Skip to content

Habari

Habari
Hifadhi

Risala na Barua

Matini
Hifadhi

Kumbukumbu na Simulizi

Kabla ya Mapinduzi
Baada ya Mapinduzi

Sauti na Taswira

Picha
Sauti
Video
Hotuba ya Kiongozi Muadhamu Mbele ya Wanafunzi na Wanachuo Chapa
31/10/2012

Ifuatayo ni hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika mkutano na wanafunzi na wanachuo kwa mnasaba wa kuwadia Siku ya Taifa ya Kupambana na Uistikbari aliyoitoa tarehe 31/102012.

Bismillahir Rahmanir Rahim

Inshallah Mwenyezi Mungu Mtukufu akujaalieni nyinyi vijana wapenzi na mimea imara inayochipua mfaidike na dua ya mtukufu Mahdi (Salamullahi alayhi wa ajjalallahu farajah). Shairi lililosomwa lilikuwa la kuvutia; mahadhi yake yalikuwa mazuri, yenye maana na madhumuni ya kina na kuwiyana na kile ambacho kijana Muislamu wa Kiirani wa leo, mwenye azma na irada anapaswa kuwa nacho ndani ya moyo wake na ndani ya nafsi yake. Inshallah Mwenyezi Mungu akupeni taufiki.
Kwanza ninakupeni mkono wa heri na baraka wa Sikukuu ya Ghadir, kuzaliwa kwa mtukufu Hadi (Alayhi ssalam) na Siku ya tarehe 13 Aban (Novemba 4) ambayo ni dhihirisho la sura yenye azma thabiti ya taifa la Iran ya kufikia malengo na kusimama imara kukabiliana na maadui. Ghadir ni tukio muhimu; ni tukio la usuli na la msingi linalobainisha umuhimu ambao Uislamu umeipa nguzo muhimu zaidi ya kuasisi mfumo wa Kiislamu na jamii ya Kiislamu. Yaani suala la Uimamu na suala la ‘Wilaya' na kuendelea kuhuisha Ghadir, maana yake ni kuendelea kuuhuisha Uislamu. Suala hili si suala la Shia tu na wale wenye imani na itikadi ya ‘Wilaya' ya Amirul Muuminin (alayhis salam). Ikiwa sisi Waislamu wa Kishia na tunaodai kuwa wafuasi wa Amirul Muuminin tutabainisha sawasawa na kwa usahihi hakika ya Ghadir, kwa sisi wenyewe kuifahamu barabara na pia kwa kuwatambulisha wengine, suala lenyewe la Ghadir linaweza kuwa chanzo cha kuleta umoja. Itikadi ya moyoni na mfungamano wa madhehebu moja ya dini na msingi na usuli mmoja wa kiitikadi hilo ni suala moja, na kulielewa barabara jambo hilo ni suala jengine. Uislamu umelidhihirisha katika Ghadir suala aali na tukufu zaidi katika uundaji wa jamii ya Kiislamu, Mfumo wa Kiislamu na Ulimwengu wa Kiislamu. Ni matumaini yetu kuwa sisi tutajitahidi kuwa wafuatiliaji wa kuelewa maana, madhumuni na makusudio halisi ya Ghadir na ‘Wilaya' kwa maana yake halisi; na inapasa nyinyi vijana muwe nalo hili akilini mwenu na inshallah mlifuatilie na kuliendeleza katika maisha yenu yote.
Kuna mengi ya kusema kuhusu suala la tarehe 13 Aban ambayo katika misamiati ya Mfumo wetu wa Kiislamu imepewa jina la siku ya Kupambana na Uistikbari. Suala si kwamba sisi tunataka kuhuisha kumbukumbu ya historia tu au kujivunia kumbukumbu hiyo; kuna mambo yenye maana na madhumuni ya kina kwenye kitovu cha suala hili. Nyinyi mnajua kuwa tarehe 13 Aban imebeba matukio matatu ya kihistoria; kubaidishwa Imam (Khomeini) katika mwaka 43 (1964), kuuawa wanafunzi wadogo katika mwaka 57 (1978) na hatimaye kutekwa Pango la Ujasusi katika mwaka 58 (1979). Katika matukio yote matatu upande mmoja kuna taifa la Iran, hisia za wananchi, dhihirisho la mapambano yaani Imamu Muadhamu na wananchi wa Iran; na upande mwengine wa kadhia kuna dola la Kiistikbari la Marekani. Kwa hivyo kuna mapambano yanayoendelea baina ya Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu, Mapinduzi ya Kiislamu na taifa la Iran lenye itikadi hizi katika upande huu na upande mwengine kuna viongozi