Skip to content

Habari

Habari
Hifadhi

Risala na Barua

Matini
Hifadhi

Kumbukumbu na Simulizi

Kabla ya Mapinduzi
Baada ya Mapinduzi

Sauti na Taswira

Picha
Sauti
Video
Hotuba ya Kiongozi Muadhamu Mbele ya Hadhara ya Wananchi wa Bojnurd Chapa
10/10/2012

Ifuatayo ni hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei mbele ya hadhara ya wananchi wa Bojnurd katika uwanja wa michezo wa Takhti, Bojnurd aliyoitoa tarehe 10 Oktoba 2012.

Kwa jina la Allah, Mwingi wa rehema Mwenye kurehemu
Hamdu na sifa zote njema ni za Mwenyezi Mungu Mola wa ulimwengu. Na rehma na amani zimshukie bwana wetu na kipenzi chetu Abul Qasim al Mustafa Muhammad, na Aali zake wema, watoharifu, na masahaba zake wema. Na amani iwashukie waja wema wa Mwenyezi Mungu. Ewe Mola Mwenyezi mteremshie rehma Ali Ibn Musa Ridha mwenye kuridhiwa, Imamu mchaMungu, mtoharifu na huja wako kwa kila aliyeko juu zaidi ya ardhi na kila aliyeko chini ya udongo, mkweli mno na shahidi. (Umteremshie) rehma nyingi, zilizokamilika, zenye baraka, zilizoungana, za mtawalia na zenye kufuatana kwa namna iliyo bora kama uliyomteremshia yeyote miongoni mwa waja wako na mawalii wako.

Ninamshukuru Mwenyezi Mungu - na nalisema hili kwa udhati wa moyoni - kwamba mkutano huu na nyinyi wananchi wapenzi wa mkoa wa Khorasan Kaskazini, ambao mji wenu na mkoa wenu ni maarufu kwa jina la Mlango wa Ridha, umefanyika katika siku ya kufanya ziara makhsusi ya kumzuru Imam Ridha. Japokuwa sisi hatujapata taufiki leo ya kuwepo karibu na Haram toharifu ya Imam wa Nane, lakini tumetuma sala na salamu zetu kutokea katika eneo hili ambalo ni eneo la mtukufu huyo.
Eneo hili ambalo hii leo linajulikana kwa jina "Khorasan Kaskazini" ni moja ya maeneo muhimu ya Khorasan; ni kwa upande wa kijiografia na kimaumbile na pia kutokana na sifa za kiutu, kiutamaduni, kihulka na kitabia za watu wake. Tokea hapo zamani tumekuwa tukiwajua watu wa eneo hili muhimu na nyeti kuwa wamepambika na sifa hizi; ni mkoa wenye mandhari ya maumbile ya kuvutia, utajiri mkubwa na wa aina mbalimbali za maliasili,utajiri mkubwa na wa kina wa utamaduni wenye sifa za aina yake na za kipekee, vipawa chungu nzima vya sekta ya kilimo na mifugo pamoja na shughuli nyenginezo zinazohusiana na eneo hili, vivutio vya utalii ambavyo havijajulikana - kwani watu wengi nchini bado hawajavijua sawasawa vivutio vya utalii vya eneo hili - na moja ya sifa yake nyengine kubwa kabisa ni kuwa kwake njia inayopitwa kila mwaka na mamilioni ya watu wasafiri wenye hamu na shauku ya kuizuru Haram ya Ali Ibn Musa Ridha (Alayhi aalafut - tahiyati wathanaa). Kutokana na kuwa na sifa hizi za kijiografia na kikanda, Khorasan Kaskazini ni eneo lenye nafasi nyeti. Lakini muhimu zaidi ya yote hayo ni sifa za watu wake. Tokea hapo zamani, tumekuwa tukiwajua watu wa hapa kuwa ni watu wenye motisha, ari na matumaini ya kimaisha katika medani zote. Katika nyuga zote ambazo ushiriki wa watu unashuhudiwa kwa uwazi kabisa, tumekuwa tukiwaelewa watu wa mkoa wa Khorasan Kaskazini, watu wa Bojnurd na watu wa maeneo mengine ya mkoa huu kwa sifa za kuwa na ari na matumaini ya maisha na motisha ya kuwa tayari kwa kazi; na hili limeonyeshwa na watu wa maeneo yote ya mkoa huu. Kutokea hapa hapa kwanza natoa shukurani zangu kwa wananchi kwa jinsi walivyojitokeza leo mabarabarani - ambapo katika kipindi cha saa moja na nusu hadi mbili cha harakati ya wananchi tulipokuwa barabarani, ilihisika waziwazi hali hiyo ya uchangamko, shauku, ari na matumaini ya maisha pamoja na moyo wa ushiriki na utayarifu; hii ni hali tunayoijua tangu zamani kuwa wamepambika nayo watu hawa - na vilevile ninaomba radhi. Vijana wapenzi walikuwa wamefurika mabarabarani kiasi kwamba kwa kweli mimi niliyekuwemo garini nimekaa nilikuwa nahofia mbinyo waliokuwa wakipata wananchi hawa wapenzi. Alaa kulli hal ninakushukuruni na pia ninakuombeni radhi.
Hii hali ya uchangamko, shauku na matumaini ya maisha inaonekana katika pande zote za maisha ya wananchi hawa. Siku ya tarehe 28 Safar ambapo watu kutoka kila pembe ya mkoa hufunga safari kuelekea haram ya Ali Ibn Ridha (alayhis salam), magari na wasafiri wanaotoka Bojnurd ndio wengi zaidi kuliko miji mingine yote. Watu wa Mashhad wanalijua hili; mimi mwenyewe ambaye ni mtu wa Mashhad ninalijua hilo. Wakati wa ufanyaji ziara, hali ya uchangamko, ushiriki na utayarifu inahisika kabisa. Katika uga wa Kujihami Kutakatifu pia wakati ulipotokea, mtu alishuhudia hali hiyohiyo pia. Makamanda hodari 50 wa vikosi vya Khorasan na brigedi za Jawadul Aimmah (alayhis salam) walitoka upande wa Khorasan Kaskazini. Mashahidi 2,772 kutoka eneo hili walitoa roho zao katika njia ya Mwenyezi Mungu. Mkoa huu una majeruhi wa vita zaidi ya 6,000; aidha una wapiganaji chungu nzima ambao walikuwa vitani, waliojitolea na wale waliokuwa mateka vitani. Hii imetokana na ule moyo wa ushiriki, utayarifu, uchangamko na ari, hamasa na matumaini ya maisha.
