Skip to content

Habari

Habari
Hifadhi

Risala na Barua

Matini
Hifadhi

Kumbukumbu na Simulizi

Kabla ya Mapinduzi
Baada ya Mapinduzi

Sauti na Taswira

Picha
Sauti
Video
Hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Alipoonana na Wanafunzi wa Vyuo Vikuu Chapa
06/08/2012
Ifuatayo ni matini kamili ya hotuba ya Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aliyoitoa tarehe 06/08/2012 mbele ya hadhara kubwa ya wanafunzi wa vyuo Vikuu hapa nchini.

Kwa jina la Allah Mwingi wa rehema Mwenye kurehemu

Karibuni sana makaka, madada na vijana azizi. Kwa hakika kikao hiki kilikuwa kizuri mno. Tab'ani, baada ya kutangazwa kwamba, muda wa wanachuo kutoa hotuba zao umefikia tamati, walijitokeza kama watu kumi hivi ambao walinyanyua juu mikono yao wakiwa tayari kabisa kuzungumza. Nilivyotazama kwa haraka haraka nimeona takribani watu kumi hivi waliinuka. Vizuri, kwanza kabisa, mimi sio kiongozi na msimamizi wa kikao; bali mimi ni mmoja wa washiriki wa kikao hiki; kuna wahusika wanaosimamia na kuongoza kikao hiki; kwa msingi huo hampaswi kuomba wakati kutoka kwangu. Pili, ni kuwa kama mimi ningelikuwa ndiye ninayetoa wakati na muda wa watu kuzungumza, basi bila ya shaka yoyote ningewapatia wakati watu wote wale kumi ili wazungumze. Yaani mimi nisingelitilia mkazo kwamba, lazima nizungumze; kwani sisitizo langu mimi hasa ni kufanyika kwa kikao hiki. Tab'an, baada ya ndugu wale kumi kumaliza mazungumzo yao, yamkini wangejitokeza watu wengine saba au nane ambao nao wangenyanyua juu mikono yao wakitaka kuzungumza! Hakuna tatizo, lakini ninadhani kwamba, makaka na madada wengi walioko hapa, wanapenda hili lisiendeelee; hivyo basi mimi naanza kuzungumza kile ambacho nimepanga kukizungumza leo.
Mambo yaliyozungumzwa hapa kwa hakika yalikuwa mambo mazuri mno. Baadhi ya matamshi ya ndugu wanachuo hapa, yaliingiliana; yaani watu kadhaa walitilia mkazo nukta maalumu, jambo ambalo linaonyesha upana wa nukta hizo au matilaba hayo; baadhi ya mambo yalizungumwa na watu maalumu hapa na hakuna mtu mwingine aliyezungumzia mambo hayo ila watu hao, na kwa hakika hili ni jambo zuri mno.
Mimi nimeomba nipatiwe (kimaandishi ) yale yaliyozungumzwa hapa na ndugu hawa - ambapo nimeshapatiwa - Inshallah, nitataka yatizamwe na kuchunguzwa. Waheshimiwa maafisa na viongozi wa serikali wapo hapa; bila ya shaka wameyasikia haya yaliyozungumzwa hapa. Ninawaomba wayape uzito na wayape umuhimu matamshi ya wanafunzi. Ni kweli kwamba, kwa sasa anayezungumza ni mwanachuo, lakini kile kilichosemwa kutokana na mtu kufahamu anga na mazingira ya kiuanachuo, anafafahamu kwamba, maneno haya si ya mtu mmoja; hivyo kuna haja ya matamshi haya kuzingatiwa na kupewa umuhimu mkubwa; fauka ya hayo katika mazungumzo haya ya wanachuo kuna nukta zenye faida ambazo ni ufunguo (wa mambo mengi sana.)
Mimi nimenukuu baadhi ya nukta zilizozungumzwa hapa; nimehisi kwamba kuna ulazima wa kutoa ufafanuzi wa mambo makubwa ya kisiasa kwa wanachuo. Hili ni jambo ambalo halina uhusiano na maafisa wa serikali na Wakuu wa Vyuo Vikuu; hili ni jambo ambalo linahusiana na jumuiya za wanachuo. Mimi ninaunga mkono fikra kwamba, kuweko ulazima wa kutoa ufafanunuzi wa mambo makubwa ya kisiasa, hakukinzani na kufungamana kikamilifu na misingi pamoja na kuchunga kwa umakini muelekeo wa kisiasa.
Miongoni mwa mambo mengine yaliyozungumzwa hapa ni suala la kwenda maafisa na viongozi wa serikali katika Vyuo Vikuu. Kwa hakika hili ni jambo sahihi kabisa. Mimi ninaamini kwamba, maafisa na viongozi wa serikali wanapaswa kutembelea mara kwa mara Vyuo Vikuu; Wakuu wa Mihimili Mikuu Mitatu ya Dola (Serikali, Bunge na Mahakama), maafisa wa daraja za kati, Mkuu wa Shirika la Utangazaji la Sauti na Televisheni la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran IRIB, viongozi wa Jeshi la Ulinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH na vikosi vingine vya ulinzi; wote hawa wanapaswa kwenda katika Vyuo Vikuu na kuwa na vikao na wanachuo na kusikiliza maneno ya wanachuo. Na mimi napenda kuwaleza hapa kwamba, wao nao wana mengi ya kuwaambia wanachuo. Hakuna kitu ambacho kinaweza kuziba pengo na kuchukua nafasi ya mazungumzo hayo ya ana kwa ana na uso kwa uso; hii ni kama ilivyokuwa ada ya kale ya masheikh wetu ambao walikuwa wakipanda juu ya mimbari na kuzungumza na watu ana kwa ana.
Kwa hakika katika hili kuna taathira kubwa mno. Mambo mengi , shubha na masuali ambayo leo yapo katika fikra za vijana na kizazi chetu kipya, yatajibiwa iwapo maafisa na viongozi nchini watajenga tabia ya kutembelea mara kwa mara Vyuo Vikuu na kuzungumza uso kwa uso na wanachuo, na bila ya shaka yoyote shubha na utata uliopo utaondoka. Mimi katika kile kipindi nilichokuwa na nguvu zaidi za mwili, nilikuwa nikishiriki sana kwenye vikao vya Vyuo Vikuu na hivi sasa pia kwa hakika kila ninapoweza, nikawa na fursa na wakati, huwa ninapenda kushiriki mara kwa mara katika vikao vya Vyuo Vikuu; isipokuwa kwa sasa ni kama anavyosema Mwenyezi Mungu: "Mwenyezi Mungu haikalifishi nafsi yoyote ila kwa kadiri ya iwezavyo" kwa hivyo kwa umri wangu mimi na watu mfano wangu, sidhani kama vijana watakuwa wanatumai kutuona tuna harakati sana; lakini maafisa wa serikali wanaweza kufanya jambo hilo na kwa msingi huo wanapaswa kutenga wakati maalumu kwa ajili ya kutembelea Vyuo Vikuu ili kwa njia hiyo waweze kutoa majibu kwa maswali mbali mbali wanayokuwa nayo vijana wanachuo hapa nchini.
