Skip to content

Habari

Habari
Hifadhi

Risala na Barua

Matini
Hifadhi

Kumbukumbu na Simulizi

Kabla ya Mapinduzi
Baada ya Mapinduzi

Sauti na Taswira

Picha
Sauti
Video
Mkutano Kiongozi Muaedhamu na Washiriki wa Kongamano la Sita la Taifa la Vijana wenye Vipawa Chapa
03/10/2012
Ifuatayo ni hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Udhma Khamenei katika mkutano na washiriki wa kongamano la sita la taifa la vijana wenye vipawa
Kwa jina la Allah Mwingi wa rehema Mwenye kurehemu
Kwanza inapasa nikupeni mkono wa hongera nyinyi nyote vijana wapenzi ambao kwa kweli ni wana vipenzi wa taifa hili na nuru ya macho yetu, kwa kuwemo kwenu katika majimui ya wenye vipawa nchini. Bila ya shaka "hongera" hii ni sawa na mkono wa hongera ya sherehe ya kuzaliwa, ambapo katika sherehe ya kuzaliwa watu humpa mtu mkono wa hongera ilhali yeye mwenyewe hakuwa na nafasi yoyote katika kuainisha wakati wa kuzaliwa kwake, tarehe ya kuzaliwa kwake wala asili ya kuzaliwa kwake. Kwa hivyo hii ina maana kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu amekupeni nyinyi fursa, na bahati nzuri nyinyi mumepata taufiki ya kuitumia fursa hii na kuwa miongoni mwa wale waliomo kwenye majimui ya wenye vipawa; kwa sababu hii hongereni; lakini kipawa hiki, uwezo huu na hali hii mliyonayo hadi sasa ni mwanzo wa safari na si mwisho wa safari; hili linapasa kuzingatiwa na vijana wetu wapenzi wenye vipawa.
Sisi hatujaridhika, na nyinyi pia msiridhike kwa sababu tu kijana wetu huyu mwenye kipawa na kipaji ameweza kuonyesha kipawa chake katika sehemu fulani na katika mtihani mmoja mkubwa; kwa kiwango hiki si mimi nimeridhika wala nyinyi pia msiridhike nacho. Matarajio yangu na matarajio yenu nyinyi yanapasa yawe ni kuona mbegu hii iliyochopua inageuka kuwa mmea imara na kugeuka kuwa mti mzuri ambao تؤتى اكلها كلّ حين باذن ربّها "hutoa matunda yake kila wakati kwa idhini ya Mola wake" (Suratu Ibrahim, aya ya 25); muwe mti unaozaa, muweze kutoa matunda yenu matamu katika zama zote na katika nyakati zote kwa nchi hii, kwa wananchi hawa, kwa historia hii na hatimaye kwa jamii nzima ya wanadamu; lengo linapasa liwe hili.
Amma kuhusu kikao cha leo. Nimeyasikiliza kwa makini maelezo yaliyotolewa na vijana hawa wapenzi waliokuja hapa. Nasadikisha kwamba maoni yao yalikuwa maoni mazuri na yaliyokamilika; si kwa maana kwamba kwa mtazamo wa kitaalamu mtu anaweza kusadikisha na kuyakubali mapendekezo yote haya - hili linahitajia uhakiki - lakini ni kwa mtazamo wa kwamba mtu anahisi na anaona kuwa maoni haya na mapendekezo haya yamefanyiwa utafiti na kutolewa baada ya kupimwa na kutafakariwa; hili ni jambo lenye thamani kubwa kwangu mimi.
Waheshimiwa viongozi wamehudhuria kikao hiki - waheshimiwa mawaziri kadhaa na mkuu wa Taasisi ya Wenye Vipawa - mategemeo yangu ni kwamba maoni waliyotoa vijana hawa wapenzi yatazingatiwa, yatashughulikiwa na kutafitiwa. Si hasha yakawa cheche zitakazogeuka kuwa nuru kubwa na mwenge utakaotanda na kuangazia anga yote. Na izingatiwe pia kuwa maoni haya yametolewa na nyoyo zenye nia safi; hili pia lina umuhimu mkubwa. Katika maelezo yote haya yaliyotolewa na jamaa, na mimi nimeziandika nukta zake kuu, mtu anashuhudia nukta hii, kwamba maelezo haya yametokana na nia safi, upendo na hisia tamu zilizomo akilini mwa kijana na moyo wa kijana, ambaye anajihisi ana jukumu na anazungumza kwa matumaini na uchangamfu. Haya ni katika mambo yanayoifanya anga iwe tamu hasa. Wakati vijana wanapozungumza kwa moyo kama ule, kwa uchangamfu kama ule na kwa matumaini kama yale, anga iliyopo inakuwa anga iliyojaa uchangamko; kwa hivyo aghalabu ya mapendekezo haya yako hivyo. Lakini maelezo haya ni maelezo yaliyokamilika pia; yaani yale waliyoyaeleza jamaa sikuyahisi kuwa ni mapendekezo machanga.
