Skip to content

Habari

Habari
Hifadhi

Risala na Barua

Matini
Hifadhi

Kumbukumbu na Simulizi

Kabla ya Mapinduzi
Baada ya Mapinduzi

Sauti na Taswira

Picha
Sauti
Video
Hotuba ya Kiongozi Muadhamu Mbele ya Walimu na Wahadhiri wa Vyuo Vikuu Khorasan Kaskazini Chapa
12/10/2012
Ifuatayo ni matini kamili ya hotuba ya Ayatullah Udhma, Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aliyoitoa wakati alipokutana na walimu na wahadhiri wa Vyuo Vikuu huko Khorasan Kaskazini mkutano ambao ulifanyika katika Msikiti Mkuu wa Imam Khomeini huko Bojnourd tarehe 12/10/2012
Kwa jina la Allah Mwingi wa rehma Mwenye kurehemu
Kikao hiki kina adhama na hamasa kubwa mno; kidhahiri na kimaanawi. Idadi kubwa ya waalimu wa mkoa huu - walimu wa mafunzo na malezi (wa Wizara ya Mafunzo na Malezi) na walimu wa Chuo Kikuu - waliohudhuria hapa wanavuka upeo wa macho (wako wengi) na kwa hakika wanazifurahisha na kuzikoga nyoyo. Maneno yaliyosemwa hapa nayo, mengi yake yalikuwa yamepimwa, ya kielimu, yenye ukomavu wa kifikra na yana utaalamu kamili ndani yake. Kwa hakika mtu anastaladhi na kuburudika anaposhuhudia kwamba, katika mkoa huu - ambao kwa yakini kwa upande wa kimaada na kisuhula unahesabiwa kuwa miongoni mwa mikoa maskini hapa nchini; licha ya kuwa kwa upande wa vipawa na tabia ya nchi ni tajiri sana - fikra zote nzuri hizi nzuri, fikra pevu, komavu na maneno yaliyopimwa vyema ambayo yote haya yapo katika mkoa huu. Nyinyi akina kaka na akina dada wapendwa msiwe na shaka kabisa kwamba, kikao hiki kwa mja dhaifu kama mimi ilikuwa ni hadia na zawadi ya Mwenyezi Mungu kwangu na ninamshukuru sana Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa kunipa tawfiki na wasaa wa kuweza kukutana na nyinyi hapa na kusikiliza maneno haya mazuri nay a kuvutia.
Kile ambacho ni mapendekezo ya ndugu hapa, ingawa baadhi ya mapendekezo hayo yanahusiana na vyombo vya utendaji na maafisa wa serikali katika sekta mbalimbali, ambapo ni kawaida sisi huchukua mapendekezo hayo na kuwafikishia wahusika na vyombo husika, binafsi sisi sio watekelezaji wa haya; lakini baadhi ya mapendekezo haya ni mapendekezo ya kimsingi mno ambayo bila shaka yanapaswa kuzingatiwa na kupewa uzito maalumu. Kile ambacho kimesmwa hapa na yule mwalimu mwanamama, kilikuwa sahihi kabisa, kimepimwa na cha kimantiki; vile vile baadhi ya mapendekezo haya yaliyotolewa na kusemwa hapa - ambapo mimi nimeyanukuu - yote haya yanahitajia kuyapitia vizuri, kuyatafakari na kufanyia kazi. Tunamuomba Mwenyezi Mungu atupe tawfiki ili tuweze kustafidi na matunda ya fikra zenu na Inshallah Mwenyezi Mungu atatujaalia katika hili kulingana na uwezo, nguvu na tawfiki anayotupatia na hivyo kunufaika na hayo katika sekta ya uongozi wa jamii ambayo kwa sasa yanahusiana na uga huo.
Napenda kutumia fursa hii adhimu kuashiria nukta moja. Wimbo ulioimbwa hapa ulikuwa mzuri na muziki (kughani) nao ulikuwa mzuri na vile vile mambo yaliyobainishwa katika wimbi huo yalikuwa ni mambo yenye faida. Mimi sibainishi nukta hii kwa ajili ya kikao hiki tu, bali napenda kuona mambo haya yakienea katika kila kona ya nchi. Bila shaka kuonyesha huba na mapenzi baina ya viongozi na wananchi na hususan watu wenye vipawa ni jambo zuri kabisa. Hii kwamba, kujitokeze kundi la watu wenye vipawa, watu wa utamaduni, walimu na wahadhiri na waonyeshe huba na mapenzi yao kwa mtu fulani anayehudumu na ambaye ana majukumu serikali, ni jambo zuri sana na kwa bahati nzuri hili ni jambo ambalo liko katika nchi yetu; lakini hili ni jambo ambalo haliko katika nchi nyingi duniani; kwa hakika hizi ni miongoni mwa baraka za Uislamu na ni katika baraka za kushikamana na dini; na jambo hili ni la pande mbili. Hili hili ni jambo ambalo lipo baina ya viongozi na wananchi au baina ya wenye vipawa na viongozi wa serikali, mapenzi na huba hii ni ya pande mbili; ukweli wa mambo ni kuwa haiwezekani pakawepo na mapenzi ya upande mmoja. Endapo kutakuwa na mvutano wa upande mmoja na mapenzi ambayo ni ya upande mmoja, huba na mapenzi hayo yataharabika na hayawezi kudumu. Kwa muktadha huo, huba na mapenzi ni kitu cha pande mbili. Isipokuwa nukta ambayo mimi ninataka kuizungumzia hapa ni hii kwamba, hii hali ya kuonyesha huba na mapenzi isiishie tu katika maneno na kusifia kwa maneno mazuri jambo ambalo linaeleweka na wote. Tab'ani, mashairi ni sehemu ya kuonyesha wasifu na balagha na kutia chumvi; lakini hii kwamba, mtu anajitokeza na kuwasifia watu wadogo na mja dhaifu kama mimi na kuwapa daraja kubwa na kisha kuleta majina ambayo ni makhsusi kwa waja wakubwa wa Mwenyezi Mungu na majina ambayo ni makhsusi na maalumu kwa Maasumina, Manabii na Mawalii wa Mwenyezi Mungu, kwa hakika hili ni jambo baya sana. Hatupaswi kuueneza utamaduni huu katika jamii. Kuondoa (kutoyatumia katika utoaji wasifu) maneno haya katu hakukinzani kwa namna yoyote ile na huba na mapenzi ya pande mbili.
