Skip to content

Habari

Habari
Hifadhi

Risala na Barua

Matini
Hifadhi

Kumbukumbu na Simulizi

Kabla ya Mapinduzi
Baada ya Mapinduzi

Sauti na Taswira

Picha
Sauti
Video
Hotuba ya Kiongozi Muadhamu Mbele ya Mabasiji wa Mkoa wa Khorasan Kaskazini Chapa
15/10/2012

Ifuatayo ni hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei aliyotoa katika mkutano na Mabasiji wa Mkoa wa Khorasan Kaskazini, katika uwanja wa Sala wa Imam Khomeini, Bojnurd aliyoitoa Oktoba 15, 2012.

Kwa jina la Allah Mwingi wa rehema Mwenye kurehemu

Na hamdu na sifa zote njema ni za Mwenyezi Mungu Mola wa ulimwengu. Na rehma na amani zimshukie bwana wetu na mtume wetu Abul Qasim al Mustafa Muhammad, na Aali zake wema, watoharifu, wateule, waongofu na wenye kuongoza kuelekea uongofu na walio maasumu na watukufu hususan Baqiyyatullah (Imam Mahdi) katika ardhi.
Hadhara ya mabasiji wapenzi wa mkoa, wenye nyuso zing'arazo za kibasiji na nyoyo zing'arazo zaidi inshallah, zimeitia nuru anga ya kikao chetu cha ikhlasi na upendo. Anga iliyopo ni anga ya umaanawi, upendo, huba na ikhlasi kama zilivyo majimui zote za Basiji na harakati za Basiji.
Programu mbalimbali zilizoandaliwa na kuonyeshwa zilikuwa nzuri sana. Hii programu ya mchezo wa jadi kwa hakika ni afadhali kuliko mambo mengi ya kuiga; ni mchezo wa watemi uliojaa mila na silka za Kiirani na za Kiislamu. Inatupasa tuzikumbuke nukta hizi kila mara, kwamba kile kinachotokana na sisi na kinachohusiana na sisi wenyewe, huwa kimechanganyika na itikadi zetu na imani zetu; amma kile kinachotoka nje, kama tutataka kukipa sura ya kiimani, ya Kiislamu na ya Kiirani itapasa tuyajaze mambo hayo ndani ya kitu hicho. Lakini kile kinachohusiana na sisi wenyewe huwa kimaumbile kina sura ya kidini na kiimani. Hadhara ya "Mikufu ya Waja Wema" ilikuwa programu nzuri sana kwani igizo la hadhara hiyo lilikuja kuonyeshwa hapa. Kasida iliyosomwa na hawa akina kaka wapenzi nayo pia ilikuwa nzuri sana; ilikuwa nzuri maana yake na vile vile usomaji wake ulikuwa mzuri na wa kuvutia. Tab'an mnajua, na mimi ninasisitiza kwamba mnaposema "Ewe sayyidi yangu, ewe bwana wangu" bila shaka anayekusudiwa iwe ni shakhsia takatifu ya Imamu wa Zama (salamullahi alayhi).
Kuna maelezo mengi yametolewa kuielezea Basiji. Yoyote yale tutakayoyaeleza kufafanua kuhusu Basiji na tukataamali na kuzibainisha nukta kwa makini bado hatutokuwa tumetoa maelezo ya ziada; kama ambavyo katika medani ya vitendo pia ikiwa tutafanya mambo mengi zaidi na kwa mtazamo wa kina zaidi kwa namna ilivyo Basiji - ambayo ni moja ya sifa zake maalumu - bado tutakuwa hatujafanya jambo la ziada. Kwa nini? Kwa sababu nchi yetu ina tajiriba nzuri ya ushiriki na kujitokeza kwa Basiji katika medani tofauti; katika kipindi cha Vita vya Kujihami Kutakatifu, kabla yake, baada yake na hadi hii leo; na ufafanuzi wake mnaujua na mumeusikia nyinyi wenyewe, na mimi pia nitauashiria kwa muhtasari. Popote pale na katika medani yoyote ile ambapo ushiriki wa Basiji na harakati ya Basiji imeshuhudiwa, basi tumeweza kupata maendeleo; hii ni tajiriba muhimu. Katika mustakabali, nchi itakuwa na masuala muhimu zaidi - sisemi matatizo muhimu zaidi - yamkini matatizo yatapungua siku baada ya siku, lakini masuala muhimu zaidi yapo na kazi kubwa zaidi za kufanywa pia zipo. Sisi tukiwa ni taifa hatutaki kujiwekea uzio wa kutuzunguka; tab'an kama tutafanya hivyo pia upigaji hatua mbele hautosita; lakini mtazamo wetu ni mtazamo mpana; mtazamo huu ni mpana kwa mtazamo wa historia na katika upeo wa ulimwengu. Taifa lenye malengo makubwa kama haya, lenye hima na bidii kubwa kama hii, lenye uoni wenye upeo wa mbali kama huu lina mambo mengi sana ya kufanya katika mustakabali. Masuala haya yanahitaji sifa mbalimbali ambazo zinapatikana kwenye majimui ya Basiji. Kwa hivyo yoyote yatakayosemwa kuhusu Basiji, yakachunguzwa kwa umakini zaidi na kutiliwa mkazo zaidi bado halijafanyika jambo kubwa na la ziada.
