Skip to content

Habari

Habari
Hifadhi

Risala na Barua

Matini
Hifadhi

Kumbukumbu na Simulizi

Kabla ya Mapinduzi
Baada ya Mapinduzi

Sauti na Taswira

Picha
Sauti
Video
Nini Kifanyike Katika Kukabiliana na Wimbi la Kuvunjiwa Heshima Matukufu ya Kiislamu? Chapa
16/09/2012
Kitendo cha hivi karibuni cha maadui wa Uislamu cha kumfunjia heshima tena Mtume Muhammad Swallallahu Alayhi Waalihi Wassallam, kimewakasirisha mno Waislamu wote ulimwenguni ambao wameonyesha majibu makali dhidi ya maadui hao. Hii si mara ya kwanza kwa maadui wa Uislamu na Waislamu, kuyavunjia heshima matukkufu ya Kiislamu. Katika nyakati tofauti, Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amekuwa akitoa miongozo mbali mbali kuhusu vitendo hivyo viovu na vya kiuadui ambapo sambamba na kuonya kuhusiana na madhara makubwa ya mwenendo huo wa hatari na kubainisha malengo yaliyoko nyuma ya pazia ya vitendo hivyo vya chuki, amekuwa akionyesha njia pia za jinsi ya kukabiliana na silisila hii chafu ya kuivunjia heshima na kuitovukia adabu dini tukufu ya Kiislamu. Ifuatayo hapa chini ni baadhi ya miongozo ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kuhusu jambo hilo:

1 Wajibu wa kutangazwa na kuarifishwa tena na tena masomo na darsa za Mtume Muhammad SAW kupitia kauli na vitendo vya mtukkufu huyo
2 Kuonyesha sura halisi na tukufu ya Uislamu
3 Kushikamana Waislamu chini ya kivuli cha Mtume Mtukufu dhidi ya maadui wa Uislamu na mfumo wa kibeberu
4 Kuzingatia mikono ya nyuma ya pazia la uvunjiaji heshima wa matukufu ya Kiislamu na malengo yao
5 Kuepusha kutokea vita baina ya Uislamu na Ukristo
6 Kuwataka viongozi wa Marekani wawape adhabu kali waliofanya jinai hiyo

Wajibu wa kutangazwa na kuarifishwa tena na tena masomo na darsa za Mtume Muhammad SAW kupitia kauli na vitendo vya mtukkufu huyo
Wazayuni na tawala zilizoko chini ya ushawishi wa Uzayuni pamoja na madola ya kibeberu yakiongozwa na Marekani mtenda jinai; kila wanapotaka kuuchokoza umma wa Kiislamu na kuonyesha hamaki na chuki zao dhidi ya dini tukufu ya Kiislamu, basi mashambulizi yao yote wanayaelekeza kwa Nabii na Mtume Mtukufu wa Uislamu. Jambo hili linatuonesha nini? Jambo hili linatuonesha kuwa, kumbukumbu za Mtume Muhammad SAW, jina la mtukufu huyo, kuzaliwa mtukufu huyo, Hijra ya mtukufu huyo, serikali ya miaka kumi ya mtukufu huyo huko Madina na kila hatua, neno, mafundisho, elimu na miongozo ya mtukufu huyo, kama leo Waislamu watayazingatia vilivyo na kutaamali ndani yake, basi wataweza kupata somo kubwa sana na kufungukiwa na mlango mpana wa ufanisi katika maisha yao. Mtume Muhammad SAW ni mwenye kutoa ilhamu kwa umma mzima wa Kiislamu. Maadui wanalitambua vyema jambo hilo. Wanauogopa sana mwamko wa umma wa Kiislamu. Zinawaogofya na kuwatia kiwewe nguvu za jamii ya Waislamu bilioni moja na milioni mia tano walioenea katika kila kona ya dunia na ambao wote wamepanga safu moja chini ya kivuli cha Mtume Muhammad SAW. Bwana Mtume ambaye ni rehema kwa walimwengu wote, ni chimbuko la kheri na baraka kubwa na adhimu sana kwa ajili ya mwanadamu, leo hii anavunjiwa hoeshima na maadui kupitia magazeti yao, lugha ya wanasiasa wao, vitabu vyao na kupitia mamluki na vibaraka wao ambao hawaoni kiwewe kumtukana na kumvunjia heshima mtu mtukufu na mwenye baraka zote hizi. Mambo haya inabidi yatuamshe sisi Waislamu na tuelewe kuwa ndani ya uwepo wa Bwana Mtume, ndani ya shakhsia ya Bwana Mtume, ndani ya kumbukumbu za maisha ya Bwana Mtume, ndani ya Hijra ya Bwana Mtume, ndani ya jihadi ya Bwana Mtume, ndani ya sira ya Bwana Mtume, ndani ya darsa za maneno na vitendo za Bwana Mtume, mna hazina kubwa na adhimu sana kwa ajili ya Waislamu. Kama tutaweza kuitumia vizuri hazina hiyo, basi umma wa Kiislamu utaweza kuwa na nafasi muhimu na tukufu kiasi kwamba hakuna mtu yeyote atakayethubutu kuwafanyia ubeberu, wala kuwachezea, wala kuwaweka chini ya mashanikizo na wala kuwatisha kwa kitu chochote kile. Hili kwa kweli ni somo muhimu mno kwetu sisi sote. [1]

