Skip to content

Habari

Habari
Hifadhi

Risala na Barua

Matini
Hifadhi

Kumbukumbu na Simulizi

Kabla ya Mapinduzi
Baada ya Mapinduzi

Sauti na Taswira

Picha
Sauti
Video
Hotuba ya Kiongozi Muadhamu Mbele ya Watu Wenye Vipawa na Viongozi wa Mkoa wa Khorasan Kaskazini Chapa
16/10/2012

Ifuatayo ni hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu mbele ya hadhara ya Wenye Vipawa na Viongozi wa Mkoa wa Khorasan Kaskazini katika uwanja wa Sala wa Imam Khomeini aliyoitoa tarehe 16/10/2012.

Kwa jina la Allah Mwingi wa rehema Mwenye kurehemu

Na hamdu na sifa zote njema ni za Mwenyezi Mungu Mola wa ulimwengu. Na rehma na amani zimshukie Mtume wetu na kipenzi cha nyoyo zetu Abul Qasim al Mustafa Muhammad, na Aali zake wema, watoharifu na wateule.
Tunamshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa kuwa katika muda huu wa siku kadhaa ametupa taufiki ya kufanya mikutano na wananchi wapenzi wa matabaka mbalimbali wa mkoa huu wenye wingi wa kheri na baraka katika anga ya furaha, ikhlasi na upendo. Kikao hiki cha leo ni cha majimui ya watendaji watoa huduma kwa wananchi katika mkoa huu azizi na vilevile kinajumuisha wawakilishi wa matabaka mbalimbali yenye harakati na yaliyo amilifu mkoani humu. Kwa hivyo hadhara hii ni hadhara yenye thamani kubwa.
Maelezo yaliyotolewa hapa na ndugu zetu, kila moja kwa upande wake yalikuwa mazuri na yenye kupasa kuzingatiwa. Ninachotaka kusema mimi ni kubainisha nukta mbili tatu muhimu; na kama sisi sote tutazizingatia nukta hizi huenda inshallah zitakuwa na kheri kwa ajili ya mustakabali wa mkoa huu.
Nukta ya kwanza ni kwamba suala la kuwatumikia wananchi wote, lenyewe ni neema ya Mwenyezi Mungu na ni hidaya na atiya; uwe utumishi huo katika majimui rasmi - kama haya majukumu mbalimbali waliyonayo jamaa, ndugu na mamudiri katika mkoa - au wale wanaohudumu katika majimui zisizo rasmi; kama kutoa huduma kwa ajili ya dini ya watu, kwa ajili ya utamaduni wa watu, kwa ajili ya maendeleo ya kielimu ya watu, kutoa huduma za ugawaji na usambazaji sahihi wa bidhaa za vyakula kwa watu pamoja na kuikidhi mahitaji yao mbalimbali kwa namna yoyote ile iwayo. Kwa hivyo kupata taufiki ya kuwatumikia wananchi, yenyewe ni neema; na inapasa kushukuru kwa kupata neema hii.
Ninayasema haya kwa udhati wa moyoni na kwa imani kamili kwamba kuwa mtumishi wa utoaji huduma kwa wananchi kwa kweli ni jambo la kujivunia; na si jambo ninalolielezea kama nara na sha'ar tu. Shakhsia wetu wakubwa wa maarifa ya dini walikuwa kila mara wakiwausia wanafunzi wao na wale waliokulia kwenye malezi yao kwamba sambamba na kufanya ibada, kuleta dhikri, kuonyesha khushuu pamoja na kufanya tawasuli, wafanye kazi pia ya kuwahudumia watu; wakati mwengine walikuwa wakifadhilisha hili kuliko ufanyaji ibada wa mtu binafsi ambao unamkurubisha mtu kwa Mwenyezi Mungu. Wewe unapofanya jambo zuri lenye manufaa kwa mtu mmoja unakuwa umetenda jambo jema; hili linakukurubisha wewe kwa Mwenyezi Mungu; hili linakupatia wewe thawabu na malipo ya akhera kwa Mwenyezi Mungu; seuze unapofanya jambo hilo kwa ajili ya majimui ya watu kadhaa, kwa ajili ya kundi la watu , kwa ajili ya watu wa mkoa, watu wa mji na watu wa tarafa. Kwa hivyo la msingi katika kadhia hii ni kwamba kama sisi tutapata taufiki ya kutoa huduma ya utumishi tushukuru kwa jambo hilo; tumshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu; tujue kuwa hii ni neema kutoka kwa Mwenyezi Mungu.
