Skip to content

Habari

Habari
Hifadhi

Risala na Barua

Matini
Hifadhi

Kumbukumbu na Simulizi

Kabla ya Mapinduzi
Baada ya Mapinduzi

Sauti na Taswira

Picha
Sauti
Video
Hotuba ya Kiongozi Muadhamu Katika Hadhara ya Wananchi wa Esfarayen Chapa
13/10/2012

Ifuatayo ni matini kamili ya hotuba ya Ayatullah Udhma, Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aliyoitoa mbele ya hadhara kubwa ya wananchi wa Esfarayen tarehe 13/10/2012.

Bismillahir Rahmanir Rahim

Hamdu zote zinamstahikia Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wa viumbe pia. Na rehma na amani zimfikie Bwana wetu na Mtume wetu Mtukufu Abul Qassim Muhammad SAW pamoja na Aali zake wema na watoharifu, wateule, maasumina na waongozaji hususan Baqiyatullah katika ardhi (Imam Mahdi roho zetu ziwe fidia kwake).
Kwa hakika nina furaha kubwa mno kutokana na kupata tawfiki katika safari yangu hii ya kukutana na nyinyi wananchi wapendwa wa mji mkongwe wa Esfarayen. Jambo la msingi ni kukutana na nyinyi wananchi na kuonyesha mapenzi maalumu na ikhalsi sambamba na kukushukuruni kutokana na mahudhurio yenu yenye hamasa kubwa na nishati ya hali ya juu katika kipindi chote hiki cha mapinduzi ya Kiislamu. Tab'an, katika safari hii tunapaswa kwa uwezo na tawfiki ya Allah kufanya hima na idili ili tuweze kuyapatia ufumbuzi baadhi ya matatizo ya kimsingi ya eneo hili kwa hima ya viongozi na maafisa wa serikali. Bila shaka matatizo yapo; lakini kwa uwezo na tawfiki ya Mwenyezi Mungu irada na azma ya kuyapatia ufumbuzi matatizo hayo nayo ipo; na vile vile tunamshukuru Allah kwani uwezo wa kupiga hatua kimaendeleo na azma ya kupatia ufumbuzi matatizo hayo nayo ipo.
Kile ambacho ni kitu kizuri na ambacho kiko katika fikra na akili zetu hususan katika fikra na akili za vijana azizi kuhusiana na mji huu wa kihistoria ni mkongwe ni hiki kwamba, mji huu umekuwa ni kituo cha shakhsia mbalimbali na wakubwa wa kielimu, kiutamaduni na kisiasa katika kipindi chote cha historia. Katika kipindi chote cha historia, walichomoza wanafasihi, malenga (washairi), mafakihi na wanafikra wakubwa na watajika kutoka katika mji huu na kulifanya jina la Esfarayen kukaririwa katika vinywa vya shakhsia wakubwa wa kihistoria.
Hii leo pia mji wa Esfarayen kwa kuwa na mazingira mazuri ya kitabia na kijiografia pamoja na vipaji vya watu unaweza kuwa kituo cha shakhsia wakubwa na wanafikra ambao nchi itajifakharisha nao na mustakabali wa nchi uwe katika tadbiri, fikra na mitazamo yao. Nyinyi vijana wapendwa wa mji huu - vijana kwa mabinti - kila mahala na katika kila sekta ambayo mtakuwa mnafanya kazi au mnasoma, mnapaswa kuutazama mustakbali na muwe na matumaini nao na muuone mustakbali wa mji huu kwamba, unawezekana na uko wazi kutokana na kuweko akiba hii kibinaadamu sambamba na hii turathi kongwe.
Wananchi wa mji wa Esfarayen wameondokea kupata umashuhuri kwa kuwa ni wema na wenye ufahamu. Hii leo mji huu una fakhari nyingine nayo ni kuwa ni kituo cha malezi na utoaji wasomi wa Qur'ani Tukufu. Vikao vya Qur'ani Tukufu, mafunzo ya Qur'ani Tukufu na uenezaji wa fikra za Ki-qur'ani kwa baraka za vikao vya Qur'ani vya mji huu ni jambo ambalo limepelekea wananchi wa mji huu walipe jina eneo hili kuwa ni Darul Qur'ani; hii nayo bila shaka ni fakhari kubwa. Tab'an, Esfarayen ya leo katu haiwezi kulinganishwa na Esfarayen ya kabla ya mapinduzi. Katika kipindi cha kabla ya mapinduzi, nilipata tawfiki ya kusimama kwa muda mfupi katika mji wenu huu. Mwaka 1347 Hijria Shamsia, kulitokea mtetemeko wa ardhi katika eneo hili la Dahaneh-ye Ojaq.
