Skip to content

Habari

Habari
Hifadhi

Risala na Barua

Matini
Hifadhi

Kumbukumbu na Simulizi

Kabla ya Mapinduzi
Baada ya Mapinduzi

Sauti na Taswira

Picha
Sauti
Video
Miongozo ya Kiongozi Alipoonana na Waendeshaji wa Kongamano la Kumkumbuka Qutbuddin Shirazi Chapa
03/12/2012
Ifuatayo ni matini kamili ya miongozo ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei aliyoitoa siku ya Jumatatu ya tarehe 3 Disemba 2012 mbele ya wasimamiaji na waendeshaji wa kongamano la kimataifa la kujadili hali na athari za ‘Hakim' Qutbuddin Shirazi. Tumeamua kuweka mtandaoni hotuba hiyo kwa mnasaba wa kufanyika kongamano hilo.
Bismillahir Rahmanir Rahim
Kuadhimisha utajo wa watu muhimu mithili ya Qutbuddin Shirazi ni jambo la busara na lenye faida kubwa. Katika akili yangu ilipata kunipitikia kuwa madaktari na watu wa masuala ya tiba walifanya busara kumchukua Qutbuddin Shirazi na kumuingiza kwenye ulimwengu wa tiba. Lakini Qutbuddin Shirazi alikuwa ni mwanafalsafa kabla ya jambo lolote. Alikuwa ni mwanafunzi wa Khoja Nasir na aliandika kitabu cha sherhe ya Hikmatul Ishraq na vitabu vingine kama hivyo. Tab'an alikuwa pia tabibu stadi na mkubwa na vile vile alikuwa mnajibu na mtaalamu bingwa wa falaki. Alichangia sana katika ujenzi wa kituo cha kuchunguza falaki na nyota cha Maragheh (kaskazini magharibi mwa Iran), yaani kwa hakika alikuwa mtu mkubwa sana. Lakini matamshi haya ya Dk Lankarani (Waziri wa zamani wa Afya wa Iran) nayo ni matamshi mazuri. Yaani tujue kuwa wasomi wetu katika vipindi mbali mbali vya Uislamu walikuwa wametabahari kwenye fununi za kila namna na wala haikuwa kwamba walipata kidogo hapa na kidogo pale, bali walikuwa wametabahari sana katika kila upande. Qutbuddin Shirazi alikuwa mtu mkubwa sana katika fani ya tiba kama ambavyo alikuwa ni gwiji katika upande wa falaki na nyota. Vile vile alikuwa mwanafalsafa kabili, alikuwa shaha wa malenga kama ambavyo pia alikuwa na umbuji wa kupigiwa mfano katika fasihi. Kama mlivyoashiria hapa, sherhe ya kitabu cha Qanun (kitabu maarufu cha tiba) cha Abu Ali Sina, imeandikwa na Qutbddin Shirazi. Alikuwa shaha wa malenga na gwiji wa anuwai ya tungo za kishairi za Kiarabu na Kifarsi na yamkini alikuwa ametabahari pia katika fani na ilimu nyinginezo. Vile vile hapa tunapata somo kwamba, kuwa mtaalamu mtu katika kitu kimoja tu na kuifunga akili katika mambo mengine si jambo kubwa. Tab'ani ni jambo zuri mtu kukifanyia kazi kitu kimoja na kuufanya mdogo mzingiro wa kitu hicho kwa ajili ya kujua zaidi na zaidi undani wake na hilo kama litakuwa ni kwa ajili ya kumtumikia mwanadamu, si jambo baya lakini vile vile utaalamu wa namna hiyo nao humbana na kumuwekea mipaka mtu wakati akili ya mwanadamu ni pana sana na inaweza kuwa na utaalamu mkubwa katika masuala yote hayo na kumfanya mtu kuwa marejeo ya watu katika fani nyingi. Si sahihi kwa mfano mtu madhali yeye ni daktari basi awe maamuma na asijue chochote katika masuala ya elimu za dini au elimu za falsafa, hapana, bali ni vizuri sana kwa mtu kuwa na utaalamu mkubwa