Kuonyesha sura halisi na tukufu ya Uislamu
Jambo lililo muhimu kwetu sisi Waislamu hivi sasa ni kuhakikisha kuwa sura halisi na tukufu, safi na isiyo na doa ya dini tukufu ya Uislamu inatambulika vilivyo. Maadui katika karne kadhaa zilizopita wa marafiki wajinga na walioghafilika katika kipindi cha nyuma zaidi waliiharibu sura ya Uislamu; na ima kwa makusudi au kwa malengo yao ya kijinga na kijahili, waliongeza au kupunguza baadhi ya mambo ndani ya Uislamu. Leo hii pia na ingawa watu wenye welewa finyu, watu wanaofikiria maslahi yao binafsi tu wamejizatiti vilivyo kuuharibu na kuupotosha Uislamu lakini uhakika ni kuwa propaganda za maadui katika suala hili ni kubwa zaidi na maadui wana njia za maudhi na tata sana za kuwashambulia Waislamu... Ndugu zangu Waislamu! Tuna kazi kubwa na muhimu sana ya kuutambulisha na kuutangaza Uislamu halisi na sahihi kama ambavyo tuna kazi kubwa na muhimu sana ya kutambuana vizuri sisi kwa sisi. [2]

☼ Kushikamana Waislamu chini ya kivuli cha Mtume Mtukufu dhidi ya mfumo wa kibeberu na maadui wa Uislamu
Uwepo na dhati takatifu ya Mtume Mtukufu na Rasulul A'adham wa Uislamu ni nukta muhimu sana ya kuweza kuleta umoja na mshikamano kati ya Waislamu. Huko nyuma pia nimewahi kusema mara nyingi kuwa, ulimwengu wa Kiislamu unaweza kuungana vilivyo kwenye nukta hii. Hii ni nukta ambayo hisia za Waislamu wote zimekusanyika ndani yake, hicho ndicho kituo kikuu cha ashiki, mapenzi na ulimwengu wa Kiislamu. Nyinyi wenyewe mnaona jinsi kalamu zinazofadhiliwa kifedha na Wazayuni zinavyokilenga moja kwa moja kituo hicho kitukufu kwa mawimbi ya mashambulizi. Maadui wanamvunjia heshima Bwana Mtume Muhammad SAW ili kwa njia hiyo waanze pole pole kuliondolea umuhimu suala la kuvunjiwa heshima na kutukanwa umma wa Kiislamu na kudhalilishwa ulimwengu wa Kiislamu. Basi tujue kuwa hii ndiyo nukta ya asili. Wanasiasa, watu wenye vipaji mbali mbali vya kielimu na kiutamaduni, waandishi, washairi na wasanii wetu wanapaswa kuipa umuhimu mkubwa nukta hii ili wazidi kuwaunganisha na kuwakutanisha Waislamu wote kwenye kaulimbiu hiyo muhimu. Tusiyape uzito masuala madogo madogo tunayotofautiana, tusituhimiane sisi kwa sisi, tusikufurishane sisi kwa sisi na wasitokezee baadhi ya Waislamu wakawatoa kwenye dini Waislamu wenzao. Nyoyo za Waislamu wote kila pembe ya dunia zinapata uhai mpya katika utajo, kumtukuza, kumnusuru na kuwa na mapenzi makubwa na Bwana Mtume Muhammad SAW. Sote tuna mapenzi makubwa sana kwa Bwana Mtume wetu Mtukufu. [3]
Vitendo vyao hivyo vya kiwendawazimu na visivyoingilika akilini na ambavyo vimejaa chuki, vimeyatimizia hoja mataifa ya Waislamu na vimesaidia katika kuzidi kushuhudiwa mwamko wa Waislamu. Leo hii ni sawa tu wakikubali au kukataa, lakini uhakika utabakia kuwa ule ule kwamba, kuna harakati kubwa na yenye msingi madhubuti imeanza katika ulimwengu wa Kiislamu na kwamba harakati hiyo itauletea tena umma wa Kiislamu istiklali, heshima, uhuru na maisha yake katika wakati unaofaa.
Kipindi cha hivi sasa ni kipindi muhimu mno kihistoria. Watu wenye vipaji, maulamaa na wasomi katika jamii za Kiislamu wana jukumu zito hivi sasa. Udhaifu wowote ule au kupuuza mambo au kufanya mambo kiubinafsi na kwa malengo yasiyohudumia Uislamu au kutotekeleza vizuri majukumu yao kunaweza kuleta maafa makubwa. Maulamaa wa kidini wasinyamazie kimya vitendo vya kuzusha mizozo na mifarakano ya kimadhehebu katika safu za Waislamu. Wasomi wasifanye uzembe katika kutimiza wajibu wao wa kupuliza roho ya matumaini kati ya vijana wa Kiislamu. Wanasiasa na viongozi wa nchi wahakikishe kuwa wananchi wao wako katika medani wakati wote na wategemee nguvu za wananchi wao. Tawala za Kiislamu zinapaswa kutia nguvu kadiri inayowezekana mshikamano baina yao na watumie nguvu hizo za kweli katika kukabiliana na mabeberu duniani. [4]

