Skip to content

Habari

Habari
Hifadhi

Risala na Barua

Matini
Hifadhi

Kumbukumbu na Simulizi

Kabla ya Mapinduzi
Baada ya Mapinduzi

Sauti na Taswira

Picha
Sauti
Video
Hotuba ya Kiongozi Muadhamu Alipokutana na Maulama na Mafudhalaa wa Khorasan Kaskazini Chapa
10/10/2012
Ifuatayo ni matini kamili ya hotuba ya Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aliyoitoa wakati alipokutana na maulamaa, mafudhalaa na matalaba (wanafunzi wa masomo ya dini) wa mkoa wa Khorasani Kaskazini (wa kaskazini mashariki mwa Iran), mkutano ambao ulifanyika katika Msikiti Mkuu wa Imam Khomeini (MA) mjini Bojnourd mnamo tarehe 10/10/2012.
Kwa jina la Allah Mwingi wa rehema Mwenye kurehemu
Hamdu zote zinamstahikia Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wa viumbe pia. Na rehma na amani zimfikie Bwana Mtume Mtukufu Muhammad SAW, Mkweli Mwaminifu na Aali zake wema na watoharifu, wateule, maasumina na waongozaji hususan Baqiyatullah katika ardhi (Imam Mahdi roho zetu ziwe fidia kwake).
Miongoni mwa vikao ambavyo katika safari zetu kwangu mimi huwa ni vizuri na maridhawa, vya kuvutia sana na vya kutua moyoni ni pale ninapopata wasaa na fursa ya kuwa na kikao na maulamaa, mafudhalaa na matalaba (wanafunzi wa masomo ya dini) vijana. Kwa hakika sababu ya hisia hii kwa mtazamo na uoni wangu iko wadhiha (wazi) na sababu hizo sio mbili wala tatu (bali ni nyingi). Endapo mtu atafahamu falsafa ya kuwa mtu wa dini, endapo mtu atakuwa na matalaba (wanafunzi wa masomo ya dini) hawa vijana katika kitovu cha Hawza (Vyuo Vikuu vya Kidini) anaweza kuainisha vyema kwamba, kwa nini mtu mfano wangu (watu kama mimi) wakiwa katika umri wa miaka sabini wanapata nguvu na moyo kutoka kwa vijana matalaba na ambao ndio kwanza wako mwanzo wa njia na wanahisi kuwa na nguvu na nishati.
Kwa bahati nzuri katika kipindi na duru ya baada ya mapinduzi, matalaba wamekuwa ni mjumuiko ambao ni wa wavulana na wasichana. Mabinti wanachuo, watoto wa kiume wanachuo, wanafunzi wa masomo ya dini na matalaba wamekuwa wakijiandaa tayari kabisa kwa ajili ya kuwa na mahudhurio na kutoa mchango wao katika maeneo nyeti katika mstari wa mbele vitani na katika maeneo nyeti ya dini. Huku ndiko kuwa mtu wa dini. Vizuri, usiku wa leo, nitajaribu kwa kadiri ya uwezo wangu kuzungumza na nyinyi na kubainisha baadhi ya mambo; nikiwa na matumaini makubwa kwamba, Inshallah, maneno haya yatakuwa na taathira katika nyoyo zenu safi na zenye nuru na kupatikana yale mabadiliko na harakati ya kukamilisha mambo katika njia ambayo yanahitajika kwa hima na matakwa yenu na irada ya waheshimiwa viongozi wa Hawza (Vyuo Vikuu vya Kidini).
Kwanza napenda kusema kwamba, eneo hili la Bojnourd yaani eneo hili ambalo leo linaitwa Khorasan Kaskazini, kuanzia Faruj mpaka karibu na mpaka wa Golestan na msitu wa Golestan - mashariki, magharibi, kaskazini na kusini kuko wazi - ni eneo ambalo kwa hakika linafukuta vipaji na lenye chemchemi ya vipawa. Kwa hakika hatutaki kutia chumvi, kuhusiana na idadi na wingi wa maulama ambao wana asili ya eneo hili na kisha tulinganishe idadi hiyo na miji ambayo ilikuwa na maulama wengi; lakini tunachotaka kusema ni kuwa, maulama ambao sisi tulikuwa tukiwafahamu ambao wanatoka katika eneo hili, wengi wao walikuwa miongoni mwa maulama stadi, mahiri na wenye vipawa.
Mmoja kati ya maulama hao, ambaye binafsi nimewahi kumtembelea na kushiriki katika darsa zake. Huyu si mwingine bali ni Marhumu Mirza Hassan Bojnourdi. Wakati mwaka 1340 na 1341 Hijria Shamsiya alipokuja kufanya ziara mjini Mash'had na Qum akitokea Najaf, Imam Khomeini MA alimsisitizia kwamba, ni lazima abakie mjini Qum. Yaani shakhsia yake ya kielimu ilikuwa kubwa kwa namna ambayo, Imam Khomeini MA pamoja na shakhsia yake kubwa aliyokuwa nayo katika uwanja wa elimu na utendaji ulioambatana na umaanawi na akhlaqi (maadili) alimwambia alimu huyu ni lazima abakie mjini Qum. Mirza Hassan Bojnourdi akakubali na hivyo akabakia mjini Qum na akatenga wakati maalumu wa kufundisha. Hata hivyo la kusikitisha ni kwamba, siku hiyo hiyo ambayo ilikuwa imepangwa aje kufundisha katika Chuo cha Feidhiyah, alipata mshtuko wa moyo; hivyo akalazimika kutobakia mjini Qum, akarejea Najaf. Tab'ani, mimi nilifanikiwa kuhudhuria darsa zake kadhaa mjini Najaf. Marhum Mirza Hassan Bojnourdi alikuwa akifundisha darsa zake katika msikiti wa Tusi na mafudhalaa kadhaa watajika walikuwa wakihudhuria na kushiriki katika darsa zake.
