutii kikamilifu maamrisho ya Mwenyezi Mungu. Katika kubainisha kila moja kati ya marhala na awamu hizo, Qur’ani Tukufu inatumia maneno ya Kiarabu kama “idh” na “waidh” na kuelezea njia walizopitia Manabii wote hadi kufikia kwa Nabii Ibrahim AS. Mwenyezi Mungu anasema:
“وَ اِذِ ابتَلَی اِبراهیمَ رَبُّهُ بِكَلِماتٍ فَاَتَمَّهُنَّ قَالَ اِنِّی جاعِلُكَ لِلنَّاسِ اِماماً قالَ وَ مِن ذُرِّیَّتی قَالَ لایَنالُ عَهدِی الظَّالِمین”
Maana yake ni kuwa: “Na (kumbukeni) Mola wake Mlezi alipomjaribu Ibrahim kwa matamko fulani na akayatimiza. (Mwenyezi Mungu) Akamwambia: Hakika Mimi nitakufanya uwe Imam wa watu. (Ibrahim) akasema: Je, na katika vizazi vyangu pia? (Yaani utawafanya kuwa Maimam). (Mwenyezi Mungu) akasema: (Ndiyo, lakini) ahadi Yangu haiwafikii madhalimu.”
Ni baada ya hapo ndipo lilipokuja suala la Hija ambapo Mwenyezi Mungu anasema:
وَإِذْ جَعَلْنَا الْبَيْتَ مَثَابَةً لِّلنَّاسِ وَأَمْناً وَاتَّخِذُواْ مِن مَّقَامِ إِبْرَاهِيمَ مُصَلًّى وَعَهِدْنَا إِلَى إِبْرَاهِيمَ وَإِسْمَاعِيلَ أَن طَهِّرَا بَيْتِيَ لِلطَّائِفِينَ وَالْعَاكِفِينَ وَالرُّكَّعِ السُّجُودِ
Maana yake ni kuwa: “Na kumbukeni tulipoifanya ile Nyumba (ya Alkaaba) iwe pahala pa kukusanyikia watu na pahala pa amani. Na alipokuwa akisimama Ibrahim pafanyeni pawe pa kusalia. Na tuliagana na Ibrahim na Ismail: Itakaseni Nyumba yangu kwa ajili ya wanaoizunguka kwa kut'ufu na wanaojitenga huko kwa ibada, na wanaoinama na kusujudu.”
Yaani Mwenyezi Mungu anaitaja Hija katika kitovu cha aya zinazozungumzia njia walizopitia Mitume watukufu huku Nabii Ibrahim AS ambaye ni Shaikhul Ambiyaa akiwa takriban ndiye muainishaji wa njia ya Hija na malengo yake ambapo moja ya malengo makuu ya Hija ni kuunganishwa umma huu na njia ya Manabii njia ambayo ndiyo inayotakiwa na Mwenyezi Mungu kwa ajili ya mwanaadamu, naam, njia ya usafi, ta’a na utiifu kwa Mwenyezi Mungu, kujiweka mbali na maasi na kujenga jamii bora inayomwabudu Mwenyezi Mungu tu.
