Skip to content

Habari

Habari
Hifadhi

Risala na Barua

Matini
Hifadhi

Kumbukumbu na Simulizi

Kabla ya Mapinduzi
Baada ya Mapinduzi

Sauti na Taswira

Picha
Sauti
Video
Hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika Mkutano na Wasimamizi wa Hija Chapa
24/09/2012
Kwa jina la Allah Mwingi wa rehema Mwenye kurehemu
Ninamwomba Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa khushuu na unyenyekevu awatakabalie mahujaji na wageni wa Nyumba Yake Tukufu na ajaalie kutakabaliwa kwa Hija yao kuwa sababu ya kupata radhi zake Mola aliyetukuka na njia ya kuteremka baraka zake Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa jamii za Kiislamu. Inapasa niwashukuru kwa dhati maafisa watendaji wa masuala ya Hija na Ziara, wawe ni wale wa majimui ya Bi'tha, taasisi ya Hija na Ziara na vile vile vyombo mbali mbali vinavyotoa ushirikiano wa moja kwa moja na usio wa moja kwa moja, na ninamwomba Mwenyezi Mungu Mtukufu awalipe ujira kila mmoja wao miongoni mwa wale wanaojituma kushughulikia suala hili pamoja na waheshimiwa wasimamizi wa Hija. Nukta zilizoelezwa - iwe ni za janabi bwana Qadhi Askari au mheshimiwa mkuu wa taasisi - na hatua walizochukua au walizopanga kuchukua, zote hizo ni hatua nzuri na za lazima. Juhudi zifanyike ili inshallah kwa kuchukua tahadhari kamili, matarajio yote waliyonayo mamudiri hawa wenye moyo wa kazi yaweze kuthibiti na hivyo tuweze kuitekeleza Hija kwa upande wa sura na maana, na kwa upande wa kalibu na muhtawa kwa namna inayokaribia vile alivyotutaka Mwenyezi Mungu Mtukufu tuitekeleze . Tuweze pia inshallah kuutekeleza wajibu huu adhimu na faradhi hii yenye umuhimu mkubwa - ambayo ina sifa isizokuwa nazo faradhi nyengine yoyote ya Kiislamu; sifa za kuujumuisha umma mzima, sifa ya kuwa na sura ya ulimwengu mzima - kwa namna aliyotaka Mwenyezi Mungu Mtukufu kwetu sisi na kwenu nyinyi.
Mazingira yanapelekea kuwa na hali tofauti. Mwaka huu mazingira ya Hija ni mazingira ya hali maalumu. Kudhihiri na kuonekana kwa uwazi adhama ya Mtukufu Mtume wa Mwisho SAW mbele ya macho ya wapenzi na watu wenye mapenzi makubwa kwake na vile vile mbele ya macho ya maadui, ni moja ya sifa maalumu ilizonazo Hija ya mwaka huu. Kadhia hii, kwamba mikono itendayo madhambi ya maadui, kuhusiana na kuuvunjia heshima utakatifu wa mtukufu huyo, imeyafanya hayo huko Marekani, ni suala lenye hali mbili na pande mbili: kwa upande mmoja linaonyesha ukubwa wa chuki na uadui walionao maadui, waistikbari na vibaraka wao kwa Mtume wa rehma, Mtume wa izza, Mtume wa ukarimu na mbeba thamani bora na tukufu zaidi za sifa za kiutu na za kibinadamu katika kipindi chote cha historia ya maisha ya mwanadamu na katika ulimwengu mzima wa viumbe. Ni suala linaloonyesha ni ukubwa ulioje wa uadui walionao watu hawa kwa Mtume. Katika upande wao mmoja wanafanya vitendo vya kutusi na vya uvunjiaji heshima; na katika upande wao mwengine, msimamo unaochukuliwa na wanasiasa wao katika kadhia hii hauna tofauti yoyote na msimamo wa kiadui! Huu ni upande mmoja wa kadhia, lakini hili lilikuwa na faida kubwa kwa Ulimwengu wa Kiislamu. Hata wale watu wagumu kabisa kuamini mambo pamoja na majimui mbalimbali za watu walifahamu kwamba kambi kuu zinazokabiliana leo hii ni kambi gani na gani; ugomvi uliopo kati ya kambi ya haki na batili ni juu ya suala gani la msingi; imejulikana kwamba ni juu ya asili ya Uislamu wenyewe, ni juu ya mwenyewe Mtume wa Mwisho (Rehma na amani ya Allah ziwe juu yake na Aali zake). Hili ni tukio lililoanzishwa na adui lakini Ulimwengu wa Kiislamu ulifaidika nalo; kwa sababu uliweza kumtambua adui, ulielewa sababu ya uadui na ulielewa chanzo kikuu cha hitilafu baina ya haki na batili. Ugomvi uliopo leo hii ni juu ya mambo haya; mambo mengine yaliyobaki yanayotolewa na kuelezwa na waistikbari wa dunia dhidi ya mataifa ya Kiislamu ni mambo ya nyongeza, ya uwongo na ya kutafuta visingizio; imeshadhihirika wazi chanzo hasa cha kadhia ni nini. Kwa hivyo huu ni upande mmoja wa kadhia.
