Skip to content

Habari

Habari
Hifadhi

Risala na Barua

Matini
Hifadhi

Kumbukumbu na Simulizi

Kabla ya Mapinduzi
Baada ya Mapinduzi

Sauti na Taswira

Picha
Sauti
Video
Miongozo ya Kiongozi Muadhamu Alipoonana na Vikosi vya Ulinzi vya Eneo la Kaskazini na Familia Zao Chapa
18/09/2012

Ifuatayo ni matini kamili ya hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Sayyid Ali Khamenei (daama dhilluh al-A'ali) aliyoitoa katika Chuo Kikuu cha Kijeshi cha Imam Khomeini MA huko mjini Nowshahr alipokutana na Vikosi vya Ulinzi vya Eneo la Kaskazini pamoja na familia zao tarehe 19/08/2012.

Kwa jina la Allah Mwingi wa rehma Mwenye kurehemu

Kwa hakika hisia ya kuwa na uwezo wa kufanya kazi kubwa huhuika katika ujudi wa kila mtu anapokuwa katika mjumuiko wenu huu nyinyi makaka na madada wapendwa. Majimui ya vijana, wafanyakazi, maafisa wachapa kazi katika vikosi vya ulinzi, wake zao na watoto wao ni mfano mmoja wa watu wateule kutoka katika taifa la Iran ambalo ndani yake kuna wimbi kubwa la malengo makuu katika hisia yake, moyo wake na fikra yake. Kwa hakika nina furaha kubwa kupata tawfiki ya kuwa na nyinyi usiku wa leo na ninamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa tawfiki ya kuweko baina yeu na katika mjumuiko na mkusanyiko wenu huu. Ninamuomba Mwenyezi Mungu Mtukufu akupeni baraka, rehma na afya nyinyi nyote. Inshallah.
Ratiba na mambo yaliyoandaliwa na kufanywa na vijana wetu azizi hapa yaani wanachuo wa Chuo Kikuu hiki, yalikuwa mambo mazuri; aya za Qur'ani Tukufu zinatoa bishara ya matumaini kwa kusisitiza kwamba, kando ya kila uzito kuna wepesi. Hii ni fikra adhimu na yenye utatuzi wa mambo kwa jamii zote ambapo nitajaribu kulizungumzia hili hapa japo kwa mukhtasari. Napenda kuwaambia nyinyi na hili ni jambao ambalo kwa haakika nawaambia wote na ninakumbuka kwamba, nimewahi kulisema hili na kulikariri mara nyingi, ya kwamba, tusije kupungukiwa na zile sifa ambazo zinaendana na uwepo wa Walii Asr, Imam Mahdi (roho zetu ziwe fidia kwake).
Kwa hakika Imam Mahdi (arwahuna fadaahu) ni Nabii Nuhu wa zama hizi yaani kwa maana kwamba, atayekuwa pamoja naye ni sawa na kupanda safina ya Nabii Nuhu AS ambapo aliyepanda aliokoka na aliyeacha hilo aliangamia. Wakati tunapotazama kiujumla historia ya Uislamu tunaona kuwa, uwepo Mtukufu wa Mtume wa Mwisho Muhammad SAW ni sawa na safina ya Nabii Nuhu ya umma huu (umma wa Muhammad). Ndio, umma huu katika kipindi chote cha historia yake ulikabiliana na milima na mabonde; kuna wakati ulipata fakhari na mafanikio na kuna wakati ulipaa hasara na kukumbwa na madhila. Kwa hakika kuna wakati umma huu ulikabiliwa na matatizo yasiyo na wasifu na kukumbwa na matatizo makubwa; hii ilitokana na kuwa umma huu haukupanda safina. Kama tutashikamana kikweli kweli na kwa dhaati kaabisa, tufanye tawasuli kwa ajili ya safina ya uongofu wa Uislamu tukiwa pamoja na Bwana Mtume (rehma na amani ziwe juu yake pamoja na Ahlul Bayt wake) bila shaka ushindi utakuwa ni wa kwetu. Tab'ani, bahari ina mawimbi makali, kuna matatizo, wakati mwingine hujitokeza hofu kubwa, lakini tutakapokuwa tumepanda safina ya mja mteule wa Mwewnyezi Mungu na ambaye ni maasumu, wakati huo kutakuwa hakuna haja ya kuwa na woga wala kukmbwa wasi wasi mkubwa. Hii ndio ile nukta fupi ambayo nilitaka kuibainisha; tambueni kwamba, sifa hizi ni makhsusi na maalumu kwa shakhsia wale wakubwa. Nuhu wa safina hii ni yeye, mlinzi na mtoa himaya kwa umma huu ni yeye, yeye ni wenzo na wasila wa rehma za Mwenyezi Mungu kwa waja wake mmoja mmoja, kwa nyoyo zetu, akili zetu, roho zetu, miili yetu na maisha ya mtu binafsi na ya kijamii; yeye (Imam Mahdi ) ni wasii wa mwisho na katika daraja ya awali ni ule uwepo wa mtukufu wa Bwana Mtume SAW.
