Skip to content

Habari

Habari
Hifadhi

Risala na Barua

Matini
Hifadhi

Kumbukumbu na Simulizi

Kabla ya Mapinduzi
Baada ya Mapinduzi

Sauti na Taswira

Picha
Sauti
Video
Khutba za Sala ya Idul Fitr 1433 Hijria Chapa
19/08/2012

Ifuatayo ni matini kamili ya hotuba ya Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aliyotoa mbele ya hadhara ya waumini waliohudhuria ibada ya Sala ya Idul - Fitri ya tarehe 19/8/2012
Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh

Kwa jina la Allah Mwingi wa rehema Mwenye kurehemu

Na hamdu na sifa zote njema ni za Mwenyezi Mungu Mola wa ulimwengu. Ninamhimidi na ninamwomba msaada na ninamwomba maghufira na ninatawakali kwake. Na ninamsalia na kumtakia rehema na amani kipenzi chake, mteule wake na mbora wa viumbe wake, mtunza siri zake na mfikishaji ujumbe wake, mtoa bishara ya rehma zake na mwonyaji wa adhabu yake, Bwana wetu na Mtume wetu Abul Qasim al Mustafa Muhammad, na Aali zake wema, watoharifu na wateule walioongoka na waongozaji kuelekea uongofu hususan Baqiyyatullah (Imam Mahdi) katika ardhi. Na uwarehemu (Ewe Allah) viongozi wa Waislamu na waongozaji wa wanyonge na watetezi wa waumini.
Ninawausia akina kaka na akina dada wote wapenzi kumcha Mwenyezi Mungu na ninatoa mkono wa kheri na baraka wa Sikukuu adhimu ya Idul -Fitri, ambayo ni siku ya rehma, siku ya maghufira na siku ya malipo na thawabu kwa waumini, kwa wafanya mema na kwa watu ambao walifanya amali njema kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na katika njia ya Mwenyezi Mungu na ambao walizikurubisha nyoyo zao kwa Mwenyezi Mungu Mrehemevu na Msamehevu. Tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia kuufikia mwezi mwengine wa Ramadhani na Sikukuu nyengine ya Idul-Fitri; tunapaswa kuienzi na kuithamini neema hii ya Mwenyezi Mungu.
Alhamdulillah mwezi wa Ramadhani wa mwaka huu, kutokana na habari tulizokuwa tukipata kutoka huku na kule na kutokana jinsi mtu alivyokuwa akishuhudia, ulikuwa mwezi wa baraka nyingi; nyoyo zilimuelekea Mwenyezi Mungu na kuzingatia mambo ya kheri na ya umaanawi. Wananchi wa matabaka mbalimbali waliojumuika pamoja kwenye mikusanyiko ya kidini, katika visomo vya Qur'ani na katika mikesha yenye baraka na kheri nyingi ya Lailatul Qadr waliifanya anga na mazingira ya nchi yawe na hali ya umaanawi wenye taathira ya kudumu. Hili ni jambo linalopasa kuenziwa na kuthaminiwa na kumshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa taufiki hiyo.
Lakini vilevile katika upande mwengine wa kadhia hiyo ambao ni wa kuangalia masuala ya Ulimwengu wa Kiislamu na masuala ya umma wa Kiislamu, wananchi walionyesha harakati ya kuvutia na yenye kung'ara; harakati hiyo ilikuwa ni ya Siku ya Quds; waliienzi na kuiadhimisha kumbukumbu adhimu iliyoachwa na Imam Muadhamu (Khomeini) kwa kulitetea na kuliunga mkono taifa madhulumu la Palestina na kuliunga mkono suala la msingi na muhimu la Ulimwengu wa Kiislamu. Walishiriki kwenye maandamano katika hali ya hewa ya joto na midomo iliyokauka kwa Saumu; ni mahala pake kutoa shukurani. Tunawashukuru wananchi wote wa Iran kutokana na harakati hii waliyoonyesha mahala pake na kwa wakati unaofaa ambayo inshallah, bila ya shaka itakuwa na athari kubwa katika Ulimwengu wa Kiislamu.
Mwaka huu mataifa mengine pia yaliungana na kwenda sambamba zaidi na taifa la Iran kuliko ilivyokuwa katika miaka iliyopita. Katika baadhi ya nchi, ambako kutokana na nguvu na udhibiti wa mabaki ya tawala za kitaghuti watu walikuwa wakizuiliwa kuonyesha hisia zao kuhusu suala la Palestina, alhamdulillah mwaka huu wananchi wameweza kujitokeza uwanjani katika nchi hizo; na hii ni harakati ambayo inshallah itaendelea. Tumwombe Mwenyezi Mungu Mtukufu atakabalie ibada za wananchi wetu wapenzi katika mwezi huu na kuzipa thamani na itibari kwa rehema, qabuli na uraufu wake mahsusi. Ni kama ilivyoelezwa katika dua ya Sahifatus-Sajjadiyyah ya kwamba:

 يا من يجتبى صغير ما يتحف به و يشكر يسير ما يعمل له ... يا من يدنو الى من دنا منه و يا من يدعو الى نفسه من ادبر عنه

"Ewe Mwenye kukikubali kidogo anachopewa na kulipa kwa kichache anachofanyiwa...Ewe Mwenye kumkaribia yule anayejikurubisha kwake na ewe Mwenye kumwita kwake yule aliyempa mgongo."
Hii ni dua ambayo Imam Sajjad AS alikuwa akiisoma na kufunza watu waisome katika siku kama ya leo, siku ya Idul-Fitri.
Pigeni hatua mbele kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu, naye Mwenyezi Mungu Mtukufu atakukurubisheni kwake. Wale watu walioipa mgongo haki, umaanawi, Mwenyezi Mungu na dini, Mwenyezi Mungu anawaita kutokana na uraufu na rehma zake; hizi ni fadhila na rehema zake Mola. Vijana wetu wapenzi wajitahidi inshallah kuitunza kwa ajili yao wenyewe athari ya nuru ya umaanawi waliyopata katika mwezi huu; hii ni akiba ya kuitunza kwa ajili ya umri wao wote au kwa uchache hadi Idul-Fitri ijayo na mwezi wa Ramadhani ujao.
Tuyatunze na kuyahifadhi matunda tuliyopata ya kujenga ukuruba na Qur'ani, kujielekeza kwa Mwenyezi Mungu, kumdhukuru na kumtaja Mwenyezi Mungu, kuhudhuria kwenye hafla ambazo Mwenyezi Mungu Mtukufu anapenda waja wake wahudhurie - ziwe ni zile za ndani ya nchi yetu au zinazohusiana na Ulimwengu mpana wa Kiislamu, jamii yetu na umma wa Kiislamu, na Mwenyezi Mungu Mtukufu atatia baraka zake.
Ewe Mola! Literemshie rehma na baraka zako taifa hili na mataifa yote ya Waislamu. Ewe Mola! Lipe ushindi taifa hili azizi na pia upe ushindi umma wa Kiislamu dhidi ya maadui zake. Ewe Mola! Tuzidishie siku baada ya siku uhusiano wetu huu wa kimaanawi na wa kinyoyo na masuala ya umaanawi na ya kiroho.

بسماللّهالرّحمنالرّحيم
قل هو اللّه احد. اللّه الصّمد. لم يلد و لم يولد. و لم يكن له كفوا احد

Kwa jina la Allah, Mwingi wa rehema Mwenye kurehemu.
Sema: Yeye Mwenyezi Mungu ni wa pekee.
Mwenyezi Mungu Mkusudiwa.
Hakuzaa wala hakuzaliwa.
Wala hana anayefanana naye hata mmoja.


Khutba ya Pili

Kwa jina la Allah Mwingi wa rehema Mwenye kurehemu.

