Skip to content

Habari

Habari
Hifadhi

Risala na Barua

Matini
Hifadhi

Kumbukumbu na Simulizi

Kabla ya Mapinduzi
Baada ya Mapinduzi

Sauti na Taswira

Picha
Sauti
Video
Hotuba ya Kiongozi Muadhamu Mbele ya Viongozi wa Mfumo na Wageni wa Mkutano wa Umoja wa Kiislamu Chapa
29/01/2013

Ifuatayo ni matini kamili ya hotuba ya Ayatullah Udhma, Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aliyoitoa alipokutana na viongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, wageni kutoka nje na wa Iran walioshiriki kwenye Mkutano wa 26 wa Umoja wa Kiislamu, mabalozi wa nchi za Kiislamu waliopo mjini Tehran na matabaka mbali mbali ya wananchi kwa mnasaba wa maadhimisho matukufu ya Maulidi yaliyojaa nuru ya Mtume wa Rehma, Mtume wa Mwisho, Muhammad al Mustafa SAW na mjukuu wake mtukufu Imam Jafar Sadiq AS tarehe 29/01/2013.

Kwa jina la Allah Mwingi wa rehema Mwenye kurehemu

Ninatoa mkono wa kheri, baraka na fanaka kwa mnasaba wa idi na sikukuu hii kubwa ( ya kukumbuka kuzaliwa Bwana Mtume SAW na mjukuu wake Imam Jafar Sadiq AS) kwenu nyinyi hadhirina nyote, wageni azizi mlioko hapa ambao mmetoka katika nchi nyingine, mabalozi wa nchi za Kiislamu (mlioko hapa mjini Tehran) na vile vile kwa wananchi wote azizi wa taifa kubwa la Iran ambao wamethibitisha kivitendo mapenzi yao na mfungamano wao kwa cheo cha Unabii. Aidha ninatoa mkono wa pongezi kwa umma mzima wa Kiislamu ambao unahisi umoja na kuwa kitu kimoja katika mhimili wa jina tukufu la Mtume wa Uislamu. Kadhalika ninatoa mkono wa pongezi kwa watu wote huru duniani; ambapo kwa hakika bishara ya kuzaliwa Bwana Mtume SAW na baraka za Mwenyezi Mungu zinazotokana na kuzaliwa huku kukubwa na kutukufu ambako ni kwa ajili ya watu wote huru duniani; ni kwa ajili ya wanaadamu wote wanaopigania uhuru, uadilifu na ni kwa ajili ya kufikia thamani aali za Mwenyezi Mungu. Baadhi ya watu wenye maarifa na silika za kimaanawi wanaamini kuwa, mwezi wa Rabiu Awwal (Mfunguo Sita) kwa maana halisi ya neno ni mwezi wa machipuo ya maisha; kwani katika mwezi huu walizaliwa Mtume Muhammad SAW na mjukuu wa Bwana Mtume SAW Imam Sadiq AS ambapo kuzaliwa Bwana Mtume SAW ni mwanzo wa baraka zote ambazo Mwenyezi Mungu Mtukufu alimpatia mwanadamu. Kwa hakika sisi tunaaamini kwamba, Uislamu ni wenzo wa saada na njia ya kumuokoa mwanadamu na hili linatokana na uwepo mtukufu wa Bwana Mtume SAW ambao ulitokea katika mwezi huu wa Rabiu Awwal (Mfunguo Sita).
Kwa hakika inapaswa kutambua kwamba, Mtume SAW ni chanzo cha baraka zote ambazo Mwenyezi Mungu ameipatia jamii ya mwanaadamu, umma wa Kiislamu na hivyo kuwanyanyua juu wafuasi wa kweli wa dini hii.