Tulikuja katika eneo hili la Dahaneh-ye Ojaq tukitokea Mash'had ili tuje kuwasaidia wananchi waliokuwa wamekumbwa na tetemeko la ardhi; kando la hilo, tukaja katika mji wa Esfarayen. Katika zama hizo Esfarayen kilikuwa kijiji kikubwa; eneo hili haliwezi kulinganishwa katu na hivi sasa katika kila upande; licha ya kuwa katika zama hizo eneo hili lilikuwa na tabia nchi nzuri kama ilivyo leo. Eneo hili ni zuri mno kwa kilimo, haya maji mengi yanayopatikana hapa na hii ardhi nzuri na yenye rutuba ambayo iko kando ya milima mirefu ya Shah Jahan na huu ufugaji mkubwa unaofanywa katika eneo hili ambalo ni maarufu katika ufugaji, ni mambo ambayo kwa hakika yanaufanya mji huu kuwa na sifa za kipekee; sio tu katika Esfarayen bali hata maeneo ambayo yanalizunguka eneo hili kuanzia Bojnourd mpaka Sabzevar - ambapo hata katika methali mashuhuri za eneo hili ambazo bila shaka mnazifahamu jambo hili limezungumziwa na kuashiriwa - katika zama hizo kulikuweko na kundi la watu wachache ambao walikuwa wakifungana na utawala na vyombo vya utawala ambao kimsingi ndio waliokuwa wakinufaika na haya yote; wananchi wa kawaida iwe ni vijijini au mjini walikuwa katika hali mbaya na magumu mno.
Hii leo sio kwamba, tunataka kusema kuwa, mji huo umefanyiwa mambo kama inavyostahiki - tab'an, ustahiki wa watu wa eneo hili ni zaidi ya haya - lakini tunachotaka kusema ni kuwa, maendeleo yaliyopatikana katika eneo hili ni makubwa mno. Mbali na suhula za kilimo na ufugaji, sekta ya viwanda imeingia katika eneo hili; kuna viwanda viwili vikubwa na miongoni mwa viwanda muhimu vya nchi hii vinapatikana hapa, kuna viwanda vingine vidogo vidogo ambavyo vinapatikana kando kando ya maeneo haya; ambapo maendeleo ya mkoa huu na ustawi wa eneo hili na mji huu unatoa matumaini kwamba, Inshallah mustakbali wa mji huu kimaada utaboreka zaidi siku baada ya siku.
Bila shaka kuna matatizo; katika uwanja wa kilimo na vile vile matatizo yapo katika uga wa viwanda; ambapo Inshallah matatizo haya yanapaswa kupatiwa ufumbuzi na kumalizwa kwa hima na jitihada ya viongozi pamoja na uzingatiaji uliopo baina ya viongozi na maafisa wa serikali wa ngazi mbalimbali kwa mji huu wa Esfarayen. Bila shaka kutakuwa na juhudi za makusudi katika uwanja huu.
Huko nyuma katika eneo hili, matumaini ya kwamba, kuasisiwe Chuo Kikuu na vituo vya elimu vya masomo ya Chuo Kikuu, ni jambo ambalo hata halikuwa likitasawariwa au kufikiriwa. Hii leo Alhamdulilahi katika eneo hili, kuna vituo vya elimu vya Chuo Kikuu; na mimi napenda kuwaeleza kwamba, hili sio jambo ambalo ni maalumu tu kwa mji wa Esfarayen; hapana, katika maeneo mbalimbali ya nchi hii mtu hakuwa akifikiria kwamba, kungeasisiwa kituo cha elimu cha Chuo Kikuu katika eneo hili, kwa bahati nzuri kuna Vyuo Vikuu mbalimbali tena ambavyo vinatoa mafunzo ya taaluma na ujuzi mbalimbali; ambapo nitalizungumzia na kuliashiria hili pia katika mazungumzo yangu ya leo hapa.
Kile ambacho ni muhimu ni kuzingatia masuala ya kimsingi ya nchi ambayo yanaweza kuainisha upande na muelekeo wa kufanya harakati wananchi katika ngazi mbalimbali. Hili ni jambo ambalo linapaswa kufanywa na kuainishwa na viongozi na maafisa wa serikali; wao ndio wanaopaswa kutwambia sisi tufanye harakati kuelekea upande gani, kesho yetu itakuwaje na leo tunapaswa kufanya nini ili tuweze kuifikia hiyo kesho yetu. Nikiwa katika hadhara ya wananchi wa Bojonourd nilibainisha nukta mbili tatu hivi katika hotuba yangu ambapo nikiwa hapa pia napenda kuzizungumzia nukta hizo japo sio kwa mapana na marefu sana, ili nifungue njia ya kuzungumzia masuala mengine.