katika kitu fulani kama tiba, lakini pia akawa na elimu ya masuala mengineyo katika elimu za kiakili na masuala mengineyo yanayohusiana na maumbile. Ni vizuri sana kama tutaweza kuliimarisha na kuliendeleza jambo hilo humu nchini. Tab'an maelezo yangu haya hayana maana kamwe ya kufunga milango ya kuwa na utaalamu wa kina juu ya kitu fulani kimoja, bali lengo langu ni kuwa tusizifunge akili zetu katika jambo moja ila tuzipe akili zetu uhuru wa kuchanua pia katika masuala mengineyo.
Naam, Shiraz ni kituo muhimu ambacho kina historia ya kuwa na watu wakubwa na hili nalo pekee ni nukta nzuri ya kuzingatiwa katika maeneo mbali mbali ya Iran yetu ya Kiislamu. Mimi nililisema pia jambo hilo wakati nilipotembelea Shiraz miaka kadhaa iliyopita. Kwa kweli Shiraz ni katika moja ya maeneo ya nchi yetu ambayo yana uwezo mkubwa usio na mipaka. Wakati mtu anapoangalia kila upande anaona kuwa Shiraz ni eneo lenye baraka nyingi katika upande wa kulea vipaji vikubwa vya watu, katika suala la malenga na washairi, upande wa fasihi, upande wa falsafa, masuala ya kielimu alimradi Shiraz ni eneo ambalo limelea watu wakubwa sana wa kila namna. Naam, hilo linaweza kuhesabiwa kuwa ni utambulisho wa eneo hilo na kwamba watu ambao wanafanya kazi za kusomesha, kulea na kukuza fikra na vipaji vya watu nchini wanapaswa kulizingatia sana jambo hilo na kujua kuwa Shiraz ina vipaji visivyoisha. Kwa mfano, Qutbuddin Shirazi ni Allama kutoka Shirazi yaani anajulikana kwa sifa ya Allama na hiyo ni kwa sababu alikuwa ametabahari katika fani tofauti. Jitahidini kumfanya mtu huyu mkubwa kuwa kigezo kwa ajili ya kizazi kimpya na vijana wetu wa leo ili kijana wa leo awe na yakini kuwa anaweza kumfanya Qutbuddini Shirazi kuwa kigezo chake. Hatuna haja ya kuhangaika kutafuta watu kutoka katika machimbo yenye kina kirefu ya Zama za Kati za kiza totoro za Ulaya na kumfanya kigezo, tunao watu wetu wengi ambao ni kigezo kizuri kwetu kama huyu (Qutbuddin Shirazi).
Pili zingatieni kuwa harakati hii ya kielimu katika nchi yetu ilikuwa imenawiri humu nchini katika zama ambazo Magharibi na Ulaya (zilikuwa kwenye kiza totoro na) hazikuwa na ustawi wowote wa kielimu. Qutbuddin Shirazi aliishi katika karne ya Saba Hijria, yaani inavyoonekana alifariki dunia mwanzoni mwa karne ya nane. Yaani katika kpindi hicho cha karne za 13 na 14 Milaadia alikuwa tayari ametabahari katika masuala yote hayo wakati Ulaya haikuwa na chochote. Hebu natujiulize Ulaya wakati huo ilikuwa na nini. Wazungu walikuwa watu wa namna gani wakati huo? Wakati huo nuru ya elimu ilikuwa haijaangaza barani Ulaya. Lakini angalia huku kwetu, kulikuwa na watu wakubwa kama huyo na kama Khoja Nasir na Katebi. Katebi ni miongoni mwa walimu wa Qutbuddin Shirazi. Katebi Qazvini alikuwa mwanafalsafa mkubwa. Watu mithili ya Qutbuddin Shirazi walikuwa wamejaa huku kwetu wakati huo.
Ni matumaini yangu Inshaallah Mwenyezi Mungu atakusaidieni ili muweze kuifanikisha vizuri sana kazi hiyo.
Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.
 
< Nyuma   Mbele >

^