Skip to content

Habari

Habari
Hifadhi

Risala na Barua

Matini
Hifadhi

Kumbukumbu na Simulizi

Kabla ya Mapinduzi
Baada ya Mapinduzi

Sauti na Taswira

Picha
Sauti
Video
Hotuba ya Kiongozi Muadhamu Alipokutana na Vijana wa Mkoa wa Khorasan Kaskazini Chapa
14/10/2012
Ifuatayo ni matini kamili ya hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aliyoitoa tarehe 14/10/2012 katika hadhara kubwa ya vijana wa mkoa wa Khorasan Kaskazini katika Msikiti Mkuu wa Imam Khomeini MA mjini Bojnourd (wa kaskazini mashariki mwa Iran).

Kwa jina la Allah Mwingi wa rehma Mwenye kurehemu

Hamdu zote zinamstahikia Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wa viumbe pia. Na rehma na amani zimfikie Bwana wetu na Mtume wetu Mtukufu Abul Qassim Muhammad SAW pamoja na Aali zake wema na watoharifu, wateule, maasumina na waongozaji hususan Baqiyatullah katika ardhi (Imam Mahdi roho zetu ziwe fidia kwake).
Kwa hakika kikao hiki ni kikao cha vijana kweli kweli na wote ninaowaona hapa wana sifa chanya za ujana. Kwa hakika matumaini pia ni kwenu vijana; nyinyi ni tumaini la leo na ni tumaini zaidi kwa ajili ya mustakbali (tumaini la kesho). Mambo yaliyozungumzwa na kubainishwa na vijana hawa hapa, nimeyasikiliza kwa umakini mkubwa. Kwa hakika hukumu yangu kuhusiana na matamshi haya ni kuwa, yalikuwa mazuri mno. Mambo haya yanaunga mkono yale maoni yangu ya huko nyuma kuhusiana na kuongezeka kiwango cha fikra na mitazamo ya kielimu katika mkoa huu. Katika siku chache hizi kila mtu aliyezungumza kutoka katika mkoa huu - kutoka katika vijana, familia za mashahidi, waalimu na wahadhiri - kwa hakika matamshi hayo yalikuwa ni yenye furaha na kuniburudisha mimi katika kila lahadha. Hii ni ishara kwamba, Alhamdulilahi mji wa Bojnourd na mkoa wa Khorasan Kaskazini una kiwango cha hali ya juu cha fikra na utamaduni; hili ni jambo ambalo mnapaswa kulilinda na mnapaswa kuongeza hali hii ya kukwea na kuwa na kiwancho cha juu siku baada ya siku; na tab'an sisi - mimi na viongozi wengine wa nchi - tuna jukumu la kuhakikisha kwamba, neema hii kubwa ambayo ni adia na tunu ya Mwenyezi Mungu, tunaitumia kwa njia sahihi kwa maslahi ya mapinduzi na kwa maslahi ya mfumo; Inshallah, tunataraji tutapata tawfiki hii.
Jambo ambalo leo ninataka kulizungumzia na kukuelezeni nyinyi vijana wapendwa katika kubainisha na kutoa maelezo ya suala ambalo nililizungumzia siku ya kwanza: Ni suala la ustawi na maendeleo. Ni maudhui muhimu sana ambayo tunapaswa kuizungumzia. Hata hivyo kuzungumzia maudhui hii, hatujikinainishi kwamba, mambo yamekwisha; la hasha, bali huu ni mwanzo tu wa safari ndefu iliyoko mbele yetu. Tumesema kwamba, mafuhumu ambayo kwa kiwango fulani chenye nguvu zaidi inaweza kukusanya malengo ya mapinduzi ya Kiislamu na kutuonesha ni mafuhumu ya maendeleo. Kisha baadaye nilitoa ufafanuzi kwamba, maendeleo ni ishara ya kuweko harakati na njia. Inakuwaje sisi tunasema kuwa, maendeleo ni lengo? Tukasema kuwa, sababu yake ni kwamba, katu maendeleo hayawezi kusimama. Ndio, maendeleo ni harakati na njia, lakini si yenye kusimama hivyo ni yenye kuendelea; kwa sababu mwanadamu ni mwenye kuendelea na kwa sababu vipaji vya mwanadamu havina kikomo. Tumesema kuwa, maendeleo yana engo tofauti; na maendeleo katika mafuhumu ya Kiislamu ina tofauti na maendeleo ya engo moja au mbili katika utamaduni wa Magharibi. Istilahi na ‘mafuhumu' ya maendeleo inahitajia kuweko harakati na kudumisha subira katika njia ya kufikia maendeleo hayo na katika maana yoyote ile ya istilahi hiyo (iwe ya kimaada au ya kimaanawi) masuala kama mtindo wa maisha, miamala ya kijamii na namna ya watu kuishi kwa pamoja ni mambo ambayo yana umuhimu mkubwa ndani yake.
Moja kati ya engo ya maendeleo kwa mafuhumu ya Kiislamu ni namna ya kuishi, miamala ya kijamii, namna ya watu kuishi, huu ni upande na engo muhimu; ninataka kuzungumzia maudhui hii leo kwa kiwango fulani. Endapo sisi tutatazama kwa mtazamo wa umaanawi - ambapo lengo la mwanaadamu ni kufaulu na kupata wokovu - kuna haja tutilie maanani namna ya kuishi; kama pia tutakuwa hatuna imani na umaanawi na wokovu wa kimaanawi, bado kuna haja ya kutilia maanani namna ya kuishi ili tuwe na maisha ya raha na ambayo yana usalama wa kisaikolojia, kinafsi na kimaadili. Kwa msingi huo, jambo hili ni jambo muhimu na la kimsingi. Tujadili kuhusiana na kuwa, katika uga wa namna ya kuishi nini kinapaswa kusemwa na nini kinawezekana kusemwa. Endapo sisi tutazingatia kwamba, maendeleo ya kila upande maana yake ni kujenga ustaarabu mpya wa Kiislamu - vyovyote itakavyokuwa, maendeleo yana misdaqi asili na ya nje kwa ajili ya maendeleo yenye mafuhumu ya Kiislamu; tusema hivi kwamba, lengo la taifa la Iran na lengo la Mapinduzi ya Kiislamu ni kuleta ustaarabu mpya wa Kiislamu; haya ni mahesabu sahihi - tunapoyaangalia maendeleo ya kila upande kwa maana halisi ya kujenga ustaarabu mpya wa Kiislamu tutaona kuwa, ustaarabu huo una nyenzo mbili kuu ambazo ni wenzo wa uhakika na wenzo wa kimsingi na kuishi maisha mepesi ya kawaida ndio wenzo wa uhakika wa maendeleo hayo. Hata hivyo la msingi ni kuwa, ni lazima kufanya hima kwa ajili ya kufikia nyenzo zote mbili. Sehemu ya wenzo ni ipi? sehemu ya wenzo au ya programu ya ustaarabu huo ni maudhui ambazo leo hii zinatangazwa kwa jina la mifano na vielelezo vya maendeleo kama vile elimu, uvumbuzi, uchumi, siasa, masuala ya kijeshi itibari ya kimataifa na mambo kama hayo. Ni kweli kwamba, kumeshuhudiwa maendeleo mazuri katika uwanja huo lakini inabidi kuzingatia kuwa maendeleo hayo ni nyenzo na njia tu za kuweza kufikia kwenye sehemu ya kweli ya wenzo wa ustaarabu wa Kiislamu yaani kuishi maisha mepesi na kuwa na utaratibu mzuri wa maisha.