Jambo la kwanza lilikuwa ni kwamba, mkoa wa Khorasan Kaskazini umetambuliwa kwa kuwa na hamu, shauku na nishari katika maisha. Tangu kale, sisi tulikuwa tukiutambua mkoa huu kwa sifa hizi na wananchi wa eneo hili ambalo leo linajulikana kwa jina la Khorasan Kaskazini walikuwa wakifahamika na kutambuliwa na watu wengine kuwa ni wananchi wa hamasa, nishati, wa maisha na wenye maandalizi ya kiroho na kimwili.
Vizuri, kwa hakika huu ni mtaji mkubwa sana. Kunyamaza kimya na kutofanya harakati taifa fulani, ni sababu kuu ya kubakia kwao nyuma kimaendeleo. Vuguvugu, nishati na uchangamfu wa maisha wa taifa fulani ni kujiandalia mazingira makuu kwa ajili ya kupiga hatua na kupata maendeleo na ustawi katika nyuga zote. Kwa hakika hili ni sharti kuu hapa.
Kuna nukta mbili tatu hivi zinazohusiana na nishati jumla ya vijana ambayo ni lazima nizieleze hapa. Nukta ya kwanza ni hii kwamba, hili vuguvugu na nishati hii vinapaswa kulindwa na kuhifadhiwa na hivyo kufanywa ibakie; haipaswi kuruhusu haya yadhoofishwe au yandolewe na sababu na mambo mbalimali. Hapana shaka kuwa, nukta ambayo inazingatiwa na kulengwa na maadui wa ustawi na maendeleo ya nchi hii ni walifanye taifa ili na wananchi wawe wasiwe na harakati wala nishati; yaani wanataka kuzima hii nishati na vuguvugu hili. Hatupaswi kusalimu amri mbele ya takwa hili la hasama na chuki la maadui. Hii kwamba nyinyi mnaona na kushuhudia kwamba, mamia ya vituo vya Radio na Televisheni sambamba na mamia ya mawasiliano ya intaneti na Mawasiliano ya Komyuta (Cyberspase) katika pembe malimbali duniani vinafanya ili kutia katika nyoyo na fikra za watu ujumbe wa hali ya kukata tamaa.
Pindi hali ya kukata tamaa inapojitokeza, nishati hutokomea na vuguvugu na harakati huzimika. Moja ya sababu kuu za propaganda za wanaohodhi vyombo vya habari duniani ni kuwafanya vijana wetu waache kufanya hima, idili na harakati ambayo chimbuko ni kutaka matukufu. Katika nukta mkabala na hili sisi tunapaswa kufanya hima kubwa ili kulinda hii. Mimi ninaamini kwamba, kukumbuka, kutukuza na kuyafanya majina ya viongozi wa mashahidi pamoja na wapiganaji mashujaa yabakie yaani wale vijana waliokuwa kabla ya kizazi hiki - ambao ni nyinyi vijana - ambao waliingia katika medani kali na ngumu kabisa tena wakiwa na hamasa na nishati ya hali ya juu, ni mambo ambayo yanaweza kuwa nyongeza katika hamasa na nishati ya vijana wetu.
Moja ya vitu vya kimsingi ambavyo leo vinaweza kuwa ni dhidi ya harakati hii ambavyo inasikitishwa kuwa mambo haya yamepanuliwa na magenge ya siri ni suala la mihadarati na madawa ya kulevya. Mimi ninaamini kwamba, vijana wenyewe wanapaswa kupambana na madawa ya kulevya kwa nishati na hamasa ile ile niliyoiashiria. Maadui wanataka kuwafanya vijana wetu wawe watumwa na mateka; wawe waraibu wa madawa ya kulevya, wasiweze kufanya chochote na kwa muktadha huo wawadondoshe chini vijana wetu. Kile ambacho kinapaswa kuwa kikwazo kikubwa na imara mkabala na njama hizi, katika hatua ya awali ni vijana wenyewe. Tab'an, viongozi na maafisa wa serikali wana masuuliya na majukumu makubwa katika hili, vyombo husika katika uga huu navyo vina majukumu; hata hivyo hakuna kitu kama sababu za ndani za wananchi ambazo zinaweza kusimama kidete mkabala na upotofu huu. Hii ni nukta moja.
Hapana shaka kuwa hii hali ya vijana wetu kusimama kidete katika mkoa huu inaweza kufubaza na kusambaratisha kile ambacho kinafuatiliwa na magenge yanayoangamiza na kudhuru. Hii ni nukta moja kuhusiana na hii hamasa na nishati. Kwanza kabisa, kuna ulazima na udharura wa kuhifadhiwa na kuwa makini kwamba, adui anafanya njama za kuwapokonya vijana wetu huu mwenge wa nishati na hamasa. Nukta nyingine ni hii kwamba, moyo huu unapaswa kutumiwa kwa ajili ya kupambana na jambo lile muhimu yaani hatari kubwa ya madawa ya kulevya na hivyo kusimama kidete kupambana na mihadarati.