Vizuri, miongoni mwa matilaba (mambo) yaliyobainishwa na ndugu hapa - jambo hilo limezungumziwa na watu wa Vyuo Vikuu na limebainishwa pia na ndugu kutoka katika mafunzo na malezi - zilikuwa nukta nzuri mno na ambazo zilikuwa na umakini wa hali ya juu. Kwa hakika sisi tunahitajia kuboresha hali ya mafunzo na elimu katika nchi yetu. Lengo la Mapinduzi ya Kiislamu na Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu halikuwa kwamba, nchi moja iongezeke katika nchi nyingine na iwe ikishindana na nchi hizo katika ushindani wa maendeleo ya kimaada, ustawi wa kielimu, maendeleo ya kijeshi na kisiasa; kama ambavyo ni jambo la kawaida na ambalo limekuwa likifuatiliwa na viongozi wa nchi mbalimbali duniani. Suala la Uislamu na kuasisi utawala katika Uislamu ni jambo la kutokea mabadiliko katika ujudi wa mwanadamu. Katika ujudi na ndani ya nyoyo zetu, hapa kuna masuala mengi. Mwenyezi Mungu anasema:
Bila shaka tumemuumba mtu (mwanaadamu) kwa umbo liliobora kabisa. Kisha tukamrudisha kuwa chini kuliko waliochini. (At-Tin 95:4-5).
Yaani maandalizi kukwea na kuwa na daraja ya juu pamoja na maandalizi ya kuporomoka na kushuka darajani yamkini kusema kuwa, ni mambo ambayo yako katika ujudi wetu sisi wanaadamu (yaani ni mambo ambayo yako mikononi mwetu). Falsafa ya mwanaadamu kuumbwa ni kuvifanya vipawa na maandalizi ya mwanadamu kuwa juu ya sifa zile mbaya zisizo za kibinaadamu kwa hima na juhudi za mwanadamu mwenyewe ambapo kama hali hii itapatikana, wakati huo hivyo hivyo vipaji na maandalizi ya kuwa ni mtu mwenye sifa mbaya zisizo za kibinaadamu hupata muelekeo sahihi. Endapo msukumo na moyo wa kuvamia utawekwa katika kuhudumia taqwa na uchaji Mungu, utazuia kuvamia mambo matukufu - matukufu ya kibinaadamu, kijamii na kiakhlaqi (kimaadili) - na hivyo hilo kutumika katika njia sahihi na inayofaa. Katika Qur'ani Tukufu na katika Uislamu suala la kukabiliana na mauaji limeamrishwa na kukokotezwa; hata hivyo kulitumia vizuri hili na msukumo pamoja na moyo ulioko katika ujudi wa mwanadamu ni jambo ambalo hulifanya hilo kuwa katika kuhudumia uongofu wa mwanadamu na katika kutengeneza dunia iliyobora, huru na tukufu. Mauaji haya au kukabiliana huku na mauaji kimsingi ni kutokomeza na kusambaratisha mwanadamu vikwazo na vizingiti kwa ajili ya kuelekea katika vilele aali vya utukufu wa mwanadamu.
Endapo sifa kama hizi za kimaumbile, vipaji hivi na maandalizi haya yatatangulizwa mbele basi bila shaka dunia hii itakuwa nzuri; itakuwaa dunia ya saada na ufanisi. Itakuwa dunia ambayo haina uvamizi, katika dunia kama hiyo kutakuwa hakuna ile hali ya kupumzishwa na kutotumika vipaji vya mwanadamu, kutakuwa hakuna hali ya kuvipeleka vipaji hivi upande wa upotofu; katika dunia kama hii hakuna ufakiri wala ubaguzi. Tazameni dunia hii itakuwa nzuri kiasi gani. Katika dunia kama hiyo, mwanadamu ataweza kutumia suhula na uwezo wote wa uwepo wake. Uwezo wa uwepo wetu sio huu ambao hadi leo mwanadamu ameweza kuufikia katika nyuga za elimu na tajiriba; hii ni sehemu tu ya uwezo wa mwanadamu lakini ukweli wa mambo ni kuwa, uwezo wa mwanadamu ni mkubwa mno kuliko hivi. Sisi katika mtazamo wa uwezo wetu wa kimwili tumekumbwa na hali ya mtazamo finyu; kwa hakika sisi hata hatutambui kwa njia sahihi uwezo hasa wa miili yetu. Kwa hakika mimi nimekuwa nikitoa mifano mara chungu nzima nikiwaambia kwamba, nyinyi mtazameni mchezaji wa sarakasi; kwa mtu ambaye si mwanamichezo na hajaleleka katika mazingira ya michezo, hivi anaweza kudhani katika fikra na akili zake kwamba, mwili wa mwanadamu unaweza kufanya harakati namna hii? Yaani harakati zinazofanywa na wachezaji wa sarakasi? Lakini ukweli wa mambo ni kuwa, hilo ni jambo ambalo linawezekana kwa kuweko mazoezi, mtu wa kawaida tu kama ataingia katika uwanja huo na kufanya mazoezi tena mtu wa kawaida tu, ambaye hana tofauti na watu wengine, anaweza kuzifanya harakati hizi. Sasa njooni na tieni katika hisabu uwezo wa maelefu kwa maelfu wa mwanadamu ambao anao katika masuala mbalimbali na muone mwanadamu anaweza kuwa vipi na ni kwa kiasi gani ana uwezo mkubwa. Haya yote yapo katika ile dunia ambayo sifa aali za Kimwenyezi Mungu na kibinaadamu zimezishinda sifa mbaya na zisizo na thamani. Huu ndio ujumbe na risala na hili ndilo lengo. Kama lengo ni hili basi kuna haja ya kufanya hima na idili kubwa.
