Skip to content

Habari

Habari
Hifadhi

Risala na Barua

Matini
Hifadhi

Kumbukumbu na Simulizi

Kabla ya Mapinduzi
Baada ya Mapinduzi

Sauti na Taswira

Picha
Sauti
Video
Hotuba ya Kiongozi Muadhamu Mbele ya Wahadhiri wa Vyuo Vikuu vya Ulimwengu wa Kiislamu Chapa
11/12/2012

Ifuatayo ni matini kamili ya hotuba ya Ayatullah Udhma, Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aliyoitoa wakati alipokutana na hadhara kubwa ya washiriki wa mkutano wa kimataifa wa wahadhiri wa Vyuo Vikuu vya Ulimwengu wa Kiislamu na Mwamko wa Kiislamu tarehe 11/12/2012.

Kwa jina la Allah Mwingi wa rehma Mwenye kurehemu

Awali ya yote napenda kutumia fursa hii adhimu kaisa kukukaribisheni nyinyi wageni azizi mliotoka katika nchi mbalimbali na vile vile nyinyi wahadhiri wapendwa na waheshimiwa wa Vyuo Vikuu vyetu hapa nchini. Karibuni sana.
Takribani ni mwaka mmoja na nusu sasa ambapo hapa Tehran kumekuwa kukifanyika makongamano, mikutano na vikao mbalimbali kuhusiana na Mwamko wa Kiislamu; lakini kwa mtazamo wangu ni kuwa, kikao na mkutano wa wahadhiri kina umuhimu maalumu; kwani kuleta fikra, mazungumzo na harakati ya kifikra katika jamii ni jambo ambalo liko mikononi mwa watu makhsusi na maalumu katika jamii; ni jambo ambalo liko mikononi mwa wanafikra katika jamii; bila shaka ni wao ndio ambao wanaweza kuziongoza fikra za jamii kuelekea upande fulani na kuwa chimbuko la kuziokoa jamii; kama ambavyo (Mwenyezi Mungu aepushe mbali) wanaweza pia kuiongoza jamii upande wa mambo mabaya, umateka (utumwa) na kuharibikiwa. Inasikitisha kwamba, hili la pili limetokea katika kipindi cha miaka 70 ya hivi karibuni katika baadhi ya nchi na katika nchi yetu.
Katika riwaya moja Mtume wa Uislamu Bwana Mtume SAW amenukuliwa akisema kwamba, "Watu wa kawaida wa umma huu hawawezi kujirekebisha isipokuwa kwa kuweko watu maalumu. Akauliza ni akina nani hao watu maalumu, akasema ni maulama". Hivyo basi, kwanza Bwana Mtume SAW amewataja maulama, kisha baadaye akataja watu wengine. Kwa msingi huo basi, wahadhiri wa Vyuo Vikuu, watu wateule na wenye vipawa vya kielimu katika nchi yoyote ile, wanaweza kuwa chimbuko la harakati kubwa na adhimu ya wananchi; tab'an, kwa sharti kwamba, wawe na ikhlasi, kwa sharti kwamba, wawe na ushujaa na wasiwaogope maadui hata kidogo. Endapo kutajitokeza woga na khofu, endapo kutakuwa na hali ya uchu na tamaa, endapo kutajitokeza mghafala (hali ya kughafilika na kujisahau) na kisha kukajitokeza hali fulani ya uvivu, basi bila shaka mambo yataharibika na hayawezi kutengemaa. Lakini kama kutakuwa hakuna woga, kukaweko na hali ya ushujaa, kisha kukawa hakuna hali ya uchu wala tamaa na wakati huo huo kukawa hakuna mghafala (hali ya kughafilika na kujisahau) na wakati huo huo kukawa na hali ya kuwa macho inayoambatana na mwamko, basi bila shaka wakati huo mambo hayatakwenda mrama wala kombo, bali kila kitu kitakwenda vizuri na hivyo kuwa na natija maridhawa.