Watu wa mkoa huu wako hivyo katika mambo yote. Wakati inapowadia zamu ya mchezo wa mieleka kwa kutumia vazi la sufu makumi ya maelfu watazamaji hukaa na kusimama huku na kule kuangalia mieleka. Sifa hizi ni sifa zenye umuhimu. Ghera ya ulindaji mipaka liliyonayo eneo hili nayo pia inahusiana na sifa hizi. Tab'an si mambo hayo tu bali mkoa huu una sifa nyingine za kipekee zaidi ya hizo.
Mkoa huu una vipawa vyenye kung'ara. Kwa mujibu wa taarifa nilizopewa, mkoa huu ni moja ya mikoa kumi nchini inayoongoza kwa vipawa na uwezo wa kielimu. Katika Olimpiadi za wanafunzi ni moja ya mikoa inayoongoza nchini. Hivyo ni vipawa. Tab'an mimi mwenyewe wakati nilipokuwa mwanafunzi wa kidini Mashhad nilijionea mifano mbalimbali ya vipawa hivi vyenye kung'ara na vya kipekee. Lakini hayo hayana ulazima wa kuyazungumza hapa; inshallah nitayaeleza katika hadhara ya maulamaa na wanafunzi wa kidini. Wananchi wa eneo hili ni watu wenye ghera; ni watu walioshika dini; ni watu wenye kuilinda mipaka ya nchi; na ni watu mashujaa, wenye uchangamko, shauku na matumaini ya maisha. Sifa hizi ni sifa za kipekee.
Kwa nini ninayasema haya? Kwa sababu ni vizuri watu wetu wa maeneo mbalimbali nchini waelewe sifa bora walizonazo na kujivunia sifa hizo. Kijana wa Bojnurd ajivunie kuwa anatoka mji huu. Kijana anayetoka mkoa huu, wa kila kaumu na kabila aone fahari na kujivunia kutoka katika mkoa huu; kuwa ni mtu wa eneo hili; kuwa ni mtu anayetokana na watu hawa. Moja ya sifa nyengine unayosifika nayo mkoa huu ni huku kuishi kwa pamoja, upendo na udugu watu wa makabila tofauti - kuanzia Wakurdi, Wafarsi, Waturuki, Watat mpaka Waturkaman - ambao wote hawa wameishi pamoja kwa salama, upendo na udugu; na hili linahisika na linaonekana kwa uwazi kabisa katika eneo hili, na ni jambo linalopasa kuthaminiwa mno.
Sasa niingie rasmi kwenye mada kuu niliyoikusudia. Ndugu zanguni wapenzi! Akina kaka! Akina dada! Mmezisikia sifa hizi. Uchangamko huu, shauku, hamasa na matumaini haya ya maisha na kuwa na utayarifu wa kazi umekuwepo nchini kote tangu baada ya Mapinduzi hadi hii leo; na hii ni moja ya hidaya kubwa kwa taifa lenye makusudio ya kupiga hatua ili kusonga mbele, lenye makusudio ya kufikia kwenye ustawi na utukukaji na linalotaka kuwa na maisha mema. Hali hii ya kuwa tayari kwa kazi, uchangamko, shauku, hamasa na matumaini ya maisha ni neema kubwa, lakini hii haitoshi. Ili kuweza kufika kileleni kuna masharti mengine pia. Kwanza inapasa iwepo ramani ya njia; yaani lijulikane lengo la harakati, yajulikane matarajio yanayokusudiwa kufikiwa, iainishwe dira na njia inayokusudiwa kufuatwa katika harakati hiyo, kisha kuwepo ufahamu thabiti na sahihi na uangalifu wa kudumu juu ya harakati yenyewe. Hili ni jamabo la lazima kwa taifa. Leo haya ni miongoni mwa masuala yetu ya msingi.
Ninasisitiza sana na hasa kwa vijana wetu wapenzi na watu wenye vipawa nchini wayazingatie masuala ya msingi kwa wakati huu; sisi leo hii tunahitajia mambo haya. Malengo ya harakati hii yalishaainishwa tangu mwanzoni mwa Mapinduzi; kiujumla ramani ya njia ilishajulikana katika sha'ar za wananchi na pia katika maneno ya Imamu (radhi za Mwenyezi Mungu Mtukufu ziwe juu yake); baadaye katika muda wote huu, katika miaka hii thelathini ramani kamili ya njia imetandikwa, imethibitishwa na kukamilishwa; leo taifa la Iran linajua linataka nini na linafuatilia kitu gani.