Kwa hakika sisi tuko mwanzoni kabisa mwa hatua zetu katika njia hii; licha ya maendeleo yote tuliyoyapata. Sio kwamba, sisi tuje na kutoyapa umuhimu maendeleo na ustawi huu wa kielimu; vizuri, mnaona ni kwa kiasi gani tunajifakharisha na maendeleo haya; tuna maendeleo ya kielimu, tuna maendeleo ya kiteknolojia, tumepiga hatua katika uga wa kisiasa, tumepiga hatua katika uwanja wa ujenzi, tuna uwezo wa kitaifa, tuna izza ya kitaifa; kwa hakika haya yote ni mambo ambayo yana thamani mno; lakini pamoja na hayo, hizi ni hatua za mwanzo wa kazi. Wakati mtu anapokuwa na mtazamo huu kuhusiana na risala ya nchi na risala ya Kiislamu ya taifa - ambayo ni harakati ya kila upande ya majimui ya nchi - wakati huo nafasi muhimu ya mafunzo, malezi na nafasi ya mazingira ya elimu hudhihirika na kujitokeza. Katika nchi yetu mafunzo na malezi pamoja na mafunzo ya juu yanazidi kuwa na nafasi. Na mimi napenda kuwaeleza kwamba; lengo hasa la kuandaliwa vikao kama hivi, iwe na wahadhiri au na wanachuo - hususan na wahadhiri au walimu - hapa au mjini Tehran kabla ya sisi kuzungumza mawili matatu au kusikiliza matilaba kutoka kwa ndugu - ambapo kwa hakika hili ni jambo lenye faida na sudi kubwa - ni kuonyesha heshima na taadhima pamoja na kumtukuza mwalimu na mhadhiri katika jamii na kulifanya hili kuwa ni jambo ambalo limekita mizizi katika jamii; kwa hakika sisi tunahitajia hili.
Kwa hakika sisi tunataka thamani ya mwalimu ifahamike na kueleweka - awe ni mwalimu wa Wizara ya Elimu na Malezi au mwalimu (mhadhiri) wa Chuo Kikuu - na wakati thamani ya mwalimu inapojulikana, katika hatua ya awali ni mwalimu mwenyewe ambaye anapaswa kutambua thamani hiyo na hivyo kumfanya aongeze bidii katika ufundishaji wake na kufundisha kwa kadiri ya uwezo wake wote na ajitahidi kuongeza uwezo wake. Na ndio maana katika kikao hiki lengo na gharadhi yetu ya asili ni kusema kuwa, tunaheshimu na kuthamini mchango wa majimui ya walimu wa mkoa huu ambao misingi yake bado mipya, na Alhamdulilahi mtu akitazama anaona ni kwa kiasi gani mkoa huu una thamani kwa upande wa kiwango cha walimu na idadi yao; iwe ni walimu wa wizara ya Elimu na Malezi au walimu wa Chuo Kikuu.
Nukta moja iliyokuwako katika mazungumzo na matilaba yaliyozungumzwa hapa na watu ambapo lilishughulisha pia fikra na akili yangu ni hili kwamba, kwa hakika katika hatua ya awali sisi tunapaswa kumpa mtoto shakhsia na utambulisho wake na hii ni moja ya majukumu makuu na ya kimsingi ya malezi katika Wizara ya Elimu na Malezi hapa nchini. Endapo sisi tutaweza kumlea mtoto na kumpa shakhsia na utambulisho wake tangu katika kipindi cha utoto wake na kisha tukaleta vipaji katika ujudi wake, kwa hakika mtu huyu atakuwa ni mwenye faida daima.
Kuna vizingiti na kikawaida vizingiti hivi hutokana na kuathirika na masuala ya kiakhlaqi; lakini kama tangu mwanzo shakhsia kama hii itajengwa na kulelewa katika ujudi wa mtoto na kukua, taathira ya vizingiti itakuwa ndogo na vitu visaidizi navyo vitakuwa na msaada wake katika njia hii. Mmoja wa akina mama aliyezungumza hapa ameashiria nukta muhimu mno katika uwanja huu ambayo ni sahihi kabisa. Hii leo katika ulimwengu wa nchi za kimaada zilizoendelea, moja ya kazi za kimsingi na moja ya taaluma muhimu ni kufundisha falsafa watoto. Kuna watu wengi katika jamii yetu ambao hawadhani kabisa kwamba, falsafa pia ni lazima kwa watoto. Baadhi ya watu wanadhani kwamba, falsafa ni jambo kubwa mno ambalo linazingatiwa na watu katika kipindi cha umri mkubwa; hapana hivi sivyo. Falsafa ni kuunda fikra, kumfundisha mtoto namna ya kufahamu mambo, kuifunza akili namna ya kufahamu, kufikiri na kuzoea; hili ni jambo ambalo linapaswa kuzingatiwa tangu mwanzo. Kwa maana kwamba, inabidi akili ya mtoto izoeshwe tangu mwanzoni kabisa mwa kipindi chake cha utotoni, utamaduni wa kutumia akili, kufikiri na kutumia hekima. Hii ni fremu muhimu.
