Skip to content

Habari

Habari
Hifadhi

Risala na Barua

Matini
Hifadhi

Kumbukumbu na Simulizi

Kabla ya Mapinduzi
Baada ya Mapinduzi

Sauti na Taswira

Picha
Sauti
Video
Ujumbe wa Hija wa Walii Amri wa Waislamu Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei 1433 Hijria Chapa
25/10/2012

Bismillahir Rahmanir Rahim

بسم الله الرحمن الرحيم
الحمد لله رب العالمين و صلوات الله و سلامه علي الرسول الاعظم الأمين و علي آله المطهّرين المنتجبين و صحبه الميامين.

Hamdu zote ni za Allah, Mola Mlezi wa viupmbe pia. Na rehema za Allah na salamu Zake zimfikie Mtume Mtukufu Mwaminifu na Aali zake watoharifu, wateule na masahaba wake wema.


Msimu wa Hija uliojaa rehema na baraka umewadia na kwa mara nyingine na watu waliofanikiwa kwenda katika miadi hii iliyojaa nuru, wamo katika kumiminiwa baraka za Mwenyezi Mungu. Hapa, ninatoa mwito kwenu nyote mahujaji kutumia fursa ya kuwepo mahala hapa na kuwemo katika wakati huu, kujiimarisha kimaanawi na kimaada. Hapa, Waislamu wanaume kwa wanawake wanaitikia labeka mlingano wa Mola wao Mkubwa wa kujipamba kwa sifa na matendo mema; kwa nyoyo na midomo yao. Hapa watu wote wanapata fursa ya kufanya mazoezi ya kudumisha udugu, mshikamano na kujiepusha na maasi. Hii ni kambi ya malezi na mafunzo, ni maonyesho ya umoja, adhama na jinsi umma wa Uislamu ulivyokusanya pamoja sura za watu tofauti, ni kambi ya kupambana na shetani na mataghuti. Hapa Mwenyezi Mungu Mwingi wa hekima na Muweza amepafanya kuwa ni mahala ambapo waumini waweze kuona manufaa yao ndani yake. Tutakapofungua macho yetu ya busara na ibra basi ahadi ya mbinguni itaweza kuenea katika maisha yetu yote; ya kila mmoja wetu na ya jamii nzima. Sifa za kipekee za amali za Hija ni kule kuchanganya kwake dunia na Akhera na kuchanganya kwake masuala ya watu binafsi na ya kijamii. Al Kaaba isiyo na doa na iliyotukuka; kutufu miili na nyoyo za watu katika mhimili mmoja madhubuti na wa milele; amali ya Sai (baina ya Safa na Marwa) na kufanya jitihada za mfululizo na za mpangilio mmoja kutoka nukta ya kuanzia hadi nukta ya kuishia; kugura mahujaji wote kuelekea kwenye nyuga za ufufuo za Arafa na Mash'ar na shauku na uhudhurishaji wa moyo katika Mahshar na maqam hayo adhimu, huleta unyofu na hali mpya, mapambano ya pamoja ya watu wote ya kukabiliana na vielelezo vya shetani, na hatimaye kwa pamoja na kutoka kila mahala na kila rangi na kila namna; wote wanashiriki kwa pamoja katika amali hizo tukufu zilizojaa neema na utukufu na zilizojaa maana na ishara za uongofu. Sifa za kipekee za faradhi hii zimejaa maana na madhumuni.
Ni amali kama hii ndiyo ambayo inauunganisha moyo na kumkumbuka Mwenyezi Mungu, na kuujaza nuru na kuunawirisha upweke wa moyo wa mwanadamu kwa imani na taqwa na wakati huo huo kumvua mwanadamu kutokana na mzingiro wa ubinafsi na kumsahilishia mambo katika jamii iliyopambika kwa sura za kila namna, ya umma wa Kiislamu na kumvisha nguo ya kujiepusha na madhambi ambayo huilinda roho yake kutokana na mashambulizi yaliyojaa sumu ya mashambulizi na vile vile humuongezea nguvu na moyo wa kupambana na mashetani na mataghuti. Ni mahala hapo ndipo ambapo hujaji anapoweza kuonana na Waislamu wenzake wengi wanaunda umma mkubwa wa Kiislamu na kuona kwa karibu nguvu na uwezo wa umma huo na hivyo kupata matumaini kuhusu mustakbali mwema na vile vile kupata hisia za wajibu wa kutoa mchango wake wa kuimarisha umma huo na pia kama atapata taufiki na msaada wa Mwenyezi Mungu aweze kutoa bay'a na kutangaza utiifu wake kwa Mtume (Muhammad) Mtukufu wa daraja na kufunga mithaki na ahadi imara kwa Uislamu azizi na kutia nia ya kweli ya kuijenga kiimani nafsi yake, kuleta marekebisho katika umma na kutia nguvu neno la Uislamu.