Kwanza kabisa ni kwamba Basiji imezaliwa sambamba na Mapinduzi. Pengine kwa maana nyengine inaweza kusemwa kuwa kujitokeza kwa sura ya kibasiji (kujitolea) kwa wananchi ndiko kulikopelekea Mapinduzi kupata ushindi au kufanyika kwa Mapinduzi. Vijana wa kujitolea na wenye shauku, waliokuwepo kila mahala kabla ya Mapinduzi - mimi ninazo taarifa kuhusu hata mji huu wa Bojnurd - walijitokeza katika nyuga mbalimbali, walisimama kidete na walitoa mchango uliokuwa na taathira. Jitihada hizi ziliunganishwa pamoja katika nchi nzima na kuwa harakati adhimu ya Mapinduzi ya wananchi wa Iran. Kwa hivyo kwa tafsiri na maana hii, kuzaliwa kwa Basiji kulikuwa kabla ya kuzaliwa Mapinduzi; lakini baada ya ushindi wa Mapinduzi, Basiji ikazaliwa katika muundo wa sasa ambao ni wa kuwa na sifa za kipekee na za kustaajabisha ambazo nitazielezea. Kwa hivyo Basiji inaweza kuelezewa kuwa mzaliwa wa pamoja na Mapinduzi.
Kwa hivyo Basiji hii ni kitu kisicho na mfano. Lakini (tujiulize) kwani mataifa mengine, mapinduzi mengine hayakushirikisha wananchi hata unasema uwepo wa Basiji ni kitu kisicho na mfano? Kwa nini; katika mapinduzi mengine na katika matukio makubwa yaliyojiri katika nchi nyengine duniani, umma wa wananchi ulijitokeza kwenye medani; lakini kuna tofauti kubwa kati ya mapinduzi hayo na yetu kwa upande wa taathira ya kujitokeza huko. Kama mtaiangalia historia mtaona kuna mapinduzi mawili yenye umaarufu kama wa mapinduzi yetu duniani yaliyotokea katika karne mbili tatu za hivi karibuni; moja ni Mapinduzi Makubwa ya Ufaransa, na mengine ni mapinduzi ya kikomunisti ya Urusi. Katika mapinduzi yote hayo mawili wananchi walikuwepo, lakini kushiriki kwa wananchi katika mapinduzi hayo - ambako kulikuwa kwa kiwango kikubwa na cha juu pia - ni tofauti na kulivyokuwa kushiriki kwa kujitolea wananchi katika mapinduzi yetu. Nitazungumzia kidogo hapa kuhusu sifa hizo za kushiriki kwa sura ya kujitolea (kibasiji).
Kwanza ni kwamba tokea hapo mwanzo majimui hii ya umma ya wananchi ilikuwa na sura ya kujipanga; hii ni sifa moja ya kipekee. Kujipanga huko kulisaidia kuifanya harakati hii adhimu ya wananchi isipoteze dira na njia yake. Unapokuwapo uratibu na kujipanga maana yake ni kuwapo dira ya muongozo, kuwapo basirat na uoni wa mbali, kuwapo mhimili mkuu wa upitishaji maamuzi, kuwapo irada ya wananchi; lakini pia unazuia misimamo ya kufurutu mpaka, kufuata njia pogo na kufanya makosa ya kutisha. Lakini muhimu zaidi ya hayo ilikuwa ni sifa ya imani na kujitokeza kutokana na kuhisi kuwa huo ulikuwa wajibu wa kidini. Kuna wakati hisia tupu za hamasa humuelekeza mtu, majimui ya watu na umma wa watu kufuata njia ya upande fulani; hili ni jambo linalowezekana na linatokea katika mahala mwingi. Mtu anayefanya jambo kwa hisia za hamasa, muongozo wake, hatamu za udhibiti wa nafsi yake na harakati yake huwa haiongozwi na wenzo wa kimaanawi, wa moyoni na wa ndani ya nafsi; na mara nyingi hufanya mambo kwa kupindukia mpaka; pale ambapo haipasi kuchukua hatua ya kuua yeye huua; pale ambapo haipasi kufanya dhulma yeye hudhulumu. Kwa hivyo mkiangalia mtaona katika haya mapinduzi niliyoyataja, mambo yaliyonakiliwa na historia - historia yao wenyewe, si kwamba hayo tunayasema sisi - yamefurika na kujaa makosa, uendaji upogo na makabiliano ya aina hii; ambapo kundi moja lilikabiliana na kupambana na kundi jengine. Ni sawa kwamba mtu muumini pia