wa Marekani na utawala wa Kiistikbari wa Marekani. Mapambano yalianza tokea lini? Nyinyi vijana mnapaswa muyapitie masuala ya nchi kihistoria na kutaamali juu ya suala hili. Hapa kuna nukta mbili kuu za msingi zinazopasa kuchambuliwa: moja ni kwamba mapambano haya yalianzia wapi, yamepitia awamu zipi na yamefikia wapi? Pili, ni nini matokeo ya mapambano haya? Kwa vyovyote vile wakati makundi mawili, pande mbili na watu wawili wanapopambana, mmoja inabidi awe mshindi na mwengine inabidi awe mshindwa. Nini matokeo yake? Katika mapambano haya ya muda mrefu nani ameshinda na nani ameshindwa? Kuhusu suali la kwanza, kwamba mapambano yalianza lini ni kuwa mapambano hayo yalianza kabla ya mwaka 43 (1964); yaani tangu mwaka 32 (1953) wakati wa mapinduzi ya kijeshi ya tarehe 28 Mordad (18 Agosti) yaliyofanywa na Wamarekani nchini Iran na kuiangusha serikali ya Dakta Mosaddegh. Maafisa wa Marekani - ambao majina yao, vyeo vyao na wasifu wao unajulikana kikamilifu, watu wote pia wanawajua maafisa hao, na kuna vitabu pia vilivyoandikwa juu ya suala hili - walikuja rasmi hapa Iran wakiwa na mabegi yaliyojaa dola wakawashawishi wahuni, wakora na majambazi pamoja na baadhi ya wanasiasa waliojirahisisha na kuanzisha mapinduzi ya Mordad 28 mwaka 32 na kuiangusha serikali ya Mosaddegh. Ajabu ambayo inabidi muijiue ni kwamba serikali ya Mosaddegh iliyoangushwa na Wamarekani haikuwa na uhasama wowote na Marekani. Yeye alisimama kukabiliana na Waingereza na alikuwa amejenga imani kwa Wamarekani; alikuwa na matumanini kwamba Wamarekani watamsaidia; alikuwa na uhusiano nao wa kirafiki, aliwaonyesha upendo, huenda ni kwa kiwango kidogo. Pamoja na hayo hivi ndivyo Wamarekani walivyoifanyia serikali hii. Si kwamba serikali iliyokuweko madarakani Iran ilikuwa serikali inayoipinga Marekani; hasha, ilikuwa na urafiki nao; lakini kwa maslahi ya Uistikbari, Wamarekani wakawa kitu kimoja na Waingereza; wakachukua fedha na kuja nazo hapa kisha wakafanya kazi yao. Mhusika mkuu wa mapinduzi ya kijeshi hapa Tehran alikuwa Mmarekani mmoja; jina lake pia linajulikana, wasifu wake pia unajulikana, mimi pia ninazo taarifa kamili na kwenye vitabu pia yameandikwa hayo. Kisha baada ya mapinduzi ya kijeshi kufanikiwa na kumrudisha hapa Shah aliyekuwa ameitoroka nchi, wao wakawa ndio wenye mamlaka ya mambo yote ya nchi; yaani walizitia mkononi hatamu za mamlaka ya nchi.
Takribani miaka kumi tangu ilipotokea kadhia hiyo likajiri tukio la mapambano ya wananchi tarehe 15 Khordad (5 Juni 1963), la Mapinduzi ya Kiislamu, mapambano ya Kiislamu na harakati ya Kiislamu. Yaani watu hao walitoa mbinyo na mashinikizo kwa muda wa miaka kumi, wakapiga watu, wakatia watu jela, wakanyonga watu na wakafanya nchini humu kila walilotaka; lakini hatimaye ukazuka mripuko katika mwezi wa Khordad mwaka 42 (1963) miaka kumi baada ya kadhia hii. Hapa pia hata kama upande mmoja wa kadhia ulikuwa ni utawala dhalimu wa taghuti wa Kipahlavi lakini Wamarekani ndio waliokuwa wamesimama nyuma ya utawala huo; ni wao ndio waliokuwa wakiutia nguvu na kudhibiti masuala yote ya nchi kupitia utawala huo. Mapambano haya yaliendelea hadi mwaka 43 (1964); hapo Wamarekani wakawa hawana budi kujiingiza moja kwa moja katika masuala hayo. Mwaka 43 (1964) wakampeleka Imam Muadhamu uhamishoni. Hapa pia kwa mahesabu ya kidhahiri waliweza kufanya walilotaka, na kwa mawazo yao wakaweza kuwashinda wananchi wa Iran; lakini wananchi wa Iran hawakushindwa.