Natija ya kuielewa neema hii ni kwamba tusimfanyie masimango mtu yeyote kwa sababu ya utumishi hii tunaotoa; hili ndilo lenye umuhimu wa kwanza. Mwenyezi Mungu Mtukufu ametupa taufiki; taufiki hii ni rehma yake Mola; inalazimu kuishukuru. Kwa hivyo kama tutakuwa tumeweza kutoa huduma ya utumishi inapasa hilo lifanyike bila masimbulizi. Hii ni nukta moja.
Nukta nyengine ni kwamba katika kutoa huduma za utumishi inapasa kusiwepo ubaguzi wa aina yoyote. Maana ya kuwa na wadhifa katika sehemu yoyote ile ni kutoa huduma za kuwatumikia wananchi wote. Kuwa huyu ni rafiki yetu, huyu ni mtu baki kwetu, huyu ni adui yetu, huyu muelekeo wake wa kisiasa ni huu, muelekeo wake wa kidini ni huu, haya ni mambo yasiyo na taathira yoyote. Huduma zinapasa ni kwa ajili ya umma na kwa ajili ya wote; kwa njia hiyo ndipo zitakapokuwa na athari katika utendaji wa watu wanaofanya kazi ya utumishi wa umma katika majimui kubwa zaidi; ikiwa ni katika mkoa au katika mji. Maeneo mbalimbali ya miji yana watu wa aina tofauti; kwa hivyo mtazamo kuhusiana na wote hao unapasa uwe wa namna moja. Huduma ni kwa ajili ya watu wote, zinawahusu watu wote, na sisi tunatakiwa tuwe watunzaji amana hii; kile kilichoko kwenye mamlaka yetu tukitoe kwa ajili ya watu wote. Nukta nyengine ni suala la kufanya bidii kubwa katika ufikishaji huduma. Mkoa huu, kama walivyoeleza jamaa - na hilo ndilo nililobaini mimi pia katika ripoti - ni miongoni mwa mikoa iliyoko kwenye nafasi ya chini kwa upande wa maendeleo ya kimaada. Kwa kiwango fulani hali hii imetokana na kuwa huu ni mkoa mchanga ambao umeanzishwa hivi karibuni; huenda zikawepo sababu nyengine pia. Kwa hivyo viongozi wa mkoa huu waelekeze hima na juhudi zao katika kuhakikisha wanapandisha juu nafasi ya mkoa kwa upande wa maendeleo na katika viwango muhimu vya kimaisha ndani ya kipindi cha muda maalumu; mathalani kwa kuipandisha kuwa katika orodha ya mikoa kumi inayoongoza nchini. Ikiwa tutakuwa na bidii kama hiyo - ambayo ni bidii maradufu - bila ya shaka bidii hiyo itahitajia uchapaji kazi maradufu. Maana ya uchapaji kazi maradufu si ufanyaji kazi nyingi tu; bali ina maana ya ubora wa kazi kuliko kuzingatia zaidi wingi na ukubwa wa kazi; yaani kazi inayofanywa kwa umakini, kazi inayofanywa kwa utaalamu, kazi inayofanywa kwa mashauriano, kazi inayofanywa kwa uendelevu na ufuatiliaji; kiasi kwamba hata kama viongozi watabadilishwa kazi huwa haisimami. Hii ni habari njema iliyoelezwa kwamba hati ya mpango wa maendeleo wa mkoa imeshatayarishwa; hili ni jambo zuri sana. Kama hati imeshatayarishwa kubadilishwa viongozi na mamudiri hakutokuwa na taathira kubwa; kazi itaweza kuendelea. Muhimu ni kwamba ramani ya njia iwe imeshaeleweka.