ana hisia za hamasa; sisi hatupigi hatua bila ya hisia za hamasa; tunazo hisia za hamasa, tunazo hisia za upendo na tunazo hisia za hasira; lakini hisia hizi zinadhibitiwa na imani zetu. Kijana Basiji anapokabiliana na watu wanafiki, kwa sababu mnafiki huyo anakuwa ni mwanamke na hivyo si maharimu yake huwa tayari hata kupoteza maisha yake ili tu asije akaushika mwili wa mwanamke huyo anayeshukiwa. Mambo kama haya yapo; haya ni miongoni mwa matukio ambayo yametokea mara kadha wa kadha. Tahadhari kubwa inayochukuliwa na Basiji katika kumnasa mnafiki imetokea katika kesi nyingi. Katika baadhi ya kesi hizo, huwa mtu huyo mathalani ni mwanamke; katika hali hiyo huyu kijana Basiji huwa hayuko tayari kuchupa mipaka ya kidini. Mnaona! huku kunaonyesha kujitokeza kwa msingi wa imani kwa mtu huyu Basiji; hili ni jambo muhimu sana. Na naam kuna wakati hali husababisha kufa shahidi mabasiji kadhaa; lakini tunapoliangalia hilo kwa mtazamo wa kiujumla hali hiyo inatupa maana yenye umuhimu mkubwa na utukufu wa hali ya juu. Kwa hivyo harakati ya umma, ya wananchi na iliyojipanga na kuratibiwa inapiga hatua mbele kwa muongozo wa imani na kuchangiwa na imani; hizi ni miongoni mwa sifa za Basiji.
Sifa nyengine ni kwamba matabaka yote ya watu yanashiriki katika Basiji; watu wa mijini wapo, watu wa vijijini wapo, vijana chipukizi wapo na wazee waliokula chumvi pia wapo. Mara chungu nzima wakati wa vita redio za nje na wafanya propaganda wenye inadi na uadui walikuwa wakisema Jamhuri ya Kiislamu inawapeleka vitani watoto ambao hawajabaleghe. Ni kweli vijana ambao hawajabaleghe walikuwa wakienda, lakini hakuna mtu aliyekuwa akiwapeleka. Wao waliweza kufika kwenye medani za vita kwa kuja na vilio na kwikwi, kadi za vitambulisho mikononi mwao, barua za ridhaa kutoka kwa wazazi wao walizozipata kwa kuangua vilio, na kwa kuchanganyika na wapiganaji wengine. Huu ndio ukweli wa mambo. Kizee kwa kijana, msomi na yule ambaye hakusoma wote hao wamo katika Basiji. Hapa wale wasomi wanafikra hawakubakia kando. Katika baadhi ya mijumuiko hii mikubwa inayokuwapo katika mapinduzi makubwa kundi la wasomi wanafikra huwa halichanganyiki na watu. Kuna wakati niliwahi kunukuu kutoka kwenye igizo moja la tamthilia ya wasomi wanafikra ambapo bwana mmoja alikuwa anaangalia harakati za wananchi kutokea juu kwenye roshani, lakini yeye mwenyewe hakuingia humo wala hakuchanganyika nao. Lakini hapa haikuwa hivyo; hapa kibarua alikuwapo, mkulima alikuwapo, mwanafunzi wa chuo kikuu alikuwapo, mwanafunzi wa shule alikuwapo, tabibu alikuwapo, mwandishi maarufu alikuwapo, mshairi malenga alikuwapo, mtaalamu bingwa alikuwapo na mbunifu pia alikuwapo na yupo; wote wameingia katika Basiji. Nyinyi nendeni mkaangalie taasisi ya Basiji, angalieni hata katika mji wenu; kila mahala hali iko hivyo hivyo. Jana hapa alikuja kijana mmoja mvumbuzi akajitambulisha kuwa yeye ni mmoja wa wavumbuzi mabasiji. Mambo haya hayana mfano wake duniani. Wavumbuzi mabasiji, wahadhiri wa vyuo vikuu mabasiji, waandishi mabasiji na washairi mabasiji. Makundi ya wasomi wanafikra wa tasnia tofauti yamo katika majimui hii adhimu, yenye siri kubwa ambayo sisi tumeipa jina la "Basiji". Kijana yumo, mzee yumo, mwanamke yumo, mwanamme yumo, mtaalamu wa kazi za viwanda na ufundi yumo na mtaalamu wa masuala ya kinafsi na kisaikolojia pia yumo; aina zote za watu zimo katika majimui hii.