Miongoni mwa mambo yaliyosemwa hapa pia ni kuhusiana na hatua zinazochukuliwa na Mahakama kuhusu vyama, mitandao ya Intaneti na weblog mbali mbali za wanafunzi wa Vyuo Vikuu. Kwa hakika hivi karibuni mimi nilitaka nipatiwe ripoti ya jambo hili na Alhamdulilahi nimepokea ripoti hiyo. Tab'an, Mahakama ina sababu zake katika kuchukua hatua hizo ambapo kama sababu hizo zitaelezwa wazi, basi zitaondoa maswali na utata unaojitokeza. Hata hivyo mimi ninaamini kwamba, si sahihi kuchukua hatua kali dhidi ya kijana wa Chuo Kikuu anayeonesha radiamali kali kuhusu jambo fulani. Bila ya shaka kuna tofauti baina ya mtu anayepinga mfumo (wa Jamhuri ya Kiislamu), ambaye ana lengo la kufanya uadui dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu na mtu ambaye yeye, hapana, yeye hapingani na mfumo lakini anabainisha jambo fulani kwa hisia kali, hata kama wakati mwingine mambo anayoyabainisha si kweli, au aina ya ubainishaji wake si mzuri, au ikawa mtu fulani kwa mfano haupendi utaratibu wake huo wa kubainisha mambo - Inshallah kama kutakuwa na wakati nitabainisha mambo na nukta zinazohusiana na hili - lakini pamoja na hayo, kuamiliana na vijana hawa, hakupaswi kuwa kwa ukali.
Jambo jingine lililokuwemo katika mazungumzo ya wanachuo hapa ni suala la kuyapa kipaumbele maeneo ya vijijini na kutazama mambo kwa uhakika wake, yaani fikira ya uchumi uliosimama juu ya misingi ya uadilifu. Mimi nimezingatia nukta moja katika mambo yaliyosemwa na wanachuo hapa kuhusu suala hili, na kwa hakika nukta hii kwangu mimi na nyinyi pia imekuwa ibra na funzo kubwa. Kijana huyu mpendwa aliyekuja hapa na kuzungumzia suala la uchumi uliosimama juu ya misingi ya uadilifu amesema mambo mazuri hapa na alipotambulishwa hapa ilielezwa kwamba anatoka katika majimui ya vijana wanaosafiri na kwenda maeneo ya mbali kwa ajili ya kufanya kazi za kujitolea.
Naam, jambo hili liko wazi sasa. Wakati mtu anapokuwa katika kikundi cha vijana wanaosafiri na kwenda maeneo ya mbali vijijini kwa ajili ya kufanya kazi za kujitolea, hujionea uhakika wa mambo kwa karibu na kwa macho yake mwenyewe, tab'an, fikra ya kufuatilia uchumi uliosimama juu ya misingi ya uadilifu huhuika namna hii katika uwepo wake; kwa hakika hii ni darsa na funzo kwetu sote. Ni lazima kuwa na mawasiliano na matabaka mbali mbali ya jamii ili kuweza kudiriki mambo yao; hili jambo ambalo huwa na taathira katika utoaji wetu wa maamuzi na katika mtazamo wetu kuhusiana na masuala mbali mbali ya nchi.
Tab'an! Kwa uoni wangu ni kuwa, mtazamo wa kiuchumi nchini Iran unapaswa kusimama juu ya misingi ya uadilifu na kwamba, jambo hilo halikinzani kivyovyote vile na sera za kiuchumi za Iran zilizoainishwa kwenye kifungu cha 44 cha Katiba ya Jamhuri ya Kiislamu. Endapo sera na siasa za kifungu cha 44 cha Katiba ya Jamhuri ya Kiislamu zitatekelezwa kama tulivyosema, kama tulivyotaka na kama tulivyobainisha - na mimi nimewahi kulizungumzia hili wakati fulani kwa mapana na marefu - basi bila ya shaka yoyote uchumi wa Iran hautakumbwa na balaa la mfumo mbovu wa kibepari na wala mfumo huo wa kibepari hautaweza kuwa na nafasi katika maamuzi makuu ya nchi.
Tab'an! Nikuambieni hapa kwamba, kile ambacho kiko leo duniani ni mfumo wa kibepari ambao dhati yake ni kuwafanya mabepari wawanyonye na kuwakalia juu watu wengine. Kwa hakika asili ya kuwa na mtaji na kuwekeza kwa ajili ya maendeleo ya nchi si kitu kibaya; ni kitu cha kusifiwa na kupongezwa; na kwa namna yoyote ile, jambo hilo si kitu kibaya na kisichopendeza. Kile ambacho ni kibaya na kisichopendeza ni kuufanya mfumo wa ubepari kuwa mhimili wa maamuzi yote muhimu na makubwa ya nchi na ya kijamii, na dhati ya mfumo huo ya kutaka kuvutia kila kitu upande wake. Ndio maana nchi inayofuata mfumo wa kibepari lazima hukumbwa na balaa kama lile lililoikumba hivi sasa kambi ya mfumo wa kibepari yaani nchi za Magharibi na kila mtu leo hii anayaona matokeo yake mabaya.
Matatizo na mashinikizo yanayoongezeka kila leo kwa wananchi na katika uchumi wa nchi za Magharibi na Ulaya hivi sasa, yanatokana na dhati ya mfumo wenyenye wa kibepari, yaani mfumo wa kuwafanya mabepari wawanyonye na kuwakalia juu watu wengine kila siku na kwa hakika huu ndio ule mfumo unaochukiza na usiopendeza. Lakini kama mambo yatafanyika kinyume chake, yaani kama watu ambao wana mitaji watachukua mitaji yao na kuwekeza kwa ajili ya ustawi wa jamii na tab'an kwa kuzingatia pia kwamba muwekezaji naye apate faida yake ya halali, basi jambo hilo ni zuri, lina faida na hakuna tatizo hata kidogo katika hilo kama mambo hayo yatazingatiwa. Kama kazi itafanyika namna hii na katika fremu hii - yaani kama utakuweko mtazamo wa misingi ya uadilifu wa Kiislamu na kuelekea katika maana hii - basi hakuna tatizo lolote. Kwa hivyo basi maneno haya ya utajiri na mwenye utajiri si mabaya hata kidogo. Tujitajidi kuhakikisha kuwa mitazamo ya Kisoshalisti na Kimaksi haitawali katika fikra zetu za kiuchumi. Wao wana mitazamo yao mingine. Mfumo wa Kisoshalisti unapinga kikamilifu suala la watu kuwa na mitaji na kuwekeza (yaani mfumo wa watu kuwa matajiri bali mfumo huo unataka watu wote wawe katika daraja sawa katika umiliki wa vitu) lakini katika mfumo wa Kiislamu hali ya mambo haiko hivi. Uislamu haupingi watu kuwa na mitaji na utajiri, bali linalopingwa ni kutumiwa vibaya mitaji na utajiri. Inawezekana kuweka mipango mizuri na usimamizi bora na hivyo utajiri ukaelekezwa na kuongozwa katika njia sahihi. ***Kwa msingi huo basi, kile ambacho sisi tumekizungumzia katika sera za kifungu cha 44 cha Katiba ya Jamhuri ya Kiislamu, katu havikinzani na uchumi ambao una misingi ya uadilifu; bali kimsingi ni kuwa kuna maana ya ukamilishaji.
Katika uwanja wa masuala ya kiuchumi, kumezungumziwa suala la "uchumi wa kimashambulizi"; hakuna tatizo, mimi sikufiria hilo. Kama kwa hakika kuna ubainishaji wa Kichuo Kikuu na Kiakademia kuhusiana na uchumi wa kimashambulizi - kama alivyosema mzungumzaji kwamba, hilo ni kamlisho la uchumi wa kimuqawama - kuna tatizo gani? Hilo nalo tulizungumzie. Kile ambacho mimi kilinipitikia ni "uchumi wa kimapambano na kimuqawama."