Huu ndio msingi mkuu wa maendeleo ya nchi. Katika moja ya matukio muhimu ya vita - na huenda wakati ule wengi wenu mlikuwa hamjazaliwa - Imamu wetu muadhamu (Khomeini) alitoa ujumbe katika kadhia ya moja ya operesheni zilizopelekea wapiganaji kupata ushindi. Katika ujumbe huo ilikuwemo nukta kwamba ushindi mkubwa kabisa wa Mapinduzi ya Kiislamu utafikiwa kwa kuwaandaa vijana hawa. Watu wote walitegemea kuwa Imamu atasema ushindi huu mliopata ndio ushindi mkubwa kabisa (fat - hul futuh); na atausifu ushindi huo; lakini Imamu hakufanya hivyo, aliwashukuru wapiganaji lakini akasema ushindi mkubwa kabisa wa mapinduzi yetu ni kuwaandaa vijana hawa; ambapo katika mazingira yale magum, wakati ulimwengu mzima wa kibeberu uliokunja uso kwa ukali ukiwa umeshikilia silaha mkononi tayari kutufyatulia, vijana hao waliweza kupata ushindi mkubwa kama huo; ilikuwa ni operesheni ya Njia ya Quds. Mimi pia ninayarudia maneno hayahaya: Huo ndio ushindi mkubwa kabisa wa Mapinduzi ya Kiislamu. Maendeleo ya kweli yatapatikana pale vijana wetu na wenye vipawa wetu watakapojihisi kuwa wana jukumu kuhusiana na mustakabali; watakapoweza kuwa na mtazamo utakaotokana na wao wenyewe; watakapoweza kubuni na kutoa taswira yenye kuhisika ya mustakabali wa nchi na kubainisha kwamba wako tayari kufanya jitihada kwa ajili ya kuufikia mustakabali huo. Hii ndio hali iliyopo leo hii; na hali hii inapasa kutiwa nguvu na inapasa kuendelezwa. Hali hii na moyo huu wa uchangamko na ukakamavu unapaswa kuimarishwa zaidi ndani ya jamii yetu siku hadi siku. Kama itakuwa hivyo hapo ndipo hii rasilimali yenu binafsi - hiki kipawa na hiki kipaji ambacho ni rasilimali binafsi - itabadilika kuwa rasilimali ya taifa; ni jambo zuri lililoje hilo. Mtu hubadilisha rasilimali yake kuwa dhahabu na sarafu za kigeni kisha akaenda kuificha sandukuni ndani ya nyumba yake; hii ni wapi na wapi kulinganisha na yule ambaye huibadilisha rasilimali yake kwa utaalamu wa kiviwanda, wa karakhana na kuitumia kwa kazi ya uzalishaji wenye thamani utakaoifanya nchi ipige hatua mbele. Kutokana na harakati yenu katika njia ya kufikia malengo haya, mnakuwa mnaifanya pia hii kazi ya pili; yaani rasilimali yenu binafsi mnaibadilisha kuwa rasilimali ya taifa, rasilimali ya wananchi wa Iran; hili ni jambo lenye thamani kubwa.