Sifa nyengine ni ya kuendelea kuwapo kilingeni. Ndugu zanguni wapenzi! Miaka thelathini na tatu ya Mapinduzi imepita. Kuendelea kuwepo umma wa wananchi katika mapinduzi mbalimbali lilikuwa suala la mwezi mmoja, miezi miwili au sana sana mwaka mmoja; kisha kukamalizika. Hapa pia, wale watu waliokuwa wakitaka kupanga na kuongoza ratiba ya maisha na ya Jamhuri ya Kiislamu kwa kufuata maelekezo ya Magharibi, nao pia walikuwa wakitoa ushauri huohuo. Mwanzoni mwa baada ya Mapinduzi walikuwa wakishauri kwa kusema, sawa, sasa Mapinduzi yametimia, watu waende zao majumbani kwao. Katika mapinduzi mengine watu walikwenda zao majumbani kwao; lakini hapa baada ya kupita miaka thelathini na tatu tokea Mapinduzi Basiji ingaliko katika medani, ingalipo uwanjani na ingalipo kilingeni. Kile kizazi ambacho wakati ule kiliingia kwenye Basiji leo kimekuwa cha watu wa rika la makamo na wa umri wa uzee, ndevu zao zimeshakuwa na mvi; wameshajukuu, wameshawapa waume binti zao, wameshawapa wake vijana wao wa kiume lakini wangali ni mabasiji. Wao wamezeeka, lakini je sura yao ya Basiji imezeeka pia, la, abadani. Sura ya Basiji ni sura kijana. Nini maana yake? Maana yake ni kwamba vizazi vipya vinavyochomoza na kufuatana moja baada ya kingine havijapoteza sura hii ya ushiriki wa wananchi na wala havijaisahau. Wakati ule baadhi ya watu walikuwa wakisema 'hawana ni vjana, ni watu wa hamasa na mori na vita ni tukio la hamasa na mori, ni hili ndilo linalowapeleka vitani, ni kwa sababu ya hamasa.' Lakini leo hakuna vita, leo hakuna mori na hamasa ya vita; kwa nini kijana anajitokeza katika medani? Haya ni masuala yanayohusiana na Basiji. Tazameni, hizi ni nukta makini kabisa ambazo wakati tunapozikusanya na kuziweka pamoja tunafikia natija kwamba Basiji ni kitu cha kustaajabisha, chenye siri kubwa na hali ya kipekee katika Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu. Majimui hii imeweza kufungua mafundo mengi, imeshiriki katika medani nyingi na imekuwa na taathira na nafasi kubwa kabisa. Kwa maana hiyo katika mustakabali pia tutauhitajia ushiriki na uhudhuriaji huu. Watu wenye kutaamali na kutadabari na wajiulize kwa nini katika sha'ar za upinzani za watu ambao maneno yao, pumzi zao na harakati zao zinapata ilhamu kutoka redio ya Israel, Basiji ndiyo ya kwanza kabisa inayolengwa na sha'ar hizo? Wao wenyewe wanafahamu kwa nini wanatoa sha'ar dhidi ya Basiji au hawafahamu? Mimi siwezi kuhukumu juu ya jambo hili. Lakini huu ndio uhakika wa mambo. Ufunguo huu wa dhahabu wa utatuzi wa matatizo mengi ya mustakabali unafanyiwa bughudha na uadui na watu ambao hawataki mustakabali wa Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu uwe mustakabali mzuri, wa heshima na wa mafanikio; kwa hivyo wanataka kuuvunja ufunguo huu wa dhahabu; au kwa uchache kuudunisha mbele ya macho yangu mimi na nyinyi. Lakini bila ya shaka ni wazi kwamba hawatoweza. Kwa hivyo haya ni kuhusu sifa za Basiji. Kuna maneno mengi ya kusema juu ya suala hili. Nimesema kwamba kadiri tutakavyofanya umakini wa kina na upembuzi wa nukta, kisha tukataamali juu ya nukta hizi na kuzichambua kwa upana zaidi na kuzifanya kuwa fikra na utamaduni wa jamii hatutokuwa tumefanya jambo la ziada. Kufanya mazingatio ya kina juu ya Basiji - kitu hiki cha ajabu ambacho Mwenyezi Mungu Mtukufu ameitunukia Jamhuri ya Kiislamu - ni suala muhimu.
Nyinyi ni miongoni mwa Basiji. Watu wote wanapaswa kujivunia kuwamo katika majimui ya Basiji. Mtu anayeingia kwenye majimui hii huwa ana sifa zinazomstahikisha kuwa hivyo; huwa ameonyesha kuwa na sifa hizo na kwa hizo akaingia katika Basiji; kwa hivyo mnapaswa kuzilinda sifa hizo. Ninachotaka kukuambieni nyinyi - ambao ni watoto wangu, ni vijana wangu - ni kwamba inapasa kuzilinda sifa hizi; na sio mzilinde tu bali pia mziimarishe.