Tab'an, uchumi wa kimuqawama hauna upande wa kukataa tu; hii haina maana kwamba, uchumi wa kimuqawama ni kujizungushia mzingiro na hivyo kufanya tu kazi za kuzuia; hapana, maana ya uchumi wa kimuqawama si kuchukuliwa hatua za kujihami na kuvunja vikwazo zinazozunguka papo kwa papo, bali uchumi wa kimuqawama ni uchumi ambao kwa taifa, huweza kuimarika na kustawi hata katika mazingira ya vikwazo na mashinikizo. Hii ni fikra na ni takwa la watu wote. Nyinyi ni wanachuo, nyinyi ni wahadhiri, nyinyi ni wanauchumi; ni vyema mno mkabainisha fikra hii ya uchumi wa kimuqawama kwa lugha ya kichuo kikuu; ainisheni mipaka yake; yaani ule uchumi ambao katika mazingira ya mashinikizo, katika mazingira ya vikwazo, katika mazingira ya (kuandamwa na) uadui na uhasama mkubwa wenyewe unaweza kuwa ni dhamana ya ustawi na uchanuaji wa nchi fulani.
Mmoja wa wanachuo azizi hapa amesema, "tunaambiwa tusisaidie kujaza fumbo la jedwali la maadui - halafu amehoji akiuliza, sasa hatima ya ukosoaji itakuwaje: ina maana tusikosoe tena? Mimi sina mtazamo kabisa wa watu kuzuiwa kukosoa; bali msimamo wangu ni kinyume kabisa, kwani katika nukuu zangu hapa nilizoziandika, - Inshallah kama muda utaruhusu nitalibainisha hili, siku zote nimekuwa nikisisitiza kuwa, jumuiya za wanafunzi wa Vyuo Vikuu zihifadhi wakati wote sifa yao ya kukosoa kila pale mambo yanapokwenda kombo. Katu mimi siungi mkono kwamba, nyinyi msikosoe. Je tufanye nini ili ukosoaji huu usiwe ni katika kumsaidia adui? Lifikirieni vizuri suala hilo. Sio tuseme kwamba, kumsaidia adui ni jambo hasi, hivyo linakinzana na jambo chanya ambalo ni kukosoa; hapana, bali nyinyi wenyewe mumesema; mimi nimekosoa na ukosoaji wangu ukanukuliwa katika kila kona ya dunia; lakini hakuna mtu katika dunia ambaye atajitokeza na kudai kwamba, fulani anachukua hatua ambayo iko dhidi ya mfumo wa Kiislamu au dhidi ya kikundi cha uongozi na utekelezaji mambo ya nchi.
Naam, huo ndio ukweli wa mambo, na nyinyi pia fanyeni ukosoaji wa namna hii. Kwa msingi wa maneno hayo ni kuwa ukosoaji wenu huo inabidi uwe kwa namna ambayo hautafanikisha malengo ya adui au kwa maneno tuliyosema sisi, yaani isiwe ni kumsaidia adui na kujaza fumbo la jedwali. Imeelezwa kwamba, kuna baadhi ya watu wanatoa nadharia za kitaalamu ambazo zinakinzana na nadharia ya Kiongozi Muadhamu; hivyo hujitokeza watu na kusema, huku ni kukinzana na Utawala wa Fakihi (Wilayatul Faqih). Kwa hakika kuweko mtazamo wowote ule wa kiutaalamu usiokubaliana na mtazamo wa Kiongozi Muadhamu hakuna maana kuwa ni kupinga Utawala wa Fakihi.
Kazi yoyote ya kiutaalamu iliyofanyika kwa uzingatiaji wa hali ya juu wa kielimu inapoibuka na natija fulani, mtazamo wa mtu huyo huwa ni wenye kuheshimiwa na si sahihi kusema kuwa, huko ni kuupinga mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu; je kuna kuliweka wazi jambo hili zaidi ya huku?! Tab'an, kuna wakati inatokea kwamba, binafsi ninakuwa na nadharia ya kitaalamu katika uga fulani; ni jambo lisilo na shaka kuwa, sisi pia katika uga fulani tuna utaalamu; yamkini nadharia hii ya kitaalamu ikawa ni tofauti na nadharia nyingine ya kitaalamu; naam, hakuna tatizo lolote hapo, kwani inapokuwa hivyo huwa kuna nadharia mbili za kitaalamu; watu ambao wanataka kuchagua, waje na kuchagua nadharia wanayoipenda. Katika upande wa masuala ya kiutamaduni, katika uwanja wa masuala ya kielimu - katika sekta makhsusi - sisi pia kwa namna fulani tuna utaalamu; tumefanyia kazi kwa kiwango fulani nyuga hizo; hivyo hii huwa ni nadharia ya kitaalamu. Ala kulli haal, haipaswi hata siku moja kuhesabiwa kwamba, nadharia ya kitaalamu na kielimu ni upinzani, mapambano, kupingana na kutangaza kujitenga na mfumo wa Utawala wa Fakihi na Fakihi Mtawala. Hilo halipaswi kuruhusiwa kuweko. Naam, kikawaida katika mikutano yetu na wanachuo, nasi hupata fursa pia ya kuzungumzia baadhi ya mambo; je huku ni kuwa na matarajio makubwa? Hili ni swali.
Kama mtu atakuja na kukusanya majimui ya hotuba zangu nilizozitoa wakati ninapozungumza na wanachuo, iwe ni katika miezi ya Ramadhani (ambapo kila Ramadhani hukutana na wananchuo) iwe ni katika Vyuo Vikuu vya mikoani au katika Vyuo Vikuu vya hapa Tehran, bila shaka atapata faharasa ndefu ya matakwa ya mimi mja dhaifu kwa wanachuo wapendwa. Yamkini akaja mtu na kusema, Bwana wee, haya ni matarajio makubwa sana. Kwa hakika mimi siamini kama kufanya hivi ni kuwa na matarajio makubwa. Kwa nini? Uzingatiaji wa watu wengi katika Vyuo Vikuu unapinga na kuondoa dhana hii ya kuwa na matarajio makubwa. Endapo nyinyi mtamtaka kijana mwanamichezo mwenye nishati na nguvu anyanyue mzigo mzito kutoka hapa na kuupeleka sehemu nyingine, kwa hakika hilo litakuwa si jambo la matarajio makubwa. Lakini, endapo takwa hilo mtataka lifanywe na mtu ambaye ni mkondefu, mzee na dhaifu, kufanya hivyo kutakuwa ni sawa na kutarajia jambo kubwa kwa mtu dhaifu na huwa ni matarajio ambayo si ya mahala pake; lakini wakati uwezo unapokuweko, ni sawa tu, litakeni hilo, hakuna tatizo.
Chuo Kikuu ni sehemu ambayo imejaa nguvu na uwezo. Uwezo mkubwa unaoshuhudiwa katika mazingira ya wanachuo unatokana na sifa mbili kuu. Mosi, ujana na uwezo wa wimbi kubwa la nguvu za vijana, ambapo mimi ninaamini kwamba, vijana walio wengi hawafahamu kiwango cha nguvu za ujana walizo nazo; yaani mpaka sasa bado hawajagundua kwamba, wana uwezo usio na mpaka na wa kipekee ambao uko katika mazingira ya ujana wao.