Kwa hakika alikusanya sifa kemkemu ikiwemo ya kipaji cha hali ya juu, dhuku na uwezo wa kuhifadhi mambo. Kwa hakika huu ni ustadi na umahiri ambao tuliouna umejipamba kwake. Kwa hakika yeye ni mtu ambaye alikuwa na asili ya eneo hili. Rafiki yake na mtu aliyesoma naye pamoja alikuwa Marhumu ni Al-Haj Mirza Ahmad Bojnourdi Murtadhawi. Watu hawa wawili - ambao kidhahiri walikuwa na asili ya Khorashah - mwanzoni mwa masomo yao ya kitalaba - masomo ya dini - walikuja Mash'had wakitokea Bojnourd na kushiriki katika darsa za Marhumu Aghazadeh na Marhumu Al-Haj Hussein Qumi. Katika zama hizo, baba yangu alikuwa miongoni mwa mafudhalaa katika mji wa Mash'had; alikuwa akiwafahamu vyema hawa, alikuwa na maingiliano na mdakhala nao na alikuwa akiwasifu sana. Kisha baadaye wakaondoka na kwenda katika Najaf Al-Ashraf. Baada ya hapo pia, Marhumu baba yangu akaelekea Najaf na akiwa huko alikuwa na mawasiliano na maingiliano nao. Hatimaye baada ya miaka kadhaa Al-Haj Mirza Ahmad akarejea Bojnourd. Akiwa katika mji wa Bojnourd alikuwa alimu na mwanazuoni mwenye nguvu za wananchi na alikuwa na ushawishi mkubwa mno katika kila kona ya eneo hili. Licha ya kuwa katika zama hizo utawala uliokuwa ukitawala hapa nchini haukuwa na muamala mzuri na viongozi wa kidini na kama ikitokea kwamba, kuna alimu ambaye ana ushawishi, basi utawala husika ulikuwa ukifanya kila uwezalo kusambaratisha satwa na ushawishi wa alimu huyo - imma utawala husika ulikuwa ukifanya kila uwezalo ili msomi huyo awe pamoja nao yaani afuate mitazamo na mambo yao au ulikuwa uking'oa mizizi ya ushawishi wake - kuhusiana na Marhumu Mirza Ahmad utawala wa wakati huo haukuweza kufanya jambo hilo. Akiwa hapa alikuwa alimu na msomi na mtu ambaye alikuwa akiheshimika sana; wakati alipokuwa akija mjini Mash'had pia - wakati huo sisi tulikuwa matalaba (wanafunzi wa masomo ya dini) wa Mash'had - maulama wa mji huo walikuwa wakimtukuza na kuonyesha heshima na taadhima kubwa mno kwake; walikuwa wakienda kumtembelea na kiujumla walikuwa wakimheshimu sana.
Kabla ya hawa alikuweko alimu mmoja na maarufu katika mji huu wa Bojnourd ambaye alikuwa akijulikana kwa jina la Sheikh Muhammad Taqi ambaye kwa sasa ni marehemu (Mwenyezi Mungu awe radhi naye). Alikuwa Imam wa Sala mwenye itibari mjini Mash'had katika msikiti wa Goharshad. Aliondokea kuwa maarufu kwa ibada, zuhd (kuipa mgongo dunia) na elimu. Kwa hakika alikuwa amekusanya sifa zote muhimu (anazopaswa kuwa nazo msomi na alimu).
Tab'ani, zama zake na kipindi chake ni cha karne kadhaa nyuma, yaani kabla yetu, aliaga dunia takribani miaka mia moja iliyopita; lakini tangu wakati huo, hadi katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni, nyumba ya Sheikh Muhammad Taqi ilikuwa juu ya barabara ya Mash'had na katika mtaa ambao ukiitwa kwa jina la: Mtaa wa Sheikh - Wanamash'hadi walikuwa wakiutambua vizuri mtaa wa Sheikh na nyumba ya Sheikh - kwani palikuwa ni mahala pa kukusanyika watu.
Majlisi kubwa kabisa za maombolezo ya siku kumi za Ashura (kukumbuka kuuawa shahidi Imam Hussein bin Ali bin Talib AS) zilikuwa zikifanyika katika nyumba hii ya Sheikh; ambapo wananchi walikuwa wakikusanya nadhiri zao nyingi na kupeleka hapo. Mwanawe yaani Marhumu Sheikh Murtadha alikuwa miongoni mwa maulama wa Mash'had, naye alikuja na kuendeleza njia ya baba yake. Baada ya mwanawe Sheikh, akaja Marhumu Sheikh Ridha (mjukuu wa Sheikh Muhammad Taqi); binafsi nilifanikiwa kukutana na kumtembelea Sheikh Ridha. Marhumu Sheikh Mirza Hassan Ali Morvarid alikuwa mkwe wa Sheikh Ridha. Tazameni hawa ni watu ambao asili yao ilikuwa katika eneo hili yaani walitokea katika eneo hili. Hapana shaka kuwa, kwa uwingi si wengi, lakini bila shaka ni wateule, stadi na mahiri mno.
Hivi vipaji na maandalizi tumeyaona katika kipindi cha uanafunzi wetu wa masomo ya dini. Nimewaambia marafiki ya kwamba, sisi tulikuwa tukishiriki darsa ya Kifaya na Makasib ya Marhumu Sheikh Hashim Qazwini, alikuwa talaba ambaye kwa hakika kipaji chake na maandalizi yake yalikuwa makubwa mno kuliko wanafunzi wengine wote ambapo yamkini walikuwa takribani wanafunzi mia mbili waliokuwa wakishiriki katika darsa hiyo na wakati huo idadi hiyo ilikuwa kubwa mno - kwa sasa idadi hiyo si kitu kutokana na kupanuka Hawza ; lakini katika zama hizo idadi hiyo ilikuwa kubwa mno - na yamkini idadi hiyo ilikuwa zaidi ya mia mbili. Alikuwa akiweka ishkali katika darsa ya Kifaya na alikuwa akilamzimisha Sheikh kufanya mjadala. Huyu alikuwa ni mtu ambaye alitokea katika eneo hili - kidhahiri alikuwa mtu wa eneo la Ashkhane - na alikuwa akijulikana kwa jina la Sheikh Kord; bwana huyu alikuwa miongoni mwa Wakurdi wa eneo hili.
Inasikitisha kwamba, katika zama zile si tu kwamba, vipaji hivi, havikuwa vikitambuliwa na hata vilipotambuliwa havikuwa vikitumiwa. Hakuna mtu aliyekuwa akiuliza mathalani mtu fulani aliyekuwa na kipaji fulani amekwenda wapi, nini kimempata, amesoma mpaka wapi na ameweza kwa kiwango gani kuwa chanzo na chimbuko katika maendeleo na ustawi wa elimu. Katika zma hizo hali ilikuwa namna hii; kwa hakika hii leo haipaswi kuwa namna hii, na bila shaka hali haiko hivi.
