Skip to content

Habari

Habari
Hifadhi

Risala na Barua

Matini
Hifadhi

Kumbukumbu na Simulizi

Kabla ya Mapinduzi
Baada ya Mapinduzi

Sauti na Taswira

Picha
Sauti
Video
Miongozo za Kiongozi Muadhamu kwa Mnasaba wa Idul Fitr 1433 Hijria Chapa
19/08/2012

Ifuatayo ni matini kamili ya hotuba ya Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aliyoitoa mbele ya hadhara ya viongozi wa Mfumo na mabalozi wa nchi za Kiislamu katika siku ya Idul -Fitri

Bismillahir Rahmanir Rahim

Ninatoa mkono wa Idi wa Sikukuu hii adhimu kwenu nyinyi nyote waheshimiwa hadhirina, wageni wapenzi, mabalozi wa nchi za Kiislamu, wananchi wote wa taifa adhimu na la watu waumini la Iran na kwa umma wote wa Kiislamu katika nchi zote duniani na ulimwenguni kote.
Suala muhimu ni kwa sisi kuelewa thamani ya fursa hizi. Mwenyezi Mungu Mtukufu ameifanya Sikukuu adhimu ya Idul - Fitri kuwa njia ya kupatia izza, hazina, heshima na utukufu kwa umma wa Kiislamu na Mtume Mtukufu mkubwa wa shani; و لمحمّد صلّى اللّه عليه و ءاله ذخرا و شرفا و كرامة و مزيدا "Na kwa ajili ya Muhammad SAW hazina na heshima na utukufu na mazidadi." Huu ni wenzo wa kuzidisha izza na heshima kwa umma wa Kiislamu na kwa Mtume Mtukufu mkubwa wa shani. Hii inategemea ni vipi sisi Waislamu tutazitumia fursa hizi na minasaba hii. Mataifa ya Kiislamu yanaweza kuufanya mwezi wa Ramadhani na Idul - Fitri kuwa wenzo wa kupatia izza na ngazi ya kukwea kuelekea kwenye utukukaji wa kimaanawi na kimaada na izza ya duniani na Akhera. Inapasa tuwe macho, inapasa kuzitumia fursa hizi.
Kwa miaka na miaka, mataifa ya Kiislamu yalikuwa chini ya ubeberu na udhalimu wa Waistikbari wa dunia. Vita vya kimataifa vilivyotokea baina ya madola ya Kiistikbari ya dunia vilianzia Ulaya; wakoloni wa dunia walivaana wao kwa wao lakini wakayatumbukiza mataifa ya Waislamu na mataifa ya eneo hili kwenye mazonge na matatizo yaliyotokana na vita hivyo. Ilikuwa ni baada ya vita hivyo pia ndipo kilipojitokeza kizaliwa hatari na angamizi cha Kizayuni katika eneo letu nyeti, baina ya nchi za Kiislamu na katika kitovu cha Ulimwengu wa Kiislamu. Ilikuwa ni baada ya vita hivyo pia ndipo ulipowekwa msingi pogo na wenye kasoro wa Umoja wa Mataifa, Baraza la Usalama na nchi zenye haki ya kura ya veto. Yaani mikono ile ile na makucha yale yale yaliyotapakaa damu ambayo ndiyo yaliyoanzisha vita angamizi yalitaka baada ya vita hivyo hatamu za mamlaka ya ulimwengu ziwe mikononi mwao na udhibiti wa eneo hili nyeti, muhimu, lililojaa neema chungu nzima na ambalo lingekuwa kitovu cha umoja kwa Ulimwengu wa Kiislamu uwe mikononi mwao, na hivyo ndivyo yalivyofanya. Sisi tulikuwa tumejisahau; mataifa ya Waislamu yalikuwa usingizini; kwa hivyo yalishambuliwa; hatima yao iligubikwa na wingu la matatizo makubwa na tata ambayo yameitinga hadi hivi sasa. Sisi tulighafilika na kujisahau. Katika kipindi fulani, viongozi wa nchi za Kiislamu walijisahau na kuhadaiwa na hila ya madola hayo.
Leo inahisika na inaonekana kwamba wingu hilo la mghafala na hali ya kujisahau limo katika hali ya kusafika ndani ya akili za watu wa nchi za eneo na za mataifa ya Waislamu; hili ni jambo linalopasa kuthaminiwa. Eneo letu nyeti, kaskazini mwa Afrika na eneo la Magharibi mwa Asia - ambalo Wazungu waliamua kwa utashi wao kulipa jina la "Mashariki ya Kati" na ambalo ni mhilimili nyeti wa kitovu cha dunia - leo kwa baraka za Mwamko wa Kiislamu limo katika hali ya kubadilisha na kuainisha hatima ya mustakabali wake. Tunapaswa kuielewa fursa hii na kuithamini. Tusiruhusu fursa hii muhimu na nyeti ipotee. Suala la Quds Tukufu na Palestina madhulumu yako kwenye katikati ya kadhia hizi na kwenye kitovu cha matukio ya Mashariki ya Kati.