Kwa hakika ujana ni chimbuko la chemchemu ya nguvu na nishati isiyokwisha. Pili, ni suala lenyewe la elimu na kuzingatia uwezo unaotokana na kutafuta elimu na maarifa. Kwa hakika Vyuo Vikuu nchini vinaweza kutoa majibu ya matarajio yote kupitia nishati na kujiamini kulikopata nguvu kubwa baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran. Kwa mantiki hiyo, kila kile ambacho sisi tuna matarajio kutoka kwa wanachuo, tukiwataka wafanye kazi ngumu, na kuwapatia matarajio yetu tuliyonayo kuhusu wao, kwa mtazamo wangu huko si kuwa na matarajio makubwa. Kuna kazi nyingi ambazo zinawezekana kufanywa. Kwa hakika sisi tuna harakati inayoambatana na nguvu isiyokwisha; endapo nguvu hii itapatiwa uhuru na kuongozwa vizuri, inaweza kuleta ufanisi mkubwa na kamili kwa ajili ya nchi. Naam, moja ya vitu ambavyo sisi tunavitaraji kutoka kwa wananchi ni jambo hilo ambalo katika hali ya kawaida lipo katika Chuo Kikuu na katika mazingira ya kijana na mimi nimekuwa nikisisitiza kwamba, hali hii ihuishwe na kutiwa nguvu katika Vyuo Vikuu sambamba na kuzingatiwa suala la kuwa na malengo maalumu. Tab'an, mimi nilibainisha kwa kiwango fulani suala la malengo matukufu na kutazama mambo kwa uhakika wake, wakati nilipokutana na maafisa na wafanyakazi wa mfumo wa Kiislamu mwanzoni mwa mwezi huu; hivyo basi baadhi ya hayo mumeshayasikia. Suala la kutazama mambo kwa uhalisia wake limehifadhiwa mahala pake na mimi nitaashiria jambo hilo baadaye; lakini malengo maalumu yanapaswa kuweko katika siasa, shabaha maalumu inapaswa iwepo katika elimu na malengo maalumu yanapaswa yawepo katika umaanawi na maadili mema.
Malengo maalumu katika elimu maana yake ni kuweko harakati katika uga wa elimu ambayo lengo lake litakuwa ni kufikia katika kilele; na natija ya hilo inapaswa kupatikana katika kusoma kwenu na kufanya hima kubwa katika masomo. Ninawaambia hapa kwamba; leo hii kusoma, kutafuta elimu, kufanya utafiti na kuwa makini na kuyapa uzito wa hali ya juu masuala ya masomo, ndiyo kazi ya msingi ya wanachuo na kwa hakika hii ni jihadi kwa wanachuo; na Inshallah kama kutakuwa na wasaa hili litabainika na kuwa wazi katika mwendelezo wa mazungumzo yangu.
Katika uga wa maadili na umaanawi, vile vile kuna haja ya kuweko malengo makuu. Kutokana na kuwa mazingira ya Chuo Kikuu ni mazingira ya vijana, kuna ulazima wa mazingira hayo kutakaswa na kuwa masafi. Baadhi ya watu wanadhani kwamba, Chuo Kikuu maana yake ni mazingira ambayo ndani yake hakuna ulazima wa suala la kufungamana na dini, maadili na akhlaqi na kwamba, si jambo linalotakiwa sana. Kwa hakika huu ni mtazamo mgando na ghalati kikamilifu na unahusiana na wakati wa kuanzishwa mfumo wa Vyuo Vikuu nchini Iran, yaani makumi ya miaka kabla ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu.
Katika kipindi hicho kuna watu ambao walileta Chuo Kikuu ambacho hakikuwa na asili na msingi wa dini, umaanawi na akhlaqi (maadili); ni kweli wakati wa kuanzishwa mfumo wa Vyuo Vikuu nchini Iran miongo kadhaa kabla ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, baadhi ya watu walifanya juhudi za kulea kizazi cha wasomi dhaifu waliojisalimisha kikamilifu kwa Magharibi, lakini si baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu hapa nchini Iran. Leo hii mazingira ya kidini na kimaadili pamoja na usafi wa nafsi na umaanawi yanashuhudiwa katika Vyuo Vikuu vya Iran na inatarajiwa kwamba, vyombo husika vifanye kazi kwa namna ambayo kila anayeingia kwenye mazingira ya Chuo Kikuu azidi kushikamana na mafundisho wa dini na maadili bora; yaani avutiwe na mazingira yanayotawala katika maeneo hayo.
Hivyo ilikuwa imepangwa kwamba, watu hawa wakiwa hapa nchini waweke mipango na ratiba ambapo katika kipindi cha utawala wa Qajar walikuwa na udhibiti kwa namna fulani, katika kipindi cha utawala wa Kifalme wa Kipahlavi wakawa na udhibiti na satwa hiyo hiyo ingawa kwa namna fulani satwa hiyo iliongezeka; hivyo basi jukumu lilikuwa ni kuwaandaa wasomi na wanafikra ambao watakuwa na mitazamo na fikra za Kimagharibi; mhusika kwa mfano ni Muirani kiasili, lakini kifikra ni Mfaransa, Muingereza na Mmarekani; matumaini na matarajio yake ni matumaini na matarajio ya Kimarekani; hatua na amali yake pia ni ya Kimarekani au Kiingereza; licha ya kuwa yeye kiasili ni Muirani (ana uraia wa Kiirani) na anaishi hapa nchini Iran; lakini kimtazamo na kifikra awe na fikra za Kimagharibi. Kwa hakika baadhi walifanya njama za kulea kizazi cha wasomi dhaifu waliojisalimisha kikamilifu kwa Magharibi, lakini si baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran. Leo hii mazingira ya kidini na kimaadili pamoja na usafi wa nafsi na umaanawi ni mambo ambayo yanashuhudiwa katika Vyuo Vikuu vya Iran na inatarajiwa kwamba, vyombo husika vifanye kazi kwa namna ambayo kila anayeingia kwenye mazingira ya Chuo Kikuu azidi kushikamana na mafundisho wa dini na maadili bora.
Kwa hakika mimi sitilii shaka na alama ya suali (mfumo jumla wa) Chuo Kikuu; uwepo wa wahadhiri waumini na watakasifu katika kipindi cha utawala wa Kitaghuti, kwa namna yoyote ile sitilii alama ya suali; vizuri, kulikuweko na watu ambao sisi tulikuwa tukiwafahamu; walikuwa watu wazuri na watakasifu sana; watu kama hao walikuweko baina ya wahadhiri na vile vile baina ya wanachuo walikuweko watu wa aina hiyo - ingawa kwa wanachuo kwa kiwango kidogo zaidi ikilinganishwa na wahadhiri - lakini kiujumla lengo la Chuo Kikuu lilikuwa namna hii; hivyo basi, wahadhiri hao walikuwa katika duara maalumu na hawakuwa na uwezo wa kuwa na taathira; na kwa muktadha huo, harakati ya Chuo Kikuu ilikuwa harakati ghalati na isiyo sahihi.
Watu ambao mtazamo wao ni ule wa mazingira ya kipindi kile wanadhani kwamba, kwenda Chuo Kikuu kunakwenda sambamba na suala la kutofungamana na maadili, akhlaqi, hijabu, usafi na utakasifu wa kidini na kimaadili. Kwa hakika hili ni jambo ambalo halina ukweli kabisa, mtazamo huu sio sahihi hata kidogo. Chuo Kikuu ni kitovu cha umaanawi; kwani elimu ni jambo la kimaanawi. Elimu - iwe elimu yoyote ile - ina thamani ya kimaanawi na thamani ya kiroho. Mazingira ya Chuo Kikuu ni mazingira ya ujana na mazingira ya kiumini. Katika nchi hii watu wetu ambao wameshikamana sana na dini wapo baina ya vijana wetu; watu wetu ambao ni wenye kujitolea mno pia nao wapo baina ya vijana; hivyo basi kuna sababu gani mazingira ya vijana ambao ni watu wa elimu yawe ni mazingira yasiyo ya kidini? Hapana, mazingira hayo (mazingira yanayotawala katika Vyuo Vikuu) ni ya kidini. Mimi ninataraji kwamba, mtu anayeingia katika Chuo Kikuu kama itakuwa kwamba, mfungamano wake na masuala ya dini ulikuwa dhaifu kabla ya kuingi katika Chuo Kikuu, basi mara baada ya kuingia katika mazingira yake, mfungamno wake na utekelezaji wake wa masuala ya kidini utaimarika na kuongezeka zaidi. Kwa hivyo basi malengo maalumu katika umaanawi na maadili ni jambo lenye itibari, kama ilivyo suala la malengo maalumu katika siasa, elimu na katika mambo yote ya maisha.