Miongoni mwa hawa mashahidi walikuweko watu wa dini, nilikuwa nikifahamiana vyema na wawili kati yao. Tab'ani, walikuwa matalaba vijana waliokwenda vitani, wakapigana jihadi na kuuawa shahidi. Nimeyaona majina yao lakini sikupata tawfiki ya kufahamiana nao kwa karibu; lakini nilikuwa nikifahamiana kwa karibu na wawili kati yao: Marhumu Sheikh Qassim Sadiqi Garmeh - aliyekuwa mtu wa Garmeh - na Marhumu Tayyibi.
Marhumu Sheikh Qassim Sadiqi nilikuwa nikifanya naye majadiliano ya kimasomo kwa miaka kadhaa; nilikuwa nikifanya naye majadiliano ya masomo katika masomo ya Sherhe ya Lum'a na Makasib. Kwa hakika alikuwa na ishara za kipaji. Laiti yeye angeendelea na masomo kama alivyokuwa akisoma, bila shaka angeondokea kuwa alimu mkubwa na stadi kabisa; lakini katika zama hizo haikuwa ada kumuuliza talaba: wewe ni nani na unataka kuwa nani?
Baadaye unataka kufanya nini? Hata ipatikane fursa ya kumuongoza, kumsaidia gharama za masomo na kumuandaliwa suhula za masomo; katika zama hizo mambo haya hayakuweko. Hivyo naye akaenda na kujishughulisha na kazi nyingine. Tab'ani, katika mapinduzi yeye na Marhumu Tayyibi walikuja na wakawa wawakilishi wa Bunge na wakawa miongoni wa watu 72 waliouawa shahidi katika mlipuko wa bomu katika ofisi ta Chama cha Jamhuri ya Kiislamu.
Hivyo eneo hili ni kitovu cha vipawa. Kuanzia Bojnourd hadi katika maeneo yanayolizunguka eneo hili - Esfarayen, Shirvan, Faruj - kisha upande huu ambao kuna miji mingine hapa; iwe ni lile eneo ambalo wanapatikana ndugu zetu Masuni, au iwe ni ule upande ambao kuna Mashia. Ndugu zetu Masuni nao wana haki. Hawa hawa Masheikh wa Kiturkimani wa Kisuni - nilisema asubuhi kwamba - walikuwa na nafasi muhimu katika kuzima fitina ambapo Wakomonisti walitaka kuzusha fitina kubwa hapa. Mimi nilikuwa nikiwafahamu kwa karibu maulama ambao walikuwa watu wa shauku na msukumo, watu wa fikra na watu wa kuchukua hatua; watu hawa walikuwa na nafasi muhimu sana. Kwa hakika hapa ni mahala ambapo uwanja unaweza kuandaliwa na hivyo kuwa ni Hawza kamili ambayo ina masomo ya juu kabisa, tena yenye kiwango kizuri kabisa. Walimu wanapaswa kuja hapa. Kwa hakika sio mantiki hata kidogo kwamba, talaba lazima ahajiri katika kipindi cha masomo yake ya awali na kwenda katika Hawza (Chuo Kikuu cha Kidini) kubwa kisha asirejee tena hapa; kwa hakika hili ni jambo ambalo halifai.
Katika eneo hili hili la miji ya kando kando na Khorasan Kubwa, kulikuweko na maulama wakubwa. Mimi nimekwenda katika miji mingi, kulikuweko na Mamujitahidi wa daraja la kwanza ambao walikuwa wakiishi katika miji hiyo. Huko Birijand kulikuwa na mujitahidi wawili ambao kama wangekuwa huko Najaf kwa asilimia kubwa wangekuwa miongoni mwa Mamarjaa Taqlidi: Marhumu Tahaami na Marhumu Sheikh Muhammad Hussein Ayati. Hawa walibakia katika mji wa Birijand wakawa ni mali ya watu wa Birijand. Huko Kuchan, mtu kama Marhumu Agha Najafi Ghoochani anakuja na kuishi huko, Bwana huyu ni mmoja wa wanafunzi mahiri wa Marhumu Akhond Khorasani. Katika mji wa Birijand - kama nilivyosema - alikuweko Mirza Ahmad Murtadhawi na katika miji mingine hali ilikuwa hivi hivi; kulikuweko na maulama wakubwa na stadi.
Baadhi wanasema, Bwana we, wakati huo mawasiliano baina ya miji mikubwa na miji midogo halikuwa jambo jepesi; ndio maana maulama walikuwa wakilazimika kubakia hapo. Hoja hii inatoa natija ambayo ni kinyume. Hii leo mawasiliano ni mepesi, mtu unaweza kuchukua Kompyuta, unaweza kukaa mbele ya Kompyuta na kuweza kusoma masomo bora kabisa ya Hawza kupitia chombo hiki. Hivyo basi kama ni hivyo, leo hakuna haja ya kwenda katika Hawza kubwa, hapana. Hii leo kama wewe utakuwa na mushkili na shubha ya kielimu, unapanda gari na baada ya masaa mawili matatu hivi unakuwa umeshafika Mash'had, hivyo unakwenda kwa alimu mmoja wa dini na anakutatulia tatizo na kukupa jibu la shubha na swali lako na kisha unarejea. Hii leo kutokana na kupatikana suhula nyingi, Hawza za mikoani zinapaswa kuwa na ustawi; zinapaswa kuboreka kwa upande wa viwango.
Huu mpango wa kuhajiri ambao mimi niliuzungumzia miaka kadhaa iliyopita unapelekea kupanuka na kuwa amilifu harakati ya wana dini katika kila kona ya nchi. Ni lazima kuhajiri katika Hawza kubwa na kuja huku mikoani; iwe ni watu wa hapa au si wa kutoka hapa. Kuna watu ambao wakati mwingine hata sio wa hapa. Marhumu Muhaqiq Sabzwari - mtunzi wa kitabu cha Dhakhirah na Kifaya pamoja na Mullah Maarufu na Sheikh Al-Islam mkubwa wa Isfahani katika kipindi cha Safavieh - waliondoka Isfahan na kwenda Mash'had na kuamua kuishi huko. Katika zama hizo mji wa Isfahan ulikuwa mji mkubwa kabisa nchini Iran na Mash'had ulikuwa mji mdogo sana kama kijiji kikubwa vile. Madrasa ya Baqiriyah mjini Mash'had - ambapo wanafunzi wa zamani wa Mash'had walisoma hapo na leo imebomolewa - ni Madrasa ambayo aliikarabati na kuitengeneza tena.