Niliposema kwamba mkoa huu ufikie kiwango cha mikoa kumi ya kwanza nchini, je hili linatekelezeka? Kutokana na yale anayoyaona mtu kuhusiana na uwezo ulionao mkoa huu, naam ni jambo linalotekelezeka kikamilifu. Kuna uwezo na vipawa vizuri sana katika mkoa huu; moja ya vipawa na uwezo muhimu ni uwezo wa rasilimaliwatu; na hili nimelihisi na kulishuhudia kwa macho nilipokutana na vijana, watu wa vyuo vikuu, wanafunzi, walimu na wahadhiri katika mikutano mbalimbali, na pia nimeliona katika ripoti zetu. Alhamdulillah kuna rasilimaliwatu yenye thamani katika mkoa huu; huu ndio uwezo mkuu na wa msingi; mbali na uwezo huo ni uwezo wa maliasili na masuala yanayohusiana na ardhi, mazingira na nafasi ya kijiografia na masuala mengine ambayo yana taathira kwa maendeleo ya mkoa. Kwa hivyo uwezo upo; kwa kweli ni jambo linalowezekana kuufanya mkoa huu upige hatua mbele na kuwa na nafasi ya juu na kustawisha maisha ya watu wake.
Wananchi hawa kwa kweli ni watu wanaostahiki kutumikiwa; kutokana na imani hizi, usafi huu wa nyoyo, uhudhuriaji huu mkubwa katika nyuga mbalimbali na kutokana na kujitokeza kwao katika eneo la mpakani, eneo nyeti la kijiografia. Kwa kweli inastahiki zitolewe huduma kubwa kwa watu azizi wa eneo hili na kuupatia mkoa maendeleo. Jamaa waliozungumza hapa wameweka mkazo zaidi juu ya nukta mbili tatu; mimi pia nilikuwa nimezifikiria na kuziandika nukta hizohizo na ndizo nitakazotilia mkazo. Huu ufafanuzi aliotoa janabi Mkuu wa Mkoa ulikuwa ufafanuzi uliokamilika; ni majimui kamili ya shughuli zilizopangwa kufanywa. Kwa kweli ikiwa kazi hii kubwa iliyopangwa itaweza kutekelezwa katika muda na wakati maalumu ulioainishwa bila ya shaka yoyote sura ya mkoa na hali ya ndani kabisa ya mkoa itabadilika - hapana shaka yoyote juu ya hili - muhimu ni kuwepo ufuatiliaji ili kazi iweze kutekelezwa.
Nukta nyengine muhimu ni kwamba shughuli hizi ziainishiwe vipaumbele. Tuzingatie uwezo wa nchi, suhula za kiitibari na za bajeti na uwezo na suhula mbalimbali ambazo serikali inaweza kutoa na kuzipatia sekta mbalimbali. Tuzingatie pia suala la miradi mbalimbali inayotoa tija ya haraka katika uzalishaji. Baadhi ya miradi ni miradi yenye faida na ulazima lakini utekelezaji wake ni mgumu; na baadhi ya miradi utekelezaji wake ni mwepesi na wa karibu. Yote haya yanachangia katika kuainisha vipaumbele.
Tuvizingatie pia vipaumbele na kufanya kazi kwa msingi wa vipaumbele hivyo. Kwa maoni yangu moja ya vipaumbele ni suala la kilimo ambalo limekaririwa na kuzungumziwa kwa sura hiyo katika maelezo waliyotoa jamaa hapa. Hapa kuna vipawa vya kilimo na pia kuna akili na bongo zinazohitajika kwa maendeleo ya kilimo - umeashiriwa hapa utafiti wa kilimo; katika moja ya vikao vingine pia kuna maelezo yaliyotolewa kuhusu harakati mpya iliyoanzishwa katika umwagiliaji maji ambalo ni suala lenye faida katika kilimo - kwa hivyo kuna suhula za utayarifu wa kiwango cha juu; ardhi ipo, maji yapo, suhula za rasilimaliwatu zipo na hali ya hewa nzuri ipo; na sehemu kubwa ya pato la watu katika kipindi chote cha mwaka inatokana na kilimo na ufugaji.