Bahati nzuri anga ya kifikra iliyotawala nchini ni ya kuelekea kwenye maendeleo ya elimu; alhamdulillah hili sasa limekuwa suala thabiti na lililoenea rasmi nchini. Harakati ya kielimu nchini ni harakati inayokwenda kwa kasi - kama ambavyo takwimu za kimataifa pia zinaonyesha hivyo - lakini hofu ni kwamba hisia ya kuridhika tunayopata kutokana na nafasi hii na hali hii isije ikatufanya tusijali chochote tena na kupunguza hima na bidii yetu. Ninayarudia yale maneno ya awali kwamba vijana wangu wapenzi! nyinyi ndio kwanza mko mwanzo wa safari, na nchi pia iko mwanzo wa safari. Hebu angalieni, sisi tumeachwa nyuma ya msafara wa harakati ya elimu duniani kutokana na uhabithi, ulegevu, uimla na utegemezi wa tawala mbalimbali tulizokuwa nazo nchini katika kipindi cha zama za hivi karibuni. Tunaweza kusema kuwa tuko nyuma kwa takribani karne tatu. Viongozi wa kisiasa nchini na washika hatamu za uongozi wa nchi waliokuwa wameghiriki kwenye starehe na anasa na kujali mahitaji yao ya binafsi tu huku wakiwatizama wananchi kwa kiburi na takaburi, walikuwa wameghafilika na hali iliyokuwepo ulimwenguni; hivyo tukapata hasara kwa upande wa kisiasa na tukapata hasara kubwa zaidi kwa upande wa maendeleo ya kielimu. Katika medani hii ya mashindano, ambapo kwa muda wa karne kadhaa zilizopita sisi tulikuwa wa mbele kuwapita wengine, baada ya wengine wote kupiga hatua mbele kwa takribani namna moja, mataifa mbalimbali yaliweza kupata wenzo wa kuongeza kasi na kututangulia; kwa sababu hiyo pengo la kubakishwa sisi nyuma likaongezeka na kuongezeka. Kwa vile wao walikuwa mbele kuliko sisi walipiga hatua mbele zaidi wakapata wenzo wa kuwafanya waongeze kasi zaidi na kwa hivyo pengo likaongezeka zaidi na zaidi - hii ni hali ya tamathali - kwa kuwa sisi tulikuwa tumesimama au sana sana tulitosheka na mabaki ya kazi zilizofanywa na wengine na vile vilivyotengenezwa na wengine pengo lililokuwepo kati yetu na dunia ambayo siku baada ya siku ilikuwa ikiendelea kugundua mambo katika medani mpya likazidi kuongezeka. Mapinduzi ya Kiislamu yalipokuja yalituamsha sisi sote, yakatutia hima na kuvifanya vipawa vijitokeze uwanjani. Kasi tuliyonayo leo hii ya kielimu ni mara kumi, mara kumi na moja bali hata mara kumi na tatu zaidi kulinganisha na kasi ya kawaida na ya wastani wa kielimu ulimwenguni. Hili ni jambo zuri sana lakini pengo lililopo ni kubwa sana. Ikiwa mathalani kwa muda wa miaka ishirini - na mimi hapa napigia mfano miaka ishirini, sisemi kwa kutumia mahesabu kamili; ninasema kwa kukisia tu - kama tutaendelea kupiga hatua kwa kasi hiihii ya mara kumi na mbili zaidi kulinganisha na maendeleo ya kielimu yaliyofikiwa duniani tutaweza kufikia kwenye ile nukta inayolaiki kufikiwa na taifa la Iran; inayolingana na historia yetu, zama zetu zilizopita, urithi wetu wa kielimu na inayolingana na umuhimu tuliolipa suala hili. Kwa hivyo tusikubali harakati hii ikabaki nyuma. Ikiwa itabaki nyuma itakuwa vigumu zaidi kuirudisha tena na kuijenga tena. Na hii ni kazi yenu nyinyi vijana. Vijana wanapaswa wazidishe hima na bidii. Mhisi kwamba nyinyi mko mwanzo wa safari ndefu na nchi pia iko mwanzo wa safari ndefu na muhimu.
Tab'an nakuusieni kuwa msishtushwe hata kidogo na maendeleo ya Magharibi, maendeleo yale yamepatikana kutokana na kuingia mapema katika awamu fulani na yametokana na dhulma, uistikbari na ukoloni. Laiti kama Waingereza wasingeikoloni India, Burma na eneo lile tajiri la Asia, kama wasingelighusubu na kunyakua utajiri wake - na wao wenyewe India wameielezea kwa uzuri kabisa hali hii katika kipindi fulani cha historia - ni wazi kwamba wasingeweza kufika hapa walipofika. Wao ni mithili ya kupe waliowanyonya wengine wakajitononesha wao; sisi hatutaki kufanya jambo hilo. Sisi hatukusudii kwa namna yoyote ile kuwanyonya wengine. Sisi tunajenga na kuimarisha uwezo wetu wenyewe wa ndani, na tunaamini kwamba itawezekana kwa njia hiyo na inshallah tutasonga mbele. Kwa hivyo hii ni nukta ya kwanza kwamba msikubali harakati hii ikabaki nyuma.