Amma kuhusiana na maudhui ya asili ambayo ndio iliyotukusanya hapa. Kwa hakika nyinyi ni miongoni mwa watu ambao mko mstari wa mbele katika harakati ya kijamii ya taifa la Iran; familia kwa upande mmoja na (nyinyi) wahusika kwa upande mwingine. Maneno makuu na ya kimsingi ni haya kwamba, nchi yetu na taifa letu kwa baraka za mwamko wa Kiislamu lilifanikiwa kuufikia mwamko huu kabla ya mataifa mengine na hivi sasa linafanya harakati katika njia hii yenye fakhari kubwa na ambayo ina hatima na mustakbali mzuri. Kila mtu ambaye atakana hili basi atakuwa ni mkanaji wa mambo ambayo ni wadhiha na ambayo yako wazi kabisa.
Kwa hakika Sisi tulikuwa taifa lililobakia nyuma ambalo halikuwa na taathira yoyote katika matukio yote ya dunia licha ya kuwa tulikuwa na vipaji vizuri na licha ya kuwa na historia kongwe ambayo ingekuwa chanzo cha kuwa kifua mbele. Vile vile licha ya taifa hili kuwa na suhula nyingi kijiografia, lakini lilikuwa miongoni mwa mataifa yaliyobakia nyuma na taifa letu lilikuwa limeathirika mno na irada ya madola makubwa ya kimataifa yenye kuingilia masuala ya ndani ya nchi nyingine. Vikosi vyetu vya ulinzi, elimu yetu, masuala yetu ya kijamii, wanasiasa wetu na kamati yetu ya utawala katika kipindi cha miaka yote ilikuwa chini ya taathira ya uingiliaji wa maadui na watu wenye chuki na malengo matukufu ya taifa hili na hivyo kuifanya nchi yetu hii kuwa katika hali mbaya na ya kusikitisha mno. Hata hivyo kulikuweko na kengele za kuzindua katika kipindi chote cha historia hususan katika kipindi cha hivi karibuni, kulikuwa kukiwaka mwanga tofauti, lakini anga ilikuwa ngumu kiasi kwamba, mwanga huo haukuweza kuwaangazia wananchi.
Hali iliendelea kuwa hivi mpaka yalipokuja Mapinduzi ya Kiislamu na mpaka zilipoanza harakati za mapambano. Kipindi cha mapambano (dhidi ya utawala wa Shah) kilikuwa kipindi kigumu mno; matumaini ya kwamba mapambano hayo yangepata ushindi kwa wengine yalikuwa madogo mno yaani sawa na asilimia sifuri; kwa wengine matumaini hayo yalikuwa juu ya sifuri; yaani kwa ifupi hakukuweko na matumaini makubwa ya kufanikiwa mapambano hao kupata ushndi. Kwa hakika Imam wetu mwenye shani (Imam Khomeini MA) akiwa na shakhsia aliyopatiwa na Mwenyezi Mungu na ambaye kwa hakika ni wa kipekee katika zama hizi, aliweza kuiendeleza njia hii. Akiwa na hali ya kujiamini, hekima, ikhlasi, kushikamana na dini na akiwa na imani kamili na Mwenyezi Mungu aliweza kuiendeleza njia hii. Watu waliokuwa katika njia hiyo kuna wengine ambao waliingia na shaka mara mia moja wakati wa kuendelea harkati, walikuwa wakikumbwa na hali ya kusitasita na kutetereka, lakini pindi walipokuwa wakiona azma thabiti ya Imam walikuwa wakiachana na shaka zao na kila kitu kuhuika tena. Mwenyezi Mungu alikuwa akimsaidia, kulikuweko na uwanja uliokuwa umeandaliwa katika ujudi wake, Allah alikuwa akichukua mkono wa Imam na kumsaidia mpaka akafikia katika hatua ya Mapinduzi ya Kiislamu na Mapinduzi haya ya Kiislamu yakapata ushindi na kuwaacha walimwengu wote vinywa wazi wasiamini ile kilichotokea hapa Iran.
