Skip to content

Habari

Habari
Hifadhi

Risala na Barua

Matini
Hifadhi

Kumbukumbu na Simulizi

Kabla ya Mapinduzi
Baada ya Mapinduzi

Sauti na Taswira

Picha
Sauti
Video
Hotuba ya Kiongozi Muadhamu katika Hadhara ya Wananchi wa Vijiji Vilivyokumbwa na Zilzala Azerbaijan Chapa
16/08/2012

Ifuatayo ni matini kamili ya hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aliyoitoa mbele ya hadhara ya wananchi wa vijiji vilivyokumbwa na mtetemeko wa ardhi huko Azerbaijan Mashariki tarehe 16/08/2012

Kwa jina la Allah Mwingi wa rehma Mwenye kurehemu
Hamdu zote zinamstahikia Allah, Mola Mlezi wa viumbe pia. Na rehma na amani zimfikie Bwana Mtume Mtukufu na Mwaminifu na Aali zake watoharifu, wateule, maasumina na waongozaji hususan Baqiyatullah katika ardhi (Imam Mahdi AS).

Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh
Mwenyezi Mungu akupeni tawfiki nyote na akupeni subira nyinyi nyote. Kwa hakika tukio chungu na la kuhuzunisha la mtetemeko wa ardhi katika eneo hili, limezihuzunisha na kuzitia simanzi nyoyo zote; na watu wote wamekumbwa na msiba huu. Tunamuomba Mwenyezi Mungu Mtukufu awape subira na uvumilivu wale wote waliopatwa na msiba kufuatia tukio hili. Tunamuomba Allah awape tawfiki wananchi wa Azerbaijan Mashariki. Na ninapenda kuwaambieni nyote kwamba, tukio hili linaweza kuwa chanzo cha nyinyi kuruka na kusonga mbele. Subira yenu, uvumilivu wenu, kusimama kwenu kidete, juhudi zenu, ushirikiano wenu na kuliwazana kwenu baina yenu, Inshallah mnaweza kulifanya tukio hili kuwa chimbuko na chanzo cha nyinyi kusonga mbele.
Tab'an, maafisa wa serikali wana majukumu makubwa. Hadi leo kuna kazi nzuri ambazo zimefanyika; bado kuna kazi kuu na za kimsingi baada ya kazi hizi; ukarabati na kuimarisha ni mambo ambayo Inshallah, yanapaswa kubadilisha sura ya eneo hili baada ya kukumbwa na janga hili la kimaumbile na mtetemeo wa ardhi. Tunamuomba Mwenyezi Mungu awape tawfiki maafisa na viongozi wa serikali na nyinyi mtoe ushikiano unaohitajika. Kwa hakika wananchi wanapaswa kushirikiana na viongozi na maafisa wa serikali. Kwa mujibu wa taarifa nilizonazo ni kwamba, wananchi wa kona mbalimbali hapa nchini wako pamoja nanyi katika msiba huu.
Sio kwamba, sehemu fulani ya nchi ikikumbwa na msiba basi wengine kwao iwe hakuna tofauti yoyote; hapana, watu wote hapa nchini wako pamoja na wananchi wa eneo hili lililokumbwa na janga la kimaumbile la mtetemeko wa ardhi. Alhamdulilahi sisi ni taifa ambalo ni moja, taifa lenye umoja na mshikamano; na bila shaka taifa hili lina nguvu kutokana na huu umoja na mshikamano uliopo. Hii nguvu ambayo leo Jamhuri ya Kiislamu (ya Iran) inayo, hii izza, heshima na utukufu ambao taifa la Iran inao, sehemu yake muhimu ya haya yanatokana na huu mshikamano, umoja na maafikiano ambayo yako baina ya matabaka mbalimbali ya wananchi katika sehemu tofauti hapa nchini.
Lengo langu la kwanza katika safari hii, katika hatua ya awali ni kuonesha kuwa pamoja na kuungana na wananchi wa eneo hili (katika janga hili lililowakumba) - eneo la Ahar, Varzaqan, Haris na vijiji na maeneo ya kando kando na miji hii mitatu - kuungana na kuwa pamoja na watu ambao wamepoteza watu wao azizi na wamepoteza watoto wao katika tukio hili; kwa hakika sisi tupo pamoja nao katika msiba na huzuni yao. Tunamuomba Mwenyezi Mungu awape subira. Hili ndilo lengo langu la kwanza la safari hii.
Katika hatua ya pili, (lengo la pili la safari hii) nilitaka kuona kwa karibu kazi ambazo mpaka sasa zimefanyika katika fremu ya kuwahudumia waathirika wa tukio na janga hili la kimaumbile. Kwa hakika nimewauliza baadhi ya watu waliokumbwa na mtetemeko huu wa ardhi na wamesema kwamba, huduma ambazo mpaka sasa wamepatiwa ni huduma nzuri na za kufaa. Inshallah, huduma hizi zinapaswa kuendelea. Tab'an, aina ya huduma zitatofautiana bila shaka (kulingana na mahitaji); baadaye kutakuwa na kazi ngumu na za kimsingi ambazo tuna matumaini Inshallah viongozi na maafisa husika watapata tawfiki ya kuzifanya kazi na kutekeleza majukumu haya. Ninakushukuruni nyote.

Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

 
< Nyuma   Mbele >

^