Licha ya kuwa katika falsafa hii hii ya watoto jambo la muhwata ni muhimu lakini njia kubwa ni kumzoesha mtoto; yaani tangu awali mtoto awe na ada ya kufikiri, kutumia hekima na kujiamini; hili ni jambo muhimu sana. Mimi nimefurahi mno kuona kwamba, watu wameliashiria na kulizungumzia hili katika mazungumzo yao. Nukta nyingine ni kujiamini. Kujiamini na kujua kwamba mtu anao uwezo wa kufanya jambo bila ya kutegemea wengine. Hivyo tunapaswa kumfundisha mtoto hali ya kujiamini na kuwa na utambulisho.
Hata hivyo hili sio jambo ambalo ni makhsusi na maalumu kwa watoto wa shule za msingi tu, hapana, bali katika Shule za Sekondari pia hili linapaswa kuweko na hata katika Vyuo Vikuu hili ni jambo ambalo linapaswa kuweko. Inasikitisha kuwa, katika nchi yetu kuna utamaduni ghalati na uliopotoka ambao umetokana na athari za huko nyuma na hadi sasa athari zake hazijaondoka - sambamba na propaganda hizi zote ambazo zimekuwa zikituandama tangu mwanzoni mwa mapinduzi hadi leo - nao ni kuwa na mtazamo wa kuwategemea Wamagharibi na kuiona Magharibi kuwa ni kitu kikubwa sana na watu kujiona duni mbele ya Magharibi; ambapo inasikitisha kwamba, mizizi ya utamaduni na ada hii hayaijang'olewa; na hii inatokana na kutokuweko hali ya kujiamiamini. Bila shaka mnaona inapotokea kitu fulani au bidhaa fulani ambayo ina nembo ya nje, basi (wauzaji) hutaka itolewe pesa zaidi, na hili lina wafuasi wengi katika jamii. Hii ni katika hali ambayo, kuna wakati bidhaa ya ndani kiwango na ubora wake unakuwa mzuri zaidi kuliko bidhaa hiyo ya kigeni hata hivyo ile ya kigeni hununuliwa na ya ndani kuachwa. Kwa hakika haya ni maradhi ambayo yanapaswa kupatiwa tiba. Ikitokea kwamba, watu wakasema unamuona mtaalamu yule katika uga fulani ni msomi mzuri, lakini ikujulikana kwamba, amesomea hapa hapa ndani na hakubahatika kwenda kusoma nje ya nchi katika hatua ya awali mtu huwa na mtazamo hasi naye. Ndio, kama ikitokea kwamba, msomi huyo wa hapa ndani ambaye hakusoma nje ya nchi amefanya mambo makubwa - ambapo katika miaka ya hivi karibuni haya yametokea mengi - wakati huo mtazamo huwa tofauti; hata hivyo madhali watakuwa wakisema tu huyu amesoma nje ya nchi na yule amesoma hapa hapa ndani, aliyesoma nje huangaliwa kwa jicho la ubora na ufadhali (hata kama aliyesoma hapa nchini atakuwa na elimu kumzidi huyo). Hii ni kasumba na ada mbaya sana. Yamkini mkawa mmenisikia sana, kwa hakika mimi sipingi mtu kwenda kusoma nje; nimesema mara kadhaa kwamba, sioni jambo baya sisi kuwa ni wanafunzi wa mtu fulani, tukaenda kwake na kujifunza jambo; lakini ni jambo mbaya kama tutahisi kwamba, tuko dhalili mbele ya fikra za wengine na kazi za wengine. Kwa hakika hili ni jambo baya sana na ambalo linapaswa kung'olewa mizizi. Jambo linaloweza kung'oa mizizi ya utamaduni huo mbovu na ghalati ni kuenea moyo wa kujiamini.
Suala la kujiamini katika wakati huu ambapo fikra ya kujiona duni mbele ya Wamagharibi imeshamiri ni jambo linalohitajia hima na idili za kuwafanya watu waliamini na inabidi lipewe umuhimu mkubwa na kustawishwa vilivyo katika fikra za watoto wadogo na vijana na bila shaka kupuliza roho ya kujiamini katika nyoyo za vijana na watoto wadogo ni moja ya majukumu muhimu na ya kimsingi ya Wizara ya Elimu na Malezi na Wizara ya Elimu ya Juu nchini. Wakati mwingine mtu anashuhudia kwamba, wakati mwingine sisi tunataka kuleta akhlaqi na maadili mazuri katika jamii mfano ambao tunaotoa kwa ajili ya kusifia tabia njema, ni lazima uwe ni wa nchi za Masharibi? Kuna ulazima gani wa kufanya hivyo. Kwa nini sisi tunataka kupandikiza moyo huu kwa tunaozungumza nao na kuimarisha hali hii katika ujudi wake kwamba, tunapotaka kutenganisha baina ya baya na zuri na jambo stadi na lisilo stadi, lazima tuelekea upande wa Magharibi? Hili ndio lile jambo ambalo baadhi ya ndugu hapa wamelisema, yaani kuwa na imani na Magharibi na kuiona Magharibi kuwa ni kitu kikubwa sana na watu kujiona duni mbele ya Magharibi hususan katika masuala ya kielimu. Hii hali ya kujiamini ni kwa ajili ya kukabiliana na kuwategemea Wamagharibi. Huku hakuna maana ya kuwa na uadui na mtu, kufanya hivi hakuna maana ya kuwa na taasubi dhidi ya eneo fulani la kijiografia au eneo fulani la kisiasa; hii ina maana kuwa, wakati taifa fulani linapoupa mgongo uwezo wake, kipaji chake na matunda yake na kutokuwa na imani nayo, hupatwa na hatima ile ile iliyoyapata mataifa yaliyokuwa tegemezi - iwe ni taifa letu wenyewe katika kipindi cha utawala wa Kipahlavi au iwe ni nchi nyingine ambazo tunazishuhudia - hukumbwa na hali hiyo.