Tab’an lengo la pili limo ndani ya njia hiyo hiyo nalo ni kuunda utu wa mwanaadamu, kumrejesha mwanaadamu kwenye dhati na maumbile yake, naam, kumrejesha kwenye njia ya kimaumbile ya kujisalimisha kikamilifu kwa Mwenyezi Mungu. Huku kujenga utu wa mwanaadamu kunaonekana wazi katika amali zote za Hija. Hivyo kuna malengo mengi makubwa katika Hija na moja ni hili la kujibari na kujiweka mbali na washirikina. Huku kujibari na washirikina kunaonekana wazi pia ndani ya dhati ya Nabii Ibrahim mwenyewe. Lengo jingine la Hija ni kuleta umoja na mshikamano katika umma wa Kiislamu. Waislamu wakiwa katika vazi moja; kwa sauti moja; kwa nia moja; wanatufu Alkaaba, wanampiga mawe shetani, wanasimama pamoja kwenye sehemu moja (Arafa), wanatoa takbiri za pamoja na kufanya ibada za namna moja; wote wanakusanyika pamoja katika eneo moja dogo na hata mavazi ambayo huwabadilisha sura zao huyavua wanapokuwa katika sehemu hiyo na kuvaa vazi moja linalowafananisha wote. Mambo yote haya yanaonesha umoja wa watu na na mshikamano wa umma wa Kiislamu. Malengo haya yanaonekana wazi zaidi katika amali ya Hija. Hivyo katika kila ujumbe alioutoa Imam Khomeni (Rahmatullahi Alayh) kwa ajili ya mahujaji na kila ujumbe unaotolewa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran (Hafidhahullah) kila moja ya ujumbe huo unalenga kwenye kufanikisha na kutilia mkazo malengo hayo matukufu ya Hija.
Amma falsafa ya kuweko ujumbe huo kila mwaka – kama ulivyoniuliza – yaani kwamba ni kwa nini Jamhuri ya Kiislamu na uongozi wake unalipa umuhimu mkubwa suala hilo ni kuwa, kuifufua Hija ni sawa na kuufufua umma mzima wa Kiislamu. Kuunganishwa ujumbe huo wa Hija kwa ajili ya kutoa sura halisi ya Hija maana yake ni kuunganika harakati ya umma wa Kiislamu. Vilevile kuna Hadithi inasema: "الحجُّ عَلَمُ الاسلام" yaani “Hija ni bendera ya Uislamu.” Nini maana ya bendera ya Uislamu? Katika mantiki ya vita ni kwamba kila wakati bendera ya jeshi inapokuwa imesimama na kupeperuka juu ya mlingoti, maana yake ni kwamba jeshi hilo liko hai na linaendelea na mapambano. Hivyo kuihuisha na kuiirejeshea uhai wake Hija ni moja ya malengo ya risala za Hija zinazotolewa na Jamhuri ya Kiislamu kwa ajili ya kufanikisha mwamko wa Kiislamu. Ni kwa sababu hiyo ndio maana tunaona katika ujumbe mbali mbali aliokuwa anautoa Imam Khomeini (quddisa sirruh) na risala za kila mwaka za Hija zinazoendelea kutolewa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, mara zote ndani yake kunasisitiziwa suala hilo na kwa hivi sasa ujumbe huo unatolewa ukiwa ni kama manifesto, hati na ilani ya kutangaza sera. Yaani hutolewa ukiwa ni muongozo mkuu wa kuongozea njia. Hakuna tofauti yoyote baina ya wakati wa Imam Khomeini (quddisa sirruh) na hivi sasa.
Swali: Inavyoonekana ni kuwa, hakujafanyika juhudi za kutosha za kuufikisha vile inavyotakiwa risala hizo mbali mbali zinazotolewa katika misimu ya Hija. Sijui wewe unasemaje?
Jawabu: Naam, ni jambo la kusikitisha kusema kuwa tumeshindwa kujua uadhama na utukufu wa ujumbe huo na si sisi binafsi tu, bali hata katika kuwaelewesha wengine pia tumeshindwa. Vyombo vya habari, mahujaji na… wanafanya juhudi mbali mbali kufikisha kwa walimwengu na hasa Waislamu yaliyomo kwenye ujumbe na risala hizo lakini jambo hilo halifanyiki kwa kiwango kinacholingana na uzito uliomo ndani ya ujumbe na risala hizo. Inabidi vyombo vyote vya habari, vituo vyote vya utamaduni, uwezo na suhula zote za kufanyia tablighi na kila chombo tulicho nacho, kitumike vilivyo katika siku za msimu huu ili kuufikisha ujumbe huo wa Hija hadi maeneo ya mbali kabisa. Inabidi tutumie nguvu zetu zote kuufikisha vizuri ujumbe huo. Naam, inabidi kazi kubwa zaidi ifanyike katika jambo hilo.