Baada ya mwaka 43 ambapo utawala uliokuwa na hatamu za kila kitu wa Muhammad Reza Pahlavi, na uliokuwa ukipewa msukumo na Wamarekani, ulifanya malefu ya jinai nchini, nao Wamarekani pia waliendelea kupora, kusomba, kujitanua na kufanya kila waliloweza kulifanya nchini Iran. Makumi ya maelfu ya washauri wao waliokuweko Iran walibeba walivyobeba, walikula walivyokula, wakamiminiwa fedha, wakatoa mafunzo ya utesaji, wakafanya maelfu ya jinai hapa nchini Iran lakini hatimaye mnamo mwaka 56 (1978) na kufuatiwa na mwaka 57(1979) harakati hii adhimu ya wananchi wa Iran kwa uongozi wa Imamu Muadhamu ilianza. Mara hii mapambano haya hayakuwa tena mapambano ya kutoa matumaini yoyote ya ushindi kwa adui. Wananchi walisimama imara, walionyesha muqawama, walijitolea mhanga; wanaume wake, wanawake wake, hata wanafunzi wake pia waliuliwa mabarabarani; lakini hatimaye katika mwaka 1357 (1979) wananchi wa Iran walipata ushindi. Yaani katika mapambano haya ya muda mrefu ya tokea mwaka 32 hadi 57 - katika muda wa miaka ishirini na tano ya mapambano - hatimaye lilikuwa taifa la Iran lililopata ushindi katika medani. Mapinduzi ya Kiislamu yalipata ushindi, utawala uliokuwa tegemezi kwa Marekani ukapinduliwa, utawala wa kidikteta, habithi, mwovu, kibaraka na wa muda mrefu wa kifalme ulitokomezwa na utawala wa wananchi wa Iran, utawala wa Mapinduzi na wa Mfumo wa Kiislamu ukaja madarakani.
Tangu siku ya kwanza Wamarekani walianzisha uadui na uvurugaji wa kila kitu; kituo kikuu cha uvurugaji na makao makuu ya njama zote lilikuwa ni hili Pango la Ujasusi, yaani ubalozi wa Marekani hapa Tehran. Ulikuwa ukifanya mawasiliano, kutoa vitisho, kushawishi, kupanga mipango na kuwavuta na kuwateka watu dhaifu, wakiwa na tamaa kwamba labda wataweza kufanya kitu; lakini tarehe 13 Aban mwaka 58 (4 Novemba 1979) wanachuo, ambao walikuwa ndio tabaka la wenye vipawa zaidi katika mapambano ya wananchi wa Iran waliendesha harakati ya kuliteka Pango la Ujasusi. Kwa mara nyengine tena Marekani ilishindwa katika njama zake dhidi ya taifa la Iran.
Silsili ya kushindwa Marekani iliendelea. Katika muda wote huu wa miaka thelathini na tatu hadi thelathini na nne - yaani kuanzia mwaka 57 (1979) hadi leo hii - Marekani imekuwa daima ikifanya hujuma za uvurugaji ili kufidia kipigo cha kushindwa katika mwaka 57. Kushindwa huko hakukuwa kushindwa kwa Marekani nchini Iran tu tuseme kwamba utawala kibaraka wa Marekani nchini Iran umetoweka na Wamarekani wametimuliwa na mikono yao kukatwa; hilo lilikuwa pigo la kushindwa Marekani katika eneo. Leo watu wanaendelea kukuona kushindwa huko kwa matukio ya Misri, matukio ya Tunisia, matukio ya kaskazini mwa Afrika, matukio ya eneo hili adhimu la Kiarabu na kwa chuki ambazo wananchi wa mataifa wamekuwa nazo dhidi ya Marekani. Wakati ule hakuna mtu yoyote miongoni mwa wananchi aliyeweza kulibaini hilo kwa umakini; lakini wananadharia wa kisiasa wa Marekani walifahamu kuwa kama mapinduzi haya yatadumu, kama yataota mizizi, kama yatazaa matunda na kuchanua majani yake sawasawa na kwa wingi, matukio haya yatatokea tu. Kwa hivyo hadi leo hii wamejaribu kutumia kila kilichoko kwenye uwezo wao dhidi ya Mapinduzi.
Sasa baada ya muda wote huu wa mapambano ni nani aliyeibuka mshindi katika medani hii? Hili ni suala muhimu sana. Tangu mwaka 32 hadi sasa ambapo tunakaribia mwaka 92 (2013) - yaani katika muda wote huu wa karibu miaka sitini - kumekuwepo na mpambano baina ya taifa la Iran katika upande mmoja na serikali ya kiistikbari ya Marekani katika upande mwengine; hili si jambo dogo, hili ni tukio muhimu sana. Hadi leo hii ni nani mshindi katika medani hii? Hili ni jambo linalopasa kuzingatiwa. Wakati tutakapofahamu kwamba yule aliyeibuka mshindi hapa ni irada na uamuzi thabiti wa wananchi yenye kushikamana na imani na kumtegemea Mwenyezi Mungu hili litakuwa somo kwa mataifa yote; huu utakuwa msingi katika mabadiliko yote ya kihsitoria; katika falsafa mpya ya historia, iliyojengeka kwa misingi ya Kiislamu kutokana na kuliangalia tukio hili kwa mtazamo huu, na ambayo imepangwa na kukubaliwa na wote; na ukweli huu ndio uliojiri; yaani katika muda wote huu hadi hii leo taifa la Iran limekuwa ndiye mshindi wa medani hii. Kwa sababu gani? Iangalieni Iran; sababu yake ni kwamba wao walitaka kuyafuta Mapinduzi lakini Mapinduzi yamebaki; na sio tu Mapinduzi yamebaki bali yamezidi kuwa imara siku baada ya siku. Leo kizazi cha vijana wetu ambao hawakuwepo wakati wa Mapinduzi, hawakuwepo katika kipindi cha Vita vya Kulazimishwa na ambao hawakumwona Imam wanasoma masomo yao, wanachapa kazi na wanaishi kwa moyo uleule na kwa azma na uthabiti uleule ambao kijana wa zama za Mapinduzi aliweza kuleta Mapinduzi kutokana na moyo, azma na uthabiti huo. Hizi ni ishara za wazi za kuwa hai Mapinduzi.