Katika upande wa nyenzo licha ya kuweko vitisho, vikwazo na mengineyo mfano wa hayo dhidi ya taifa hili, lakini nchi yetu imepata maendeleo mazuri. Lakini upande wa uhakika, ni kile kitu ambacho kinaunda maisha yetu; ambapo nimesema ni namna ya kuishi au mtindo wa maisha. Upande huu wa uhakika ndio sehemu kuu ya ustaarabu; kama vile masuala ya namna ya kuoa, aina ya nyumba, mtindo wa nguo, kigezo cha matumizi, aina ya vyakula, mapishi, suala la hati, burudani, kutafuta rizki na miamala ya mtu binafsi na jamii nzima katika mazingira tofauti, Chuo Kikuu, miamala yetu shuleni, miamala yetu katika harakati za kisiasa, miamala yetu katika michezo, miamala yetu katika vyombo vya habari ambavyo viko katika miliki yetu, muamala wetu na wazazi wetu (baba na mama), muamala wetu na wake zetu, muamala wetu na watoto wetu, muamala wetu na tunaowaongoza, muamala wetu na polisi, muamala wetu na afisa wa serikali, safari zetu, usafi, muamala wetu na rafiki na muamala wetu na adui haya yote ni sehemu kuu ya ustaarabu ambao ni mtindo wa maisha.
Ustaarabu mpya wa Kiislamu - ndio kile kitu ambacho tunataka kukitoa - ni ile inayounda sehemu ya uhakika. Katika maarifa na mafundisho matukufu ya Kiislamu, istilahi ya akili ya maisha inashabihiana na istilahi ya mtindo wa maisha sahihi na utamaduni mzuri wa kuishi katika maana yake pana na kwamba, kuna aya nyingi za Qur'ani Tukufu zinazolizungumzia jambo hilo. Haiwezekani kufikiwa malengo ya ustaarabu mkubwa wa Kiislamu bila ya kuwa na maendeleo katika sehemu halisi ya ujenzi wa ustaarabu mpya wa Kiislamu, yaani kuwa na mtindo sahihi wa maisha na utamaduni mzuri wa kuishi na kuongeza kuwa, ni jambo la kusikitisha kuona kuwa sisi katika sehemu hii ya ustaarabu mkubwa wa Kiislamu tumeshindwa kuwa na maendeleo mazuri bali tumeshindwa kuwa na maendeleo katika masuala yake ya kimsingi kama vile elimu, ufundi na vitu kama hivyo.
Vizuri, sehemu hii inahesabiwa kuwa sawa na program ya ustaarabu; na ile sehemu ya kwanza inahesabiwa kuwa sehemu za vifaa vya kompyuta. Ikiwa sisi hatutapiga maendeleo katika mtindo huu wa maisha, maendeleo yote tuliyoyapata katika sehemu ya kwanza hayawezi kutufanya sisi tufaulu; hayawezi kutupatia sisi usalama na utulivu wa kisaikolojia; kama ambavyo mnaona katika ulimwengu wa Magharibi hili hawajaweza kulipata. Katika ulimwengu wa Magharibi kuna msononeko, kukata tamaa, msambaratiko wa ndani, kutokuweko usalama wa watu katika mikusanyiko na katika familia, hakuna malengo; licha ya kuwa kuna utajiri, kuna bomu la atomiki, kuna maendeleo tofauti katika nyuga mbalimbali na kuna nguvu ya kijeshi. Hivyo basi asili ya kadhia ni hii kwamba, tuweze kufanyia marekebisho mtindo wa maisha katika sehemu hii kuu ya ustaarabu. Tab'an, katika mapinduzi na katika uga huu, maendeleo yetu sio makubwa; katika uga huu, sisi hatukufanya harakati kama tulivyofanya katika sehemu ya kwanza, hivyo hatukupata maendeleo katika uga huu. Hivyo basi kimsingi ni kuwa, haiwezekani kufikiwa malengo ya ustaarabu mkubwa wa Kiislamu bila ya kuwa na maendeleo katika sehemu halisi ya ujenzi wa ustaarabu mpya wa Kiislamu yaani kuwa na mtindo sahihi wa maisha na utamaduni mzuri wa kuishi na jambo la kusikitisha ni kuona kuwa sisi katika sehemu hii ya ustaarabu mkubwa wa Kiislamu tumeshindwa kuwa na maendeleo mazuri bali tumeshindwa kuwa na maendeleo katika masuala yake ya kimsingi.