Swali: Je, viongozi wa nchi nyinginezo duniani nao wanatoa ujumbe kama huo wakati msimu wa Hija?
Jawabu: Hapana, si kwa sura hii. Rais wa Saudi Arabia huwa anatoa ujumbe mmoja tu kwa ajili ya kufanyia propaganda. Kimsingi kutoa ujumbe kwa mahujaji ulikuwa ni ubunifu wa Imam (Khomeini – Quddisa Sirruh).
Swali: Je, tangu mwanzo ujumbe huo ulikuwa unatolewa katika ule wakati wa kutangaza kujibari na kujiweka mbali na washirikina?
Jawabu: Hapana, awali ujumbe huo haukuwa kwa ajili ya siku ya kutangaza kujibari na washirikina, bali Imam alikuwa akiainisha wakati wake na kwa kweli ulikuwa unasomwa katika kipindi chote cha Hija. Lakini baada ya kushambuliwa mahujaji wa Iran (na watawala wa Saudia) jambo ambalo lilipelekea kupita miaka kadhaa bila ya kutumwa mahujaji wa Iran, kulifikiwa makubaliano maalumu baina ya pande mbili na mimi nilikuwa mmoja wa wajumbe walioshiriki kwenye mazungumzo yaliyofanikisha makubaliano hayo. Kwa mujibu wa makubaliano hayo, pande mbili ziliafikiana kuwa, mikusanyiko ya kujibari na kutangaza kujiweka mbali na washirikina isifanyike tena mjini Makkah, bali mahujaji wakusanyike siku ile ile ya Arafa, yaani mwezi tisa Dhulhijjah katika jangwa la Arafa, mahema ya mahujaji wa Kiirani yote yaunganishwe pamoja na mahujaji wakusanyike kwa wingi kwenye mahema hayo na kusoma ujumbe huo wa Hija.
Swali: Je, makubaliano ya kusomwa dua ya “Kumeil” katika mji mtakatifu wa Madina nayo yalifikiwa wakati huo huo?
Jawabu: Hapana, suala la kusomwa dua ya “Kumeil” katika mji wa Madina liliafikiwa katika vikao vingine. Makubaliano hayo yalikuwa mengine baada ya kutokea mivutano na misuguano mingi.
Swali: Sisi tunaamini kwamba ujumbe huo wa Hija unatolewa kwa ajili ya Waislamu wote duniani. Hadi hivi sasa ujumbe huo umekuwa na taathira gani za kivitendo kwa Waislamu duniani?
Jawabu: Kwanza kabisa, mahujaji wengi sana wa mataifa tofauti hushirikiana na mahujaji wa Kiirani katika ibada hiyo ya kutangaza kujibari na kujiweka mbali na washirikina. Pili ujumbe huo hufasiriwa katika zaidi ya lugha 10 tofauti duniani na kuenezwa kwa watu wa mataifa tofauti katika msimu wa Hija ukiwa ni ujumbe wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa mahujaji wote. Katika baadhi ya vyombo vyetu vya habari pia, ujumbe huo hutangazwa kwa lugha tofauti na kwa kweli risala hiyo imekuwa na taathira nzuri katika nyoyo za Waislamu na ushahidi wa jambo hilo ni kuwa, vyombo vyote vya kiistikbari na kibeberu duniani pamoja na taasisi za serikali za Kiarabu na nchi nyingine zisizopenda risala hiyo isiwafikie Waislamu, hujaribu sana kuuzima ujumbe huo. Kuna wakati ujumbe mmoja wa Hija ulichapishwa katika moja ya magazeti ya nchini Uingereza, lakini baada ya kuchapishwa risala hiyo, Uzayuni wote wa kimataifa ulisimama vikali kulishambulia gazeti hilo na kulisababishia matatizo na mashaka mengi.
Swali: Tukio hilo lilitokea mwaka gani?

Jawabu: Kwa kweli sikumbuki lakini ilikuwa ni katika muongo wa 70.