Hamdu na sifa zote njema ni za Mwenyezi Mungu Mola wa ulimwengu. Na rehema na amani zimshukie Bwana wetu na Mtume wetu Muhammad na Aali zake watoharifu. Na rehema na amani zimshukie Ali, Amirul Muuminin na Siddiqah Taahirah, siti wa wanawake wa ulimwengu wote, na Hassan na Hussain, wajukuu wa rehema na maimamu wa uongofu, na Ali Ibn Hussain, na Muhammad Ibn Ali, na Jaafar Ibn Muhammad, na Mussa Ibn Jaafar, na Ali Ibn Mussa, na Muhammad Ibn Ali, na Ali Ibn Muhammad, na Hassan Ibn Ali na Imam wa mwisho aliye hai al Mahdi. Rehema zako ziwashukie wao wote. Na rehema zako ziwashukie viongozi wa Waislamu na watetezi wa wanyonge na waelekezaji wa waumini kuelekea uongofu. Ninakuusieni waja wa Mwenyezi Mungu kumcha Mwenyezi Mungu.
Ninawausia akina kaka na akina dada wote waliopo katika mjumuiko huu adhimu wa Sala kuchunga taqwa na kumcha Mwenyezi Mungu. Katika hotuba hii nitazungumzia masuala mawili matatu yanayohusu nchi yetu na jamii yetu au yanayohusu umma wa Kiislamu. Kwa upande wa yale yanayohusu nchi yetu, lenye umuhimu wa kwanza kabisa ni tukio chungu na la msiba mkubwa wa tetemeko la ardhi lililowafika baadhi ya wananchi wenzetu. Japokuwa tukio hili limetokea kwenye sehemu moja ya nchi na ni kundi moja la watu ambao wamedhurika, lakini ni la majonzi kwa watu wote nchini. Mtu analijua hili na analihisi, na tajiriba pia inaonyesha kuwa wananchi wetu hawajawahi abadani kuonyesha hali ya kutojali wakati matukio kama haya yanapojiri katika sehemu fulani nchini; katika eneo hili pia alhamdulillah wananchi walijitokeza, na moyo huu unapasa uendelezwe. Tukio hili ni tukio chungu; uharibifu mkubwa umetokea; yametokea maafa ya roho pia, na viongozi husika wametoa takwimu za maafa na matukio yaliyojiri. Wanachopaswa kufanya viongozi husika na wananchi wote kwa ujumla ni kusaidia katika kutekeleza jukumu hili lililoko mabegani mwetu.
Alhamdulillah kazi nzuri imefanyika; na hilo mtu anajionea wakati anapofuatilia masuala kwa karibu. Na wakati anapowauliza watu wenyewe walioathiriwa ndipo anapoelewa kuwa kazi nzuri imefanyika; lakini kazi ingali inaendelea kufanywa; majukumu yaliyopo mbele yetu ni mazito zaidi na makubwa zaidi; inshallah viongozi waweze kufuta kikamilifu athari za tukio hili.
Mbali na kufanya hivyo walitumie suala hilo kama wenzo ili eneo hili inshallah liyaanze maisha yake kwa kufungua ukurasa mpya na wenye kung'ara. Na kwa ujenzi mpya utakaofanyika huko kutokana na juhudi za wananchi wenyewe na hima ya viongozi pamoja na ushirikiano uliopo baina ya pande mbili, inshallah wafute kikamilifu kumbukumbu za majonzi na huzuni za eneo hili.
Suala jengine ni la Siku ya Quds. Siku ya Quds ni harakati aliyoianzisha Imam wetu muadhamu (Khomeini) na alhamdulillah siku baada ya siku na mwaka baada ya mwaka, harakati hii inaendelea kwa ubora na uchangamfu zaidi. Hii ni harakati yenye maana kubwa na ya kina. Haya si maandamano tu; ni damu inayozunguka katika siku hii ndani ya mishipa ya damu ya umma wa Kiislamu. Licha ya hatua ya watu wanaotaka suala la Palestina na taifa la Palestina lisahaulike, suala hili linazidi kupata uhai zaidi siku hadi siku na litaendelea kuwa hivyo. Viongozi wa nchi za Kiislamu wana majukumu mazito mabegani mwao. Tunatumai kuwa inshallah Mwenyezi Mungu atawahidi na kuwaongoza viongozi wote katika kutekeleza lile ambalo ni jukumu lao na kuwasaidia ili waweze kuyatekeleza majukumu haya.