Bila ya shaka ukame wa mara kwa mara, wa mtawaliwa na wa kuendelea umesababisha madhara; hakuna shaka yoyote juu ya hilo. Kwa mujibu wa ripoti nilizopewa na baadhi ya jamaa moja ya mambo yaliyosababisha madhara kwa kilimo cha mkoa na maendeleo ya kilimo na kusababisha matatizo ni kuwa ndogo rasilimali za mapato ya matumizi ya ardhi; yaani ardhi zimegaiwa; ardhi zimekuwa ndogondogo. Moja ya mipango muhimu ambayo ilizingatiwa tangu katika serikali zilizopita, na mimi nilikuwa nikiitilia mkazo ni kuweza kuziunganisha pamoja rasilimali hizi za ardhi ili hatua hiyo iweze kusaidia kilimo cha sura ya kitaalamu; kilimo cha kisasa na kilimo cha utumiaji zana za kisasa; hili ni mojawapo ya mambo muhimu. Haya ndiyo madhara iliyopata sekta ya kilimo. Kumekuwepo pia sababu nyengine mbalimbali.
Kilimo kinapasa kipewe kipaumbele cha kwanza kiumuhimu; na hii maana yake si kwamba tuisahau sekta ya viwanda ya mkoa; hapana, mkoa una sekta mbalimbali za viwanda ambazo zikishughulikiwa, zikizingatiwa na kupewa umuhimu zinaweza kutoa ajira, zinaweza kutoa faida chungu nzima kwa mkoa; lakini katika daraja ya kwanza ni suala la kilimo; yaani kama tutaweza kufufua kilimo kulingana na hali kiliyonayo suala la ajira litatatuka na pia matatizo mengine mbalimbali yanayosababishwa na ukosefu wa ajira - hii hali ya kujikunyata pembeni, uraibu wa mihadarati na mfano wake - yatatoweka au mizizi yake itadhoofika. Kuna nukta kuu tatu kwa ajili ya suala la kilimo: moja ni kukifanya kilimo kuwa cha kitaalamu; tukifanye kilimo na ukulima wa konde uwe wa kitaalamu na wa kisasa. Jengine ni suala la ufundi mbadala na wa suhula za kukamilisha sekta ya kilimo pamoja na maghala ya kuhifadhia mazao na vitu kama hivyo. Ikiwa ukulima wa konde hapa, mbali na utaratibu wake wa sasa, utatumia pia utaalamu mbadala unaoweza kupatikana, hali yake itabadilika kikamilifu; maghala ya kuhifadhia mazao pia ni hivyo hivyo.
Tab'an kesho inshallah viongozi husika wa serikali watakuwa na kikao na mimi, na bila ya shaka wao wenyewe wanayaelewa haya - katika aghalabu ya hivi vikao vinavyofanyika tunaona maoni na mapendekezo yanayotolewa na viongozi wa serikali - na sisi pia inshallah tutayatilia mkazo; masuala haya yanapasa yazungumziwe katika kikao hicho. Mimi ninayaeleza haya ili iweze kubainika wazi kwamba upeo wa maendeleo ya mkoa ni upeo wenye kung'ara. Kwa hivyo suala mojawapo ni hili la tasnia mbadala za viwanda na jengine ni kubuni muundo wa ugavi na masoko - ambalo lilizungumziwa pia katika maelezo ya mmoja wa majanabi hapa - ubora wa masoko ya mazao na miamala ya bidhaa hizo, biashara zake za ndani, kisha ni suala la usafirishaji na bishara za nje ambayo yote hayo yanapasa yawekewe nidhamu na ratiba ya kimantiki na yenye tadbiri; haya yatasaidia maendeleo ya mkoa. Kwa hivyo moja ya vipaumbele vya mkoa ni suala la kilimo likiwa na sura na hali hizi mbalimbali.