Wazayuni wanazuia kuenezwa risala hiyo. Utawala wa Saudia nao si tu hausaidii kuusambaza ujumbe huo lakini katika baadhi ya miaka hata unazuia usitolewe. Baadhi ya wakati watu wengi wanatiwa mbaroni ili kuzuia kusambaa risala hiyo. Tab’an katika miaka ya hivi karibuni utiaji mbaroni wa aina hiyo umepungua. Lakini sehemu zote wanajaribu kuzima sauti ya ujumbe huo. Baadhi ya wakati sisi hujaribu kuusambaza ujumbe huo kupitia magazeti ya kigeni, fedha za kuchapishia ujumbe huo nazo tunatoa, lakini mwisho tunaona hauchapishwi. Magazeti mengi sana hayaruhusu au hayaruhusiwi kuchapisha risala hiyo ya Hija.
Swali: Kuhusu nchi za Ulaya je?
Jawabu: Si nchi za Ulaya tu, bali hata katika nchi za Kiislamu, aslan hawaruhusu kuchapishwa na kusambazwa ujumbe huo, tab’an kama nilivyosema, sisi pia tumezembea kiasi fulani.
Swali: Ujumbe huo huwa wa aina gani? Je, huwa ni ujumbe wa kisiasa kutoka kwa mtu wa serikali kwa ajili ya watu?
Jawabu: Hapana, bali huwa ni ujumbe wa Walii kwa umma wake. Huwa ni ujumbe wa Kiongozi wa kidini na Marja’a wa kidini ambaye pia ni Kiongozi wa Mapinduzi kwa ajili ya umma mzima wa Kiislamu. Wakati wa kusomwa ujumbe huo huko Makkah, mahujaji ambao huwa ni wawakilishi wa umma mzima wa Kiislamu huwa wamekusanyika hapo. Kwa kweli hiyo huwa ni kama vile wawakilishi wa umma mzima wa Kiislamu wamekusanyika hapo kwa ajili ya kutafuta radhi za Mwenyezi Mungu na kujikurubisha Kwake. Watu wote sehemu hiyo hufanya mambo yao kwa kaulimbiu moja, wote hao huongozwa kwenye nara na kaulimbiu moja, naam hupata malezi ya kivitendo katika sehemu hiyo. Hujaji wakati wote anapaswa kuchunga macho yake. Anapaswa kuchunga harakati ya mkono na mguu wake. Anapaswa kuchungua mdomo na ulimi wake. Kitendo chenyewe cha kuvaa Ihram pekee huwa ni mlezi mwema wa mahujaji.
Ujumbe wa Kiongozi Muadhamu nao hutolewa katika malengo hayo hayo. Ni kwa sababu hiyo ndio maana mimi nimefanyia utafiti wa maana na mafuhumu iliyojikita katika risala mbali mbali za Hija alizotoa Kiongozi Muadhamu katika miaka ya hivi karibuni, kama unataka niko tayari kutoa ufafanuzi juu yake.
- Tafadhal.
Kama mtu utakaa na kuchunguza kwa kina ujumbe mbali mbali alioutoa Kiongozi Muadhamu katika miaka ya hivi karibuni utaona kuwa jambo la kwanza kabisa linalosisitizwa ndani yake ni nafasi muhimu ya Hija katika kujenga umma wa Kiislamu. Ujumbe unaotolewa kila mwaka na Kiongozi Muadhamu unafuatilia jambo hilo katika Hija. Mfano mmoja ni nafasi ya Hija katika kuondoa udhaifu wa umma wa Kiislamu. Katika baadhi ya ujumbe huo, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu anasema kwamba sisi Waislamu tuna udhaifu wetu wa ndani na baadhi ya udhaifu ni kutoka nje. Utaona risala zake za Hija na maana zake zimejaa sisitizo juu ya taqwa, kuisafisha nafsi na kujiweka mbali na mghafala na huu ndio udhaifu uliopo.
