Skip to content

Habari

Habari
Hifadhi

Risala na Barua

Matini
Hifadhi

Kumbukumbu na Simulizi

Kabla ya Mapinduzi
Baada ya Mapinduzi

Sauti na Taswira

Picha
Sauti
Video
Hotuba ya Kiongozi Muadhamu mbele ya Rais na Baraza la Mawaziri Mwanzoni mwa Wiki ya Serikali Chapa
23/08/2012

Ifuatayo ni Hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika mkutano na Rais na Baraza la Mawaziri kwa mnasaba wa kuanza Wiki ya Serikali tarehe 23/8/2012

Kwa jina la Allah Mwingi wa rehema Mwenye kurehemu

Naona muda uliosalia sio mwingi; hivyo inabidi nifupishe yale ninayotaka kuyaeleza. Ninakushukuruni kwa maelezo ya ufafanuzi mliyotoa. Ni matumaini yangu kuwa inshallah yale mliyoyapanga na mliyokusudia kuyafanya yataweza kuthibiti kutokana na ufatiliaji wenu; inshallah hivyo ndivyo itakavyokuwa.
Mnasaba huu umefuatana na kuchanganyika na kumbukumbu ya mashahidi wetu wapenzi, shahidi Rajai na shahidi Bahonar na vilevile shahidi Araqi, ambao ni shakhsia wenye majina yanayong'ara. Kwa hakika kudumisha kumbukumbu ya majina ya mashahidi hawa ni kudumisha misingi ya Mapinduzi na utukufu wa kufa shahidi. Mnasaba huu aidha ni fursa kwetu ya kutoa shukurani kwa kazi zinazofanywa na serikali, iwe ni zile wanazofanya mamudiri na viongozi waandamizi au zile zinazofanywa na vyombo vyote vya serikali kwa ujumla wao. Bahati nzuri leo kuna juhudi zinazofanywa kwa ushirikiano wa pamoja. Fursa hii ya Wiki ya Serikali inatupa fursa sisi ya kutoa shukurani kwa juhudi na kazi hizo. Kwa kweli hii ni fursa hata kwenu nyinyi wenyewe pia; na si fursa ya kutoa ripoti tu na kazi zilizofanywa ili wananchi wapate kuelewa ukweli wa mambo - ambalo bila ya shaka hilo pia ni jambo la lazima - lakini mbali na hilo hii ni fursa ya kujitathmini wao wenyewe viongozi wa serikali; kuamua kwa dhati kuchunguza na kutathmini kazi nzuri na kazi dhaifu walizofanya na kuelewa yale yaliyowafanya wapige hatua na hivyo kuyapa nguvu zaidi, na vilevile kuyaelewa na kuyaondoa yale yaliyozorotesha kazi na kuleta udhaifu ambayo athari zake zinaonekana waziwazi katika jamii na katika maisha ya watu. Inapasa muuchukulie mnasaba huu wa Wiki ya Serikali kuwa ni fursa kwenu, na hasa kwa vile huu ni mwaka wa mwisho wa serikali hii.
Mimi ningali ninakumbuka katika kikao tulichofanya katika mnasaba wa kwanza wa Wiki ya Serikali na jamaa ambao wengi wao wako hapa nilisema kwamba fursa zinapita kwa kasi mithili ya umeme na upepo. Na ndio mnaona sasa sehemu kubwa ya wakati wa fursa hizi nzuri na za muda mrefu imepita; umebakia mwaka mmoja tu. Tab'an mwaka mmoja pia ni fursa kubwa. Watu wasihisi kwamba ni kazi gani tunayoweza kufanya katika mwaka huu mmoja uliosalia; isifikiriwe hivyo, katika mwaka huu huu mmoja kuna kazi nyingi na zenye umuhimu mkubwa mnazoweza kufanya. Mwaka huu wa mwisho wa serikali yenu ni mwaka muhimu pia; ni mwaka wenye umuhimu mkubwa mno, kwanza kwa kuzingatia mazingira ya kimataifa na mazingira yaliyopo - yaani nyinyi mnakabiliana na utumiaji mabavu wa madola ya Kiistikbari yanayotumia nguvu na uwezo wao wote kwa tamaa kwamba huenda yataweza kukulazimisheni mlegeze msimamo na kukubali kushindwa, ambapo na nyinyi pia inalazimu mtumie nguvu na uwezo wenu wote ili kuweza kuondoa dhana hii batili na potofu ndani ya fikra za adui - na vilevile mwaka huu una umuhimu mkubwa mno kutokana na kuwa mwaka wenu wa mwisho. Ukweli ni kwamba katika mwaka huu wa mwisho nyinyi mnataka kukitia jalada, kukitayarisha na kukikabidhi kitabu hiki kikubwa na kilichosheheni cha huduma za utumishi na utendaji wa serikali. Yaani inavyopasa hasa mwaka huu, kama hatutosema kwamba uchapaji kazi ufanyike kwa hima na bidii zaidi, basi bila ya shaka katika mwaka huu wa mwisho inabidi kusiwepo na aina yoyote ya uzembe na ulegevu katika ufanyaji kazi.