Moja ya sifa nyingine ni kujijenga nafsi. Sisi tunapaswa kuzilea nafsi zetu. Mimi mzee niliyekula chumvi pia ninahitaji kuilea nafsi yangu, kujidhibiti nafsi yangu na kuilinda nafsi yangu. Amma harakati kwa upande wa kijana huwa za kasi zaidi, upitishaji uamuzi huwa wa kasi zaidi na uchukuaji hatua huwa wa haraka zaidi; kwa hivyo kujichunga, kujilinda na kujijenga nafsi yake pia huwa nyeti zaidi. Kujijenga nafsi ni kazi nyepesi na pia isiyowezekana; na vilevile ni rahisi na pia ni ngumu. Kama tutakuwa katika mazingira mwafaka na maridhawa litakuwa jambo rahisi. Kwa mfano nyinyi ni watu wa kumuelekea Mwenyezi Mungu, ni watu wa dua, ni watu wa kunyenyekea na watu wa kulia. Kuna wakati mtu anakuwa katika mazingira ambayo ni ya kunyenyekea, kulia na kumuelekea Mwenyezi Mungu; nyoyo zote huwa zimemuelekea Mwenyezi Mungu, machozi yote yanabubujika; hapo hali ya unyenyekevu huifanya kazi ya mtu iwe nyepesi. Haya ni mazingira mwafaka. Mazingira mwafaka huifanya kazi ya kujijenga nafsi iwe nyepesi. Moja ya mazingira mwafaka yalikuwa ni ya majimui ya hali za kipindi cha Kujihami Kutakatifu; lakini mazingira mwafaka zaidi ni Basiji yenyewe. Nyinyi ambao mko katika majimui hii, kwa kweli mko katika anga mwafaka kwa ajili ya kujijenga nafsi. UchaMungu, subira, kujiweka mbali na madhambi, kutekeleza mambo ya faradhi, kusali kwa sura ya fursa ya kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu, kuzingatia maana halisi ya Sala, mahudhurio ya moyo, kuwa na umakini ndani ya Sala; yote hayo ni nyenzo za kujijenga nafsi. Wakati mnapokuwa katika mazingira mwafaka nyenzo hizi za kujijengea nafsi huweza kukusaidieni zaidi na kwa ufanisi mkubwa zaidi. Wakati inapokuwa hivyo uwezo wenu wa kiroho unakuwa mkubwa zaidi; na pia istiqama yenu, kusimama kwenu imara, subira yenu, kutawakali kwenu na vilevile ubunifu na vipawa vyenu vya ndani; yote hayo kwa pamoja. Tunapokuwa hatujaingia katika medani fulani huwa tunahisi hofu, huwa tuna woga; na hata kama tutakuwa na kipawa na uwezo fulani hubaki kuwa umefichika; lakini mnapoondoa woga huo, mkajusuru kukabili hatari na kujitosa kwenye medani, vipawa hivi navyo huanza kuchanua; na namna hivi huwezekana yale yasiyowezekana. Kama alivyosema sasa hivi hapa kamanda Naqdi, kijana moja mwanachuo mwenye umri mdogo, akiandamana na majimui fulani ya watu ambayo mwenyewe ameipa jina la brigedi - brigedi ni watu mia moja?! Watu mia moja na hamsini ndio brigedi moja?! Yeye mwenyewe anaiita brigedi! - anaelekea magharibi au kusini mwa nchi pamoja na brigedi hii ya watu waumini na wenye ikhlasi kwenda kupigana vita na upande wa adui uliojizatiti kwa vikosi vya deraya na kamanda mwenye uzoefu mkubwa. Yeye hana zana zozote ghairi ya zana duni, lakini yule yeye amejizatiti kwa zana za kisasa; huyu yeye hana tajiriba na uzoefu wa ukamanda lakini yule yeye amekuwa kamanda umri wake wote. Pande mbili zinakabiliana, na upande huu unashinda; unaviteka vifaru vya upande ule, unaziteka zana za upande ule na kurudi na ushindi. Haya yanapatikana kwa kujijenga nafsi. Pasi na kujijenga nafsi huwa haiwezekani kujitosa kwenye medani hizi.
Baadhi ya watu walikuwa wanaogopa. Baadhi ya watu walikuwa wakijikatia tokea mwanzo kwamba haiwezekani - walikuwa wakisema hasa haiwezekani - na walikuwa wakipinga kila mahala alipojitokeza Basiji. Katika zama zetu zile mimi nilikuwa nikiwaona watu waumini waliokuwa na sifa kamili za kuongoza jeshi rasmi lenye nidhamu ambao walikuwa wakiafiki wazo la kuandamana na kuwa pamoja na majimui ya Basiji; hili nililiona mimi mwenyewe mara kadha wa kadha katika kipindi cha vita; katika kambi ya Abu Dhar, kusini, na kaskazini magharibi. Kamanda mwenyewe wa jeshi alikuwa akishikilia kwamba majimui ya Basiji iandamane na yeye; alikuwa akipenda iwe hivyo na akiliafiki wazo hilo; kule Tehran baadhi ya watu walikuwa wamekaa wakilalamika kwamba vipi bwana! kwa nini wameingia? Kwa nini wamekwenda bila ya ruhusa? Kwa nini wamechukua hatua fulani? Walikuwa wanachukia kuwepo Basiji. Kwa kuwa hawakuwa na matumaini, kwa kuwa walikuwa wamekata tamaa walikuwa wakisema haiwezekani kufanya chochote; lakini wakati walipoingia walikuona kuingia huko kuwa kunaleta matumaini; kunapelekea kuchanua kwa vipawa.