Kama tutataka kueleza kwa muhtasari kuhusu malengo ya taifa la Iran, kwa maneno yatakayoweza kwa kiasi kubwa kubainisha na kujumuisha matakwa makuu ya taifa na wananchi wote nchini, neno kuu linalobainisha matakwa hayo ni maendeleo; lakini ni kwa tafsiri inayotolewa na Uislamu kuhusu maendeleo. Maendeleo katika mantiki ya Uislamu ni tofauti na maendeleo katika mantiki ya ustaarabu wa kimaada wa Magharibi. Wao wanaangalia katika upande mmoja tu, wao wanayaangalia maendeleo kwa mtazamo mmoja tu ambao ni mtazamo wa kimaada. Katika mtazamo wao wao, maendeleo, kwanza kabisa na yenye umuhimu zaidi ni maendeleo ya utajiri, maendeleo katika elimu, maendeleo ya kijeshi na maendeleo ya teknolojia. Hayo ndiyo maendeleo katika mantiki ya Kimagharibi; lakini katika mantiki ya Uislamu maendeleo yana sura nyingi zaidi: maendeleo katika elimu, maendeleo katika maadili, maendeleo katika uadilifu, maendeleo katika ustawi wa jamii, maendeleo katika uchumi, maendeleo katika izza, heshima na itibari kimataifa, maendeleo katika kujitawala na kujitegemea kisiasa - hayo yote yamejumuishwa kwenye tafsiri ya maendeleo katika Uislamu - maendeleo katika kuabudu na kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu; yaani upande wa kimaanawi, upande wa kidini; hii pia ni sehemu ya maendeleo ambayo imo katika Uislamu na ni moja ya ghaya na malengo makuu katika mapinduzi yetu: kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu. Katika maendeleo haya imezingatiwa "dunia" na pia imezingatiwa "akhera". Uislamu umetufunza kwamba
«ليس منّا من ترك دنياه لأخرته و لا ءاخرته لدنياه»
Si katika sisi anayeiacha dunia yake kwa ajili ya akhera yake na wala anayeiacha akhera yake kwa ajili ya dunia yake. Haitakiwi kuiacha dunia kwa sababu ya akhera, kama ambavyo haitakiwi kuitoa mhanga akhera kwa ajili ya dunia. Katika hadithi moja inaelezwa kwamba «اعمل لدنياك كأنّك تعيش ابدا» Fanya kwa ajili ya dunia yako kama kwamba utaishi milele; yaani usipange mipango na ratiba ya dunia kwa ajili ya siku chache tu za maisha yako mwenyewe; panga ratiba kwa ajili ya miaka hamsini. Hili linapasa kuzingatiwa na viongozi nchini pamoja na wakuu wanaohusika na upangaji mipango kwa ajili ya wananchi. Tusiseme kwamba kuna haja gani ya kuratibu mipango wakati hakuna uhakika kama tutakuwa tungali hai miaka hamsini ijayo. Hapana, panga ratiba kwa namna ambayo kama vile imepangwa ubaki hai mpaka mwisho wa dunia; kama ambavyo unakuwa na uangalifu na umakini mkubwa unapotaka kupanga mambo kwa ajili yako na kwa manufaa yako, basi upange na ufanye hivyo hivyo kwa ajili vizazi vijavyo vya wakati huo ambapo wewe utakuwa hupo; «اعمل لدنياك كأنّك تعيش ابدا» kwa hivyo fanya kwa ajili ya dunia yako kama kwamba utaishi milele. Mkabala na hilo pia ni kwamba «و اعمل لأخرتك كأنّك تموت غدا» na fanya kwa ajili ya akhera yako kama kwamba utakufa kesho; yaani fanya kwa ajili ya akhera yako kama kwamba imepangwa kesho wewe uondoke duniani. Yaani ujipinde kikamilifu kwa ajili ya dunia na pia ujipinde kikamilifu kwa ajili ya akhera. Hii ndiyo maana ya maendeleo ya Kiislamu, maendeleo katika mantiki ya Uislamu, yaani maendeleo ya pande zote. Lengo ni maendeleo; lakini kuna ulazima wa kuwa na uangalifu na usimamizi katika awamu hadi awamu, na hii ni kazi ya wenye vipawa. Leo tuko kwenye hali gani, tunakabiliwa na vizuizi gani, nukta zetu chanya ni zipi, nukta za udhaifu wetu ni zipi, ni fursa gani tulizonazo, matishio yanayotukabili ni yepi, nini tunapaswa kufanya, tupange vipi mambo yetu ili kuweza kufaidika na fursa na kuzuia hatari ya matishio; hizi ni kazi zinazopasa kufanywa na wenye vipawa katika kila awamu; tuzitumie katika upangaji ratiba na mipango na pia tuwaeleweshe wananchi; kwa sababu wananchi wanataka kupiga hatua katika harakati hii wakiwa wanajua kinachoendelea na wakiwa na urazini na uoni wa mbali wa mambo, wajue wanafanya nini na wajue wanaelekea wapi. Itakapokuwa hivyo wananchi wataweza kujitolea katika medani ngumu kwa uwezo wao wote.
Sasa kama nitataka kutoa tathmini yangu kuhusu lengo lililoelezwa, tathmini yangu ni kwamba imefanyika kazi nzuri. Katika muda wa kipindi cha miaka thelathini ya Mapinduzi, sisi tumeweza kupiga hatua mtawalia. Bila ya shaka kumekuwepo hali ya kupwa na kujaa, ya kasi na ya kujikokota, na ya nguvu na udhaifu lakini maendeleo ya nchi na taifa kuelekea kwenye kilele kilichokusudiwa hayakusita abadani. Kumekuwepo udhaifu pia; inapasa wananchi, viongozi na wenye vipawa - wenye vipawa vya kisiasa, wenye vipawa vya kielimu, wenye vipawa vya kidini - wachukue hatua na maamuzi ya kuondoa udhaifu huo. Tuongeze kasi ya maendeleo nchini. Ni vitu gani vinaweza kutuwezesha kupata mafanikio na vitu vinaweza kutuletea matatizo? Nitakupigieni mfano: jaalieni kuna kundi moja la wapanda mlima ambao wanataka kufikia kileleni kabisa mwa mlima huo ambao una manufaa na mambo ya kujivunia kwao. Hima kubwa watakayokuwa nayo watu hao ni kupiga hatua mbele na kufanya bidii na jitihada. Bila ya shaka watakapokuwa njiani inawezekana watakabiliwa na matatizo na kutakawepo hatari mbali mbali. Lakini lililo na umuhimu wa kwanza kwao wao ni kufanya idili na jitihada, kuonyesha harakati, kuwa na azma thabiti, kutopoteza matumaini, kutokata tamaa ya kufikia malengo, kuwa na subira, kupanga ratiba na mikakati, kuwa macho na kuwa na utayarifu wa kukabiliana na matatizo. Yamkini njiani yatajitokeza matatizo na hatari mbalimbali. Kuhusu hilo, nitaashiria yale yaliyowakabili wananchi wetu wapenzi katika miaka thelathini ya Mapinduzi na jinsi wananchi wetu walivyoweza kuyavuka matatizo hayo. Kwa hivyo dira na mwongozo mkuu wa harakati hii kubwa na adhimu ni huko kuwa na azma thabiti, ni huko kuwa na matumaini, ni huo uchapaji kazi na juhudi za mtawalia, ni huo upangaji ratiba na mipango na huo utayarifu na kuwa macho na makini. Ikiwa itakuwepo dira na mwongozo huu mkuu, ikiwa tutakuwa nazo nguzo hizi za msingi, majimui yetu hii iliyoko katika harakati - ambapo katika mfano wetu sisi ni mithili ya wapanda mlima; na katika hakika yake ni taifa la Iran - itayashinda matatizo yote na itaweza kuwapigisha magoti maadui zake wote. Huu ndio msingi mkuu wa kila kitu. Ikiwa dira na mwongozo huu utakuwepo tatizo lolote lile katika maana yake halisi halitokuwa tatizo kwetu, hatari yoyote ile haitokuwa hatari kwetu. Hatari halisi ni ipi? Hatari halisi itakuwepo pale taifa litakapopoteza dira na mwongozo huu mkuu; yaani litakapopoteza moyo wa juhudi na uchapaji kazi, litakapoingiwa na uvivu na ugoigoi, litakapopoteza moyo wa matumaini, litakapokata tamaa; litakapopoteza subira na muqawama; litakapoingiwa na pupa na papara; litakaposahau kupanga na kuratibu mambo na litakapojifanyia mambo bila mipango na kupatwa na hali ya mkanganyo; hizo ndizo hatari. Ikiwa taifa litakuwa limeweza kulinda moyo huu wa kipekee ambao ni wa kupiga hatua mbele kwa matumaini, azma, imani na juhudi, tatizo lolote lile linalolikabili haliwi tatizo kwake.