Mambo yote haya mawili, yaani kuijenga nafsi na kuujenga umma (wa Kiislamu) ni faradhi zisizoishiwa na wakati na wala zisizofungwa. Njia za kuweza kufanikisha faradhi hizo mbili si nzito kwa watu wenye mazingatio na wanaoangalia mambo kwa kina katika utekelezaji wa majukumu ya kidini na kutumia vizuri akili, tabasuri na wenye mtazamo wa mbali.
Kujenga nafsi huanzia kwenye kupambana na hisia za kishetani na kufanya juhudi za kujiepusha na madhambi na kujenga umma huingia sura kwa kumjua adui na njama zake, kufanya jitihada za kupelekea mashambulizi, hadaa na uadui wa maadui usiwe na athari zozote na hadi kufikia kwenye kuziunganisha nyoyo na mikono pamoja na lugha za matabaka yote ya Waislamu na mataifa yote ya Kiislamu.
Katika wakati huu tulio nao hivi sasa, moja ya masuala muhimu zaidi ya umma wa Kiislamu ambalo lina mfungamano (wa moja kwa moja) na mustakbali wa umma wa Kiislamu, ni matukio ya mapinduzi katika nchi za kaskazini mwa Afrika na katika eneo la Mashariki ya Kati ambayo hadi sasa yameshapelekea kuanguka tawala kadhaa fasidi na vibaraka wa Marekani na waitifaki za Uzayuni na kuzitikisa tawala nyingine kama hizo. Kama Waislamu watapoteza fursa hii adhimu na iwapo watashindwa kutumia fursa hii katika kuujenga vizuri na kuleta marekebisho kwenye umma wa Kiislamu, basi watakuwa wamepata hasara kubwa. Hivi sasa mabeberu wavamizi na waingiliaji wa masuala ya ndani ya mataifa mengine wanafanya juhudi zao zote kujaribu kupotosha harakati hizo adhimu za Kiislamu.
Katika harakati hizo kubwa, Waislamu wake kwa waume wamesimama kupambana na ukandamizaji wa watawala (wao madhalimu) na kupambana na udhibiti wa Marekani ambao umepelekea kudhalilishwa na kudunishwa mataifa ya Waislamu na kusababisha kushuhudiwa ushirikiano baina ya tawala za nchi hizo na utawala mtenda jinai wa Kizayuni. Waislamu wamegundua kuwa kitu kinachoweza kuwaokoa katika mapambano haya ya kufa na kupona ni Uislamu, mafundisho ya dini hiyo tukufu na nara na kaulimbiu zake zenye uwokovu na hilo wamelitangaza wazi wazi. Ajenda yao kuu wameifanya kuwa ni kulitetea taifa madhulumu la Palestina na kupambana na utawala ghasibu (wa Kizayuni). Wamenyoosha mkono wa urafiki kwa mataifa yote ya Waislamu na wanataka kuona umma wa Kiislamu unashikamana na kuwa kitu kimoja.
Hii ndiyo misingi mikuu ya harakati za wananchi kwenye nchi ambazo katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, wananchi wake wamenyanyua bendera ya uhuru na mabadiliko na kujitokeza kwa viwiliwili na roho zao kwenye medani za mapinduzi na ni mambo kama haya ndiyo yanayoweza kuwa misingi mikuu ya kuleta marekebisho katika umma mkubwa wa Kiislamu. Kusimama imara na kushikamana vilivyo na misingi mikuu ni sharti la lazima la kuweza kupata ushindi wa mwisho wa harakati za wananchi kwenye nchi hizo.
Lengo la adui ni kutaka kuhakikisha anateteresha misingi hii mikuu. Mikono fasidi ya Marekani na NATO na Uzayuni inatumia baadhi ya mighafala na mitazamo finyu kujaribu kupotosha wimbi la harakati ya vijana Waislamu na wanatumia jina la Uislamu kuwagombanisha Waislamu na wanaiita jihadi ya kupambana na ukoloni na Uzayuni kuwa ni ugaidi usio na macho katika ulimwengu wa Kiislamu ili Waislamu wauane wao kwa wao na hivyo maadui hao wa Uislamu waweze kuokoka na Uislamu na wanajihadi wake watazamwe kwa sura mbaya na chafu.
Baada ya maadui kukata tamaa kwa kuona kuwa hawawezi kuushinda Uislamu wala kuzima nara na kaulimbiu zake, hivi sasa wameamua kuzusha fitna kati ya makundi tofauti ya Waislamu na wanafanya njama za kueneza chuki dhidi ya Ushia na chuki dhidi ya Usuni ili kuzuia kupatikana mshikamano na umoja katika umma wa Kiislamu.