Walikuwa wakija na kubakia licha ya kuwa haukuwa mji wao wa asili. Marhumu Mirza Mahdi Shahid mwenye asili ya Isfahan ambaye ni mmoja wanafunzi wanne mahiri wa Marhumu Wahid Bahbahani - ambapo alikuwa na wanafunzi wanne waliokuwa wakiitwa Mahdi ambapo watu walikuwa wakiwaitwa Mahdi Wanne - anakuja Mash'had na kubakia mjini humo na kisha anakuja kuuawa shahidi hapo hapo katika mji wa Mash'had. Katika kipindi chote hiki kumepita maulama wengi. Kuna tatizo gani hata kama watakuwa si watu wenye asili ya hapa, lakini waje hapa? Seuze wakiwa ni wa asili ya hapa, bila shaka kama asili yao ni hapa wanapaswa kuja hapa.
Mafudhalaa wa Kibojnourdi walioko Mash'had na Qum wakae na kuwachagua watu kumi baina yao na kisha wawatume hapa, Hawza nayo ina jukumu la kuandaa suhula; waja hapa ni kufundisha. Kwa sasa tunasema kwamba, waje na kufundisha mpaka Sat'hi ya Kumi (daraja ya kumi), waje na kufundisha zaidi ya hapo na hata wafundishe Masomo ya Khariji (masomo ya juu kabisa). Ndio, mwanafunzi ambaye amesoma hapa mpaka kiwango cha Masomo ya Khariji (masomo ya juu kabisa) na kukaribia ijtihadi (kuwa mujitahidi), hakuna mushkili wowote akaondoka na kwenda katika Hawza nyingine kubwa - kwa mfano Hawza ya Qum au Mash'had - na kubakia huko mia miwili, mitatu au mitano kisha akarejea hapa na kuendelea na harakati za ufundishaji. Endapo Sheikh atakuwa na elimu na upana wa fikra katika zama hizi - ambazo ni zama za fikra, utamaduni na kuenea fikra mpya katika ulimwengu wa Kiislamu - namna hii katika mji fulani, mnajua nini kitatokea?
Hii leo mji huu au mkoa huu una wanachuo wapatao elfu arobaini. Kati ya hawa wanachuo elfu arobaini ni wangapi kati yao ambao wana mahusiano na mawasiliano na nyinyi matalaba (wanafunzi wa masomo ya dini). Ni wangapi kati yao ambao mnakaa nao na kuzungumza nao? Watu kadhaa miongoni mwenu yamkini mkaalikwa na kuitwa katika mikusanyiko yao na kisha mkaenda kutoa hotuba katika mkusanyiko wao wa watu khamsini au mia moja hivi. Hili sio jambo la kimsingi. La msingi ni kuwa, mnapaswa kuuelewa upande wa pili; hili ni jambo ambalo linahitajia muda, kazi na ambalo linahitajia elimu ya kutosha, linahitajia fikra na utamaduni na linahitajia mapenzi; kazi hii inapaswa kufanyika.
Vizuri, Alhamdulilahi mko wengi - madada na vile vile makaka - na hili ji jambo ambalo mtu analishuhudia wazi. Ni lazima msome vizuri, muwe wasomi, masheikh, wenye nguvu na muwe na uwezo wa kupambanua na kuchanganua fikra na mambo mbalimbali.
Muwe na mutwalaa (kujisomea) wa pembeni pia mbali na masomo yenu ya kawaida. Baadhi ya masomo haya ambayo yamezoeleka katika Hawza (Vyuo Viku vya Kidini) Qum au Tehran yanaweza kutumika kama mutwalaa (kujisomea) wa pembeni; kama vile Fasihi ya Kifarsi, Akhlaqi (maadili) na masomo mengine - Tab'ani, Fasihi ya Kiarabu ni lazima; hizo ni miongoni mwa suhula zetu za kazi - hakuna ulazima masomo haya yaingizwe katika mitalaa ya masomo. Tab'ani, mimi siingilii, naelezea dhuku tu; waandaaj wa ratiba wanapaswa kukaa na kufikria njia ya hili.
Talaba hapaswi kuachana na kitabu; asome kitabu, asome kwa kila namna, asome akiwa katika rika la ujana. Akiba hii ya uwezo wa kuhifahi ambao ina nafasi isiyo na kikomo, mnapaswa kuijaza katika rika la ujana kadiri mnavyoweza. Sisi kila ambacho tulikihifadhi katika kipindi cha ujana, hii leo kipo; na kila ambacho tunakipata na kukihifadhi katika zama za uzee - ambapo binafsi hata sasa hivi pamoja na mazonge yote niliyonayo ninafanya mutwalaa kuliko vijana - hakidumu na kubakia kama ilivyokuwa katika zama za ujana. Katika hali ya sasa nyinyi ni vijana. Kijazeni chanzo hiki chenye thamani, kifanyeni kadiri mnavyoweza kijae taarifa zenye thamani, ufahamu na welewe wenye sudi na wa lazima ambao mnauhitajia katika uwanja wa tablighi kwani mtakuja kustafidi na haya. Kile ambacho ni lazima kukieleza - na ambacho ni muhimu kuliko haya yote - ni uhusiano wa Hawza na mapinduzi au Mfumo wa Kiislamu.
Kwa hakika hakuna mtu katika ulimwegu wa watu wa dini kama atakuwa na insafu na hekima ambaye anaweza kujitenga au kujiweka mbali na Mfumo wa Kiislamu. Mfumo wa Kiislamu umewawekea suhula kubwa wanaolingania katika njia ya Mwenyezi Mungu na Mubalighina wa Uislamu. Lini mlikuwa na kitu kama hki? Hii leo talaba fudhalaa anakaa katika televisheni na kuzungumza (mathalani) kwa muda wa nusu saa huku kukiweko na watu milioni kumi au milioni ishirini ambao wanasikiliza maneno yake kwa hamu na shauku kubwa. Lini kitu kama hiki kilikuwako kwa ajili yangu na nyinyi katika kipindi chote cha historia ya watu wa dini kuanzia mwanzoni mwa Uislamu mpaka leo hii?
Mikusanyiko hii mikubwa lini ilikuweko? Sala hizi za jamaa lini zilikuweko? Vijana wote hawa wenye shauku pamoja na kiu na maarifa lini walikuweko? Hii leo hawa vijana wanachuo na wasio wanachuo ambao mnawashuhudia - ambapo kwa sasa mimi ninawazungumzia wanachuo - wote takribani na akthari yao ni wenye shauku na uchu na maarifa, mafahimu na maarifa ya Kiislamu na wanataka kujua kitu kuhusiana na maarifa ya Kiislamu. Mimi na nyinyi tuandae uwanja ili tuweze kutoa majibu ya haya.