Nukta nyingine ni kubainisha nafasi ya Hija ya kwamba Hija ni bendera ya Uislamu. Katika moja ya ujumbe wake, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aliashiria kwamba Hija ni dhihirisho la harakati ya umma na ni ubainisho wa nafasi ya Uislamu wa kisiasa.
Kama tutaiangalia misingi ya Hija tutaona kwamba moja ya nguzo zake ni kutufu Alkaaba. Maana ya jambo hilo ni kitu gani, maana yake ni kwamba umma mzima wa Kiislamu unapaswa kujikusanya pamoja na kushikamana kwenye wigo wa sheria za Kiislamu na uongofu wa Mwenyezi Mungu Mtukufu. Nguzo nyingine ya Hija ni kumpiga mawe shetani, yaani kukusanyika pamoja umma wa Kiislamu na kuzipiga mawe nembo na alama za mataghuti na watu waovu.
Ujumbe mwengine muhimu uliomo katika Hija ni kuuhamasisha na kuushajiisha umma kusimama imara mbele ya changamoto zinazoikabili dini tukufu ya Kiislamu. Suala hili pia limesisitizwa katika ujumbe mbali mbali wa hivi karibuni wa Hija alioutoa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu. Kiujumla ni kwamba mambo ya kwanza kabisa muhimu yanayoashiriwa na risala hizo mbali mbali ni nafasi ya Hija katika kutia nguvu njia ya kuweza kufanikisha ustaarabu wa umma wa Kiislamu.
Suala la pili ni nafasi ya Hija katika kulea maadili bora ya kila mtu katika jamii. Jambo hili nalo linashuhudiwa katika risala hizo tofauti. Kuanzia mwanzo wa risala hizo za Hija hadi mwisho, utaona lazima kumeashiriwa suala la malezi mazuri na uharura wa kustafidi kwa njia iliyo bora na fursa nzuri ya kuweko katika maeneo matakatifu kunakofanyika amali tukufu ya Hija.
Suala la tatu katika ujumbe huo mbali mbali wa Hija unaotolewa kila mwaka na Ayatullah Udhma Khamenei ni kuonyesha uadhama na utukufu wa Uislamu na risala zake, ikiwa ni pamoja na kuashiria utukufu wa njia za Uislamu katika utatuzi wa matatizo yanayomkabili mwanaadamu leo hii.
Suala jingine ni kusisitiza juu ya kadhia ya umoja na mshikamano katika safu za Waislamu jambo ambalo linashuhudiwa zaidi katika risala na ujumbe mbali mbali wa Hija wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ambaye amekuwa akisisitiza kuwa dhihirisho na njia bora kabisa ya kufanikisha umoja huo wa Kiislamu ni kuweko mwamko wa Kiislamu. Mwamko wa Kiislamu uliojaa kwenye risala hizo za Hija ni moja ya matukio muhimu na jamali sana tunayoyashuhudia hivi sasa. Risala hizo zimekuwa zikijaribu sana kuutia nguvu mwamko huo, kuukuza na kuustawisha kadiri inavyowezekana. Katika ujumbe huo tofauti kumekuwa kukiashiriwa pia mambo yanayoonyesha kuweko kivitendo umoja huo ikiwa ni pamoja na vile kuweko nguo za namna moja, njia na kaulimbiu pamoja na misimamo ya pamoja, eneo moja la kufanyia tawafu na… na hata katika ujumbe wake wa mwaka huu kwa mahujaji, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria kuwa Alkaaba ni nembo ya neno la tawhidi na ni dira na muongozo wa harakati kuelekea kwenye umoja wa umma wa Kiislamu.
Vile vile risala hizo zimekuwa zikibainisha uwezo mkubwa ilio nao umma wa Kiislamu, uwezo wa kimaada, kimaanawi, kijiografia na kiutamaduni yaani huwa zinatoa ukumbusho kuhusu wajibu wa kutumiwa vizuri suhula na uwezo huo adhimu wa umma wa Kiislamu ambao kwa bahati mbaya unatumiwa vibaya kuwanufaisha maadui.