Sasa turudi na kuuangalia uga wa Iran azizi na taifa adhimu la Iran. Ningependa yale ninayoyasema na yale ninayofikiria yawiyane na mantiki; sitaki kusema maneno ya nara na sha'ar. Mimi sikubaliani na uelezaji mambo hasa wa masuala ya Mapinduzi kwa kutumia lugha ya ukuzaji mambo na utiaji chumvi. Na tuangalie ni lipi la kimantiki, na ukweli halisi ni upi.
Taifa la Iran liko katika uga na medani ya kukabiliana na mjumuiko wa maadui, ni wao ndio walioanzisha uadui huo na kinara wa maadui hao ni mtandao hatari na habithi wa Kizayuni, na kwa bahati mbaya baadhi ya wakati madola ya Magharibi na hasa serikali ya Marekani inaathiriwa na mtanadao huu. Wao tokea mwanzo wa Mapinduzi waliyapinga Mapinduzi ya Kiislamu na Jamhuri ya Kiislamu; nyoyoni mwao wamekuwa na kinyongo na uadui na wananchi waliofanya mapinduzi haya; hivi sasa pia wana hali hiyohiyo. Katika medani hii ya mkabiliano, upande mmoja liko taifa la Iran na upande mwengine yako baadhi ya madola ambayo yana uadui wa bughudha na chuki na taifa la Iran. Wakati tunapoiangalia medani hii tukilitupia jicho taifa letu azizi tunaona taifa letu ni lenye azma thabiti, ni lenye matumaini, ni lenye vipawa vya hali ya juu na ni taifa lenye kizazi cha vijana wenye moyo wa hali ya juu na bidii kubwa. Huku kujitokeza kwa kizazi cha vijana katika medani zote kwenyewe kunadhihrisha jambo hilo: katika medani ya sayansi leo dunia inakiri juu ya jambo hilo; katika medani ya teknolojia, katika medani mbalimbali za kijamii; katika wakati ule ilikuwa ni kujitokeza kwenye medani ya Kujihami Kutakatifu (vita) na leo hii wako tayari kujitokeza katika medani nyengine mbalimbali. Hayo ni mambo liliyonayo taifa la Iran hii leo; lina mpango wa matarajio ya miaka ishirini pia, linazo suhula zinazohitajika kwa ajili ya kupiga hatua kuelekea mbele, lina rasilimali za maliasili na lina madini ya thamani kubwa pia.
Akiba tuliyonayo nchini ya maliasili kuu ni kubwa zaidi kulinganisha na wastani wa madini hayo yaliyoko duniani. Nimewahi kueleza mara kadhaa kuwa sisi ni takribani asilimia moja ya idadi ya watu wote duniani, ardhi ya nchi yetu takribani ni asilimia moja pia ya ukubwa wa eneo la dunia; lakini maliasili kuu tulizonazo ni kubwa zaidi ya asilimia moja. Katika baadhi ya maliasili tunaongoza kati ya nchi zote duniani; kwa mfano maliasili za nishati - mafuta na gesi - leo sisi ndio tunaoongoza katika orodha ya nchi zote duniani. Hizi ndizo hali tulizonazo.
Ardhi yetu ni ardhi yenye hali za hewa za aina tofauti. Nchi yetu ni nchi yenye ardhi kubwa. Kuna kila kitu kulingana na mahitaji yetu. Tuna hali nzuri ya maumbile, tuna madini mazuri, tuna watu wazuri, tuna vipawa vizuri, tuna viongozi wenye uchungu wa wananchi pia katika mihimili mitatu ya dola, tuna vikosi vya ulinzi shujaa vilivyojizatiti na kujiweka tayari, tuna maulamaa wema, wenye uchungu na mapenzi na watu, tuna vyuo vikuu na maskuli yaliyojaa wanafunzi - idadi ya wanachuo ni milioni nne na kuna mamilioni kadhaa ya wanafunzi - hizi ni suhula tulizonazo na uwezo na vipawa tulivyonavyo; taifa letu lina azma, irada na matumaini pia.