Napenda kuwaambia kwamba, hii leo kuna baadhi ya nchi katika ulimwengu wa Kiislamu ambazo zina mwamko wa Kiislamu na bila shaka hili ni jambo lenye baraka sana na sisi tulilipokea hili mwanzoni kabisa; lakini kuna tofauti kubwa. Tunachosema ni kwamba, mwamko wa Kiislamu katika baadhi ya nchi za eneo la Mashariki ya Kati na kaskazini mwa Afrika ni tukio lililojaa baraka nyingi lakini katika upande wa kina, uzito, upana, misikumo na malengo, Mapinduzi ya Kiislamu yaliyofanywa na taifa la Iran yana sifa za kipekee na za aina yake kabisa (ambazo haziwezi kulinganshwa naa mapinduzi yaa hii karibuni Mashariki ya Kati na Kaskazini mwa Afrika). Baadhi ya sifa hizo za kipekee ni pamoja na kushikamana vilivyo wananchi wote wa Iran na nara, kaulimbiu na shabaha za Mapinduzi yao ya Kiislamu, kuenea shauku na hamasa kubwa katika kila kona ya Iran ya Kiislamu pamoja na uwepo makini wa makundi kwa makundi ya watu wenye imani thabiti, irada imara na walioko tayari kujitolea muhanga wakati wowote katika medani ya mapambano kwa ajili ya kulilinda na kuliletea fakhari taifa lao. Wananchi (wa Iran) walikuwa wakitoa nara kwa nyoyo zao na walikuwa wakimiminika mabarabarani na kukabiliana na utaghuti kwa miili yao; hakuna kitu kama hiki duniani.
Mmoja wa viongozi maarufu duniani ambaye sitaki kutaja jina lake alikuja nchini Iran. Nilipokutana naye nilijaribu kumpa maelezo kuhusiana na jinsi Mapinduzi ya Kiislamu yalivyopata ushindi; nikamwambia, hapa kwetu hakukutokea mapinduzi ya kijeshi, hakukujitokea maafisa jeshi vijana kama ilivyo ada ulimwenguni na kuja katika medani ili wauuangushe utawala wa kitaghuti, si vyama vya kisiasa ambavyo vilikuwa na uwezo wa kufanya kitu, na wala si wenye vipaji ambao walikuwa na nafasi muhimu katika hilo, bali ni wananchi na mkusanyiko wao ndio ulliokuwa na nafasi katika hilo na tena wananchi hao walikuwa mikono mitupu yaani bila silaha.
Hii leo tazameni katika baadhi ya nchi wananchi wanaonekana wakiwa wamebeba silaha na kufanya harakati kwa ajili ya kufikia malengo yao; wananchi wa Iran hawakuwa na silaha mkononi. Wananchi wa Iran waliingia uwanjani wakiwa mikono mitupu wakiwa na miili yao tu. Walishikilia nyoyo na roho zao pamoja na damu zao mkononi na kuja uwanjani. Vizuri, hili ni jambo ambalo bila shaka haliwezekani pasina ya kuwa na imani; hili ni jambo ambalo bila ya kuwa na imani thabiti katu haliwezekani. Imani hii thabiti ilienea baina ya wananchi, wakaja katikati ya medani na damu ikapata ushindi dhidi ya upanga na hili ni jambo la kawaida kabisa. Uhakika wa mambo ni kuwa, hakuna nguvu yoyote inayoweza kukabiliana na taifa lolote lile ambalo wananchi wake wanaingia kwenye medani kwa imani na kujitolea muhanga, kwani kwa mujibu wa sunna ya Mwenyezi Mungu, damu huushinda upanga katika mapambano.
Siku zote damu hupata ushindi dhidi ya upanga, pindi wananchi wanapoamua kujitokeza uwanjani na kusimama kidete pasina ya kutetereka. Wakati mimi nilipombainishia kiongozi yule wa nchi moja ya bara la Afrika kuhusiana na ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, alishangaa na kustaajaabu sana kwani kwa hakika hili lilikuwa jambo la kuvutia na jipya kwake. Wakati nilipoona kwamba, baada ya muda katika nchi yake kumetokea harakati ya wananchi, nikahisi kwamba, amepata ilhamu ya muamala na harakati ya Imam wetu (Imam Khomeini) na muamala na harakati ya wananchi wa Iran na harakati hiyo ikapata ushindi. Akafanikiwa kupata ushindi dhidi ya moja ya madola makubwa, khabithi na yaliyokuwa yakitumia mabavu na ukandamizaji ulimwenguni.