Tunapaswa kuimarisha hali ya kujiamini kwa vijana na kwa watoto wetu. Yaani tupulizie roho ya kujiamini katika nyoyo za vijana na watoto wadogo. Mimi ninaona wakati mwingine kuna ripoti zinanifikia ambazo zinaonyesha kuwa, mwalimu fulani au mhadhiri fulani akiwa darasani ameonyesha shaka aliyonayo kuhusiana na maendeleo fulani ya kielimu ambayo kimsingi yako wazi na hayana shaka; jambo hili linatokea. Jaalieni kwa mfano katika uga wa seli shina, katika uwanja wa teknolojia na katika nyuga tofauti tofauti za kielimu - ambapo kwa sasa kwa bahati nzuri kuna maendeleo mengi ya kielimu katika sekta na nyuga mbalimbali - hili ni jambo ambalo limetokea; hili ni tukio la kweli, sio la kutilia shaka, liko mbele ya macho, linahisika; lakini anajitokeza bwana huyu akiwa darasani katika Chuo Kikuu au katika shule ya sekondari na kuanza kutia dosari na kutilia shaka: hapana, bwana sio hivi; maraa ooo jambo hili halifahamiki vyema! Sisi tuna msukumo gani? Kama tutajaalia kwamba, sisi wenyewe tuna shaka kwamba, maendeleo haya yamepatikana, kuna haja gani ya kuwaeleza vijana mambo haya? Vizuri, twendeni na tufanye uhakika; ili jambo hili liwe wazi na lenye kueleweka kwetu. Hivyo basi kupuliza roho ya kujiamini katika nyoyo za vijana na watoto wadogo ni moja ya kazi ambazo ni muhimu na za kimsingi.
Nukta nyingine ni uvumilifu na ustahamilivu. Moja ya mambo ambayo sisi tunayahitajia katika maingiliano na mahusiano ya kijamii ni moyo wa kuvumilia na kustahamili; yaani ustahamilivu. Hii kwamba, katika Uislamu na katika akhlaqi (maadili) za Kiislamu suala la ustahamilivu limekokotezwa na kutajwa namna hii, ni kutokana na sababu hii. Kutokuweko ustahamilivu ndio chanzo kikuu cha matatizo mengi ya kijamii na ya mtu binafsi. Kwa maana kwamba, kukosekana kwa sifa hii ya kimaadili hupelekea mtu na jamii kukumbwa na matatizo chungu nzima. Kama makundi ya kisiasa yataamiliana kwa uvumilivu na kustahamiliana, basi anga ya kisiasa itakuwa nzuri zaidi. Kama wafuasi wa kundi hili na wa kundi lile wataamiliana na kufanya mambo kwa uvumilivu anga na hali ya mambo itakuwa bora sana. Kuamialiana kwa uvumilivu na ustahamilivu, hakuna maana ya kufumbia macho mambo mabaya na machafu; hakuna maana ya kutokuwa na imani na mambo ya asili, yenye thamani na matukufu katika itikadi zetu; moja ya aina ya kuamiliana ni hii inayoelezwa na Mwenyezi Mungu Mtukufu katika Qur'ani Tukufu:
Waite waelekee kwenye Njia ya Mola wako Mlezi kwa hikima na mawaidha mema, na ujadiliane nao kwa namna iliyo bora. (An-Nahl 16:125). Hivyo basi hata kufanya mjadala na mdahalo na mtu mwingine kuhusiana na itikadi fulani au kuhusiana na jambo fulani muhimu, kunapaswa kufanya kwa njia iliyo bora.
Suala jingine ni kadhia ya udadisi na moyo wa kupenda kufahamu mambo jambo ambalo nalo lilikuweko katika matamshi ya ndugu hapa; yaani hali ya kuuliza na kudadisi mambo kwa nia ya kutaka kufahamu na kufuatilia. Nukta nyingine ni Kueneza na kutia nguvu moyo wa kudadisi na kupenda kutambua mambo, kufanya kazi za pamoja na za kushirikiana, kupenda kuchapa kazi na kujiweka mbali na uvivu, kupenda kusoma na kutalii vitabu kati ya watoto wadogo na kizazi cha vijana. Hivyo basi kuna haja na udharura wa kuwazoesha watoto na vijana juu ya kuwa na hima kubwa.
Kuna masuala tofauti tofauti ambayo yanapaswa kutazamwa katika kiwango cha kimataifa na sio katika uga wa kieneo, seuze mtu atake kuyatazama mambo hayo katika kiwango cha nchi au atake kuyatazama mambo katika kiwango cha Mkoa na Wilaya. Kuna masuala ambayo yapo na ambayo yanapaswa kutazamwa katika upeo wa miaka mia moja, miaka mia moja na hamsini, na sio katika upeo wa miaka hamsini, kumi au kidogo zaidi. Haya ni mambo ambayo yanahitajia hima kubwa; kuna haja ya kuwa na mtazamo na upeo wa mbali kuhusiana na masuala mbalimbali. Huyu mwanafunzi au mwanachuo ambaye leo nyinyi mnamlea, siku chache zijazo atakuwa mwalimu, atakuwa mkurugenzi amilifu, mtaalamu stadi, mtu mwenye taathira katika harakati ya kisiasa ya kijamii; muda si mrefu atakuwa mtu mwenye taathira katika jamii. Mleeni na muandaeni mwanafunzi huyu namna hii ili aje kuwa mtu mwenye taathira katika jamii. Hivyo basi mnapaswa kumlea mwanafunzi huyu namna hii ili aje kuwa mtu mwenye hima kubwa.