Nukta ya pili ni kwamba viongozi na mamudiri wa vyombo na taasisi husika wana jukumu katika harakati ya kielimu na vilevile wenye vipawa wenyewe, nao pia wana jukumu. Mimi nimefurahi baada ya kuona vijana kadhaa miongoni mwa vijana wetu wapenzi wameeleza bayana hapa kwamba vipawa vyao haviwafanyi wajikweze mbele ya Mfumo wala haviwafanyi wajikweze mbele ya wananchi - maelezo waliyotoa yana maana hiyo - bali wanajihisi wao ni watu wanaoweza kuwatumikia wananchi hawa na ni wajibu wao kutekeleza utumishi huo. Huu ni moyo mzuri sana. Na wakati huohuo kuna hisia za kuwa na majukumu.
Bila ya shaka viongozi pia wamefanya kazi nzuri. Nimefanya uchunguzi na kupokea ripoti za karibu. Mnajua kwamba mimi huwa sitosheki na ripoti wanazokuja kutoa hapa jamaa na mamudiri. Ripoti zinazotolewa kwa njia rasmi aghalabu huwa ni ripoti nzuri za kuridhisha na zilizorembwa na kupambwa; lakini mtu anaweza kugundua ukweli kupitia njia nyengine pia. Mbali na kwamba ripoti walizotoa mamudiri zilikuwa ripoti nzuri na leo hapa pia Bibi Rais wa Taasisi ya Wenye Vipawa ametoa ripoti, lakini mimi nimefanya utafiti pia kupitia njia nyengine nikaona kusema kweli na kwa insafu kuna nzuri inafanywa katika Taasisi ya Wenye Vipawa, na juhudi zinazofanywa ni juhudi nzuri sana.
Nukta nyengine ni kwamba katika uga wa sayansi ya ufundi na uga wa sayansi ya jamii vipimo ni vya namna mbili tofauti. Tab'an kuna kijana mmoja mpenzi hapa anaamini kwamba kuna tofauti pia katika sayansi za ufundi, baina ya sayansi halisi na sayansi za viwanda na ufundi; ambayo hii nayo ni nukta ya kuzingatiwa. Lakini alaa kulli hal kuna upambanuzi katika vipimo na vigezo vinavyotumiwa kivipawa na kitaalamu katika sayansi ya ufundi na sayansi ya jamii. Vipimo si vya hali moja, vipimo si vya namna moja; nukta hii inapasa izingatiwe. Sisi tunahitaji kuandaa mazingira ya kuhakikisha kuwa katika sayansi ya jamii - ambayo leo hii ni hitajio la msingi mno la nchi yetu - tunafikia kwenye ubunifu wa mambo mapya na ya ugunduzi; huu ndio ufunguo wa kufikia kwenye upeo wa maendeleo ya kina na ya msingi ya nchi. Kwa hivyo kuna ulazima wa kuchaguliwa vipimo kwa usahihi.
Nukta nyengine ni kwamba kuwaunga mkono wenye vipawa, katika hatua ya kwanza kabisa kunapasa kuwe na maana ya kuandaa fursa ya utafiti, masomo na maendeleo. Tab'an mimi sipingi asilani utoaji misaada ya kifedha na kimaada na ya vitu kama hivyo bali kuna ulazima hasa wa kufanywa mambo hayo; lakini lililo muhimu zaidi ni kumfanya mtu mwenye kipawa ahisi kuwa anga iliyopo ni ya kumwezesha kupumua kielimu. Taarifa tunazofikishiwa mara kwa mara ni kwamba wenye vipawa na wenye vipaji wana hamu ya kupatiwa uwanja mpana zaidi ili waweze kujifaragua kulingana na vipawa na vipaji vya juu walivyonavyo. Bila ya shaka hili linaweza kufanywa kwa njia mbalimbali. Kutambua njia hizo, kubainisha njia hizo na kutoa mapendekezo si kazi yangu mimi; ni kazi ya wataalamu wanaohusika. Bila ya shaka vijana wana mawazo kadha wa kadha. Mawazo haya yanapasa kuzingatiwa ili kijana mwenye kipawa aweze kuhisi kwamba iko medani na uwanja kwa ajili yake wa kufanyia kazi na kupiga hatua mbele.
