Skip to content

Habari

Habari
Hifadhi

Risala na Barua

Matini
Hifadhi

Kumbukumbu na Simulizi

Kabla ya Mapinduzi
Baada ya Mapinduzi

Sauti na Taswira

Picha
Sauti
Video
Hotuba ya Kiongozi Muadhamu Alipoonana na Mjumuiko wa Mateka Walioachiliwa Huru Chapa
15/08/2012

Ifuatayo ni matini kamili ya hotuba ya Ayatullah Udhma, Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aliyoitoa tarehe 15/08/2012, siku alipokutana na na mamia ya mateka wa Kiirani waliowahi kuwa mateka katika vita vya miaka minane vilivyoanzishwa na utawala wa zamani wa Iraq chini ya uongozi wa dikteta Saddam dhidi ya Iran.

Kwa jina la Allah Mwingi wa rehema Mwenye kurehemu

Ninatumia fursa hii kukukaribisheni hapa makaka wapendwa; nyinyi vito na johari (zenye thamani kubwa) zilizotokana na akiba ya imani katika Jamhuri ya Kiislamu (ya Iran). Katika kipindi cha karne zote, kitu kigumu kisicho na thamani hubadilika na kuwa almasi kama kitakuwa na maandalizi ya hilo. Kipindi kigumu cha kuishi katika maisha ya kushikiliwa mateka kwa karne kadhaa sasa kimewabadilisha watu wenye maandalizi na kuwa almasi zinazong'ara. Kwa hakika hizi ni lahadha nzuri mno kwangu kukutana na nyinyi na ninasikitika kwamba, nimepata tawfiki chache ya kukutana na nyinyi wapendwa mateka mlioachiliwa huru katika vikao mfano wa hiki. Napenda kutumia fursa hii adhimu ya kuonana na nyinyi na ya kikao hiki cha kimaanawi, kilichojaa huba na mapenzi makubwa na cha kidugu, kutoa salamu kwa mateka wote walioachiliwa huru walioko katika kona mbalimbali hapa nchini; kuna takribani mateka elfu arobaini walioachiliwa huru wenye thamani na waliopata mateso katika kipindi (kile) ambacho kwa hakika kilikuwa kipindi kigumu mno.
Suala la kuwa mateka linaweza kutazamwa na kuzingatiwa katika engo mbalimbali. Moja kati ya engo hizo, ni hizi hizi kumbukumbu zenye thamani aali ambazo zimebainishwa na ndugu hapa. Tab'an, binafsi nimepata kutwalii vitabu vinavyohusiana na kumbukumbu za mateka walioachiliwa huru na vile vile kile ambacho kinahusiana na Sayyid wetu mkubwa na azizi, Bwana wa mateka walioachiliwa huru, Marhumu Bwana Abu Turabi. Kwa hakika inawezekana kukisia kwamba, kile kilichobainishwa na kusemwa katika matamshi na maandiko kuhusiana na kipindi cha kuwa mateka, ni sehemu ndogo tu ya kisa kirefu na sisi vile vile tunahitajia kusikia kisa hiki kirefu.
Mimi napenda kusema hapa ya kwamba, kwa hakika katika kipindi hiki cha miaka 22 tangu kurejea hapa nchini wananchi wetu mateka walioachiliwa huru, kuna hali ya kutofanya mambo kama inavyotakiwa ambayo imejitokeza. Sisi tunapaswa kuwa na vitabu mara kadhaa ya vitabu ambavyo hadi sasa vimeandikwa kuhusiana na jambo hili. Sisi tunapaswa kuwa na filamu muhimu za kisanii kuhusiana na hali ya mateka wetu walioachiliwa huru katika kambi na magereza.