Mwanzoni mwa mapinduzi, takribani miaka 31 au 32 hivi iliyopita, kulijitiokeza jambo muhimu sana. Mimi na watu wengine wawili ambao katika zama hizo tulikuwa wajumbe wa Baraza la Mapinduzi, tuliondoka Tehran na kwenda Qum kwa shabaha ya kwenda kukutana na Imam (Imam Ruhullah Khomein MA) - kwani Imam wakati huo alikuwa bado yuko mjini Qum na alikuwa hajahamia Tehran - ili tushauriane naye na kupata mtazamo wake kuhusiana na jambo hilo muhimu. Baada ya kumtolea ufafanuzi Imam (Imam Khomeini MA) kuhusiana na jambo hilo, Imam alitutazama kisha akatuuliza, mnaiogopa Marekani? Tukamjibu kwa kumwambia, hapana. Akasema, basi nendeni na fanyeni jambo hilo. Tukaondoka na kisha tukalifanya jambo hilo na kwa kweli tukafanikiwa. Hivyo basi kama kutakuwa na hali ya woga, uchu na tamaa, au mghafala (kughafilika) au kwa mfano kukawa na hali fulani ya muelekeo wa upotofu, hapana shaka yoyote ile kwamba, kazi na mambo husika yatakabiliwa na mushkili na matatizo.
Hii leo ulimwengu unakabiliwa na tukio adhimu; tukio hili adhimu ni Mwamko wa Kiislamu; huu ni uhakika ulio wazi kabisa na ambao unaonekana wazi katika Mashariki ya Kati na kaskazini mwa Afrika. Mataifa ya Kiislamu na umma wa Kiislamu, hatua kwa hatua umeamka. Hii leo sio jambo jepesi kuyadhibiti mataifa ya Kiislamu na kuwa na satwa dhidi yao baada ya Vita Vikuu vya Kwanza vya Dunia na katika kipindi kirefu cha karne ya 19 na 20 Miladia. Endapo leo Waistikbari wa dunia wanataka kuwa na satwa na udhibiti kwa mataifa ya Kiislamu watakabiliwa na kibarua kigumu sana. Mwamko umeingia katika umma wa Kiislamu na umepenya na kujikita sasa. Katika baadhi ya nchi mwamko huu umegeuka na kupelekea kutokea mapinduzi duniani na pia wananchi kuzipindua tawala fasidi katika baadhi ya nchi. Hata hivyo hii ni sehemu moja tu ya Mwamko wa Kiislamu; sio mwamko wote wa Kiislamu. Mwamko wa Kiislamu ni kitu chenye upeo na kina kirefu sana.
Tab'an, maadui wanaogopa neno " Mwamko wa Kiislamu; na wanafanya njama kubwa ili kuzuia kutumika jina "Mwamko wa Kiislamu" kuelezea harakati adhimu inayoshuhudiwa hivi sasa katika eneo la Mashariki ya Kati na kaskazini mwa Afrika. Kwa nini? Kwa sababu kama Uislamu utakuwa katika sura yake ya kweli, ukajitokeza katika haiba na sura yake halisi; ni jambo ambalo linawatisha na kuwaogopesha sana maadui hawa. Maadui hawaogopeshwi na Uislamu ulio mtumwa wa fedha na mali, Uislamu ulioghariki katika ufisadi na anasa na Uislamu usio na nguvu za wananchi, lakini wanatetemeka na kuingiwa na hofu kubwa wanaposikia jina la Uislamu wenye nguvu za makundi kwa makundi ya wananchi, Uislamu wa kuchapa kazi na kuchukua hatua za maana, Uislamu wa kutawakali kwa Mwenyezi Mungu na Uislamu wa kuwa na hisia na yakini ya kutimia ahadi ya Mwenyezi Mungu (ya kuwapa ushindi wanaoinusuru dini Yake), kama anavyosema Mwenyezi Mungu:
"Na bila ya shaka Mwenyezi Mungu humsaidia yule anaye msaidia." (AL Hajj 22:40). Huu ndio Uislamu ambao wao wanauogopa. Wakati jina la Uislamu linapotajwa na kukaweko na ishara za kweli za Uislamu, basi Waistikbari wa ulimwengu huingiwa na woga na kutetemeka. Na hukumbwa na hali kama ya punda amuanapo Simba. Mwenyezi Mungu anasema katika Kitabu Chake cha Qur'ani Tukufu:
"Kama kwamba wao ni mapunda walio timuliwa. Wanao mkimbia simba!" (Muddathir 74:50-51).