Haitoshi kufanya sherehe na kuadhimisha tu kumbukumbu na Maulidi ya kualiwa Mtume Mtukufu SAW; bali katika hatua ya awali ni lazima tuimarishe na kukuza mafungamano yetu ya kimoyo na Bwana Mtume SAW. Ulimwengu wa Kiislamu unapaswa kuimarisha siku baada ya siku mahusiano yake ya kimaanawi, kimoyo na kihuba na Nabii wa rehma; hii ni nukta ya pamoja ya Waislamu wote duniani. Wale watu ambao nyoyo zao zinaguswa na zinakwenda mbio kwa ajili ya kuunda umma wa Kiislamu wanapaswa kusimamia na kutilia mkazo nukta hii: mahusiano ya kimaanawi na huba kwa uwepo mtukufu wa Bwana Mtume SAW. Yaani katika hatua ya awali na kwa jaddi kabisa kuweko na uamuzi na azma ya kumfuata mbora huyo wa viumbe katika mambo yote. Katika aya Tukufu za Qur'ani kumetolewa maelezo kuhusiana na tabia ya Bwana Mtume SAW kwa watu, kuhusiana na miamala ya kisiasa ya Mtume SAW, kuhusiana na aina ya utawala wa Bwana Mtume SAW, kuhusiana na hisia ya mbora huyo wa viumbe kwa watu na - iwe ni kwa Waislamu au wasiokuwa Waislamu - na kadhalika. Malezi ya masahaba wa Mtume SAW katika zama na Mtume SAW pamoja na miamala yao inaonesha ishara za ule upande wa mafundisho na malezi ya umma wa Kiislamu yanayozingatiwa na Uislamu pamoja na Nabii huyo wa rehma. Haya ni mambo ambayo tunapaswa kuyatekeleza kivitendo katika maisha yetu (ya kila siku), tunapaswa kuyafanyia kazi haya; kwani hatupaswi kutosheka tu na kuyasema.
Hii leo uwanja wa jambo hili umeandaliwa. Mwamko wa Kiislamu ni uhakika ambao umetokea hii leo. Baada ya kupita makumi ya miaka ya mashinikizo ya maadui wa Uislamu dhidi ya jamii za Kiislamu, iwe ni kwa ukoloni wa moja kwa moja, au kwa sura ya ukoloni mpya na usio wa moja kwa moja, au iwe ni kwa njia ya ubeberu wa kiutamaduni, kiuchumi na kisiasa; baada ya miaka mingi ya mataifa ya Kiislamu kuwa chini ya mbinyo na chini ya mashinikizo makubwa ya ubeberu wa kimagharibi, madola ya Ulaya na Marekani, hatua kwa hatua mbegu ya mwamko (wa Kiislamu) imeanza kuchipua na kukua katika ulimwengu wa Kiislamu na sasa inaanza kuonekana na kujidhihirisha. Wananchi wa ulimwengu wa Kiislamu hii leo wanahisi kwamba, Uislamu ndio wenzo wa kuwaletea izza, heshima na mamlaka yao ya kujitawala. Kwa baraka za Uislamu, matarajio ya kitaifa ya wananchi yanaweza kufikiwa katika ulimwengu wa Kiislamu. Kwa baraka za Uislamu, mataifa ya Kiislamu yanaweza kusimama mkabala na ubeberu wa Magharibi, mkabala na ujeuri wa madola ya Magharibi, mkabala na uvamizi wa kidhulma wa madola ya Magharibi na mkabala na unyonyaji na Uistikbari wa madola ya Magharibi. Ulimwengu wa Magharibi hauna budi isipokuwa kurudi nyuma na kulegeza kamba; hii leo nyinyi mnashuhudia tajiriba hii katika ulimwengu wa Kiislamu. Jambo hili lilitokea nchini Iran miaka thelathini na ushei iliyopita; hii leo pia jambo hilo mnalishuhudia katika ulimwengu wa Kiislamu na katika eneo la kaskazini mwa Afrika. Hatua zimekuwa zikipigwa kuekea upande wa ushindi. Tab'an, bila shaka matatizo yapo; lakini kama sisi tutakuwa macho na makini matatizo hayawezi kuzuia njia yetu. Mwenyezi Mungu anasema katika Kitabu Kitakatifu cha Qur'ani:
"Maadui hawatakudhuruni ila ni maudhi tu." (Al-I'mran 3:111). Ni kweli wataudhi, watatuletea matatizo; lakini kama sisi tutakuwa na azma thabiti, tukatawakali na kumtegemea Mwenyezi Mungu na wakati huo huo tukawa tumeazimia kufanya harakati, basi bila shaka maadui hawawezi kututuwekea kizuizi katika njia yetu.
Hii leo wananchi wa mataifa ya Kiislamu wameamka; kwa baraka za Uislamu, wanahisi kwamba, wanaweza kusimama dhidi ya maadui wa Uislamu, wanahisi kwamba, wanaweza kusimama mkabala na kanali za kifasidi za Kizayuni ambazo zina udhibiti katika siasa za madola ya Marekani. Waislamu hivi sasa wanahisi kwamba, wanaweza kusema maneno yao na kuyatekeleza. Ushindi huu una thamani sana. Mwenyezi Mungu anasema:
"Mwenyezi Mungu anakuahidini ngawira nyingi mtakazo zichukua, basi amekutangulizieni hizi kwanza, (Al-Fat'h 48:20). Hii ni sehemu ya ahadi za Mwenyezi Mungu ambazo zimetimia. Mwenyezi Mungu anasema:
"na akaizuia mikono ya watu isikufikieni, na ili hayo yawe ni Ishara kwa Waumini, na akakuongozeni Njia Iliyo Nyooka." (Al-Fat'h 48:20).
Kila ushindi ambao taifa fulani linapata dhidi ya maadui, propaganda na mbinu na mikakati yao michafu, ni bishara ya Mwenyezi Mungu, ni ishara ya Mwenyezi Mungu na aya ya Mwenyezi Mungu ambapo kama mtafanya harakati basi mtapata natija yake.
Hii leo ulimwengu wa Kiislamu unakabiliwa na njama za maadui (kutoka kila upande). Napenda kuwaambia nyinyi makaka na madada wapendwa - iwe ni Wairani na wasio Wairani - ya kwamba, wenzo muhimu kabisa wa adui katika kukabiliana na mwamko huu wa Kiislamu ni kuzusha hitilafu na mifarakano baina ya Waislamu. Maadui wanawagombanisha Waislamu na kuwagonganisha vichwa Waislamu, wanawatumia Waislamu kuwaangamiza Waislamu wenzao, wanawashughulisha Waislamu na mambo haya; ni kitu gani bora kwa maadui ghairi ya kuwashughulisha Waislamu na mambo haya? Kuanzia siku ya kwanza ambapo mapinduzi ya Kiislamu yalipata ushindi nchini Iran, maadui walifuatilia na kutekeleza siasa za kuzusha na kupandikiza hitilafu na mifarakano baina ya wananchi wetu na katika nchi yetu; hata hivyo Jamhuri ya Kiislamu imekabiliana vilivyo na jambo hili na kwa nguvu zake zote. Katika uga wa kimataifa pia, maadui wamekuwa wakizusha hitilafu za kimadhehebu, lakini Jamhuri ya Kiislamu imetundika na kunyanyua juu bendera ya umoja na mshikamano. Sisi tumetangaza kuwa, Imamu wetu wa shani (Imamu Khomeini MA) alilisema hili mara chungu nzima na katika kipindi cha uhai wake na baada ya kufariki kwake dunia pia, wananchi wa Iran na taifa hili la Kiislamu walilikaririri na kulitilia mkazo jambo hili ya kwamba, sisi tunaamini kuhusiana na udungu wa Kiislamu.