Harakati yetu tangu mwanzoni mwa Mapinduzi hadi hii leo imo katika hali ya kusonga mbele. Matokeo ya harakati hii ya usongaji mbele ni maendeleo ambayo yamepatikana hadi leo hii. Matunda tuliyopata katika kipindi cha miaka hii kwa kuzingatia uadui uliofanywa dhidi yetu ni ya mafanikio na ya maendeleo ambayo yameshuhudiwa na macho ya watu wote. Katika masuala ya msingi na ya miundombinu nchi imepiga hatua; katika utoaji huduma kwa wananchi nchi imepiga hatua; katika masuala ya umaanawi nchi imepiga hatua; katika utaalamu na teknolojia pia hali ni hiyohiyo. Miundombinu, ambayo maendeleo yake ni makubwa zaidi na ya kupigiwa mfano, ya kwanza kabisa ni ya uthabiti wa kisiasa wa nchi. Serikali tofauti zimeingia madarakani, na licha ya kuwepo hitilafu za mitazamo na za utashi wa kisiasa lakini uthabiti nchini umeendelea kuwepo tangu mwanzoni mwa Mapinduzi hadi leo hii na nchi imekuwa ikipiga hatua kuelekea kwenye malengo yake. Mizozo na mikwaruzano ya kimielekeo, kimirengo na kisiasa haijaweza kuondoa uthabiti wa kisiasa wa nchi; huu ndio muundombinu muhimu zaidi.
Bila ya shaka kuna miundombinu muhimu sana ya kiuchumi pia kwa upande wa kisheria na kwa upande wa uhalisia na utekelezaji. Hizi sera za ibara ya 44 (ya katiba) ni mojawapo ya miundombinu ya kisheria. Miundombinu ya mawasiliano, usafirishaji na uchukuzi, barabara, barabara kuu, njia za reli, njia za anga, fibere nuri??? Vinu vya nishati na mabwawa; zote hizo ni kazi zilizofanywa tangu mwanzoni mwa Mapinduzi hadi hii leo; na aghalabu ya karibu ya zote zimefanywa na vijana na wataalamu wa elimu wa nchi yetu wenyewe. Hayo si mambo machache, hayo ni mambo ambayo tumeweza kuyapata.
Moja ya vitu vyetu muhimu zaidi vilivyopo na vyenye thamani ni hiki kizazi cha vijana wasomi. Kizazi cha vijana wasomi kina ushujaa, kina matumaini na pia kina uchangamko na harakati. Nitoke nje kidogo ya maudhui hapa kwa kusema kwamba moja ya makosa tuliyofanya sisi wenyewe - na mimi mwenyewe nimechangia katika kosa hili - ni hili suala la kudhibiti kizazi ambalo lilipasa kusimamishwa kuanzia katikati ya muongo wa 70 (1997) kujia huku. Bila ya shaka pale mwanzo lilikuwa jambo zuri na la lazima kutekeleza sera ya kudhibiti kizazi lakini ilipasa kusimamishwa kuanzia katikati ya muongo wa 70 (1997). Hatukuisimamisha; hili lilikuwa kosa. Nimesema kwamba viongozi nchini wamechangia katika kosa hili, mimi mwenyewe al hakiri pia nimechangia katika kosa hili. Itabidi Mwenyezi Mungu Mtukufu na historia itusamehe kwa hili. Kizazi cha vijana kinapasa kiendelezwe. Kama tutaendelea na mwenendo huu wa sasa - na nilisema katika hotuba niliyotoa kitambo nyuma katika mwezi wa Ramadhani - nchi itakuwa ya jamii ya vizee. Inapasa familia na vijana waongeze idadi ya watoto; waongeze kizazi. Hili ni kosa linalofanyika hii leo la udhibiti wa namna hii wa idadi ya watoto unaofanyika majumbani. Kama hiki kizazi cha vijana tulichonacho hii leo tutaweza kukiendeleza katika miaka kumi ijayo, miaka ishirini ijayo na katika vipindi na awamu zijazo za nchi hii, kitatatua matatizo yote ya nchi kutokana na utayarifu na uchangamko kilionao kizazi cha vijana na kutokana na uwezo na kipawa kilichonacho kizazi cha Kiirani. Kwa hivyo sisi hatuna tatizo la msingi la kutuzuia tusipate maendeleo. Bila ya shaka matatizo mbalimbali pia yapo - nami nitayaashiria matatizo hayo - kuna matatizo yaliyoko nchini kote, na eneo lenu nyinyi pia linayo matatizo hayo; lenye umuhimu wa kwanza kabisa ni suala la kupanda bei za bidhaa na suala la ajira; hayo ni miongoni mwa matatizo waliyonayo wananchi; na hili halipo hapa tu bali liko nchi nzima. Jamaa hapa walifanya uchunguzi wa maoni kabla ya safari yangu na kuwauliza wananchi; tulichoona ni kwamba hapa pia kuna hali sawa na ile iliyoko katika sehemu nyenginezo. Suala la kupanda bei za bidhaa na suala la ajira na ukosefu wa kazi ni moja ya matatizo makuu. Matatizo haya yapo; lakini hakuna matatizo makubwa na ya msingi ambayo nchi, wananchi na viongozi hawawezi kuyatatua.
Katika kipindi cha miaka thelathini na tatu ya Mapinduzi zimetokea hatari kubwa zaidi ya hizi. Lakini nchi imeweza kuziondoa na kuzivuka hatari hizo. Walitaka kuwasha moto lakini hawakuweza kupata makusudio yao. Kwanza kabisa ilikuwa ni katika miezi ya mwanzoni kabisa baada ya ushindi wa Mapinduzi lilipozuka suala la kuchochea ukaumu na ukabila katika kila pembe ya nchi. Nchi yetu ni nchi ya kaumu mbalimbali. Kwa hivyo walitaka kuzichonganisha kaumu hizi. Katika eneo lenu hili kundi moja la wakomunisti wasio na imani ya dini wala nchi walijaribu kuzichochea kaumu za watu sharifu na waumini wa Kiturkamani wayapinge Mapinduzi. Ni watu gani waliosimama imara kukabiliana nao? Wa kwanza kabisa ni watu waumini wa Kiturkamani ndio waliosimama kukabiliana na watu hao. Maulamaa wenye sauti wa Kiturkamani - ambao baadhi yao wameshaaga dunia na baadhi yao alhamdulillah wangali wako hao - wao wenyewe walisimama kukabiliana na watu hao. Vijana wa maeneo mengine nchini pia pamoja na wa hapa na wa maeneo mengine tofauti walikwenda kukabiliana na watu hao. Walikuwa wakifanya uchochezi, walikuwa wakiwasha moto, walikuwa wakimimina mafuta juu ya moto na walikuwa wakitumia njia tofauti ili kuusambaza zaidi moto huo; lakini moto huo ulizimwa na wananchi wa Iran na hasa wale watu wenyewe ambao watu hao walitaka kuwafanya wasimame dhidi ya Mapinduzi ya Kiislamu. Katika eneo la Kurdistan pia ni Wakurdi wenyewe, ni watu waliokuwa tayari kufa kwa ajili ya Uislamu wa Kikurdi na maulamaa waumini wa Kikurdi ndio waliotangulia na kuwa mstari wa mbele. Katika maeneo mengine pia ilikuwa hivyo hivyo. Hili lilikuwa balaa la kwanza walilotuletea. Kisha baada ya hapo wakaanzisha Vita vya Kulazimisha. Vita vya miaka minane ni jambo la mzaha? Walitaka kuyasambaratisha Mapinduzi na kuyapigisha magoti lakini hawakuweza. Taifa liliweza kuvuka pia.
