Skip to content

Habari

Habari
Hifadhi

Risala na Barua

Matini
Hifadhi

Kumbukumbu na Simulizi

Kabla ya Mapinduzi
Baada ya Mapinduzi

Sauti na Taswira

Picha
Sauti
Video
Hotuba ya Kiongozi Muadhamu Mbele ya Hadhara Kubwa ya Wananchi wa Shirvan Chapa
15/10/2012
Ifuatayo ni matini kamili ya hotuba ya Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aliyoitoa katika mkutano wa hadhara na mjumuiko mkubwa wa makumi ya maelfu ya wananchi wa mji wa Shirvan na maeneo ya pembeni mwa mji huo tarehe 15/10/2012.

Kwa jina la Allah Mwingi wa rehma Mwenye kurehemu

Hamdu zote zinamstahikia Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wa viumbe pia. Na rehma na amani zimfikie Bwana Mtume Mtukufu Muhammad SAW, Mkweli Mwaminifu na Aali zake wema na watoharifu, wateule, maasumina na waongozaji hususan Baqiyatullah katika ardhi (Imam Mahdi roho zetu ziwe fidia kwake).
Ninamshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu ambaye amenipa tawfiki mimi mja dhaifu ya kuweza kukutana na nyinyi wananchi azizi, wenye imani na wenye mapenzi makubwa wa Shirvan na kuwa katika mkusanyiko wenu huu uliojaa hamasa, huba na mapenzi makubwa. Kwa hakika nina kumbukumbu nzuri na mji wenu huu na nyinyi pia wananchi wa mji huu. Katika kipindi cha mitihani mikubwa na tata, mji wa Shirvan ulikuwa ni miongoni mwa maeneo ambayo yalifaulu vizuri katika mtihani huo na kujijengea jina zuri kabisa.
Mbali na wananchi azizi wa mji wa Shirvan na viunga vyake kutoa maelfu ya mashahidi na majeruhi wa vita katika kipidi cha kujihami kutakatifu (katika vita vya kulazimishwa vya miaka minane vilivyoanzishwa na utawala wa dikteta wa zamani wa Iraq Saddam Hussein) pia kuna majina ya makamanda saba kati ya mashahidi wa eneo hili. Kuwatayarisha makamanda na kuwapeleka katika medani ya vita kwa ajili ya kuongoza na kusimamia medani ngumu na kisha kuuawa shahidi katika njia hiyo sio matukio ambayo historia inaweza kuyasahau. Hii leo licha ya kweko maelfu kadhaa ya mabasiji katika mji huu, kuna kamati pia za kidini ambazo ziko amilifu katika mji huu. Aidha kuna watu wenye vipaji vya kiutamaduni na michezo ambao nao wanapatikana katika mji huu. Haya ni mambo ambayo yanaonesha utambulisho wa kila eneo hapa nchini. Vijana wetu azizi - iwe ni wa mji huu au wa miji mingine ya mkoa huu - wanapaswa kujifakarisha kutokana na mafanikio haya na wajiandae kwa ajili ya kazi kubwa zaidi katika mustakbali.
Moja ya mambo yanaoufanya mji huu na mkoa huu kuwa muhimu - ambapo mambo muhimu na mahiri ya mji huu yanahisika kikamifu - ni kuishi pamoja kaumu mbalimbali; kwani kuna Wakurdi, Waturuki, Wafaursi na Watati ambao wanaishi pamoja katika mji huu. Kwa hakika kaumu hii zimekuwa zikiishi pamoja kidugu na kwa amani na bila matatizo yoyote yale baina yao. Inshallah, vijana wenu, wake kwa waume wataweza kuipatia jamii sura zingine zenye kung'ara katika mstakbali wa nchi yao azizi na kwa ajili ya izza na heshima ya mapinduzi yao na kwa hakika haya ni matumaini ambayo sio vigumu kuyafikia. Kile ambacho mimi ninapenda kuwaeleza nyinyi makaka na madada wapendwa wa Shirvan ni kuwa, hima na idili ya wananchi wetu azizi, kuwa macho, makini, kuwa na welewa na ufahamu sambamba na kuwa na muono wa mbali wa wananchi azizi wa mkoa huu na wa mikoa mingine ya hapa nchini, kumeifanya nchi yetu iwe na uthabiti wa kudumu wa kisiasa; huu ni ujazi na neema kubwa. Moja ya silaha zinazotumiwa na madola makubwa, ya kibeberu na vamizi ulimwenguni ni kuzusha