Bahati nzuri nchi imo katika hali ya kusonga mbele kimaendeleo - mbali na mtazamo usio na shaka wa takwimu tunazotoa sisi wenyewe - lakini hata wachunguzi wa kimataifa pia wanasema hivyo; wanakiri na kukubali kwamba nchi yetu imo katika hali ya kusonga mbele kimaendeleo katika nyanja mbalimbali. Bila ya shaka wako baadhi ya watu wanaojitia shaka, na si sawa kuwa na hali ya shaka na hilo halitokani na tathmini sahihi.
Maadui zetu wamo kuchukua hatua mpya, na kukabiliana na hatua hizo kunahitajia tadbiri na mikakati mipya; hili linapaswa kuzingatiwa kila mara. Baadhi ya jamaa hapa wameashiria kwamba wakati maadui wanapochukua uamuzi fulani sisi pia tunajipanga na kuchukua hatua. Sawa kabisa, hiyo ni kazi nzuri sana; lakini lililo bora zaidi ni kwamba kabla upande wa pili haujachukua uamuzi, nyinyi mtabiri na kukisia yale utakayoyafanya. Chukulia mfano wa tatizo la kuhamisha fedha zinazotokana na mauzo ya mafuta. Ilipasa muwe mmekadiria hapo kabla; au kuhusu tatizo la uuzaji na ununuzi wa mafuta na uhamishaji mafuta, bima na masuala mengine kama hayo, ilipasa tuwe tumeyatabiri yote hayo tokea hapo kabla. Inabidi muandae tangu kabla njia za kukabiliana nayo. Hivi sasa pia ni hivyohivyo. Yaani isidhaniwe kwamba adui ameamua kutoendeleza uadui wake; isidhaniwe hivyo, wanatafuta njia nyengine. Madamu njia walizotumia hazikuwa na tija bila shaka yoyote wataamua kutafuta njia nyengine - ambazo bila shaka hata na hizo pia hazitofika popote - nyinyi pia anzeni kukadiria na kujiweka tayari mapema.
Kuna maelezo yametolewa hapa, na hapo kabla pia yaliwahi kuzungumziwa mbele yangu, kwamba kuna ulazima wa kuwepo uchukuaji maamuzi ya pamoja serikalini juu ya masuala ya uchumi. Mimi nakubaliana kikamilifu na jambao hili; bila shaka yoyote katika uchukuaji maamuzi makuu, katika kuamua juu ya masuala ya msingi - ambapo kwa hivi sasa ya msingi zaidi kati ya yote hayo ni masuala ya uchumi; na hasa yale yanayohusiana na maisha ya wananchi na mashinikizo ambayo adui anataka yawakabili wananchi - inapasa kuwepo msimamo wa pamoja wa uchukuaji maamuzi; tab'an makusudio ya uchukuaji huo wa maamuzi ya pamoja ni ndani ya serikali; yaani watu wote walioko katika vitengo mbalimbali vya serikali watoe mashirikiano kwa Rais na wajihisi kuwa wana jukumu la pamoja - na maana yake ni kwamba kuwepo na uratibu na mashauriano ya pamoja - ndani ya serikali na kuchukua maamuzi ya pamoja. Kuhusiana na nukta hii suala la kujihisi kuwa na jukumu la pamoja linapasa kupewa uzito hasa ndani ya serikali. Katika kazi yoyote inayofanywa na Wizara fulani, mawaziri wote na viongozi wengine wanaoshiriki kwenye vikao vya Baraza la Mawaziri wanatakiwa wajihisi kuwa ni washiriki na wanachangia katika uamuzi unaopitishwa au hatua inayochukuliwa. Kama itakuwa hivyo hapo ndipo kazi zitakuwa zinafanyika kwa uratibu na maelewano; hakutotokea hitilafu katika utendaji, ufahamu wa masuala wala katika utoaji takwimu.
Uwezo na vipawa vyote aidha vinapaswa vitumike na kufanyiwa kazi. Nchi yetu ina uwezo na vipawa vizuri; ndani ya serikali kuna watu wenye vipawa na uwezo mzuri na pia nje ya serikali. Kuna wakati huwa ninawaona baadhi ya viongozi wa vitengo wanaomba msaada wa fikra kwa watu walioko nje ya taasisi za serikali; hili ni jambo zuri; zidisheni kufanya hivyo kwa kuvitumia vipawa hivyo. Kuna watu wenye uchungu, hamu na shauku ya kutoa ushirikiano na kufanya kazi bega kwa bega na serikali; itumieni nguvukazi ya watu hao; hao ni sehemu ya vipawa vya nchi. Bahati nzuri ndani ya serikali pia kuna watu wenye vipawa na uwezo mkubwa.
Kuna nukta za mafanikio na pia za kasoro. Wakati tunapoangalia na kutoa tathmini ya ujumla juu ya mafanikio na kasoro tunafadhilisha kutanguliza mafanikio; lakini hii haimaanishi kwamba kasoro zilizopo tusiziondoe. Katika kipindi chote hiki cha miaka kadhaa kuna kazi nyingi za ujenzi zimefanyika nchini hususan katika maeneo ya mbali, katika sekta mbalimbali; kwa kweli hizo ni kazi muhimu; huu ni muelekeo muhimu sana ulioonyeshwa katika utendaji wa serikali. Kuanzia suala hilo mpaka kwenye maendeleo makubwa yaliyopatikana katika nyanja za sayansi na teknolojia. Maendeleo haya yaliyopatikana kwa kipindi cha miaka kadhaa tu katika nyanja za sayansi na teknolojia ni ya kuzingatiwa sana.