Kisha wakaleta suala la vikwazo. Leo maadui zetu, redio na baadhi ya watu wanaungana na watu hao kulikuza kwa sura ya mtawalia suala la vikwazo. Vikwazo si suala la jana na leo; vikwazo vilikuwepo tokea hapo mwanzo. Lakini walivizidisha na havikuwa na athari; wakaamua kufikiria tena njia nyengine lakini havikuwa na athari tena. Vikwazo vimekuwepo tangu mwanzo. Leo maadui zetu - iwe ni serikali ya Marekani au baadhi ya nchi za Ulaya - wamevihusisha vikwazo na suala la nishati ya nyuklia. Wanasema uwongo. Siku ile walipoanza kutuwekea vikwazo nishati ya nyuklia haikuwapo nchini na wala haikuwa ikizungumziwa pia. Kinachowahamakisha hawa kuhusiana na taifa la Iran na kuwafanya walazimike kuchukua maamuzi kama haya ni heshima liliyopata taifa la Iran na ukaidi wa taifa la Iran dhidi yao. Moyo huu wa kujitawala, moyo huu wa kuitambua thamani tuliyonayo, moyo huu wa kukataa kusalimu amri ambalo limekuwa nao taifa la Iran kwa baraka za Uislamu na Qur'ani ndio unaowakasirisha; na ni kwa sababu hiyo ndio maana wana ubaya na Uislamu, ni kwa sababu hiyo ndio maana wanamtusi na kumvunjia heshima Mtume wa Uislamu; wanajua kwamba Uislamu unapopenya na kukita ndani ya nchi moyo wa kujitawala utajitokeza ndani ya nchi hiyo kwa namna itakayoifanya isikubali tena kuburuzwa na wao. Wao huwaweka madarakani au kuwateua kushika hatamu za uongozi wa nchi watu duni na dhaifu ili waweze kuwatii wao. Wakati inapotokezea katika nchi kama yetu ambapo viongozi wanaainishwa na wananchi, na wananchi hao wanajitokeza na kushiriki kikamilifu katika medani zote ni nini watakachoweza kufanya watu hao? Wananchi walio waumini, wananchi wenye imani na misingi ya Kiislamu, wananchi wenye moyo wenye athari za baraka za Uislamu hawatosalimu amri mbele yao; kwa sababu hiyo pia watu hawa wamehamaki; lakini leo sababu yake wanaipa jina la nishati ya nyuklia! Wanataka ionekane kwamba ikiwa taifa la Iran litaachana na suala la nishati ya nyuklia vikwazo vitaondolewa. Wanasema uwongo. Wanaweka vikwazo visivyo na mantiki kwa sababu ya bughudha na chuki walizo nazo; vikwazo ambavyo wale wenye akili na watu wote wenye insafu duniani wakati wanapoangalia wanahisi watu hao wanafanya mambo yasiyo ya kimantiki na kwa kweli ni ya kishenzi; hivi ni vita dhidi ya taifa la watu. Lakini kwa taufiki ya Mwenyezi Mungu, katika vita hivi pia watu hao watashindwa na taifa la Iran.
Bila ya shaka wao wanasababisha matatizo mbalimbali, na baadhi ya watu, kutokana na kutokuwa na tadbiri wanayazidisha matatizo hayo - hayo yapo - lakini haya si mambo ambayo Jamhuri ya Kiislamu inashindwa kuyatatua. Kwa taufiki ya Mwenyezi Mungu taifa la Iran litayavuka matatizo yote haya. Wananchi wa Iran na viongozi wa nchi wameweza kuyatatua matatizo makubwa na magumu zaidi ya haya; haya si lolote si chochote. Ukitokezea mushkili mdogo tu wanafurahia. Katika hiki kipindi cha siku chache ambapo kupanda na kushuka kwa bei ya sarafu za kigeni na riyali waliifanya kuwa ndio habari kuu za mashirika yao ya habari, walionyesha furaha waziwazi. Hawajali na wala hawaheshimu hata uungwana na murua wa kidiplomasia; wanafurahia kama watoto wadogo kwamba eti tumeweza kulitia matatizoni taifa la Iran, tumeweza kuitia kwenye mazonge Jamhuri ya Kiislamu; wanalisema hili kinagaubaga! Kisha kwa muda wa masaa mawili matatu kikundi kimoja cha watu wanajitokeza kwenye barabara mbili za Tehran na kuchoma moto mapipa kadhaa ya taka na kisha wao katika upande ule wa dunia wanafurahia na kusema ndiyo, kuna fujo, kuna fujo! Hali yetu sisi ni mbaya zaidi au hali yenu nyinyi? Ni karibu mwaka mzima sasa katika barabara za nchi nyingi za Ulaya kuna maandamano usiku na mchana; Ufaransa kuna maandamano, Italia kuna maandamano, Uhispania kuna maandamano, Uingereza kuna maandamano na Ugiriki pia kuna maandamano. Matatizo yenu nyinyi na tata zaidi mara kadhaa kuliko yetu sisi. Uchumi wenu nyinyi umekwama kikamilifu, mnafurahia kuona uchumi wa Iran umekuwa dhaifu? Nyinyi mumeshaharibikiwa, nyinyi mnaelekea kwenye kuanguka na kusambaratika. Jamhuri ya Kiislamu haisambaratiki kwa matatizo haya.
