Skip to content

Habari

Habari
Hifadhi

Risala na Barua

Matini
Hifadhi

Kumbukumbu na Simulizi

Kabla ya Mapinduzi
Baada ya Mapinduzi

Sauti na Taswira

Picha
Sauti
Video
Hotuba ya Kiongozi Muadhamu Alipokutana na Watafiti na Maafisa wa Mashirika ya Elimu za Kimsingi Chapa
29/07/2012
Ifuatayo ni matini kamili ya hotuba ya Ayatullahil Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu alipokutana na kundi la watafiti na maafisa wa mashirika ya elimu za kimsingi tarehe 29/07/2012
Kwa jina la Allah Mwingi wa rehema Mwenye kurehemu
Kwanza kabisa natumia fursa hii kukukaribisheni marafiki, ndugu, makaka, madada na viongozi. Nina matumaini kwamba, kikao hiki na vikao vingine mfano wa hiki, vitaweza kusaidia haya mahitaji ya kimsingi ambayo nchi yetu inayo, ambayo ni ustawi wa kielimu, utafiti, teknolojia, kulea vipaji na kuenea siku baada ya siku wasomi na wenye vipawa mahiri wa nchi yetu katika maisha ya wananchi katika taifa hili.
Kikao cha leo kimeandaliwa kwa lengo la kuimarisha mashirika ya elimu za kimsingi na kiujumla, kuleta ubunifu na mambo mapya katika elimu na teknolojia sambamba na kuimarisha hali ya kuingia bidhaa za mashirika haya katika masoko na matumizi. Vizuri, kwa hakika ndugu waliozungumza hapa wamebainisha mambo na matilaba nzuri sana. Kwa bahati nzuri, kuna maafisa wa serikali katika kikao hiki na bila shaka wameyasikia mapendekezo hayo. Tab'ani, ndugu ambao wamezungumza hapa katika fremu ya kutoa mapendekezo, baadhi yao wameelezea manung'uniko waliyonayo pia ambapo kwa mtazamo wangu haki iko pamoja nao. Malalamiko na manung'uniko yaliyobainishwa hapa ni sahihi; na kupatiwa kwake ufumbuzi kutafikiwa tu kwa kuzingatiwa mapendekezo haya (na kufanyiwa kazi). Vizuri, maafisa wa Serikali wapo hapa; mheshimiwa Makamu wa Rais na baadhi ya mawaziri wanaohusika na masuala haya na vile vile kuna maafisa wengine wa Serikali ambao wamehudhuria kikao hiki na yaliyosemwa hapa wameyasikia bilaa shaka. Tab'ani, kuna matarajio ambayo yamebainishwa hapa ambayo watu wanayo kwa kiongozi Muadhamu, Inshallah tutayafuatilia hayo yote; iwe ni yale mambo ambayo yanahusika na Serikali na chombo cha utekelezaji - ambapo sisi ni lazima kutilia mkazo - au iwe ni yale masuala ambayo kwa namna moja au nyingine yanahusika na Kiongozi Muadhamu. Inshallah, sisi tutayafuatilia haya. Tab'ani, mimi nimenukuu hapa mfano wa mapendekezo na matarajio yaliyotajwa hapa na ndugu wapendwa; ambapo kwa mtazamo wangu, aghalabu ni matarajio sahihi na nina matumaini Inshallah, haya yatafuatiliwa na kufanyiwa kazi ipasavyo. Hapa mimi nitaashiria baadhi ya mapendekezo na matarajio hayo.
Kile ambacho tunakitilia mkazo na kukisisitiza, ni hiki kwamba, elimu ni mtaji usio na mwisho na usiokwisha wa nchi. Endapo mzunguko wa uzalishaji elimu utakuweko katika nchi, kama kutakuweko na vipaji na kushughulishwa na kama uwezo uliopo utaanza kutumiwa na kudhihiri, wakati huo hiki kitakuwa ni chanzo kisichokwisha. Elimu ni tukio la ndani; sio kitu ambacho mtu analazimika au anakuwa hana budi kuwa tegemezi na kitu hicho. Ndio, kama nyinyi mtataka mchukue elimu kutoka mhala fulani ilipo, ndivyo itakavyokuwa; yaani kuna hali ya kutegemea, kuna ulazima wa kunyoosha mkono; (kwa ajili ya kuomba kupatiwa elimu hiyo); lakini baada ya kuwa katika nchi tayari kuna misingi ya kielimu, kisha kukawa na vipaji katika nchi husika wakati huo hujitokeza hali ya kufanya utafiti. Endapo sisi tutajihusisha na suala la kufuatilia utafiti, elimu na kufanya uchunguzi, endapo suala hili ambalo Inshallah limekuwa likifuatilia kwa jaddi kwa miaka kadhaa sasa hapa nchini, kwa kasi hii hii bali kwa shauku na msukumo zaidi na kwa kutilia umuhimu zaidi, hapana shaka kuwa, nchi itafikia katika kilele.