Kushiriki kwa Basiji mwenyewe katika uwanja wa mapambano kunamtia nuru. Ulikuwa msemo maarufu kwa watu katika kipindi cha vita vya Kujihami Kutakatifu kusema fulani anang'ara kwa nuru, ikiwa na maana kwamba karibuni hivi atakufa shahidi. Nuru hiyo ilitokana na ushiriki wa Basiji; na hili nililishuhudia mimi kwa macho yangu; si mara moja si mara mbili. Si vibaya nikiielezea kesi moja ambayo inahusiana na huu mkoa wenu. Meja mmoja wa jeshi ambaye tulikuja kufahamu baadaye kuwa ni mtu wa Ashkhaneh - Meja Rostami - aliamua kwa hiyari yake mwenyewe kuwa Basiji akaenda kujiunga na majimui ya kundi la shahidi Chamran. Nilikuwa nikumwona akifanya safari za kwenda na kurudi mara kwa mara. Usiku mmoja tulikuwa tumekaa na marehemu Chamran tukawa tunazungumzia masuala ya vitani na kazi ambazo ilikuwa tuzifanye kesho yake; mara mlango ukafunguliwa akaingia yeye shahidi Rostami. Siku kadhaa zilikuwa zimepita nikiwa sijamwona. Nikamwona ametapakaa tope mwili mzima; mabuti yalikuwa yamejaa tope, mwili wake ulikuwa umetapakaa tope, sura yake iliyokuwa na ndevu ndefu ilionyesha amechoka, lakini nilipomwangalia usoni nilimwona anang'ara mithili ya mwezi; alikuwa aking'ara kwa nuru. Siku za kabla yake sikuwahi kumwona yeye katika katika hali ile. Alikuwa amekwenda katika eneo moja ya operesheni ya shambulio na alikuwa na kazi nyingi huko; wakati huo alikuwa amerudi akitaka kutoa ripoti. Muda si mrefu baada ya siku hiyo alikufa shahidi. Alikuwa mwanajeshi lakini aliamua kujiunga na Basiji; akiendesha harakati, akifanya juhudi na idili na alishiriki kwa moyo wa kujitolea mhanga katika majimui hiyo ya Basiji ya shahidi Chamran na baadaye akafa shahidi. Hali hii ya nuru waliiona watu wengi; sisi pia tuliiona na wengine pia waliiona zaidi yetu sisi. Hali hii inatokana na mahudhurio hayo ya namna ya kipekee. Kuna suala moja pia katika Basiji nalo ni suala la 'Ithar' yaani moyo wa kusabilia kila kitu. Kujitolea kwa kusabilia kila kitu kilugha ni kinyume na "Isti'thar' yaani moyo wa kutaka kila kitu. Isti'thar maana yake ni sisi kutaka kila kitu kilichopo kiwe ni kwa ajili yetu. Baadhi ya wakati katika dua za Maimamu (Aalayhimu ssalam) wamekaripiwa 'must'athirin'. Must'athirin maana yake ni watu ambao hutaka kila kilichopo kiwe chao wao; wanajali manufaa yao binafsi na kunyang'anya walivyonavyo wengine. Ithar ni kinyume na hivi; yaani kujitolea kwa kusabilia na kusamehe fungu lako na kusamehe haki yako kwa ajili ya wengine na kufumbia macho haki yako kwa manufaa ya wengine. Sifa hii imekuwepo kwenye vilele vya juu kabisa vya Basiji. Na mimi napenda nikuelezeni nyinyi vijana wapenzi; jitahidini kuimarisha sifa hii ndani ya nafsi zenu. Sisi wanadamu huwa daima tunakabiliwa na hatari ya kuteleza katika mwendo wetu. Vitu vyenye mvuto hutaka kutuvutia na kututeka upande wake. Tunashughulika kufanikisha maslahi yetu binafsi. Maslahi ya binafsi yanatuvuta. Baadhi ya wakati tunakuwa tayari kukanyaga haki za wengine kwa sababu ya manufaa ya nafsi zetu. Inabidi tuzichunge nafsi zetu. Kuijenga nafsi kibasiji, moja ya sifa zake ni huku kuimarisha moyo huu ndani ya nafsi na kuikuza nafsi ili iwe na moyo wa kujitolea na kusabilia kila kitu. Vile vilele vya Basiji nilivyovieleza ni wale watu waliozitoa mhanga roho zao wakaenda vitani kupigana kwa ajili ya kuulinda Uislamu, kwa ajili ya kuyalinda Mapinduzi, kwa ajili ya kumlinda Imamu (Khomeini), kwa ajili ya kuilinda nchi na kwa ajili ya kuilinda mipaka ya nchi. Kuna kujitolea kukubwa zaidi ya huku? Kwa kiwango cha juu zaidi ya hiki? Hiki ndicho kilele cha 'ithar' (kujitolea kwa kusabilia kila kitu).