machafuko na hali ya ukosefu wa uthabiti ambapo mifano ya haya mnaishuhudia katika eneo letu hili (Mashariki ya Kati) na katika maene mengine duniani. Mnaona madola ya kibeberu kila mahala yalipoweza na kila mahala yalipoingiwa na tamaa na uchu, ili yawe na satua na ushawishi wake pamoja na kukita makucha yake katika nchi hizo yalileta hali ya ukosefu wa amani na uthabiti baina ya wananchi wa nchi hiyo na nchi jirani; huzusha hitilafu na machafuko ili kuweko na hali ya ukosefu wa amani na uthabiti. Kwa muktadha huo, watumie hali hiyo ya ukosefu wa amani na uthabiti kwa ajili ya kutegeneza silaha na hivyo kuyapatia faida kubwa mashirika makubwa ya kiuchumi ambayo yana udhibiti na ushawishi katika vyombo vya kisiasa vya Magharibi. Hii leo moja ya sera za siasa za vyombo vya Uistikbari ni kuzusha vurugu, machafuko na hali ya ukosefu wa uthabiti. Wakati huo katika mazingira kama haya Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu kwa baraka za imani yenu nyinyi wananchi, kwa baraka za muono wa mbali ambao umepatikana baina ya wananchi kwa fadhila za Mwenyezi Mungu, taifa hili limeweza kutoa pigo kwa maadui na hivyo kufanikiwa kuleta nchi ambayo ni imara na yenye uthabiti.
Kwa hakika wananchi wenyewe ndio ngao ya uimara na uthabiti huu ambao unashuhudiwa hapa nchini; tab'an, faida ya uimara na uthabiti huu ambao upo katika mfumo wa kisiasa hapa nchini inawarejea zaidi wananchi wenyewe wa taifa hili la Kiislamu. Endapo taifa fulani litakuwa na amani, litakuwa na uthabiti wa kisiasa na wananchi kunufaika na utulivu wa vyombo husika na vinavyotawala serikalini, wananchi ha watapata fursa ya kuingia katika medani mbalimbali na kuwa mstari wa mbele katika nyuga mbalimbali kwa ajili ya taifa lao. Usalama na utulivu wa nchi ni miongoni mwa matakwa na faida zinazowarejea wananchi wa taifa husika. Katika Qur'ani Tukufu katika Surat al-Fat'h - ushindi wa Waislamu unaarifishwa kwa Mtume SAW na watu kuwa ni neema kubwa - Mwenyezi Mungu anasema:
Mwenyezi Mungu aliteremsha utulivu juu ya Mtume wake na juu ya Waumini, na akawalazimisha neno la kuchamngu. Na wao walikuwa ndio wenye haki nalo na wenye kustahili (Al-Fat'h 48:26).
Katika aya hii Mwenyezi Mungu analitaja suala la kuteremshiwa Mtume SAW na waumini utulivu wa Kimwenyezi Mungu kuwa ni neema kwa jamii ya Kiislamu. Neno sakina katika aya hii lina maana ya utulivu na kutokuwa na wasiwasi. Kuna wakati inatokea kuwa, baina ya watu kuna hali ya ukosefu wa utulivu, kuna hali ya mtazamo mbaya baina ya watu na hali ya kutazamana kwa jicho baya; vyombo vinavyotawala viko mkabala na wananchi na wananchi wako mkabala na vyombo vya serikali; nchi kama hii ambayo haina usalama, haiwezi kusonga mbele na kujiletea elimu, uchumi, viwanda wala izza ya kitaifa; lakini wakati kunapokuweko usalama na utulivu katika nchi, taifa husika hupata fursa ya kuonyesha maandalizi yake sambamba na kudhihirisha vipawa vyake; kama ambavyo mnaona, licha ya kuweko vitisho vya maadui, vikwazo vya maadui na ukhabithi wa maadui, lakini taifa la Iran na vijana wetu azizi wameweza kujitokeza na kutangaza uwepo wao katika medani mbalimbali; wamejitokeza na kuonyesha adhama yao, vipaji vyao na maandalizi yao katika nyuga na medani mbalimbali na kuwadhihirishia walimwengu kwamba, wanaweza kufanya mambo tofauti; kwa hakika haya yote yamepatikana kwa baraka ya uthabiti. Maadui wetu walifanya njama tofauti huku wakitumia mbinu na mikakati mbalimbali ili kuvuruga uthabiti