Skip to content

Habari

Habari
Hifadhi

Risala na Barua

Matini
Hifadhi

Kumbukumbu na Simulizi

Kabla ya Mapinduzi
Baada ya Mapinduzi

Sauti na Taswira

Picha
Sauti
Video
Hotuba ya Kiongozi Muadhamu Mbele ya Maafisa wa Jeshi la Anga la Jamhuri ya Kiislamu Chapa
07/02/2013

Ifuatayo hapa chini ni matini kamili ya hotuba ya Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aliyoitoa mbele ya hadhara kubwa ya makamanda, maafisa na wafanyakazi wa Jeshi la Anga la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran tarehe 07/02/2013.

Kwa jina la Allah Mwingi wa rehema Mwenye kurehemu

Nina furaha mno na ninamshukuru Mwenyezi Mungu kwani kwa mara nyingine tena nimeweza kukutana nanyi makaka, wanangu azizi, vijana azizi wa kikosi cha jeshi la anga la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika miadi ya kila mwaka. Karibuni nyote. Wimbo ulioimbwa hapa, ulikuwa na mashairi mazuri, uliiimbwa vizuri na kwa hakika ulikuwa umebeba maana kubwa; Inshallah nyoyo zetu na zenu daima ziwe na dondoo za rehma na hidaya ya Mwenyezi Mungu ambapo hii ni kinga muhimu kabisa.
Mtu akikitazama kikosi cha anga cha Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa mtazamo wa kawaida na uliozoeleka ataona na kudiriki uhakika na ukweli muhimu katika kipindi cha miaka yote hii. Kuna kipindi fulani nyinyi hata ndege ambayo mlikuwa nayo hamkuwa na uwezo na hamkuruhusiwa kuifanyia marekebisho na hivyo kuifanyia kazi. Hii leo nyinyi (mmepiga hatua )mnatengeneza ndege za mafunzo; ndege za kijeshi; mnafanya kazi muhimu; na mnazalisha na kutengeneza vipuli nyeti kabisa. Harakati adhimu, mapenzi, ubunifu na harakati ya kuelekea upande wa kujiamini na kujitosheleza katika jeshi la anga, katika jeshi lote, katika vikosi vya ulinzi na katika nchi nzima ni harakati ambayo hata wapinzani wa Jamhuri ya Kiislamu hawawezi kuikana. Mfumo wa kibeberu ambao ukipata msaada wa mabavu na msaada wa silaha na hujuma za kijeshi ulifanya njama za kuyapokonya mataifa duniani mamlaka na maamuzi na yayafanye mataifa hayo kuwa tegemezi kwa madola makubwa na yenye satwa na udhibiti duniani - ambapo nyuma yao kuna makampuni ya Kizayuni na yasiyo ya Kizayuni ambayo yamepanga safu - hayawezi kupata njia ya kukabiliana na adhama, shakhsia, utambulisho na mamalaka ya kujitawala, nyinyi (maadui) mmeshindwa katika uga huu. Hii leo nyinyi mnaona wazi kabisa kabisa; hebu lilingalisheni taifa la Iran na mataifa mengine ambayo yalikuwa chini ya satwa na udhibiti wa Marekani kwa muda wa miaka thelathini; hebu tazameni na muone nyinyi mko wapi na wao wako wapi sasa. Taifa la Iran kwa muda wa miaka thelathini limezungumzia suala la mamlaka yake ya kujitawala; limekariri suala la haki yake; limesimama na kuwaambia mabeberu "hapana" na sasa limefikia hapa lilipo. Kulikuweko na tawala na mataifa ambayo katika kipindi hiki cha miaka thelathini yalikuwa chini ya udhibiti na satwa ya Marekani - tawala ambazo ziliwekwa madarakani na Marekani na kutumbukiza wananchi wao katika satwa na udhibiti wa Marekani - bado zipo katika hali hiyo hiyo hadi leo; hebu tazameni hii leo wao wako wapi na nyinyi mko wapi. Taifa la Iran kwa kufanya harakati yake, kwa kuwa na mamlaka yake ya kujitawala, kwa kuwa na hali ya kujiamini kwake na kwa kumtegemea kwake Mwenyezi Mungu limethibitisha kwamba, inawezekana na ni lazima kusimama mkabala na ubeberu wa wageni na madola