Leo matatizo makubwa na ya msingi yamewazonga Wamagharibi. Hivi sasa moja ya masuala makuu yanayozungumziwa katika uchaguzi wa rais wa Marekani ni matatizo ya uchumi; watu wana hali mbaya, wametingwa na matatizo, matabaka dhaifu huko yanaumia. Hii iliyoelezwa kuwa ni harakati ya asilimia 99 ni ukweli halisi; na bila ya shaka wanaikandamiza. Nchi zao ndizo zenye mazonge ya kiuchumi; kisha wao wanafurahia hali ya hapa ambayo matatizo yake ni machache zaidi na madogo zaidi kulinganisha na yao!
Waelewe kwamba kwa fadhila za Mwenyezi Mungu, kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu, Jamhuri ya Kiislamu itayashinda matatizo haya na wao wataendelea kutamani tu laiti wangeweza kulishinda taifa la Iran. Kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu na kutokana na kuwa macho wananchi na kwa tadbiri za viongozi matatizo yaliyopo yatatatuliwa. Wananchi wana wajibu na viongozi pia tuna wajibu; sote tunapaswa kutekeleza wajibu wetu. Tutakapotekeleza wajibu wetu, kazi zitapiga hatua mbele. Kuwa macho kwa wananchi kuna mchango wake. Angalieni Tehran, idadi fulani ya watu waliojiita wahusika wa soko la biashara (bazaar) waliingia barabarani na kuanzisha fujo, lakini waheshimiwa wahusika halisi wa soko la biashara, walichukua hatua haraka na kwa wakati ya kutoa tangazo wakatangaza kuwa hawa wanasema uwongo, hao si katika sisi. Hii ni hatua sahihi. Ikiwa kuwa macho kwa matabaka mbali mbali ya wananchi kutafanyika kwa wakati na kusoma kwao alama za nyakati kutafanyika kwa wakati, hilo litakuwa jambo la thamani. Hatua hii waliyochukua jamaa hao ilikuwa hatua yenye thamani. Na haya pia ndio maneno niliyoyasema wakati wa fitina ya mwaka 88 (2009). Katika fitina ya mwaka 88, siku chache baada ya uchaguzi uliokuwa na adhama kama ile, baadhi ya watu walijitokeza kuupinga na baadhi ya wengine wakaitumia fursa hiyo kubeba silaha na kuzusha ghasia na machafuko, wakaishambulia kambi ya Basiji (jeshi la kujitolea). Maneno niliyoyasema wakati ule ni kwamba wale watu ambao mambo yaliyotokezea yalifanywa kwa kutumia jina lao, walipaswa watoe tangazo wakati uleule ili kuonyesha kuchukizwa na mambo yale na kueleza kwamba wanaofanya haya si katika sisi; lakini hawakufanya. Laiti kama wangefanya hivyo fitina ile ingetokomezwa mapema; masuala yaliyojiri baadaye yasingetokea. Sifa hizi za kuwa macho, kusoma alama za nyakati na kuzitumia fursa vizuri ni sifa kubwa na muhimu ambazo wananchi wetu wanapaswa kuzitilia maanani katika matukio yote; pale unapohisika uadui na njama za adui watu wote wanapaswa waonyeshe haraka kuguswa na hali hiyo. Hii ni kwa upande wa wananchi.
Kwa upande wa viongozi nchini pia wao wanapaswa kuwa na umoja unaohitajika; wawe kitu kimoja, wawe na ratiba na mipango, watambue kuwa wana jukumu na wakubali kwamba wana jukumu, wasitupiane lawama na wachunge mipaka waliyoainishiwa na katiba. Katiba yetu haina kasoro wala haina upungufu. Mamlaka ya Bunge yanajulikana, mamlaka ya Serikali yanajulikana, mamlaka ya Rais yanajulikana, na mamlaka ya Mahakama yanajulikana; kila moja ana mamlaka na majukumu yake na hivyo kila mmoja atekeleze majukumu yake; nyoyo zao ziwe kitu kimoja, washirikiane pamoja na wawe na kauli za pamoja. ‘Wanaokuwa pamoja nyoyo zao ni bora zaidi ya wanaozungumza lugha moja.'
Alhamdulillah katika suala hili pia sisi hatuna mushkili wowote. Viongozi nchini ni watu wenye uchungu wa nchi. Sisi sote ni binadamu, sisi sote ni watu, tunakosea na tunafanya makosa; lakini makosa yote yanaweza kurekebishwa. Bahati nzuri viongozi ni watu wenye uchungu wa nchi; katika nafasi za juu kabisa za mihimili mitatu ya dola, katika vyombo vikuu vya mihimili ya dola hakuna uhaba wa watu wenye uchungu wa nchi, hakuna uhaba wa watu wenye mapenzi juu ya hatima ya Mfumo wa utawala; wote ni watu wenye uchungu, wote ni watu wenye mapenzi; inshallah wanaifanya kazi ipige hatua mbele, na hivi sasa wamo katika kufanya jitihada hizo.
Nasaha zangu ni hizi: tusisahau kwamba kazi, juhudi, matumaini, subira na kuwa na mipango ni mambo ya lazima kwa ajili ya kupiga hatua harakati hii muhimu. Njia tunayoifuata sisi ni njia muhimu; ni njia inayoweza kubadilisha historia ya dunia; kama ambavyo hivi sasa inabadilisha historia ya eneo; na nyinyi mnaona. Ni nani aliyekuwa akidhani kwamba katika eneo muhimu na nyeti la kaskazini mwa Afrika na Magharibi mwa Asia - sehemu hii ambayo Wazungu wa Ulaya wanapenda kuiita Mashariki ya Kati - yatatokea matukio haya muhimu? Lakini yametokea na wala hayajamalizika. Matukio yanayojiri yana madhara kwa Magharibi na hasa kwa Marekani na ni tishio kwa utawala wa Kizayuni. Huu upayukaji wa viongozi wa utawala wa Kizayuni hauna umuhimu wa kiasi hicho cha kumfanya mtu atake kuutolea jibu. Kiwango fulani wanausema wao na kiwango kingine wanausema baadhi ya Wamagharibi. Kwa sehemu kubwa unasemwa na Wamarekani na wale wanaowafuata; Wazungu wa Ulaya hawana ushawishi sana. Ushirikiano waliotoa Wazungu wa Ulaya kwa Marekani katika kadhia hii si ushirikiano wa kimantiki na busara; wanajifanya wako tayari kuwa wa mbele kufa kwa ajili ya Marekani, wanajifanya mhanga kwa Marekani; wanafanya ujinga. Wananchi wetu hawana kumbukumbu mbaya kwa nchi nyingi za Ulaya. Sisi hatuna kumbukumbu mbaya kwa Ufaransa, kwa Italia wala kwa Uhispania. Ni kweli tuna kumbukumbu mbaya sana kwa Uingereza; tunaiita "Uingereza habithi"; lakini hatusemi hivyo kwa nchi nyingine za Ulaya. Lakini kwa itendo hiki wanachofanya - cha kushirikiana na Marekani - ambacho kwa mtazamo wetu sisi si cha busara hata chembe, wanatafuta uadui na taifa la Iran; wao wenyewe wanajifanya wachukiwe mbele ya macho ya wananchi wa Iran.