huu wa kisiasa. Mwanzoni mwa mapinduzi, maadui walifanya njama za kuzusha mapigano ya kikaumu mashariki na magharibi mwa nchi, kaskazini na kusini mwa nchi ili kuyafaya mapinduzi yasipate utulivu na kuifanya nchi itumbukie katika machafuko; lakini hata hivyo hawakufanikiwa katika njama zao hizo. Baada ya hapo, maadui wakafanya njama za kumsadia jirani yetu mwendawazimu - yaani Saddam Hussein ambaye kwa hakika alikuwa mwendawimu, katili, jeuri na hatari - ili aishambulie nchi yetu na kuvuruga amani na usalama wa nchi; ndani ya nchi pia kuna makundi ambayo yalimsaida mwendawazimu huyo; makundi ambayo baadaye yalikmbilia kwa Saddam na kuomba hifadhi. Bila shaka mumeona kile walichokita hawakufanikiwa kukipata kwani mambo yalikwenda kinyume kabisa na matarajio yao. Vita vya kulazimishwa na shambuloi la adui sio tu kwamba, hayakuvuruga amani na uthabiti wa nchi, bali mambo hayo yalipelekea kuimarika zaidi umoja na mshikamano wa kitaifa.
Nyinyi tazameni katika hili hili eneo lenu, katika eneo la kaskazini mwa Khorasan ambalo leo ni mkoa wa Khorasan Kaskazini, lina masafa marefu na medani ya vita - eneo la kusini na kaskazni magharibi mwa nchi wapi na wapi? Mkoa wa Khorasan Kaskazini, Shirvna na Bojnourd wapi na wapi? - lakini wananchi hawa hawa waliungana katika kukabiliana na adui; wakati huo hakukuweko na suala la Uturuki, Ufursi, Uturkemani na kaumu nyingine; masuala haya hayakuwa na nafasi, hakukweko na suala la Usuni na Ushia; watu wote walikuwa kitu kimoja na wakasimama kukabiliana na adui; waliwatoa vijana wao waende vitani huku wanaume wa maeneo haya wakitoka na kwenda vitani kupambana na adui. Wakati mwingine katika familia moja ikliuwa ikitokea kwamba, vijana wanne wanatoka na kuelekea katika medani ya vita. Baba wa vijana hawa wanne alikuwa akisema, "mmoja wenu abakie ili asimamie masuala ya nyumba ili mimi niende katika medani ya vita." Mashidano haya ya kuwa tayari kufa yanapatikana wapi?
Adui alikuwa anataka kuvuruga hali ya mambo hapa nchini, alikuwa anataka kulipokonya taifa la Iran amani na uthabiti; hata hivyo natija yake ikawa kinyume kabisa na matarajio yake, Mwenyezi Mungu alivifanya vitimbi na kedi za adui huyo kushindwa. Mwenyezi Mungu anasema kuhusiana na kedi na vitimbi vya maadu kwamba:
Na (Makafiri) wakafanya vitimbi na Mwenyezi Mungu akafanya vitimbi, na Mwenyezi Mungu ni mbora wa wenye kufanya vitimbi (Al-I'mran 3:54)
Taifa la Iran kwa baraka za kujihami kutakatifu (vita vya kulazimishwa vya miaka minane vilivyoanzishwa na dikteta wa wakati huo wa Iraq Saddam Hussein) limeweza kupiga hatua na kusonga mbele kuliko pale lilipokuwa; maandalizi na uwezo wake umeongezeka. Hizi njama za maadui Waistikbari na makatili hazijaweza kuwa na tathira yoyote ile katika irada na azma ya taifa la Iran.
Kisha baadaye wakaamua kutumia mbinu ya kutoa pigo kwa uthabiti huu kwa ndani. Kwa hakika hapa mimi ninaashiria tu; sitaki kuingia katika maudhui hii kwa undani. Mwaka 1378 na mwaka 1388 Hijria Shamsia - yaani tofauti ya miaka kumi - njama, mpango na mkakati wa adui ulikuwa mmoja. Katika matukio yote mawili, jitihada za maadui zilikuwa ni kutaka kuvuruga uthabiti wa kisiasa hapa nchini; walikuwa wakitaka kuvuruga hali ya mambo hapa ndani; maadui walikuwa wakitaka kulipokonya taifa hili huu utulivu.
