Skip to content

Habari

Habari
Hifadhi

Risala na Barua

Matini
Hifadhi

Kumbukumbu na Simulizi

Kabla ya Mapinduzi
Baada ya Mapinduzi

Sauti na Taswira

Picha
Sauti
Video
Hotuba ya Kiongozi Muadhamu Mbele ya Familia za MashahidiMkoani Khorasan Kaskazini Chapa
13/10/2012
Ifuatayo ni matini kamili ya hotuba ya Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aliyoitoa tarehe 13/10/2013 mbele ya hadhara kubwa ya familia za mashahidi, majeruhi wa vita na watu waliojitolea katika njia ya haki wa mkoa wa Khorasan Kaskazini .

Kwa Jina la Allah Mwingi wa rehma Mwenye kurehemu

Hamdu zote zinamstahikia Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wa viumbe pia. Na rehma na amani zimfikie Bwana wetu na Mtume wetu Mtukufu Abul Qassim Muhammad SAW pamoja na Aali zake wema na watoharifu, wateule, maasumina na waongozaji hususan Baqiyatullah katika ardhi (Imam Mahdi roho zetu ziwe fidia kwake).
Kwa hakika kikao cha leo kilikuwa kizuri mno na kilikuwa kimejaa nuru na umaanawi. Mbali na kuwa kila mahala ambapo kuna majimui na mkusanyiko wa familia tukufu na azizi za mashahidi, akina baba, akina mama, wake, watoto na watu wengine wa karibu na mashahidi huifanya anga hiyo kujaa nishati ya mapinduzi, jihadi na kusimama kidete - ambapo hili linahusiana na mikusanyiko yote ambayo sisi tumekuwa nayo na familia tukufu za mashahidi - kikao cha leo kwa hakika mpaka katika lahadha hizi kimekuwa ni kikao chenye wingi wa maarifa. Matamshi yaliyotolewa hapa, mashairi yaliyosomwa yote yalikuwa na nukta na mambo ambayo ni ya kina na thamani kubwa. Binafsi nimesikiliza kwa umakini mkubwa; kile ambacho kimesemwa hapa kwa mtazamo wa ukosoaji, kwa hakika nimeyaona kuwa yalikuwa ni mambo yenye thamani kubwa mno; na kwa hakika baadhi ya mambo hayo binafsi yamekuwa yakishughulisha fikra na akili yangu.
Kwanza kabisa napenda kuzungumzia jambo moja hapa kuhusiana na mashahidi azizi wa mkoa huu. Kwa hakika baadhi ya mashahidi hawa nilikuwa nikifahamiana nao kwa karibu; na nina ufahamu kuhusiana na maisha yao. Katika upande huu pia mkoa wenu ni moja ya mikoa yenye nafasi muhimu sana. Kijiorafia mkoa huu uko mbali na eneo la vita; lakini mwanzoni tu mwa ushindi wa mapinduzi ya Kiislamu, vijana wa eneo hili waliingia katika uwanja wa jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu. Baada ya kipindi hicho pia, vijana wa eneo hili waliendelea kushiriki mtawalia katika kazi za jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu.
Shahidi azizi wa hivi karibuni katika eneo hili ni Shahidi Rajabali Muhammadzadeh ambaye kwa hakika amepata ujira kutokana na kufanya jihadi kubwa katika kipindi cha kujihami kutakatifu na kusimama kwake kidete katika nyuga tata na ngumu katika kipindi cha miaka ya baada ya kipindi hicho na hivyo Mwenyezi Mungu akalikamilisha faili lake; Shahidi Khidmat na Shahidi Vahdat. Kwa hakika hawa ni watu wenye thamani wa eneo hili wanaoishi watu waumini; kwa hakika haya ni mambo yenye thamani kwa mkoa na mji fulani. Ni lazima kuonyesha heshima na taadhima kwa majimui ya familia za watu waliojitokea katika njia ya haki wa mkoa huu, familia za mashahidi, majeruhi azizi wa vita ambao wamestahamili matatizo na masaibu mengi ya athari na majeruhi ya vita katika kipindi cha miaka yote hii, hawakuacha azma yao, hawakupoteza hali yao ya kusimama kidete pamoja na imani yao thabiti; walisimama kidete na wangali wanasimama kidete.
