Skip to content

Habari

Habari
Hifadhi

Risala na Barua

Matini
Hifadhi

Kumbukumbu na Simulizi

Kabla ya Mapinduzi
Baada ya Mapinduzi

Sauti na Taswira

Picha
Sauti
Video
Hotuba ya Kiongozi Muadhamu katika Kikao cha Nne cha Fikra za Kistratijia Kuhusu Maudhui ya Uhuru Chapa
13/11/2012

Ifuatayo ni hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu tarehe 13/11/2012 katika kikao cha nne cha Fikra za Kistratijia kuhusu maudhui ya Uhuru.

Bismillahir Rahmanir Rahim

Kwanza nimefurahi sana, na kwa kweli ninatoa shukurani kwa kila mmoja kati ya hadhirina hususan akina kaka na akina dada waliosumbuka, wakafanya utafiti, wakaandaa makala, kisha wakafanya juhudi za kuzifupisha makala hizo - ni wazi kwamba makala hizo zilikuwa zimefanyiwa muhtasari - nasi tunahitaji taufiki ya Mwenyezi Mungu ya kuweza inshallah kupata wakati wa kuziangalia makala kamili za asili ambazo wamezichapisha na kuziwasilisha. Ni jambo lililo mbali kwa upande wangu kwamba nitabahatika kupata wakati huo, lakini ni vyema kwa jamaa wengine kufuatilia makala hizo za asili na kuzisoma kwa mazingatio; kwa sababu sisi tunahitaji kuzifanyia kazi makala hizi. Aidha ninamshukuru mheshimiwa mfawidhi wetu mpenzi wa kikao Janabi Dakta Vaez Zadeh, ambaye kama ilivyo kawaida yake hueleza mambo mengi kwa kutoa maelezo mafupi; na ambaye hujitokeza hadharani kwa nadra lakini anatekeleza kazi kubwa na ngumu kwa kufuatilia mambo huku na kule. Ninajua kwamba kwa kweli yeye na wenzake wanasumbuka na kufanya kazi kubwa sana.
Inanibidi nitoe shukurani nyengine maalumu pia kwa wahusika wote wa utendaji. Siku hizi mmekuwa mkishuhudia ukabaji koo huu unaofanywa na Uistikbari wa dunia, na kwa kweli wa adui nambari moja wa uhuru dhidi ya nchi yetu na dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu - ni juu ya masuala haya ya uchumi na athari zake kwa utendaji wa majimui nzima ya serikali na kwa maisha ya wananchi - na tab'an hili linasababisha kuwepo daghadagha na hamaniko katika anga ya kisiasa nchini; yaani hakuna yeyote kati yetu ambaye fikra zake hazishughulishwi na hali hii; lakini pamoja na hayo kazi hii ya msingi, ya asili na ya malengo ya muda mrefu haikusita wala kusimamishwa; yaani kikao hiki kimeweza kufanyika takribani katika wakati uleule kama jamaa walivyokuwa wamepanga. Hili linanifurahisha mimi na pia linanifanya niwashukuru wahusika wote wa utendaji.
Jamhuri ya Kiislamu ina malengo makuu kadhaa inayofuatilia katika kuitisha vikao vya Fikra za Kistratijia; na sisi hatutaki tuyasahau malengo haya na kuyaondoa mbele ya macho yetu. Moja ni kwamba nchi yetu inahitajia mno fikra, mawazo na ubunifu wa fikra. Kuna maudhui nyingi za msingi ambazo tumekuwa tukizizungumzia, hiki kikiwa ni kikao cha nne, na tunahisi kuwa tunahitaji kuwa na ubunifu wa fikra na kuzifanyia kazi fikra hizo juu ya maudhui hizi. Katika mkutano mmoja wa mwezi wa Ramadhani uliofanyika katika Husainiya hii na majimui ya watu wa Vyuo Vikuu - sikumbuki tena kama ulikuwa wa wahadhiri au wanafunzi - niliashiria moja ya maneno aliyonieleza mmoja wa hadhirina na wazungumzaji katika kikao hicho hicho cha mwaka uliopita ambaye alinihutubu mimi kwa kuniambia, kwa kuwa kwa miaka kadhaa sasa, umekuwa ukitilia mkazo kiasi hiki juu ya suala la elimu na maendeleo ya kielimu pamoja na ustawi wa kielimu ingefaa utilie mkazo na kusisitiza juu ya fikra pia. Mimi nilifikiri, nikahisi maneno aliyosema yana umuhimu mkubwa sana. Na hapa pia tumesema kwamba twendeni tukatafakari juu ya fikra, juu ya ubunifu wa fikra na juu ya namna ya kuzifanyia kazi fikra hizo. Tab'an suala hili lina masharti yake, linahitajia mazingira ya matayarisho na linahitajia nyenzo zake; baadhi yake tunazo na baadhi yake hatuna lakini tunaweza kuzipata. Hizi ni miongoni mwa changamoto za msingi kwa taifa lolote. Taifa kama letu ni taifa ambalo halijatuama tu kama kidimbwi; limo katika hali ya harakati mithili ya mto. Hivi ndivyo tulivyo; sisi tumo katika hali ya harakati, tunapiga hatua kwenda mbele. Tunajikwaa huku na kule na kukabiliana na vizuizi hivi na vile lakini upigaji hatua mbele hausiti. Sisi ni taifa la namna hii; kwa hivyo tunahitaji kulitafakari suala hili. Hivyo basi hitajio kubwa ililonalo nchi juu ya kufikiri na kutafakari, hususan katika maudhui za masuala ya msingi ni moja ya malengo ya vikao hivi.