Tunapaswa kutambua thamani ya amani na uthabiti. Wananchi wanapaswa kutambua thamani ya hili. Nawaambia nyinyi na kwa hakika maneno yangu haya yanawalenga watu ambao wanatangaza kutotambua thamani mkabala na uthabiti huu; watu ambao kwa harakati zao wanafanya mambo ambayo sio sahihi na ambayo hayafai kwa mkengeuko wao wanataka kuvuruga hali ya amani na uthabiti ulioko hapa nchini.
Tab'an, maafisa na viongozi wa serikali wako makini na wanafanya mambo yao kwa tadibiri; mimi pia ninasisitiza; ninawataka maafisa wa serikali, maafisa wa Bunge na vile vile Chombo cha Mahakama wawe makini na wasiruhusu wanaolitakia mabaya taifa hili na maadui wa taifa hili wafikie malengo yao ya kuvuruga huu utulivu ulioko katika kila kona ya nchi - ambayo ni ishara ya wazi na kubwa ya uwezo na nguvu za taifa hili, ambayo inaweza kujivutia kwake kila kheri - hivyo kuna haja ya kuwa macho.
Miezi michache ijayo tutakuwa na uchaguzi. Kabla ya uchaguzi na katika uchaguzi wenyewe, viongozi na maafisa wote wanapaswa kufanya hima ili kulindwa utulivu wa kisiasa hapa nchini; wasiruhusu anga ya kisiasa hapa nchini itumbukie katika makelelezo na ukosefu wa utulivu; haya ni miongoni mwa mambo ambayo viongozi na maafisa wa serikali wanapaswa kuyafanya kwa umakini mkubwa ili Inshallah lengo hili liweze kufikiwa.
Tab'an, kwa hakika wananchi wako macho na ni wenye muono wa mbali. Mtu aseme nini mkabala na hali hii ya kuwa macho na muono wa mbali walionao wananchi? Kwa hakika wananchi wa kawaida wana mtazamo sahihi na wamekuwa wakitazama mambo kwa maslahi ya nchi; hii ni tajiriba yetu Katika kipindi chote hiki cha miongo mitatu, kila mahala ilipotokea kwamba, kuna majukumu ambayo wananchi wanapaswa kuyatekeleza, hujitokeza na kutekeleza masuuliya hayo kwa njia bora kabisa. Maadui walitaka kuwaondoa wananchi katika medani ambayo ni lazima kuhudhuria, lakini hawakuweza; walitaka kuwafanya wananchi wawe na mitazamo na mingongano tofauti, wawe na hitilafu, wavutane mashati, na hivyo waghafilike na maendeleo ya nchi yao, lakini hawakuweza kufanikiwa pia katika hilo.
Wananchi walijitokeza na kuonesha muono wa mbali walionao. Kwa haki na insafu, muono wa mbali walionao wananchi ni wa kupigiwa mfano; hii nayo ni kazi ya Mwenyezi Mungu. Nyoyo ziko mikononi mwa Mwenyezi Mungu na irada ni zenye kusalimu amri mbele ya irada ya Allah.
Wananchi waumini wanafahamu hakika na ukweli huu; maagizo yetu tunayatoa zaidi kwa maafisa na viongozi wa serikali, kwa wanasiasa kwa mamudiri na wakurugenzi mbalimbali; wawe makini na wahakikishe kwamba, adui hawezi kuvuruga utulivu huu ambao uko hapa nchini kwa fadhila na baraka za Mwenyezi Mungu; adui alifanya njama ya kulivuruga hili pia lakini hakuweza kufanikiwa; maafisa na viongozi wa serikali wanapaswa kufanya kila wawezalo kuhakikisha kwamba, utulivu huu unahifadhiwa; wasiruhusu ijitokeze hali ya vurugu. Kwa hakika wakati mwingine, matamshi fulani mtu anayoyatoa au kitendo fulani anachokifanya au hatua fulani ambayo si ya mahala pake, hupelekea anga ya kisiasa (hapa nchini) kuvurugika na kuchafuka; hivyo kuna haja ya kuwa macho na makini.
Tab'an, wananchi hawa azizi kwa hakika wana haki viongozi watumie muda wao wote na kufanya hima na juhudi zao zote kwa ajili ya kusukuma mbele kazi za wananchi hawa. Mimi ninatazama masuala yanayohusiana na mkoa wa Khorasan Kaskazini - haya haya masuala ya Bojnourd, Shirvan, Esfarayen na miji mingine na maeneo mengine ya mkoa huu - na kuona kwamba, kuna kazi nyingi; hizi ni kazi ambazo kwa hakika zinapaswa kufanywa na maafisa na viongozi wa serikali. Wawakilishi wa Bunge au wa serikali wote kwa pamoja wana jukumu la kufanya kazi kwa ajili ya wananchi na kuwahudumia wananchi hawa azizi. Katika mji huu huu wa Shirvan, kuna kazi nyingi ambazo zinapaswa kufanywa.