Hivyo kuna haja ya kuchunguza mambo yanayoweza kukwamisha mambo; kwa nini hatukuweza kupata maendeleo katika uga huu? Baada ya kupata sababu, wakati huo sasa tuchunguze ni namna gani tunaweza kuyatibu haya. Haya ni majukumu ya nani? Haya ni mambo ambayo yanapaswa kufanywa na wenye vipaji - wenye vipawa vya kifikra na wenye vipaji vya kisiasa - yaani haya ni mambo ambayo ni majukumu yenu na nyinyi ndio mnaopaswa kuyafanya, nyinyi vijana. Endapo katika mazingira yetu ya kijamii kutajitokeza mazungumzo ambayo yanasimamia namna ya kuondoa mambo na vitu vinavyokwamisha mambo katika uwanja huu, tunaweza kuwa na uhakika kwamba, nishati ambayo Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu na taifa la Iran inayo sambamba na vipawa vilivyopo, tunaweza kupiga hatua na kupata maendeleo mazuri; bila ya shaka yoyote taifa la Iran litazidi kung'ara ulimwenguni na wakati huo huo ueneaji wa fikra za Kiislamu za taifa la Iran na Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran litakuwa jambo jepesi zaidi. Hivyo basi ni lazima kuweko jitihada za kweli za kuweza kujua masuala yanayoweza kukwamisha sehemu hiyo muhimu ya ustaarabu mpya wa Kiislamu na hatimaye kutafuta njia za kuondoa vizuizi hivyo na kisha kuyapatia tiba na ufumbuzi. Wenye majukumu katika uwanja huu ni wenye vipaji, Hawza (Chuo Kikuu cha Kidini), vyombo vya habari, Chuo Kikuu, watu wenye ushawishi; watu wenye jukumu la kuandaa vitabu vya masomo, watu wenye ushawishi wa masuala ya utamaduni na ufundishaji pamoja na vijana na watu ambao wanaandaa mitaala ya masomo kwa ajili ya shule na Vyuo Vikuu; hivyo basi wote hawa wana majukumu katika uwaja huu. Sote tunapaswa kufanya hima kubwa, tunapaswa kufanya kazi katika uwanja huu na kufanya harakati.
Hivyo basi ni lazima kuyafahamu masuala yanayokwamisha mambo; yaani kuna haja ya kuweko uzingatiaji katika uwanja huu kuhusiana na masuala yanayokwamisha mambo yaani kutafuta vitu vinavyokwamisha mambo. Tab'an, sisi hapa hatutaki kuonyesha kwamba, mambo yamekwisha; bali tunatoa faharasa: Kwa nini utamaduni wa kufanya kazi kwa pamoja katika jamii yetu ni dhaifu? Hiki ni kikwanzo kimoja. Licha ya kuwa, utamaduni wa kufanya kazi pamoja (yaani kushirikiana) unadaiwa kuandikishwa kwa jina la Wamagharibi, lakini Uislamu ulikwishalizungumzia jambo hilo miaka mingi. Mwenyezi Mungu anasema:
Na saidianeni katika wema na uchamngu. (al-Maida 5:02). Vile vile Mwenyezi Mungu anasema: Na shikamaneni kwa Kamba ya Mwenyezi Mungu nyote pamoja (Al-I'mran 3:103); yaani hata kushikamana na kambo ya Mwenyezi Mungu kunapaswa kufanyika kwa pamoja; "wala msifarikiane" (Al-I'mran 3:103); Kwa nini talaka ni nyingi katika baadhi ya maeneo? Kwa nini katika baadhi ya maeneo kunaongeza suala la vijana kuelekea katika madawa ya kulevya? Kwa nini hatuzingatii mambo yanayopaswa kufanywa katika mahusiano na majirani zetu? Kwa nini katika utamaduni wa kuendesha magari hakuchungwi sheria kama inavyotakiwa? Sheria za kuishi kwenye nyumba za ghorofa ni zipi na je zinachungwa? Ni vipi vielelezo vya burudani salama? Je tunaambiana ukweli wakati wote katika maisha yetu ya kila siku? Kusema uongo kumeenea kiasi katika jamii?
Ni kwa sababu gani kunashuhudiwa baadhi ya watu kupenda kuwashutumu wengine na kunakosekana hali ya kuvumulimiana baadhi ya watu katika jamii? Kazi ya kubuni mavazi na muundo wa miji ni kwa kiasi gani inakubalika kiakili na inafanyika kimantiki? Je sheria za watu zinachungwa katika vyombo vya habari na kwenye Intaneti? Ni zipi sababu za kuzuka ugonjwa hatari wa kukwepa sheria baadhi ya watu na baadhi ya sekta? Tunaheshimu kiasi gani jukumu la kutekeleza ipasavyo kazi zetu na mshikamano wa kijamii? Ni kwa kiasi gani tunazingatia ubora katika uzalishaji wa bidhaa zetu za ndani? Kwa nini baadhi ya fikra na mawazo mazuri yanaishia kwenye maneno tu? Kwa nini masaa ya kufanya kazi inavyotakiwa katika taasisi mbali mbali ni machache? Tufanye nini ili kufuta kabisa na kikamilifu mizizi ya riba? Je haki za mume, mke na watoto katika familia zinachungwa kikamilifu na kama inavyotakiwa? Kwa nini imekuwa ni fakhari kwa baadhi ya watu kutumia vibaya mali na vitu mbali mbali? Tufanye nini kuhakikisha kuwa heshima ya kifamilia ya mwanamke inalindwa na wakati huo huo aweze kutekeleza majukumu yake ya kijamii? Tufanye nini ili mwanamke asilazimike kumchagua mtu mmoja baina ya watu kadhaa? Kwa hakika haya ni miogoni mwa mambo ya kimsingi. Kwa nini katika baadhi ya miji mikubwa kuna nyumba za watu ambao hawajaoa wala kuolewa? Maradhi haya ya Magharibi yameweza vipi kupenya katika jamii yetu? Kupenda mapambo ni nini? Ni jambo zuri au baya? Ni baya kiasi gani? Ni zuri kiasi gani? Tufanye nini ili jambo hili lisifikie katika hatua mbaya? Kwa hakika sehemu mbalimbali za mambo yanayohusiana na mtindo wa maisha na kuna makumi ya masuala mengine; na haya niliyosema ni muhimu zaidi. Hii ni faharasa ya vitu ambavyo vinaunda mtindo wa maisha. Kutoa hukumu kuhusiana na ustaarabu fulani kunafungamana na mambo haya. Haiwezekani kutoa hukumu kuhusiana na ustaarabu fulani na kuusifia kutokana na kuwa una magari, una vuwanda na utajiri; ilhali ndani yake kuna matatizo haya mengi ambayo yamezunguka na kugubika jamii na maisha ya watu. Haya ndio mambo ya kimsingi; hizi ni nyenzo kwa ajili ya kudhamini sehemu hii ili wananchi wawe na raha, waishi wakiwa na matumaini, wakiwa na amani, wasonge mbele, wafanye harakati na hivyo kukwea daraja za juu za utu ambazo zinafaa.