Moja ya jambo jingine kubwa ambalo limekuwa likionekana wazi katika ujumbe huo mbali mbali wa Hija wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ni kufichua kwa uwazi njama za mabeberu wa dunia. Risala zote hizo zimekuwa zikionyesha wazi njama za kishetani za waistikbari wa dunia za kutaka kuuangamiza umma wa Kiislamu na zimekuwa zikibainisha pia sababu za kuweko jinai hizo za maadui. Risala hizo zimekuwa zikibainisha kwa uwazi jinai hizo kuanzia zile zinazofanyika hivi sasa na vile vile masuala na taarifa za mambo yanayofanyika katika nchi za Kiislamu kuanzia suala la kueneza upotofu, uadui na fitna za kimadhehebu na kikabila hadi kwenye kueneza ufisadi na kufanya mauaji makubwa pamoja na kuendesha propaganda chafu dhidi ya umma wa Kiislamu. Vitisho vyote hivyo ambavyo vimeongezeka zaidi baada ya matukio ya Septemba 11 ya nchini Marekani, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu anayazungumzia katika risala na ujumbe wake mbali mbali wa Hija kila mwaka. Kutokana na kwamba njama za mabeberu wa dunia za kutaka kuukalia kwa mabavu ulimwengu wa Kiislamu zimezimwa kutokana na mwamko wa Kiislamu, hivi sasa maadui wameshadidisha njama za kutaka kuugawa vipande vipande umma wa Kiislamu kupitia kueneza vitendo viovu na vichafu na ufisadi wa kimaadili. Ni kwa sabu hiyo ndio maana tunaona risala mbali mbali za Kiongozi Muadhamu zikiutaja uistikbari kuwa ni adui wa wanyonge, ni adui wa haki za binaadamu, ni muungaji mkono wa ugaidi na ni muenezaji wa unafiki na ubeberu duniani.
Tab’an jambo jingine muhimu linaloonekana katika risala hizo za Hija za Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ni kufichua sura halisi ya tawala za vibaraka wa mabeberu katika ulimwengu wa Kiislamu, tawala ambazo zimekuwa zikifanya juhudi kubwa kwa ajili ya kujaribu kufanikisha malengo ya mabeberu na kuitoa Hija katika sura na dhati yake tukufu. Jambo hilo pia limekuwa likisisitizwa mara kwa mara katika ujumbe mbali mbali wa Hija unaotolewa na Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei.
Nukta nyingine muhimu inayoonekana kwenye risala hizo za Hija ni kuionyesha Jamhuri ya Kiislamu kuwa ni kigezo chenye mafanikio makubwa cha muqawama na mapambano dhidi ya ubeberu wa dunia na ni nembo na kigezo cha kutekeleza mafundisho ya Uislamu katika maisha ya kila siku ya mwanaadamu na kwamba Jamhuri ya Kiislamu ni mlinganiaji mkubwa wa umoja na mshikamano katika safu za Waislamu. Ujumbe huo tofauti umekuwa ukionyesha kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni kigezo cha mshikamano baina ya Kiongozi na wananchi, ni nembo ya demokrasia ya kidini na mapenzi na huruma pamoja na kuwasaidia wanyonge. Kama tutaziangalia risala na ujumbe mbali mbali wa Hija unaotolewa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kila mwaka tutaona kuwa, kwa kawaida yamezungumziwa mambo hayo muhimu kwa namna moja au nyingine.
Swali: Taathira na matunda ya kutiliwa mkazo mambo hayo katika risala za Hija za Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika nchi nyingine ni zipi? Je jambo hilo limekuwa na taathira kwa shakhsia muhimu na wanasiasa waandamizi katika nchi za Kiislamu au za Kiarabu?