Kiwango cha chini ya hiki ni kufumbia macho na kusamehe yale tunayoyaelezea sisi wenyewe kuwa ni manufaa na maslahi yetu ya kimaada ya muda mfupi. Tujitahidi kusamehe na kufumbia macho maslahi yetu ya binafsi kwa ajili ya maslahi ya umma, kwa ajili ya maslahi ya Uislamu, na kwa ajili ya maslahi aali na matukufu. Hii maana yake si kuipa mgongo dunia; hapana. Dunia ni mahala pa juhudi na harakati; kwa ajili ya maisha ya mtu binafsi na pia kwa ajili ya maisha ya jamii; kwa ajili ya mambo ya kimaada na pia kwa ajili ya mambo ya kimaanawi; lakini pale tunapoona kuwa ili kupata haki ya binafsi inabidi tukiuke haki za wengine, tukiuke sheria na tukiuke insafu hapo inabidi tushike hatamu za udhibiti wa nafsi zetu na kuamua kusamehe na kufumbia macho kwa ajili ya manufaa na maslahi ya wengine kile ambacho tunaweza kukipata kwa ajili ya manufaa na maslahi yetu; na hiyo itakuwa ni 'ithar' (kujitolea kwa kusabilia kila kitu).
Bila ya shaka moja ya masuala muhimu ni suala la basirat (uoni wa mbali). Ninachotaka kukuelezeni ni kwamba kuwa na uoni wa mbali katika zama hizi na katika zama zote maana yake ni nyinyi kuelewa ulipo mstari wa mpambano na adui; ni wapi pa kupambana na adui? Baadhi ya watu wanafanya makosa katika kufahamu nukta ya mpambano; hufyatua guruneti na makombora yao ya mizinga kuelekea nukta pasipo na adui, bali ni mahali alipo rafiki. Baadhi ya watu huwachukulia washindani wao katika uchaguzi kuwa ni "Shetani Mkubwa"! Shetani Mkubwa ni Marekani, Shetani Mkubwa ni Uzayuni; mshindani wa kimrengo si Shetani Mkubwa, mshindani katika uchaguzi si Shetani Mkubwa. Mimi namuunga mkono Zaid, wewe unamuunga mkono Amru; sasa mimi nikuone wewe Shetani Mubwa? Kwa nini? Kwa mnasaba gani? hali ya kuwa Zaid na Amru wote wawili wanadai kuwa wako kwa ajili ya Mapinduzi na Uislamu, wako kwa ajili ya kuutumikia Uislamu na kuyatumikia Mapinduzi. Tuainishe wazi mstari wa mpambano na adui. Baadhi ya wakati hutokea mtu aliyevaa vazi letu sisi lakini ulimi wake unakariri maneno ya adui! Huyo inabidi apewe nasaha; kama hakubadilika kwa nasaha inabidi mtu aainishe mstari wa mpaka kati yake na yeye: mstari wa kutengana. Kama wewe utataka kusimama na kutamka maneno dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu kwa hisia zilezile ulizonazo utawala wa Kizayuni kuhusiana na Jamhuri ya Kiislamu hata kama utatumia misamiati mingine, utakuwa na tofauti gani na utawala wa Kizayuni? Ikiwa utataka kuamiliana na Jamhuri ya Kiislamu kwa kutumia mantiki ileile inayotumia Marekani kukabiliana na Jamhuri ya Kiislamu, hutokuwa na tofauti yoyote na Marekani. Kwa hivyo hili ni suala jengine. Lakini kuna wakati huwa si hivyo. Inawezekana zikawepo hitilafu, tena hitilafu zenyewe zikawa za kina, zikawa ni hitilafu kubwa lakini mtu asifanye makosa katika kumpambanua adui na asiyekuwa adui; adui ana hesabu nyengine na asiyekuwa adui ana hesabu nyengine. Inabidi uainishwe mstari wa mpambano na adui, uwekwe wazi; na hili linahitajia uoni wa mbali. Na hii ndiyo basirat tunayoizungumzia.
Kundi moja linajitokeza upande ule na kundi jengine linajitokeza upande huu. Kundi moja linaamiliana kirafiki hata na adui pia, linashindwa kuelewa sauti ya kelele za adui kwa kuwa inatokea kwenye koo nyengine. Kundi jengine katika upande huu linamchukulia kila mtu mwenye hitilafu ndogo tu za kiutashi na wao kuwa ni adui! Basirat ni ule mstari wa kati kati; ule mstari sahihi.