Upande mwengine wa kadhia ni hii harakati adhimu ya Waislamu. Tizameni ni nini kinachojiri hii leo katika Ulimwengu wa Kiislamu; ni vuguvugu gani la hamasa inayoonyeshwa na wananchi wa mataifa ya Kiislamu. Wengi wao hawajaiona hii filamu; kwa kupata hii taarifa tu kwamba umefanyika uvunjiaji heshima kama huu, angalieni ni taharuki kubwa iliyoje imetokea katika Ulimwengu wa Kiislamu. Pasina kutakiwa na mtu, pasina kuhamasishwa na mtu, wananchi wa nchi za Kiislamu, wananchi wa mataifa ya Kiislamu wanajitokeza kwa ujudi wao wote, kwa moyo wao wote na kupaza sauti zao ili kuonyesha na kudhihirisha mahaba na mapenzi makubwa waliyonayo kwa Mtume wao; hili ni jambo lenye thamani kubwa. Imekuwa ni hali ya kustaajabisha. Katika nchi zenyewe za Mgharibi, huko ambako masanamu makubwa, waistikbari na mataghuti yenye nguvu yamekaa na kupanga kila wakati njama na mipango dhidi ya Uislamu na umma wa Kiislamu, huko Ulaya, Marekani na katika nchi nyengine mbalimbali zisizokuwa za Waislamu, Waislamu na baadhi ya wakati hata wasiokuwa Waislamu wamejitokeza uwanjani. Na huu nao ni upande mwengine wa kadhia. Hii ni kadhia muhimu sana; hii inaonyesha uwezo wa Ulimwengu wa Kiislamu wa kuonyesha harakati.
Tulieleza hapo kabla kwamba kiunganishi cha Waislamu ni shakhsia tukufu ya Mtume. Yaani kinachowaunganisha na kuwakutanisha pamoja Waislamu wote, matapo tofauti, mapote tofauti, madhehebu na itikadi tofauti, na hakika ambayo wote wanaiitakidi na kuikubali ni ujudi na shakhsia takatifu ya Mtume wa Mwisho. Hapa tena haileti maana kuzungumzia Suni na Shia na matapo tofauti yenye mielekeo ya wastani na wa kati na kati, misimamo mikali na kufurutu mpaka na mambo kama hayo. Wote hao, na kwa udhati wao wa moyoni wameungana na wako kitu kimoja juu ya kitovu hiki na mhimili huu na kuhusiana na ngome hii kuu ya itikadi na mafundisho ya Kiislamu. Hii ndio hali inayoonekana leo hii katika Ulimwengu wa Kiislamu; hili linapasa kupewa thamani kubwa.
Hapa ndipo inapopatikana maana ya "Kujibari na Washirikina "katika Hija. Hija ni mahali wanapokusanyika pamoja Waislamu kutoka kila pembe ya Ulimwengu wa Kiislamu. Tamaduni tofauti, rangi na asili tofauti, lugha tofauti, lafudhi na lahaja za aina mbalimbali - kama anavyoeleza Imam Hussein (Alayhi ssalam) katika dua tukufu ya Arafa - wote wanajumuika hapo wakiwa na lengo moja. Umoja huu, ambao sura na muundo wake wa nje unaonekana katika mjumuiko adhimu wa Hija, unapaswa kuimarishwa zaidi; wote wajihisi wanakabiliwa na hatari ya aina moja, wanakabiliana na adui mmoja; wote wajibari na kujiweka mbali na adui huyu kwa udhati wa nafsi zao. Hapo ndipo inapodhihirika maana ya kujibari na washirikina katika Hija.