yenye kutaka kuwa na satwa na udhibiti, na kwamba, hilo ni jambo ambalo linawezekana. Hili ni jambo ambalo taifa la Iran limelithibitisha (kivitendo na sio kwa nara na kaulimbiu) . Miaka thelathini iliyopita, taifa la Iran lilikuwa wapi katika kafila (msafara) wa elimu, ustaarabu, maendeleo, teknolojia na ushawishi wa kisiasa? Na hii leo liko wapi? Hii leo kwa baraka ya kusimama kwake kidete, kwa baraka ya kutawakali kwake na kumtegemea Mwenyezi Mungu na kwa baraka ya kuleta kwake uwanjani vipaji vyote, limeweza kufikia hatua hii na hii ni tajiriba kwa taifa la Iran na kwa vizazi vijavyo. Aidha hii ni tajiriba kwa mataifa mengine; na kwa hakika kikosi cha anga cha Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni mfano wa wazi katika kusimama kidete na kufanya harakati kwa kujitegemea na kujiamini. Hili ni jambo ambalo mnapaswa kuliendeleza na kulifanya liwepo. Sisi tukiwa kama taifa la Iran tunapaswa kuliendeleza hili. Hii ni njia ambayo ina baraka tele (na kila anayeshikamana nayo anafanikiwa).
Katika kipindi hiki cha miaka thelathini na ushei, maadui wa taifa la Iran wamefanya kila waliloweza dhidi ya taifa hili; hakuna jambo au njama ambayo hawajaifanya dhidi ya taifa la Iran; walifanya uchochezi, walianzisha vita, kadiri walivyoweza walimpa himaya na kumsaidia adui wa Jamhuri ya Kiislamu (ya Iran) na kwa nguvu zao zote, waliendesha upinzani mkali, walifanya upinzani laini; walipambana na taifa la Iran kadiri walivyoweza na kwa kutumia nguvu zao zote; lakini taifa la Iran limesimama kidete; sio tu kwamba hawakuweza (kufikia malengo yao) na kulipigisha magoti taifa hili, bali hawakuweza pia kulizuia taifa hili lisijipatie maendeleo - taifa hili limepata maendeleo makubwa mno - kila jambo ambalo lilikuwa katika uwezo wao walilifanya katika kipindi hiki cha miaka thelathini; walifanya njama, walianzisha mapinduzi, walifanyaa uchochezi wa kijeshi, walishambulia ndege, walitekeleza vikwazo vigumu na shadidi; waliongeza na kushadididisha vikwazo siku baada ya siku, kwa matumaini kwamba, labda wataweza kuwatoa wananchi wa Iran katika medani; wataweza kuwafanya wananchi wa Iran wakate tamaa; wataweza kuwafanya wananchi wa Iran wawe na mtazamo mbaya na Uislamu na Jamhuri ya Kiislamu; lakini wameshindwa na kugonga mwamba kwani kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu na baraka Zake, wananchi wa Iran wamezidi kuwa na hamasa, wako imara na ni waaminifu na waamilifu zaidi. Hili ndilo faili la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Masiku haya ni masiku ya Alfajiri Kumi, ni fursa nzuri na maridhawa ambayo watu wetu wateule, watu wetu wenye welewa na muono wa mbali, vijana wetu na wananchi wetu wanaweza kuitumia kwa ajili ya kufanya tathmini ya kazi katika kipindi cha miaka hii thelathini na ushei (tangu kupatikana ushindi wa mapinduzi ya Kiislamu hapa nchini mwaka 1979 kwa uongozi wa busara wa Imam Ruhullah Khomeini MA); waone maendeleo waliopiga; waone juhudi zao zilizokuwa na mafanikio; waone auni na msaada wa Mwenyezi Mungu; waone udhaifu wa hila na kedi za maadui; ambapo Mwenyezi Mungu anasema: Na Makafiri wakafanya vitimbi na Mwenyezi Mungu akafanya vitimbi, na Mwenyezi Mungu ndiye mbora wa wenye kufanya vitimbi (Al-I'mran 3:54). Kwa hakika hii imekuwa ni kanuni na muongozo jumla wa kazi kwa ajili yetu ambao tunatumia kwa ajili ya kuchagua njia yetu ya mustakbali. Nyinyi katika kikosi cha anga mnapaswa kufanya harakati mkiwa na mtazamo huu; songeni mbele mkiwa na mtazamo huu. Nyuga na sekta mbalimbali hapa nchini, wananchi na maafisa wa serikali hapa nchini wanapaswa kufanya harakati wakiwa na mtazamo huu.