Suala jengine ambalo niliona katika ripoti nilizoletewa kabla ya safari na ambalo nililitalii kwa umakini na likanipa mguso na kisha baadaye nikaona limezungumzwa tena katika maelezo yaliyotolewa na viongozi, jamaa na wenye vipawa wa mkoa ni suala la utalii katika mkoa huu. Vivutio vya utalii katika mkoa huu ni vingi; kuna vivutio vya hali ya maumbile na pia vivutio vya kihistoria; yaani eneo zuri na maumbile mazuri ya kuvutia ya hapa na pia vitu vya kihistoria vilivyopo. Kwa mujibu wa ripoti nilizopewa - mimi kwa kawaida huwa sipati taufiki ya kuvitembelea vitu hivi - ngome iliyoko karibu na Asfarayin inayofanana na jengo maarufu la Arge Bam ambalo watu walikuwa wakija kutoka nje kwenda kuliangalia. Kwa nini hakuna mtu yoyote anayekuja hapa? Kwa nini hapa hapajatangazwa? Kwa nini watu hawapajui? Ilhali hapa ni rahisi zaidi kufikika. Kupitia njia hii hapa, nyinyi kila mwaka mnapokea mamilioni ya wasafiri wanaopita njia hapa - takwimu zinatafautiana; baadhi ya watu wanasema ni milioni ishirini, baadhi ya wengine wanasema ni milioni kumi na tano - ambao ni wafanya ziara wa Mashhad wanaopita hapa. Ikiwa suhula zinazohitajika zitaandaliwa, hata kama si wote hao, bali hata baadhi yao ikiwa watasimama siku moja katika mkoa huu, hilo litakuwa na athari kubwa iliyoje kwa hali ya mkoa. Si kwamba nyinyi mnataka mumvute msafiri na mtalii kutoka katikati ya mji au kutoka pembe hii na ile ya nchi na kumleta mahala ambapo ni mbali kufikika. Hapa si mahala mbali kufikika; hapa ni mahala inapopita misafara ya wafanya ziara; watu wamo kwenye harakati za kwenda na kurudi. Siku moja, kutwa na kucha moja, na isiwe wasafiri wote hawa, bali baadhi yao tu na wabaki katika mji huu na kwenda kutembelea maeneo ya mandhari za maumbile za hapa na kwenda kutembelea sehemu hizi za kihistoria. Mtaona mabadiliko makubwa yatakayotokea hapa katika kazi na ajira na hali ya maisha. Kwa hivyo hiki pia ni kipaumbele. Suala la utafiti pia lililoashiriwa hapa ni suala sahihi kabisa; kwa kweli nalo pia ni kipaumbele. Tija ya kazi ya uchunguzi na utafiti haionekani waziwazi; lakini ukweli ni kwamba tija na matunda yake ni sawa kabisa na kile kilichoashiriwa na Qur'ani Tukufu:
انبتت سبع سنابل فى كلّ سنبلة مئة حبّة
iliyochipuza mashuke saba. Katika kila shuke zimo punje mia. Ni punje moja ambayo wakati unapoipanda inakupa badala yake punje mia saba. Hivi ndivyo ilivyo kazi ya utafiti. Wakati wewe unapopanda mbegu nzima, au unapofanya utafiti wa mbinu nzuri ya kilimo, au unapofanya utafiti kuhusiana na mada fulani yenye taathira katika suala la ufundi, kilimo, utoaji huduma na mengineyo hii itapelekea kupatikana ghafla faida kubwa na ya pande zote kwa nchi baada ya kustahamili na kuvumilia kwa muda fulani. Kwa hakika hili pia ni miongoni mwa vipaumbele. Kwa hivyo kazi za kufanywa ni nyingi, mazingira ya ufanyaji kazi yako mengi na wananchi hawa pia ni watu wazuri.
Leo nchi inahitajia kazi na juhudi; ndugu zanguni wapenzi! viongozi wa sehemu mbalimbali! wateule wa matabaka mbalimbali! mnapaswa kulifikisha hili kwa maneno na pia kwa vitendo kwa majimui za watu wote wanaokusikilizeni au wanaofanya kazi chini ya uongozi wenu: Nchi inahitajia uchapaji kazi. Tunapaswa kufanya kazi, tunapaswa kufanya kazi kwa bidii; kazi inayofanywa kwa ratiba maalumu, kazi yenye mpangilio na nidhamu na kazi nzuri.