Nyinyi watazameni Wamagharibi na taasisi kubwa za utengenezaji filamu, ni jinsi gani zimeandaa na kutengeneza filamu kuhusiana na matukio ya mateka katika Vita Vikuu vya Pili vya Dunia au katika Vita Vikuu vya Kwanza vya Dunia; filamu nzuri na filamu stadi; licha ya kuwa kile kilichoko katika filamu hizo kinaonesha roho ya kimaada ya mateka hao; ambapo hilo linaonekana wazi katika maisha yao, mazungumzo yao na muamala wao. Vile vile nimesikia kwamba, maafisa na wafanyakazi wa Shirika la Msalaba Mwekundu waliokuwa na mateka wetu walioachiliwa huru walikuwa wakisema kwamba: Sisi tulipokuwa tukienda katika kambi za mateka wa vita katika nchi nyingine tulikuwa tukishuhudia hali ya msononeko, kujiinamia, mawazo na hata kujiuawa mateka, kwa nini nyinyi hamna mambo haya? Hili ni swali ambalo lilikuwa ni lazima liulizwe na afisa wa Shirika la Msalaba Mwekundu.
Jibu la swali hili liko wazi: Pindi moyo unapokuwa hauna utambuzi na ufahamu na maanawi na wala hauna utambuzi na Mwenyezi Mungu, natija yake huwa hiyo. Pindi moyo unapokuwa na utambuzi na Mwenyezi Mungu, wakati moyo huo unapohisi kuwa na mawasiliano, wakati unapohisi kujiamini, wakati unapojihisi kwamba, hauko peke yake, wakati moyo unapoona seli na mateso kuwa ni pepo ya kimaanawi - kama ambavyo haya yamebainishwa na kushuhudiwa katika mazungumzo ya wapendwa hapa na hilo limeandikwa pia katika kumbukumbu zao - hali ya kusononeka haina nafasi, kuzongwa na mawazo hakuna nafasi na suala la kujiua halina maana. Hii ni sehemu moja ya kadhia ambapo sisi tunapaswa kutwalii bahari hii yenye kina kirefu na kipana kuhusiana na maisha na mateka hao waliokombolewa. Inasikitisha kwamba, hatujatwalii sana katika uwanja huu.
Kuna ulazima wa kutengenezwa filamu nzuri, kuandikwe vitabu vizuri na kusimuliwa kumbukumbu nzuri kuhusiana na mateka (wa Kiirani) walioachiliwa huru. Hizi hizi kumbukumbu ambazo zimebainishwa leo hapa, zina mengi ya kusemwa ndani yake; ni vizuri kiasi gani kama mambo haya yataonyeshwa. Mtazamo wangu ni kuwa, hizi hizi kumbukumbu zilizobainishwa leo, zinapaswa kuonyeshwa na kutangazwa kama zilivyo katika Radio na Televisheni, ili wananchi wasikie na kuona; hizi ni akiba zetu, hizi ni rasilimali zetu; ni rasilimali ambazo zimehifadhiwa na Uislamu na Ushia na hivyo kuifikisha Jamhuri ya Kiislamu katika nguvu, uwezo na izza na kulifanya pia taifa la Iran kuwa na izza hapa duniani. Huu ni upande mmoja wa kadhia.
Upande mwingine wa kadhia ni suala la ibra na sunna ya Mwenyezi Mungu. Ala kulli haal, katika maisha yetu mafupi ya hapa duniani ambayo ni makumi kadhaa ya miaka, daima hukabiliwa na changamoto. Changamoto daima hazitoki kwa Marekani na ubeberu peke yake. Kuna changamoto tofauti tofauti; lakini kwa upande wa mapinduzi ya Kiislamu, kuna changamoto za ndani, changamoto za kishetani, changamoto za nafsi inayoamrisha mno maovu, changamoto za madola ya kibeberu na wanaotaka kuhodhi mambo, changamoto za kutaka makuu na changamoto za ubeberu. Kwa hakika sisi tunahitajia kupata ibra na hali ya kutaamali katika sunna hizi za Mwenyezi Mungu.
Yamkini ule wakati ambapo wana wa taifa hili la Iran walipokuwa mateka na wakipata mateso katika kambi na vituo walivyokuwa wanashikiliwa mateka, kidhahiri na kijuu juu ilionekana kana kwamba, dirisha la matumaini ya ushindi kwa watu hao lilikuwa limefungwa, lakini kutokana na kushikamana kwao na Uislamu na kutekeleza kivitendo mafundisho ya Mwenyezi Mungu, hatimaye sunna isiyobadilika ya Mwenyezi Mungu ilitimia juu yao na kufanikiwa kurejea nyumbani kishujaa. Leo hii tazameni uhakika uliopo na muone nini kimetokea; wao wako wapi na nyinyi mko wapi? Hii ni ibra na funzo; hili ni jambo linaloonesha kuwa kweli na sahihi ahadi ya Mwenyezi Mungu. Tuwe na imani na ahadi ya Mwenyezi Mungu. Tuwe na imani kwamba, ahadi ya Mwenyezi Mungu ni ya kweli. Tunapaswa kudiriki pale Mwenyezi Mungu anaposema:
"Na bila ya shaka Mwenyezi Mungu humsaidia yule anayemsaidia Yeye. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu Mtukufu." ( al-Haj 22:40). Tudiriki maana hii. Siku ile ambayo nyinyi mlikuwa mbele ya afisa mtesaji au mkubwa wa jela au afisa wa kibaathi (afisa wa utawala wa zamani wa Iraq), na hizi changamoto ambazo taifa la Iran inakabiliwa nazo kutoka kwa Marekani, ni kadhia ile ile. Ahadi ya Mwenyezi Mungu ya "Na bila ya shaka Mwenyezi Mungu humsaidia yule anayemsaidia Yeye. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu Mtukufu, ni ahadi ya kweli na sahihi. Watu ambao hawana imani na ahadi ya Mwenyezi Mungu, Allah anawatambua watu hao kuwa waliofukuzwa, waliolaaniwa na ambao wanahesabiwa kuwa wako mbali na rehma za Mwenyezi Mungu. Ahadi ya Mwenyezi mungu ni ya haki. Hii leo pia jambo hili liko kwa taifa la Iran. Endapo sisi tutakifanya kile ambacho Mwenyezi Mungu amekisema (na kukitaka kifanywe) - kama ambavyo ninyi mlikifanyia kazi hicho katika kipindi cha kuwa kwenu mateka - bila shaka taifa la Iran litapata ushindi; hii ni ibra na funzo.
Wale ambao walikuwa wakikuambieni ni lazima mbakie katika jela na magereza haya milele, au walikuwa wakikwambieni kwamba, nyinyi mtanyongwa wametupwa katika debe la taka za historia, wenyewe ndio wamenyongwa, wenyewe ndio wameangamia; Alhamdulilahi hii leo nyinyi mnaishi katika Jamhuri ya Kiislamu kwa izza na heshima; hili ni funzo na darsa.
Sisi tuliwahi kupata tena darsa na funzo hili huko nyuma. Baadhi yetu hawakuwa wakiamini. Katika kipindi cha ukandamizaji, katika zama za kitaghuti, kulikuweko na mashinikizo mengi; kuna watu walikuwa wakisema nyinyi mnasimama kidete bure bila ya faida yoyote, mnafanya muqawama usio na maana yoyote; kuna wengine ambao wao walikuwa wakisema, hapana, na walikuwa wakisema kama anavyosema Mwenyezi Mungu:
Miongoni mwa Waumini wapo watu waliotimiza waliyoahidiana na Mwenyezi Mungu. Baadhi yao wamekwishakufa, na baadhi wanangojea, wala hawakubadilisha (ahadi) hata kidogo. (al-Ahza'b 33:23), Mwenyezi Mungu mtukufu ameleta tukio ambalo hakuna mtu yeyote ambaye alikuwa akiamini kwamba, lingeweza kutokea; sio kwamba, ndani ya Iran watu walikuwa hawaliamini hilo, bali duniani kwa ujumla hakuna mtu ambaye alikuwa anaamini kwamba, tukio hili linaweza kutokea. Hakuna mtu ambaye alikuwa akiamini kwamba, kile ambacho Wamarekani wanakitambua kuwa ni kisiwa thabiti (cha amani), kingekuja kupigwa na tufani namna hii na mwishowe jambo hili lipelekee kutengwa Marekani, kutengwa ubeberu, Uingereza pamoja na vibaraka wao. Hii leo hali iko namna hii.