Masuala na matatizo mengi yaliyolitinga eneo letu hili nyeti yametokana na kuwepo dondandugu hili la saratani la Uzayuni ambalo mikono iliyotapakaa damu ya madola makubwa inataka kulihifadhi kwa uwezo wake wote. Wamarekani wanaeleza kinagaubaga, na madola mengine ya kibeberu duniani nayo pia yanatamka waziwazi kwamba, yameifungamanisha hatima yao na hatima ya utawala wa Kizayuni. Hili lina madhara kwao.
Kwa baraka za Mwamko wa Kiislamu, leo suala la Palestina limegeuka kuwa suala kuu la Ulimwengu wa Kiislamu; msiruhusu fursa hii adhimu na ya kipekee ipotee na kufichika chini ya njama na hila za maadui wa Waislamu na maadui wa umma wa Kiislamu. Palestina ni suala kuu na la msingi. Kwa muda mrefu wananchi wa mataifa ya Kiislamu wanazitathmini serikali zao kulingana na misimamo yao katika kadhia ya Palestina. Tab'an mashinikizo ya udikteta, Uistikbari, mabavu na ukandamizaji hayakuwa yakiruhusu matakwa ya wananchi wa mataifa yadhihirike na kujulikana. Katika matukio ya mwaka huu ya Siku ya Quds na maandamano ya wananchi wa mataifa ya eneo na licha ya kuchukizwa Wazayuni na watakufa na chuki zao, wananchi hao wameweza kubainisha yaliyomo nyoyoni mwao, na inshallah kadiri siku zinavyosonga mbele hali hiyo itazidi na itakuwa na msisimko mkubwa zaidi.
Bila ya shaka adui hajakaa na wala hatokaa hivi hivi tu; njama za adui zimekuwa tata zaidi. Viongozi wa nchi za Kiislamu, serikali za nchi za Kiislamu, shakhsia wenye vipawa maalumu - iwe ni wenye vipawa vya kisiasa, wenye vipawa vya kiutamaduni, wanafikra au maulama wa dini - wote hao wana jukumu la kuwabainishia wazi ukweli wananchi wa mataifa. Leo maadui wanatumia tena silaha ile ile ya zamani, ambayo sikuzote imekuwa mikononi mwa madola ya Kiistikbari na ya kiimla na kutumiwa kama wenzo wa kuyashinda mataifa; silaha hiyo ni ya kuzusha hitilafu; hitilafu kati ya viongozi wa nchi, baina ya serikali na baina ya mataifa kwa kutumia visingizio mbalimbali. Njama ya sikuzote na ya kudumu ya Uistikbari ni kuchochea hitilafu; au kufufua ukabila na hisia za utaifa kati ya wananchi wa mataifa; kukuza hitilafu ambazo ni kitu cha kawaida kuwepo kwa upande wa lugha, asili, rangi ya ngozi na kati ya madhehebu. Hii ndio kazi ya Uistikbari; hii ndio kazi uliyoifanya kila mara. Ilishasemwa tokea hapo zamani kuwa:"Farakanisha utawale". Leo hii wanaitekeleza njama hii hii. Tunapaswa tuzinduke, tunapaswa tujitambue na kuwa macho; serikali na wananchi.
Kinyume na ukweli halisi, wanaficha kile ambacho ndio hatari kubwa na ndio tishio hasa kwa eneo hili bali hata kwa wanadamu wote, nao ni Uzayuni. Leo serikali za Magharibi pia zinatumiwa vibaya na Wazayuni; nazo pia zinaonja machungu ya vitimbi vya vituo hivi vya nguvu za utajiri na mamlaka; kwa upande wa mataifa ya eneo inajulikana ni balaa gani limewafika kutokana na Wazayuni. Mauaji haya ya kigaidi ni kazi yao wao, hizi hitilafu za mifarakano kati ya mataifa ni kazi yao wao ambayo wanaifanya kwa kutumia nyenzo mbalimbali; kwa hivyo inabidi tuzinduke. Hatari hii, ambayo ndiyo hatari hasa kwa eneo wanaificha, wanaififiliza na kuifanya ndio hali halisi; badala yake wanayakuza kwa kutumia uwongo yale ambayo si hatari na kuchochea hitilafu baina ya Waislamu. Kwa hivyo inapasa tuwe macho na makini. Uarabu na Uajemi, Ushia na Usuni, madhehebu tofauti na rangi za ngozi mbalimbali zisisababishe hitilafu baina yetu;