Nukta nyengine ni kwamba tuliweke suala la kuwazingatia wenye vipawa na kuwaangalia wenye vipawa katika sura ya mtandao maalumu. Sisi tunamtafuta na kumtambua kijana mwenye kipawa, tunamchagua, tunamsaidia na tunamwandalia mazingira ya utulivu kwa ajili ya kukifanyia kazi kipawa chake; lakini hili halitoshi. Inapasa kuwepo harakati ya kimtandao iliyo amilifu na ya mzunguko ambayo inaanza kwa kumlea na kumwandaa mwenye kipawa; yaani hatua ya malezi na mafunzo. Chimbuko na awamu ya msingi ni katika Wizara ya Elimu na Maandalizi, kama alivyosema mmoja wa vijana. Tunapaswa kuelewa uwezo wa vijana wenye vipaji na kuukuza, kisha baada ya hapo kuna ulazima wa kufanya mchujo na uteuzi; baadhi yao wana vipawa vikubwa zaidi; baadhi yao wana uwezo mkubwa zaidi; kwa hivyo ni kuchagua walio bora zaidi. Baada ya hapo ni hatua ya kuwatunza na kuinua zaidi vipawa vyao; sio kuwatunza tu, bali ni kuwatunza sambamba na uinuaji na uendelezaji vipawa vyao. Wapeni msaada ili kama leo kijana huyu mwenye kipawa yuko katika daraja ya kumi, baada ya muda si mrefu ujao afikie daraja ya kwanza; apande daraja ya juu. Kisha baada ya hapo yeye mwenyewe aingie kwenye mzunguko wa ujengaji wenye vipawa - yaani aingie kwenye hatua ya kimtandao - yeye mwenyewe kijana mwenye kipawa awe mjengaji na mleaji vipawa. Katika hali hiyo itajitokeza hali ya uzalishaji vipawa kutokea ndani na harakati yenyewe itakuwa na uwezo maradufu. Kama sisi tutatumia mbinu kama hii, kazi itaweza kupiga hatua mbele. Nukta nyengine ambayo inawahusu waheshimiwa viongozi husika ni kuhusiana na hati ya mkakati na stratijia ya wenye vipawa; na hii imeshatolewa mapendekezo. Kwa bahati imeandaliwa hati nzuri. Mimi mwenyewe sijaiona lakini mtazamo wa jamaa walioipitia ni kwamba hati hii ya stratijia ni hati nzuri sana na imeandaliwa kwa kujumuisha kila kitu. Imeshapasishwa pia katika awamu ya kwanza na Baraza Kuu la Mapinduzi ya Kiutamaduni, pamoja na hayo inapasa ipasishwe rasmi pia na kutangazwa haraka. Wakati itakapotangazwa, vyombo vyote vishirikiane na kuungana pamoja katika utekelezaji wake. Ikiwa hati ya stratijia - itakuwa imetayarishwa kama nilivyotaarifiwa - itapasishwa na kutangazwa, mengi ya haya masuali na nukta zenye utata zitaondoka wenyewe kwa wenyewe.
Amma kuhusu jukumu lenu nyinyi wenye vipawa wapenzi nimesema kwamba mnatakiwa mjihisi kuwa ndio kwanza mko mwanzo wa safari. Jitahidini kuhakikisha mnabaki katika kiwango cha wenye vipawa. Leo nyinyi ni watu wenyewe vipawa, lakini mko katika shindano; inawezekana kiwango cha elimu nchini kikafikia hadi ambayo kiwango hiki mlichonacho kisiwe ni cha kipawa; ikawa ni lazima mtu afikie kiwango cha juu zaidi ya hapo. Tumeeleza katika hati ya malengo ya miaka ishirini kwamba katika mwaka 1404 (2025) tunataka tuwe tumeshika nafasi ya kwanza kielimu katika eneo. Baadhi ya viongozi wanasema, janabi, wewe umesema ni katika mwaka 1404 lakini hivi sasa ambapo ni mwaka 1391 (2012) sisi tumeshika nafasi ya kwanza kielimu katika eneo. Maneno haya ni sahihi; lakini haya sio makusudio ya maneno yale. Huu sio mwisho wa safari, ni katikati ya safari, ni mwanzo wa safari. Inapasa muwe na uwezo wa kuendelea kuishikilia nafasi hii ya kwanza kuanzia mwaka 1391 - ambao ni mwaka huu - hadi mwaka 1404; angalieni ni mambo gani yanayolazimu kufanywa ili muendelee kuishikilia. Kuna kazi kubwa inayohitaji kufanywa. Mumesema yaa Ali na kupiga hatua kubwa; ni vizuri sana kuwa mumeweza kufikia nafasi ya kwanza; lakini watu wengine nao pia hawajakaa hivi hivi tu. Katika eneo, wengineo pia wanataka wawe katika nafasi ya kwanza, wawe katika nafasi ya juu zaidi; na wao pia wanafanya jitihada. Kwa hivyo inapasa muwe na uwezo wa kuendeleza hali hii ya kipawa. Kuhusiana na nyinyi wenyewe pia ni hivyo hivyo; inapasa muwe na uwezo wa kutoa taathira. Kama nilivyoeleza ni kwamba katika mtandao huu wa wenye vipawa, inapasa muwe na uwezo wa kuyaelekeza mazingira yaliyokuzungukeni kwenye hali ya vipawa; hii ni kazi muhimu, ni moja ya majukumu muhimu ya wenye vipawa.