Zaidi ya yote haya uangalieni Mfumo wa Kiislamu; Mfumo wa Kiislamu umekuwa thabiti, umekita mizizi umeweza kueneza ujumbe wake, umeyafanya mataifa yaungame na kukiri juu ya adhama uliyonayo, umeweza kuwa na hadhi kubwa mbele ya macho ya wananchi wa mataifa ya Kiislamu na yasiyo ya Kiislamu. Imamu wetu Muadhamu amekuwa na shakhsia adhimu na ya daraja ya juu hata mbele ya macho ya maadui zake. Taifa la Iran sasa linajulikana duniani kama taifa ngangari, taifa la muqawama, taifa la watu waumini na taifa la watu wenye basira (uono wa mbali), na hapa nchini Mfumo wa Kiislamu umeweza kuibadilisha nchi.
Iran mnayoiona nyinyi leo haiwezi kulinganishwa na Iran ya zama za kabla ya Mapinduzi. Iran ya zama za kabla ya Mapinduzi ilikuwa nchi iliyobaki nyuma kimaendeleo, nchi iliyosahaulika, na taifa lisilo na ubunifu. Licha ya kuwa na vipawa vyote hivi, licha ya kuwa na turathi zote hizi za kihistoria, licha ya kuwa na utamaduni wenye utajiri wote huu taifa hili halikuweza kujitokeza na kujionyesha katika uga wowote ule, si uga wa elimu duniani, si uga wa siasa za dunia na si katika uga wa teknolojia duniani. Halikuwa na neno jipya la kuuambia ulimwengu na wala halikuwa na ubunifu kuhusiana na masuala ya eneo na ya ulimwengu kwa ujumla; lilikuwa mfuata mkumbo kikamilifu. Humu nchini ukiondoa maeneo kadhaa tu yaliyokuwa yakishughulikiwa na viongozi na washika hatamu za nchi, maeneo mengine yaliyosalia nchini yalikuwa na hali ya magofu na yasiyo ya ustawi wowote. Leo wakati inaposikika habari ya masaibu yaliyotokea kwenye pembe moja ya nchi watu wote wanaguswa na suala hilo. Wakati ule aghalabu ya maeneo nchini yalikuwa na hali hiyo; hali ya masaibu, watu hawakuwa na maisha, hawakuwa na maji, hawakuwa na umeme, hawakuwa na barabara na wala hawakuwa na suhula za maisha. Wale waliokuwa wakiyajua hayo walikuwa wakiyaangalia kwa masikitiko; kuna wengi mno pia ambao hawakuwa wakijua asilani kinachoendelea; watu wakiishi katika hilaki. Lakini Iran ya leo ina maendeleo haya; ina mambo haya iliyofanya, ina ubunifu huu na kuna vijana hawa wanaojitokeza katika medani ya elimu na ujenzi wa nchi na wenye kujitokeza kwa wingi katika sekta zote. Mambo haya hayakuwepo katika zama zile. Nchi imepiga hatua; na huu ni ushindi. Mapinduzi yamebaki hai, Mfumo unazidi kunawiri na kukita mizizi zaidi siku baada ya siku, na uelewa wa wananchi unazidi kuwa mkubwa zaidi siku hadi siku. Kiwango cha uelewa juu ya masuala ya dunia na uwezo wa kufahamu na kuhakiki mambo mlionao leo hii nyinyi vijana wa sekondari na vijana chipukizi mlioko masomoni hawakuwa nao wasomi - wanafikra wengi wa zama zile; hawakuweza kuelewa kwa kiwango kama hiki. Leo basira, uelewa na uhakiki wa kina wa kisiasa juu ya masuala ya nchi umeenea kwa watu wote. Sisi tumepiga hatua; tumepiga hatua za maendeleo katika upande wa kimaada, tumepiga hatua katika upande wa kimaanawi; ni huu ushughulikiaji wa masuala ya kimaanawi, ni haya mahudhurio katika nyuga za kimaanawi. Mliona jinsi hali ilivyokuwa nchi nzima katika wiki iliyopita wakati wa dua ya Arafa. Ni watu gani waliokuwepo kwenye dua ya Arafa? Wote walikuwa vijana. Katika masiku ya Itikafu na mwezi wa Ramadhani kwa namna moja na katika masiku ya Muharram, maombolezo na siku za furaha kwa namna nyengine. Hali katika uga wa elimu ni ile, uga wa masuala ya dini ni huu na katika uga ule wa siasa na basira ndio kama vile.