Kila pale tunapoonyesha kuwa tuko dhaifu maadui zetu waliotukamia hupata moyo; kama ambavyo kila pale tunapoona harakati yenye taathira inafanyika nchini kwa lengo la kuwapa motisha na kuwashajiisha wananchi, na kuongeza basira na uono wa mbali wa wananchi, mara tunaona adui anajaribu kufanya kila awezalo kuzima hatua hiyo. Watu wanaofuatilia kwa makini masuala ya kimataifa, masuala ya kisiasa, masuala ya habari na matukio mablimbali ya kimataifa wanalielewa vizuri suala hili. Wakati wowote inapofanyika kazi muhimu nchini - mathalani chukulia mfano maandamano makubwa, uchaguzi mkubwa, mafanikio makubwa ya kielimu na kiviwanda, hatua muhimu na yenye taathira ndani ya serikali - wao huchukua hatua haraka kujaribu kuififiliza kazi hiyo; ni kwa kuzusha jambo fulani. Vile vile kama kuna wakati sisi tutaonyesha udhaifu, tutaonyesha kuchoka, hii huwa ndio radiamali inayoonyeshwa haraka duniani: wapinzani wa Mfumo wa Kiislamu na wapinzani wa Uislamu hupata moyo, hujawa na furaha; huwa kama kwamba wamepata nguvu mpya wanataka kushambulia. Inapasa kuyazingatia mambo haya. Haya yanatufunza sisi kwamba kwanza tusiache asilani juhudi na kazi; pili tujitahidi kueneza na kuimarisha moyo wa kazi, moyo wa jitihada na moyo wa matumaini ndani ya nyoyo za watu wote wanaotusikiliza katika sehemu zetu za kazi; huu ni wajibu wetu. Kauli yoyote ile inayojenga hisia za kukatisha tamaa, kuchosha, kutia simanzi na kuleta hitilafu, bila ya shaka ina madhara kwa maslaha ya nchi; ina madhara kwa maendeleo ya nchi, ina madhara kwa izza ya taifa.
Sisi tuna kila kitu kwa ajili ya kukabiliana na maadui. Uwezo wetu ni wa juu; hatusemi hili kwa kujidai - hatutaki kukuza mambo na kutia chumvi - bali huo ndio ukweli. Ushahidi muhimu zaidi wa kuthibitisha ukweli huu ni kwamba kwa miaka thelathini na tatu kila mara wanatupaka matope, wanatuandama na wanafanya hujuma; kama tungekuwa dhaifu bila ya shaka hadi wakati huu mti huu ungekuwa umeshakauka, hadi sasa ungekuwa umeshaanguka; lakini kwa nini umekua mara kumi zaidi? Kwa nini umekuwa

تؤتى اكلها كلّ حين باذن ربّها
Hutoa matunda yake kila wakati kwa idhini ya Mola wake Mlezi. Leo nchi ikilinganishwa na miaka kumi iliyopita, na miaka ishirini iliyopita kwa mtazamo wa nafasi ya kielimu, nafasi ya kiviwanda, nafasi ya kijamii na moyo wa wananchi, imepiga hatua zaidi; uimara wa Mfumo umekuwa mkubwa zaidi. Nini sababu yake? Sababu yake ni kwamba humu nchini kuna nguvu ya ndani ya ujengaji kwa maana halisi ambayo imeweza kuzishinda hila zote, njama zote na ukorofi wote unaofanywa na adui; hili ni jambo lililo wazi kabisa. Kwa hivyo sisi tuna kila kitu, kwa hivyo uwezo tunao. Lakini pia tunaweza kuuvunja uwezo huu kwa mikono yetu wenyewe. Kama tutaudhoofisha moyo wa hamasa uliopo, kama tutapunguza matumaini, kama tutazipoteza fursa na kama tutaufanya upeo wa mustakabali uonekane mbele ya macho ya vijana wetu, ambao ndio tumaini letu, kuwa ni mweusi na wa giza tutakuwa tumejidhoofisha kwa mikono yetu wenyewe. Haifai kufanya hivi; hili liko mikononi mwetu wenyewe. Viongozi wote; lakini hasa hasa mamudiri na wakuu wa idara mbalimbali za serikali, wao wana jukumu kubwa zaidi.