  و جعلناكم شعوبا و قبائل لتعارفوا

"Na tumekujaalieni kuwa ni mataifa na makabila ili mjuane." Kipimo kikuu ni kitu kingine kabisa. Uwepo ushindani baina ya mataifa ya Waislamu katika kuutekeleza Uislamu, katika kujenga udugu, katika kufanya juhudi za kuwahudumia wananchi wao na katika kukabiliana na irada na matakwa ya madola makubwa yakiongozwa na Marekani. Kila pale mataifa ya Waislamu yatakapoona siasa za Marekani na siasa za Kizayuni zinalenga kuzusha hitilafu yajue kwamba hitilafu zina madhara kwao, hivyo yasikubali kuhadaiwa.
Matukio ya eneo letu ni matukio muhimu; mataifa yameamka. Kutokana na athari za mwamko huo nchi kadhaa za Kiislamu na mataifa kadhaa ya Waislamu yameweza kuipindua hali iliyokuwa ikipendelewa na Uistikbari. Wananchi wa mataifa hayo wameufuta, wameuchoma moto na kuutokomeza uwekezaji wa miaka na miaka uliokuwa umewekwa na Marekani katika nchi za Misri, Tunisia na baadhi ya maeneo mengine. Huu ndio mwamko na unapaswa kudumishwa na kulindwa. Inapasa kipimo kiwe ni kuangalia adui hasa na wa dhahiri wa Uislamu na Waislamu yuko upande gani; upande huo ni wa batili, na upande mkabala na huo ndio upande wa haki; hiki ndicho kipimo; tunatakiwa tuzingatie kipimo hiki. Na kwa maoni yangu kielelezo cha wazi kabisa cha mkabala huo ni hili suala la umoja na maelewano baina ya mataifa. Wao wanataka kuzusha hitilafu kati ya mataifa ya Kiislamu; tunachotakiwa sisi ni kuelewa kwamba hitilafu hizi ni kitu batili; hili ni jambo linalokatazwa na aya za Qur'ani; mifarakano, hitilafu na kukabana koo wenyewe kwa wenyewe na baina ya mataifa ya Kiislamu hiyo ni sumu yenye kuangamiza; haya ni mambo tunayopaswa kujiepusha nayo.
Tumwombe msaada Mwenyezi Mungu Mtukufu. Fursa hii ya mwezi wa Ramadhani ilikuwa fursa muhimu mno ambayo inshallah wananchi wa mataifa ya Kiislamu wawe wameitumia vizuri. Fursa ya Idul - Fitri ni fursa adhimu. Fursa ni kitu kinachomalizika na kupita kwa kasi kama yapitavyo mawingu hivyo inapasa kuzitumia kila zinapopatikana.
Ewe Mola! Yape mataifa ya Kiislamu taufiki ya kuzitumia kwa namna inayostahiki fursa unazowajaalia. Ewe Mola! Liwafikishe taifa hili madhulumu kuleta umoja na mshikamano ndani ya umma wa Kiislamu. Tupe taufiki ya kutekeleza jukumu na wajibu wetu katika njia hii.
Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh

 
< Nyuma   Mbele >

^