Nimetaja kuhusu mshindani wa uchaguzi. Uchaguzi uko mbele yetu, bila ya shaka hauko karibu hivyo. Baadhi ya watu wameshaanza tokea sasa kujitosa kwenye masuala ya uchaguzi. Si sawa, sisi hatuungi mkono kufanya hivyo asilani. Kila kitu kina wakati wake na mahala pake. Lakini ninachotaka kueleza kuhusu uchaguzi ambacho ndio kilichomo katika fikra zetu, matakwa yetu na matarajio yetu ni haya mambo kadhaa: la kwanza ni kwamba kushiriki kwa wananchi katika uchaguzi kuwe kushiriki kwenye adhama; hii ni kinga kwa uchaguzi. Juhudi za watendaji wote wa leo, kesho, siku ya uchaguzi wenyewe na katika kipindi cha utangulizi na uhitimishaji wa uchaguzi zinapasa ziwe ni za kutaka kuhakikisha mahudhurio ya wananchi yanakuwa mahudhurio makubwa.
Jengine ni kwamba tumwombe Mwenyezi Mungu na sisi wenyewe tufumbue macho yetu kuhakikisha kuwa matokeo ya uchaguzi yanatokana na kufanya chaguo zuri litakalokuwa na maslahi na faida kwa Mapinduzi na nchi. Hii haina maana kwamba kama tutakuwa hatujampenda mtu basi tuamiliane naye vibaya, kwa ukali na kwa njia isiyo sahihi; isiwe hivyo. Wale watu ambao wenyewe wanajihisi ni watu wazuri na wana sifa zinazostahiki, wajitose uwanjani. Na sisi tunaotaka kuchagua tuangalie na kuhakikisha tunawalinganisha wagombea kulingana na vipimo tunavyoviamini na vinavyokubalika kwetu sote. Inaweza kusemwa kwamba vipimo hivyo vinakubalika takribani mbele ya Wairan wote wanaoyakubali Mapinduzi. Yeyote yule tutakayemwona ana sifa na vipimo hivyo, tujitahidi, tufanye hima na tufanye kampeni kwa namna sahihi ili muelekeo wa uchaguzi ufuate njia ya kuwezesha kuchaguliwa mtu huyo.
Nukta ya tatu ya msingi - na kwa leo nitakomea kwenye nukta hiyo; tab'an hapo baadaye yamkini nitakuja kuwa na mengi ya kusema kuhusu uchaguzi - ni kwamba uchaguzi katika nchi yetu ni jambo la kutuletea heshima na fahari. Watu wote wajihadhari uchaguzi usije ukawa sababu ya kupotea heshima ya nchi; kama ilivyokuwa katika mwaka 88 (2009) ambapo baadhi ya watu walitaka kuufanya uchaguzi uonekane kuwa dhihirisho la hitilafu na kubadilisha makelele ya kawaida ya kisiasa ya uchaguzi kuwa fitina kubwa; lakini tab'an wananchi wa Iran walisimama kukabiliana na fitina hiyo, na wakati wowote ule itakapotokea hali itakayofanana na hiyo wananchi watasimama kidete kukabiliana nayo.
Bila ya shaka uchaguzi kuwa safi ni suala muhimu na la msingi. Hata hivyo tunavyochukulia sisi ni kwamba viongozi husika nchini wanasimamia suala hilo kwa dhamiri ya Kiislamu na ya kidini na kwa hivyo uchaguzi wetu ni safi.
Huko nyuma pia ambapo uchaguzi umefanyika katika serikali tofauti - iwe ni uchaguzi wa rais, uchaguzi wa bunge au chaguzi nyenginezo - sisi tumekuwa tukichukulia kuwa uchaguzi ni safi, huru na wa haki. Tab'an kuna ulazima wa kuchukuliwa tahadhari mbalimbali na za pande tofauti. Tunamwomba Mwenyezi Mungu Mtukufu aujaalie mtihani huu pia uwe na baraka kwa taifa letu azizi.
Ewe Mola! Wateremshie rehma na fadhila zako vijana hawa azizi. Ewe Mola! Mhimili imara wa Mfumo, yaani Basiji ujaalie kuwa imara zaidi siku baada ya siku. Zijaalie kuwa na thamani dhikri zetu, utajo wetu na unyenyekevu wa nyoyo zetu Kwako. Ewe Mola! Yajaalie mauti yetu yawe ni kwa ajili Yako na katika njia Yako. Ewe Mola! Ujaalie moyo mtakatifu wa Imamu wa Zama uwe radhi nasi. Zijaalie roho toharifu za mashahidi na roho ya Imamu wa mashahidi (Khomeini) ziwe radhi nasi.
Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

 
< Nyuma   Mbele >

^