Hali iko hivyo hivyo pia katika kuinua nafasi ya nchi katika uga wa siasa za nje na masuala ya kimataifa. Leo katika uga wa siasa nje uzito na uzani ilionao nchi yetu ni tofauti na ilivyokuwa miaka kadhaa kabla yake. Sasa tumekuwa na taathira katika masuala mbalimbali; hili ni jambo muhimu. Tumekuwa na taathira pia katika matukio yaliyojiri - suala ambalo linahitajia mjadala wake mbali - na kwa maoni yangu hilo pia lina umuhimu mkubwa.
Suala jengine linaloingia kwenye nukta za mafanikio na ambalo kwa maoni yangu linapasa kuwekewa mkazo ni suala la kudhihirika zaidi thamani za Mapinduzi. Katika kipindi cha miaka hii tangu serikali ya tisa na ya kumi ziingie madarakani hadi hii leo, bahati nzuri misingi ya Mapinduzi, thamani tukufu za Mapinduzi na masuala ambayo Imam (Khomeini) alikuwa akiyausia ambayo tulijifunza kutokana na Mapinduzi yamedhihirika na kujiakisi kwa uwazi kabisa: Suala la viongozi kuishi maisha ya watu wa kawaida, kupiga vita Uistikbari na pia kujivunia na kuyaonea fahari Mapinduzi. Tumewahi kupita katika kipindi ambapo jina la Mapinduzi, mielekeo ya Mapinduzi na masuala yanayohusiana na hayo yalikuwa yamepuuzwa; kuna watu walikuwa wakijaribu kuyaonyesha hayo kuwa ni vitu vyenye thamani hasi kwa kutoa matamshi na kuandika makala. Bahati nzuri leo hali haiko hivyo, ni kinyume kabisa na hivyo. Muelekeo jumla wa wananchi na viongozi nchini ni wa harakati ya Kimapinduzi, ni wa kufuata dira ya Mapinduzi, thamani pamoja na misingi ya Mapinduzi. Inafaa mzingatie suala hili, kwani hii ni moja ya sababu zinazowafanya wananchi waipende serikali, yaani wananchi wanazipa umuhimu thamani hizi tukufu. Suala la kushajiisha uadilifu, suala la kuishi maisha ya watu wa kawaida na kujiweka mbali viongozi na vitu vya anasa hayo ni mambo yenye umuhimu mkubwa.
Juhudi zinazofanywa na serikali ili kujenga mawasiliano na wananchi na juhudi kubwa mno za uchapaji kazi ambazo bahati nzuri zinaonekana kufanywa ndani ya serikali, hizo ni hatua nzuri. Tab'an mzingatie pia kwamba juhudi zenu hizi nyingi mno mnazofanya zinapasa ziambatane na hali ya ubora pamoja na kutimiza ahadi ya kile mnachoahidi kufanya; mtilie mkazo juu ya suala hili. Bila ya shaka, na inajulikana kwamba mnachotaka nyinyi wenyewe ni kuweza kutekeleza kile mnachokisema - hakuna shaka yoyote juu ya hilo - lakini mtilie maanani sana nukta kwamba kila kinachotoka kwenu kama ahadi, wananchi wanatake waone kimetekelezwa katika muda ule ule ulioahidiwa. Kama kuna kazi mia moja mmeahidi kuzifanya, hata kama mtatekeleza tisini lakini kama kumi zitasalia, hilo litatia doa katika fikra za wananchi. Lile ambalo mtu anahisi kuna uwezekano halitotekelezeka alieleze kwamba huenda litafanyika, asiseme kwamba ana uhakika na yakini kuwa litafanyika. Kwa maoni yangu hili ni jambo muhimu sana.
Kila mwenye kuangalia mambo anahisi na anaona kwamba njama za maadui za kukabiliana na Jamhuri ya Kiislamu zimeonegzeka zaidi katika miaka ya hivi karibuni na hasa katika miaka hii sita saba iliyopita na hususan katika miaka hii miwili mitatu iliyopita. Kwa maoni yangu kuna sababu mbili tatu zenye taathira nazo ni kwamba kama tutaelewa sababu ya adui kufanya hivyo, tutaweza kufahamu vizuri zaidi jinsi ya kuratibu mipango yetu. Kwa mtazamo wangu moja ya sababu za uadui huu ni haya maendeleo yenu; yaani wanataka kuzorotesha maendeleo haya. Jamhuri ya Kiislamu ni hatari kwa mfumo wa Uistikbari duniani kutokana na msimamo wake wa kutetea Uislamu, msimamo wake wa kutetea mfumo wa utawala wa Kiislamu unaotokana na wananchi na kutokana na kupinga na kukataa kwake kwa hoja Demokrasia ya Kiliberali. Kila nyinyi mnavyosonga mbele hatari hiyo inakuwa kubwa kwao. Kwa hivyo wanataka kuzuia maendeleo hayo.
Sababu ya pili ya uadui huu ni kuhuika na kupata uhai tena sha'ar za Mapinduzi. Wakati sha'ar za Mapinduzi zinapofifia, zinapofichika, bila shaka wao hufurahia sana jambo hilo na hata nyuso zao hukunjuka na kuridhika; lakini kadiri nyinyi mnavyohuisha zaidi sha'ar za Mapinduzi nyuso zinakunjana zaidi na zinaonyesha kuchukizwa zaidi; hili ni jambo la kawaida.