Leo pia nyinyi itazameni dunia; mtaona kuna ishara. Nimesema mara kadha wa kadha kwamba, ulimwengu unapita katika kivuko na kufika katika hali mpya na matukio mapya. Muamala wetu, nia yetu na utendaji wetu una taathira na ni wenye kuainisha mambo katika hatua hii ya uundikaji wa hali mpya. Ili nyoyo zetu ziwe imara na ili tusipotee njia, maisha yenu nyinyi mateka mlioachiliwa huru yanaweza kuwa nyota ya uongozaji kwetu sisi. Mimi ninaamini na ninasisitiza kwamba, kuna ulazima wa matukio ya wakati wa kuwa katika maisha ya umateka yasemwe na kuandikwa, yaundiwe taswira katika kalibu ya athari za sanaa na kadhalika. Hii haina maana ya kutoa himaya na uungaji mkono kwa tabaka fulani, au kutetea tukio fulani; bali maana ya hii ni kutia saini na kupasisha kwa nguvu zote hatua ya ushindi wa taifa la Iran; na kazi hii ni lazima ifanyike. Ninawataka wasanii wa nchi yetu na maafisa wa vyombo vya habari waifanye kazi hii na nyinyi (mateka mlioachiliwa huru) mnapaswa kusaidia katika hili. Kwa bahati nzuri watu wamenufaika na yale yaliyoielezwa na ndugu hapa, binafsi pia sio kwamba, sina habari na kinachojiri, kuna hati na ushahidi mwingi na kwa hakika nyinyi (mateka mlioachiliwa huru) ni hati ambazo ziko hai; pateni msaada wa kumbukumbu zenu na mhadithie matukio yalivyotokea (wakati huo) pasina ya kuongeza, kupunguza au kutia chumvi; bali bainisheni tukio kama lilivyokuwa.
Pindi mambo haya yatakapoandamana na ubainishaji wa kisanii, kutapelekea ari fulani katika nyoyo. Huu nao ni upande (miongoni mwa pande za) wa kadhia yenu ya kuwa mateka na kuachiliwa kwenu huru.
Upande mwingine ni thawabu kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Siku ile kwa mara ya kwanza wakati mateka wetu walioachiliwa huru walipowasili hapa nchini na mimi nikakutana na mjumuiko wao - ambao ulikuwa takribani watu elfu kadhaa - katika Husseinia hii ambapo Sayyid wetu Marhumu Abu Turabi alihutubia, kwa hakika moyo wangu ulikuwa na hali maaalumu kutokana na kuona mandhari ile na hawa vijana wenye thamani waliokuwa wamerejea hapa nchini.
Nilisema kuwaambia: tambueni kwamba, kila lahadha ya maisha yenu imehifadhiwa katika kumbukumbu za Mwenyezi Mungu. Hivi sasa pia bado nina itikadi na imani hiyo hiyo: lahadha hizi zimehifadhiwa mbele ya Mwenyezi Mungu; na hili ni jambo ambalo mtu hawezi kutoa wasifu wake, haya ni mambo ambayo hayawezekani kuyaaona kwa macho yoyote yale na nyinyi mumepitisha lahadha na masaa haya kwa miaka kadhaa. Hakuna hata chembe moja ya lahadha zenu ngumu na za kufanya jihadi na hima ambazo zinasahaulika katika diwani na kumbukumbu za Mwenyezi Mungu. Sisi tunasahau na hata nyinyi mnasahau, lakini Kiraman Katibin (Malaika wanaoandika amali) wa Mwenyezi Mungu hawasahau; hivyo hima na juhudi hizo huhifadhiwa. Hata hivyo fanyeni hima kuyalinda na kuyahifadhi haya; kwa hakika hapa naiusia nafsi yangu na kuzuiusia nafsi zenu pia nyinyi ndugu wapendwa na azizi.
Ujira wa mateka walioachiliwa huru kwa upande mmoja na ujira (thawabu) wa familia - wake, watoto, akina baba, akina mama na watu wa karibu - kwa upande mwingine. Kuna wakati sisi tulikuwa tukipata tawfiki ya kwenda katika nyumba ya shahidi fulani na kukutana na baba, mama au watu ambao mmoja wa watu wa familia hiyo alikuwa mateka, kwa hakika mtu hufahamu familia yenye mtu ambaye ni mateka ina hali gani, ina hisia gani; kwa hakika hisia za familia kama hizi ni ngumu na chungu zaidi kuliko hisia za familia za mashahidi.