Bahati nzuri nchi yetu imepiga hatua nzuri pia katika kutumia lugha ya kukabiliana na ulimwengu wa kiistikbari na utumiaji mabavu wa Magharibi. Leo viongozi wa nchi yetu wakati wanapozungumza kwenye meza ya mazungumzo ya aina mbalimbali na katika viriri tofauti, wanasema maneno yaliyokomaa, yaliyokamilika, ya kuvutia na kwa usahihi. Moja ya sehemu za mpambano na medani za mchuano ni uzungumzaji katika uga wa kimataifa. Aghalabu ya vyombo vya habari vya Ulaya ni vyombo vya Kizayuni; huenda mnalijua hili na mlijue. Aghalabu ya vyombo hivi tunavyosikia majina yao duniani vilikuwa katika mawazo ya mabepari wa Kizayuni tokea miaka mingi nyuma na kwa hivyo wakaviweka chini ya udhibiti wao; na ndivyo vinavyopanga habari na kuainisha muelekeo wa habari. Vyombo hivi vya habari ndivyo vinavyowaelekeza pia wanasiasa nini la kusema. Hili ndilo suala muhimu. Kwa hivyo pamoja na wanasiasa wa Magharibi kuwa na uhabithi na uafriti wao, vyombo hivi vinavyopanga habari navyo pia vinawatia shemere ya kuwaelekeza nini cha kusema. Moja ya maneno yaliyoenea hivi sasa ni haya: Sisi tunaishinikiza Iran ili irudi kwenye meza ya mazungumzo. Meza gani ya mazungumzo? Ni lini Iran iliondoka kwenye meza ya mazungumzo juu ya masuala mbalimbali ya ulimwengu likiwemo suala la nyuklia hata irudi hivi sasa?! Huu ni udanganyifu na hadaa ya kipropaganda. Sisi tunafanya jitihada ili Iran irudi kwenye meza ya mazungumzo! Hii ni hadaa na udanganyifu wa kipropaganda. Wamekuwa wakilikariri hili ulimwenguni na kulirudia mara kwa mara. Maneno haya yanakaririwa kiasi kwamba mimi nadhani wanasiasa wenyewe wa Magharibi pia wanaamini kuwa huu ndio ukweli wenyewe; ilhali yule mtu aliyebuni maneno haya na kwa mpangilio huu ana makusudio mengine. Yeye haitaki Iran irudi kwenye meza ya mazungumzo; yeye anataka wakati wa mazungumzo, Iran isalimu amri mbele ya watumiaji mabavu wa Magharibi. Sasa jibu kutoka upande wa Iran ni hili, hapana; nyinyi si lolote si chochote wa kuweza kulipigisha magoti na kulifanya litii uchu na matakwa yenu taifa la kimapinduzi, la watu wanamapambano na wenye uono wa mbali na uelewa. Tatizo la wanasiasa watumiaji mabavu wa Magharibi si kutofanya mazungumzo Iran kuhusu kadhia ya nyuklia au kadhia nyenginezo; la hasha, tatizo lao hawa ni kwamba Iran haikubali kutii wanayotaka. Na bila ya shaka tatizo hili litaendelea kuwepo; hili liko wazi kabisa.
Ajabu ni kwamba leo Wazungu wa Ulaya wangali wanazungumza lugha ya zama za karne ya kumi na tisa! Zama zile meli ya Uingereza ilikuwa ikija Ghuba ya Uajemi, na kutokea ndani ya meli hiyo kamanda wa Kiingereza alikuwa akiwapelekea ujumbe wafalme wa Ghuba ya Uajemi fanyeni jambo fulani na msifanye jambo fulani; na wao walikuwa wakiinama mithili ya watumwa na kuitika hewala! Wazungu wa Ulaya wanadhani hivi sasa pia ni karne ya kumi na tisa. Tawala zilizokuwepo madarakani katika nchi yetu hazikuwa tawala zenye ghera na uchungu wa kuweza kuakisi katika miamala yao utambulisho na heshima ya taifa la Iran; walikuwa wakiendeshwa, walikuwa dhaifu kuathiriwa. Wao wazungu wa Ulaya waliweza kuathiri katika siasa na utamaduni wa viongozi hawa; waliwashinda na kuwadhoofisha viongozi hao katika batini zao. Mnaona hivyo, shakhsia mmoja, mtu mmoja au taifa zima - hakuna tofauti - hushindwa na kudhoofika katika medani za nje wakati anapokuwa amedhoofika katika batini ya nafsi yake. Kwa kuwa watu hao (Wazungu wa Ulaya) walikuwa wafanya mashambulio, na kwa vile upande huu pia ulikuwa wa wapenda dunia, wapenda umaada, wa watu walioshughulishwa na ufalme wao tu, walioshughulishwa na utawala wao tu, walioshughulishwa na pesa zao na walioshughulishwa na mali na biashara zao tu - hawakuwa wakijali malengo matukufu; walikuwa wakishughulishwa na matakwa duni ya kibinadamu - kwa hivyo upande ule uliushinda upande huu. Leo pia wanadhani hali iko kama vile.