Sababu nyengine ni haya matukio ya eneo; huu Mwamko wa Kiislamu na yale matukio yaliyojiri katika eneo letu ni kadhia yenye umuhimu mkubwa mno. Kwa maoni yangu ukubwa na uzito wa tukio hili lililojiri kaskazini mwa Afrika na katika eneo letu la Kiislamu bado watu wengine hawajaufahamu sawa sawa; ni tukio adhimu na kubwa mno lililojiri. Nyuma ya pazia la kadhia hii kuna mkono wa qudra ya Mwenyezi Mungu.
Ikiwa katika mazingira haya, Iran iliyopo itakuwa nchi isiyosumbua wala kushughulishwa na jambo, ikawa na sha'ar zake hizi hizi zilizopo na ikawa inafanya kazi zake hizi hizi inazofanya na maendeleo yake haya haya yanayohisika waziwazi, kama watakuja watu kutoka nchi hizo (yalikotokea mageuzi) na kujionea viwanda vilivyoko, vyuo vikuu, vituo vya utafiti, hali za maisha ya watu, masoko yaliyojaa bidhaa na serikali inayofanya kazi zake bila shida yoyote, ni wazi na bila shaka yoyote watasema hiki ni kigezo na mfano mzuri wa kuigwa. Wao wanataka hili lisitokee. Wanataka kusiwepo hii hali ya Jamhuri ya Kiislamu kuwa kigezo cha kuigwa. Yaani waisababishie matatizo ya kila aina Jamhuri ya Kiislamu ili zile nchi yalikotokea mageuzi na kuingia katika awamu mpya zisiifanye Iran kuwa kigezo cha kufuata katika kuendeleza harakati yao.
Bila ya shaka kuna baadhi ya watu wanaoandika na kuhoji katika magazeti, katika kurasa za intaneti na katika majukwaa mbalimbali ya uzungumzaji kwamba kwa nini sisi tumejitafutia maadui duniani mpaka watu wakawa na uadui na sisi kiasi hiki! Kwa maoni yangu huku ni kubwabwaja. Haya yanayosemwa hayatokani na uhakiki na uchambuzi makini. Si hivyo kabisa, kuwepo uadui ni jambo la kutarajiwa. Wakati Imam muadhamu (Khomeini) alipokuwepo uadui uliokuwepo ulikuwa mkubwa mno, na hiyo ilitokana na misimamo thabiti ya Imam. Kadiri misimamo yetu inavyokuwa dhaifu zaidi na sisi tukalegeza misimamo zaidi bila ya shaka nyuso zao zitajionyesha kuwa na bashasha zaidi. Na tab'an wataendelea kutuandama zaidi. Yaani wanapoonyesha uso wa bashasha na tabasamu wanafanya hivyo ili waweze kutuandama zaidi na kuyatia mkononi maeneo yetu na kutuzuia tusisonge mbele kufikia malengo yetu. Kadiri sisi tunapokuwa makini zaidi na kuwa na azma thabiti zaidi katika harakati yetu wao huchukia na kukunja nyuso zao. Tab'an hadi sasa katika kipindi hiki cha miaka thelathini na tatu hawajaweza kutusimamisha na inshallah baada ya hapa pia hawatoweza. Kwa hivyo bahati nzuri hivi ndivyo hali ya nchi ilivyo. Bila ya shaka mazonge yapo, kasoro zipo na matatizo yapo ambayo inapasa tuyashughulikie; lakini kwa ujumla ni kwamba mtu anapoangalia anaona harakati ya nchi ni harakati ya kusonga mbele kuelekea kwenye maendeleo.
Kwa maoni yangu sehemu kubwa ya matatizo ni ya masuala yanayohusu hali ya maisha ya matabaka ya kati na ya wanyonge katika jamii. Hali hii inatokana na nini? Mimi hapa sitaki kufanya uchambuzi. Bila shaka yoyote zipo kasoro; na kasoro hizo inatakiwa mtu azizungumze na mamudiri wenyewe. Hakuna ulazima wowote kwa watu wanaomiliki majukwaa ya vipaza sauti, mimbari na vitu kama hivyo kutaka kuorodhesha hadharani kasoro zilizopo; kwa sababu kubainisha kasoro katika anga ya jamii hakutatui tatizo lolote. Kama kuna kasoro inapasa kuieleza kwa mtu mwenyewe mwenye kasoro hiyo; lakini athari na taathira za kasoro hizo ni wazi kuwa zinashuhudiwa dhahiri; hizo mtu anaweza kuzieleza.