Tab'an, adui anaudhi na kusumbua, lakini hawezi kufanya kazi nyingine ghairi ya hii. Siku chache zilizopita nilisema kuwa, Mwenyezi Mungu anasema katika Kitabu kitakatifu cha Qur'ani kwamba:
Maadui hawatakudhuruni ila ni maudhi tu. Na wakipigana nanyi watakupeni mgongo, na tena hawatanusuriwa (Al-I'mran 3:111).
Hivyo basi kazi ya maadui ni kuudhi lakini hawawezi kukuzuieni nyinyi msifanye kitu, hawawezi kufunga njia yenu. Katika kipindi chote cha miaka hii thelathini, Wamarekani wamefanya kila waliloweza dhidi ya taifa lran, wamesema kila walilokuwa na uwezo nalo, wamefanya kila walilokuwa na uwezo nalo, wameendesha propaganda, wametekeleza utawala khabithi wa vyombo vya habari dhidi ya taifa la Iran; natija yake imekuwa hii ambayo inaoneakna leo, ambapo kwa fadhila za Mwenyezi Mungu taifa la Iran limekuwa na nishati zaidi, taifa hili limekuwa azma zaidi, imara zaidi, taifa hili limekuwa amilifu zaidi na zaidi, limekuwa ni lenye hamasa zaidi na lenye ustawi zaidi katika nyuga na nyanja mbalimbali; Wamarekani walikuwa wakitaka kuwatenganisha wananchi wa Iran na mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu (unaotawala hapa nchini) na mapinduzi. Kila mwaka wananchi wa Iran hujitokeza kwa wingi katika maandamano ya tarehe 22 Bahman (maandamano ambayo hufanyika kwa mnasaba wa kumbukumbu ya ushindi wa mapinduzi ya Kiislamu) ambapo hutangaza na kuonyesha uwepo wao wa kitaifa na kimapinduzi na hivyo kumkwamisha tena adui; hivyo lengo la maadui ni kuwatenganisha wananchi na mfumo wa Kiislamu pamoja na mapinduzi yao ya Kiislamu. Waziri wa Mashauri ya Kigeni asie na tajiriba aliyepita wa Marekani alisema dhahiri shahiri kwamba, "sisi tunaweka vikwazo ili tuwafanye wananchi wa Iran wakabiliane na mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu; bila shaka wananchi wa Iran watawapa majibu kwa harakati yao na kwa kujitokeza kwao kwa wingi katika maandamano ya Bahman 22 na mtaona katika siku hiyo jinsi wananchi wa Iran watakavyotoa jibu lao kali na hivyo kumkwamisha adui kwa mara nyingine. Bahati nzuri na adhimu kwa taifa hili ni kwamba, wananchi wameamka na wako makini, wanafahamu maana ya kazi ya maadui, wanaelewa harakati ya adui; wanafahamu kwa nini adui anatekeleza siasa hizi, hivyo wanafanya harakati katika upande ambao ni kinyume na malengo ya adui, wanasisitiza misimamo yao, wanaonesha mahudhurio yao makubwa katika uga wa izza (heshima) ya kitaifa, wanaonesha uwepo wao na kuthibitisha uwepo wao; hii ndio bahati nzuri na adhimu na bila shaka huu ni uzuri wa kaadhia. Wananchi kwa kujipamba kwa sifa ya kuwa macho na kuwa na muono wa mbali wa kitaifa, wanazijua vizuri njama za Wamarekani na Wazayuni katika harakati zao zote na bila shaka wananchi wa Iran hawafanyi kosa katika matendo na misimamo yao na uhakika huo. Kwa hakika hii ni bahati nzuri na kubwa katika mambo yetu adhimu na ya kitaifa.