Licha ya uadui, nchi imepiga hatua kimaendeleo na kustawi katika pande zote. Nchi ambayo kwa muda wa karne kadhaa mtawalia ilikuwa imezoea kuwa chini ya utawala wa mtu mmoja na utawala wa kiimla imeshuhudia kuchipua kwa moja ya tawala bora kabisa zinazotokana na ridhaa ya wananchi; katika uhudhuriaji wa wananchi wakati wa uchaguzi na katika uhudhuriaji kwenye masuala ya umma na ushiriki kwenye masuala ya kijamii. Haya ndiyo yale mapinduzi ambayo Wamarekani walitaka yasiwepo, walitaka kuyafuta, walitaka yadhoofike na ambayo walikuwa wakijiahidi wao wenyewe kwamba yatatoweka baada ya miezi michache tu. Wamarekani walikuwa wakiwafurahisha hawa vibaraka wao madikteta wa eneo kwamba subirini kidogo tu mapinduzi yatasambaratika na kutoweka! Alhamdulillah Mapinduzi yamezidi kukua siku baada ya siku. Huu ni upande mmoja wa kadhia.
Upande ule mwengine wa kadhia ni viongozi wa Marekani; ni serikali ya kiistikbari ya Marekani. Hakuna mtu yeyote duniani mwenye shaka juu ya suala hili, kwamba katika kipindi hiki cha miaka thelathini kiwango cha nguvu na haiba ya Marekani kimataifa kimeporomoka kwa zaidi ya mara thelathini; watu wote wanaliona hili na wanalijua; wao Wamarekani wenyewe pia wanakiri. Hawa wanasiasa wakongwe na wa zamani wa Marekani wanazifanyia stihzai serikali na viongozi wa sasa kwa kuwaambia kwamba nyinyi mmeitoa Marekani kule na kuifikisha hapa. Ni kweli wanayosema; Marekani imeporomoka. Leo hakuna serikali yoyote duniani inayochukiwa kwa kiwango inavyochukiwa serikali ya Marekani. Kama serikali za eneo letu na serikali nyengine zitakuwa na ujasiri wa kuainisha siku moja kuwa siku ya kujibari na kuonyesha chuki dhidi ya serikali ya Marekani na kuwaambia watu njooni muandamane katika siku hii, yatashuhudiwa maandamano makubwa zaidi katika historia ya dunia! Hii ndio nafasi ya heshima ya Marekani.
Kwa upande wa nafasi ya kimantiki na kifikra ni kwamba kwa vyovyote vile kila serikali na kila taifa linasimama kwa kutegemea fikra na mantiki linayoitangaza taifa hilo. Mataifa huwa hayajipatii itibari duniani kwa kutegemea fedha tu; inapasa kuwepo fikra na mantiki pia. Wamarekani walikuwa wakisema, sisi tunayo misingi - kama wanavyodai wenyewe - tunazo thamani zetu; thamani za Kimarekani. Walikuwa wakipiga kila aina ya makelele kwa ajili ya misingi na thamani hizo. Angalieni leo muone hali ya thamani za Kimarekani imefikia wapi.
Walikuwa wakidai kwamba wanapinga ugaidi; leo katika eneo letu na katika maeneo mengine mengi duniani wanashirikiana na magaidi, wanakwenda kukaa nao pamoja na kupanga nao, wanawapa fedha na silaha ili waende kufanyia kazi zao za ugaidi! Kundi la Munafiqina, ambao wao wenyewe wamekiri kuwa wamewaua kigaidi maelfu ya watu hapa nchini, wanawahami na kuwaunga mkono; kama wanavyosema wenyewe wamewaondoa kwenye orodha yao nyeusi! Wanadai kuwa wanaunga mkono demokrasia; wanasema sisi tunataka kuleta mfumo wa utawala wa wananchi, demokrasia na wananchi kuwa na haki ya kupiga kura; lakini wanawaunga mkono kwa nguvu zao zote watawala madikteta wakubwa zaidi duniani na katika eneo hili! Watu wote wanaliona hili; hili halifichiki tena. Huku ndiko kuporomoka kwa thamani. Serikali inayodai kuunga mkono haki za binadamu, kuunga mkono demokrasia wakati huohuo inatoa himaya kubwa zaidi na uungaji mkono mkubwa zaidi kwa serikali ambazo haziijui hata harufu ya demokrasia!
Wanadai kwamba waunga mkono haki za binadamu - moja ya thamani za Kimarekani ambayo walikuwa wakiipigia kelele kila mara ni hii - walikuwa wameibeba bendera ya haki za binadamu; lakini vitendo vibaya zaidi vilivyo dhidi ya haki za binadamu vinafanyika chini ya himaya ya Marekani, na sio tu hawakabiliani navyo bali wanaviunga mkono pia! Ni miaka sitini na tano sasa haki za taifa la Palestina zinakanyagwa waziwazi na bila kificho na wahuni hawa wasio na haya wa Kizayuni katika Palestina inayokaliwa kwa mabavu; Marekani sio inashindwa hata kukunja uso tu bali inawaunga mkono na kuwasaidia Wazayuni hao!