Bila ya shaka masuala ya Ulimwengu wa Kiislamu katika kipindi hiki yana hali isiyo na mfano. Matukio yaliyojiri katika Ulimwengu wa Kiislamu ni matukio ya kustaajabisha, yenye kutoa mtikisiko na kuainisha njia ya kufuatwa na umma wa Kiislamu katika mustakabali. Ni matumaini yetu kwamba inshallah, kama ambavyo hadi sasa wananchi wa mataifa ya eneo hili wameweza kufanya kazi kubwa, na viongozi nao wameweza kufanya kazi inayostahiki, muelekeo na mwenendo huu utaendelea, na maadui wa umma wa Kiislamu - ambao kadiri siku zinavyosonga mbele wanatekeleza njama tata zaidi na ambao kwa uwezo wao wote na nguvu zao zote wanajiingiza katika medani hii kutokea kila upande - hawatoweza kuishinda hima na bidii ya umma wa Kiislamu; na bila ya shaka yoyote hawatoweza kuishinda. Zama mpya zimeanza, hali mpya imejitokeza katika Ulimwengu wa Kiislamu, na hali hii inshallah itaweza kuleta taathira kidogo kidogo kwa maisha ya mataifa yote duniani.
Tujitahidi tusifanye makosa katika kuhakiki na kuelewa kwetu matukio. Tuelewe kwamba Marekani na Uzayuni ni maadui wa umma wa Kiislamu; viongozi wa tawala za kijabari ni maadui wa umma wa Kiislamu. Kama tutawaona wanafuata muelekeo mmoja katika mahali fulani tujue kwamba muelekeo huo ni muelekeo batili, ni muelekeo potofu, kwa hivyo tusifanye makosa katika kuhakiki. Wao katu hawayaonei uchungu mataifa ya Waislamu; wanafanya uharibifu kadiri wanavyoweza na wanafanya hujuma za kukwamisha michakato ya ufanyaji mambo. Leo haya makelele - ambayo kwa hakika ni wao ndio wanaoyaanzisha, japokuwa baadhi ya wakati yanakaririwa kutokea vinywani mwa baadhi ya watu waliojisahau - ya hitilafu za kimadhehebu, hitilafu za kikabila, hitilafu za rangi na za lugha, ni wao ndio wanaozikuza ilhali mambo haya hayako katika Uislamu; انّ اكرمكم عند اللّه اتقيكم yaani "Hakika aliye mtukufu zaidi kati yenu kwa Mwenyezi Mungu ni huyo aliye mchamngu zaidi katika nyinyi." Watu wote ni kitu kimoja, watu wote ni ndugu. Hivyo inatupasa sote tuwe macho, tuwe na uoni mpana, tufumbue macho yetu na wala tusifanye makosa katika kuhakiki mambo.
Ewe Mola! Tunakuomba kwa jaha ya Muhammad na Aali zake Muhammad uifikishe kwenye kheri na saada harakati hii adhimu ya umma wa Kiislamu. Wafanye wawe dhalili maadui wa umma wa Kiislamu.

 بسماللّهالرّحمنالرّحيم
والعصر. انّ الانسان لفى خسر. الّا الّذين ءامنوا و عملوا الصّالحات
و تواصوا بالحقّ و تواصوا بالصّبر

Kwa jina la Allah, Mwingi wa rehema Mwenye kurehemu. Naapa kwa zama! Hakika binaadamu bila ya shaka yumo katika hasara. Ila wale walioamini na wakatenda mema, wakausiana kwa haki na wakausiana kusubiri.
Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.

 
< Nyuma   Mbele >

^