Ndio maana hawataki kuona kunaweko na jina " Mwamko wa Kiislamu". Hata hivyo sisi tunaamini kwamba "hapana" harakati adhimu iliyojitokeza hivi sasa katika eneo hili ni mwamko wa kweli wa Kiislamu wenye sifa ya kuendelea zaidi na zaidi, harakati ambayo imekijita na ni harakati ambayo maadui hawawezi kuipotosha kirahisi na kuifanya ikengeuke na kuacha njia yake ya asili.
Tab'an, kuna haja ya kufanya uchunguzi kuhusiana na mambo yanayodhuru; na hii ni nukta ya kwanza ambayo ninataka kukuelezeni nyinyi leo. Harakati hizi zilizotokea katika ulimwengu wa Kiislamu, mapinduzi haya yaliyotokea huko Misri, Tunisia, Libya na kadhalika na kupata ushindi, kaeni chini na mtafute mambo yanayodhuru; ni hatari gani zinazoyakabili mapinduzi haya? Matatizo yake ni yepi? Kwa nini tunasema kuwa, kile kilichotokea ni Uislamu mia kwa mia? Tazameni nara za wananchi hawa; katika kipindi chote hiki. Nara na kaulimbiu za Kiislamu za wananchi katika Mapinduzi ya eneo la Mashariki ya Kati na kaskazini mwa Afrika pamoja na nafasi ya kiitikadi ya Uislamu katika kuundika mikusanyiko mikubwa kwenye nchi hizo na vile vile kuangushwa tawala fisadi zisizopenda dini ya Kiislamu kwa pamoja ni ushahidi na mambo ambayo yanazidi kuthibitisha kuwa harakati hizo ni harakati za Kiislamu. Mashinikizo ya harakati ya wananchi na mahudhurio yao makubwa yameweza kuliangusha jengo lililochakaa la kama Hosni Mubarak (wa Misri) na Bin Ali (wa Tunisia). Wananchi hawa walikuwa Waislamu na walikuwa wakipiga nara za Kiislamu. Nafasi ya watu wenye mielekeo ya Kiislamu katika kuziangusha tawala hizi, huu nao wenyewe ni ushahidi mkubwa na wa kutosha kwamba, harakati hizi ni harakati za Kiislamu. Kisha baadaye, kila mahala ambapo ulipowadia wakati wa kupiga kura, wananchi walijitokeza na kwenda kuwapigia kura watu wenye mielekeo ya Kiislamu; wakawaimarisha na kuwafadhilisha (kuwapa kipaumbe) hao (yaani watu wenye mielekeo ya Kiislamu) mbele ya watu wengine. Na mimi napenda kuwaeleza kwamba, ; hii leo takribani kila nukta ya ulimwengu wa Kiislamu - yumkini katika baadhi ya maeneo hali ikawa sio hivyo - endapo kutafanyika uchaguzi mzuri huru na wa haki na kisha viongozi wa Kiislamu na wanasiasa wa Kiislamu wakajitokeza uwanjani kugombea (nafasi mbalimbali), sina shaka wananchi watawapa kura wao. Kila mahala hali iko namna hii. Hivyo basi, hakuna shaka kuwa, harakati hii ni harakati ya Kiislamu (mia kwa mia).