Hivi karibu Wamarekani wamekuja tena na suala la kutaka kufanya mazungumzo, wanakariri wazi wazi kwamba, Marekani iko tayari kufanya mazungumzo ya moja kwa moja na Iran; kwa hakika matamshi ya viongozi hao hayana mapya kwani wamekuwa wakiyatoa na kuyakariri katika nyakati tofauti na mara zote taifa la Iran limekuwa likiyapima matamshi hayo ya viongozi wa Marekani na vitendo vyao viongozi hao; yaani je matamshi yao hayo yanaendana na vitendo na miamala yao wanayoifanya dhidi ya Iran?. Hii sasa imekuwa zamu ya walioingia uwanja kukariri tena kwamba, Marekani iko tayari kufanya mazungumzo na Iran. Wanadai kwamba, sasa mpira uko katika uwanja wa Iran, mpira uko katika uwanja wenu, ni nyinyi ambao mnapaswa kutoa majibu, ni nyinyi ambao mnapaswa kusema kwamba, mazungumzo yanayoambatana na mashinikizo na vitisho yana maana gani? Mazungumzo ni kwa ajili ya kuonesha nia njema. Nyinyi makumi ya kazi (dhidi ya Iran) ambazo kimsingi zinaonesha kwamba, mna nia mbaya (hamna nia njema kabisa) kisha mnasema mnataka "mazungumzo"? Hivi mnataraji kwamba, taifa la Iran litakubali na kuridhika kwamba, nyinyi mna nia njema? Tab'an, sisi tunadiriki na kufahamu ni kwa nini Wamarekani katika masiku haya wanazungumzia na kukariri tena suala la kutaka kufanya mazungumzo na Iran, wamekuwa wakilikariri hili kwa lugha tofauti; sisi tunafahamu sababu ya hilo ni nini? Chambilecho Wamarekani wenyewe " siasa zao katika Mashariki ya Kati zimegonga mwamba". Kwa hakika siasa za Marekani zimeshindwa na kugonga ukuta katika Mashariki ya Kati. Wanahitajia kitu ambacho kitakuwa kama ni kuonesha karata ya ushindi; karata hiyo ya ushindi kwa mtazamo wao ni: Kuuleta katika meza ya mazungumzo mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ambao umetokana na mapinduzi ya wananchi; hivyo basi (kwa sasa) wanahitajia hili. Eti wanataka kuitangazia dunia kwamba, wao wana nia njema. Hapana, kwa hakika sisi hatuoni nia yao yao njema hata kidogo. Miaka minne iliyopita - mwanzoni mwa serikali ya sasa ya Marekani - wakati Wamarekani walipokuwa wanasema maneno haya (kwamba, wanataka mazungumzo na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran) mimi nilitangaza kwamba, hatutoi hukumu kabla ya kitu, hatuhukumu mapema, sisi tunatazama na kuona vitendo vyao vikoje; baada ya hapo ndipo tutakapotoa hukumu. Sasa baada ya miaka minne, hukumu ya wananchi wa Iran ni ipi? Wamarekani waliunga mkono fitina ya ndani, wakawasaidia walioendesha fitina, katika kiwango cha kieneo, walituma majeshi yao katika nchi kama Afghanistan kwa madai ya kupambana na ugaidi, wakawakandamiza na kuwauwa watu wote hawa wasio na hatia yoyote; hii leo wanashirikiana na magaidi wale wale huko Syria, wanawasaidia; wale wale magaidi ambao waliwatumia kadiri walivyoweza nchini Iran, vibaraka wao, washirika wao na majasusi wa utawala wa Kizayuni wa Israel wamewauwa wanasayansi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, hawakuwa tayari hata kulaani bali walisimama na kuunga mkono mauaji hayo; huu ndio utendaji wao (hii ndio Marekani); wametekeleza vikwazo walivyokuwa wakitaka dhidi ya taifa la Iran na wanasema wazi kwamba, vikwazo hivi ni vya kulemaza kabisa. Mlikuwa mnataka kumlemaza nani? Mlikuwa mnataka kulilemaza taifa la Iran? Nyinyi mna nia njema kweli nyinyi? Mazungumzo (ya kweli na ambayo hayana hadaa ndani yake) yanapaswa kuwa na nia njema na katika masharti na mazingira sawa. Katika mazingira kama haya ndipo mazungumzo yanapokuwa na maana; hii inatokana na kuwa, hakuna upande ambao unataka kuuhadaa upande mwingine; (kinyume na hivyo mazungumzo hayo yatakuwa hayana maana yoyote ghairi ya kuhadaa na kupotezeana muda)