Kuna jambo moja hapa linazungumziwa nalo ni utamaduni wa maisha. Sis tunapaswa kufuatilia suala la kubainisha utamaduni wa maisha, tuuandike na tuufanye Uislamu uwe na nafasi kama inavyotakiwa. Tab'an, Uislamu umetubainishia misingi ya utamaduni kama huu. Uislamu unalihesabu suala la kutumia busara, maadili bora na kuchungwa vizuri haki kuwa ni misingi mikuu ya utamaduni sahihi na sisi pia tunapaswa kulipa uzito wa hali ya juu suala hilo, vinginevyo maendeleo ya Kiislamu na ustaarabu mpya wa Kiislamu kamwe hautaweza kujengeka. Haya ni mambo ambayo Uislamu umetupatia.
Endapo sisi hatutajihusisha na haya kwa jaddi, maendeleo na ustawi wa Kiislamu hautopatikana na ustaarabu mpya wa Kiislamu hautaundika. Kadiri tutakavyopiga hatua katika uga wa viwanda na kusonga mbele, kadiri tutakavyosonga mbele katika uwanja wa uvumbuzi na ugunduzi, kama katika uga huu hatututengeneza mambo, tutakuwa hatujapata maendeleo ya Kiislamu kwa maana halisi ya kalima. Tunapaswa kufuatia uwanja huu pia, tufanye kazi sana; na tufanye hima na idili ya hali ya juu.
Kuna nukta mbili tatu ambazo zinapelekea hali hii ambazo tunapaswa kuzizingatia. Utamaduni sawa wa maisha sahihi unatokana na tafsiri zetu kuhusu maisha. Lengo la maisha ni nini? Lengo lolote tutakaloliainishia maisha yetu, ndilo litakaloainisha mtindo na muundo wa maalumu wa maisha hayo. Kuna nukta ya kimsingi ambayo ni imani. Tunapaswa kuainisha lengo fulani - lengo la maisha - na kisha tuliamini. Hakuna lengo lolote linaloweza kufanikishwa bila ya kuweko kwanza imani juu ya lengo hilo.
Bila ya imani, hakuwezi kupatikana maendeleo katika uwanja huu; kazi sahihi haiwezi kufanyika. Sasa kitu ambacho tunakiamini kinaweza kuwa ni uliberali, kinaweza kuwa uliberali, kinaweza kuwa ukomonisti, kinaweza kuwa ni ufashisti na kuweko na imani juu ya kila kimoja, ni kwa imani hii ndipo itikadi inaposonga mbele. Suala la imani ni muhimu. Imani ni asili na imani ni nguzo kuu ya itikadi; kuna haja ya kuweko imani kama hii. Ni kwa mujibu wa msingi wa imani hii ndipo mtindo wa maisha utakapochaguliwa. Katika hili kuna ukanganyaji mambo ambapo mimi ninawaambia kwamba, kuna wanafalsafa kadhaa wenye nembo ya Umagharibi wamezungumzia suala la kupingana na aidiolojia. Bila shaka mnaona katika baadhi ya makala za wanafikra kuna jambo linalozungumziwa kwa anuani ya kupambana na aidiolojia: Wanadai, haiwezekani kuiongoza jamii kwa aidiolojia. Wanafalsafa kadhaa au wanafalsafa wenye nembo ya Umagharibi wamesema hili kisha baadhi ya watu hapa nchini bila ya kudiriki uhakika na ukweli halisi wa maneno haya na bila hata ya kufahamu malengo na engo ya maneno haya ni nini, wamekuja na kukariri haya haya, na bado wanakariri haya. Hakuna taifa lolote lile linalodai kuunda ustaarabu, ambalo linaweza kufanya harakati bila ya kuwa na aidiolojia. Hakuna taifa lolote lile ambalo linaweza kuunda ustaarabu bila ya kuwa na fikra, aidiolojia na chuo.
Haya haya ambayo mnayashuhudia leo yameletwa katika ulimwengu wa ustaarabu wa kimaada, yamekuja na kuingia kwa wenzo wa aidiolojia; walisema kweli; walisema, sisi ni Wakoministi, walisema sisi ni mabepari, walisema sisi tunaamini ubeberu wa kiuchumi; walikuja na kulizungumzia hilo, wakaliamini na kisha wakalifanyia kazi; tab'an, walikumbana na matatizo katika hilo na waligharamika mno. Hivyo basi bila ya kuwa na chuo, bila ya kuwa na fikra, imani na bila ya kufanya hima na juhudi kwa ajili ya hilo na kugharamika kwa ajili ya jambo hilo, kuunda ustaarabu ni jambo ambalo halitawezekana.
Ni kweli kuna baadhi ya nchi zinafuata tu ustaarabu wa Magharibi bila ya kutumia vyuo vyao vya kifikra na kiaidiliojia na nchi hizo hata zinaweza kupata maendeleo ya kiasi fulani lakini madhara ya utegemezi wao kwa Magharibi ni makubwa mno, na utambulisho wa nchi hizo hupotea na ndio maana kinapotokezea kimbunga, nchi hizo zinakuwa dhaifu na haziwezi kabisa kukabiliana na kimbunga hicho, kutokana na kuwa haziko imara na hazina msingi madhubuti. Mbali na kuwa kazi yao ni ya kuiga, na kuiga huko kunawadhuru, hufanikiwa kupata baadhi ya manufaa ya kimaada ya Kimagharibi na mengi kati ya hayo hawayapati, lakini wakati huo huo madhara yote hupata wao.
Tofauti na nchi hizo zinazofuata tu ustaarabu wa Magharibi, mataifa ambayo yanasimama kukabiliana na ustaarabu huo huchagua kufuata chuo cha Tawhidi na hivyo kupata maendeleo ya kweli na ya pande zote na kufanikiwa pia kujenga ustaarabu wenye mizizi madhubuti na makini ya kuwezesha fikra na utamaduni wao kuenea kote ulimwenguni.
Kwa hakika mimi sitaki kutaja majina ya nchi. Kuna baadhi ya nchi ambazo ustawi na ukuaji wa uchumi wao ni kigezo na mfano wa kuigwa na katika maneno na maandishi baadhi ya wanafikra wetu hutajwa. Ndio, yamkini nchi hizo zikafanikiwa kupata teknolojia ya viwanda na zikapata maendeleo pia katika uga wa kimaada au katika uwanja wa elimu na viwanda, lakini kwanza maendeleo hayo ni ya kuiga; ni ya madhila na yamepigwa alama (muhuri) muhimu katika nyuso zao kwamba, maendeleo na ustawi huo sio wa kwao ni tegemezi; fauka ya hayo, hivi sasa zina madhara yanayotokana na ustaarabu wa kimaada wa Kimagharibi ilhali hazina manufaa mengi; kwa maana kwamba, madhara ni makubwa na mengi kuliko manufaa. Hii leo ustaarabu huu wa kimaada wa Magharibi unaonesha matatizo mengi ambayo umemletea mwanaadamu na wafuasi wake.