Matilaba ya pili ambayo niliibainisha nilipokutana na wananchi wa Bojnourd na jambo hilo likakufikieni ni suala la ustawi na maendeleo. Sisi tumesema kuwa, lengo ni ustawi na maendeleo. Maendeleo kwa maana ya harakati ya daima. Endapo tutakuwa makini tutaona kuwa, maendeleo ni njia na lengo. Sisi tunasema kuwa, maendeleo ni lengo; kupata maendeleo maana yake ni kupiga hatua kuelekea mbele. Vipi kupiga hatua kuelekea mbele kunaweza kufanywa kuwa ni lengo? Ufafanuzi wake ni huu kwamba, maendeleo ya mwanadamu katu hayawezi kusimamishwa. Yaani Mwenyezi Mungu Mtukufu amemuumba mwanaadamu kwa namna ambayo harakati yake katika medani mbalimbali ya kuelekea mbele na hakuna wakati ambao inafikia hatua ya kusimama. Kila hatua na marhala mtakayoifikia - iwe ni katika hatua ya kimaada au marhala ya kimaanawi - hapana shaka kuwa, kusimama na kutosonga mbele kwa mtu ambaye anapenda maendeleo ni jambo ambalo halina maana. Kwa msingi huo basi, maendeleo ni njia na wakati huo huo ni lengo.
Ni lazima daima kufanya harakati kwa ajili ya kuelekea mbele. Taifa la Iran lina kipaji na maandalizi haya kwamba, lipige hatua kiasi kwamba, liwe ni kigezo na mfano wa kuigwa ulimwenguni katika nyuga na nyanja mbalimbali. Kwa nini tujitazame kwa mtazamo mbaya? Kwa nini tujitazame sisi, taifa letu na mustakbali wetu kwa jicho la kujidunisha? Maadui wanataka kulitia hili ndani ya taifa letu na tumeona jinsi walivyofanya harakati ya kufikia hilo katika kipindi chote cha miaka hii (baada ya ushindi wa mapinduzi).
Maadui wanataka kuwafanya wananchi wetu waamini kwamba, ulimwengu wa Magharibi uko mstari wa mbele na ni lazima kufanya harakati nyuma yao; hapana, siku moja historia yetu ilituonyesha kwamba, hali haiko hivyo ni kinyume chake. Kwa hakika sisi tulikuwa mstari wa mbele duniani; tulikuwa mstari wa mbele katika elimu, tulikuwa katika mstari wa kwanza kwenye viwanda, tulikuwa mbele katika kutengeneza ustaarabu na tulikuwa mbele katika utamaduni; watu wengine walikuwa wakijifunza na kuchukua mambo kutoka kwetu; kwa nini leo tusiwe kama hivyo? Hima ya vijana wetu na mtazamo wao kuhusiana na neno ustawi au maendeleo unapaswa kuzingatia mustakbali wetu.
Hivi karibuni niliwaambia vijana wanachuo na wenye vipaji nukta hii kwamba, ni lazima hima yenu ifikie hatua hii kwamba, kama mtu ulimwenguni anataka kujifunza mambo mapya ya kielimu, basi alazimike kujifunza Lugha ya Kifarsi.
Vijana wetu wanapaswa kuutazama mustakabali kwa anuani ya mustakbali usio na shaka na wafanya hima na kazi kwa ajili ya mustakbali huo. Watu wetu wenye vipawa, watu wetu wenye vipawa vya kisiasa, watu wetu wenye vipaji vya kielimu na kiutamaduni, wanapaswa kufanya harakati kuelekea mbele wakiwa na mtazamo huu, waandae ratiba na mipango na katu wasifikie hatua ya kukinaika na kuridhika. Hii ndio maana ya neno maendeleo.
Vizuri, maendelezo yana vigezo. Moja kati ya vigezo vya maendeleo ya taifa fulani, ni izza ya kitaifa na hali ya kujiamini kitaifa. Madai yangu ni kwamba, taifa letu limepata maendeleo na kupiga hatua kwa kuzingatia vigezo hivi. Hii leo taifa letu linajiamini katika uga wa siasa za kimataifa. Hii kwamba, nyinyi mnaona kwamba, viongozi wa nchi hii wamekuwa wakizungumza kwa kujiamini kikamilifu katika kukabiliana na kadhia za kimataifa, huku kunatokana na kwamba, taifa letu linahisi kuwa na izza (utukufu) na hali ya kujiamini. Dini Tukufu ya Kiislamu ndio iliyotupatia hali hii ya kujiamini. Kadiri tutakavyokuwa na ufahamu kuhusiana na Uislamu na hukumu za Qur'ani na maarifa ya Qur'ani, ndivyo hali hii ya kujiamini itakavyoongeza. Neno izza ya kitaifa na hali ya kujiamini kitaifa, ni jambo ambalo linahisika kabisa hapa nchini. Katika nyuga za masuala ya kimataifa; iwe ni katika mashindano ya kielimu ya kimataifa au katika ushindani wa kisiasa kimataifa, hii leo taifa la Iran lina mambo ya kusema.