Hii ndio iliyokuwa hali ya wananchi wa Iran wakati huo; wote walijitokeza na kuja uwanjani. Ni kutokana na sababu hiyo ndio maana kuanzia siku ya mwanzo viongozi wa nchi hii hawakuhisi kwamba, kuna haja ya kulazimika kusema sana na kutaraji mengi kutoka kwa madola yenye nguvu duniani. Msidhani kwamba, katika nchi fulani ambako kumetokea mapinduzi ya wananchi hivi karibuni na Wamarekani wanaishikiza nchi hiyo, Wamagharibi wanashinikiza na wanawalazimisha viongozi wao kuchukua misimamo fulani, mambo kama haya hayakuweko hapa nchini Iran; kwa nini? Kwa hakika mambo kama haya yalikuweko pia hapa Iran. Hapa nchini pia mashinikizo haya haya yalikuweko, isipokuwa hakuna mtu ambaye alikuwa akiyapa umuhimu na kuyazingatia mashinikizo haya.
Viongozi walikuwa na himaya na uungaji mkono wa wananchi na walikuwa wakitegemea irada ya wananchi, walikuwa hawana wasi wasi na imani ya wananchi juu yao; hivyo basi medani hiyo ilikuwa imejaa kikamilifu watu ambao wana azma na irada thabiti ambayo inaambatana na ghera na uchungu. Hivyo hili lilikuweko na kwa msingi huo hakukuweko na haja ya kuwa na wasi wasi. Hadi leo hali (ya mambo hapa nchini) iko namna hii. Hii leo pia kwa uwezo na tawfiki ya Mwenyezi Mungu Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu haulazimiki kukubali maneno ya dola lolote lile lenye nguvu au kukubaliana na matakwa ya dola lolote lile lenye kuingilia masuala ya ndani ya nchi nyingine. Mfumo unaotawala hapa nchini, unakubaliana na kukipokea kila lile ambalo lina maslahi nalo na unalifanyia kazi na kila ambalo si kwa maslahi yake haukubaliani nalo na unalitupa mbali, hata kama madola yote yenye nguvu yatakasirika na kughadhibika kwa hatua hiyo; hii ndio sera. Hii ni kutokana na kutegemea imani na himaya ya wananchi.
Kuanzia siku ya kwanza ya mapinduzi mpaka leo, malengo makuu ya mapinduzi yamezidi kuwa wazi kwa wananchi. Wakati huo tulisema, Jamhuri ya Kiislamu, wakati huo tulisema, ustawi na maendeleo ya Kiislamu, hatua kwa hatua fasili na maana ya maneno haya yakazidi kueleweka na kufahamika zaidi mbele ya wananchi katika kipindi cha miaka yote hii. Sasa tunafahamu Jamhuri ya Kiislamu ni nini. Baada ya kupita muda, mafuhumu, fasili na maana za istilahi kama vile Jamhuri ya Kiislamu, demokrasia ya kidini ya Kiislamu, uhuru na istiklali, zimezidi kuwabainikia wazi wananchi pamoja na watu wenye vipawa na wanasiasa na mambo ya lazima na yasiyo ya lazima, yanayotakiwa na yasiyotakiwa nayo pia yamezidi kuwa wazi kama ambavyo katika miaka yote hii harakati ya kufanikisha malengo hayo imekuwa ikiendelea na jambo hilo ndiyo maendeleo makubwa zaidi ya taifa la Iran.
Kwa hakika maendeleo ya kustaajabisha katika sekta tofauti za kielimu na kiteknolojia bila shaka ni vitu vinavyoonyesha upya na ustawi wa hali ya juu wa matawi yaliyojaa majani ya kijani kibichi ya Mti Mzuri wa mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Mwenyezi Mungu anasema katika Kitabu Kitakatifu cha Qur'ani:
"Ni kama mti mzuri, mizizi yake ni imara, na matawi yake yako mbinguni. Hutoa matunda yake kila wakati kwa idhini ya Mola wake Mlezi. Na Mwenyezi Mungu huwapigia watu mifano ili wapate kukumbuka." (Ibrahim 14:25).
Moja ya maendeleo ya mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu unaotawala hapa nchini ni kwamba, kadiri muda unavyosonga mbele ndivyo mizizi yake inavyokuwa imara na madhubuti, matawi na majani yake yanakuwa makubwa na mapana na hivyo kuufanya mwili wa mfumo huu kuwa imara na wenye nguvu zaidi na zaidi. Hii leo mwili wa Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu una nguvu zaidi ikilinganishwa na miaka ya 59, 60 na 61 (Hijria Shamsiya).