Kile ambacho kwa maoni yangu kina umuhimu ni kutatua matatizo ya kiuchumi yaliyopo yanayoyakabili matabaka dhaifu. Sehemu moja ya matatizo hayo yanatokana na ughali wa maisha. Sisi hatuna uhaba wa bidhaa nchini; bahati nzuri bidhaa mbalimbali zinazohitajiwa na wananchi zinapatikana kwa wingi; lakini suala lililopo ni ughali wa maisha na kupungua uwezo wa kununua; hili inapasa mlitafutie dawa; jukumu lake liko kwa vitengo mbalimbali vya kiuchumi; yaani vitengo vya tume kuu ya uchumi na pia vitengo vya utendaji wa kiuchumi - kama Wizara ya Viwanda, Madini na Biashara, Wizara ya Jihadi ya Kilimo, na vitengo vinginevyo - ambavyo vinapaswa kushughulikia kwa dhati suala hilo. Watu ambao ni wataalamu wa uchumi, wawe ni wale waliomo serikali au nje ya serikali wananieleza kwamba suala hili linahusiana na kuongezeka kwa matumizi ya fedha taslimu; yaani ongezeko la matumizi ya fedha taslimu ndio sababu kuu ya tatizo hili. Hili hatulisikii kutoka kwa watu walioko nje ya serikali tu bali hata watu waliomo serikalini pia tunapowauliza wanatueleza na kuripoti haya haya. Inapasa mtafute njia ya kudhibiti ongezeko la matumizi ya fedha taslimu. Hili linajulikana wazi; ikiwa katika kukabiliana na matumizi ya fedha taslimu kutakuwapo na uzalishaji, kutakuwapo na bidhaa na ikawa hakuna uhaba, matumizi ya fedha taslimu hayasababishi mushkili wowote. Lakini kama haitokuwa hivyo, yaani ikiwa matumizi ya fedha taslimu yatakuwa ya kiwango kikubwa zaidi kuliko uzalishaji bidhaa wa ndani au kama hayatokuwa wa namna sahihi kulingana na bidhaa zinazoingizwa nchini, bila shaka yatasababisha matatizo.
Mambo yanayosababisha kuwepo ongezeko la matumizi ya fedha taslimu ni mengi. Hizi ruzuku za fedha taslimu zinazotolewa - ambalo ni jambo lenye faida kwa matabaka kadhaa - zenyewe zinasababisha kuongezeka matumizi ya fedha taslimu. Hizi kazi za ujenzi mnazofanya - ambazo taathira zake chanya zinachukua muda kuonekana - bila ya shaka yoyote nazo pia zinasababisha ongezeko la matumizi ya fedha taslimu. Hili suala la ujenzi wa nyumba za kuishi wa 'Maskani za Mehr' lililozungumziwa, au hii miradi ambayo haijakamilika mnayoipa uzito zaidi wa kuikamilisha ambayo ni kazi nzuri na ya lazima inayofanywa na serikali, hiyo pia inasababisha kuongezeka matumizi ya fedha taslimu. Inabidi mtafute njia ya kulishughulikia suala hili. Nyinyi ni watu wenye ujuzi, ni watu wenye tajiriba, mikono yenu ina nafasi ya kufanya kazi; kwa hivyo tafuteni njia ya ufumbuzi wa masuala haya. Matumizi haya ya fedha taslimu yaliyoongezeka yaelekezeni kwenye mambo ya msingi yatakayosaidia kurahisisha mahitaji ya wananchi, kwa mfano katika suala la uzalishaji.
Sekta ya binafsi inapasa kusaidiwa. Tulipozungumzia "Uchumi wa Muqawama", uchumi huo una masharti kadhaa na misingi kadhaa; moja ya masharti yake ni hili suala la kuwategemea wananchi; hizi Sera za Ibara ya 44 ya Katiba inapasa zifuatiliwe kwa kutiliwa mkazo, kupewa umuhimu na kutekelezwa kwa umakini mkubwa; hii ni mojawapo ya kazi za msingi kwenu. Baadhi ya wakati huwa ninawasikia viongozi wenyewe wanasema kwamba sekta ya binafsi haijitokezi kutokana na uwezo mdogo ilionao. Kama ni hivyo inabidi mfikirie la kufanya ili kuiwezesha sekta ya binafsi, iwe ni kwa kutumia mabenki, kwa kupitisha kanuni na sheria zinazohitajika au kwa njia nyengine yoyote ile inayolazimu kutumiwa ili sekta ya binafsi, sekta ya wananchi iweze kuwa amilifu na yenye harakati. Kwa vyovyote vile Uchumi wa Muqawama maana yake ni sisi kuwa na aina ya uchumi ambao utaendeleza mwenendo wa ukuaji uchumi wa nchi na vile vile utauwezesha uchumi huo kutoathirika na kudhurika kirahisi. Yaani hali ya uchumi wa nchi na ya mfumo wa uchumi iwe ya namna ambayo inapokabiliwa na hila na vitimbi vya maadui ambavyo vitaendelea kuweko daima na kwa sura tofauti, kuathirika kwake na kuyumba kwake kuwe ni kwa kiwango kidogo. Moja ya masharti yake ni huu utumiaji wa vipawa na uwezo wa serikali na wa wananchi; tumieni fikra, mitazamo na njia za utendaji zinazotolewa na wataalamu na pia zitumiwe rasilimali zilizopo.