Binafsi ninaona kuwa mbali na kuwa ni lazima kuonyesha heshima, taadhima na mapenzi maalumu kwa akina baba, akina mama, wake na watoto wa mashahidi ni lazima pia kuonyesha huba, mapenzi, heshima na taadhima kwa familia tukufu za majeruhi azizi wa vita pamoja na wake zao wapendwa ambao wanastahamili adha, taabu na usumbufu wa ndugu hawa wapendwa waliojeruhiwa katika vita. Hima na juhudi hizi ni jitihada ambazo zimehifadhiwa Inshallah katika kumbukumbu zenye thamani za Mwenyezi Mungu na bila shaka haya kwenu ni mambo yenye thamani kubwa kabisa. Haya ni mambo ambayo yanaifanya jamii na taifa fulani kuwa katika hali ya juu ya uhai na yanaliandaa taifa na jamii husika kwa ajili ya kujitengeneza.
Nukta nyingine katika mlango wa mashahidi wetu azizi nayo ni hii kwamba, wao ndugu na wapendwa! Mimi ninamini kwa dhati kabisa kwamba, sisi sote leo tumekaa katika kitanga cha chakula cha mashahidi. Kubaki kwa mapinduzi haya kumetokana na damu tukufu ya mashahidi; na hii ni moja ya nukta ambazo zimezungumziwa na ndugu hapa, yakasomwa mashairi na wakatilia mkazo katika hili. Ndio, ni kweli kabisa; ni shahada na kufa shahidi ndiko kunakotoa saini ya kubakia na kudumu kwa matukufu na mambo yenye thamani. Ujira mkubwa hapa duniani wanapatiwa mashahidi; kudumu, kuwa imara na kubakia kwa uhakika huo ndio mambo ambayo mashahidi walijitolea na kufidia roho zao kwayo. Mwenyezi Mungu Mtukufu ameuhifadhi uhakika na hakika hii kwa baraka za damu ya mashahidi. Jambo la kimantiki na kiakili hapa linaeleweka wazi; wakati jamii fulani inapoamua kufidia roho yake, uwepo wake na kuzipa mgongo raha zake kwa ajili ya hakika na jambo lenye thamani, huthibitisha hapa duniani kwamba, iko katika haki; na ni haki ambayo hubakia; kwa hakika hii ndio mipango ya Mwenyezi Mungu.
Mashahidi wetu azizi na watu waliojitolea katika njia ya haki ni watu ambao waliweka kando na kufumbia macho matakwa yao binafsi. Kwa hakika kwa lugha nyepesi tunaweza kusema hivi; yaani sio kwamba, ni watu ambao waliamua kuzipa mgongo, fedha, mali na mtaji, bali ni kuyapa mgongo hata mambo ya kihisia. Shahidi anaachana na mapenzi ya mama, kivuli cha baba, tabasamu la mtoto na huba na mapenzi ya mkewe kisha kuamua kufanya harakati kuelekea katika kutekeleza majukumu. Majeruhi hawa wa vita nao ni mashahidi. Kila mahala watakapokuwa watu waliojitolea katika njia ya haki kwa hakika wanakuwa wameweka mguu katika njia ya shahada na kuuawa shahidi katika njia ya Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu Mtukufu amewachagua baadhi ya watu wakaenda (yaani wakauawa shahidi) baadhi ya wengine wakabakia kwa ajili ya majaribu na mtihani inayofuata; lakini kuna daraja ya shahidi na kuuawa shahidi kwa ajili ya watu waliojitolea katika njia ya haki.
Mimi napenda kuongezea nukta nyingine katika yale yaliyozungumzwa na ndugu zetu wapendwa hapa. Wamesema: Wale watu ambao katika kipindi cha jihadi tukufu na kujihami kutakatifu, walikwenda katika medani za vita huko kusini na magharibi na kuingia katika medani za vita huku wakiwa wamejitolea na wako tayari kufa katika njia hiyo wanagawanyika katika sehemu na makundi matatu: Baadhi yao hujuta kutokana na historia yao ya huko nyuma, baadhi yao huwa hakuna tofauti kwao na wengine hubakia na kudumu. Wale ambao hubakia na kutobadilika ni lazima wawe na huzuni. Kwa hakika mimi sikubaliani na sentesi hii ya mwisho. Wale ambao wanabakia wakiwa wamesimama kidete hukaa na kushuhudia matunda ya mche huu na kukua kwa mti huu. Kwa hakika kuondoka na kurejea baadhi ya watu kutoka katika kafila hii adhimu, katu hakuufanyi msafara huu ukwame njiani, la hasha: Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema katika Kitabu cha Qur'ani kwamba:
Enyi mlio amini! Atakaye iacha miongoni mwenu Dini yake, basi Mwenyezi Mungu atakuja leta watu anao wapenda nao wanampenda, wanyenyekevu kwa Waumini na wenye nguvu juu ya makafiri, wanapigania Jihadi katika Njia ya Mwenyezi Mungu, wala hawaogopi lawama ya anaye laumu. Hiyo ndiyo fadhila ya Mwenyezi Mungu, humpa amtakaye. Na Mwenyezi Mungu ni Mkunjufu na Mwenye kujua. (Al-Maidah 5:54). Hili ni jambo ambalo Mwenyezi Mungu aliwaambia Waislamu mwanzoni wa Uislamu, watu ambao walifanya jihadi bega kwa bega na Bwana Mtume SAW na kujitolea roho zao; Qur'ani Tukufu inabainishia ukweli na uhakika huu. Kuna haja ya kuzihifadhi na kuzilinda nyoyo. Baadhi ya nyoyo zinatetereka na kuteleza, haziwezi kusimama kidete na kuendelea na njia; hivyo huteleza na kuanguka.
Qur'ani Tukufu imewataja watu hawa kwa ibara ya: "Atakaye iacha miongoni mwenu Dini yake". (al-Maidah 5:54). Neno "Irtidad" kiujumla sio kila mahala lina maana kuiacha dini, kurejea nyuma na kuipa mgongo dini; hapana, bali maana yake ni kuiacha njia ambayo ulikuwa ukiifuata. Ndio, kuna baadhi ya watu waliokuweko katika mapinduzi yetu, mwanzoni mwa Uislamu walikuweko pia, katika njia ambayo walikuwa wakifanya harakati pamoja na Mtume SAW hawakuendelea, yaani walirejea nyuma; je harakati hiyo ilisimama? Je kwa wao kufanya hivyo harakati husimama? Je kafila (msafar) husimama kwa mtu mmoja kuondoka katika msafara huo? la hasha! msafara huo huendelea na safari yake: Mwenyezi Mungu anasema:
"basi Mwenyezi Mungu atakuja leta watu anao wapenda nao wanampenda, wanyenyekevu kwa Waumini na wenye nguvu juu ya makafiri, wanapigania Jihadi katika Njia ya Mwenyezi Mungu, wala hawaogopi lawama ya anaye laumu." (al-Maidah 5:54); kutakuja watu wengine, mbinu na mikakati mingine. Moja kati ya mbinu hizo ni nyinyi vijana. Nyinyi ambao hamkuweko katika kipindi cha vita na wala hamkuvishuhudia vita hivyo, nyinyi hamkumuona Imam Ruhullah Al-Musawi Al-Khomeini MA na nyinyi ambao kwa hakika hamkuweko katika medani ya vita; lakini leo hii mapinduzi yetu ya Kiislamu yanajifakharisha katika kila kona ya nchi hii kutokana na moyo wenu huu wa kujitolea na kusimama kidete na kwa hakika nchi hii na mapinduzi haya yanahisi izza na utukufu kwa ajili yenu.
Hii leo kusimama kwenu kidete mkabala na kupenda makuu, kujitanua na uvamizi wa madola ya kibeberu ulimwenguni kunakoongezeka kila siku ni tishio kubwa kwao. Hii leo taifa la Iran ni tishio kwa madola hayo kutokana na misimamo yake thabiti na kutokubali kunyongeshwa. Mapinduzi ambayo yamepata ushindi katika mwamko wa Kiislamu - tab'an, sisi tunaheshimu mapinduzi yote haya na tunayathamini - linganisheni mapinduzi haya na Jamhuri ya Kiislamu, Mfumo wa Kiislamu na mapinduzi ya Kiislamu; muona huu uwezo, kusimama kidete na hii hali ya kujiamini ya taifa na wananchi wa Iran inapatikana wapi?
Madola ya kibeberu duniani yamejizioesha yenyewe kwamba, yanazungumza kwa niaba ya watu wote duniani, kwa ajili ya maslahi yao duni, kwa ajili ya mabepari wao; yamezoea kuingilia masuala ya ndani ya kila nchi nyingine na kufanya mambo kwa ajili ya matakwa yao ya kibeberu. Baadhi ya wakati mataifa hupiga ukulele wa malalamiko, wakati mwingine hupiga mayowe; lakini ni nani anayeweza kusimama mkabala na nguvu za madola haya? Ni taifa gani ambalo limesimama mkabala na hatua za kupenda makuu za madola ya kibeberu kwa kutumia mantiki, hoja na kutotetereka? Je kuna taifa jingine ghairi ya taifa la Kiislamu la Iran? Mataifa mengine kadiri yanavyofanya hayawezi kuvuka nafasi ya Iran. Mwenyezi Mungu ajaalie ifike siku watupite - hatuna neno - ni vizuri sana kama mataifa ya Kiislamu na mataifa mengine yatakuja na kutupita katika hili; hata hivyo uhakika wa kadhia sio huu; hii leo taifa la Iran liko mbele na ndio kinara wa hili.