Hakika sisi tunapinga kabisa kuweko mifarakano ya aina yoyote ile baina ya Waislamu; jambo hili kwa hakika ni kinyume kabisa na vibaraka wa maadui ambao wamekuwa wakitumia kila tukio na jambo dogo kwa ajili ya kuzusha mifaraano na hitilafu baina ya Waislamu (na ndio maana maadui wa Uislam wamekua wakiyakuza mambo madogo madogo na hitilafu ndogo ndogo na kuzifanya kuwa kubwa ili kwa nia hiyo waweze kufikia malengo yao). Endapo nyinyi mtatazama vyema na kwa umakini mtaona kuwa, siasa za maadui wa mwamko wa Kiislamu katika nchi za kaskazini mwa Afrika (na Mashariki ya Kati) ni kuzusha hitilafu na mifarakano. Hizi ndizo sera na siasa za ubeberu; maadui hawa wanafanya njama za kuwagombanisha Waislamu na kuwafanya Waislamu wakabiliane wao kwa wao.
Tiba mujarabu ya maradhi haya (hitilafu) ni kuhisi umoja baina ya Waislamu (na kudumisha umoja na mshikamano baina ya Waislamu sambamba na kujiepusha na kila aina ya hatua za kuleta hitilafu na mifarakano) ; mataifa ya Kiislamu yanapaswa kuungana na kuwa kitu kimoja. Ndani ya kila nchi, makundi tofauti, mapote mbalimbali, mirengo tofauti na madhehebu mbalimbali yanapaswa kuungana na kuwa kitu kimoja; wasiruhusu hitilafu za kifikra, kiitikadi kisiasa, kidhuku na kimirengo zitawale harakati zao za kimsingi, ili kwa njia hiyo waweze kukabiliana na adui; kwa hakika hii ndio njia pekee leo (ya kukabiliana na adui). Mabeberu wanatumia kila nui ya hila na kedi akifanya hima ya kuzusa hitilafu na mifarakano na bila shaka mnayaona hayo. Wakati Waislamu watakapokuwa wameshughulishwa na hitilafu baina yao, kadhia kama ya Palestina husahaulika; suala la kusimama kidete wa ajili ya kukabiliana na uendaji makuu wa Marekani husahalika; kwa msingi huo mabeberu hao hupata fursa ya kutekeleza kivitendo mipango na mikakati yao.
Hii leo kunashuhudiwa kwamba, Wamagharibi wameanzisha harakati mpya huko Afrika ka ajili ya kuwa na udhibiti wa mataifa ya bara hilo na hivyo kuweko tena (mabeberu hao) katika maisha ya wananchi wa bara la Afrika. Wakati moto wa hitilafu na mifarakano unapowaka, adui hupata wasaa na muda wa kufanya mambo yote (ayatakayo). Katika majirani zetu yaani Pakistan, bila shaka mnaona jinsi maadui walivyozusha hitilafu na mifarakano na kusababisha kutokea maafa makubwa katika nchi hiyo. Nchini Syria, mnashuhudia pia jinsi maadui hawa wanavyosababisha wananchi wauwane wao kwa wao. Nchini Bahrain mnashuhudia pia jinsi sauti (ya kutaka mageuzi) ya wananchi wanchi hiyo inavyozimwa na kukandamizwa kwa nguvu zote; wananchi wa nchi hiyo wamekuwa wakikandamizwa vibaya na kwa kila wenzo. Nchini Misri na katika maeneo mengine duniani, mnashuhudia jinsi (maadu wa mageuzi na mwamko wa Kiislamu) wanavyowagonganisha vichwa wananchi. Hizi ni siasa ambazo yumkini zikawa na msukumo na matashi ya mtu binafsi na msukumo wa kiitikadi wa baadhi ya watu; lakini kimsingi mkakati na mpango jumla ni maadui.