Vizuri, katika suala la malengo maalumu kuna nukta moja mbili hivi ambazo ninataka kuzizungumzia. Tusikosee kuhusiana na suala la kuwa na fikra na malengo maalumu na suala la ugomvi na ushari. Haya ni mambo mawili tofauti kabisa. Kuwa na fikra na malengo maalumu, hakuna maana ya kufanya uchokozi na ushari, bali inawezekana kama kufanikisha malengo maalumu na wakati huo huo mtu kushikamana vilivyo na kwa njia bora na mambo yake ya thamani na misingi yake mitukufu. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema katika Kitabu cha Qur'ani:
"wana nguvu mbele ya makafiri, na wanahurumiana wao kwa wao" ( Fat'hi 48:29). Lafudhi ya Kiarabu ya "Ashiddau" ni wingi wa neno la Kiarabu la "Shadidi" yaani ngumu na yenye nguvu na isiyopenyeka. Kila mwili ambao ambao ni imara na una nguvu na mgumu unapokutana na mwili mwingine huacha athari, lakini mwili ule mgumu wenyewe hauachiwi athari. Sote tuwe namna hii, yaani tuwe ni wenye nguvu na wagumu na imara na madhubuti. Hata hivyo kuwa na nguvu na madhubuti hakuna maana ya kuwa mtu mgomvi. Kuna wakati mtu anashindwa kudhibiti (kuzuia) hisia zake na wakati huo anataka kufanya jambo fulani. Kuna haja ya kudhibiti hisia na kujiepusha na kuchukua maamuzi ya pupa na chini ya hisia kali. Kipindi hiki ni zama zenu za hisia, kipindi cha ujana, sisi pia tulikuwa vijana wenye hisia kali, hivyo tunafahamu kipindi hiki ni kipindi cha aina gani. Hivyo kuna mahala hisia kali zipo, la msingi ni kudhibitiwa na kuzuiwa hisia hizo.
Tab'an, mimi ninashukuru sana jumuiya hizi za wanafunzi. Mwaka jana mimi au mwaka juzi nilisema katika kikao kama hiki nikiwahutubu wanafunzi ya kwamba, kwa nini hamuonyeshi msimamo katika masuala ya kijamii na hamuingii katika uwanja huu? Kwa bahati nzuri, katika kipindi hiki cha miaka miwili mitatu hivi ninaona wazi kuna misimamo ya wanachuo katika masuala mbali mbali, katika mazingira ya wanachuo na vijana wanachuo; vizuri, hili ni jambo zuri sana; hili ni jambo ambalo mimi ninalipongeza na kulitolea shukurani; isipokuwa kuna wakati kwa mfano jaalieni kwamba, kunajitokeza suala la Gaza; linajitokeza kundi la wanafunzi fulani na kusema kwamba, kumetokea hili na hili na kwamba, Wazayuni makhabithi wanafanya unyama dhidi ya watoto wa Kipalestina kwa kuwadondoshea mabomu hivyo twendeni tukawape somo; wanaondoka na kwenda uwanja wa ndege!, vizuri, kwa hakika hisia hizi ni hisia takatifu na za usafi wa nafsi. Mfano wa watu kama mimi ambao tumekaa kando na tunalitazama hili, kwa hakika mtu anatamani kufidia roho yake kwa ajili ya hisia kama hizi; kwa hakika hili ni jambo lenye thamani kubwa. Hii kwamba, Imam (Imam Khomeini radhiallahu anhu) amesema kwamba, "ninabusu mikono ya Mabasiji" mahala pake ni hapa. Wakati mtu anapoona kwamba, kijana fulani yuko nyumbani kwao na wakati wa msimu wa joto ana kiyoyozi na jokofu; na wakati wa msimu wa baridi ndani kwao kuna mashine na suhula za kutia joto nyumba, anakwenda Chuo Kikuu, anasoma na ana mafanikio, mara ghafla kunajitokea suala la Gaza na kumfikisha katika hatua ya mlipuko na hivyo hujitokeza na kusema, ninataka kwenda Gaza (na yuko tayari kuacha raha zote anazopata nyumbani kwao), hisia kama hii kwa hakika ni hisia ambayo ina thamani mno; lakini kwenda ni kufanya makosa.
Hisia ni nzuri, lakini hisia hii haipaswi kutufanya sisi tufunge safari na kuondoka kuelekea Gaza. Kwenda Gaza katika kipindi kile lilikuwa ni jambo ambalo haliwezekani na wala halikuwa jambo linaloruhusiwa, na hata kama lingekuwa linawezekana, isingeruhusiwa. Vizuri, hapa kunajitokeza hali ya mkinzano baina ya malengo maalumu na uhakika wa mambo pamoja na amri ambayo ilinukuliwa kwamba, ni kutoka kwa Kiongozi Muadhamu katika fikra za kijana huyu ambayo ilikuwa inawakataza wanafunzi wasiende Gaza. Hapana, kwa hakika hakuna mkinzano wowote ule. Hisia zile zilikuwa hisia nzuri tu; hivyo basi, ushiriki wa vyama vya wanachuo katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni kwenye masuala tofauti ya kijamii na kisiasa ni hatua nzuri na inayostahiki kupongezwa, lakini pamoja na hayo kuna baadhi ya maamuzi na hatua zilizochukuliwa na wanafunzi ambazo hazikuwa sahihi; kwani inabidi kuweko na maamuzi yanayotokana na uchunguzi wa kina na wa umakini wa hali ya juu na si hisia na hamasa. Kuchukua maamuzi katika hali ya hisia wakati mwingine hupelekea uamuzi huo kutokuwa sahihi.
Inabidi kutambua pia kuwa hakuna migongano wala ukinzani wowote baina ya wajibu wa wanachuo wa kutekeleza majukumu yao ya kufanikisha malengo matukufu na wakati huo huo kuzingatia maslahi ya nchi kupitia kutekeleza na kuheshimu sheria. Yaani inawezekana mtu akawa kijana mwenye hamasa na hisia kubwa zinazojenga na wakati huo huo akafanya mambo yake bila ya kugongana na masuala ya kuendesha nchi na maslahi ya taifa. Hivyo haipaswi kusemwa katu kwamba, Bwana ee, kuna mkinzano na mgongano daima baina ya uhakika na maslahi; hapana, kwani uhakika wenyewe ni moja ya maslahi na maslahi yenyewe ni moja ya uhakika. Endapo kutazama maslahi kutakuwa sahihi, ni lazima kuchunga maslahi; kwa nini haipaswi kuchungwa maslahi? Ni lazima kuona maslahi. Jaalieni kwamba, kwa upande wa msimamo wa mfumo tunapinga harakati fulani na kambi fulani kwa mfano ya Kitaghuti na majimui ya udikteta na uimla, hatuko pamoja nao na wala hatusaidii katika hilo. Mwenyezi Mungu anasema katika Kitabu Kitakatifu cha Qur'ani kwamba:
"Hakika nyinyi mna mfano mzuri kwenu kwa Ibrahim na wale walio kuwa pamoja naye, walipowaambia watu wao: Hakika sisi tumejitenga nanyi na hayo mnayoyaabudu badala ya Mwenyezi Mungu. Tunakukataeni; na umekwisha dhihiri uadui na chuki baina yetu na nyinyi mpaka mtakapo muamini Mwenyezi Mungu peke yake." (al-Mumtahinah 60:04).