Jukumu jengine ambalo nimeliandika hapa ni kwamba juhudi mnazofanya mzielekeze katika mahitaji ya nchi. Tab'an hilo limo pia kwenye maelezo waliyotoa jamaa; walilikariri pia katika mikutano na wanachuo na watu wa vyuo vikuu tuliyofanya katika mwezi wa Ramadhani na miezi isiyokuwa ya Ramadhani; lakini linapasa lifikiwe kwa kutekelezwa kivitendo. Ripoti zinazotufikia hivi sasa zinaonyesha kwamba asilimia sabini ya makala zetu za kielimu hazizingatii mahitaji ya nchi. Sijui takwimu hizi zina uhakika wa kiwango gani, lakini hivi ndivyo ninavyopewa ripoti. Mnasumbuka kwa kiwango chote hiki, mnaandaa makala za kielimu kisha ni asilimia thelathini tu kati ya makala hizo za kielimu zinazingatia mahitaji ya nchi, asilimia sabini haziko hivyo! Mtu anahisi kuwa hiyo ni hasara. Inapasa asilimia mia moja ya kazi za kielimu, jitihada za kielimu na uandaaji wa makala za kielimu izingatie mahitaji yenu. Shirikianeni na taasisi ya I.S.I pia kwa msingi huu. Pale ambapo makala inayokubaliwa na I.S.I itakuwa ni ya kitu mnachoweza kukitumia hapa nchini, ifanyieni kazi makala hiyo. Sisi tunacho kipimo chetu cha msingi; kipimo chetu ni kwamba nchi yetu ina mamia ya mishkili, upungufu na hali tupu zilizo wazi, tunataka kujaza uwazi huo. Hii pia ni nukta ya msingi hasa. Tab'an hili linahitajia zaidi ya kitu chochote kile ile njia ya mpangilio maalumu ambayo mmoja wa jamaa hapa ameiashiria, nayo Taasisi ya Wenye Vipawa inapaswa ielekeze jitihada zake katika suala hili.
Nasaha yangu nyengine ni kwamba vijana wangu wapenzi! Jichungeni nafsi zenu. Madhumuni yangu ni si kujichunga kimwili. Jichungeni katika umaanawi, katika kuzitakasa nafsi; hili litakusaidieni. Inabidi tujitahidi ili kuweza kuwa na sura yenye kukubalika mbele ya Mwenyezi Mungu. Nyinyi ni vijana; nyoyo zenu ni safi, roho zenu ni angavu. Pengine tunaweza kusema kwamba kufikia kwenye hadhi na daraja ya juu ya kimaanawi na kiroho ni rahisi zaidi katika umri wenu kuliko kwa mtu wa umri wangu mimi. Nyinyi mnaweza kujenga hali ya kukuelekezeni kwa Mwenyezi Mungu, mnaweza kufanya tawasuli, mnaweza kujenga ukuruba na Mwenyezi Mungu, mnaweza kujiweka mbali na madhambi; hizi ni miongoni mwa sifa za kijana. Angalieni mathalani mwili wa mwanasarakasi kijana katika harakati zake mbalimbali anazofanya, muone jinsi misuli na viungo vyake vya mwili vinavyoweza kunyumbulika; hali ambayo mtu mwenye umri kama wangu mimi hawezi asilani kuufanyia mwili wake hata kwa kiwango cha asilimia moja. Nguvu hii ya mnyumbuliko inatokana na uwezo. Uwezo sawa na huu umo ndani ya roho pia; ndani ya nafsi ya mtu, ndani ya moyo wa mtu. Nyinyi mnao uwezo wa kuzielekeza nafsi zenu kwenye daraja za juu na nafasi aali za kimanawi; lizingatieni hilo kwa ajili ya nafsi zenu. Kuizingatia Sala, kuipa umuhimu Sala ni jambo lenye taathira kubwa. Kuisali Sala kwa mazingatio, kuisali katika wakati wake wa mwanzo, kuisali moyo ukiwa umetulia na kuisali kwa umakini kuna taathira kubwa sana. Kuwa na ukuruba na Qur'ani ni jambo zuri sana. Kila siku someni Qur'ani kwa kiwango fulani hata kama ni nusu ukurasa; jihadharini msiache jambo hilo. Fungueni msahafu; someni