Mmoja wa kaka wa mateka ambaye hajulikani alipo aliniambia kwamba: wewe umeona hali waliyonayo wana familia wenye kijana aliyeko vitani katika usiku wa operesheni? Kwa hakika alikuwa akisema kweli; pindi inapokuwa ni usiku wa kufanya operesheni (ya mashambulio) wote hufahamu kwamba, huu ni usiku wa operesheni, zile familia ambazo zina kijana wao vitani nyoyo zao huwa na hali maalumu. Kaka wa ndugu aliyepotea na asiyejuliakana alipo (baada ya kwenda vitani) aliniambia kwamba:
Kwetu sisi kila usiku ni usiku wa operesheni, kila usiku nyoyo zote huwa na hali maalumu na wasi wasi kwamba, ndugu yetu yuko katika hali gani na leo atakuwa katika hali gani. Haya ndio magumu ambayo yanavumiliwa na familia hizi; kwa hivyo basi, ujira (thawabu) wao ni mkubwa mno.
Vizuri, msimu huu wa matukio ya maisha ya taifa la Iran umepita na taifa la Iran limepata faida. Izza ya taifa fulani, nguvu yake na kuongoza kwake katika historia ni mambo ambayo yanafungamana na jihadi na mapambano ya watoto wake (watoto wa taifa hilo). Mapambano haya wakati mwingine ni katika uwanja wa vita na wakati mwingine ni katika medani ya kushikiliwa mateka; wakati mwingine ni kwa ushindi huu ambao nyinyi mumeuonesha katika medani ya kushikiliwa mateka; huku kusimama kwenu kidete na huku kuonesha kwenu muqawama.
Vizuri, kuna watu ambao waliuawa shahidi katika zama hizo; shahidi Tondgooyan na kuna mashahidi wengi ambao hawakuweza kustahamili maisha ya kushikiliwa mateka; na akthari yao waliachiliwa huru na kurejea hapa nchini kwa fakhari kubwa. Tuna matarajio Inshallah Mwenyezi Mungu atakulipeni ujira na kuuhifadhi ujira wenu na wale watu ambao walikuwa na taathira katika duru hii, ambao walikuwa wahudumu na waliwaongoza wengine, kinara wao akiwa shahidi mwenye adhama na azizi wetu Marhumu Abu Turabi, Mwenyezi Mungu aikweze daraja yake.
Vizuri, leo sisi tuna suala la kimsingi katika ulimwengu wa Kiislamu nalo ni kadhia ya Quds. Kwa nini tunasema kwamba, ni suala la kimsingi? Kwa sababu tukio la msingi mbovu na wenye mapungufu wa uhandishi wa Mashariki ya Kati - katika eneo letu hili na la nchi zetu - umefanyika kwa msingi wa njama za kuwaleta Wazayuni hapa na kuwapatia makazi. Hivyo basi hiki ndicho chanzo cha matatizo yote yaliyoshuhudiwa kwenye eneo hili (Mashariki ya Kati) kwa makumi ya miaka sasa. Kama wizi na uporaji huo usingelikuwepo, bila shaka eneo la Mashariki ya Kati na ulimwengu wa Kiislamu kiujumla usingelishuhudia vita vyote hivi, wala usingeshuhudia hitilafu zote hizi na wala uingiliaji wote huu wa madola ya kiistikbari na kibeberu katika masuala ya ndani ya nchi za eneo hili (Mashariki ya Kati). Haya yote yametokana na kadhia hii; ambapo hili lina kisa kirefu.
Wazayuni na waungaji mkono wao wanafanya njama kubwa kuyasahaulisha mataifa ya dunia na fikra za walio wengi ulimwenguni kuhusiana na kadhia ya Palestina, hivyo ulimwengu wa Kiislamu unapaswa kusimama imara na kidete ili kukabiliana na hadaa, hila na njama hizo za Wazayuni na waitifaki wao. Katika kipindi cha miaka yote hii Wazayuni na waitifaki wake wamefanya kila wawezalo ili kadhia ya Palestina isahaulike na kwa kiwango fulani wamefanikiwa katika hili. Tukio la mkataba wa Camp David na yaliyokuja baada ya mkataba huo - ambao ni moja ya nukta zenye kiza za historia ya leo - lengo lake lilikuwa ni kuwafanya wananchi wa Mashariki ya Kati waisahau kabisa nchi inayojulikana kwa jina la Palestina.