Vizuri, tumesema, tafuteni mambo yanayodhuru. Kando ya kutafuta mambo yanayodhuru, kuweko na hali ya kubainisha malengo. Endapo malengo hayatobainishwa, bila shaka kutajitokeza hali ya kupotea na kutajitokeza hali ya kusambaratika. Hivyo kuna haja ya kubainisha malengo. Moja kati ya malengo haya muhimu kabisa ya mwamko huu ni kujikomboa kutoka katika shari ya ubeberu na uistikbari wa kimataifa; hili ni jambo ambalo linapaswa kusemwa kwa uwazi na pasina ya kificho chochote. Hii kwamba sisi tudhani uistikbari wa dunia ukiongozwa na Marekani, yamkini ukakubaliana na harakati za Kiislamu, ni kosa kubwa sana. Kama (mahal fulani na katika nchi fulani) kuna Uislamu, hali ya Uislamu na watu ambao ni wafuasi wa Uislamu, basi Marekani hufanya kila iwezalo kutokomeza yote haya; tab'an, kidhahiri itatoa tabasamu. Harakati za Kiislamu hazina budi kwani ni lazima ziainishe mpaka wake. Hatusemi ziende na kupigana vita na Marekani, hapana, bali tunasema kuwa, wanapaswa kujua msimamo wa Marekani na uistikbari wa Kimagharibi kuhusiana na wao ni upi? Hili ni jambo ambalo wanapaswa kuliainisha kwa njia sahihi. Endapo hawatoliainisha hili, bila shaka watahadaika na kutapeliwa.
Hii leo mabeberu wa dunia wanatumia nyenzo za fedha, silaha na elimu kwa ajili ya kudhibiti dunia; hata hivyo licha ya kuweko nyenzo hizo lakini moja ya matatizo makubwa yanayoukabili ulimwengu wa Magharibi hivi sasa ni kutokuwa na fikra na nadharia mpya za kumwonyesha mwanadamu, wakati ambapo ulimwengu wa Kiislamu una fikra na aidiolojia mpya za kuweza kumletea ufanisi wa kweli mwanaadamu. Wakati ambapo sisi tuna fikra, wakati ambapo sisi tuna ramani ya njia, bila shaka tunaweza kuainisha malengo yetu, tunaweza kusimama kidete; katika mazingira kama haya silaha zao, fedha zao na elimu zao haziwezi kuwa na taathira kama ile iliyokuwa nayo huko nyuma; tab'an, sio kwamba, haina taathira kabisa. Kwa hakika sisi tunapaswa kuwa na fikra moja mkabala na wao (maadui) - kama kutakuwa na wakati nitalizungumzia zaidi hili - lakini katika hatua ya awali ni kwamba, tunapaswa kuwa na fikra, ramani ya njia na aidiolojia; tujue kwamba, tunataka kufanya nini.
Malengo yanapaswa kuanishwa. Moja ya malengo muhimu katika mapinduzi ambayo yanapaswa kuzingatiwa ni kwamba, watu wasitokea katika mhimili wa Uislamu. Uislamu unapaswa kuwa ndio mhimili mkuu na dira yao kuu. Fikra na nadharia za Kiislamu pamoja na sharia za Kiislamu zinapaswa kuwa mhimili mkuu (wa kufuata). Wamefanya njama (madui) za kutaka kuonesha kwamba, sharia za Kiislamu hazioani kabisa na maendeleo, mabadiliko, ustaarabu na mambo mengine kadhaa wa kadhaa. Haya ni maneno ya adui; sisi tunasema, "hapana", sharia za Kiislamu zinaendana na kuoana kabisa na yote haya. Tab'an, katika ulimwengu wa Kiislamu watu wenye moyo na fikra za mgando, kujitenga, fikra zilizopitwa na wakati na kutokuwa na uwezo wa ijtihadi sio wachache na kwa namna fulani wameweza kubainisha na kuthibitisha maneno haya ya adui. Hawa ni Waislamu lakini wanawahudumia maadui wa Uislamu. Sisi katika maeneo yaliyoko kando yetu, katika baadhi ya nchi hizi za Kiislamu, tuna mambo kama haya; majina yao ni Waislamu, lakini mtu hashuhudii watu hawa wakiwa japo kidogo na kidogo fikra mpya, mtazamo jadidi na ufahamu mpya kuhusiana na maarifa ya Kiislamu. Uislamu ni wa vipindi na zama zote, Uislamu ni wa karne zote, Uislamu ni wa zama zote za maendeleo ya mwanadamu na Uislamu unatoa jibu sahihi kwa kila mahitaji na hawaiji za wanaadamu na katika karne zote na vipindi vyote vya maendeleo ya mwanaadamu. Fikra ya Kiislamu ambayo inaweza kutoa majibu ya mahitaji yote inapaswa kutafutwa na kufahamika. Baadhi ya watu hawana fikra hii; wanachojua wao ni kuwakufurisha watu wengine, kuwapa watu wengine majina kama ya mafasiki na halafu eti wanajiita kuwa wao ni Waislamu. Baadhi ya wakati mtu anashuhudia kwamba, watu hawa wapo pamoja na vibaraka wa maadui! Tunapaswa kuzifanya sharia za Kiislamu na fikra za Kiislamu kuwa ndio mhimili wa harakati zetu zote; hili nalo ni moja ya malengo.