Maafisa na viongozi wa nchi wanasimama kidete katika masuala mbalimbali ya kimataifa kwa kutegemea hali ya kujiamini ya wananchi wa taifa hili na hivyo kufanya na kuzungumza mambo yao. Hiki ni kigezo kimoja.
Kigezo kingine kwa ajili ya maendeleo ni uadilifu. Endapo nchi itapiga hatua katika elimu, teknolojia na kuwa dhihirisho la ustaarabu tofauti wa kimaada, lakini kukawa hakuna uadilifu wa kijamii, kwa mtazamo wetu na kwa mujibu wa mantiki ya Kiislamu, haya sio maendeleo. Hii leo kuna nchi nyingi ambazo zimepiga hatua na kupata maendeleo katika elimu, katika viwanda na katika masuala mbalimbali ya namna ya kuishi, lakini kumeongezeka tofauti ya kimatabaka; haya sio maendeleo; haya ni maendeleo ya kidhhiri na kijuujuu. Wakati inapotokea kwamba, katika nchi fulani kuna idadi ya watu wachache wananufaika zaidi kimaada na utajiri wa nchi hiyo na wakati huo huo katika nchi hiyo hiyo kuna watu wengine wanakufa barabarani kwa baridi na joto, uadilifu katika nchi hiyo hauna maana na mafuhumu na haujafanyiwa kazi kivitendo.
Tunasoma kuhusiana na habari za kimataifa kwamba, katika msimu wa joto katika miji na majimbo ya mbalimbali ya Marekani watu hufa kwa joto! Kwa nini mtu afe kwa joto? Je hii haitokani na kuwa mtu huyo hana pa kujistiri, hana nyuma na hana pa kukaa? Marekani ndio ile nchi ambayo ina watu matajiri kabisa duniani na ndio yenye mashirika makubwa kabisa duniani; faida kubwa kabisa ya uuzaji silaha ni ya nchi hiyo; lakini katika nchi hiyo ambayo utajiri umeenea, kuna watu ambao wanakufa kwa joto katika msimu wa joto na katika msimu wa baridi wanaaga dunia kwa baridi kutokana na kutokuwa na mahala pa kujihifadhi! Hii ina maana kwamba, katika nchi hiyo hakuna uadilifu wa kijamii.
Sasa tunaona kuna filamu zinazotengenezwa nchini Marekani ambazo zina visa vinavyoonyesha kuweko uadilifu katika nchi hiyo; kwa hakika haya ni mambo ambayo yako mbali mno na uhakika na uhalisia wa mambo. Katika nchi ambazo zinaongozwa kwa mfumo wa uchumi wa kibeberu na jina la uliberali ambalo zimejiwekea zina mashaka na matatizo kama haya; katika nchi hizo uhakika wa maisha uko namna hii. Lakini kama tunataka kupiga hatua kimaendeleo, katika hatua ya awali moja ya vigezo muhimu ni uadilifu. Madai yangu ni kuwa, sisi tumepiga hatua na kupata maendeleo katika uga huu; tab'an, sio kwa kiwango ambacho tunataka.
Endapo tutalinganisha hali yetu ya sasa hivi na ile tuliyokuwa nayo kabla ya mapinduzi, tutaona kuwa tumepiga hatua na kupata maendeleo; endapo tutajilinganisha na nchi nyingi ambazo wananchi wake wanaishi chini ya mifumo tofauti tofauti, tutaona kuwa, kweli tumepata maendeleo; lakini kama tutajilinganisha sisi wenyewe na kile ambacho Uislamu umekisema na ambacho Uislamu umetutaka tukifanye, tutaona kuwa, hapana, tungali tuna pengo na masafa mengi ili kulifikia hilo; hivyo ni lazima tufanye hima na idili. Hima na juhudi hizi zinapaswa kufanywa na nani? Jitihada hizi zinapaswa kufanywa na viongozi na wananchi yaani wote kwa pamoja wafanye hilo.