Jawabu: Watu wote wanatueleza kuwa risala hizo kwao ni sawa na kupata uhai mpya na wanazisifu sana kwa jinsi zilivyo na taathira katika nyoyo za wapenda haki na jinsi zilivyo na muono wa mbali. Katika safari zote tunazokwenda nje ya nchi na katika kila mkutano tunaoshiriki – ambapo kila mwaka huwa tunatembelea karibu nchi 50 tofuati duniani na huwa tunaonana na watu mbali mbali, na jumuiya tofauti na viongozi mbali mbali wa Kiislamu hususan viongozi wa vyama na jumuiya za kisiasa za Kiislamu katika nchi tofauti pamoja na wanamapambano mbali mbali – wote hao huashiria jambo hilo na husifu risala hizo. Yaani pamoja na kuwepo udhaifu wetu mkubwa katika kufikisha kwa walimwengu yaliyomo kwenye risala hizo, lakini popote pale zinapofika risala hizo, basi siku zote hutoa taathira kubwa mno.
Swali: Hivi sasa kunazungumziwa suala la udiplomasia wa umma duniani, yaani viongozi wa nchi za duniani hivi sasa wanawalenga zaidi wananchi katika matamshi yao kuliko tawala za nchi. Je, ujumbe wa Hija nao unaweza kuhesabiwa kuwa ni sehemu ya nguzo muhimu za udiplomasia wa umma wa Jamhuri ya Kiislamu na ni wenzo wa kuweza kutangaza na kuwaelewesha walimwengu uhakika wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran?
Jawabu: Ni jambo lisilo na shaka kwamba moja ya njia nzuri za kuweza kuyatangaza Mapinduzi ya Kiislamu nje ya Iran ni huu ujumbe wa Imam (Khomeini) na wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa mahujaji kila mwaka. Moja ya njia za kulipa uhai kongamano la Hija na kukabiliana na njama za kufifiliza malengo matukufu ya Hija katika maisha ya kila siku ya Waislamu ni ujumbe na risala hizo za Hija ambapo kwa mtazamo wangu risala hizo zimefanikiwa kutoa athari zake njema katika nyoyo za Waislamu. Ijapokuwa hata hivyo kama nilivyosema, kwa upande wetu sisi nasi tumefanya uzembe wa kiasi fulani katika kuufikisha ujumbe huo kwa walimwengu vile inavyotakiwa.
Swali: Je una ujumbe wowote wa kumalizia mahojiano yetu haya?
Jawabu: Ninatamani na ninamuomba Mwenyezi Mungu awajaalie Waislamu wazielewe vile inavyotakiwa falsafa za ibada za Kiislamu na ujumbe muhimu uliomo ndani yake. Udhaifu na mapungufu yaliyopo ni kwamba mahujaji wengi hutoka maeneo ya mbali sana wakiwa wamevumilia mashaka na tabu nyingi kwenda kwenye maeneo matakjatifu huko Saudi Arabia, lakini pamoja na hayo wakirejea makwao huwa hawakupata ule ujumbe hasa wa Hija kwa vile inavyotakiwa. Imepokewa katika Hadithi kwamba, “Nuru ya Hija huendelea kuwemo ndani ya hujaji madhali hajatenda madhambi.” Yaani hujaji hurejea nyumbani akiwa na nuru ya Hija. Nuru hiyo huendelea kuwemo ndani ya dhati ya mtu, ndani ya matendo yake na ndani ya jamii hadi pale ambapo Mwenyezi Mungu apishie mbali, hujaji anapofanya maasi na ni kuanzia hapo ndipo pole pole nuru hiyo huanza kutoweka. Ni matumaini yetu mahujaji nao watafanya juhudi zao zote kuhakikisha wanapata nuru ya Hija na vile vile watafanya idili kubwa ya kulinda na kuhifadhi ujumbe wa Hija na watalifanya somo walilolipata katika Hija liwe ni mithili ya kambi ya kiibada ili Hija iweze kuchukua nafasi yake inayostahiki kuwa nayo katika kuulea vizuri umma wa Kiislamu.
 
< Nyuma   Mbele >

^