Kwa kuzingatia uhakika ambao tunaushuhudia leo na ambao uko mbele ya macho yetu, hii hali ya kufikia kilele, hii hali ya kukwea na kupata maendeleo na ustawi, sio kuota ndoto za alinacha; bali ni kutazama mambo kwa uhalisia wake; tajiriba ya miaka kadhaa ya hivi karibuni, inaonyesha hili. Katika takwimu hizi hizi zilizotolewa, bila shaka mumehabarika na hili kwamba, ustawi na maendeleo ya nchi katika sekta muhimu na elimu mpya na zenye taathira katika maisha yameweza kupatikana kwa muda wa miaka michache tu; (yaani maendeleo hayo hayakuweko katika miaka michache iliyopita); hii inaonyesha kwamba, kuna vipawa, uwezo na maandalizi hapa nchini. Kwa hakika sisi tunapaswa kulipa uzito jambo hili; yaani tulipe umuhimu suala la elimu hapa nchini; yaani tulifanye hili kuwa msingi wa kazi. Maneno yetu kwa hii miaka kadhaa yalikuwa haya haya. Endapo elimu itapewa uzito katika sekta mbalimbali, wakati huo haya mashirika ya elimu za kimsingi ambayo yanafanya kazi kwa msingi wa elimu, yanazalisha na kuleta utajiri, yataweza hatua kwa hatua kuleta ustawi na uchanuaji wa kweli wa uchumi wa nchi.
Kupata utajiri kupita uuzaji wa vyanzo vya utajiri kama mafuta na mfano wake, sio ustawi, sio maendeleo; huku ni kujidanganya. Sisi tumeangukia katika mtego huu. Ni lazima tulikiri hili, tukubali kwamba, ni mtego kwa ajili ya nchi. Sisi tumekumbwa na hali ya kuuza mali ghafi. Huu ni uhakika ambao sisi tumeurithi na nchi yetu imezoeshwa na hili. Tab'ani katika miaka ya hivi karibuni kumefanyika jitihada ili kuondoa na kuweka kando kwa kiwango fulani ada hii yenye madhara, hata hivyo hili bado halijafanyika kikamilifu.
Kwanza sisi tunapaswa kuwa na imani kwamba, nchi inapaswa kufikia mahala ambapo itaweza kufanya mambo kwa irada na hiari yake, ifunge visima vyake vya mafutal tunapaswa kufikia hali hii ya kujiamini. Kuna hali hii ya uuzaji mali ghafi katika sekta mbalimbali na katika madini; na hili kwa hakika ni miongoni mwa udhaifu wetu; ni moja ya matatizo ya nchi yetu. Kama isisi tunataka kuokoka na hali hii, kama tunataka kufikia katika ustawi wa kweli wa kiuchumi, njia ya hilo ni kutegemea elimu; na hili litawezekana kwa kuimarisha kivitendo mashirika haya ya elimu za kimsingi. Tunapaswa kufanya harakati kuelekea upande huu.
Tab'ani, kuna kazi ambazo tayari zimefanyika tena kazi zenye thamani. Ripoti ambayo imetolewa hapa na mheshimiwa Makamu wa Rais - tab'ani, mimi nilikuwa na taarifa kamili kwa namna fulani juu ya kile kilichofanyika kwani hapo kabla nilipata ripoti ya maandishi kuhusiana na hilo - inatia moyo sana; inaonyesha kwamba, vyombo vyetu Alhamdulilahi vinafanya jitihada nzuri katika uwanja huu; isipokuwa, tutazame, tuchunguze na kutambua mapungufu na nakisi katika sekta mbalimbali na kisha tufanye hima na juhudi za kuondoa nakisi na mapungufu haya.