Ndio, sisi tumepiga hatua katika uwanja wa kugawa vyanzo vya utajiri kwa maeneo yote ya nchi. Kuna siku vyanzo hivi vya utajiri vilikuwa ni maalumu kwa maeneo fulani tu ya nchi na vilikuwa vikitumiwa tu na watu wenye nguvu, watawala na waliokuwa wakifungamana na utawala; akthari ya miji na mikoa mikubwa ya nchi hii - tab'an, sitaki kutaja majina; huko nyuma nimewahi kusema kuwa - kulikuweko na viwanja vitano maalumu vya ndege katika nukta tano za mkoa ambavyo vilikuwa mali ya watu wanaofungamana na utawala wa Kifalme wa Shah; lakini katika mkoa huo hakukuweko na hata kiwanja kimoja cha ndege ambacho ni cha umma (cha watu wote)! Yaani wananchi hawakuwa na uwanja wa kutumia kwa ajili ya safari za ndege; hii ni katika hali ambayo, katika mkoa huo huo kulikuwa na viwanja vya ndege vitano maalumu kwa ajili ya viongozi wa utawala wa Kifalme na watu waliokuwa wakifungamana na utawala huo; kwa hakika huu ulikuwa ni ukosefu wa uadilifu.
Hii leo tunapotazama tunaona kuwa, kwa upande wa utoaji huduma, ujenzi wa barabara na mambo mengine ambayo ni mahitaji ya wananchi yamejaa katika kila kona ya nchi hii. Kama nilivyoashiria, katika zama hizo maeneo mengi ya nchi hata miji ilikuwa na hali ngumu hata ya shule za msingi. Kipindi fulani nilikuwa naishi uhamishoni huko Sistan Baluchistan; nilikuwa nikiona hali ya mambo katika eneo hilo. Kwa upande wa shule za msingi, mji huo ulikuwa katika hali mbaya sana ikilinganishwa na miji mingine ya mkoa huu. Kulikuwa na kituo kimoja kidogo ambacho kilikuwa ni cha daraja ya tatu au ya nne ya Chuo Kikuu katika mkoa wote.
Hii leo wakati nyinyi mnapotazama mkoa huo na mikoa mingine nchini, mnaona kuwa kuna Vyuo Vikuu katika mikoa yote ya nchi hii; yaani kuna suhula za usomaji. Vizuri, huu ni uadilifu. Hii ina maana kwamba, suhula na uwezekano wa elimu umegawiwa baina ya maeneo yote ya nchi; uwezo wa suhula za kimaada, vyanzo vya utajiri na elimu vimegawiwa; hili ni jambo zuri sana. Huko nyuma, wenye vipaji vya elimu waliokuwa katika miji ya mbali na watu wenye maandalizi na ubunifu, hawakuwa na uwezo wa kudhihiri na kujitokeza; leo mambo yako kinyume, kwani uwezekano wa kujitokeza watu hao na kuonekana upo kutokana na kuandaliwa mazingira ya hilo.
Katika eneo la Esfarayen na katika kila nukta nyingine, wakati inapotokea kwamba, kuna mtu mwenye kipawa na maandalizi na akaweza kuonyesha hali yake ya kuwa na kipaji, vyombo mbalimbali hapa nchini hulipokea hilo, humtukuza na hunufaika na mtu huyo. Huko nyuma hali haikuwa namna hii. Kwa muktadha huo, ikilinganishwa bila shaka hiki kigezo cha ustawi na maendeleo - ambacho ni kigezo na kielelezo cha uadilifu - ni stadi; hata kuhusiana na kile ambacho sisi tumekifahamu kutoka katika Uislamu, hapana, bado tuko nyuma; ni lazima tufanye hima na kuchapa kazi.
Kile ambacho mimi ninataka kufikia natija katika hadhara yenu hii nyinyi wapendwa, hususan vijana wapendwa - wake kwa waume, mabinti kwa vijana - ni hiki kwamba, nchi yetu na taifa letu hili kwa sasa liko katika medani kubwa ya mapambano ya irada na nia thabiti ambapo katika medani hiyo na licha ya kuwepo vizuizi vingi vya kimaumbile na vya kutwishwa lakini kamwe taifa hili halihisi kuchoka wala kuwa udhaifu na upeo wa mustakbali wake wa kufikia kwenye maendeleo makubwa zaidi unang'ara, unavutia na unameremeta.
Kwa hakika sisi hatuhisi udhaifu. Tunatambua kwamba, kwa kufanya hima na idili inawezekana kuondoa vikwazo na vizingiti vyote vilivyoko njiani. Baadhi ya vizingiti hivyo ni vya kawaida hivyo kuna haja ya kuamiliana na vizingiti hivyo kikawaida. Lakini baadhi ya vizingiti hivyo ni vya kutwishwa; vizingiti vya kisiasa na matatizo ambayo yamepandikizwa na maadui wa maendeleo ya taifa hili na katika njia ya wananchi wa taifa hili; kuna haja ya kuamiliana na hayo kwa namna nyingine ambayo ni tofauti na ile ya kwanza.