Hivyo basi bila chuo, bila ya kuwa na aidiolojia haiwezekani kuleta ustaarabu fulani; kuna haja ya kuwa na imani. Ustaarabu huu utakuwa na elimu, utakuwa na teknolojia ya viwanda na vile vile utakuwa na maendeleo; na utamaduni huu utakuwa mwongozaji na utakuwa msimamizi wa yote haya. Kile kinachokifanya chuo cha Tawhidi kuwa msingi wa kazi zake, ni ile jamii ambayo inafanya harakati kufuata Tawhidi ambayo kwa hakika itafanikiwa kupata kheri zote hizi ambazo zinategemea ujengaji wa ustaarabu; na kwa muktadha huo kutapatikana ustaarabu mkubwa, wa kina na wenye mizizi na utaweza kueneza fikra na utamaduni wake ulimwenguni. Kwa msingi huo, haya matilaba ya kwanza yanahitajia imani. Kuivuta jamii kuelekea upande wa kutokuwa na imani, ni moja ya zile njama za maadui wa uundwaji wa ustaarabu wa Kiislamu ambao wamekuwa wakilifuatilia hilo daima na hivi sasa wanalifuatilia hilo kwa nguvu na kasi kubwa.
Hii leo katika mazingira ya kuainisha fikra, kuna watu ambao wakiwa na nyuso tofauti tofauti wamekuwa wakitutahadharisha kuhusiana na nara za chuo, nara hizi ambazo kimsingi kilele chake kilikuwa muongo wa 60 wanakuja na kuzitilia alama ya swali; hii leo pia wana shaka na kukaririwa nara za chuo na nara za mapinduzi na nara za Kiislamu, hivyo wanataka watu wengine pia wawe kama wao; wanadai kwamba, bwana wee kuna gharama, kuna mushkili, kuna vikwazo na kuna vitisho; yaani kushikamana na chuo na maktaba ya Kiislamu ni jambo ambalo litapelekea kuandamwa na mambo haya. Kwa mtazamo wa mzuri tunaweza kusema kuwa, watu hawa hawajasoma historia - tab'an, kuna mtazamo mbaya pia kuhusiana na watu hawa - laiti kama watu hawa wangelisoma historian na wangekuwa na ufahamu kuhusiana na na chimbuko na chanzo cha staarabu ambazo ziko leo na staarabu hizi za kimaada za Magharibi ambazo leo zinataka kuidhibiti duniani, wasingeyasema haya. Tunapaswa kusema kuwa, watu hawa hawajui kitu na hawajasoma historia.
Jamii ambayo haina matukufu, haina chuo na haina imani, yamkini ikapata utajiri, yamkini ikafanikiwa kuwa na nguvu, lakini wakati inapofikia katika utajiri na nguvu, ndio kwanza huwa mnyama aliyeshiba na mwenye nguvu - na thamani ya mwanadamu mwenye njaa ni bora zaidi ya mnyama aliyeshiba - Uislamu hautaki hili. Uislamu ni mfuasi wa binadamu ambaye ana nguvu, mwenye kushukuru na wakati huo huo ni mja wa Mwenyezi Mungu; ajenge kambi ya uja na kumuabudu Mwenyezi Mungu katika ardhi. Kuwa na ubinadamu, kuwa na nguvu, kuwa ni mja wa Mwenyezi Mungu; hivi ni vitu ambavyo Uislamu unavitaka; unataka kumjenga mtu na kujenga kigezo kwa ajili ya mwanaadamu.
Hivyo basi katika hatua na daraja ya kwanza, hitajio la kujenga ustaarabu mpya wa Kiislamu ni imani. Ni kwa imani hii ndipo sisi tumekuwa ni wenye kuitakidi na kuuamini Uslamu. Imani yetu ni imani kwa Uislamu. Katika kivuli cha akhlaqi na maadili ya Kiislamu na katika adabu za maisha ya Kiislamu tunaweza kupata kila ambacho ni hitajio kwetu; hivyo tunapaswa kuyafanya haya kuwa mhimili wa mjadala na uhakiki wetu. Sisi katika Fikihi ya Kiislamu na Sharia za Kiislamu tumefanya kazi nyingi; tunapaswa pia kufanya kazi kubwa katika uga wa akhlaqi na maadili ya Kiislamu, akili na amali ya Kiislamu na tuyafanye hayo kwa ubora kabisa - Vyuo Vikuu vya Kidini (Hawza zina majukumu katika hili, wasomi, wahakiki, watafiti, Chuo Kikuu na wanachuo wana majukumu katika hili pia - tuyafanye hayo kuwa msingi wa uandaaji ratiba zetu, tuyaingize haya katika mitaala yetu ya masomo; hiki ni kitu ambacho kwa hakika tunakihitajia leo na ni lazima tukifuatilie. Hii ni matilaba na nukta ya kwanza katika mlango wa uundaji wa ustaarabu mpya wa Kiislamu na katika kupata na kufikia sehemu hii muhimu na ya kimsingi ya ustaarabu ambayo ni tabia ya kivitendo.
Hakuna hata kitu kimoja kati ya hivi ambavyo mimi nimevitaja ambavyo nyinyi mnaweza kuvipata iwe ni kwa sura jumla au makhsusi ya kwamba, havijazungumziwa katika Uislamu.
Aina ya tabia na miamala ya mtu na watu ambao ana mahusiano nao, aina ya miamala yetu, aina ya vitu ambavyo viko katika maisha ya kijamii kwa ajili ya mwanadamu, haya ni mambo ambayo yako katika Uislamu; mambo yanayohusiana na safari yapo, kuhusiana na kwenda na kurejea pia nayo yapo, mambo yanayohusiana na kupanda na kuteremka yapo, mambo yanahusiana na baba na mama yapo, mambo yanayohusiana na ushirikiano yapo, katika uwanja wa jinsi ya kuamiliana na rafiki yapo na mambo yanayohusiana na jinsi ya kuamiliana na adui nayo yapo na yamezungumziwa na Uislamu. Uislamu umezungumzia kuhusiana na kila kitu, imma mambo hayo yamezungumziwa kwa sura maalumu katika vyanzo vyetu vya Uislamu au chini ya anuani jumla; ambapo watu ambao ni wasomi na wana nadharia wanaweza kuyachimbua mambo hayo ambayo ni hitajio na kuyaweka wazi mbele ya macho ya watu.