Lengo jingine ni kuunda mfumo na kuja na mfumo mpya na jadidi. Kama katika nchi zilizofanya mapinduzi hakutaandaliwa mazingira ya kuundika mfumo mpya maalumu wa kuweza kulinda mapinduzi hayo, basi bila shaka hatari nyingi zitayakabili mapinduzi ya wananchi wa nchi hizo. Katika nchi hizi hizi za kaskazini mwa Afrika, sisi tuna tajiriba na uzoefu ambao ni wa miaka sitini hadi sabini iliyopita; katikati mwa karne ya ishirini. Katika nchi hii hii ya Tunisia, kulitokea mapinduzi, kukaibuka harakati, kisha wakaja watu wakaingia madarakani; katika nchi hii hii ya Misri, kulitokea mapinduzi, kukaibuka harakati kisha wakaja watu na kuingia madarakani - katika maeneo mengine pia hali iko hivi hivi - lakini (wahusika) hawakuweza kuunda mfumo; kutokana na kutounda kwao mfumo, jambo hilo sio tu kwamba, lilipelekea mapinduzi hayo kusambaratika na kutoweka, bali hata watu ambao waliingia madarakani kwa jina la mapinduzi, walibadilika kutoka msimamo huu hadi ule, walibadilika moja kwa mia; wao wenyewe pia wakaharibika. Jambo hili lilitokea nchini Tunisia, Misri na Sudan katika zama hizo. Takribani ilikuwa katika miaka ya 1343 au 1344 au 1345 Hijria Shamsiya. Mimi nikiwa na watu kadhaa marafiki zangu. Tulifungua redio wakati huo tuko Mash'had, Radio hiyo ilijulikana kwa Saut al-Arab (Sauti ya Kiarabu), tukawa tunategea sikio idhaa hiyo - ambayo ilikuwa ikirusha matangazo yake kutoka Cairo, Misri - basi ikawa inarusha hotuba za Jamal Abdul Nasser (Rais wa wakati huo wa Misri), Kanali Muammar Gaddafi (Kiongozi wa wakati huo wa Libya) na Jafar Al-Numeri (Kiongozi wa zama hizo wa Sudan) waliokuwa wamekusanyika pamoja. Wakati huo sisi mjini Mash'had tulikuwa chini ya mashinikizo ya kidikteta na udhalimu, lakini tulikuwa tukipata hamasa kubwa na kustaladhi na maneno haya makali na ya hamasa yaliyokuwa yakitolewa na viongozi hao.
Vizuri, Jamal Abdul Nasser amefariki dunia na mumeona mrithi wake amefanya nini; Gaddafi naye mumeona nini kimempata; Numeri naye hali yake ilikuwa ikijulikana ikoje. Hivyo basi, wanamapinduzi wenyewe walibadilika; kwanza hawakuwa na fikra na vile vile hawakuweza kuunda mfumo mpya. Nchi hizi ambazo zimefanya mapinduzi, zinapaswa kuwa na muundo wa mfumo; ni lazima kuweko na kanuni imara. Hili nalo ni miongoni mwa mambo muhimu.
Miongoni mwa masuala mengine muhimu ni kulinda himaya na uungaji mkono wa wananchi; haipaswi kujitenga na kujiweka mbali na wananchi. Wananchi wana matarajio na wana mahitaji wanayotaka watekelezewe. Nguvu ya kweli nayo iko mikononi mwa wananchi; yaani wananchi ndio wenye maamuzi ya mwisho na maamuzi yao yana nguvu.