☼ Kuzingatia mikono ya nyuma ya pazia la uvunjiaji heshima wa matukufu ya Kiislamu na malengo yao
Kilichoko nyuma ya pazia la vitendo hivi vya kishari na kishetani ni nini na ni nani? Unapoviangalia vitendo hivi vya kishetani katika miaka hii ya hivi karibuni na kuvipima na jinai zinazofanyika Afghanistan, Iraq, Palestina, Lebanon na Pakistan utaona kuwa mambo haya yote yanakwenda sambamba na kwa utaratibu uliopangiliwa vizuri sana. Hivyo hapabakii shaka hata chembe kwamba wapangaji na waendeshaji wakuu wa vitendeo hivyo vya kishetani ni mikono ya viongozi wa nchi za kibeberu na utawala wa Kizayuni (wa Israel), Wazayuni ambao wana ushwishi mkubwa ndani ya serikali ya Marekani na taasisi za usalama na kijeshi za nchi hiyo pamoja na ndani ya serikali ya Uingereza na baadhi ya tawala za nchi nyingine za barani Ulaya. [5]
Zilizoko nyuma ya pazia la vitendo hivi vya kishetani na kishari ni siasa za kiuadui za Uzayuni na Marekani na baadhi ya viongozi wa ubeberu wa kimataifa ambao kwa ndoto zao batili wanataka kufifiliza heshima tukufu ya matukufu ya Kiislamu katika suduri na vifua vya vijana wa ulimwengu wa Kiislamu na kuzima hisia za kidini ndani ya nyoyo za vijana hao. Kama wasingeliziunga mkono kongwa na sehemu za silisila na mnyororo huu mchafu yaani Salman Rushdi, mchora vikatuni wa Denmark na kasisi wa Kimarekani aliyechoma moto Qur'ani Tukufu na kama wasingelidhamini na kuruhusu makumi ya filamu zilizo dhidi ya Uislamu kutengenezwa na kusambazwa na mabanda ya propaganda ya mabepari wa Kizayuni, basi leo hii tusingelishuhudia kufanyika dhambi hii kubwa mno ambayo haistahiki kabisa kusamehewa. Mtuhumiwa nambari moja ya jinai hii ni Uzayuni na serikali ya Marekani. [6]

Kuepusha kutokea vita baina ya Uislamu na Ukristo
Matukio ya Septemba 11 yalitoa sababu na kisingizio kwa Rais wa wakati huo wa Marekani - ambaye ni mtenda jinai na mikono yake imejaa damu za watu - kuvamia nchi za (Waislamu) za Afghanistan na Iraq na alitumia kisingizio hicho kutangaza "Vita vya Msalaba" dhidi ya Waislamu ambapo kwa mujibu wa ripoti mbali mbali, rais huyo alitangaza kuwa vita hivyo vya msalaba vilikamilika kwa kuingia Kanisa katika medani ya vita. Lengo la hatua ya hivi karibuni ya chuki na uadui dhidi ya Uislamu (kuchomwa Qur'ani Tukufu) ni kuwa, kwa upande mmoja maadui wanataka kuwafanya watu wote katika jamii za Wakristo wakabiliane na waifanyie uadui dini tukufu ya Kiislamu na Waislamu ili uadui wao dhidi ya Uislamu uingie sura ya kidini kwa kuingia ndani yake maanisa na makasisi na hivyo kushadidisha chuki na taasubu za kidini; na kwa upande wa pili mataifa ya Waislamu ambao wamekasirishwa mno na jeuri na jinai hiyo kubwa, washughulishwe na mambo mengine na wasahaulishwe masuala na matukio yanayoendelea hivi sasa katika ulimwengu wa Kiislamu na katika eneo la Mashariki ya Kati. [7]
Watu wote wanapaswa kutambua kuwa, tukio hili la hivi karibuni (la kuchomwa moto Qur'ani Tukufu) halina uhusiano wowote na Kanisa na wala Ukristo, bali ni kitendo cha baadhi chache tu ya makasisi majahili na vitimbakwiri na si sahihi kukihusisha kitendo chao hicho cha kipunguwani na Wakristo na viongozi wengine wa dini ndani ya Ukristo. Sisi Waislamu kamwe hatuwezi kufanya kitu kama hicho dhidi ya matukufu ya dini nyinginezo. Wanachotaka maadui na wapangaji wa tamthilia hizi chafu za kiwendawazimu ni kuona kunazuka mizozo kati ya Waislamu na Wakristo katika jamii mbali mbali duniani, lakini mafundisho ya Qur'ani tukufu yako kinyume kabisa na malengo hayo ya maadui. [8]