Endapo sisi Inshallah tutaweza kuendeleza kazi za kiuchumi ambazo zimejengeka juu ya msingi wa elimu na ambazo tayari zimeanzishwa hapa nchini na kuzibadilisha kuwa ziwe zinaongoza katika masuala ya uchumi, jambo hili sio tu kwamba, litaipa nchi nguvu ya kiuchumi, bali litaipa nchi hii pia nguvu ya kisiasa na nguvu ya kiutamaduni. Wakati nchi inapohisi kwamba, inaweza kuendesha na kusimamia maisha yake na ya wananchi wake na kuhudumia mataifa mengine kwa kutegemea elimu yake na utaalamu wake lenyewe, huhisi kuwa na utambulisho, huhisi kuwa na shakhsia na hadhi; hiki kwa hakika ndio kile kile kitu ambacho mataifa ya Kiislamu hii leo yanakihitajia mno.
Kabla ya mapinduzi ya Kiislamu hapa nchini, kwa miaka mingi taifa letu lilikuwa mtumwa wa kudhoofika moyo wa kujiamini; yaani lilikuwa limepoteza kabisa ile hali ya kujiamini. Kuanzia wakati ambao maafisa na viongozi wa serikali walifungua macho na kisha hatua kwa hatua wananchi nao wakafanya hivyo na kisha kubakia kinywa wazi kwa mshangao mbele ya maendeleo ya kustaajabisha ya elimu ya Wamagharibi, hatua kwa hatua taifa hili lilihisi kuwa na mapungufu, udhalili, uduni na hali hiyo ikaenea baina ya wananchi. Kwa bahati nzuri, kulipopatikana ushindi wa mapinduzi hapa nchini, mapinduzi haya yakabadilisha kila kitu; ikiwemo hali hii na moyo huu tulioubainisha.
Kwa msingi huo, kuasisi kazi za kiuchumi zilizojengeka juu ya msingi wa elimu na utaalamu, hupelekea kuimarika moyo, ari, shakhsia na utambulisho wa kitaifa na vile vile jambo hilo huifanya nchi ipate nguvu ya kisiasa. Haya mamlaka ya kujitawala yenyewe na hali ya nchi kujitosheleza, ni jambo ambalo hulipatia nchi nguvu ya kisiasa; fauka ya hayo huwepo nguvu ya kiuchumi, jambo ambalo nalo bila shaka ni la kawaida.
Kile kitu ambacho kwa hakika sisi tunataka kiweko katika kikao hiki Inshallah kiujumla ni mambo mawili. Mosi, ni kushajiishwa watu wenye vipawa, wateule, wasomi na watu ambao wanajishughulisha na kazi ya utafiti ili waelekee upande wa kuasisi mashirika na vile vile kufikisha masokoni bidhaa za mashirika haya pamoja na utafiti wao na kuzifanya bidhaa hizo zifikiwe na wananchi na kisha kuyaingiza haya katika mzunguko wa biashara. Hili ni lengo letu la kwanza. Tab'ani kuongeza elimu, utajiri na mali, ni fasili ya awali ya mashirika haya.
Kwa msingi huo, watu wa elimu na watu ambao ni wa kuwekeza fedha, wafanye hima ili mashirika haya yaongezeke na kuwa mengi. Sasa hapa imeelezwa kwamba, hadi kufikia mwisho wa Mpango wa Tano wa Maendeleo nchini Iran, kutakuwa na mashirika elfu ishirini; hata hivyo kwa mtazamo wangu ninadhani kwamba, idadi ya mashirika hayo inapaswa kuwa kubwa zaidi ya hii na tuyazingatie na kuyapa umuhimu mashirika ya elimu za kimsingi. Tab'ani, idadi na ubora wake nao yote kwa pamoja yashuhudiwe; ambapo suala la ubora ni suala jingine.
Lengo la pili ni hili kwamba, matatizo ya mashirika haya yapatiwe ufumbuzi. Kuna matatizo - kuna matatizo ya kifedha na matatizo ya misaada mbalimbali ya kimaanawi ambapo katika hili kulikuweko na mapendekezo - serikali inaweza kuyapatia ufumbuzi matatizo haya. Hizi hizi sekta zinazohusika na kadhia hii; iwe ni ofisi ya mheshimiwa Makamu wa Rais, au iwe ni Wizara za Viwanda, Elimu, Afya na Matibabu na Jihadi ya Kilimo na wizara ambazo zinahusika na masuala haya; zinaweza kutoa ushirikiano, zikagawana majukumu na kukaainishwa mipaka na majukumu ya kila sekta na hivyo matatizo yaliyopo yakapatiwa ufumbuzi. Miongoni mwa mambo ambayo yamezungumziwa hapa na kwa mtazamo wangu ni sahihi kabisa ni mfumo wa zamani katika benki na vituo vya fedha. Kwa hakika asasi hizi zinapaswa kubadilisha mitazamo yao kwa mashirika haya. Matatizo ya fedha ni matatizo makubwa ya mashirika haya.