Tab'an, mimi napenda kuwaambia nyinyi wananchi ya kwamba, kuweni na imani na viongozi wenu. Viongozi wanataka kufanya kazi na wanataka kufanya juhudi katika uga huu. Nia ni nzuri. Kwa hakika kuna nia na lengo la kuwahudumia wananchi; ingawa baadhi ya wakati dhuku huwa sio sahihi na wakati mwingine huwa kuna upungufu wa suhula. Watu wanapaswa kufanya hima na idili na tena bega kwa bega na hivyo kutatua kile vambacho ni matatizo katika uwanja wa kiuchumi au katika uga wa kiutamaduni.
Katika mji huu kama ilivyo kwa miji mingine ya mkoa huu na kama ilivyo pia katika mikoa mingine ya nchi hii, tatizo kubwa na la kimsingi ni suala la ukosefu wa ajira; ambapo Inshallah kuna haja ya kufanyika juhudi maradufu katika uwanja wa kuzalisha na kuandaa nafasi za ajira. Jambo jingine ni suala la uraibu wa vijana katika mkoa huu na katika eneo hili. Kwa hakika katika safari yangu hii nimetoa indhari na kuwataka vijana wenyewe kwa kuwaambia; vijana azizi! Sisi tunakutambueni nyinyi kwamba, ni wenye hamasa, irada na kusimama kidete na hivi ndivyo tunavyokuoneni. Ukweli uko namna hii. Kwa upande wa kiwango cha utamaduni, welewa na hekima vijana wa mkoa huu ni miongoni mwa vijana ambao wako mstari wa mbele kabisa. Mtu akitazama anaona kuna vijana katika mkoa huu ambao wako mstari wa mbele.
Vijana wenyewe hawa ambao ni mashujaa na walioko mstari wa mbele wanapaswa kusimama kidete na kupambana na uraibu mbaya na uchafu wa matumizi ya mihadarati; wao wenyewe wanapaswa kusimama kidete na wao ndio wanaopaswa kusimama na kupambana na hili. Haya ni mapambano ya pamoja na yanayohitajia ushirikiano yaani ni jukumu ambalo liko katika mabega ya maafisa na viongozi wa serikali pamoja na wananchi wenyewe. Kwa hakika mimi nina mtazamo mzuri sana na vijana. Ninaamini kwamba, kama vijana wetu hawa azizi wakiazimia wanaweza kupambana na kukabiliana na hatari kubwa ikiwemo hatari ya madawa ya kulevya katika mkoa huu.
Alhamdulilahi, wananchi wa kila kona ya nchi hii wana nishati na uchangamfu; hili ni jambo ambalo maadui zetu wanapaswa kuliona na kulitambua. Wale ambao walikuwa wanataka kutumia fimbo ya vikwazo kama wenzo wa kuwafanya wananchi wa taifa hili wakate tamaa, wakumbwe na hali ya msononeko na kuwafanya wananchi hawa wachoke, wanapaswa kuona harakati hii ya wananachi, mkusanyiko huu adhimu na hii harakati ya kujitolea wenyewe ya wananchi wa mkoa huu ambayo imejaa nishati na hamasa - kama ambavyo hali kama hii iko katika mikoa mingine ya nchi hii - wafungue macho yao naa kuona ni jinsi gani wananchi wana mahudhurio katika medani na irada yao kwa ajili ya kulinda na kutetea mfumo huu (Mfumo waa Jamhuri ya Kiislamu) ni imara na madhubuti kiasi gani.
Haya yote ni mambo ambayo yameja ibra na mazingatio. Kidhahiri ni kuwa, watu ambao wanataja jina la wananchi wa Iran - kuanzia viongozi wa Marekani na wasiokuwa wao - hawakufahamuni nyinyi wananchi wa Iran! Kwa mtazamo wao ni kuwa, wananchi wa Iran ni kiumbe ambaye ana taswira ya ajabu katika fikra na akili zao: Kiujumla hawawafahamu wananchi wa Iran ndio maana wanajisemea tu kwamba, eti wananchi wa Iran wanaupinga mfumo unaotawala hapa nchini na kwamba, eti wananchi wa Iran wanaupinga Uislamu.