Inapasa wananchi wapatiwe fursa ya kweli. Tab'an katika maelezo yaliyotolewa na jamaa yameashiriwa baadhi ya haya matukio yanayotokana na kuwafatilia mafisadi wa uchumi na ufisadi wa uchumi. Kwa kweli haiwezekani kufanya kazi sahihi na yenye taathira ya kiuchumi pasina kupambana na ufisadi wa kiuchumi; kwa kweli jambo hili haliwezekani. Hata miaka michache nyuma wakati nilipozungumzia kadhia hii na kuwaeleza viongozi nchini baadhi ya masuala nilitilia mkazo juu ya nukta hii kwamba isifikiriwe kuwa tutaweza kupata uwekezaji wa mitaji, vitega uchumi vya wananchi na kazi safi inayotokana na wananchi pasina kupambana na ufisadi wa uchumi; na isidhaniwe pia kwamba kupambana na ufisadi wa uchumi kutasababisha kupata ushiriki mdogo wa wananchi na uwekezaji wa wananchi; sio hivyo kabisa, kwa sababu watu wengi wanaotaka kuingia kwenye medani ya uchumi ni watu wanaofanya kazi safi na isiyo na mazonge, ni watu safi na wazuri; ni sawa kwamba anaweza kutokezea mtu mmoja wawili ambao si watu safi na wazuri. Inapasa mchunge kwa kuwa na macho makali na muangalie kwa uoni wa kina na wa mbali ili wasije wakatokezea watu wanaodai kwamba wanataka kuanzisha ajira na kuandaa nafasi za kazi wakatumia suhula za benki pasina kuanzisha ajira na fursa za kweli za kazi. Inapasa nyinyi muwe makini juu ya suala hili na pia vyombo vya mahakama pia vinapaswa kuwa makini. Kwa maoni yangu kuna ulazima mkubwa wa kuwepo ushirikiano baina ya serikali na vyombo vya mahakama katika suala hili.
Nguzo nyengine ya Uchumi wa Muqawama ni kutoa himaya na msukumo kwa uzalishaji wa taifa; wa viwanda na kilimo. Takwimu zilizotolewa na jamaa hapa ni takwimu nzuri; lakini kwa upande mwengine ndani ya serikali yenyewe, viongozi husika wanatueleza kwamba baadhi ya karakhana zina matatizo na katika baadhi ya mwahala kuna karakhana zimefungwa - kuna ripoti mbalimbali zinazotufikia na nyinyi wenyewe pia mnatoa ripoti; yaani ninataka kusema kwamba ninazo ripoti nyengine pia lakini sitegemei zaidi ripoti za watu wengine; kuna ripoti zenu nyinyi wenyewe pia zinazotufikia - kwa hivyo hili litafutiwe dawa. Bila shaka hali hii inasababisha matatizo. Kwa hivyo kama isingekuwapo hii sehemu ya pili ya kadhia - yaani ile nusu ya pili tupu ya gilasi - kwa upande wa kiuchumi, leo hii nyinyi mngeweza kuwa na hali bora zaidi katika uendeshaji nchi na wananchi wangeweza kupatiwa misaada mingi zaidi. Kwa hivyo kutoa msukumo kwa uzalishaji wa taifa (wa ndani) ni kuimarisha sekta ambayo chimbuko lake linatokana na uchumi wetu wenyewe na inapasa kutilia mkazo suala hili.
Zifanyeni sekta ndogo ndogo na za kati ziwe amilifu. Bahati nzuri sekta zetu kubwa kubwa zina hali nzuri na zinatia faida nzuri, kazi zao ni nzuri na hali yao ya ajira pia ni nzuri; nyingi kati ya sekta zetu kubwa zina hali hii - kwa hivyo kama mlivyosema uzalishaji wetu wa saruji, uzalishaji wetu wa chuma cha pua na uzalishaji wetu wa bidhaa nyengine za aina hii ni mzuri - lakini inabidi mzifikirie sekta za kati na sekta ndogo ndogo; hizo zina umuhimu mkubwa na zina taathira ya moja ya kwa moja kwa maisha ya wananchi.
Suala la mapato ya fedha za kigeni ni suala muhimu na nyinyi wenyewe mnajua. Muwe makini juu ya suala hili na inapasa mlifanyie kazi sana. Kwa kweli mapato ya fedha za kigeni yanapasa yasimamiwe na kutumiwa kwa namna sahihi. Imeashiriwa hapa kuhusu mtaji wa fedha za kigeni. Kuhusu suala hili zimetolewa kauli kadha wa kadha kutoka upande wa serikali. Yaani katika magazeti kiongozi mmoja amenukuliwa akitoa kauli hii kisha kesho yake au siku mbili baada yake ikatolewa kauli nyengine. Msiruhusu kitu kama hiki kitokee. Kwa kweli inataka uchukuliwe uamuzi madhubuti kisha mlishughulikie suala hili kwa kushikamana kikamilifu na uamuzi mliopitisha. Alaa kulli hal, mapato ya fedha za kigeni yanapasa yasimamiwe kwa umakini.
Kuna suala jengine pia katika uchumi wa muqawama la kusimamia matumizi. Matumizi pia yanapasa kuwekewa usimamizi. Hii kadhia ya israfu na utumizi wa fujo ni kadhia muhimu nchini. Ni vipi israfu itaweza kuzuiwa? Kuna ulazima wa kujenga utamaduni na ulazima wa kuchukua hatua za kivitendo. Kwa sehemu kubwa jukumu la kujenga utamaduni liko mikononi mwa vyombo vya habari. Kuhusiana na suala hili kwa kweli vyombo vya Redio na Televisheni ndivyo vya kwanza na vyenye jukumu kubwa zaidi kuliko wengine na tab'an vyombo vyengine pia jukumu. Inapasa mjenge utamaduni. Sisi ni taifa la Waislamu wenye mapenzi na mafundisho ya Kiislamu. Katika Uislamu israfu imekatazwa mno lakini inasikitisha kuona kwamba sisi ni watu wa israfu katika maisha yetu! Kwa upande wa hatua za kivitendo, kwa maoni yangu hili linapasa lianzie serikalini. Nimesoma katika ripoti zenu na sasa hivi baadhi ya jamaa wameeleza hapa kwamba serikali imekusudia kubana matumizi na inataka kuanza kubana matumizi; ni jambo zuri sana na lina ulazima; inapasa mlipe uzito. Serikali yenyewe ni moja ya watu wenye matumizi makubwa mno. Kuanzia kwenye petroli mpaka kwenye vitu vingine mbalimbali mmoja wa watumiaji wakubwa ni serikali. Kwa kweli inapasa mubane gharama katika suala la matumizi. Kubana matumizi ni jambo la lazima na lenye umuhimu mkubwa.