Hapa kuna nukta ya pili nayo ni hii kwamba, ili sisi tujenge sehemu hii ya ustaarabu mpya wa Kiislamu, tunapaswa kujiepusha mno na suala la kuiga na kufuata; kuwaiga wale watu ambao wanafanya kila wawezalo kuwatwisha watu mitindo ya maisha, aina na miamala ya maisha. Hii leo madhihirisho kamili yaliyoko ni madhihirisho ya huu utumiaji mabavu na utwishaji mambo wa ustaarabu wa Kimagharibi.
Kwa hakika kuwa na uadui na Magharibi na kuwachukia Wamagharibi sio jambo la hisia, bali jambo hili linatokana na uchunguzi. Baadhi ya watu linapotajwa tu jina la Magharibi, ustaarabu wa Magharibi, mitindo ya Magharibi, njama za Magharibi na uadui wa Magharibi, huanza kushambulia suala la chuki dhidi ya Magharibi: hujitokeza na kusema, bwana we nyinyi mna uadui na Magharibi. Hapana, sisi hatuna uadui na Magharibi kiasi hicho - tab'an, tuna uadui! - Hatuna misingi ya kupinga Magharibi lakini kwa mujibu wa uchunguzi na uhakiki wa kina ni kuwa, kuifuata Magharibi hakulifikishi popote taifa lolote lile.
Kuifuata Magharibi kwa nchi ambazo ambazo zimeamua kufanya hivyo ni jambo ambalo halijawa na faida kwao ghairi ya madhara na maafa; hata zile nchi ambazo kidhahiri zimeweza kufikia hatua ya kuitwa nchi za viwanda, uvumbuzi na utajiri, bado zingali zinafuata na kuiga. Sababu ni kuwa, utamaduni wa Magharibi kimsingi ni utamaduni wa kushambulia. Utamaduni wa Magharibi ni utamaduni ambao unaangamiza tamaduni nyingine. Kila mahala ambapo Wamagharibi waliingia, tamaduni za kienyeji ziliangamia na misingi ya kijamii ikateketea; walifanya njama za kubadilisha historia kadiri walivyoweza, wakabadilisha lugha ya wenyeji na hata hati zao. Kila mahala ambapo Waingereza waliingia, walibadilisha lugha ya wenyeji na kuifanya kuwa Kiingereza; kama kulikuwa na lugha ya mshindani mwenzao basi waliiangamiza na kuiteketeza.
Katika bara Hindi, kwa karne kadhaa lugha ya Kifarsi ilikuwa lugha rasmi; maandiko yote, mikataba rasmi, barua za utawala, serikali, wananchi, wanafunzi, shule na shakhsia mahiri zilikuwa zikiandikwa kwa lugha ya Kifarsi. Waingereza wakaja na wakapiga marufuku lugha ya Kifarsi huko India kwa kutumia mabavu na kisha wakaeneza lugha ya Kiingereza. Bara Hindi, kilikuwa moja ya kituo muhimu cha lugha ya Kifarsi, hii leo lugha ya Kifarsi katika eneo hilo ni ngeni; lakini lugha ya Kiingereza, ni lugha ya mahakama; maandiko ya serikali yanaandikwa kwa lugha ya Kiingereza na hata watu wenye vipawa wa bara Hindi wanazungumza Kiingereza - ni lazima wazungumze Kiingereza - hili ni jambo ambalo limetwisha na kulazimishwa. Katika nchi zote ambazo katika kipindi cha ukoloni Waingereza walikuweko huko, jambo hili lilitokea; lilitwishwa na kulazimishwa. Kwa hakika sisi hakuna mahala ambapo tumeitwisha lugha ya Kifarsi.
Lugha ya Kifarsi ambayo katika India ilikuwa imeenea, ilipokelewa kwa mikono miwili na Wahindi wenyewe; shakhsia wa Kihindi walijitokeza wao wenyewe na kutunga mashairi kwa lugha ya Kifarsi.
Kuanzia karne ya saba na nane Hijria hadi katika kipindi cha mwishoni kabla ya kuingia huko Waingereza, kulikuwa na washairi na malenga wengi ambao walikuwa wakitunga na kusoma mashairi kwa lugha ya Kiafarsi; kama vile Amir Khusrau Dehlavi - ambaye asili yake ilikuwa ni mjini Delhi - na washairi wengine wengi. Allama Iqbal Lahore ambaye alikuwa mtu wa Lahore lakini mashairi yake ya Kifarsi ni mashuhuri zaidi kuliko ya lugha nyingine. Kwa hakika sisi hatukufanya jitihada za kueneza Kifarsi huko India kama walivyofanya Waingereza ili Kiingereza kienea katika India; lugha ya Kifarsi ilienea kwa mapenzi na shauku ya watu wa India sambamba na safari za washairi, maurafaa, wasomi na kadhalika; lakini Waingereza wao walikuja na kuwalazimisha watu wasiongee Kifarsi; hawakukataza kwa mdomo tu bali waliainisha adhabu maalumu kwa mtuatakayepatikana anazungumza au anaandika kwa lugha ya Kifarsi.
Wafaransa nao katika nchi ambazo zilikuwa makoloni yao katika zama za ukoloni, nao waliwatwisha watu lugha ya Kifaransa. Kuna wakati mmoja wa Marais wa nchi za kaskazini mwa Afrika - ambayo kwa miaka kadhaa ilikuwa chini ya udhibiti wa Ufaransa - alikutana na mimi kipindi hicho nikiwa Rais. Akawa anazungumza na mimi kwa lugha ya Kiarabu; kisha akataka kusema kitu lakini neno la kiarabu la kitu hicho likawa limemtoka, yaani hakuwa akijua neno hilo kwa Kiarabu. Makamu wake au waziri wake ambaye alifuatana naye, akamwambia kwa Kiafaransa kwamba, neno hilo kwa Kiarabu ni nini? Kisha naye akasema ndio neno hili kwa Kiarabu ni hivi.