Mazungumzo kwa sura ya mbinu na mkakati na mazungumzo kwa ajili kuonyeshasura na umbo la dola lenye nguvu duniani (kuonesha ubabe), mazungumzo kama haya ni harakati ya hila na hadaa; hii sio harakati ya kweli. Mimi sio mwanadiplomasia, mimi ni mwanamapinduzi, ninasema kwa uwazi na bila kificho. Mwanadiplomasia anasema kitu huku akiwa na irada nyingine. Sisi tunasema kwa uwazi na kwa ukweli kabisa; sisi tunasema maneno yetu kwa azma na irada kamili. Katika mazingira kama haya mazungumzo huwa na maana, kwani kuna hali ya kuonyesha nia njema; wakati upande wa pili unapokuwa hauonyeshi nia njema, nyinyi wewe mnasema "mashinikizo na mazungumzo"; haya ni mambo mawili ambayo hayaoani kabisa, yaani kutaka kufanya mazungumzo na mtu na wakati huo huo unamuwekea vikwazo na kumtisha. Nyinyi mnataka kulionyeshea silaha taifa la Iran, semeni hili: hivyo basi imma fanyeni mazungumzo au fyatueni risasi. Kama mnataka kulitisha taifa la Iran tambueni kwamba, taifa ili halitishiki ng'o na vitu kama hivi.
Baadhi ya watu nao kutokana na kuwa na fikra finyu na welewa mdogo na baadhi ya wengine wakiwa na gharadhi na lengo fulani - haiwezekani tu kuhukumu moja kwa moja kuhusiana na watu, lakini kazi ya mtu mwenye fikra finyu na mtu mwenye malengo fulani kiasili haina tofauti - wanafurahia wakisema ndio njooni; hapana, hali haiko namna hii, mazungumzo hayatatui kitu; kufanya mazungumzo na Marekani hakutatui matatizo; ni mahala gani ambapo (Wamarekani) wametekeleza ahadi zao walizotoa? ni miaka sitini sasa ambapo kuanzia tarehe 28 Mordad 1332 (Agosti 1953) Hijria Shamsiya mpaka leo kila mahala ambapo viongozi wa nchi hii waliwaamini Wamarekani basi walipata pigo na kudhurika. Kuna siku Musaddiq (Waziri Mkuu wa zamani wa Iran) aliwaamini Wamarekani, akawategeme na kuwahesabu kuwa ni marafiki zake likaja kutokea tukio la mapindzi ya Mordad 28 (Agosti 1953) ambapo mahala pa kufanyika mapinduzi pakawa mikononi mwa Marekani ambapo kibaraka wa mapinduzi aliyekuja mjini Tehran akiwa na mabegi yaliyojaa pesa ambazo alizigawa baina ya wahuni ili wafanye mapinduzi alikuwa Mmarekani.
Wamarekani walikuja kukiri ubunifu wa hili na kwamba walihusika. Kisha baadaye wakaja kuwa na satwa na udhibiti wa miaka mingi kwa utawala wa kidhulma wa Kipahlavi, wakaunda SAVAK (Shirika la Usalama wa Ndani la utawala wa kidikteta na kitaghuti wa wakati huo nchini Iran) , wakawatesa na kuwaadhibu wanamapambano; haya ni mambo ambayo yalifanyika katika zama zile. Baada ya mapinduzi pia katika kipindi fulani maafisa na viongozi wa serikali (wa wakati huo) kutokana na kuwa na mtazamo mzuri (na Marekani) wakawaamini (Wamarekani) katika hali ambayo Marekani ilikuja na kuiweka Iran katika mhimili wa shari. Nyinyi (Marekani) ndio dhihirisho la shari; ni nyinyi ambao mnafanya ushari duniani, mnaanzisha vita, mnapora mali za mataifa mengine, mnauunga mkono utawala wa Kizayuni wa Israel, (unaotenda jinai kila siku dhidi ya Wapalestina) mataifa ambayo leo yamesimama katika tukio hili la mwamko wa Kiislamu mnafanya kila muwezalo kuwakandamiza wananchi wake, mnawadunisha na kuzusha hitilafu baina yao; ushari ni mali yenu nyinyi (Marekani) na hii ndio sifa yenu. Wamelituhumu taifa la Iran kwamba, ni taifa la ushari; kwa hakika hili ni tusi na udhalilishaji mkubwa. Kila mahala ambapo Wamarekani waliaminiwa, wao walifanya harakati namna hii. Hivyo wanapaswa kuonyesha nia njema. Anuani ya mazungumzo na pendekezo la mazungumzo ni mambo ambayo hayaendani na mashinikizo; mazungumzo yana njia yake na mashinikizo nayo yana njia yake yaani mawili haya hayawezi kuwa katika njia moja; hakuna uwezekano wa taifa la Iran kukubali kukaa na kufanya mazungumzo na mtu mwenye lugha ya mashinikizo na vitisho. Tufanye mazungumzo ili? Tufanye mazungumzo ili iweje?