Wananchi wa Iran ni hawa ambao mumewaona wakijitokeza katika medani mbalimbali kubwa. Katika siku hizi kadhaa, wananchi wa Bojnourd, Esfarayen, Shirvan na wa maeneo mengine ya mkoa huu, wananchi hawa wamewaonyesha walimwengu wote hamasa walionayo. Hata hivyo maadui wanafanya njama katika vyombo vyao vya habari za kufifiliza habari hizi na wasioneshe jinsi hali halisi ya mahudhurio ya wananchi na kujitokeza kwao ilivyo; lakini wao wenyewe (wahusika) wanafahamu na kuona uhakika na uhalisia wa mambo.
Kile ambacho sisi tutawaagiza waheshimiwa viongozi wa nchi katika uga wa masuala ya kiuchumi - ambayo ni masuala ya kimsingi na adui amejikita zaidi katika masuala haya - ni kwamba, katika suala la maendeleo na ustawi wa kiuchumi wayazingatie mambo haya matatu: kwanza, katika suala la uchumi, kama yalivyo masuala mengine, kuna haja ya kutazama mambo kwa mtazamo wa kielimu. Pili, kuna haja ya kuweko ratiba ya lazima yenye tadibiri ambayo ndani yake hakupaswi kuweko hatua za pupa na wakati huo huo kusiweko na mwendo wa kinyongo katika suala hilo. Katika masuala yote hali inapaswa kuwa hivi na katika suala la uchumi pia hali iwe hivi. Tatu, kuna haja ya kuweko sera thabiti na za kuendelea. Kama Inshallah maafisa na viongozi wa serikali watazingatia misingi hii katika suala la maendeleo na ustawi wa kiuchumi, bila shaka watayazingatia haya - viongozi nao wanakunwa na wana uchungu mkubwa (na nchi) na wakati huo huo wana tadibiri katika mambo hayo na wana ujuzi na elimu pia - na kwa tawfiki ya Mwenyezi Mungu, nguvu na auni yake, maadui zetu kama ilivyokuwa katika mambo mengine hawataweza kufanya kitu katika kukabiliana na uchumi wa taifa hili. Alhamdulilahi kwa huba na mapenzi ya Mwenyezi Mungu wataendelea kuweko katika medani mbali mbali wakiwa na hamasa na nishati; mahudhurio yao yaambatane na muono wa mbali, azma na irada thabiti. Maadui wanafanya njama za kuonesha kwamba, wananchi wa Iran wamechoka, wamekata tamaa na eti hawana hamu na shauku ya kufanya kitu.
Wananchi wa Iran wanafanya harakati na kwa harakati yao hiyo wanaonesha kwamba, maadui wanasema uongo; maadui wanahukumu vibaya. Tab'an, inasikitisha kwamba, kuna baadhi ya watu hapa ndani wanafanya mambo kwa mujibu wa matakwa ya adui - hatusemi kwamba, wanafanya hivyo kwa makusudi, la, bali kwa kughafilika - kwa kusema na kukariri maneno ambayo ni ya maadui. Baadhi ya watu wao wenyewe wamechoka halafu wanadai kwamba, wananchi wamechoka! Kwa hakika wananchi hawajachoka.
Wananchi wapo katika medani na wako tayari kwa ajili ya kazi. Kuna haja ya kuandaa uwanja kwa ajili ya wananchi na kufungua njia na wakati huo mtaona jinsi wananchi watakavyojitokeza katika kila kona ambayo wanahisi wana majukumu na masuuliya tena wakiwa na shauku na hamu kubwa na wataingia katika medani hiyo wakiwa na azma na irada thabiti; kama ambavyo tunaona jinsi walivyongia katika medani hiyo hii leo. Tunamuomba Mwenyezi Mungu Mtukufu akushushieni fadhila, rehhma, kheria na baraka Zake nyinyi wananchi azizi wa mji wa Shirvan na Inshallah Mwenyezi Mungu atawajumuisha vijana wetu katika huba na mapenzi Yake, atawapa tawfiki na kuwajalia hatima njema. Inshallah siku baada ya siku Mwenyezi Mungu atakufanyeni kuwa ni wenye furaha zaidi na wenye mafanikio zaidi. Tunamuomba Allah azifufue roho takasifu za mashahidi na roho ya Imam wa mashahidi (Imam Khomeini) pamoja na mawalii Wake. Natumia fursa hii kutoa shukurani zangu za dhati kwenu nyinyi wananchi kutokana na kuonyesha mapenzi na hamasa yenu kubwa kwangu.
Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.
 
< Nyuma   Mbele >

^