Ni jambo lililo wazi kwamba, misimamo yetu kuhusiana na baadhi ya mirengo ya kisiasa ambayo leo iko duniani au katika eneo (Mashariki ya Kati) iko wazi; hata hivyo pamoja na kuwa misimamo ya Iran kuhusu mifumo hiyo iko wazi kikamilifu, lakini si sahihi kufuata hisia na hamasa katika jambo hilo na kusahau udiplomasia unaojulikana (uliozoeleka) ulimwenguni na ulioenea hivi sasa duniani. Yaani kazi ya kidiplomasia inapaswa kufanyika, isipokuwa muelekeo uwe ni huu.
Kama ambavyo maadui zetu wao wanafanya hivi. Maadui zetu wanafanya mambo katika uadui wao, lakini wakati huo huo wanafanya pia ada (zilizozoeleka) za udiplomasia. Tab'an, sisi hatuhadaiki katika ada na miamala hiyo ya kidiplomasia; tunafahamu vyema kwamba, nyuma yake kuna nini. Kwa msingi huo basi inabidi kutilia maanani, maana na ukubwa wa suala hilo zima la kuwa na malengo makuu matukufu na wakati huo huo kuchukua maamuzi na hatua mbali mbali kwa kujiepusha na misimamo mikali kwa kuzingatia uhalisia wa mambo na maslahi ya taifa. Inabidi kuzingatia wakati wote kwamba, kuwa na malengo makuu matukufu maana yake ni kushikamana na misingi na matukufu ya taifa sambamba na kuuathiri vizuri upande wa pili na mtu kutokubali kuharibiwa na wala kuathiriwa vibaya na upande huo.
Nukta nyingine ni ushiriki wa kivitendo na kifikra wa wanafunzi katika masuala mbali mbali ya nchi ambapo hili ni jambo la lazima. Ushiriki wa kifikra ni jambo la lazima; kushiriki kifikra kupitia kazi za kiutamaduni kwenye vyombo vya habari vya wanachuo na kutoa mitazamo na fikra na mawazo mazuri ni jambo linalowezekana, kama ambavyo inawezekana pia kufanyika mikusanyiko ya wanachuo iliyosimama juu ya misingi sahihi sambamba na kushiriki kivitendo katika harakati mbali mbali na kutumia fursa hiyo kutoa nadharia zenu kwa vyombo husika vilivyoko chini ya wizara - kama ni watu wa uchumi, toeni nadharia zenu kwa vyombo husika katika uga wa masuala ya kiuchumi; kama nyinyi ni watu wa masuala ya kiutamaduni, basi andikeni barua, toeni nadharia, mapendekezo na maoni yenu na mueleze mtazamo wenu - na vile vile mahudhurio na ushiriki wa kivitendo nalo ni jambo la lazima; kuna wakati inakuwa ni lazima mshiriki katika mijumuiko na mikutanio ya wanachuo. Kwa hakika kwa namna yoyote ile mimi sipingi na kukataa bali ninaunga mkono kwamba, inafaa kuweko baadhi ya mikusanyiko ya wanafunzi ambayo itajadili masuala mbali mbali, kwa mfano suala la Bahrain na kadhalika. Tab'an, ninapinga kuchukuliwa misimamo mikali katika mikusanyiko hiyo na ninapinga kuchukuliwa au kufanywa mambo ambayo hayajapimwa vizuri katika mikusanyiko hiyo. Kwa hakika, kuchukua maamuzi chini ya hisia kali za hamasa katika mikusanyiko kama hiyo kuna madhara mabaya, kwani yamkini kukafanyika makosa ya watu kadhaa na ghafla moja hilo likaungwa mkono na wanachuo wengine chini ya hamasa, mimi siafikiani na hili.
Sasa tiba ya hili ni nini? Nini kinapaswa kufanyika? Mimi binafsi ninadhani kwamba, ili kuepusha kuchukuliwa hatua na maamuzi ya namna hiyo kuna haja ya vyama vya wanachuo kuwa ni chombo kimoja cha kuchukua maamuzi na hatua mbali mbali na kuhakikisha kwamba, chombo hicho kinachukua maamuzi mamoja katika masuala tofauti kupitia mashauriano na uangalifu wa hali ya juu. Iwapo hilo litatendeka, basi kutaondoka uwezekano wa wanachuo kuchukua maamuzi na hatua zinazotokana na hisia kali na hamasa zisizo na umakini ndani yake. Kwa maana kwamba, kufanya hivyo kutapelekea maamuzi yanayochukuliwa kuwa ni ya kimantiki na yaliyopimwa vyema. Jaalieni kwamba, katika kadhia fulani ambapo nimetoa mifano kadhaa hapa, katika kadhia fulani itakuwa bora wanafunzi wafanye nini. Kundi la wanachuo hao ambao lina kipawa, likae chini na kutafakari kisha baadaye maamuzi yachukuliwe kwa sura ya pamoja yaani katika fremu ya mjumuiko wa kundi la wanachuo. Ieleweke na kubainishwa wazi kwamba, endapo mtu atakiuka hilo na kuchupa mipaka, kitakachotokea litakuwa jambo ambalo si katika maamuzi ya wanachuo na harakati ya wafunzi wa Chuo Kikuu.
Vizuri, mimi hapa nimenukuu kwamba, hakuna migongano wala ukinzani wowote baina ya wajibu wa wanachuo wa kutekeleza majukumu yao ya kufanikisha malengo matukufu na wakati huo huo kuzingatia maslahi ya nchi kupitia kutekeleza na kuheshimu sheria. Yaani inawezekana mtu akawa kijana mwenye hamasa na hisia kubwa zinazojenga na wakati huo huo akafanya mambo yake bila ya kugongana na masuala ya kuendesha nchi na maslahi ya taifa. Kwa msingi huo kwa mtazamo wangu, matarajio (waliyonayo watu) kwa wanachuo, sio matarajio makubwa kupita kiasi; bali inawezekana kuwa na matarajio kama haya kutoka kwa wanafunzi na wanachuo.
Vizuri, katika suala la maadili (akhlaqi) ninapenda kusema nukta hii pia - nilitaka kulisema na kulibainisha hili baadaye, lakini kwa kuwa nahofia muda yamkini ukatubana, nimeamua kulisema sasa hivi na kulitanguliza kwani ni miongoni mwa mambo ya kimsingi na muhimu kabisa - yaani kusema mambo bila ya kuwa na ujuzi wa kitu hicho, kusengenya na kutuhumu. Ninakuombeni nyinyi vijana azizi mlizingatie na kulipa umuhimu jambo hili. Kama ambavyo katika nyuga mbali mbali mnalipa uzito wa hali ya juu suala la utakasifu katika amali - mnaipa umuhimu ibada ya Sala na Saumu - basi ninakuombeni mlipe uzito wa hali ya juu pia hili suala la kujiepusha na kusengenya, kutuhumu watu na kusema mambo ambayo hamna elimu nayo. Endapo sisi tutamnasibisha mtu na kitu ambacho hajakifanya au hanacho, hii huwa ni tuhuma ya wazi kabisa. Endapo tutasema kitu ambacho hatuna elimu na ujuzi nacho; kwa mfano tetesi fulani - mtu fulani amesema jambo fulani naye amenukuu tu kutoka kwa mtu na kisha sisi kuja na kulikariri jambo hilo tena - kwa hakika kufanya hivi ni kusaidia kueneza uvumi na tetesi na kusema kitu pasina ya kuwa na elimu nacho. Kwa hakika kusema kitu bila ya kuwa na elimu nacho, lenyewe jambo hilo lina mushikili; Mwenyezi Mungu anasema: "Wala usiyafuate usiyo na ujuzi nayo." (al Israai 17:36). Neno " La taqif" lililotumika katika aya hii maana yake ni kwamba, usifuate kitu ambacho huna elimu au ujuzi nacho. Kufuata kulikokusudiwa hapa ni katika uwanja wa amali na vile vile katika uga wa maneno. Mwenyezi Mungu anaendelea katika aya hiyo kwa kusema:
"Hakika masikio, na macho, na moyo - hivyo vyote vitasailiwa" (al Israai 17:36).