Fursa hii imewahi kuweko huko nyuma? Fauka ya hayo, suhula kama vile Kompyuta, mawasiliano ya intaneti na Mawasiliano ya Kompyuta (Cyberspace) haya yote mnayo leo, mambo ambayo huku nyuma hayakuweko. Kama mtaweza kujifunza haya, mnaweza kuwafikishia maneno yenu mazuri maelfu ya watu msiowajua; hii ni fursa isiyo ya kawaida; tuwe makini na tuhakikishe kwamba, tunatumia vyema fursa hii na hivyo kutoruhusu ipotee. Endapo fursa hii itapotea bure, Mwenyezi Mungu Mtukufu ataniuliza mimi na nyinyi Siku ya Kiyama: ya kwamba, mlitumia vipi fursa yote hii ya ujana, fursa yote hii ya udadisi, kutaka kujua mambo, huu msukumo wote na shauku ya kutaka kujua mambo kwa ajili ya kueneza maarifa ya Kiislamu? Mfumo wa Kiislamu umetoa huduma namna hii kwa masheikh, watu wa dini na vilemba.
Kwani inawezekana sisi kujiweka kando? Hii kwamba, atokee Sheikh fulani akunje mavazi yake ya kidini na kujiweka kando kisha aseme kwamba, mimi sina kazi na mambo ya nchi, au aseme mimi sina kazi na mfumo unaotawala hapa nchini; hii sio fakhari; bali ni aibu kubwa. Kiongozi wa dini anapaswa kupokea kwa mikono miwili na kwa ujudi waje wote uwepo wa mfumo kama huu ambao tui lake ni Uislamu na sheria zake ni Fikihi ya Kiislamu. Marajii Taqlidi wa sasa, wamenieleza mara kadhaa kwamba, wao wanatambua kuwa ni haramu hatua yoyote ile ya kudhoofisha mfumo huu. Wengi wao wamekuwa wakinitumia jumbe wakinieleza kwa mapenzi maalumu kwamba, wananiombea dua daima. Hii ni ishara ya kutambua thamani ya Mfumo wa Kiislamu.
Sasa hii kwamba, atokee Sheikh fulani na kujiweka kando na mfumo unaotawala hapa nchini; kisingizio cha hilo kiwe kwamba, "sisi tuna ukosojia fulani". Vizuri sana, kuwa na ukosoaji mia moja; kuwa na ukosojia mia mbili kutuhusu sisi masheikh. Kwani sisi hatukosolewi? Kuweko ukosoaji na mapungufu katika majimui fulani kwani kunapelekea mtu asahau na kutoona mazuri yote yaliyoko katika majimui hiyo? Bila shaka mapungufu yapo. Mimi ni Sheikh na ni talaba, nimekuwa talaba (mwanafunzi wa masomo ya dini) tangu sijabaleghe hadi sasa; njooni tukuandikieni orodha ya mapungufu yetu. Kuna ishkali na mapungufu mia moja (mengi) tuliyonayo; lakini mapungufu haya mia moja (yaani mengi) haina maana kwamba, hatuna mazuri. Mkabala na matatizo na mapungufu haya mia moja, kuna mazuri elfu moja. Katika ukamilifu na upungufu na uzuri na ubaya, ndipo mwanadamu huweza kupata njia sahihi na iliyonyooka.
Hawza (Vyuo Vikuu vya Kidini) inapaswa kujitambua kuwa, ni mwanajeshi na askari wa vitani; ifanye kazi kwa ajili ya mfumo (unaotawala hapa nchini), awe na uchungu na mfumo na afanye harakati katika kalibu ya kuupatia nguvu na kuuimarisha mfumo unaotawala hapa nchini; na hili ni jambo ambalo liko kinyume kabisa na kile kinachotakiwa na kufuatiliwa na mashirika ya kiusalama ya Uingereza, Marekani, utawala wa Kizayuni wa Israel na madola mengine. Licha ya kuwa siasa za mashirika ya usalama ya maadui wa Jamhuri ya Kiislamu iwe ni Marekani au Uingereza au utawala wa Kizayuni wa Israel ni kupandikiza fikra kwamba, kuna hitilafu baina ya watu wa dini na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, lakini ukweli wa mambo ni kuwa hakuna mtu yeyote wa dini anayeweza kujivua na mfumo huu wa Kiislamu.
Ndio maana inapotokea kwamba, kuna mtu wa dini katika kona fulani ya nchi amezungumza kitu ambacho kidhahiri kinaonekana kuwa kiko kinyume na matakwa, ufahamu na itikadi jumla ya mfumo, hulikuza jambo hilo, ikiwa mtu aliyezungumza ni mdogo, basi maadui hawa hufanya kila wawezalo kumkuza mhusika huyo ili kuzusha hitilafu baina ya mfumo na watu wa dini; waonyeshe taswira kwamba, kuna hitilafu kama hii. Kwa msingi huo Hawza hizi (Vyuo Vikuu vya Kidini) haziwezi kuwa ni za kisekula. Hii kusema kwamba, hatujihusishi na masuala ya kazi za mfumo na masuala yanyohusiana na utawala, kufanya hivyo ni kuwa na mitazamo ya kisekula. Maana ya maneno yangu sio kwamba, kuanzia siku ya kwanza sote tuje na kufanya kazi katika mfumo unaotawala hapa nchini; hapana, bali tunapaswa kusoma vizuri.
Katika kipindi cha mapambano mimi nilijihusisha na harakati za mapambano (ya mapinduzi ya Kiislamu). Wakati huo nilikuwa nikifundisha somo la Kifaya na Makasib mjini Mash'had. Kuna wanafunzi wangu wengi ambao walikuwa wakishiriki katika harakati za mapinduzi. Walikuwa wakijishughulisha na harakati za mapinduzi, kiasi kwamba, walikuwa wakifikia hatua ya kujiuliza haya mambo yaliyoko kwenye somo la Kifaya na Makasib yana faida gani. Nilikuwa nikiwaambia mara kadhaa kwamba, haiwezekani kufanya kitu bila ya kuwa na kitu, endapo mtakuwa na kitu wakati huo mtaweza kufanya harakati na kuwa na nafasi kama aliyokuwa nayo Imam Khomeini MA. Mfumo unaotawala hapa nchini una mawasiliano na mafungano na watu wa dini. Tambueni kwamba, kama wasingewa watu wa dini, basi mfumo huu (mfumo wa Kiislamu) usingeliundwa, kama watu wa dini wasingelikuwepo, basi Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran kamwe yasingeliweza kupata ushindi, kwani wasomi, makundi na vyama visivyo vya Kiislamu havikuwa vinakubalika na wala havikuwa na ushawishi mkubwa kama waliokuwa nao watu wa dini nchini.