Katika vita kama hivyo kitu ambacho kinaweza kuainisha mambo ni irada na nia ya kweli, tabasuri na muono mpana wa mbali, umoja na kutambua wajibu (majukumu) wa matabaka yote ya wananchi kutekeleza vizuri majukumu yao pamoja na viongozi kuwa na misimamo na kauli moja sambamba na kuwepo ushirikiano mzuri baina ya taasisi mbali mbali. Kwa hakika haya ni mambo ambayo yanaweza kulifikisha taifa la Iran kwenye hadhi yake ya kimaendeleo linayostahiki kuwa nayo. Maadui wanapanga njama; wakijidanganya kwamba, kwa kutumia njama, mipango, mikakati na juhudi kubwa za watu wanaolitakia mabaya taifa la Iran wataweza kulifanya taifa hili lisiweze kuendelea na hivyo kukwama katika jitihada zake za kujiletea maendeleo.
Ukweli wa mambo ni kuwa, kama ambavyo njama zote za maadui zimeshindwa tangu mwanzoni mwa Mapinduzi ya Kiislamu hadi hivi sasa, katika wakati huu pia hila, kedi na njama zote za maadui hao zitashindwa na kusambaratika pia. Kuna wanasiasa mbalimbali katika nchi ambazo zinatupinga ambao wamekuja na kuondoka - nchini Marekani, nchini Uingereza na katika baadhi ya nchi nyingine - kila aliyekuja aliingia madarakani akiwa na chuki na hasira kubwa dhidi ya harakati ya Kiislamu, mapinduzi ya Kiislamu na Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu; wakapanga mikakati na mipango yao; wakafanya hima na idili kadiri walivyoweza; kwa kudhani kwamba, kwa kufanya hivyo wataweza kuipigisha magoti Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kuifanya iwatii. Wakaondoka, baadhi yao hata majina yao yamesahauliwa; lakini taifa la Iran lingali limesimama kidete, imara na kifua mbele na Alhamdulilahi lingalipo uwanjani na limekuwa likisonga mbele katika njia yake hii likiwa na irada thabiti na maamuzi madhubuti. Kushindwa maadui wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kulipigisha magoti ya kuwatii maadui hao katika kipindi chote hiki cha miaka 33 ya tangu kupatikana ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran hadi hivi sasa kuwa kunaonesha kwamba, Jamhuri ya Kiislamu na taifa la Iran limezidi kuimarika na kuwa na nguvu.
Tab'an, jambo hilo halipaswi kutufanya tupande kiburi na kuingiwa na ghururi na hatimaye kutufanya tusahau hilam inda na inadi za adui; kwani kufanya hivyo kuna hatari kubwa. Hivyo hatupaswi kuingiwa na kiburi. Mimi daima nimekuwa nikiwasihi viongozi kwa kuwaambia wawe imara; lakini pia wasiwe na mawazo kuwa adui ni dhaifu wala wasisahau hila zake; kwani adui anatumia mbinu na hila mbali mbali tena tata na kujipenyeza katika sehemu tofauti hivyo wanapaswa kuwa macho wakati wote. Adui anaingia na kupenya kupitia njia mbalimbali; kuna siku linazungumziwa suala la vikwazo, siku nyingine kuvamiwa kijeshi, siku nyngine maadui wanazungumzia vita laini, mara hujuma za kiutamaduni na mashambulio ya kiutamaduni. Hivyo basi kuna haja ya kuwa macho hasa kutokana na kuwa adui anatumia njia mbalimbali kupenya na kuingia.
Haya maendeleo ambayo nimeyazungumzia, huu mustakabli ulio wazi ambao nimeuchora na kuuainisha, huu muelekeo mzuri na wenye kuvutia ulioko mbele yetu, unaweza tu kupatikana endapo tutakuwa makini, macho na tusikumbwe na mghafala. Tusijidangaye na kudhani kwamba, sasa kila kitu kiko vizuri; hivyo tufanye mambo yetu mengine ya kibinafsi pasina ya kuwa na wasi wasi; yaani, tughafilike na mustakbali wa nchi; hapana hatupaswi kufanya hivyo.
Moja ya sifa za wananchi wa Esfarayen ni ushiriki wao wa kiwango cha juu na kushikilia kwao nafasi ya kwanza nchini Iran katika kiwango cha kushiriki kwenye chaguzi zinazofanya kwa nyakati na zama tofauti humu nchini; kwa hakika hili ni jambo muhimu sana. Mkoa wa Khorasan Kaskazini unashikilia moja ya nafasi za juu kabisa za ushiriki katika uchaguzi; aidha Wilaya ya Esfarayen inashikilia nafasi ya kwanza katika mkoa wa Khorasan Kaskazini katika ushirikiri wa wananchi kwenye chaguzi mbalimbali zinazofanyika hapa nchini. Kuhudhuria katika uchaguzi ni kuwa na ufahamu na welewa sambamba na kuwa na muono wa mbali.