Pale ambapo wananchi wanajikusanya, pale ambapo wananchi nyoyo zao ziko pamoja, pale ambapo wananchi wanapokuwa pamoja wakiwaunga mkono maafisa wa serikali na viongozi, basi Marekani na hata wakubwa zaidi ya Marekani hawawezi kufanya chochote kile. Ni lazima kuwahifadhi wananchi na kuwa pamoja nao na hili ni jambo ambalo liko mikononi mwenu; liko mikononi mwa wanafikra, waandishi, washairi na maulama wa dini. Watu ambao wana taathira zaidi ya wote ni maulama wa dini ambao kwa hakika wana jukumu zito mno; maulama wanapaswa kuwabainishia watu wawawekee wazi watu mambo kwamba, wanataka nini, wawabainishie watu mambo kwamba, wako katika njia gani, wawabainishie watu vizingiti ni vipi, adui ni yupi; wawafanye wananchi wabakie kuwa na ufahamu, welewa na muono wa mbali. Katika mazingira kama haya hakuwezi kuweko na pigo.
Jambo jingine ni kuwalea vijana kielimu. Nchi za Kiislamu zinapaswa kupiga hatua kimaendeleo katika uga wa elimu na teknolojia. Nimesema kuwa, Marekani na Magharibi wameweza kuwa na satwa na udhibiti kwa nchi nyingine duniani kwa baraka za elimu; moja ya nyenzo na suhula zao ilikuwa ni elimu; na hata utajiri wao wameupata kupitia elimu. Tab'an, sehemu fulani ya utajiri huo wameupata kwa hila, hadaa, kedi pamoja na ukhabithi pamoja na mchezo (mchafu) wa kisiasa, lakini elimu pia ilikuwa na taathira katika hilo. Hivyo basi kuna haja ya kuwa na elimu. Kuna riwaya inasema kuwa, "Elimu ni nguvu, mwenye kuipata hutawala na mwenye kuikosa hutawaliwa." Hivyo ipateni elimu. Endapo mtapata elimu na endapo mtakuwa na elimu basi mtakuwa mmepata nguvu. Iwapo mtakuwa hamna elimu, watu ambao wana nguvu watakubinyeni na kukukaandamizeni. Washajiisheni vijana wenu kuhusiana na suala la elimu; hii ni kazi ambayo inawezekana kuifanya; sisi tumefanya kazi hii hapa nchini Iran. Kwa hakika sisi kabla ya ushindi wa mapinduzi ya Kiislamu hapa nchini, tulikuwa katika faharasa ya mwisho mwisho kabisa katika masuala ya elimu duniani, ambapo hakukuwa na upande wowote ule duniani uliokuwa ukivutiwa na sisi. Lakini hii leo kwa baraka za mapinduzi, kwa baraka za Uislamu na kwa baraka za sharia (za Kiislamu), Iran leo ni nchi ya 16 katika orodha ya nchi zenye kuongoza katika masuala ya elimu ulimwenguni. Haya sio maneno yetu, bali haya ni mambo ambayo yanasemwa na watu ambao wanafanya tathmini na uhakiki na kutoa ripoti kuhusiana na orodha ya nchi zenye mchango mkubwa katika uga wa elimu ulimwenguni. Vituo ambavyo vinabainisha haya vinatabiri kuwa, katika miaka kadhaa ijayo - wameainisha kabisa miaka mingapi, kwa mfano miaka kumi ijayo au kumi na mbili ijayo - Iran itakuwa miongoni mwa nchi 9 duniani katika uga wa masuala ya elimu; wamesema kuwa, Iran itashika nafasi ya nne duniani kielimu. Hii inatokana na kuwa, kasi ya elimu nchini Iran ni kubwa mno. Tab'an, kwa sasa sisi duniani bado tuko nyuma sana. Kasi yetu ni mara kadhaa ya kasi ya katikati ya kiwango cha dunia katika elimu, lakini pamoja na hayo bado tuko nyuma. Endapo tutasonga mbele tukiwa na kasi hii, bila shaka tutafika mbele. Hivyo basi inabidi tajiriba hii iliyofanikiwa iendelee na ishuhudiwe pia katika nchi nyingine za Kiislamu. Kuna vipawa katika ulimwengu wa