Kuwataka viongozi wa Marekani wawape adhabu kali waliofanya jinai hiyo
Wanachotakiwa kufanya Waislamu hivi sasa ni kuwashikilia viongozi wa serikali ya Marekani na wanasiasa wa nchi hiyo kuwaadhibu waliotenda jinai hiyo (ya kutengeneza filamu ya kumtukana na kumvunjia heshima Mtume Muhammad SAW). Kama wanasiasa wa Marekani ni wakweli katika madai yao ya kutohusika na jinai hiyo, basi wanapaswa kuwapa adhabu inayolingana na uhalifu huu mkubwa, wale wote waliotenda jinai hiyo ovu na chafu pamoja na waungaji mkono na wafadhili wao wa kifedha ambao wamezijeruhi mno nyoyo za Waislamu bilioni moja na nusu ulimwenguni. [9]
Sisi hatung'ang'anii kuthibitisha kosa la watu fulani au viongozi fulani au maafisa fulani kuhusiana na jinai hiyo, bali tunachosema sisi ni kuwa sera na mbinu za kisiasa zinazotumiwa na wanasiasa wa Marekani na baadhi ya nchi za Ulaya ndizo zinazowafanya walimwengu wawahesabu kuwa ndio wakosa wakuu, hivyo wanachopaswa kufanya wanasiasa hao ni kuonyesha kivitendo kuwa hawahusiki na uhalifu huo mkubwa sana na wasiishie tu kusema kwa maneno matupu. Wanapaswa kuchukua hatua za kweli za kuzuia vitendo kama hivyo, tab'an ni wazi kuwa hawatozuia. [10] Mtuhumiwa nambari moja ya jinai hii ni Uzayuni na serikali ya Marekani. Hivyo kama wanasiasa wa Marekani ni wakweli katika madai yao ya kutohusika na jinai hiyo, basi wanapaswa kuwapa adhabu inayolingana na uhalifu huu mkubwa, wale wote waliotenda jinai hiyo ovu na chafu pamoja na waungaji mkono na wafadhili wao wa kifedha ambao wamezijeruhi mno nyoyo za Waislamu kote ulimwenguni. [11].

MAREJEO
[1] Sehemu ya hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika maadhimisho ya maulidi ya Mtume Muhammad SAW - 13/09/2007.
[2] Sehemu ya hotuba ya Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika ufunguzi wa mkutano wa viongozi wa OIC - 9/9/1997.
[3] Sehemu ya miongozo ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aliyoitoa kwa mnasaba wa maulidi ya Mtume Muhammad SAW na Wiki ya Umoja - 16/4/2006.
[4] Sehemu ya ujumbe wa Hija - 29/12/2006.
[5] Sehemu ya ujumbe alioutoa Ayatullah Udhma Khamenei kufuatia kuchomwa moto Qur'ani Tukufu - 13/09/2010.
[6] Sehemu ya ujumbe wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kufuatia kuvunjiwa heshima Mtume Muhammad SAW - 13/9/2012.
[7] Sehemu ya ujumbe wa Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei kufuatia kuchomwa moto Qur'ani Tukufu - 13/09/2010.
[8] Sehemu ya ujumbe alioutoa Ayatullah Udhma Khamenei kufuatia kuchomwa moto Qur'ani Tukufu - 13/09/2010.
[9] Sehemu ya ujumbe wa Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, kufuatia kuchomwa moto Qur'ani Tukufu - 13/09/2010.
[10] Sehemu ya miongozo ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aliyoitoa katika Chuo Kikuu cha Elimu za Baharini cha mjini Nowshahr, kaskazini mwa Iran - 16/9/2012.
[11] Sehemu ya ujumbe wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kufuatia kuvunjiwa heshima Mtume Muhammad SAW - 13/9/2012.

 
Mbele >

^