Muupe umuhimu pia uzalishaji wa ndani. Katika vyombo vyenu, katika wizara zenu, ikiwa kuna kazi mpya ya kufanywa, ikiwa kuna kitu kipya cha kununuliwa na ikiwa mnataka kutayarisha hata hivi vifaa vya kila siku vinavyohitajiwa na wizara jaribuni kuhakikisha vifaa vyote hivyo viwe vilivyozalishwa ndani; tilieni mkazo suala hili; hii peke yake ni moja ya bidhaa zenye umuhimu mkubwa. Pigeni marufuku hasa na mseme kwamba si ruhusa kwa mtu yeyote katika wizara hii kutumia bidhaa ya kigeni. Kwa maoni yangu kufanya hivyo kunaweza kusaidia.
Suala jengine katika misingi ya uchumi wa muqawama ni kuwa na uchumi wenye misingi ya utaalamu. Baadhi ya watu wanaofanya kazi kwenye mashirika yenye misingi ya utaalamu walikuja hapa mwezi wa Ramadhani na wakazungumza juu ya mambo mbalimbali. Bahati nzuri mtu anaona kuna kazi nzuri walizofanya. Sekta hii ya mashirika yenye misingi ya utaalamu na shughuli za uchumi wenye misingi ya utaalamu ni njia safi na ya matumaini. Tab'an walikuwa pia na manung'uniko na malalamiko yao. Kwa maoni yangu jamaa wanaohusika serikalini ambao kazi zao zinahusiana na sekta hii - iwe ni wizara ya Viwanda, Madini na Biashara au Wizara ya Elimu - walishughulikie suala hili la mashirika yenye misingi ya utaalamu, wasikilize manung'uniko yao na kuyatatua. Kuna mazingira mazuri sana. Tuna watu wenye vipawa vikubwa ambavyo vinaweza kusaidia katika suala hili.
Kwa mawazo yangu, suala la umoja na mshikamano wa kitaifa ni jambo muhimu sana; nimelikariri mno suala hili kama kwamba maneno peke yake yamepoteza sifa ya kufikisha maana iliyokusudiwa! Inapasa tunachokisema sote kiwe kitu kimoja. Viongozi wanapaswa waratibu kwa makini mitazamo yao na kuwa na muelekeo wa pamoja; huu ni wajibu wa viongozi wote. Isiwe kila mmoja anamtupia lawama mwenzake. Hakuna atakayekubali hii hali ya mhimili mmoja wa dola au vitengo mbalimbali kwa kila mtu kumtupia lawama mwenzake na kuwaambia watu kwamba e bwana sisi tunataka kufanya jambo fulani lakini hawaturuhusu; au tulifanya kazi fulani lakini wakatukwamisha; au tulipitisha uamuzi fulani lakini hawakuutekeleza. Kwa vyovyote vile kila mmoja anaelewa jukumu lake; mmoja anapaswa kutunga sheria, mwengine anapaswa kuwa mtekelezaji, mmoja anapanga sera na mwengine anaziingiza kwenye utendaji. Inapasa wote hao watekeleze majukumu hayo kwa uratibu wa pamoja. Tusilichukulie kwa uzito mdogo suala la maelewano kati ya mihimili ya dola. Na bila shaka wanaokusudiwa hapa si serikali peke yake; Idara ya vyombo vya Mahakama na Bunge nao pia ni walengwa wa suala hili; vyombo mbalimbali vya utendaji hata vilivyoko nje ya serikali - kama vikosi vya ulinzi na venginevyo - navyo pia vinaingia katika wakusudiwa wa maneno haya. Wote hao wanapaswa kulizingatia suala hili. Bila ya shaka vyombo vya habari, watu wenye majukwaa ya uzungumzaji na vyombo vya upazaji sauti nao pia wana mchango wa kutoa. Vyombo vya habari vina nafasi kubwa mno katika ama kuleta umoja au kuzusha hitilafu. Kutokana na leo hii kuenea vituo na vyombo vya upashaji habari na taarifa na vya intaneti, maneno yanayotolewa kwa kila lugha na kutoka kila sauti yanawafikia watu wote. Na wengi wa watu hawachungi wanayosema. Wale watu wenye nyadhifa, iwe ni wale wa serikalini au walioko nje ya serikali wanapaswa walipe umuhimu mkubwa suala hili kuhakikisha kwamba huu uhuru wa maoni uliotolewa na Mfumo wa Kiislamu kwa ajili ya kubainisha ukweli wa mambo unatumiwa katika njia na muelekeo sahihi; unatumiwa kuleta mazingira ya uchangamko kwa ajili ya kazi na kujenga matumaini, kuwa kitu kimoja na kuleta na mshikamano.