Wakati huo maadui zetu walikuwa na matarajio zaidi kwamba, wanaweza kuuangusha mfumo unaotawala hapa nchini. Kuzidi kina cha mizizi na msingi madhubuti wa jengo la Jamhuri ya Kiislamu ni kielelezo kingine cha maendeleo uliyopata mfumo wa Kiislamu nchini Iran. Unapokisia miaka ya awali ya Mapinduzi ya Kiislamu na hivi sasa utaona kuwa, sasa hivi adui amezidi kuwa dhaifu katika njama zake za kutaka kuupindua mfumo wa utawala wa Kiislamu ambao taifa la Iran limejichagulia na kwa sehemu kubwa adui amekata tamaa na kuvunjika moyo kabisa. Bilaa shaka uhakika huo unazidi kuthibitisha jinsi uimara na umadhubuti wa Jamhuri ya Kiislamu usivyopenyeka.
Kwa hakika haya ni mambo ambayo yanaonesha kwamba, Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu una nguvu. Huku kuwa imara na madhubuti Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu na mizizi yake kuzidi kuwa na kina ambako kunaongezeka siku baada ya siku kunatokana na nini? Je kunatokana na imani madhubuti na imara? Je kunatokana na maarifa na upeo wa hali ya juu (wa wananchi) ? Je kunatokana na kupenya imani na kuingia katika nyoyo? Kunatokana na kuwa salama kwa nara? Je kunatokana na uongozi madhubuti, imara na wenye busara wa Imam Khomeini (quddisa sirruh) Mwasisi na Mwazilishi wa Jamhuri ya Kiislamu? Kunatokana na nini hasa? Tab'ani, hii ni mijadala muhimu kwa vijana wetu, wanachuo wetu wa Vyuo Vikuu na Vyuo Vikuu vya Kidini (Hawza). Wanachuo huo wamefanya mijadala hii, wanafanya na bado wanatakiwa kuifanya. Kwa hakika mimi sina kazi na mijadala hii, kile ambacho kiko ni harakati hii ambayo ni ya maendeleo na ya kusonga mbele. Maendeleo haya yamepatikana. Huu ndio msingi wa kadhia.
Wakati mnapoingia katika matawi, pia mnashuhudia ishara za ustawi na maendeleo. Kwa mfano tumepiga hatua katika uga wa elimu na vile vile katika uwanja wa teknolojia tumepiga hatua kubwa. Nakumbuka miaka 20, 24 na 25 iliyopita, niliwahi kukitembelea hiki hiki Chuo Kikuu cha Jeshi la Majini. Tab'ani, tangu wakati huo hadi sasa nimekitembelea Chuo Kikuu hiki mara kadhaa. Kwa hakika hali kilichokuwa nacho Chuo Kikuu hiki wakati huo na sasa haiwezi kulinganishwa hata kidogo. Sasa hivi hali ya shauku na msukumo imekuwa na kuongezeka, harakati ya elimu nayo imeongezeka kwa hakika hili ni tukio la kustaajabisha ambalo linamfanya mtu kuwa na utulivu mkubwa; mtu ambaye ana welewa na ufahamu hupatwa na hali ya kustaajabisha. Tab'ani, kila mahala hali iko namna hii; hali iko namna hii katika Vyuo Vikuu mbalimbali hapa nchini na katika vituo vya utafiti hapa nchini pia hali iko namna hii. Katika vituo ambavyo havikuweko, vikanzishwa nako kuna hali kama hii, matumaini ya wasomi wetu yako namna hii.
Wasomi wetu wa vizazi vilivyotangulia, ambao uwepo wao ni wa kuheshimiwa sana kwetu, ambapo sisi tunamtukuza na kumheshimu kila mtu ambaye amefanya hima na juhudi katika njia ya elimu. Kwa hakika hivi sasa pia wasomi vijana wa Kiirani wanaendelea kupata maendeleo na mafanikio makubwa katika nyuga mbali mbali za kielimu, uvumbuzi, ubunifu na utengenezaji wa vitu mbali mbali vinavyohitajia ujuzi na utaalamu wa hali ya juu kiasi kwamba, inakuwa ni vigumu kwa watu wengine kuamini mafanikio hayo. Kupita kwa zama pia kumeonesha kwamba, maendeleo haya yamepatikana. Na mimi napenda kuwaambia nyinyi kwamba, vijana wetu hawa wanafanya kazi na mambo makubwa katika uga wa elimu, maendeleo ya kielimu na ubunifu ambao yamkini mafanikio haya yasiaminiwe na kizazi chetu cha kati, ingawa kwa sasa inaoneka kuwa, kidogo kidogo maendeleo haya yanaanza kuaminiwa na wote.