Nukta nyingine ni kufanya kazi. Moja ya matatizo yetu ni uvivu. Suala la kutwalii na kusoma vitabu. Katika jamii yetu kuna hali ya kupuuza suala la usomaji vitabu. Kuna wakati mtu anaona katika televisheni watu wakiuliza swali hili kwamba: Ndugu yangu wewe kwa siku unatumia masaa mangapi kutwalii, au una muda kiasi gani wa kutwalii na kujisomea? Anatokea mtu mmoja kwa mfano anajibu kwa kusema, dakika tano, mwingine anasema nusu saa! Kwa hakika mtu anashangaa kusikia haya. Tunapaswa kuwazoesha vijana ada ya kutwalii na kujisomea vitabu, tunawazoeshe watoto kujisomea; tukifanya hivi ataendelea kuwa hivi mpaka mwishoni mwa umri wake. Kusoma na kujisomea katika umri wangu - tab'ani mimi ninasoma zaidi na kutwalii vitabu kuliko vijana - aghalabu taathira yake ni ndogo zaidi kuliko kujisomea na kusoma vitabu katika umri wa ujana na akthari ya nyinyi ambao mko hapa. Kile ambacho hubakia daima kwa ajili ya mwanadamu ni kusoma vitabu katika umri mdogo. Hakikisheni vijana wenu na watoto wenu wanajisomea kadiri wawezavyo; someni vitabu vya taaluma na fani mbalimbali, kwa njia tofauti na hivyo mjifunze mambo mbalimbali. Tab'ani, kuna haja ya kujiepusha na uchafuzi katika mazingira ya kitabu. Suala la kwanza kabisa ni kujifunza, kuwafanya watoto na vijana wawe na ada ya kujisomea na kurejea katika vitabu yaani kuchukua kitabu na kukipitia. Tab'ani vyombo husika vinapaswa kuwa makini, watu wanaohusika katika uga huu wawe makini na watoe miongozo ya vitabu vizuri; mtu asipoteze umri wake bure kwa kusoma kitabu kibaya na kisichofaa.
Nukta nyingine ni hii ambayo ilisemwa na mmoja wa akina mama hapa na nimeinukuu; nukta ambayo ni muhimu sana: Hizi sifa ambazo sisi tunataka kuzifanya zijipambe katika ujudi wa watoto wetu - sasa yamkini wakawa wamesema haya kuhusiana na Wizara ya Mafunzo na Malezi - haziwezi kuja hivi hivi; haya ni mambo ambayo yanahitaji kuyafanyia kazi. Nani afanye kazi? Walimu; iwe ni katika kiwango cha Mafunzo na Malezi (Wizara ya Malezi) au iwe ni katika kiwango cha Chuo Kikuu. Walimu wanapaswa kuwa na maandalizi kwa ajili ya kazi hii; wawe na tajiriba na ustadi katika kazi hii; hili linahusiana na vyombo vya juu ambavyo vinaandaa na kuleta malezi haya. Ndio, kufanya hivi ni mantiki. Kwa sasa mheshimiwa Waziri wa Elimu na Malezi yupo hapa; nendeni na mkalizungumzie hili serikalini na nyinyi wenyewe mtazame ni kazi gani mnaweza kufanya.
Wanasema kweli; kama sisi tunataka kuzifanya sifa nzuri ziwepo kwa watu tunaowahutubu darasani, tunahitajia kuwa na mwalimu ambaye anajua afanye nini. Sio wote wanaofahamu hili; hivyo kuna haja ya kujifunza. Kuna haja ya kuanzishwa vituo; hapa imeelezwa kuwa vituo vya utafiti wa kiutamaduni wa familia au utamaduni wa familia; haya ni miongoni mwa yaliyokuwa mapendekezo yaliyotolewa na baadhi ya watu hapa; kwa hakika haya ni mapendekezo mazuri sana na yaliyo sahihi kabisa; kuna haja ya hili kufanyiwa kazi. Haya yote yanasimamia usalama wa kimaadili wa familia, lakini yote haya yawepo pia katika shule na katika Vyuo Vikuu. Kwa hakika maendeleo ambayo tumeyapata sisi na ambayo kimsingi ni mambo ambayo tunayapenda na yanapendwa na majimui ya tabaka la wanautamaduni na watu wa masuala ya elimu hapa nchini, ni maendeleo yasiyo ya kawaida (makubwa). Yaani hatupaswi kutilia shaka hata kidogo kwamba, sisi tunaweza.