Suala lililopo leo hii ni la ‘ujumbe mpya' ambao Jamhuri ya Kiislamu imeutangazia ulimwengu na kuwahamanisha waistikbari wa dunia. Leo waistikbari wa dunia hawako katika hali ya kuweza kuzungumza na Mapinduzi ya Kiislamu kwa lugha ya mfanya mashambulio. Leo Mapinduzi ya Kiislamu yameweza kueneza fikra yake ulimwenguni. Licha ya uchujaji wao wote wa habari waliofanya, licha ya mashinikizo yao yote waliyotoa, leo fikra hii ni fikra iliyoenea kila mahala. Fikra ya Utawala wa Wananchi Unaoendeshwa Kidini, fikra ya kutawala umaanawi na kutawala dini, fikra ya kujitokeza wananchi katika medani mbalimbali, fikra ya kusimama kukabiliana na utumiaji mabavu wa madola yenye nguvu duniani na kambi zenye nguvu ulimwenguni; fikra hizi leo zimeenea ulimwenguni. Nyinyi mnashuhudia kuwa fikra hizi zimeenea duniani; kama hazijaenea kwa jina la Iran, na zisienee; sisi hatung'ang'anii kuwa lazima zienee kwa jina la Iran; lakini hakuna mtu yeyote ulimwenguni anayekana taahira ya Mapinduzi ya Kiislamu na ya kusimama imara taifa la Iran katika matukio haya. Hii ndio hali iliyoko leo hii.
Kwa hivyo kila kitu kinafanyika kwa kufuata njia sahihi. Tunachohitaji ni kufanya juhudi, kuwa na harakati, kuwa na fikra sahihi, kufanya mambo kwa usahihi, kuwa na umoja na mshikamano na kuifanya anga na mazingira kuwa ya ufanyaji juhudi, uchapaji kazi, ikhlasi na umaanawi na kujiweka mbali na ufanyaji mambo kwa kujionyesha na mambo mengine kama hayo; hii ndio medani iliyoko leo hii. Nyinyi ndugu wapenzi ambao mna nyadhifa katika sehemu mbalimbali - kuanzia kwenye ngazi za juu za mkoa hadi ngazi za kati na ngazi nyengine tofauti - kila mmoja wenu ana nafasi na mchango wa kutoa. Kama nilivyosema; iwe ni watu wenye nyadhifa rasmi na zilizopangwa na kubainishwa kisheria au wenye nyadhifa na majukumu ya kijamii; kama mashekhe, kama wasomi wanafikra, kama wahadhiri wa vyuo vikuu, kama wataalamu, kama wanaharakati mbalimbali wa kijamii ambao wana mchango wenye taathira, wote hao wana jukumu; hata kama majukumu yao hayatokuwa na sura ya wadhifa wa kiserikali. Sisi sote tuna majukumu. Ni matumaini yangu kuwa inshallah Mwenyezi Mungu Mtukufu atatusaidia ili tuweze kutekeleza majukumu yetu.
Ninamwomba Mwenyezi Mungu akuhifadhini nyinyi nyote akina kaka na akina dada wapenzi. Inshallah Mwenyezi Mungu akupeni taufiki nyinyi nyote.
Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

 
< Nyuma   Mbele >

^