Kilichokuja kuwa kikwazo na kutoa pigo kwa mipango yao hiyo ni ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran ambao kwa hakika umekuwa ni kikwazo cha kihistoria mbele ya njama za mabeberu za kujaribu kuisahaulisha kadhia ya Palestina na yanazidi kufichua jinsi ardhi hiyo ya Waislamu inavyopata mateso kutokana na kukaliwa kwa mabavu na Wazayuni maghasibu.
Kwa muktadha huo basi, Imam Ruhullahi Khomeini (quddisa sirruh) na ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu yalitoa pigo kwa Wazayuni na waitifaki wake. Tangu siku ya kwanza mapinduzi ya Kiislamu yalipopata ushindi hapa nchini Iran, bali hata kabla ya mapinduzi hayo kupata ushindi, yaani mwanzoni mwa harakati, kadhia ya Palestina ilikuwa miongoni mwa masuala makuu na ya kimsingi ya mapinduzi haya; na suala hili ni moja ya mambo yaliyoufanya ulimwengu wa Kiislamu uyazingatie mapinduzi haya; licha ya kuwa kulikuweko na mambo mengine. Hii leo hima yao kubwa ni kusambaratisha hili. Ulimwengu wa Kiislamu haupaswi kuruhusu (hata kidogo) hili litokee.
Hii leo kuna njama za kuushughulisha ulimwengu wa Kiislamu na masuala ya pembeni ambayo hayana umuhimu wala maana. Anakuja mtu (kwa mfano) na kuanza kuzungumzia suala la Ushia na Usuni au anazungumzia suala la hilali (mwezi mwandamo) ya Kishia ili kuwatia hofu Waislamu na kujaribu kuwagombanisha wao kwa wao wakati ambapo taifa la Palestina linakaliwa kwa mabavu na Wazayuni kwa miaka 60 (miongo sita) sasa huku wananchi wa taifa hilo wakiishi katika shida na ukandamizaji mkubwa, lakini hakuna mtu anayesikiliza sauti ya kilio chao.
Utawala wa Jamhuri ya Kiislamu (ya Iran) umekuja na kutundika juu bendera hii na kukarabati hamasa hii ulimwenguni, kisha mnakuja (nyinyi maadui na kuiarifisha Iran kwamba, ni hatari na tishio? Kuna khiyana na usaliti zaidi ya huu? Kwa hakika taifa la Iran halijaruhusu (kadhia ya Palestina isahaulike) na wala halitaruhusu hilo litokee. Je, kuzungumzia Jamhuri ya Kiislamu ambayo imelijenga upya na kulihuisha suala la Palestina ndiyo hatari katika ulimwengu wa Kiislamu au kunyamaza kimya mbele ya jinai na maafa makubwa yanayofanywa na Wazayuni dhidi ya wananchi wasio na ulinzi wa Palestina? Kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu, mwaka huu pia taifa la Kiislamu la Iran litashiriki kwa wingi mno katika maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Quds (Ijumaa ya mwisho ya kila mwezi mtukufu wa Ramadhani) na kutoa pigo jingine kubwa kwa maadui wa Uislamu na maadui wa taifa madhulumu la Palestina.
Kwetu sisi (Jamhuri ya Kiislamu )kadhia ya Quds si suala la "kimbinu" bali ni jambo ambalo limejengeka juu ya misingi mikubwa ya itikadi za Kiislamu na sisi tunalichukulia suala la kuikomboa nchi hiyo ya Kiislamu kutoka kwa mabeberu na kutoka kwenye makucha ya maghasibu Wazayuni na waungaji mkono wao wa kimataifa na kisha kuwakabidhi Wapalestina, kuwa ni jukumu letu la kidini; ni jukumu la Waislamu wote; mataifa yote ya Kiislamu, madola yote ya Kiislamu yana jukumu la kufanya kazi hii; kwa hivyo hili ni jukumu la Kiislamu. Sisi tunaitazama kadhia ya Palestina kwa jicho hili, wengine nao wanapaswa kuitazama kadhia hii kwa mtazamo huu. Wasiiweke kadhia hii katika michezo ya kisiasa, ushirikiano wa kisiasa na wakati mwingine katika usaliti; kadhia hii ni kadhia ya kidini na ya kiitikadi, hivyo inapaswa kufuatiliwa.