Ushindani katika cheo na madaraka. Tab'an kuna kipindi fulani, vyama na taasisi zinazopigania malengo makuu matukufu za wanachuo zilikuwa zimetengwa, lakini hivi sasa hali si hiyo tena na inawezekana kukajitokeza suala la nyadhifa na uongozi kwa ajili ya baadhi ya majimui na wanachama wa taasisi hizo, hivyo nyinyi vijana mnapaswa kuwa macho na kuchukua tahadhari kubwa ili msije mkatumbukia kwenye mtego wa kujiweka mbali na malengo yenu matukufu. Moja kati ya maeneo ya kuteleza sisi wanadamu, ni katika masuala haya ya ushindani wa cheo na madaraka ambapo wakati mwingine huwaangusha watu wenye nguvu na satwa. Tab'an, mimi ninaamini kwamba, vijana kama ambavyo wana nguvu kuliko wazee, wana irada, uwezo na udhibiti wa nafsi pia kuliko wazee.
Endapo kijana atafanya hima na idili namna hii, awe na shauku na msukumo na kisha atake kufanya kazi, basi bila shaka kijana huyu atakuwa imara na madhubuti katika uga wa kimaanawi na kiroho na katika uwanja wa kupambana na nafsi kuliko hata watu wazee na wenye umri mkubwa kama sisi, na hata kiuwezo, bila shaka uwezo wake utakuwa ni mkubwa zaidi. Kwa msingi huo basi, nyinyi mnaweza. Sasa hapa nataka kusema machache kuhusiana na vita laini. Kwa hakika hapa kuna nukta kadhaa ambazo zimeziandika, ingawa naona wakati wa adhana nao unakaribia; na sitaki wakati (wakati wa Sala) utupite. Kutokana na itikadi zenu nzuri ninaona wamo kati yenu maafisa wa vita laini na ni kwa sababu hiyo, ndio maana nasisitiza kuwa, liangalieni kwa umakini na kwa tahadhari kubwa lengo kuu la adui katika vita vyake laini, yaani (lengo ni) kutaka kuwalazimisha wananchi na viongozi nchini mwetu wabadilishe misimamo na mahesabu yao kwa faida ya adui. Hii leo kwa bahati nzuri, hatuna vita vya kijeshi; na endapo itafikia wakati tukawa na vita vya kijeshi bila shaka watakaokuwa mstari wa mbele (kupigana na adui) ni vijana (wa taifa hili).
Hii leo kuna suala la vita laini; sio leo, bali vita hivi vimekuweko kwa muda wa miaka thelathini sasa. Katika vita laini, kitu ambacho kinapaswa kuzingatiwa ni hiki kwamba, katika vita laini na vita vya kisaikolojia - ambapo vita vya kisaikolojia ni sehemu ya vita laini - lengo la adui ni kubadilisha mahesabu ya upande wa pili. Vita laini sio kama vita vya kijeshi. Katika vita vya kijeshi, lengo la adui ni hili kwa mfano, ni kuja na kushambulia kambi za kijeshi za nchi husika na kuisambaratisha au kuzikalia kwa mabavu ardhi za nchi hiyo.
Katika vita vya kiuchumi lengo la adui ni kusambaratisha na kutokomeza miundo mbinu ya kiuchumi. Katika vita laini, lengo sio mambo haya; mambo haya baadhi ya wakati ni wenzo tu (wa maadui) kwa ajili ya lile lengo la vita laini. Katika vita laini lengo ni kile kitu ambacho kiko katika mioyo yenu, katika fikra zenu na katika akili (bongo) zenu; yaani irada yenu (ndiyo yenye kulengwa na adui katika vita laini). Adui anataka irada yenu ibadilike. Tab'an, haya sio maneno ya siri.
Mwanzoni (maadui) hawakuwa wakiyasema (wazi) haya, lakini (hivi sasa) ni muda sasa ambapo maaduyi zetu wanayasema haya na kuyatamka bayana na kinagaubaga. Maadui wanasema wazi kuwa, lazima wafanye mambo yao kwa namna ambayo itawafanya Wairani kubadilisha misimamo na mahesabu yao yaani wawafanye Wairani wafike mahala wahisi kuwa si kwa faida yao kuendelea kusimama kidete na imara mbele ya waistikbari na mabeberu wa dunia, hivyo maafisa wa vita laini nchini wanapaswa kulitambua vizuri lengo hilo la adui na kupambana nalo kwa njia sahihi na inayofaa. Moja ya njia za kupambana kwa njia sahihi na lengo hilo la adui ni kuongeza kiwango cha welewa na mwamko na kwa hakika hii ni nukta muhimu sana. Kwa hakika sisi tumechagua mahesabu na njia fulani. Mapinduzi ya Kiislamu yamekuja na kuleta mabadiliko makubwa na ya kimsingi katika nchi hii; yakabadilisha mfumo wa kifalme na kuufanya kuwa utawala wa wananchi, yaani utawala ambao ndani yake wananchi wana sauti; yakabadilisha utawala tegemezi uliokuwako na kuleta utawala unaojitegemea; yakabadilisha (yaani Mapinduzi ya Kiislamu) hali ya kubaki nyuma (kimaendeleo) na kuleta ustawi na maendeleo - kama ambavyo mnaona - mapinduzi haya yakabadilisha ile hali ya kudhalilika na kuleta hali ya kujiamini na kujihsi kuwa na izza na utukufu; haya ni mambo na kazi ambazo zimefanywa na Mapinduzi. Vizuri, maadui zetu, yaani vile vyombo vyenye nguvu vya kimaada ambavyo kabla ya kupata ushindi Mapinduzi ya Kiislamu hapa nchini, vilikuwa na satwa na udhibiti katika uchumi, katika siasa za nchi, utamaduni wa taifa hili pamoja na vyanzo vya utajiri wa nchi na vilikuwa na sauti na udhibiti hata katika maamuzi ya viongozi wa nchi hii, sasa vimekasirishwa mno na hali ya hivi sasa inayotawala hapa nchini; vinataka kubadilisha hali hii? Adui huyu kwa sasa afanye nini? Kwa hakika yeye amebakiwa na njia moja tu ambayo ni kuwafanya viongozi na wananchi wa taifa hili wafikie mahala na kuhisi kwamba, kuendeleza njia hii sio kwa maslahi wala manufaa yao. Kwa hakika adui anataka kuyatia kwa nguvu mambo haya katika fikra zenu; anataka mimi na nyinyi tufikie natija hii kwamba, sio maslahi kusimama mkabala na Marekani, sio kwa manufaa yetu kusimama kwa ajili ya kukabiliana na ubeberu ; kwa hakika (sisi tunasema kwamba) kuna haja ya kusimama kidete na kupambana sambamba na kudumisha muqawama dhidi ya mabeberu; kuna haja pia ya kuacha kusema baadhi ya mambo.
Kuna kipindi kulikuweko baadhi ya watu ambao walikuwa wakisema, Bwana wee achaneni na kadhia ya Israel, achaneni na kadhia ya Palestina, achaneni na kadhia ya uadilifu katika kiwango cha dunia na acheni kuyaunga mkono mataifa yenye kupigania uadilifu, achaneni na haya; yanakuhusuni nini nyinyi? Jizingatieni nyinyi wenyewe na mambo yanayokuhusuni. Kwa hakika hii ndio ile hali ya kubadilisha mahesabu. Ukweli wa mambo ni kuwa adui analitaka hili. Mkabala na hili kuna haja kwa maafisa wa vita laini kusimama kidete na kufanya muqawama. Muqawama na kusimama kidete huku kufanyike vipi? Kwanza kabisa ongezeni maarifa yenu.