Hii ina maana kwamba, mtu ambaye asili yake ni Mwarabu, lakini hawezi kufikisha madhumuni yake kwa lugha ya Kiarabu na badala yake analazimika kumuuliza rafiki yake kwa Kifaransa, kisha naye aje na kusema neno hilo! Yaani hali imefikia hatua hii mtu kusahau lugha yake ya asili na kuwa mbali na lugha hiyo kiasi hiki? Hili ni jambo ambalo nchi yao ilitwishwa kwa miaka mingi. Wareno nao ni hivyo hivyo, Waholanzi nao kadhalika, Wahispania nao walifanya hivyo hivyo; kila mahala walipokwenda waliwatwisha watu lugha yao; kwa hivyo huu unakuwa ni utamaduni wa kushambulia. Kwa muktadha huo basi, utamaduni wa Magharibi siku zote ni utamaduni wa kushambulia.
Wamagharibi walifanya kadiri walivyoweza kusambaratisha misingi ya utamaduni na kiitikadi. Katika nchi kama yetu hakukuweko na ukoloni na hali ya kukoloniwa ya moja kwa moja na kwa baraka za mapambano ya shakhsia fulani wakubwa, Waingereza hawakuweza kuingia hapa nchini kwa njia ya moja kwa moja, walikuja na kuwafanya baadhi ya watu kuwa ni vibaraka wao. Kama mkataba wa mwaka 1299 yaani 1919 Miladia - ambao ni maarufu kwa mkataba wa "Vossouqoddowleh" - usingekabiliwa na upinzani nchini Iran wa watu kama Marhumu Mudarres na baadhi ya wapigania ukombozi na hivyo kutekelezwa kivitendo mkataba huo, kukoloniwa Iran lingekuwa jambo la lazima kutokea - kama India - lakini shakhsia hao hawakuruhusu hilo litokee.
Hata hivyo Waingereza wakiwatumia vibaraka wao, kwa kumpandikiza Rezakhan Pahlavi, wakampa nguvu sambamba na kuwaweka kando yake wanafikra na watu tegemezi kwa Magharibi - ambapo sio lazima pia kutaja majina hapa, sipendelei kutaja jina - wakatutwisha (Waingereza) utamaduni wao. Baadhi ya mawaziri na wenye vipawa vya kisiasa katika utawala na serikali ya Pahlavi walikuwa ni wanautamaduni, lakini walikuwa vibaraka wa Magharibi waliowekwa hapo kwa ajili ya kuusambaratisha na kuubadilisha utamaduni wa nchi yetu; na walifanya kadiri walivyoweza; mfano wake ni kuondolewa hijabu, mashinikizo dhidi ya watu wa dini na mifano mingine mingi ambayo ilikuwa ikifuatiliwa katika kipindi cha utawala wa Rezakhan Pahlavi.
Utamaduni wa Magharibi ni utamaduni wa kushambulia; kila mahala unapoingia huharibu mambo na kupambana na utambulisho; na hivyo kusambaratisha utambulisho wa wananchi wa taifa husika. Utamaduni wa Magharibi unazifanya fikra na akili kuwa ni za kimaada, unalea watu wawe na mitazamo na fikra za kimaada; hivyo malengo ya maisha yanakuwa ni fedha na utajiri na wakati huo huo, malengo makuu, matukufu na malengo ya kimaanawi na aali ya kiroho hufutwa katika fikra na akili za watu. Hii ndio sifa maalumu ya utamaduni wa Magharibi.
Sifa nyingine ya utamaduni wa Magharibi ni kulifanya suala la dhambi kuwa ni jambo la kawaida; utamaduni huo (utamaduni wa Magharibi) unafanya madhambi ya uasherati kuwa ni jambo la kawaida. Hii leo hali hii imeuumbua hata ulimwengu wa Magharibi wenyewe; kwanza Uingereza na kisha baadaye katika nchi nyingine na Marekani. Inasikitisha kwamba, dhambi kubwa ya mahusiano haramu ya watu wa jinsia moja imegeuka na kuwa ni thamani! Hata imefikia hatua mwanasiasa fulani analamikiwa eti kwa nini anasimama na kupinga mahusiano ya watu wa jinsia moja, au anawapinga watu wenye mahusiano ya jinsia moja! Tazameni mmonyoko wa maadili umefikia kiwango gani. Huu ndio utamaduni wa Magharibi. Vile vile kusambaratika familia, kuenea ulevi na utumiaji wa pombe sambamba na kukithiri utumiaji (uraibu) wa madawa ya kulevya. Mimi miaka ya nyuma - katika muongo wa 30 na 40 - nilikutana na shakhsia na watu wakubwa wa kifikra na wazee wenye hekima katika eneo la kusini mwa Khorasan ambao walikuwa wangali wanakumbuka jinsi Waingereza walivyokuwa wakieneza kasumba baina ya wananchi kwa kutumia mbinu maalumu; kwa hakika kiasili wananchi hawakuwa watumiaji wa kasumba; vitu hivi havikuweko kabisa. Watu hawa walikuwa wakikumbuka. Na ni kwa mikakati na mbinu hizi hizi suala la madawa ya kulevya likaenea ndani ya nchi. Utamaduni wa Magharibi uko namna hii.
Utamaduni wa Magharibi sio ndege, suhula za kurahisisha maisha na nyenzo za haraka na wepesi tu; hapana, gamba la juu la utamaduni wa Magharibi linaonesha kuwa utamaduni umeleta maendeleo ya kijuu juu lakini unapoangalia batini na dhati ya utamaduni huo utaona kuwa umejengeka juu ya msingi wa mtindo wa maisha ya kimaada na uasherati, hawaa na matamanio yaa nafsi na uchafu wa kimaadili, kukosa utambulisho na kupambana na umaanawi. Sharti la kufikia ustaarabu mpya wa Kiislamu katika hatua ya awali ni kujiepusha na suala la kufuata na kuiga Wamagharibi. Inasikitisha kuwa, sisi katika kipindi cha miaka mingi tumezoea kuiga mambo mbalimbali.
Mimi sio kwamba, ni mfuasi wa kwamba, kwa mfano kuhusiana na suala la mavazi, nyumba na vitu vingine ghafla moja kufanyike harakati ya pamoja na ya wote ya mabadiliko; hapana, kazi hii inapaswa kufanyika hatua kwa hatua; sio amri pia; haya ni mambo ambayo yanahitajia uundaji wa utamaduni. Kama nilivyosema, hii ni kazi ya wenye vipawa na watu wa masuala ya kiutamaduni. Na nyinyi vijana mnapaswa kujiandaa kwa ajili ya hili; huu ndio ujumbe mkuu.