Mimi simtuhumu mtu ya kwamba, anatekeleza mpango wa adui kwa kujua na kwa makusudi, lakini ninasema kwa yakini kabisa kwamba: Kila harakati ya kuzusha harakati kwa sura yoyote ile baina ya wananchi wa mataifa ya Kiislamu au ndani ya nchi fulani baina ya wananchi ni kucheza katika uwanja ambao adui ameainisha yaani ni kufanya mambo ambayo adui anayataka; ni kumsaidia adui. Watu wote wanapaswa kulipa uzito suala la umoja; katika hatua ya awali yaani watu wanaopaswa kuwa mstari wa mbele katika hili ni wenye vipaji, wenye vipaji vya kisiasa, wenye vipawa vya kidini, watu wa vyuo vikuu wenye vipaji, watu wenye vipawa katika Hawza (Chuo Kikuu cha Kidini) na kila mahala. Watu wote wanapaswa kulizingatia na kulipa uzito mkubwa suala la umoja. Kuzusha hitilafu za kimadhehebu baina ya makundi mbalimbali ya Waislamu ni hatari kubwa mno. Kama maadui wataweza kuwasha moto wa hitilafu mahala, basi kuuzima moto huo ni miongoni mwa kazi ngumu kabisa. Hivyo kuna haja ya kuzuia mambo haya; na hili halitawezekana isipokuwa kwa kuweko ubunifu wa amali, hima na ikhalasi ya watu wenye vipawa katika kia nchi; maulama, watu wa vyuo viku, wanasiasa na watu ambao wana taathira na ushawishi (katika jamii); wawabainishie wananchi mikakati ya adui, mtazamo wenye matumaini wa adui wa kuzusha hitilafu baina ya wananchi, baina ya nchi za Kiislamu, baina ya Suni na Shia na baina ya mapote mbalimbali katika madhehebu tofauti ya Kiislamu; wanapaswa kufanya hima ya kuwaamsha watu na kuwajulisha haya.
Hii ni hatari kubwa sana na adui ana tajiriba na hili. Waingereza wana tajiriba kubwa na ya muda mrefu katika uwanja huu. Kwa hakika sisi tunasoma haya katika historia na tunaona ni mambo gani waliyoyafanya kwa ajili ya kuzusha hitilafu. Waingereza wanafahamu hili na wengine wamejifunza kutoka kwao. Wanafanya juhudi kubwa ya kuzusha hitilafu; kuna haja ya kujiepusha na kuwa makini tusinase katika mtego wao. Tunapaswa kuwa makini na hatupaswi kufanya mambo kwa hisia za kijuujuu na hivyo kuzidi kuuwasha moto huo (wa hitilafu uliowashwa na maadui); hili ni jambo ambalo linaharibu mustakbali wa mataifa; na kuyafanya mataifa kukumbwa na hatima mbaya; kwa hakika jambo hili linawasaidia maadui wa Uislamu, maadui wa Waislamu na maadui wa mamlaka ya kujitawala katika kazi zao; linasaidia mipango yao kufanikiwa; hivyo kuna haja ya kuwa macho.
Nara na shaari ya umoja wa Kiislamu ni kaulimbi takatifu. Kama leo Bwana Mtume Muhammad SAW angekuweko baina yetu basi angetulingania umoja na kujiepusha na hitilafu kama hizi. Bwana Mtume SAW angetegemea aya tukufu ya Qur'ani isemayo:
Hakika amekwisha kujieni Mtume kutokana na nyinyi wenyewe; yanamhuzunisha yanayo kutaabisheni; anakuhangaikieni sana. Kwa Waumini ni mpole na mwenye huruma. (At-Tawba 9:128).
Endapo sisi tuna mapenzi kiasi hiki na Mtume wa Uislamu yaani Nabii Muhammad SAW basi tunapaswa kuhakisha kwamba, takwa hili lisilo na shaka la Nabii huyo wa rehma litatimia.
Tunamuomba Mwenyezi Mungu atupe tawfiki sote ili tuweze kukifanyia kazi kile tunachokisema.
Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

 
< Nyuma   Mbele >

^