Kwa hakika mimi ninalisema hili nikiwa na hoja, ya kwamba, kama jamii ya watu wa dini isingelikuweko, basi mapinduzi haya yasingepata ushindi; hata miaka mingine mia moja yasingepata ushindi. Baadhi ya wanafikra wetu ambao baadhi yao walikuwa watu wazuri tena walikuwa watu wenye uchungu - wote hawakuwa watu wabaya na wapotofu) hawakuwa na uwezo na hawakuwa wakikubalika, hawakuwa na ushawishi baina ya watu na hawakuwa wakiweza kuzitawala na kuziteka nyoyo za watu. Mtu ambaye alikuwa wa kwanza kufanya jambo hilo, kiheshima kuwa na taathira katika kila kona ya nchi na pili kwa upande wa taathira ya ndani na kubwa hadi katika nyoyo alikuwa mtu wa dini; ambaye alikuweko kila mahala. Mimi kuna wakati mwanzoni mwa mapinduzi nilisoma aya hii tukufu iliyoko katika Sura ya An-Nahal isemayo:
"Na Mola wako Mlezi amemfunulia nyuki: Jitengenezee majumba yako katika milima,na katika miti, na katika wanayo jenga watu. Kisha kula katika kila matunda, na upite katika njia za Mola wako Mlezi zilizo fanywa nyepesi kuzipita. Na kutoka matumbo yao kinatoka kinywaji chenye rangi mbali mbali; ndani yake kina matibabu kwa wanaadamu." An-Nahl 16:68-69. Nilisema ndio, hawa vijana matalaba wako kama nyuki (wa asali) wamekwenda juu ya maua ya maarifa, wakakaa na kunyonya maji ya maua hayo kisha baadaye wakaenda katika maeneo mbalimbali ya nchi na kuwapa wananchi asali, wakawadunga maadui; asali na vile vile kudunga. Hakuna chama, mkusanyiko na tabaka ambalo linaweza kufanya kazi hii ghairi ya watu wa dini. Na kama hili lisingewezekana, mapinduzi haya ya kijamii yasingeweza kutokea; mapinduzi ambayo nara na kauli mbiu zile zile zilizokuwa zikipigwa mjini Tehran siku ya Ashura, ndizo hizo hizo zilizokuwa zikitolewa na wananchi wa eneo fulani la mbali nchini katika maandamano, walikuwa wakisema maneno yale yale na kukariri matakwa yale yale.
Namna hii ndivyo yanavyokuwa mapinduzi ya kijamii; ambapo natija na matunda yake ni kuanguka utawala kama ule (utawala wa Shah), na kuundwa mfumo kama huu (Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu). Uimara, umadhubuti na mizizi mikubwa na yenye kina ya mfumo huu (mfumo wa Kiislamu unaotawala hapa nchini) iko kwa namna ambayo kwa tawfiki ya Mwenyezi Mungu, mfumo huu utabakia na kuendelea kuweko kwa karne kadhaa. Inshallah.
Misingi ya kifikra nayo ilikuja kuwekwa na watu wa dini. Watu mfano wa Shahidi Mutahhari, Allamah Tabataba'i na shakhsia wakubwa mfano wao, ndio waliokuja na kuweka misingi imara na madhubuti ya kifikra; miundo mbinu na misingi hii ya kifikra inawezekana kwa misingi hiyo kuandaa vikao vya kifikra, kueneza na kugawa na hivyo kutoa majibu kwa mahitaji ya kifikra ya vijana hii leo. Katika nchi yetu, maneno madhubuti ambayo yalifanikiwa kusambaratisha fikra na mitazamo ya Kimaxi na kuzipeperusha kama upepo ni maneno ya Marhumu Shahidi Mutahhari - yeye alikuwa mwanafunzi wa Bwana Tabataba'i - na baadhi ya wanafunzi wa Marhumu Allamah Tabataba'i.
Mfumo huu umekuja katika mazingira kama haya. Kwa muktadha huo jukumu ni kubwa na kazi za kufanya ni nyingi. Majukumu yenu ni mengi sana. Mnapaswa kujijenga kimaanawi; vile vile mnapaswa kujijenga kiakhlaqi (kimaadili), kimalezi, kitabia kushikamana na dini na vile vile katika kushikamana na kufungamana na faradhi na Sunna pamoja na kusoma Qur'ani Tukufu. Talaba (mwanafunzi wa masomo ya dini) huyu aliyesoma Qur'ani hasa, amesoma vizuri sana Qur'ani na hata aya alizozichagua nazo zilikuwa nzuri sana. Miongoni mwa aya hizo ni ile isemayo:
Hakika nyinyi mnayo ruwaza njema kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu kwa anaye mtaraji Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho, na akamkumbuka Mwenyezi Mungu sana. (Al Ah'zab 33:21). Hivyo kama sisi ni wenye kumtaraji Mwenyezi Mungu na tunaamini Siku ya Kiyama, basi kigezo na ruwaza njema kwetu ni Bwana Mtume SAW. Si kwamba, tufanye kama yeye hapana - bila shaka hili haliwezekani na ni muhali - lakini tunalopaswa kufanya ni kuendeleza njia yake. Katika aya inayofuata Mwenyezi Mungu anamuwekea wazi Bwana Mtume SAW kuhusiana na hali ya waumini pale anaposema:
Na Waumini walipo yaona makundi, walisema: Haya ndiyo aliyo tuahidi Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Na Mwenyezi Mungu na Mtume wake wamesema kweli. Na hayo hayakuwazidisha ila Imani na ut'iifu. (A-Ahzab 33:22). Katika vita vya Ahzab, maadui walikuwa wakifanya mashambulio kutoka kila upande. Katika Vita vya Badr kulikuwa na kundi moja na katika Vita vya Uhud kulikuweko na kundi na katika vita vingine kulikuweko na makabila madogo; lakini katika Vita vya Ah'zab makabila yote ya Makka kwa pamoja na yasiyo ya Makka kama ya Thaqifa na mengineyo yote yaliungana na kuwa kitu kimoja; wakaandaa jeshi la wapiganaji elfu kumi; Mayahudi ambao walikuwa majirani wa Bwana Mtume SAW na ambao kimsingi walikuwa wamepata amani (wamesalimika na kila maudhi na mashambulio) ya Bwana Mtume SAW na Waislamu, walifanya khiyana na usaliti; hawa nao walisimama na kushirikiana na makabila hayo katika vita dhidi ya Bwana Mtume SAW na wafuasi wake.