Kiislamu. Tuna vijana wazuri; tuna vijana wazuri na wenye vipaji vizuri mno. Kuna kipindi katika historia, elimu ya dunia ilikuwa mikononi mwa Waislamu; kwa nini leo hili lisiwezekane? Kwa nini tusiwe na matarajio kwamba, miaka thelathini ijayo ulimwengu wa Kiislamu utaweza kufikia katika hatua ambayo utakuwa (yaani ulimwengu wa Kiislamu) ni marejeo ya kielimu ulimwenguni na watu wote wawe wakirejea katika nchi za Kiislamu kwa ajili ya masuala ya kielimu. Huu ni mustakabali ambao unawezekana kufikiwa; tufanye hima, idili na bidii. Haya yote yanawezekana kufikiwa kwa baraka za Uislamu na kwa baraka za mapinduzi. Mfumo wa Kiislamu nchini Iran umethibitisha kuwa inawezekana kuwa na kasi kubwa ya kielimu na pia kuwa na nafasi muhimu na ya juu ya kielimu kwa kutegemea Uislamu na sharia za Kiislamu.
Suala jingine muhimu - naona adhuhuri nayo imekaribia, wakati wa Sala unawadia hivyo lazima twende - ni kadhia ya umoja. Hii leo napenda kuwaambia kwamba: Makaka! Madada wapendwa! wenzo ambao uko mikoni mwa maadui zetu na ambao unaweza kutumiwa na maadui hao vizuri kabisa ni suala la hitilafu; Magharibi na Marekani zinafanya njama za kutumia majina mbali mbali kama vile "Ushia na Usuni", "Ukabila" na "Utaifa" ili kuzusha mifarakano na migongano kati ya Waislamu, hivyo Waislamu wote inabidi kuwa macho na wanapaswa wachanganue mambo kwa mtazamo huo na kuchukua maamuzi sahihi ya kukabiliana na njama hizo za maadui. Maadui wamekuwa wakizikuza hitilafu za Ushia na Usuni, lengo lao likiwa ni kupandikiza hitilafu. Mnaona katika nchi za Kiislamu, katika nchi hizi hizi ambazo zimefanya mapinduzi, maadui wamekuwa wakizusha hitilafu; wamekuwa wakizusha hitilafu na mifarakano pia katika maeneo mengine ya ulimwengu wa Kiislamu; kuna haja ya kufanya harakati kwa uono na mtazamo huu; watu wote wanapaswa kuwa macho na makini. Magharibi na Marekani ni maadui (wakuu) wa ulimwengu wa Kiislamu, kuna haja ya kufanya harakati na kuchanganua mambo sambamba na kuchukua hatua sahihi. Maadui wamekuwa wakifanya uchochezi, mashirika yao ya kijasusi yanafanya kazi; kila wanachokifikia wanakiharibu. Katika kadhia ya Palestina wamefanya njama na kukwamisha mambo kadiri walivyoweza; tab'an wameshindwa. Sisi tunasonga mbele na ulimwengu wa Kiislamu unasonga mbele.
Kadhia ya hivi karibuni ya Palestina, ni suala muhimu sana. Kulitokea vita vya siku nane baina ya Gaza na utawala wa Kizayuni wa Israel ambao unadai kuwa na jeshi imara na lenye nguvu zaidi katika Mashariki ya Kati; kisha wakati upande ule wa pili ulipotaka kusitisha vita, unaweka masharti, hawa ni Wapalestina! Hili ni jambo ambalo mtu anaweza kuliamini? Miaka kumi iliyopita kama wewe ungekuja na kusema maneno haya nani angeyaamini kwamba, kuna siku Wapalestina - sio Wapalestina wote, bali sehemu ndogo tu kijiografia ya Palestina yaani Ukanda wa Gaza - watakuja kupigana vita na utawala wa Kizayuni wa Israel, na kisha Wapalestina ndio watakaokuja kuweka masharti kwa ajili ya kusitisha vita hivyo? Hongereni sana Wapalestina! Hongereni! Hongera ziwaendee Hamas, Jihadul Islami na Brigedi za mapambano huko Palestina, na Gaza ilipigana na kuonesha ushujaa mkubwa na wa hali ya juu! Huu ndio ushujaa.