Napenda kuwaeleza kwamba, kama ambavyo nyota yenye kutia matumaini ya mapambazuko ya asubuhi ilichomoza na kuangaza wakati wa ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu na katika hamasa ya vita vya kujihami kutakatifu (vita vya kichokozi vya miaka minane vilivyoanzishwa na dikteta Saddam wa Iraq dhidi ya Iran) na kwa mara nyingine katika kukombolewa na kurejea nyumbani mateka wa Kiirani waliokuwa mikononi mwa utawala wa wakati huo wa Iraq, (utawala wa Kibaath); hivi sasa pia kwa uwezo na nguvu za Mwenyezi Mungu Mtukufu, nyota hiyo itachomoza na kuangaza pia katika kadhia ya Palestina na bila ya shaka yoyote ardhi hiyo ya Kiislamu itarejea kuwa mikononi mwa taifa la Palestina baada ya kufutika pandikizi hili yaani utawala wa Kizayuni wa Israel katika jiografia ya dunia; hili ni jambo ambalo halina shaka kabisa.
Suala la kuhuzunisha na kutia simanzi katika masiku haya ni tukio la mtetemeko wa ardhi; ambapo ni lazima kwangu hapa kukumbusha nukta kadhaa na kutilia mkazo baadhi ya mambo. Wananchi wote wa Iran bila shaka wamepatwa na msiba katika tukio hili; kwa sababu kuna baadhi ya ndugu zetu ambao wamekumbwa na mtetemeko wa ardhi na kupoteza maisha yao. Kwa hakika tukio hili ni chungu; limetokea katika masiku ya mwezi mtukufu wa Ramadhani. Tuna matarajio Inshallah kwa auni na msaada wa Mwenyezi Mungu pamoja na mapenzi Yake atawasaidia maafisa na viongozi wa serikali pamoja na wananchi wetu azizi ili waweze kuwapunguzia masaibu na matatizo wananchi wa Azerbaijan yaliyotokana na mtetemeko huu wa ardhi, na Inshallah bila shaka atasaidia katika kusukuma mbele kazi zao.
Tunamuomba Mwenyezi Mungu awape subira na uvumilivu na azitulize nyoyo zao. Tuna matarajio kwamba, Mwenyezi Mungu Mtukufu atashusha baraka Zake kwa taifa azizi la Iran na kuufanya mwezi huu Mtukufu wa Ramadhani kuwa mwezi wa kimaanawi kwa maana halisi ya neno na wenye baraka ya kweli kwa wananchi wetu na kwa Jamhuri ya Kiislamu (ya Iran) kwa ujumla.
Ewe Mwenyezi Mungu ! tunakuomba uwajumuishe katika rehma Zako na baraka Zako hawa waliokumbwa na masaibu. Ewe Mwenyezi Mungu! tunakuomba uwape uthabiti, uimara na thawabu wale wote wanaopiga hatua katika njia ya kuhakikisha kalima (neno la) ya Mwenyezi Mungu inakuwa juu. Tunakuomba umfufue pamoja na mawalii Wako Imam wetu mwenye shani ambaye alitufungulia njia hii. Ewe Mwenyezi Mungu! Wafufue pamoja na mawalii Wako mashahidi wa kipindi cha kushikiliwa mateka pamoja na Marhumu Abu Turabi, alimu, mwana jihadi, mwenye subira, mratibu mambo na mja mwema; tunakuomba umfufue pamoja na mawalii wako baba yake mwema.
Ewe Mwenyezi Mungu! Tunakuomba utupe tawfiki ya kuwa miongoni mwa watu wenye kuhudumu kwa ikhlasi na nia ya kweli kabisa.
Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

 
< Nyuma   Mbele >

^