Vijana wetu ambao hawakuweko katika zama zile, hii leo wapo; hii ni habari na bishara njema. Watu wa fikra, walio macho, weledi wa uhakika wa matukio yanayojiri duniani kila leo na waliopevuka katika masuala mbali mbali ya kisiasa waegemee katika tukio hili lililoko katika Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu, ambapo licha ya kuweko hali fulani ya mkengeuko katika baadhi ya kona, hii leo msukumo huu, kusimama huku kidete, weledi huu, welewa huu na azma hii thabiti iliyoko baina ya vijana wetu kama tutasema hawakishindi kizazi cha vijana wa wakati wa vita vya kujihami kutakatifu (vilivyoanzishwa na utawala wa wakati huo wa Iraq dhidi ya Iran) basi tutakiri kuwa hakishindwi na kizazi hicho.
Vipi inawezekana katika taifa fulani mikakati na kusimama kidete kunakuwa ni zaidi ya kutetereka? Ndio, bila shaka kuna hali ya kutetereka; Baadhi ya watu kutokana na sababu mbali mbali kama vile kuchoka au kuwa na shaka na misimamo yao ya huko nyuma au kudanganyika na tabasamu za adui, wametoka katika harakati ya Mapinduzi ya Kiislamu, lakini katika mkabala wa watu hao na kutokana na baraka za damu za mashahidi kuna watu wengi na hasa vijana wameingia kwenye msafara wa harakati ya Mapinduzi ya Kiislamu na kuifanya kila kona ya Iran kujaa moyo wa kusimama kidete, kuwa imara na kulinda heshima ya taifa. Hii leo hali yetu iko namna hii. Kuna baadhi ya watu ambao wanatazama mambo kidhahiri, wanahukumu vibaya na kudhani kwamba, vijana wameacha dini. Hapana; vijana wanaipenda njia hii, wanapenda kitu ambacho kinaifanya imani yao kuwa thabiti na imara; na kwa hakika hili ni jambo ambalo linahusiana na akthari ya vijana wa nchi hii; kwa hakika hili linatokana na baraka za damu ya mashahidi; hili linatokana na baraka ya kujitolea muhanga na kufidia roho zao wapendwa wenu na vijana wenu. Nyinyi mumewalea na kuwakuza vijana wenu, mkapata usumbufu mkubwa na mkawalea kwa malezi bora kabisa na mkawakabidhi kwa jamii kama maua yavutiayo; nao wakaenda na kuuawa shahidi katika njia ya Mwenyezi Mungu. Taifa zima la Iran linapaswa kukushukuruni nyinyi. Watu wote wanapaswa kukumbuka utajo wa mashahidi. Watoto wa mashahidi wanapaswa kujifakharisha na baba zao. Watoto wa mashahidi wanapaswa kukabidhi njia na mirathi ya baba zao kwa ajili ya vizazi vijavyo. Kwa hakika taifa la Iran linajifakharisha na mashahidi wake. Kwa hakika sisi tunajifakharisha na irada, mapenzi na ikhlasi kwa familia za mashahidi na tunaamini kwamba, mashahidi walifanya harakati wakiwa katika mstari wa mbele; nyuma yao bila kupoteza muda wako baba, mama na wake zao; hawa pia walikuja na kusimama kidete na wakajitolea. Hii leo kwa baraka za kujitolea, harakati adhimu ya mapinduzi ya wananchi wetu imesimama imara na Inshallah siku baada ya siku itazidi kuwa imara na madhubuti.
Tunamuomba Mwenyezi Mungu ashushe rehma, baraka na fadhila Zake kwa mashahidi aziz, kwa familia zao, kwa majeruhi na kwa familia zao na tunamuomba pia ashushe baraka zake kwa mateka walioachiliwa huru na watu wote waliojitolea katika njia ya haki na aufanye moyo Mtukufu wa Walii Asr (Baqiyatullah katika ardhi) uwe radhi na nyinyi nyote.
Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.
 
< Nyuma   Mbele >

^