Wanadai kuwa wanaunga mkono matakwa ya wananchi; lakini kila mahali ambako wananchi wa mataifa wanaanzisha harakati ya kupigania uhuru, ya kupigania mageuzi au harakati ya kimapinduzi dhidi ya maovu, wao wanasimama kukabiliana na wananchi!
Wanajidai kuwa wao ndio taifa na nchi tajiri zaidi duniani - bila ya shaka Marekani ni nchi tajiri; rasilimali za maliasili, za chini ya ardhi na za juu ya ardhi, ni nchi yenye kila kitu - lakini viongozi wao wameifikisha Marekani mahali ambapo leo hii ndio nchi yenye madeni makubwa zaidi duniani; madeni ya Marekani yamefikia kiwango sawa na Jumla ya Pato lake la Taifa (GNP)! Hakuna fedheha kubwa zaidi na mbaya zaidi kwa nchi kuliko hii.
Wanajidai kuwa watetezi wa uhuru; lakini hakuna nchi duniani yenye jela nyingi zaidi kulinganisha na idadi ya watu wake kama Marekani! Wana idadi ya karibu watu milioni mia tatu; lakini zikilinganishwa jela zao na idadi hii ya watu, idadi ya jela hizo ni nyingi zaidi kuliko nchi nyengine zote duniani kulinganisha na idadi ya watu wa nchi hizo. Sambamba na suala hili kuna mahakama za kimaonyesho na za kizandiki pia. Tab'an katika filamu za sinema na filamu za televisheni huonyesha taswira za namna tofauti; mahakama zenye kufuata ada na taratibu; lakini hayo ni mambo ya Hollywood tu; hayo ni mambo ya mchezo wa vita vya nyota na mchezo wa wasanii; lakini ukweli ni kinyume na hayo.
Wanadai kwamba taifa lao ni taifa lenye kuheshimika. Leo serikali za Marekani zimewadhalilisha wananchi wao, zimewapotosha; kama inavyoeleza Qur'ani kuhusu Firauni kwamba و اضلّ فرعون قومه و ما هدى Na Firauni aliwapoteza watu wake wala hakuwaongoa.(Suratu Taha 20:79).Wamewapoteza watu wao; hawaruhusu waelewe hakika ya mambo. Hii harakati ya asilimia 99 na harakati dhidi ya Wall Street iliyoanzishwa nchini Marekani, kwa kuzingatia kwamba wananchi wa Marekani hawana habari ya hakika ya mambo mengi, lau kama watapata habari, huenda harakati hii ikapamba moto mara kumi zaidi. Wamewatia watu wao kwenye pingu za Wazayuni. Hii si idhilali kwa nchi, kwamba wagombea wake wa urais wanazungumza katika mijadala na kampeni za uchaguzi kwa namna watakayohakikisha wanazifurahisha nyoyo za Wazayuni; ili kuthibitisha mbele yao kuwa wao ni watumwa wao na ni watiifu kwao?! Hivi mnavyoona, kwamba katika midahalo ya uchaguzi wanayofanya wagombea wawili wa sasa wa Marekani, kila mmoja anajaribu kuonyesha utiifu wake kwa jamii ya Mayahudi wa Palestina na jamii ya mabepari wa Kizayuni wa Israel, wanafanya hivi kwa sababu wamebanwa na pingu za Wazayuni hao. Viongozi wanaoongoza nchi kubwa kama hii, yenye maendeleo kama haya ya kielimu wamelitia taifa lao kwenye pingu za kikundi za Wazayuni wachache!
Haya yote mnayoyaona ni hali ya kurudi nyuma. Nini matokeo ya kurudi nyuma huku? Matokeo ya kurudi nyuma huku ni kwamba sasa hawana heshima duniani; duara la satua yao duniani linazidi kuwa dogo siku baada ya siku; katika vita vingi wanashindwa. Wamarekani wameshindwa kufikia lengo lao na wameshindwa nchini Iraq; huko Afghanistan pia ni hivyo hivyo; katika vita dhidi ya muqawama nchini Lebanon - ambavyo vilianzishwa na Wazayuni wenye mfungamano na wao - ni hivyo hivyo pia; katika kukabiliana na mataifa ya kaskazini mwa Afrika ni hivyo hivyo pia; wameshindwa kila mahali.