Vituo vya kielimu vya kimataifa vinatangaza kwamba, ukuaji wa elimu nchini Iran uko mbele mara kumi na moja na wakati mwingine mara kumi na tatu katika takwimu zao mbalimbali ikilinganishwa na kiwango cha kati cha ukuaji wa elimu duniani! Hata hivyo hii haina maana kwamba, sisi tuko mbele kielimu ikilinganishwa na vituo vyote vya elimu duniani; hapana, bado tuko nyuma sana, ukuaji wetu katika uga wa elimu ni wa kasi. Ndio, endapo tutaendeleza ukuaji huu (wa elimu) kwa kasi hii hii iliyopo, bila shaka katika miaka ijayo, katika kipindi cha miaka kumi ijayo au kumi na tano ijayo, tutakuwa katika daraja ya kwanza katika nyuga zote za kielimu, na kiteknolojia, lakini kwa sasa hapana, bado tuko katikati ya njia na tunafanya harakati. Hii ni katika sekta ya elimu. Hali hii hii iko katika uwanja wa kisiasa, hali kama ambapo hali hii pia iko katika suala la mahudhurio katika masuala ya kimataifa na vile vile hali kama hii inashuhudiwa katika asasi za kijamii na katika sekta mbalimbali, kiujumla kuna maendeleo tofauti tofauti katika viwango mbalimbali ambapo katika sekta fulani kuna maendeleo makubwa na yanayoonekana wazi zaidi na katika baadhi ya maeneo yanaonekana kidogo. Nchi iko katika hali ya kupata maendeleo na kupiga hatua.
Maendeleo haya yanapaswa kuendelea. Maneno yangu ni haya: kila mtu ambaye yuko ndani ya jengo la Iran chini ya bendera ya Uislamu, na anafanya harakati na kukaribia malengo matukufu, basi (atambue kwaamba) ana hisa na bila shaka uwepo wake una thamani. Kila mtu hisa yake imma ina taathira zaidi au inaambatana na hatari zaidi au ni miongoni mwa watu walioko mbele katika kafila (msafara), hisa yake ina fakhari zaidi na humfanya awe juu ya wengine.
Hatupaswi kuchoka wakati wowote ule. Mwenyezi Mungu anasema katika Kitabu Kitakatifu cha Qur'ani kwamba:
"Na ukipata faragha, fanya juhudi" (Ash'Sharh 94:07).
Katika aya hii inaonesha kwamba, wakati unapomaliza kazi (yaani unapopata faragha) usimame na kuacha kufanya juhudi kwa maana kwamba, yaani unapaswa kuanza kufanya kazi nyingine; suala la kusimama na kuacha kufanya kazi halipo hata kidogo. Allah anasema: "Na ukipata faragha, fanya juhudi. Na Mola wako Mlezi ndio mshughulikie." (Ash'Sharh 94:7-8).
Fanyeni harakati nzuri kuelekea upande wa malengo makuu na matukufu yaliyokubaliwa na yaliyotangazwa na Uislamu, huku ndiko kumshughulia Mwenyezi Mungu. Tab'ani, masuala ya kimaanawi yana nafasi muhimu katika mahuasiano na mawasiliano ya nyoyo na Mwenyezi Mungu. Hili ni jambo ambalo linapaswa kufahamika na wote.
Vizuri sasa tunafika katika suala la familia. Familia tukufu za wapiganaji (mujahidina) wetu, iwe ni wapiganaji katika jeshi, au Kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH, au iwe ni katika jeshi la polisi au wawe ni wafanyakazi katika Wizara ya Ulinzi - hawa hawa ambao kamanda hapa ametaja majina yao - na wake zao, wanapaswa kutambua kwamba, wanamsaidia nani, mshirika wa maisha yao ni nani. Mshirika wa maisha yenu ni watu ambao wana nafasi muhimu katika jengo hili refu na lenye hamasa; vikosi vya ulinzi navyo kwa upande mwingine.
Kama anavyosema Imam Ali bin Abi Talib (Alayihs Swalaat Wassalaam) ni husuni (ngome) ya raia na husuni na ngome ya kimaanawi ya nchi. Uwepo wa vikosi vya ulinzi vyenye kujitegemea, vyenye ufahamu na welewa, ubunifu, ushujaa, kujitolea ni vyenye kuleta na kusimamia amani na usalama wa nchi bila hata ya kufyatua risasi; hukabiliana na maadui na kuwashinda. Vikosi vya ulinzi vina umuhimu wa namna hii. Hivyo basi, nyinyi ni wake wa watu hawa (wa namna hii na wenye umuhimu huu).