Kujitokeza na kwenda katika vituo na masanduku ya kupigia kura sio kwamba, kunatokana na mtu kutokuwa na kazi; hasha (bilikuli), bali hiyo nayo ni kazi; ni kazi njema. Kuhusiana na suala la uchaguzi Inshallah nitalibainisha katika safari yangu hii katika mikutano mingine nitakayokuwa nayo na wananchi - kwa sasa sitaki kuingia katika maudhui hii - lakini ukweli wa mambo ni kuwa, sifa hiyo muhimu ya kuhisi kuwa na jukumu la kupigania mustakbali bora wa taifa, kuwa uchaguzi huo ni wa wananchi, kutaka kuwa na nafasi katika uongozi wa nchi na kujitokeza katika medani ni jambo linaloonesha kuwa mwamko na utambuzi wa watu wa eneo hilo una thamani kubwa na inabidi sifa hiyo idumishwe na ilindwe katika maeneo yote nchini. Kwa hakika hili ni jambo ambalo liko dhidi ya kile ambacho adui anataka kututwisha.
Moyo huu unapaswa kulindwa na kuhifadhiwa; moyo wa kuwa na mahudhurio, moyo wa kushiriki, moyo wa ushirikiano; yote haya yanapaswa kuweko na kudumishwa. Amma kuhusiana na suala la uchumi, kuna haja ya kuweko moyo wa kutumia vitu na bidhaa za hapa ndani (yaani kutumia bidhaa zinazozalishwa hapa nchini); ambapo hili nalo ni jambo muhimu; hata hivyo kwa sasa sitaki kulizungumzia hili. Kwa hakika sisi tunatilia mkazo juu ya uzalishaji wa bidhaa za ndani na tulilibainisha hilo mwanzoni mwa mwaka (Mwaka wa Hijria Shamsia mwaka mpya wa Kiirani) na kuliweka hilo katika nara na kauli mbiu ya mwaka huu. Aidha tumelizungumzia hilo na kulitilia mkazo katika hotuba na mazungumzo yetu katika kipindi chote cha miezi hii.
Uzalishaji wa ndani unahitajia matumizi ya ndani; hili ni jambo ambalo liko mikononi mwa wananchi. Tunapaswa kufadhilisha bidhaa za ndani. Kufadhilisha kutumia bidhaa za nje kuliko bidhaa za ndani si tabia nzuri na wala si jambo sahihi kwani haiwezekani kuusaidia na kuuunga mkono uzalishaji wa taifa bila ya kuwaunga mkono na kuwasaidia wazalishaji wa bidhaa za ndani yaani kununua bidhaa za hapa ndani. Endapo uzalishaji wa ndani utapewa kipaumbele na kuungwa mkono basi itawezekana kuondoa matatizo mengi ya kiuchumi kama vile ukosefu wa kazi (ajira) na kupanda gharama za maisha. Kutumia bidhaa za ndani hupelekea kuongezeka uzalishaji wa bidhaa hizo, haya haya matatizo yaliyotajwa hapa na mheshimiwa Khatibu wa Sala ya Ijumaa yatapatiwa ufumbuzi; na suala la ukosefu wa ajira litatatuliwa, ughali wa bidhaa utapungua na nafasi za ajira kuongezea; haya yote ni mambo ambayo yana mfungano baina yao; hivyo haya ni mambo ambayo yako mikononi mwetu sisi wananchi ya kwamba, ni vipi tuchague bidhaa za matumizi yetu.
Ala kulli haal, majukumu yako mengi, lakini tawfiki ya Mwenyezi Mungu nayo ni nyingi. Tunamuomba Mwenyezi Mungu Mtukufu alipatie tawfiki na baraka hizi taifa la Iran na kuifanya hali hiyo kuwa ni yeye kuendelea. Tunamuomba Mwenyezi Mungu akufanyeni nyinyi kuwa ni wenye kujumuishwa katika mapenzi ya Mwenyezi Mungu na dua takasifu za Mtukufu Baqiyatullah katika ardhi, Imam Mahdi (roho zetu ziwe fidia kwake).
Natumia fursa hii kukushukuruni tena kutokana na mahudhurio yenu haya yenye hamasa kubwa na ambayo yana huba na hamasa kubwa. Ninakushukuruni pia kutokana na kuwa na mahudhurio katika katika marasimu zote za mapinduzi na katika masuala muhimu yanayohusiana na nchi; na ninatumia fursa hii pia kuonyesha huba na mapenzi yangu maalumu kwa mashahidi wenu azizi, shakhsia wenu wakubwa na waliotangulia. Ni matarajio yangu kuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu atakushushieni nyinyi nyote rehma, baraka na fadhila Zake. Amiin.

Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

 
< Nyuma   Mbele >

^