Kwa hakika binafsi natumia fursa hii na kwa hisa yangu kuwashukuru wanamapambano na wanamuqawama wote wa Kipalestina; kutokana na jinsi walivyojitolea, kutokana na hima waliyoionyesha na kutokana na subira kubwa waliyoionyesha na bila shaka mumeona kama anavyosema Mwenyezi Mungu:
"Basi kwa hakika pamoja na uzito upo wepesi" (Ash-Sharh 94: 05).
Endapo sisi tutasubiri namna hii, basi Mwenyezi Mungu Mtukufu atatupa faraja na ushindi. Wapalestina wamesubiri na wakasimama kidete, Mwenyezi Mungu Mtukufu akawapa faraja na ushindi; hili ni somo; ni somo kwao wao wenyewe na ibra na mazingatio pia kwa watu wengine. Msipuuze na kudharau huu umoja baina ya Waislamu; kadhia hii ni muhimu sana.
Nukta ambayo imezungumziwa hapa na ndugu kutoka Bahrain - kimya cha ulimwengu wa Kiislamu kuhusiana na kadhia ya Bahrain - ni kweli kabisa. Kile ambacho kinawafanya baadhi ya watu kunyamazia kimya kadhia ya Bahrain, ni suala la madhehebu na hili ni jambo linalosikitisha sana. Yaani endapo wananchi wa taifa fulani watasimama na kuanzisha harakati dhidi ya utawala fasidi na dhalimu, basi linalopaswa kufanyika ni kuwasaidia wananchi hao na kuwauinga mkono; isipokuwa kama wananchi hao ni Waislamu wa madhehebu ya kishia - kama Bahrain - wakati huo haifai kuwaunga mkono, kuwatetea wala kuwasaidia! Inasikitisha kwamba, hii ni mantiki ambayo ipo baina ya watu. Haya ni mambo ambayo yanapaswa kuwekwa kando kabisa. Kuna haja ya kumtambua adui, kuna haja pia ya kutambua na kufahamu nyenzo za adui na vile vile inapaswa kutambua hila na kedi za adui; zinaingia kutokea wapi? Mtazamo sahihi kuhusu masuala ya eneo hili ni kuyaangalia mambo hayo kwa kuzingatia njama, mbinu na hila za maadui. Msimamo wa Iran kuhusu kadhia ya Syria umesimama juu ya msingi huo huo. Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inapinga kumwagwa hata tone moja la damu ya Muislamu, lakini wanaokosea katika hali inayoshuhudiwa hivi sasa Syria ni wale watu ambao wameitumbukiza nchi hiyo katika hali ya machafuko na vita vya ndani, kuiharibu nchi hiyo na kuwafanya ndugu wauwane wao kwa wao. Sisi tunasema kuwa, watu ambao wanaivuta Syria upande wa kuitumbukiza katika kuiharibu na wamefanya hivyo, ndio wanaokosea. Matakwa yote ya wananchi inabidi yapiganiwe kwa njia maarufu zinazojulikana na kujiepusha na utumiaji mabavu na umwagaji wa damu.
Tuna matumaini kwamba, Mwenyezi Mungu Mtukufu atatuongoza. Tuna matumaini kwamba, Mwenyezi Mungu Mtukufu atazipa baraka harakati zenu. Inshallah Mwenyezi Mungu Mtukufu ataufanya mwamko huu adhimu katika ulimwengu wa Kiislamu uwe na mustakbali mzuri, mwema, unaong'ara na wenye baraka tele kwa Umma wa Kiislamu.
Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

 
< Nyuma   Mbele >

^