Vile vile miongoni mwa mambo yaliyozungumzwa hapa - ambayo kwa mtazamo wangu ni sahihi kabisa - ni suala la kuzingatia kukubali hatari katika mashirika haya; kwani kama mashirika haya hayatakuwa tayari kuikubali hatari na kukawa hakuna hali ya kuwa tayari kukabiliana na au kuwa tayari kubahatisha, kwa hakika kazi haiwezi kusonga mbele. Tab'ani, kuna njia za kuyafanya mashirika haya yasikabiliwe na madhara na hatari; kama vile bima maalumu na inayoeleweka ili kuweze kutabiriwa mambo kwa ajili ya kazi hii; ambapo hii nayo ni kazi ya vyombo vya serikali.
Jambo muhimu ni kuwa, taasisi na vyombo vya serikali inabidi vichunguze na kugundua vipawa, uvumbuzi na wavumbuzi wake pamoja na viwaendee watu wenye vipaji vya kifikra na baadaye kuwasaidia na kuwaunga mkono ili kwa njia hiyo iwezekane kuanzisha mashirika mengine mapya ya elimu za kimsingi. Vyombo vyetu havipaswi kukaa chini na kusubiri wavumbuzi wavifuate na kazi kuangukia mikononi mwa kona za kiidara, urasimu na matatizo ya kiidara yaliyopo; bila shaka haya ni mambo ambayo yatadhoofisha shauku, hamu, vipawa na maandalizi. Kwa mujibu wa ripoti nilizopatiwa ni kuwa, madola ya kigeni yamekuwa yakitafuta na kuchungua vipawa vya nchi yetu; kila mahala ambapo wanaona panawafaa hujitokeza na kuwekeza katika hilo na kisha kuhamishia kwao.
Vizuri, kipaji cha kibinaadamu na nguvu kazi ni kitu chenye thamani kubwa zaidi kwa nchi. Hatupaswi kuruhusu na hatutakiwi kuachia hilo litokee, na huku kutoruhusu kimantiki maana yake ni kutoandaa uwanja, tujiandae, tushajiishe, tuwapate (wasomi na wataalamu wenye vipawa) na kuwaingiza uwanjani na kuwafanya wajishughulishe na kazi na wawe mashughuli; wakati huo itajitokeza ile chemchemi isiyokwisha.
Miongoni mwa matilaba yaliyotajwa na kuzungumziwa hapa na ambayo ni sahihi pia ni hili suala la kutekelezwa sheria ya kuuunga mkono mashirika ya elimu za kimsingi ambazo ni miaka miwili sasa tangu zipasishwe. Kwa hakika moja ya matatizo ambayo yanayakabili mashirika ya elimu za kimsingi ni kutotekelezwa sheria ya kuyaunga mkono mashirika hayo na ni lazima hati ya utekelezaji wa sheria hiyo iwasilishwe haraka iwezekanavyo. Serikali iliwasilisha muswada na bunge likapasisha. Hata hivyo hadi sasa bado hati ya utekelezaji wa sheria hiyo haijapasiswhwa; kwa hakika kazi hii inapaswa kufanyika haraka. Inshallah, maafisa na viongozi wa serikali ambao wako hapa, walifuatilie hili. Kuna kiwango fulani cha fedhan pia ambacho kimekadiriwa, suala la kuanzisha mfuko limepasishwa na hilo liko tayari. Endapo Inshallah, sheria hiyo itaanza kufanya kazi, bila shaka hilo litasaidia maendeleoa na ustawi wa mashirika ya elimu za kimsingi.
Nukta nyingine ambayo imeashiriwa - ambayo tab'ani ilikuwa katika fikra zangu pia na ambayo ilizingatiwa na kutiliwa maanani pia katika ripoti niliyopatiwa - ilikuwa hii kwamba, katika misaada ya kifedha na himaya, mashirika ya serikali yasichukue hisa zaidi na hivyo kuyafanya mashirika binafsi na yasiyo ya kiserikali yabakie nyuma. Hapa pia nimeona baadhi ya ndugu waliozungumza wamekumbushia nukta hii; na katika ripoti zetu, nukta hii pia imetiliwa maanani.