Hii leo taifa la Iran limeamka. Sura (halisi) ya Marekani imefahamika sio ndani ya Iran tu bali hata katika eneo (Mashariki ya Kati); wananchi duniani wana dhana mbaya na Marekani na dhana hii mbaya ina ushahidi mwingi; taifa la Iran limetambua hila na njama za Marekani, linaelewa kusudio na dhumuni la Marekai ni lipi na wakati huo taifa hili limeamka. Hivyo kama watatokea watu na kutaka kurejesha tena satwa ya Marekani katika nchi hii, wakataka kufumbia macho maslahi ya kitaifa, maendeleo ya kielimu na harakati ya mamlaka ya kujitawala ili kuiridhisha Marekani, watashikwa mashati na wananchi; mimi pia kama nitataka kufanya harakati ambayo ni kinyume na matakwa jumla ya wananchi, wananchi watalalamika; hili ni jambo ambalo liko wazi. Viongozi wote wana jukumu la kulinda maslahi ya taifa, kulinda mamlaka ya kitaifa ya kujitawala na kulinda heshima ya nchi.
Sisi tumefanya mazungumzo na mataifa ambayo hayana na hayajawahi kufanya njama dhidi ya Iran, tumefunga nao mikataba (ya ushirikiano) na kuwa na mahusiano nao; nchi ya Iran ni nchi ya amani; nchi ya subira na uvumilivu; umoja wa taifa la Iran uko kwa ajili ya kuhudumia maslahi jumla ya mwanaadamu; hii leo kile ambacho kinafanywa na taifa la Iran kwa ajili ya maslahi ya kitaifa ni kwa ajili pia ya maslahi ya umma wa Kiislamu na manufaa ya mwanadamu. Na bila shaka auni na msaada wa Mwenyezi Mungu upo pamoja na taifa la Iran. Wananchi wa Iran kwa kuwa na muono huu wa mbali, azma hii thabiti walioyonayo, kusimama kwao huku kidete katika njia hii walikokuonyesha, Inshallah hali hii itaendelea hivi, wataweza sio tu kulifanya taifa la Iran likwee vilele vya fakhari, bali hata umma wa Kiislamu. Njia ya hili ni sisi kulinda huu muono wa mbali; njia ya hili ni kulinda na kudumisha huu umoja wetu; njia ya hili ni maafisa na viongozi wa serikali kulinda na kuhifadhi maslahi ya nchi. Hizi tabia mbaya zinazoshuhudiwa katika baadhi ya nyanja, medani na baina ya baadhi ya viongozi wa nchi - ambapo mimi nitalizungumzia hili hapo mbeleni, Inshallah nitazungumza na wananchi kuhusiana na tabia hizi mbaya - zinapaswa kuwekwa kando. Taifa la Iran ni moyo mmoja, limeazimia na ni amilifu. Endapo kuna hitilafu za kimizatamo na kinadharia katika masuala mbalimbali baina ya wananchi, watu wote wanapaswa kuweka kando hayo na kusimama katika safu moja dhidi ya adui na kukabiliana na watu ambao wamejizatiti ili kutoa pigo kwa taifa hili na kwa mfumo huu. Wananchi wa viongozi wote kwa pamoja wanapaswa kuungana na kuwa kitu kimoja; hakuna tofauti baina ya wananchi katika upande huu.
Inshallah tarehe 22 Bahman kwa maara nyingine tena wananchi watajitokeza na kwa fadhila na baraka za Mwenyezi Mungu na tawfiki Yake, wananchi wote watajitokeza uwanjani kwa ajili ya kuhifadhi na kulinda misingi na nguzo za mapinduzi haya na wako tayari na kwa moyo mmoja na bila shaka tawfiki ya Mwenyezi Mungu itakuwa pamoja nao.

Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

 
< Nyuma   Mbele >

^