Sisi tutavivuka vizuizi hivi. Taifa letu limechangamka zaidi, liko shujaa zaidi na lina uwezo mkubwa zaidi wa kuliwezesha livivuke vizuizi hivi. Kwa muda wa miaka thelathini na tatu sasa tumo katika hali ya kukabiliana na matatizo haya; misuli yetu inazidi kuwa imara zaidi siku baada ya siku, inazidi kuwa na utayarifu mkubwa zaidi na tajiriba na uzoefu tuliopata ni wenye thamani kubwa zaidi. Sisi hatutokwama, nyinyi ndio mnaokwama.
Nyinyi mnajitafutia matatizo kutokana na chuki mnazopalilia ndani ya taifa la Iran. Hawa wanafanya makosa. Taifa la Iran litavivuka vizuizi hivi. Tab'an kwa shuruti zilezile: taifa, wananchi wote wa matabaka mbalimbali, kusimama kwao kidete, uchapaji kazi wao, uthabiti wao, kuwa macho kwao na uelewa wao wa alama za nyakati viwepo pale pale kama ilivyokuwa katika vipindi vyote baada ya Mapinduzi hadi hii leo; viongozi nao watimize wajibu wao; itakapokuwa hivyo bila ya shaka yoyote na kama wanavyotamani wananchi, masuala yote yatapiga hatua mbele na haya matatizo ya uchumi pia yatatatuliwa.
Bila ya shaka suala la msingi hivi sasa ni 'uzalishaji wa taifa'. Dawa kuu na ya msingi ni uzalishaji wa taifa; ni suala lile lile tulilolieleza katika sha'ar ya mwaka huu: uzalishaji wa taifa, kazi na rasilimali za Kiirani. Haya yataondoa ughali, yataongeza uzalishaji, yatazalisha ajira, yatamaliza ukosefu wa kazi, yatawezesha kutumiwa rasilimali za taifa na yataimarisha moyo wa kukinai ndani ya taifa la Iran. Viongozi nchini katika ngazi mbalimbali wanapaswa wajitahidi kadiri ya uwezo wao kulipa umuhimu suala la uzalishaji wa taifa. Tab'an wa kwanza kabisa ninaowahutubu kuhusu hili ni viongozi wa ngazi za juu kabisa nchini; iwe ni katika Bunge au Serikali; lakini katika ngazi zinazofuatia, ngazi za chini na ngazi za mikoani na wao wote pia wanapaswa kulizingatia hili.
Katika mkoa huu, kama ilivyo mikoa mingine, suala la kuzingatiwa na viongozi - iwe ni wawakilishi wa wabunge au wawakilishi wa serikali - liwe ni kutatua matatizo ya wananchi; ambapo kipaumbele cha kwanza kabisa kinapasa kiwe ni hili suala la uzalishaji na utumiaji wa suhula za ndani. Bila ya shaka yoyote katika mkoa huu kutokana na kuwepo maji, kuwepo ardhi yenye rutuba, kuwepo hali nzuri ya maumbile kwa ajili ya kilimo, kuwepo utajiri wa mifugo ambao umeweza kukidhi mahitaji makubwa hata nje ya mkoa huu pia, kuwepo tasnia kubwa kubwa za viwanda ambazo zinaweza kusaidia viwanda vingine vidogo vidogo - katika mkoa huu kuna viwanda vikubwa na vile vidogo vidogo vilivyoko chini ya viwanda hivi vinaweza kupewa umuhimu pia - na kuongeza ajira, uzalishaji, harakati pamoja na uchangamko wa wananchi. Haya ni mambo yanayopasa kufanyiwa bidii kubwa na viongozi wahusika wa mkoa huu. Mazungumzo yamekuwa marefu. Sikupenda kukuwekeni juani kwa muda mrefu kama huu akina kaka na akina dada wapenzi. Bila ya shaka, ya kusema ni mengi. Maneno yangu bado hayajaisha; lakini katika siku chache zijazo nitakuwa mgeni wenu wananchi wapenzi katika sehemu mbalimbali za mkoa huu; maneno mengine niliyonayo nitayasema huko. Katika mikutano na vijana, na mashekhe, na viongozi mbalimbali wa kiutamaduni na kielimu, na Basiji, na matabaka mengine tofauti katika baadhi ya miji, kuna masuala chungu nzima ambayo nafikiri yana faida kukuelezeni, hivyo nitayaeleza. Ni matumaini yangu kuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu atakuteremshieni baraka zake.
Ewe Mola! Tunakuomba kwa jaha ya Muhammad na Aali zake Muhammad uteremshe baraka zako, rehma zako, fadhila zako na afya kwa watu wa mkoa huu. Ewe Mola! Wahifadhi vijana. Ewe Mola! Ikate mikono ya maadui. Ewe Mola! Tunakuomba kwa jaha ya Muhammad na Aali zake Muhammad utupe uthabiti katika kufuata njia inayoridhiwa na wewe na inayoridhiwa na mawalii wako. Wafufue mashahidi wetu wapenzi na roho toharifu ya Imamu wa mashahidi pamoja na mawalii wako.
Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

 
< Nyuma   Mbele >

^