Maadui wanawatumia vibaraka wao katika eneo (la Mashariki ya Kati), kuzusha mgogoro nchini Syria ili kuzishughulisha akili za mataifa ya dunia na kuzifanya zisahau masuala muhimu ya nchi zao na zisahau pia hatari zinazowakabili. Maadui hao wanajaribu kuwashughulisha (Waislamu) na masuala ya umwagaji wa damu ambayo maadui wameyazusha wao wenyewe. Vita vya ndani nchini Syria na kuuliwa vijana wa Kiislamu kwa mikono ya Waislamu wenzao ni jinai ambazo zilianzishwa na Marekani na Uzayuni na tawala tiifu kwa maadui ambazo wanazidi kuchochea moto huo. Nani anaweza kuamini kuwa, tawala ambazo zilikuwa waungaji mkono wa madikteta waovu wa Misri na Tunisia na Libya, hivi sasa wamekuwa waungaji mkono wa kutaka demokrasia taifa la Syria? Kadhia ya Syria ni suala la kulipiza kisasi dhidi ya utawala wa nchi hiyo ambao katika kipindi cha miongo mitatu ulikuwa umesimama peke yake kupambana na Wazayuni maghasibu na kuyaunga mkono makundi ya wanamuqawama wa Palestina na Lebanon.
Sisi tunaliunga mkono taifa la Syria na tunapinga uchochezi na uingiliaji wa aina yoyote ile wa kigeni nchini humo. Marekebisho ya aina yoyote ile nchini humo inabidi yafanywe na wananchi wenyewe na kwa kutumia njia zinazokubaliwa kikamilifu na wananchi wa taifa hilo. Hatua ya mabeberu wa kimataifa ambao kwa msaada wa tawala za vibaraka wao katika eneo hili wanatumia kisingizio cha kuenea mgogoro na wakati huo huo kutumia kisingizio cha kuweko mgogoro kuhalalisha kufanya kila aina ya jinai nchini humo ni hatari kubwa ambayo kama tawala za eneo hili hazitajieupusha nayo basi inabidi zisubiri zamu yao ifike ya kukumbwa na hadaa hizo za kibeberu.
Makaka na madada! Msimu wa Hija ni fursa ya kutaamali na kuyaangalia kwa kina masuala muhimu ya ulimwengu wa Kiislamu. Hatima ya mapinduzi ya eneo hili na juhudi za madola makubwa yaliyojeruhiwa kutokana na mapinduzi (ya wananchi wa eneo hili) za kutaka kuyapotosha mapinduzi hayo ni miongoni mwa masuala hayo (muhimu ya ulimwengu wa Kiislamu ambayo inabidi kuyaangalia kwa kina). Njama za wasaliti za kutaka kuzusha hitilafu kati ya Waislamu na kuleta ugomvi na suutafahumu kati ya nchi ambazo zimeamua kushirikiana na Jamhuri ya Kiislamu; kadhia ya Palestina na juhudi za kuifanya itengwe na kuizima jihadi ya Wapalestina; propaganda za kueneza chuki dhidi ya Uislamu zinazofanywa na tawala za Magharibi na uungaji mkono wa tawala hizo kwa watu wanaomvunjia heshima Mtume Muhammad SAW; kuandaa mazingira ya kuzuka vita vya ndani na kugawanywa vipande vipande baadhi ya nchi za Waislamu; kuzitisha tawala na wananchi wa nchi za Kiislamu zilizofanya mapinduzi kuhusiana na hatari za kupinga siasa za kibeberu za Magharibi na kueneza dhana potofu kuwa mustakbali wao unategemea kujisalimisha kwao mbele na madola ya kibeberu na masuala mengine muhimu sana kama hayo, ni miongoni mwa kadhia muhimu ambazo inabidi ziangaliwe kwa taamuli na kwa mazingatio makubwa katika fursa inayopatikana kwenye Hija na chini ya kivuli ya kupendana na kuwa na fikra moja nyinyi mahujaji.
Ni jambo lisilo na shaka kwamba uongofu na msaada wa Mwenyezi Mungu utawamwilikia njia za salama na amani waumini wenye kufanya jitihada katika mambo yao, والذين جاهدوا فينا لنهدينهم سبلنا Na wanaofanya juhudi kwa ajili Yetu, Sisi tutawaongoa kwenye njia Zetu. (al Ankabut - 29:69).
Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.
Sayyid Ali Khamenei,
30/Mehr/1391 (Hijria Shamsia) inayosadifiana na tarehe tano Dhulhijjah 1433 Hijria.

 
< Nyuma   Mbele >

^