Kama leo tunataka kufanya ulinganishaji tunaona kuwa, Marekani ndio inayopingana Uingereza inayopingana na utawala wa Kizayuni wa Israel ndio inayopinga na zinazoongoza upinzani. Maadui hao walitumia fedha zao, wakakusanya vikosi vyao na kuanzisha vita vya Ah'zab; vita vya Ah'zab ambavyo vilizitisha nyoyo za wengi. Mwanzoni mwa Suran hii Mwenyezi Mungu anasema:
Na kundi moja katika miongoni mwao liliposema: Enyi watu wa Yathrib! Hapana kukaa nyinyi! Rudini. (Al'Ahzab 33:13). Hivyo walikuwa wakiwatisha watu. Hii leo pia hali iko namna hii. Hii leo pia kuna baadhi ya watu ambao wanawatisha wananchi: Bwana ee ogopeni. Unadhani kukabiliana na Marekani ni mzaha? Ohoo. Mtapata kipigo! Kuanzia vile vita vyao vya kijeshi, hivi vikwazo vyao, na hizi harakari zao za kipropaganda na kisiasa. Mwishoni mwishoni mwa sura hii mwenyezi Mungu anasema:
Kama wanafiki na wale wenye maradhi nyoyoni mwao, na waenezao fitna katika Madina hawatoacha, basi kwa yakini tutakusalitisha juu yao, kisha hawatakaa humo karibu yako ila muda mchache tu. ( Al Ah'zab 33:60). Waenezao fitna ndio hawa. Katika mazingira kama haya, ufafanuzi wa hali ya waumini ni huu: "Haya ndio aliyotuahidi Mwenyezi Mungu na Mtume Wake"; sisi hatushangai; Mwenyezi Mungu na Mtume Wake wametwambia kwamba, kama mtakuja na kushikamana na Tawhdi, mkashikamana na imani juu ya Mwenyezi Mungu basi tambueni kwamba, mna adui, na maadui watakufuateni. Ndio walisema (Mwenyezi Mungu na Mtume SAW) na sasa ukweli huo umedhihirika na kuonekana wazi; kweli tumeona maadui wamekuja na kujitokeza; Mwenyezi Mungu anasema: Na Waumini walipoyaona makundi, walisema: Haya ndiyo aliyotuahidi Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Na Mwenyezi Mungu na Mtume wake wamesema kweli. Na hayo hayakuwazidisha ila Imani na ut'iifu (Al-Ah'zab 33:22). Hivyo imani yao huongezeka.
Mnafiki ni dhaifu wa imani ni katika wale ambao nyoyoni mwao kuna maradhi - watu wa aina tofauti tofauti - wakati wanapomuona adui miili yao hutetemeka; na huanza kuwaandama na kuwashinikiza wanaomuamini Mwenyezi Mungu na wanaofanya hima na idili kubwa katika njia ya Mwenyezi na kuwaambia; Bwana wee, kwa nini mnafanya hivi? Kwa nini hamlegezi kamba? Kwa nini hambadilishi siasa zenu na kuzifanya hivi na hivi? Hivyo watu hawa wanafanya mambo yale yale ambayo yanatakiwa na adui. Lakini katika upande ule wa pili, waumini wakweli wanasema: kwa hakika sisi hatuyashangai haya; bila shaka wanapaswa kufanya uadui; Haya ndiyo aliyotuahidi Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Na Mwenyezi Mungu na Mtume wake wamesema kweli. Na hayo hayakuwazidisha ila Imani na ut'iifu. (Al-Ah'zab 33:22).
Mwenyezi Mungu anasema: Mayahudi haawawi radhi nawe, wala Wakristo, mpaka ufuate mila yao". (Al-Baqarah 2:120). Hivyo basi hawa maadui hawatatuacha sisi mpake tufuate yale wanayaotaka wao. Hivyo basi jiimarisheni ili msiathiriwe na maadui; msiwe madhaifu kiasi kwamba, kitu kidogo tu cha maadui kikakuathirini na kukutikiseni. Kwa nini mnajidhoofisha mbele ya adui, hata mjisalimishe mbele yake? Mnapaswa kuwa kama alivyosema Mwenyezi Mungu; Na hayo hayakuwazidisha ila Imani na ut'iifu (Al-Ah'zab 33:22).
Kuweni namna hii ndugu zanguni, watoto wangu, wapendwa wangu, vijana matalaba (wanafunzi wa masomo ya dini)! Someni masomo yenu kwa nia safi na ya kweli, kwa nia ya kwamba, mtakuwa katika safu za mbele kabisa katika medani hii, kuweni miongoni mwa watu ambao ni stadi na wako mstari wa mbele. Kwa hakika mimi ninaviagiza vituo vya kiutamaduni msisahau sanaa ya msikiti, tab'ani kwa kushirikiana na Basiji.
Ni jambo baya sana kujitokeza hitilafu baina ya Sheikh (Imam) wa msikiti na Basiji wa msikiti. Shirikianeni na basiji na ifanyeni utamaduni wa misikiti uwe na taathira, fanyieni kazi ustaarabu huu. Kaeni chini na mtafakari, fanyeni mutwalaa na andaeni mambo na maneno ambayo yanakwenda sambamba na mahitaji ya kijana yule ambaye anahudhuria hapo (yaani kijana ambaaye anakuja msikiti). Fanyeni mutwalaa kadiri mnavyoweza. Kuna vitabu ambavyo inawezekana kuvitumia na kustafidi navyo katika uwanja huu. Kimsingi vitabu vipo, nendeni mkaulize, fanyeni uhakiki na muwaulize watu ambao wana ujuzi na weledi katika uwanja huu. Jizatitini na mjiimarishe kwa silaha ya maarifa na ujengeaji hoja mambo na kisha nendeni katika vituo hivyo vya kiutamaduni na mkae kwa ajili ya kuwapokea vijana wanaokuja hapo wakiwa na maswali tofauti tofauti.