Hadhi na daraja ya shakhsia takatifu ya Mtume Mtukufu si kitu ambacho sisi watu tunaweza kukibainisha na kukielewa hakika yake kwa ndimi zetu hizi zenye upungufu na fahamu zetu hizi ndogo. Sisi tunadhihirisha mapenzi yetu tu, sisi tunaonyesha ikhlasi zetu na unyenyekevu wetu tu; hakuna tunaloweza kufanya zaidi ya hili. Mtume, ni mtu ambaye Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema kuhusu yeye kwamba: انّ اللّه و ملائكته يصلّون على النّبىّ "Hakika Mwenyezi Mungu na malaika wake wanamsalia Nabii". (Suratul Ahzab, aya ya 56).Yaani dhati takatifu ya Mwenyezi Mungu inamsalia yeye, malaika wa Mwenyezi Mungu Mtukufu wanamuombea rehma yeye; sisi ni akina nani wa kuweza kufahamu na kuelewa cheo na daraja yake? Lakini tunampenda yeye, tuna mahaba na mapenzi makubwa kwake yeye; tunasikiliza na kuyatii maneno yake. Hili ni jambo la msingi ambalo linapasa kuenziwa na kudumishwa: tunapaswa kuyasikiliza na kuyatii maneno ya Mtume; nayo ni maneno ya Tauhidi, maneno ya Uislamu, ni Qur'ani. Hija inapasa kuwa dhihirisho la mambo haya.
Moja ya njama kubwa za adui - ambayo alhamdulillah imezimwa kwa kiwango kikubwa lakini tunapaswa sote kuwa na hadhari - ni kuzusha hitilafu ndani ya umma adhimu na ulioshikamana pamoja. Kwa sababu ya baadhi ya hitilafu za kinadharia, wao wanatugonganisha vichwa sisi, ambao tunaungana pamoja katika usuli, misingi mikuu na katika masuala makuu na ya asili ya Uislamu. Ni sawa kwamba madhehebu za Kiislamu na matapo ya Kiislamu yanahitilafiana katika masuala mbalimbali; lakini pamoja na hayo tuseme kwamba: Sisi tumeungana na tuna mtazamo mmoja katika kukabiliana na nyinyi ambao ni maadui wa Uislamu, na katika kukabiliana na nyinyi ambao mnafanya vitendo viovu kama hivi kuhusiana na shakhsia tukufu ya Mtume. Maadui wa dini, waistikbari na waendeshaji wa kambi inayoupiga vita Uislamu wajue kwamba umma wa Kiislamu umeungana na uko kitu kimoja katika kukabiliana na wao; wafute kabisa dhana ya kuzusha hitilafu; wasiwe na tamaa kwamba wataweza kuzusha hitilafu baina yetu. Wafanya tabilighi wetu, wananchi wetu wote, mamudiri wetu, wafuasi wetu wa madhehebu mbalimbali, masuni wetu, mashia wetu, wote hao wanapaswa wawe macho na suala hili; tujihadhari tusije tukaruhusu adui akaanzisha hitilafu baina yetu - akatufanya sisi tutumie hasira zetu na ghadhabu zetu ndani yetu na dhidi yetu sisi wenyewe - na yeye akaweza kujinusuru na hasira za umma wa Kiislamu; hili litakuwa ni kosa. Hii ni nukta kuhusu Hija na hususan kuhusiana na Hija ya mwaka huu.
Nukta nyengine ambayo imekuwa ikisisitizwa mara kadha wa kadha na ambayo ina ulazima wa kuizungumzia tena ni kwamba ikiwa Hija ni faradhi ya kisiasa, ikiwa ni wajibu wa kijamii, ikiwa ni dhihirisho la umoja, ikiwa ni kielelezo cha mjumuiko wa Waislamu na ikiwa ni kwa ajili ya kubainisha bara'a (kujibari) - na hakuna shaka yoyote juu ya ha yayo - lakini pia ni majimui iliyofurika hisia za kimaanawi; hili halipasi kusahauliwa. Kuanzia mwanzo wa ibada ya Hija, kuanzia pale nyinyi mnapofanya ihramu kwa ajili ya Umra katika miqati, hadi mnapotekeleza wajibu na faradhi ya mwisho kabisa iliyomo katika Hija, dhikri na utajo wa Mwenyezi Mungu unashuhudiwa katika hali zote; hili ni jambo tunalopaswa kulikumbuka. Dhikri na utajo wa kumkumbuka Mwenyezi Mungu Mtukufu unatusafisha, unatutoharisha, unaondoa kutu ndani ya nyoyo zetu, unatuvua mghafala uliotuvaa na unapunguza na kufifiliza mapenzi tuliyonayo juu ya dunia na kupaparikia kwetu mapambo ya kimaada, pesa, cheo, shahawa na matamanio ya kijinsia na yasiyo ya kijinsia na mambo mengine kama haya. Sisi leo hii na wakati wote tunahitajia mambo haya. Ili mwanadamu aweze kufuata njia kwa usahihi na ili asije akaikengeuka njia iliyonyooka