kwa mazingatio hata kama ni nusu ukurasa au aya mbili. Hayo ni mambo ya kuyaendeleza. Kuyafanya hayo ndio kule kuchunga umaanawi na kuitakasa nafsi. Mpeni nafasi kijana mwenye kipawa cha elimu - ambaye inshallah iko siku atafikia kwenye kilele cha elimu - aghiriki kwenye umaanawi kwa kiasi ambacho ataweza kuifanyia kazi elimu hii kikamilifu na kwa asilimia mia moja kwa manufaa ya wanadamu. Wakati nyoyo zenu zinapokuwa pamoja na Mwenyezi Mungu, elimu yenu haitotumika tena kuundia bomu la atomiki, silaha za sumu au kwa ajili ya mifumo ya uchumi inayoangamiza utajiri wa mataifa. Leo mwanazuoni wa uchumi duniani, mwanazuoni wa atomiki duniani, wanazuoni mbalimbali duniani wa elimu zinazohusiana na maisha, sehemu kubwa ya matunda ya elimu zao inatumika kuwaangamiza wanadamu, kuangamiza kiwiliwili cha mwanadamu au roho ya mwanadamu. Ni elimu ndiyo inayoweza kuleta maada yenye kuua mithili ya mada hizi zilizoko leo hii; hizo pia zimekuja kupitia njia ya elimu; huo ndio usaliti mkubwa wa watu wenye elimu; wanausahau umaanawi kikamilifu kutokana na kuwa na nyoyo zilizojisahau na macho yenye uchu wa pesa na maisha ya kimaada ya dunia. Wakati nyinyi mnapokuwa mumezitakasa nyoyo zenu elimu yenu itatumika kwa asilimia mia moja kwa ajili ya manufaa ya wanadamu. Huku ni kujichunga kwa kwanza.
Kujichunga kunakofuatia ni kujichunga katika fikra. Imeelezwa kuwa ibada kubwa kabisa ni kutafakari; kutafakari juu ya uumbaji, kutafakari kuhusu wajibu alionao mtu, kutafakari kuhusu maisha ya dunia, kutafakari juu ya Akhera, kutafakari juu ya hali ya kisiasa ya ulimwengu na kutafakari juu ya masuala ya usuli na ya msingi ya maisha ya mwanadamu. Sisi tumekuwa na mageuzi katika elimu na katika maendeleo ya elimu, inapasa tuwe na maendeleo katika fikra pia. Ni fikra na kutafakari ndivyo vinavyotoa dira, mwongozo na muelekeo wa juhudi za kielimu, kiuchumi, kijamii na kisiasa wa jamii mbalimbali. Huku ndiko kujichunga kwa pili.
Kisha kunafuatia kujichunga kuhusiana na hali ya nchi yenu; ni kwa kuwa na mtazamo sahihi na makini juu ya masuala ya nchi na kuyahakiki masuala ya nchi. Leo watu wetu wenye vipawa wanaweza kufanya kazi nyingi nzuri katika masuala haya. Leo sisi tuko kwenye medani kubwa tukikabiliana na kambi ya adui; kambi hiyo si kambi dhaifu; si kambi isiyo na kitu; ina pesa, ina propaganda, ina vyombo vya habari, ina elimu, ina siasa na uwezo wa kisiasa; lakini taifa la Iran na Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu umesimama imara kukabiliana na mashinikizo yote ya kambi hiyo. Wanatoa mashinikizo ya kila namna; kuanzia mashinikizo ya kiusalama, kijeshi, ya mauaji ya kigaidi na ya kuzusha fujo na machafuko na mengineyo mpaka kwenye mashinikizo ya kisiasa, mashinikizo ya kiuchumi, vikwazo na mambo mengine kama hayo. Taifa letu limeweza kusimama imara kukabiliana na yote hayo na kuweza kusonga mbele. Mashinikizo haya yamekuwepo kwa miaka thelathini na tatu, na taifa la Iran, Mapinduzi ya Kiislamu na Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu umeweza kusimama imara kwa uwezo na ushujaa na kuweza kuyazima mashinikizo na pia kuwa imara na wenye nguvu.