Wapokeeni vijana hao kwa hisani na wema mkubwa na muamiliaene nao vizuri. Yamkini dhahiri yao ikawa sio nzuri, hakuna taabu na wawe hivyo. Baadhi ya hawa walikuweko katika mapokezi ya leo na nyinyi mlikuweko - Janabi Bwana Mehman - Nawaz na mabwana wengine - mumewasifia hapa, kulikuweko na akina dada ambao kwa mujibu wa ada ya kawaida wanaitwa kuwa hijabu yao sio kamili; machozi ya mapenzi yalikuwa yakititirika pia kutoka katika nyuso hizi. Sasa tufanye nini? Tuwafukuze? Je ni maslahi kufanya hivyo? Na je ni haki kufanya hivyo? Hapana, nyoyo zao zinafungamana na kambi hii; nyoyo zao zipo pamoja na malengo haya makuu (malengo makuu na matukufu ya Mapinduzi ya Kiislamu). Yeye (mtu wa aina hiyo kwa mfano binti ambaye hijabu yake sio kamili) ana mapungufu. Kwani mimi sina mapungufu? Mapungufu yake ni ya kidhahiri, mapungufu yangu mimi mja dhaifu ni ya kibatini; watu hawayaoni.
Hivyo basi sisi tuna mapungufu na yeye ana mapungufu. Fanyeni mambo kwa uoni na kwa mtazamo huu. Tab'ani, mtu anapaswa kukataza mabaya; kukataza mabaya kwa lugha nzuri na sio kwa njia ya kuleta chuki. Kwa msingi huo mnapaswa kuwa na mahusiano na maingiliano na tabaka la wanachuo. Kwa hakika Bwana Farjam amekumbusha jambo zuri hapa kuhusiana na vazi la masheikh na watu wa dini. Wale ambao wamepiga hatua kwa kiwango fulani katika masomo yao (masomo ya kidini) basi na wavae vazi hili (joho la kilemba); lakini wanapaswa kufahamu kwamba, kuvaa vazi hili humfanya mtu kuwa na maasuuliya (majukumu) mazito. Kilemba hiki mnachokivaa kichwani mwenu ni kizito mno (kina majukumu na masuuliya mazito). Watu wakikuona tu uvemaa kilemba, basi huanza kuuliza mlolongo wa maswali yao na kutaka ufafanuzi kuhusiana na shubha (ishkali) na utata tofauti walionao katika mambo mbalimbali. Kama utaulizwa kitu na ukawa hukijuia na ukasema wazi kwamba, sifahamu, kisha ukaenda na kufanya utafiti na uhakiki na kisha ukaja na kutoa jibu la swali hilo, hapana shaka kuwa, jambo hilo litakuwa zuri na la kuvutia mno; lakini ikiwa jambo uliloulizwa ukawa hulijui na ukajibu kimakosa, au kwa kuwa hufahamu jibu la swali hilo hivyo ukaghadhibika kwamba, kwa nini amekuuliza swali kama hilo (ambalo kimsingi hujui jibu lake), kwa hakika hili litakuwa jambo baya. Kama itakuwa kwamba, mtu awe namna hii basi, basi kutokuweko kwake ni bora.
Mpeni heshima imamu anayesalisha na mpeni umuhimu. Watu wanaostahiki ndio ambao wanapaswa kuwa Maimamu wa kusalisha, kwa hakika kuwa imamu ni jambo muhimu sana. Zungumzeni na watu katika kila baada ya Sala au kwa uchache katika kila siku. Jitahidini kuzungumza na watu japo mara moja kwa siku na chambueni na kutolea ufafanuzi wa fikra na mambo mbalimbali (ya kidini na kisiasa). Zing'arisheni nyoyo (za waumini) kwa kueleza uhakika wa dini na sifa za Ahlul Bayt (Alayhims Salaam); kwani kwa kufanya hivyo nyoyo zitapata nuru.
Vizuri, naona mazungumzo yetu yamekuwa marefu sana. Tunamuomba Mwenyezi Mungu Mtukufu alilinde na kulihifadhi eneo hili kwa baraka za uwepo wa Janabi Bwana Mehman-Nawaz. Katika mikutano ambayo wakati mwingine tumekuwa nayo na yeye, kwa hakika daima alikuwa akizungumzia suala la kuja hapa Bojnourd na sisi tulikuwa tukimjibu kwa kusema, hamna taabu Inshallah tutaitikia na kutii wito huo kwani mambo yamewekwa rehani kwa wakati wake (yaani kila jambo linafungamana na wakati na wakati wake unapowadia jambo hilo hufanyika). Vizuri, sasa wakati wake umewadia. Yeye (Bwana Mehman-Nawaz) amebakia hapa Bojnourd, kwa hakika mefanya jambo zuri sana; kwa hakika yeye ni baraka kwa ajili ya mji huu. Ana majukumu na ni Khatibu wa Sala ya Ijumaa, Alhamdulilahi mtu akitazama anamuona kuwa yeye ni mwanabalagha mzuri, mtu mwenye fikra nzuri na komavu na ana uwezo mkubwa na kazi hii, Inshallah tunataraji kwa baraka za Mwenyezi Mungu ataweza kufanya kazi yake hii (ya kuwa Khatibu wa Sala ya Ijumaa) kwa njia bora kabisa. Hili ni miongoni mwa yale mambo ambayo nilikuwa nikiyatamani: hatujapoteza kitu, bali tumepata kitu kingine na kukitia mkononi. Alhamdulilahi, mji wa Bojnourd haujampoteza Bwana Mehman-Nawaz pamoja na baraka za uwepo wake, watu wameendelea kumrejea kwa ajili ya kutaaradhiwa shida zao kama ilivyokuwa huko nyuma; tumepata pia kitu kingine, ambacho ni kwamba, yeye ni Khatibu wa Sala ya Ijumaa.
Ewe Rabi! kile ambacho tunakifanya, tunachokisema na kile tunachonua kukifanya, tunakuomba ukifanye kiwe kwa ajili Yako na kiweke katika njia Yako; kitakabali hiki kutoka kwetu kwa ukarimu na fadhila Zako. Ewe Mola! Ufanye moyo wa Mtukufu Imam Mahdi (roho zetu ziwe fidia kwake) uwe radhi na sisi; tufanye sisi kuwa ni wenye kuombewa dua na mtukufu huyo (Baqiyatullah katika ardhi). Tunakuomba Ewe Mwenyezi Mungu Mtukufu! Ufanye mkusanyiko huu wa hadhira, matalaba, mafudhalaa na watu wengine wa dini walioko hapa na wanaojishughulisha kufanya kazi katika eneo hili wote wawe askari wakweli wa (kutetea) Uislamu na Qur'ani Tukufu. Tunakuomba uyazidishe mapenzi na huba hii siku baada ya siku ambayo tumeishuhudia leo imetawala baina ya ndugu Mashia na Masuni; wote hawa tunakuomba uwaongoze katika njia ya kheri, bora na njia ya uongofu wa umma.
Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabakaatuh.
 
< Nyuma   Mbele >

^