Sisi tunaeneza elimu., tunaeneza viwanda, tunaeneza uvumbuzi na mambo mapya, tunamheshimu kila mvumbuzi na uvumbuzi na tunaupokea kwa heshima na taadhima kubwa na kuuthamini - haya ni mambo ambayo yanahifadhiwa - lakini kama tulivyosema, asili ya kadhia ni sehemu nyingine; asili ya kadhia ni kutengeneza mtindo wa maisha, miamala ya kijamii, maadili ya jamii na utamaduni wa maisha. Tunapaswa kusonga mbele katika uga huu; ni lazima tufanye hima na idili. Ustaarabu mpya wa Kiislamu ambao sisi tunaudai, tunaufuatilia na mapinduzi ya Kiislamu yanataka kuuleta, katu hili halitowezekana pasina ya kuweko sehemu hii. Endapo ustaarabu huo utapatikana, wakati huo taifa la Iran litakuwa katika kilele cha izza, heshima na utukufu; hilo litafuatiwa na utajiri, litafuatia na maisha mazuri, litafuatiwa na usalama, izza ya kimataifa pia itapatikana; hivyo kila kitu kitapatikana sambamba na umaanawi.
Moja kati ya nukta ambazo ni lazima kuzingatia kikamilifu katika kukabiliana na ulimwengu wa Magharibi ni nyenzo na suhula za kisanaa ambazo ziko katika ulimwengu wa Magharibi. Kwa hakika ulimwengu wa Magharibi umestafidi kadiri unavyoweza na sanaa kwa ajili ya kueneza utamaduni ghalati, mbovu na unaoua utambulisho; hususan sanaa ya maonyesho, hususan sanaa ya sinema wametumia kadiri walivyoweza.
Kwa hakika ulimwengu wa Magharibi hutelekeza mpango wa kulisoma kwanza taifa fulani, huchunguza na kugundua nukta dhaifu za nchi husika, huwatumia wataalamu wa masuala ya kisaikolojia, wataalamu wa masuala ya elimu jamii, historia na wasanii na kisha kufahamu njia za kuweza kulidhibiti taifa hilo; kisha baada ya hapo huitaka taasisi fulani ya sanaa katika Hollywood (Taasisi ya Kutengeneza Filamu Marekani) kutengeneza filamu na taasisi hiyo hutekeleza agizo hilo. Akthari ya filamu zinazotengenezwa kwa ajili yetu na kwa ajili ya nchi mfano wetu huwa namna hii.
Mimi sina habari na filamu za ndani ya Marekani; lakini kuhusiana na kile wanachokiteneza kwa ajili ya mataifa mengine huwa ni za kushambulia. Miaka kadhaa iliyopita kulitangazwa habari kwamba, baadhi ya nchi kubwa za Ulaya zimeamua kukabiliana na filamu za Marekani. Wao sio Waislamu, lakini wanahisi filamu hizo ni tishio na hatari kwao; wao pia walikuwa wanahisi kushambuliwa na filamu hizo. Tab'an, tukija katika nchi za Kislamu hisia hiyo ni kubwa zaidi na kuhusiana na nchi yetu ya kimapinduzi hisia hii ni maalumu; hutazama na kupima sifa na hali ya nchi yetu na kisha kutengeneza filamu kwa mujibu wake, huandaa habari kwa mujibu wake na huanzisha vyombo vya habari kwa msingi ule na kutangaza habari. Haya ni mambo ambayo yanapaswa kuzingatiwa sana na kupewa kipaumbele maalumu. Huandaa mambo kwa dhuku zao na hutengeneza utamaduni; baada ya kuwa wamebadilisha dhuku, wakati huo kama kutahitakika utumiaji mabavu, basi hutumia mabavu na kama kutahitajika kununua watu kwa dola (za Kimarekani), basi humimina dola hizo na hata ikibidi huingiza wanajeshi na majerali ili wafikie lengo lao.
Huu ndio mkakati na mbinu za harakati za Wamagharibi; kwa msingi huo, bila shaka kuna haja ya kuwa macho na makini. Watu wote wanapaswa kuhisi kwamba, jukumu la kuleta ustaarabu mpya wa Kiislamu liko mabegani mwao; na moja ya kulifikia hilo ni kupambana na ustaarabu wa Magharibi, kwa namna ambayo itapelekea watu wasifuate na kuiga utamaduni na ustaarabu wa Magharibi.
Mwishoni, ninapenda kuongezea nukta moja: Kwa hakika mjadala wetu wa leo ni mwanzo wa mjadala; Inshallah tutazungumza katika fursa nyingine katika uwanja huu. Tuna matarajio kwamba, watu wa fikra na watu wenye maoni katika vituo husika ambao wanaweza na ni watu wenye ustahiki na kazi hii, watafanya kazi katika uga huu, watafikiri na kufanya utafiti, ili tuweze kusonga mbele. Tuwe makini tusije tukakumbwa na hali ya kutazama mambo kijuujuu na kidhahiri, tusikumbwe na hali ya kutazama mambo kwa mgando (ufinyu) wa fikra - huu ni upande mmoja wa kadhia - tusikumbwe na hali ya usekula uliojificha. Wakati mwingine kidhahiri, tablighi huwa ni tablighi za kidini; maneno huwa ni maneno ya kidini; nara na kauli mbinu huwa ni za kidini; lakini katika batini huweko hali ya usekula; kutenganisha dini na maisha; kile ambacho kinatamkwa hakiko katika mipango na katika utekelezaji. Tunadai, tunasema na kutoa nara; lakini inapofikia suala la kutekeleza mambo hayo kivitendo, huwa hakuna kabisa yale tuliyokuwa tukiyasema, kuyapigia upatu na kuyatolea nara.
Mapinduzi ya Kiislamu yana nguvu. Ule uwezo na nguvu pamoja na utajiri mwingi ulioko katika Mapinduzi ya Kiislamu, mapinduzi haya yana uwezo wa kuondoa vikwazo na vizingiti vyote tulivyovitaja na vingi ambavyo hatujavisema na hivyo kuweka mbele ya macho ya walimwengu ule ustaarabu ambao ni bora na mzuri wa Kiislamu; na hili ni jambo ambalo litatokea katika zama zenu, Inshallah litafanywa na nyinyi na kwa hima na idili yenu hili litatokea. Hivyo jiimarisheni kielimu, kivitendo, kujitakasa kinafsi, kiroho na kimwili kadiri mnavyoweza - kama ambavyo nimesema mara nyingi - jiandaeni ili Inshallah muweze kubeba katika mabega yenu huu mzigo mzito.

Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

 
< Nyuma   Mbele >

^