Hili ni jambo ambalo liko mbele ya macho ya watu wote. Sisi mwanzoni mwa mapinduzi tulikuwa na wanafunzi takribani laki moja na elfu sabini, hii leo tuna wanachuo zaidi ya milioni nne. Katika zama hizo, tulikuwa na wanachama elfu tano wa Bosi ya Elimu. Pale pale mwanzoni, binafsi ninakumbuka jinsi idadi hiyo ya wanachama elfu tano wa Bodi ya Elimu ilivyokuwa ikisemwa na kurejewarejewa. Yaani idadi hiyo ilikuwa inawezekana kuhesabiwa; baadhi walikuwa wakisema, mmoja amepungua bwana au kwa mfano kumi wamepungua! Hii leo idadi ya wanachama wa bodi yetu ya elimu ni kubwa mno. Kwa bahati nzuri sisi tuna makumi ya maelfu ya wanachama wa Bodi ya Elimu. Hii leo kuna Vyuo Vikuu vilivyokamilika (ambavyo vimejumuisha kila kitu) mia mbili katika kila kona ya nchi na kuna Vyuo Vikuu na Vituo vya Elimu ya Juu hapa nchini; kwa hakika haya sio mambo machache. Kwa hakika sisi tumeyafanya na kuyapata haya katika mazingira magumu. Hivi hivi vikwazo ambapo sasa maadui wanasema wamevishadidisha au wamo katika pirika pirika za kushadidisha vikwazo (dhidi ya taifa hili) hivyo daima, vilikuweko tangu mwanzoni mwa Mapinduzi ya Kiislamu. Fauka ya hayo tulitwishwa vita vya kichokozi vya miaka minane (vita vya kichokozi dhidi ya Iran vilivyoanzishwa na utawala wa dikteta wa zamani wa Iraq, Saddam Hussain) ; na mbali na hayo, katika duru mbalimbali tulikabiliwa na hali ya kushuka kwa bei ya mafuta; kuna matatizo mengi ya ndani ambayo tulitwishwa; tulikuwa pia na ongezeko la watu - mwanzoni mwa mapinduzi idadi ya wananchi wa Iran ilikuwa milioni 35; idadi hiyo imekuwa mara mbili sasa - masuala yote haya yalikuweko; licha ya hayo yote, Alhamdulilahi tumepiga hatua kubwa leo katika nyga mbalimbali.
Napenda kuwaambia kwamba; maendeleo haya yaliyopatikana katika nyuga za kielimu, yametokana na nukta fulani maalumu (kikundi fulani cha watu kilichoko katika kona fulani ya nchi); hapana, haya yamepatikana kwa juhudi na hima za pamoja na za kila upande; katika sehemu nyingi ambazo sisi tumepata ustawi na maendeleo, kuna kundi fulani lenye mapenzi na kipaji ambalo lilipata himaya ya kiwango fulani kutoka katika nukta fulani na ghafla moja jambo hilo likashika kasi na kufikia katika kilele. Miaka ya nyuma walikuja hapa viongozi na maafisa wa moja ya nchi ambazo ni marafiki zetu - sitaki kutaja jina la nchi - wakatwambia, wao wametenga kiwango fulani cha bajeti kwa ajili ya jambo fulani - kwa mfano kwa ajili ya uga wa teknolojia - na nchi zote zimejikita katika hilo. Sisi hatujafanya hilo. Kile ambacho kimetokea sababu yake ni uwepo wa vipawa, kutokana na kuweko shauku na hamu kutoka kwa makundi mbalimbali; baadhi yao wamejitokeza tu, sio kwamba, nchi nzima imejikita kwa mfano (jaalineni) katika suala la seli shina; hapana, vijana kadhaa wenye vipawa na ambao wana hamu na shauku na seli shina wamelifuatilia hili na kupata himaya fulani kutoka kona fulani; ghafla moja kama mnavyoona vijana hawa wameondokea kuwa miongoni mwa watu stadi ulimwenguni. Kuhusiana na suala la Teknolojia ya Nano, hali iko namna hii pia na vile vile katika masuala mengine hali iko namna hii pia. Huu mjadala kuhusiana na makombora, iwe ni makombora ambayo yanahusiana anga, makombora ya kurushia satalaiti, iwe ni makombora ya kijeshi, hizi zote ni kazi ambazo zimefanyika kwa msukumo, shauku, mapenzi na raghba ya makundi ya vijana wataalamu wa hapa nchini. Kilijitokeza kikundi cha watu kadhaa kikaanza kufanya hili na kisha baadaye watu wote wakaja kuona natija yake. Ninataka kusema kuwa, vipawa na uwezo katika kiwango cha nchi, hakina kikomo. Kwa hakika sisi tunaweza kusonga mbele zaidi ya hapa.
Hivi sasa katika kiwango cha dunia (kimataifa), nafasi ya 16 inashikiliwa na Iran. Je kuna mtu ambaye alikuwa akiliamini hili kwamba, linaweza kutokea? Takwimu hizi zinatolewa na vituo vya elimu ambavyo vina itibari duniani. Kisha kinajitokeza kituo kimoja cha elimu na kutabiri kwamba, hadi kufikia mwaka 2018, Iran itakwea na kufikia nafasi ya nne katika masuala ya elimu duniani. Hivyo basi, suhula na uwezo wa nchi yetu uko namna hii. Hisa ya Iran katika kuzalisha elimu duniani kwa sasa ni asilimia mbili; yaani ni mara mbili ya kile ambacho Iran inaweza kukifanya katika hali ya kawaid na ambacho inapaswa kuwa nacho katika kuchangia hisa ya elimu duniani. Haya ni mambo makubwa na ni mambo muhimu mno.
Kwa muktadha huo, tunapaswa kuongeza hali yetu ya matumaini, hili ndilo ninalotaka kulisema kwa sasa. Kwa hakika sisi tunapaswa kufanya kazi nyingi na kubwa serikali na viongozi wa ngazi za juu tunapaswa kufanya hilo; lakini kile ambacho ni msingi wa kadhia nyinyi mnapaswa mkiwa madarasani iwe ni katika Wizara ya Elimu na Malezi au katika Vyuo Vikuu, ni kupanda mbegu ya matumaini ya harakati katika nyoyo za vijana na mnaowalenga; kufanya hivi kutaifanya harakati hii isonge mbele kwa kasi kubwa, na bila shaka itasonga mbele. Kama hili litatokea, nchi itaweza kustafidi na kijana huyu kadiri inavyowezekana. Tufanye hima ili kuleta nishati na matumaini. Kuna hatari ziko njiani ambazo zinawakabili vijana; moja ya hatari hizo ni kukata tamaa; ambapo inapaswa kadiri inavyowezekana kujiepusha na suala la kupandikiza hali ya kukata tamaa.