Tab'an kuna mengi sana ya kusema kuhusiana na masuala haya; kama mtu atataka kuzungumzia pande zote za kadhia hii huenda yakachukua masaa kadhaa; lakini inawezekana kufanya majumuisho kwa sentensi chache kwa kusema: nguvu za Marekani, serikali ya Marekani na uistikbari wa Marekani ambao ulikuwa umesimama kukabiliana na taifa la Iran na ambao ulikuwa umeanzisha mpambano huu wa muda mrefu dhidi ya taifa la Iran tangu mwaka 32 - ambapo hivi sasa tuko katika mwaka 91 (2012) - aliyeshindwa katika mpambano huu ni hii serikali ya kiistikbari, yenye kutakabari, yenye kujikweza ya Marekani; na yule aliyeshinda ni taifa lenye kuheshimika, lenye nguvu na lenye azma thabiti la Iran.
Ni natija gani inapatikana hapa? Hatutaki kutia chumvi, wala hatutaki kutoa kauli za hamasa; tunataka tujifunze, tunataka tupate somo; tunataka kwa baraka ya uongofu wa Kiislamu tutambue njia yetu ya kufuata kutokana na hakika ya mambo na ukweli halisi wa matukio ya ulimwengu. Somo lililopo hapa ni kwamba taifa lolote lile wakati linaposimama imara na azma thabiti na likajitutumua lenyewe (bila ya utegemezi), likatawakali na kumtegemea Mwenyezi Mungu Mtukufu na likaamua bila ya ajizi kujitolea heshima yake, roho na mali zake katika medani ya mapambano, hata kama taifa hilo halitokuwa na kiwango cha fedha kama alichonacho adui yake, halitokuwa na kiwango cha silaha kama za adui yake, kiwango cha elimu kama alichonacho adui yake, hata kama idadi ya watu wake itakuwa ndogo kulinganisha na adui yake na hata kama kiwango cha vyombo vyake vya habari kitakuwa chini ya asilimia moja kulinganisha na adui yake, taifa hilo litaibuka mshindi katika mpambano mkubwa kabisa na mgumu zaidi dhidi ya adui yake.
Changamoto tulizonazo za kukabiliana na uistikbari wa dunia hazijaisha - na wala hazitoisha, lakini haidhuru - changamoto na kupimana misuli kwa taifa ni mithili ya mazoezi ya viungo ambayo hulifanya lizidi kuwa na nguvu siku baada ya siku; sisi tunakuwa imara na wenye nguvu kutokana na changamoto hizi; hata hivyo inapasa tuwe macho kwa kuelewa kwamba changamoto zingaliko, kwa kuelewa ni nini adui anataka kufanya, kwa kuelewa njia ya kukabiliana na adui ni ipi. Kama hatutoyafahamu hayo, kama tutashindwa kuwa na ufahamu, kama tutashughulishwa na kupenda raha na kama tutaghafilika na kushindwa kuelewa ukweli na mambo yaliyo wadhiha kabisa, hapo tutashindwa; Mwenyezi Mungu hana nasaba na mtu. Kama mtasimama imara - kama mlivyosimama hadi sasa - na mkawa mumemtegemea Mwenyezi Mungu na dini yake, bila ya shaka yoyote mtashinda tu; lakini kama hatutosimama imara, kama hatutozingatia masharti yanayotakiwa kwa ajili ya mapambano yenye adhama kama hii, bila ya shaka Mwenyezi Mungu Mtukufu hayajali mataifa ya watu goigoi na watu wanaoshughulishwa na masuala duni na yasiyo na thamani. Rehma za Mwenyezi Mungu na msaada wa Mwenyezi Mungu unawafikia watu wa mataifa yanayosimama imara, yenye ufahamu, yenye basira (uono wa mbali), yenye utambuzi na yenye harakati.
Moja ya mambo ya msingi kwetu ni kuendeleza irada na azma hii inayofungamana na kumtii Mola wa ulimwengu; hili ndilo sharti la kwanza. Sharti jengine ni umoja wetu, na jengine ni juhudi na jitihada zetu. Mmoja anapaswa kufanya juhudi katika masomo, mwengine anapaswa kufanya juhudi katika utafiti, mwengine anapaswa kufanya juhudi katika kazi za ujenzi wa nchi, mwengine anapaswa kufanya juhudi katika katika kazi za uendeshaji, mwengine anapaswa kufanya juhudi katika biashara, mwengine anapaswa kufanya juhudi za mtawalia na zenye nidhamu na mpangilio ili kutafuta njia kwa ajili ya maendeleo ya nchi; kila mtu ana aina fulani ya juhudi za kufanya; watu wote wanapaswa kufanya juhudi. Pale watu wote watakapofanya juhudi, watu wote watakapofanya kazi, ustawi utafikiwa kwa kasi, maendeleo yatakuwa mengi zaidi na uhakika wa kupata ushindi utakuwa mkubwa zaidi.