Tujitahidi ili kuhakikisha kwamba, sekta ya binafsi inaweza kujitegemea kwa maana halisi ya neno katika uwanja wa mashirika ya elimu za kimsingi na hivyo kuyafanya mashirika hayo kukua. Kama hali hii itajitokeza katika uwanja huu, basi sekta binafsi itakuwa na kustawi na kwa mtazamo wangu, hili ni jambo ambalo litakuwa na manufaa mengi kwa taifa. Serikali itakuwa na nafasi yake ya kuunga mkono, kuelekeza na kutoa msaada; lakini katika uwanja, mhimili wa harakati utakuwa mikononi mwa sekta binafsi. Hii ni moja ya nukta za kuzingatiwa.
Miongoni mwa mambo muhimu yaliyopo pia ni Benki ya Kutoa Taarifa. Moja ya faida za kikao hiki ni hii kwamba, watu ambao wanakuja wanawapatia wenye vipaji, wasomi wateule na maafisa wa Serikali; kazi hii inapaswa kuenea kwa wote. Ni lazima kuweko na Benki ya Kutoa Taarifa; sisi tunapaswa kufahamu mambo tuliyonayo na yale ambayo hatunayo; vitu ambavyo vinahitajika. Yaani kuna haja ya kuweko Benki ya Kutoa Taarifa kwa ajili ya kugundua uwezo mbali mbali wa kielimu nchini na vile vile kutambua mapungufu yaliyopo, kupanua wigo wa kazi za mashirika ya elimu za kimsingi na kutia nguvu sekta binafsi katika mashirika ya elimu za kimsingi na kadhalika. Hasa kwa kuzingatia kwamba, baadhi ya sekta za serikali zilizotajwa hapa - kama mafuta, kujihami na kilimo - haya kwa hakika ni mambo ambayo ni mahitaji makubwa mno; ambapo kama mahitaji haya yataeleweka kwa ajili ya kuanzisha mashirika ya elimu za kimsingi, watu ambao wako tayari kuwekeza katika masuala ya elimu na fedha, wanaweza kufuatilia mahitaji haya na kuhakikisha kwamba, taifa hili linapata mahitaji hayo. Kwa muktadha huo, kuanzishwa Benki ya Utoaji Taarifa na kwa ajili ya kutoa taarifa za lazima kwa wote, ni kitu ambacho kwa hakika ni cha lazima mno.
Nukta nyingine ni hii kwamba, mashirika ya elimu za kimsingi yanaweza kuwa amilifu katika nyuga na nyanja mbalimbali hapa nchini; yasiishie kujifunga na nyuga chache tu; kuna haja ya vipawa hivi kutumiwa katika maeneo yote ambayo kuna haja na mahitaji ya hili na Inshallah mashirika haya yataweza kuwa na nafasi.
Kile ambacho ninataka kukisema ingawa kwa mukhatasri mwishoni mwa hotuba yangu hii ni hiki kwamba, Vyuo Vikuu, Vyuo Vikuu vya Serikali na wananchi pia kwa ujumla kwa bahati nzuri wana uwezo na vipaji vya kazi hii, iwe ni kielimu au iwe ni uwezo wa kifedha, hivyo basi ni lazima wafanye bidii na kufahamu majukumu yao na kipindi chao nyeti cha kihistoria na kisha kuyafanya kazi haya. Hii kwamba, sisi tumesema "uchumi wa kimapambano na wa kimuqawama" kwa hakika hii sio nara na kaulimbiu tupu; huu ni uhakika wa mambo. Nchi imo katika hali ya kustawi na kupata maendeleo. Vizuri, hapana shaka kuwa, kuna harakati inayoelekea upande huu ambayo ina wapinzani. Baadhi ya upinzani huu una msukumo wa kiuchumi na baadhi ya upinzani mwingine una msukumo wa kisiasa; baadhi ya upinzani huu ni wa kieneo na mwingine ni wa kimataifa .Upinzani huu katika baadhi ya mambo hufikia na kuishia katika mashinikizo mbalimbali kama haya mnayoyashuhudia; mashinikizo ya kisiasa, vikwazo, visivyokuwa vikwazo, mashinikizo ya kiproganda - haya yapo - lakini pamoja na matatizo haya, katikati ya mambo haya, kuna hatua thabiti na madhubuti, pamoja na hima na maamuzi ambayo yatapita katika mishkili na matatizo haya na kisha kufanikiwa kufikia katika nukta iliyokusudiwa; hali ya nchi katika hali ya hivi sasa iko namna hii.