Ndio, kamanda mheshimiwa amesema kwa niaba yangu hapa - mimi pia yamkini nikawa nimelisema hili mara kumi au zaidi - ya kwamba, nyinyi wanaume kila fadhila na utukufu ambao mnaupata katika medani ya jihadi na mapambano, nusu yake ni mali ya hawa wanawake ambao ni washirika wenu katika maisha, wanaishi na nyinyi. Endapo mume wa mtu ataingia katika medani - ataingia katika medani ya jihadi, mapambano, kazi na hima - mkewe akawa hayuko pamoja naye au amsumbue au akayafanya maisha na yeye kuwa magumu, kwa hakika mume huyo hawezi kufanya kitu, yaani hawezi kupata mafanikio katika kazi na shughuli zake kama inavyotakiwa. Hivyo basi yafaa mtambue kwamba, kama mnaweza kufanya kazi vizuri na kupata mafanikio katika kazi zenu, hili linatokana na baraka za uwepo wa mke huyu mwema na mwenye huruma.
Hili ni jambo ambalo kwanza wenyewe wake wanapaswa kulianisha na kuliona. Nyinyi (wanawake) wenyewe mnapaswa kutambua thamani ya hili kwamba, mume ambaye anafanya hima na juhudi, nusu ya ujira wake ni mali yenu. Kwa hakika nyinyi mnapaswa kutambua thamani ya mume ambaye anafanya hima na idili na ana nafasi muhimu katika jengo refu la Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu na Mfumo wa Kisasa wa Kiislamu; na Inshallah hili liwe ni uwaandaaji uwanja na mazingira ya Ustaarabu wa Kisasa wa Kiislamu. Mwanaume huyu ni mumeo, anatambulika kwako kwa utambulisho huu. Watoto nao ni hivyo hivyo. Watoto wa wafanyakazi wa vikosi vya ulinzi wanapaswa kujifakharisha na baba zao.
Kwa hakika naona ni lazima hapa nionyeshe heshima na taadhima pamoja na kutoa salamu kwa familia tukufu za mashahidi na kutuma salamu kwa roho tukufu za mashahidi; shahidi ambaye ameutoa ujudi na uwepo wake wote, yaani rasilimali yake kuu katika njia Tukufu ya Mwenyezi na katika kumhudumia Mwenyezi Mungu na akakubaliwa katika hilo (yaani akapata fakhari ya kuuawa shahidi). Kuna watu wengi ambao walikwenda vitani lakini hawakukubaliwa, kutokana na sababu mbalimbali; wengine Mwenyezi Mungu aliwaona hawana ustahiki na baadhi ya wengine Mwenyezi Mungu aliwabakisha kwa ajili ya majukumu, masuuliya na kazi nyingine ambazo ni lazima kufanywa. Sasa wale ambao walistahiki wakaenda (yaani wakauawa shahidi) kwa hakika hawa wana daraja na thamani kubwa mno.
Kwa hakika mashahidi ni nuru ing'arayo katika jamii, nuru ambayo inaangazia mustakbali na historia (ya jamii). Familia zao nazo zimesubiri; subira katika mapambano na jihadi ya mashahidi hao na subira ya watu wao kwenda katika medani hatari ya vita. Kwa maneno mepesi zaidi ni kwamba: mke ambaye anaona mumewe anakwenda na kuelekea katika upande wa medani hii ambayo ina hatari naye anasubiri na kustahamili, kwa hakika kazi yake hii ya kusubiri ina thamani sana, kazi ya mk huyu ina thamani mno; kisha pindi mume huyo anapouawa shahidi, mke huyu anasimama imara na kuvumilia hili akiwa ameshikamana kikamilifu na subira. Napenda kusema hapa kwamba, kama uvumilivu wa familia za mashahidi usingelikuweko, basi harakati hii ya kuuawa shahidi katika njia ya Mwenyezi Mungu isingekuwa ya kustaajabisha na yenye nishati namna hii (kama ilivyo leo) katika jamii yetu. Ni familia hizi za mashahidi ndizo ambazo zimeiletea fakhari kubwa jamii yetu na kulionyesha suala la kuuawa shahidi kuwa tamu kiasi hiki. Ala kulli haal, kuonyesha heshima, taadhima pamoja na kutoa salamu ni jambo la lazima. Watoto wao (watoto wa mashahidi) na watoto wenu nyinyi wafanyakazi wanapaswa kujifakharisha, wanapaswa kujifakhrisha kwamba, baba zao walifanya harakati katika njia hii.