Moja ya njia za kufuatwa ni kujenga umoja. Hitilafu zina madhara. Hitilafu baina ya viongozi zina madhara; na baya zaidi ya hilo ni kuwaingiza wananchi kwenye hitilafu hizo. Ninatoa onyo juu ya suala hilo kwa viongozi na kwa wakuu waheshimiwa. Mimi nimekuwa nikitoa himaya na uungaji mkono kwa wakuu wa mihimili ya dola na nitaendelea kufanya hivyo - wao wana majukumu na inapasa wasaidiwe - lakini ninawaonya kwamba wawe na hadhari. Si kwamba huu uandikaji barua una umuhimu mkubwa sana; hapana, na waandike barua mia moja; lakini wafanye kazi zao wanazopaswa kufanya, wasiwaingize wananchi kwenye hitilafu hizo, wasifanye vitu vidogo vidogo ambavyo huwa sababu ya kuzushwa zahama na makelele, kutumiwa kipropaganda na adui na kuwa chachu ya kufanyiwa propaganda na redio na televisheni za kigeni; na waandike barua mia moja, barua tu haina faida. Muhimu ni sisi sote kujua kwamba tuna majukumu, sisi sote kujua kwamba tuko katika hali nyeti.
Leo adui ameudhika na kukasirika kwa sababu ya matukio ya kaskazini mwa Afrika, kwa sababu ya maendeleo ya kielimu ya Iran - tab'an wao wanasema ni maendeleo ya nyuklia lakini ni waongo; tatizo lao kuu ni maendeleo yenu ya kielimu - ni kwa sababu ya taathira iliyosababishwa na taifa la Iran kwa mataifa mengine, kwa sababu ya Mwamko huu wa Kiislamu uliojitokeza. Adui anahisi ameshindwa, anahisi amegonga mwamba; kwa hivyo amekasirika. Tab'an pozi wanazoonyesha viongozi wa Marekani ni pozi za mtu aliyeshinda; kwa kujidai kwamba sisi tumefanya hili na tushafanya lile; lakini wao wenyewe wanajua, wengine pia wanajua, duru za kisiasa na duru za magazeti duniani pia zinajua ukweli wa kadhia ni upi; wanajua kwamba serikali ya Marekani imeshindwa katika mapigano haya, katika mpambano huu mkubwa na katika matukio haya; kwa sababu hiyo viongozi wao wamekasirika.
Wao kila mara wanashughulika kutafuta kitu cha kufanya. Moja ya mambo muhimu kwao wanayotaka kufanya ni kutumia njia za maudhi za kuchokoa mitihili ya mchwa ili kuzusha hitilafu baina yetu; hii ni moja ya kazi zao kubwa walizozoea, ni kazi ambayo walikuwa wakiifanya tokea zamani.Tab'an Waingereza mahabithi ndio wataalamu wakuu na waliobobea katika kazi hii; wao ni wataalamu zaidi kuliko watu wote katika suala la kuchochea hitilafu; Wamarekani ni wanafunzi wao wanajifunza kwao wao! Kuchochea hitilafu kwa njia ya kujipenyeza na kuchokoa mithili ya panya wezi, mithili ya mchwa na kujiingiza na kujpenyeza; hizo ni miongoni mwa kazi zao maarufu. Hivyo tunapaswa tuwe macho. Inapasa hitilafu zihafifishwe.
Bila ya shaka tofauti za mawazo ziko nyingi mno; na hakuna ubaya wowote juu ya hilo - watu wawili ambao ni viongozi, marafiki wanaweza kutofautiana kimawazo; hili limekuwepo siku zote - lakini tofauti za mawazo zisipelekee kuzuka hitilafu katika utendaji, hitilafu katika miamala mbalimbali, hitilafu za hadharani, hitilafu za kukabana koo na kusakamana mbele ya macho ya wananchi; kwa sababu hitilafu hizo hazina umuhimu wa kiasi hicho. Kuna wakati masuala yaliyopo ni yenye umuhimu, hapo ni sawa wananchi wanapaswa kuelewa; lakini hitilafu hizi anazoshuhudia mtu zinazuka baina ya hawa waheshimiwa si za mambo yenye umuhimu kiasi hicho wa kuzikuza kwa kutoa madai ya aina mbalimbali, kuzitangaza mbele ya wananchi na kuzipa umuhimu; hakuna umuhimu wa kufanya hivyo. Haifai kutangaza hitilafu hadharani; haifai kuwaingiza wananchi kwenye hitilafu; haifai kuzichochea hisia za wananchi kwenye masuala yanayozusha hitilafu. Kuanzia leo hadi siku ya uchaguzi, mtu yeyote atakayezitumia hisia za wananchi kwa ajili ya kuzusha hitilafu, bila ya shaka atakuwa ameifanyia nchi usaliti.
Bahati nzuri viongozi nchini ni watu wanaotaabika kuchapa kazi na wenye uchungu; wanataka kufanya kazi kwa ajili ya nchi. Bila ya shaka upo uwezekano wa kutokea hali za kujisahau, lakini inshallah nia zilizopo ni kwa ajili ya kufanya kazi. Ni matumaini yangu kuwa inshallah Mwenyezi Mungu Mtukufu atawapa wao wote jaza kutokana na nia hizi njema, na bila ya shaka inshallah atalipa taufiki taifa la Iran katika medani zote.
Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

 
< Nyuma   Mbele >

^