Katika ramani ya sasa ya dunia, katika hii karatasi inayoainisha nafasi ya nguvu za kisiasa za ulimwengu na jiografia ya kisiasa ya dunia, tusiidogeshe nafasi yetu, nafasi ya taifa la Iran na nafasi ya Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu; sisi tuko katika nafasi gani? Tuko katika hali gani? Utizameni upimanaji misuli, angalieni mashinikizo na jioneeni kushindwa na kufeli kwa adui. Bila ya shaka mashinikizo ni mengi mno - kutokea pande tofauti - lakini sio sahihi na ni makosa kudhani kwamba kwa kuchukua uamuzi fulani, na tadbiri na hatua fulani tumeweza kumvuta adui upande wetu. Taifa la Iran limeandamwa na hujuma hizi kwa sababu ya kuwa na misimamo huru na kwa sababu ya kutosalimu amri mbele ya mfumo wa ubeberu wa kimataifa. Kwa kuwa taifa letu halijakubali kusalimu amri mbele ya mfumo huu wa kibeberu wanaliwekea mashinikizo ili walipigishe magoti. Lakini sio tu hawajaweza kulilazimisha lisalimu amri bali limeendelea kushikilia zaidi msimamo wake, na nguvu na uwezo wake umekuwa mkubwa zaidi. Hili limewahamakisha maadui na kuwatia kiwewe, na matokeo yake wanafanya makosa mbalimbali kutokana na athari ya kiwewe hicho; na kuna faida na manufaa anayoweza kupata mtu kutokana na makosa hayo wanayofanya. Kwa hivyo vijana wapenzi wenye vipawa waijue nafasi ya Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu.
Na mimi nikuelezeni jambo hili; kutokana na utajiri wa rasilimaliwatu ambayo bahati nzuri iko katika nchi yetu hii leo, tutaweza kuvivuka vigingi vyote vigumu. Ni dhana potofu kudhani kwamba inayumkinika kufikia kwenye kilele pasina kuvivuka vigingi. Kuna wakati wewe unakuwa umekaa nyumbani mwako - ninaupiga mfano huu mara kadha wa kadha - unaangalia nje kupitia dirishani, unaiona milima ya Alborz ambapo watu katika siku ya Ijumaa na siku zisizokuwa Ijumaa huwa wanaelekea juu kuanzia kwenye nukta fulani. Kutokea mle ndani anapokuwa amekaa, mtu huweza kujihisi yeye mwenyewe kuwa yuko pamoja na watu hao katika kilele cha mlima hali ya kuwa hayuko kileleni huko. Ikiwa unataka kufikia kileleni inakubidi uende ukaanzie palepale chini ya mlima, uanze kupiga hatua, uvumilie tabu, utokwe na kijasho, upate machovu na ustahamili matatizo chungu nzima ya njiani mpaka mwishowe uweze kufika kileleni. Kufikia kileleni katika kupanda mlima ni suala la kimichezo tu kwa kufikia kwenye anga ya hewa safi na kuhisi ukunjufu na furaha ya moyo; lakini katika harakati ya taifa kufikia kwenye kilele maana yake ni kufikia kwenye saada ya duniani na Akhera, kufikia kwenye utulivu, raha na kheri zote ambazo taifa linaweza kuzifanyia kazi na kuzifikia. Kutokana na utajiri huu ilionao nchi yetu - utajiri wa watu na pia utajiri wa rasilimali za maliasili - kwa taufiki ya Mwenyezi Mungu taifa la Iran litaweza kuvivuka vigingi hatari vyote hivi pamoja mizunguko hii tata na miinuko hii migumu na inshallah litafikia kileleni.
Ni matumaini yangu kuwa inshallah Mwenyezi Mungu Mtukufu atakuhifadhini nyote na atawapa taufiki pia viongozi ya kutekeleza wajibu muhimu walionao, na inshallah siku baada ya siku tukuoneni mkiwa katika hali ya kupiga hatua na kusonga mbele, na inshallah Mwenyezi Mungu Mtukufu ataiwezesha nchi yetu na taifa letu litoke kifua mbele na kwa heshima katika medani zote hizi.
Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.
 
< Nyuma   Mbele >

^