anahitaji kukithirisha kila mara ndani ya moyo wake dhikri na utajo wa Mwenyezi Mungu; na kwa ajili ya hili, Hija ni moja ya fursa bora kabisa; ina hali kadhaa za kipekee. Ninakuombeni katika kila amali na faradhi mnazotekeleza, na katika labbayka ambayo ndiyo amali ya kwanza mnayofanya mzingatie kwa makini kwa kuelewa kile mnachokifanya; na kwa kuelewa ni nani mnayezungumza naye. Katika kutufu, katika sa'ai, katika miqati, katika sehemu za visimamo na katika kila amali ya Hija, tujue tunazungumza na nani, tunaamiliana na nani na tunayojitahidi kuyafanya tunayafanya kwa ajili ya nani. Tusikubali ukatuponyoka hata kwa lahadha ndogo utajo huu, dhikri hii na khushuu hii; hili ni moja ya mambo muhimu. Nukta hii izingatiwe na hususan waheshimiwa maulama, viongozi wa msafara na wale wanaojenga mawasiliano na watu. Nukta ya mwisho kabisa ni kwamba inapasa kuhuisha mawasiliano na ndugu zetu Waislamu wa Ulimwengu wa Kiislamu katika mahala hapo muhimu. Mawasiliano si ya baina ya serikali. Mawasiliano kati ya serikali ni mawasiliano yaliyo rasmi, ni mawasiliano ya maneno kwa ajili ya masuala mengine. Mawasiliano baina ya watu wote wa umma wa Kiislamu ni mawasiliano ya nyoyo; na haya yatapatikana kwa kuwepo mawasiliano baina ya watu wenyewe wa mataifa. Katika mikutano na ndugu zetu Waislamu watakaokuja huko kutoka nchi nyengine, kwa wale wanaoweza kuwasiliana na watu kwa lugha wanaweza kutumia ndimi zao kujenga mawasiliano na wao, kudhihirisha upendo kwao, kulahikiana nao na kutilia mkazo juu ya masuala ya pamoja; kwa wale wasioweza kuwasiliana kwa njia ya lugha, wafanye hivyo kwa vitendo vyao: msogee kuwapa nafasi, muwe na huruma na upendo kwao, mvumilie baadhi ya tabu na usumbufu mtakaopata; yawezekana akatokea mtu mmoja akakupiga kibega lakini wewe onyesha tabasamu kwake. Katika matendo jaribuni kujenga mawasiliano haya; na si kwa sababu ya kulinda heshima na izza ya Iran na taifa la Iran - na tab'an hili lenyewe ni suala muhimu sana; ni uzuri ulioje kwa taifa kuweza kuonyesha heshima yake, thamani zake, na kushikamana kwake na desturi na akhlaqi za kiutu na za Kiislamu - bali ni kwa ajili ya kujenga mawasiliano haya ya kinyoyo. Mtu wa rangi yoyote ile, mtu wa lugha yoyote ile na mtu wa madhehebu yoyote ile yeye ni Muislamu; kama ulivyo wewe, yeye pia amekuja huko kwa sababu ya mapenzi ya al Kaaba, kwa sababu ya mapenzi ya Mtume; yeye pia anapita njia hiyohiyo na yeye pia anazungumza na Mwenyezi Mungu Mtukufu. Yabainisheni baina yenu masuala haya yanayokuunganisheni pamoja kwa kadiri mnavyoweza ili waweze kuelewa kwamba kuna mambo haya yanayokuunganisheni pamoja. Wakati Muislamu kutoka pembe ya mbali ya dunia anapohisi kuwa ana ndugu katika nchi nyengine na katika mataifa mengine anapata moyo zaidi, anakuwa na moyo wa kujiamini na anajivua na hali ya udhaifu waliyotwishwa Waislamu na mikono michafu ya Waistikbari. Hali hii inapasa kuimarishwa.
Tunamwomba Mwenyezi Mungu Mtukufu ateremshe baraka zake kwa mahujaji wetu na kwa mahujaji wote wa Ulimwengu wa Kiislamu. Inshallah nyote muwe miongoni mwa watakaonufaika na dua tukufu na mtukufu Baqiyyatullah (roho zetu ni mhanga kwa ajili yake), na inshallah kwa msaada wa roho toharifu za mawalii, roho toharifu za mashahidi na roho toharifu ya Imam wetu muadhamu (Khomeini) sisi sote tuweze kufuata njia itakayotufanya tupate radhi za Mwenyezi Mungu, Mola wa ulimwengu.
Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.
 
< Nyuma   Mbele >

^