Ndugu zanguni wapendwa! Msiongeze kiwango chenu cha maarifa kwa kutegemea mitandao ya Intaneti, weblog, magazeti, mitandao ya kisiasa na vitu kama hivyo, kwa hakika kiwango chenu cha maarifa sio mambo haya. Kwa hakika mimi nimesladhi na kuburudika na maneno yaliyozungumzwa hapa leo; maneno yaliyosemwa hapa ni maneno mazuri, yanayoonyesha ukomavu; kwa hakika hili ni jambo linalofurahisha mno. Mimi ninataka kusema kwamba, fanyeni hima katika uwanja huu kadiri mnavyoweza. Ongezeni kiwango chenu cha maarifa na jitahidi kadiri mnavyoweza kushikamana na mafundisho ya Qur'ani Tukufu na maandishi ya wanafikra kama vile Shahid (Ayatullah) Mutahhari na shakhsia wengine wakubwa na muhimu katika masuala ya dini, na vifanyeni vitu hivyo kuwa chanzo kikuu cha kuongeza welewa na kiwango chenu cha maarifa. Alhamdulilahi hii leo watu kama hao wanapatikana leo katika Vyuo Vikuu vya Kidini (Hawza), fanyeni juhudi na muwafahamu.
Hii leo mafudhalaa vijana wapo katika Chuo Kikuu cha Kidini (Hawza) ambao wanaweza kusaidia majimui ya vijana katika Vyuo Vikuu; kama ambavyo kuna kazi nzuri ambazo zimekuwa zikifanyika. Kiwango cha maarifa na ufahamu wa dini kiongezeke; hizi ni miongoni mwa kazi ambazo bila shaka ni lazima zifanyike. Kwa uoni na mtazamo wangu ile kazi ambayo ni muhimu kufanyika, ni mutwalaa wa Kiislamu. Usimamiaji na kuzingatia masuala na hali ya nchi. Kutazama mambo kwa kutaka ufafanuzi na kisha kutafuta ukweli sanjari na kukosoa. Niliwahi kusema huko nyuma kwamba, hakuna tatizo katika ukosoaji.
Hakuna tatizo kutazama mambo kwa mtazamo wa ukosoaji; isipokuwa la muhimu ni kufanya ukosoaji ambao ni sahihi na wa mahala pake; yaani usifanyike ukosoaji ambao si wa kiadilifu na ambao hauzingatii ukweli na uhakika wa mambo. Kwa hakika kuongeza muda wa kutwalii na kusoma athari za Kiislamu, kuyaangalia kwa tabasuri na mtazamo mpana masuala ya nchi, kukosowa kiinsafu, na kusimamia mambo bila ya kuchoka tena kiuadilifu, ni miongoni mwa majukumu makuu ya wanachuo na vyama na taasisi za wanafunzi wa Vyuo Vikuu nchini Iran.
Wakati mwingine tunashuhudia ukosoaji usio wa kiinsafu. Sasa nyinyi kwa namna fulani mna msimamo mkali na ni vijana na bila shaka mtu hana matarajio sana; lakini kwa wale ambao ni watu wazima na wenye mvi, kuna wakati mtu anaona kwamba, wanafanya mambo ambayo si ya kiinsafu; katika kubainisha mambo na wamekuwa wakizingatia katika kuzungumza juu ya huyu na yule.
Tafadhalini, kuweni makini na mjichunge kusije kukatokea hali ya kutokuweko insafu. Kwa msingi huo, ukosoaji wa kuendelea, usimamizi mtawalia wenye uwiano na hali ya nchi pamoja na uongozi ni miongoni mwa kazi ambazo ni lazima kufanywa; tab'an, hayo yanapaswa kufanyika yakiambatana na akili na umakini, bila ya kufurutu ada; lakini wakati huo huo kuweko na mtazamo wa ukosoaji mambo. Kwa uoni na mtazamo wangu ni kuwa, hizi nazo ni kazi ambazo ni za lazima kufanywa. Kuweko mawasiliano baina ya vikundi na jumuiya za wanachuo na ulimwenguni wa Kiislamu nazo ni kazi ambazo ni za lazima kufanywa ambapo mmoja wa ndugu aliyezungumza hapa amelizungumzia hilo; nami naliunga mkono hili kikamilifu.
Hii leo katika ulimwengu wa Kiislamu kupitia mwamko wa Kiislamu, majimui na jumuiya za wanachuo - sasa ni jumuiya na vikundi vya aina, yamkini vyote vikawa sio vya aina moja - ni majimui amilifu, huko nyuma pia majimui hiyo ilikuwa amilifu; baadhi yake vimekuwa na nafasi muhimu na ya kuzingatiwa katika harakati hii. Hali ya mambo nchini Iran inaongeza matumaini nyoyoni mwa watu, hivyo jitahidini kadiri mnavyoweza kuhakikisha kuwa mwanga huu unaong'ara wa matumaini unazidi kupata nguvu na kung'aa zaidi ndani ya nafsi zenu na ndani ya nyoyo za wananchi. Vyombo mbali mbali vya sekta tofauti vinapaswa kukusaidieni katika uga huu; tab'an, sisi pia tutaagiza hilo lifanyike.
Mmoja wa ndugu hapa amesema kwamba, imepita miezi mitano tangu kuundwa Baraza Kuu la Mawasiliano ya Mawasiliano ya Mtandao; lakini hadi sasa baraza hilo halijafanya kazi yoyote. Kwa hakika mimi napenda kusema kwamba, kadhia hii, sio kitu cha miezi minne au mitano; kadhia hii ni jambo la miaka kadhaa. Kazi hii ambayo sisi tumeanza kuifanya, matarajio yangu pia mimi ni kwamba, tuone natija yake baada ya miaka minne au mitano, Inshallah. Sasa hii kwamba, ninyi mnatarajia kwamba, baada ya miezi mitano au sita, mtu aone masuala ya intaneti na mawasiliano ya mtandao wa kompyuta yamefanyiwa mabadiliko na kujitokeza kanali ya intaneti ya taifa na kadhalika, hapana, hili ni jambo ambalo haliwezi kuwa na natija kwa kipindi kifupi namna hii; vyovyote itakavyokuwa ni lazima kutumia suhula hizi hizi ambazo zipo.
Ndugu zanguni wapendwa! Msingi mkubwa wa kazi hii ni matumaini. Mimi ninapenda kuwaambia kwamba; miongoni mwa kazi ngumu zinazofanywa dhidi yangu na yenu ni kuua hali ya matumaini katika moyo na ujudi wetu. Hivyo fanyeni hima na kuhakikisha kwamba, mnahuisha hali ya matumaini katika ujudi wenu. Inawezekana kupata ustawi, maendeleo na kusonga mbele kwa kuwa na matumaini. Fanyeni kadiri mnavyoweza ili kuwasha mwenge wa matumaini katika nyoyo zenu na katika nyoyo za mnaozungumza nao. Tab'an, yawe ni matumaini ya mahala pake na sio matumaini yasiyo ya mahala pake; yaani matumaini ambayo yanatufanya sisi kuelekea katika uhakika wa kweli.
Ewe Mwenyezi Mungu! Kwa haki ya Muhammad na Aali za Muhammad, kwa mapenzi, huba na rehma Zako tunakuomba uwape hidaya na uongofu wanachui na ushushe hidaya katika mkusanyiko huu na kwa taifa zima la Iran. Ewe Mwenyezi Mungu; kile ambacho tumekisema na tumekisikia kifanye kiwe kwa ajili Yako na ukiweke katika njia Yako na uwape baraka. Yafanye maisha yetu yawe ni maisha ambayo yanaridhiwa na Walii Asr, Imam wa zama (roho zetu ziwe fidia kwake).
Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

 
< Nyuma   Mbele >

^