Tab'ani, katika mkoa huu kuna matatizo mengi, katika uga wa mafunzo na malezi na vile vile kuhusiana na suhula na nyenzo katika uga huu. Aidha katika Vyuo Vikuu pia kuna matatizo; ambapo sehemu ya matatizo hayo yamo katika ripoti niliyopatiwa na vile vile sehemu ya hayo yamebainishwa na ndugu waliozungumza hapa. Tuna matumaini, Inshallah mambo haya yatatuliwa na kupatiwa ufumbuzi. Tab'ani, sisi tutawafikishia maafisa wahusika serikalini. Kazi za kiutendaji na masuala kama haya, yanahusiana na majukumu maalumu; haipaswi kufanya uingiliaji katika haya. Tab'ani, sisi tunasisitiza, tunathibitisha na kuyafikisha haya kwa wahusika na tunawataka wahusika wayafanye haya kadiri wanavyoweza na kadiri suhula zinavyowaruhusu. Wakati huo huo, katika mazingira ya kijana mnapaswa kuchunga irfani za uongo; hasa kwa kuzingatia kwamba mambo haya yamekuwa yakiingizwa katika Vyuo Vikuu. Moja kati ya mikakati ya (maadui) ni kuingiza irfani za uongo ndani ya Vyuo Vikuu; na hivi ni miongoni mwa vitu na mambo ambayo yanalemaza na kukwamisha mambo. Kama mtu atanasa na kuwa mtumwa na mateka wa haya mambo yasiyo na asili wala msingi yaani irfani za uongo - ambapo aghalabu zimeingia na kupenya hapa nchini zikitokea nje - atakuwa amekwenda ndiko siko kwani kwa hakika irfani hizi zinalemaza na kukwamisha mambo. Kigezo ambacho sisi tunacho kwa ajili ya kufanya harakati kuelekea upande wa daraja za juu za kimaanawi na kiroho na kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu, ni taqwa na uchaji Mungu, kujiweka mbali na madhambi na kufungamana na utakasifu wa nafsi. Vijana wetu - iwe ni mabinti zetu au watoto wetu wa kiume (vijana) - kama watakuwa watakasifu wa nafsi, kama wataitanguliza mbele taqwa na uchaji Mungu, kama watafanya hima ya kujiweka mbali na kufanya madhambi, endapo watasali kwa umakini na kumzingatia Mwenyezi Mungu na kutosimamisha (yaani kuendeleza) hali yao ya kuainisika na kushikamana na Qur'ani Tukufu, bila shaka hawawezi kuwa watumwa wa irfani hizi za uongo na zisizo na msingi wala thamani yoyote.
Aghalabu mimi nimekuwa nikiwausia na kuwasisitizia vijana washikame na kuanisika na Qur'ani Tukufu. Jitahidi msikate mahusiano yenu na Qur'ani Tukufu. Jitahidi msome Kitabu cha Mwenyezi Mungu (Qur'ani Tukufu) kila siku japo ukurasa mmoja; haya yote ni mambo ambayo yanamkurubisha mwanaadamu na Mwenyezi Mungu; kufanya hivyo humfanya mwanadamu kupata sifa nzuri za kiroho na kimaanawi. Hupatikana ile hali ya utulivu, subira na utulivu wa moyo ambayo ni hitajio la mwanadamu - ambapo Mwenyezi Mungu anasema:
Mwenyezi Mungu aliteremsha utulivu juu ya Mtume Wake na juu ya waumini na akawalazimisha neno la kumcha Mungu. ( Al-Fat'hi 48:26). Kwa hakika hii neema ambayo Mwenyezi Mungu amewapatia waumini kama anavyosema kwamba, aliteremsha utulivu juu ya Mtume Wake na juu ya waumini. Hivyo basi taqwa na uchaji Mungu unapatikana kupitia mambo haya; katika hatua ya awali ni kujiweka mbali na madhambi. Hii kwamba, tunasema kujiweka mbali na madhambi hakuna maana kwamba, muache kwanza dhambi zote na kisha muingie katika marhala na hatua ya pili; hapana, haya ni mambo ambayo yanakwenda sambamba na pamoja. Hima na idili inapaswa kuwa hii kwamba, tufanye kila tuwezalo ili tusifanye dhambi. Taqwa nayo ni hivyo hivyo. Kushikamana na ibada ya Sala, kusoma Qur'ani na amali nyingine njema mfano wa hizo ni vitu ambavyo vinatupatia sisi sifa za kiroho; vinatupa sisi ile hali ya utulivu wa nafsi, uhakika na pozo la moyo linalohitajika; hivyo hakuna haja ya kwenda katika nyumba zenye irfani zisizo na ukweli ndani yake, kufuata urongo, kuelekea upande wa kimaada, kukimbilia mambo ambayo hayana uhalisia wowote ndani yake. Wanachuo na vijana wa sekondari kuweni makini na hili na mzingatie na kushikamana na upande huu wa kufungamana na dini na kuwa watu wa dini. Lifanyeni suala la kushikamana na dini kuwa msingi wa mnaozungumza nao na tambueni kwamba, Inshallah Mwenyezi Mungu atatoa auni na msaada.
Vizuri, muda nao naona umetupa mkono. Tuna matarajio kwamba, Mwenyezi Mungu atakifanya kile tulichokisema na kile tulichokisikia kuwa chenye faida na sisi na atatupa tawfiki ili tuweze Inshallah kutekeleza majukumu yetu kwa njia bora kabisa na kama inavyopaswa.
Wassalaamu Alaykum Warahmatullah Wabarakaatuh.
 
< Nyuma   Mbele >

^