Kwa namna yoyote ile sisi katu hatuko katika mkwamo; na katu sisi hatuwezi kuzuiwa kutoendelea mbele na mambo ambayo tumeyaamua kutokana na kukabiliwa na matatizo; hakuna kitu kama hicho; ni kweli kwamba, matatizo yapo; lakini matatizo yote haya ni madogo ikilinganishwa na irada, azma thabiti, malengo na malengo matukufu ya taifa na nchi hii. Mambo haya hayawezi katu kupatikana na kufikiwa kwa kutaka raha, kubweteka, kustarehe na kulala; hapana, mambo haya yanapatikana katikati ya uwanja; lakini medani hii ni uwanja mkuu na wakati huo huo ni wenye (uwanja huo) kuleta shauku; yaani hali hii ni sawa na medani ya kuleta shauku na wakati huo huo ikieleweka vyema kwamba njia hiyo ina mashaka yake. Hali iliyonayo Iran ya Kiislamu hivi sasa ni mithili ya medani ya mashindano ya michezo ambayo ingawa ndani yake mnakuwa na machofu na huzuni, lakini kuweko katika medani hiyo huleta shauku, kwani wanamichezo hushiriki katika mashindano kwenye medani hizo kwa shauku, nishati na hamasa ya hali ya juu. Yaani kuweko hali ya uchofu hakuwafanyi wanamichezo hao waache kushiriki na kujitokeza katika medani ya mashandano; bali huja tena wakiwa na hamu na shauku kubwa. Kazi hii ina mashaka - mashinikizo ya mwili na akili - lakini wanamichezo huja uwanjani. Kwa hakika hali yetu iko namna hii.
Hivyo uwanja huu ni uwanja wa harakati ya jumla na ya kudumu na ya kihistoria ya wananchi. Kwa upande wa kihistoria, harakati yetu ya leo ni harakati yenye kubakia. Yaani hatima na mustakbali wa Iran unaainishwa leo na wananchi wa Iran kwa ajili labda ya karne kadhaa zijazo. Kwa hakika fursa kama hii haijitokezi na kuja mara zote; kwa bahati nzuri fursa hii imejitokeza katika zama zetu hizi. Mapinduzi haya yameiweka nchi na wananchi wa taifa hili katika harakati yenye taathira na ya kubakia kwa muda mrefu na ya kihistoria. Vizuri, kwa hakika sisi tunapaswa kila mmoja wetu kufahamu vyema nafasi yake na kisha kulitekeleza hilo. Moja ya sekta zetu ni uchumi na sifa ya uchumi katika mazingira kama haya ni uchumi wa kimapambano na kimuqawama; yaani uchumi ambao unaambatana na muqawama na kusimama kidete mbele ya njama za maadui na ukhabithi wa adui; maadui ambao sisi tunao.
Kwa mtazamo wangu ni kuwa, miongoni mwa sekta muhimu ambazo zinaweza kuufanya uchumi wa kimapambano na kimuqawama usimame na kudumu, ni hii kazi yenu; haya haya mashirika ya elimu za kimsingi; kwa hakika hii ni moja ya madhihirisho bora kabisa na moja ya mambo yenye taathira kubwa sana katika kuunda uchumi wa kimapambano na kimuqawama; hili ni jambo ambalo linapaswa kufuatiliwa. Inshallah, mustakbali utakuwa unaong'ara. Nina matarajio kwamba, Mwenyezi Mungu Mtukufu atakupeni tawfiki nyinyi nyote; atawapa tawfiki pia waheshimiwa maafisa na viongozi wetu azizi na wapendwa ili waweze kutekeleza vizuri nafasi yao pamoja na majukumu waliyonayo; Inshallah na nyinyi tekelezeni nafasi yenu na haya mapendekezo yaliyotolewa hapa, Inshallah yatafanyiwa kazi na kufanikiwa. Akthari ya mapendekezo haya ni mapendekezo mazuri; Inshallah mapendekezo haya yatachunguzwa na kufanyiwa kazi. Ninakuombeeni dua na nina matarajio kwamba, kesho ya taifa la Iran itakuwa bora kuliko leo na jana.
Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.
 
< Nyuma   Mbele >

^