Fursa haikupatikana kwa waheshimiwa kutoa ripoti juu ya suala la utamaduni. Nieleze mawili matatu: msitosheke na kazi zenye athari ya kijuujuu. Zipeni umuhimu kazi zenye taathira ya kina zaidi, kazi za msingi zaidi na kazi ambazo kutokana na moja kati ya hizo yanachipuka na kuzalika makumi ya kazi nyengine. Kuna wakati niliwahi kumpatia mheshimiwa Rais orodha ya kazi zenye ulazima; ni hizo ambazo zinapasa, bali zilipasa kufuatiliwa hapo kabla. Katika suala la utamaduni inapasa tutahadhari sana kufanya mambo yatakayosaidia "utamaduni wa hujuma". Utamaduni wa hujuma ni hatari. Ikiwa hatutoweza kuulinda na madhara ya adui utamaduni wa jamii nchini na utamaduni unaoongoza watu wenye vipawa, wananchi na matabaka mbalimbali kwenye lengo fulani, kazi itakuwa ngumu mno; maamuzi yoyote mtakayochukua yatakuja kuharibiwa na kuakisiwa namna nyengine kabisa.
Suala la Mfumo wa Mawasiliano ya Kompyuta (Cyberspace) nalo pia lina umuhimu lakini hakuna muda tena wa kueleza chochote. Suala la diplomasia ya Mapinduzi ni lenye umuhimu mkubwa mno, lakini na hili pia hakuna fursa ya kulizungumzia kwa upana. Kwa maoni yangu, katika suala la diplomasia kuna harakati nzuri zinazofanyika. Diplomasia yetu inapasa iambatane na moyo wa Mapinduzi - yaani Uislamu wa Kimapinduzi - na na ni hili ndilo linalotupa sisi nguvu na uwezo. Leo wananchi wa mataifa ya eneo wanaipenda Jamhuri ya Kiislamu kwa sababu ya msimamo wake huru wa Kiislamu na wa kishujaa; hili linapasa lidumishwe. Katika sehemu mbalimbali duniani watu wanavutiwa zaidi na viongozi wa Jamhuri ya Kiislamu kutokana na kuonyesha zaidi ushujaa huu, msimamo huu huru na huku kutokuwa kwao na woga. Hii inaonyesha kuwa njia sahii ni hii. Diplomasia yetu inapasa ifuate dira na muelekeo huu; na bahati nzuri jamaa wanafanya kazi kubwa sana.
Inapasa pia kuyatumia vizuri kwa kadiri iwezekanavyo matukio haya yanayojiri katika eneo kwa manufaa ya malengo ya Mapinduzi. Matukio haya ya eneo - kama nilivyoashiria - ni matukio muhimu sana na yamekuwa ni pigo kubwa kwa malengo ya Uistikbari katika eneo hili. Bila ya shaka nyinyi mnajua; Marekani na Uzayuni - na si serikali ya Kizayuni peke yake, bali mfumo mzima wenye nguvu, amilifu na wenye ushawishi mkubwa wa Uzayuni duniani - kwa hivi sasa tu hawatoweza kujiopoa na dhoruba za harakati hii adhimu iliyojiri. Matukio haya yamewashtukiza kwa maana halisi ya kushtukizwa. Bila ya shaka wamo wanajaribu kujiokoa na kupandia wimbi la harakati hii. Inawezekana wataweza kufanya hivyo katika baadhi ya sehemu lakini kwa upeo mpana hawajaweza na wala hawatoweza. Hii ni fursa muhimu sana kwa Jamhuri ya Kiislamu ya kuitumia nafasi na fursa hii.
Ni matumaini yangu kuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu atakusaidieni inshallah. Mjue kwamba kila hatua mnayopiga, kila chembe ya kazi mnayoifanya, kila moyo wa huruma mnaoonyesaha na kila jitihada mnayofanya inahifadhiwa mbele ya Mwenyezi Mungu Mtukufu; iwe mtu kama mimi binafsi au kwa kuwa na wadhifa fulani nijue hivyo au nisijue, nitoe shukurani au nisitoe. Yale mnayoyafanya katika mambo mema na ya kheri na mkayafanya kwa nia njema yanahifadhiwa mbele ya Mola wa ulimwengu. Qur'ani inasema: انّ الله شاكر عليم Hakika Mwenyezi Mungu ni mwenye kushukuru na pia ni mjuzi. Kwa hivyo inawezekana watu mithili yangu mimi tusijue mathalani ni kwa kiwango gani mumejituma na kiasi gani cha muda wa ziada nje ya wakati wenu wa kazi mumeutumia ofisini au kwenye kituo cha kazi; kama hatujui bila ya shaka hatutotoa shukurani; lakini kila lahadha ya muda huo haitofichika mbele ya Kiramal Katibin wanaohifadhi matukio - kwani Qur'ani inasema: انّا كنّا نستنسخ 'Hakika Sisi tulikuwa tukiyaandika mliyokuwa mkiyatenda.' Mwenyezi Mungu Mtukufu anayaandika matendo yetu yote, yaani anaorodhesha punje na chembe moja moja ya amali hizo.
Mwenyezi Mungu Mtukufu atakupeni malipo yenu. Inshallah mwende mkaendelee na kazi kwa umakini na kwa bidii zaidi. Serikali ya tisa na ya kumi ni maarufu kwa uchapaji kazi bila kuchoka; jitahidini kudumisha hali hii, na sifa hii nzuri hadi dakika za mwisho; na inshallah Mwenyezi Mungu atakusaidieni.
Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh

 
< Nyuma   Mbele >

^