Napenda kusema hapa pia kwamba, muelekeo uko wazi na wenye kuonekana. Tab'ani, hatutaraji kuona kanali fulani ya televisheni ambayo ni kibaraka na serikali fulani ya Kiistikbari ije na kunibainishia mimi na nyinyi uhakika huu; hapana, watu hawa wanaionesha anga kwamba, ina kiza. Maadui hao wanafahamu na kuamini kwamba, moja ya njia za kulisimamisha taifa hili na kulifanya lisisonge mbele ni kulinyang'anya matumaini lililonayo. Ndio maana wanafanya njama kila leo za kuonyesha kiza na weusi. Pembe tatu ya shari na ufisadi ni nyinyi wenyewe ambao mmeleta jina hili na kuwapatia wengine. Sasa sisi hatujasema, lakini nyinyi mumesema; Marekani, Uzayuni na Uingereza ni makhabithi na kwa hakika hawa wako namna hii. Vyombo vyao vya kipropaganda vinafanya njama usiku na mchana ili viathiri akili na fikra za wananchi wa Iran na kama nilivyosema hivi karibuni ni kuwa, wanataka kubadilisha mahesabu ya wananchi na mahesabu ya watu wenye vipaji hapa nchini. Alhamdulilahi kadiri wanavyofanya juhudi wanaanguka na kukwama, mustakbali uko wazi; na muelekeo ni muelekeo mzuri isipokuwa hii haina maana kwamba, tuchukue mto mlaini na tuegemeze kichwa chetu na kulala usingizi mnono, hapana, ni lazima kufanya kazi na ni lazima kufanya hima na juhudi.
Hima haitambui wakati wala zama na wala haitambui kustaafu. Katika kipindi chote katika maisha ya mwanadamu, kuna uwezekano wa kufanya hima, ni lazima tuupate uwezekano huu na tufanye, hima, idili na juhudi na tufanye harakati tukiwa jaddi kabisa. Katika Dua Kumayl, Amir al-Muminina Imam Ali bin Abi Talib (Alayihs Swalaat Wassalaam) anamwomba Mwenyezi Mungu akisema:
Nifanye niwe na nguvu ya kutoa huduma na unijaalie azma thabiti. Na unipe azma thabiti katika kukuogopa".
Kwa maana kwamba, tumfanye na kumtambua Mwenyezi Mungu kuwa yupo na Ndiye Mwenye kusimamia mambo yetu na tuwe na hisia ya jaddi; isiwe kwamba, ni kutamka tu haya kwa ulimi yaani kwa kucheza na ulimi tu.
Kisha Imam Ali bin Abi Talib (Alayihs Swalaat Wassalaam) anaendelea kusema katika Dua Kumayl akisema kwamba, anamuomba Mwenyezi Mungu amjaalie kuwa ni mwenye kudumu katika kumhudumia Mwenyezi Mungu. Yaani awe na hali ya kuendelea katika hilo na isiwe ni ya msimu na ya muda fulani tu. Inshallah, vijana wetu wakiwemo vijana wa Chuo Kikuu hiki na vijana wengine, Mabasiji Azizi, vijana waumini, wenye kujitolea, wanachuo mbalimbali, mabinti na vijana wa kiume katika sehemu mbalimbali za uwanja wa kiuanafunzi, matalaba (wanafunzi wa masomo ya dini) azizi na vijana, vijana wa matabaka mbalimbali watatuonesha sisi wazee nguvu na nishati kwa kazi zao, hima na juhudi zao na watatufundisha tufanye vipi harakati.
Ewe Mwenyezi Mungu! Tunakuomba ushushe baraka na rehma Zako kwa mjumuiko huu; tunakuomba ulishushie taifa la Iran baraka na rehma Zako. Tunamuomba Mwenyezi Mungu ayafanye mataifa ya Kiislamu popote yalipo duniani yawashinde maadui. Tunamuomba Allah! Atupe sote sisi baraka za dini na dunia.
Ewe Mwenyezi Mungu! Tunakuomba uufanye moyo mtakatifu wa Walii Asr (roho zetu ziwe fidia kwake) na awe radhi nasi; tunamuomba Allah atujaalie kwa miongoni mwa wanaoombewa dua na Imam wa Zama (Imam Mahdi roho zetu ziwe fidia kwake). Tunamuomba Allah aifufue roho takasifu ya Imam Khomeini (quddisa sirruh) pamoja na mashahidi wetu azizi na mawalii Wake.

Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.

 
< Nyuma   Mbele >

^