Kuna lengo jengine pia ambalo ni umuhimu wa kuwa na mawasiliano ya moja kwa moja na wenye vipawa. Inawezekana mimi nikachukua kitabu chako nikasoma; lakini hii ni tofauti na kusikia maneno yako kutoka kwako wewe mwenyewe moja kwa moja hata kama kwa sura ya muhtasari tu. Suala hili linawahusu hadhirina wote waliopo hapa. Wahutubiane na wasikilizishane maneno yao baina yao moja kwa moja; hii pia ni nukta moja muhimu.
Nukta nyengine ya tatu - ambayo hii pia ni nukta muhimu sana - ni kuandaa mazingira ya kielimu kwa ajili ya kupata majibu ya masuali muhimu katika maudhui za msingi. Kama mlivyoashiria baadhi ya jamaa, sisi tunakabiliwa na masuali kadhaa; na masuali haya yanapasa yapatiwe majibu. Masuali haya si ya kuzusha utata na si ya kuleta tashiwishi na utatizaji wa akili; bali ni ya kubainisha masuala ya msingi ya maisha yetu ya kijamii. Kutokana na msimamo tulionao wa kueleza kwamba sisi ni Jamhuri ya Kiislamu na Mfumo wa Kiislamu kufanya hivi ni kuzungumzia masuala ya msingi. Inapasa yazungumzwe na inapasa yapatiwe majibu. Je suala hili limetatuliwa? Lina jibu la wazi kabisa au halina? Tunahitaji kufanya kazi katika uwanja huu. Na haya ndiyo malengo ya kikao hiki.
Bila ya shaka kikao hiki tunachofanya usiku huu na vikao vingine vitatu vya kabla yake, havijafanyika kwa lengo kwamba uamuzi wa mwisho utolewe hapa. Si nyinyi mnaotoa uamuzi wa mwisho wala si mimi ninayefanya hivyo; hapa ni mahala pa kuandaa mazingira tu. Sisi tunataka harakati hii ianze kufanya kazi; harakati hii ni mfano wa chemchemi ichemkayo, kwa hivyo ichimbuliwe ifunguke iwe wazi ili itiririke. Kazi hasa ya msingi inapasa ianze baada ya kikao hiki; na hiyo itafanywa na watafiti na wahadhiri wenye ari na wenye fikra nzuri katika Vyuo vya Kidini na katika Vyuo Vikuu pia. Kazi zilizofanywa baada ya kikao cha kwanza - ambacho kilikuwa kikao kuhusu Maendeleo kwa Kufuata Kigezo cha Kiirani na Kiislamu - janabi Dakta Vaez Zadeh alizitolea ufafanuzi; kazi nzuri na za msingi zimefanyika. Kikao kilichofuatia pia ambacho kilihusu maudhui ya Uadilifu, ufuatiliaji wake ulikabidhiwa kwa tume ile ile. Kikao cha tatu kilikuwa ni kuhusu Familia. Kuna kazi muhimu zimefanyika katika uwanja huo; iwe ni katika kituo kikuu au katika baadhi ya taasisi za utafiti na vituo vya kitaalamu. Kazi imo katika hali ya kuendelea. Kutoakisiwa kwa matangazo kazi hii kumetokana na ombi nililolitoa mimi mwenyewe. Tokea hapo mwanzo hatukupendelea kuweka tangazo kwa ajili ya kazi hii. Sisi tunataka kazi ifanyike; wakati kazi itakapokuwa imefanyika hapo tangazo litajitokeza. Tab'an hivi karibuni niliwaambia jamaa kwamba ili kuiendeleza harakati hii na kuweza kutekelezeka kivitendo hususan katika maudhui yenye changamoto kama Uhuru tuliwaomba wahusika watekeleze sera ya kudumu ya upashaji habari, ili wanafikra, watu wenye hamu ya suala hili na watu ambao pengine wamepatwa na ukimya au wanatafuta kisingizio cha kuwahamasisha, wote hao waweze kunufaika na kikao chetu cha leo usiku na kujitosa kwenye harakati hii. Ama kuhusu ufanyaji tablighi na utangazaji - kwa maana yake halisi - hatuna lengo la kufanya hivyo.
Ama kuhusu maudhui ya kikao cha usiku wa leo - yaani cha suala la Uhuru - kuna nukta kadhaa za kuzingatiwa. Maelezo waliyotoa jamaa yalikuwa maelezo mazuri sana. Yaani kwa kweli wakati mtu anaposikiliza - na mimi ni msikilizaji mzuri na huwa ninayasikiliza maneno kwa makini - hufaidika hasa. Kwa kweli tumefaidika kutokana na maelezo yote haya yaliyotolewa na jamaa - baadhi yao sana na baadhi yao kwa kiwango cha wastani - yalikuwa na nukta za kuzingatiwa. Tab'an nilieleze hili pia bila ya kujifanyia muhali: kutokana na majimui ya maelezo waliyotoa majanabi tumeweza kufahamu pia pengo kubwa tulilonalo katika uwanja huu. Maelezo na utafiti wenu, wenyewe umezidisha imani niliyokuwa nayo, ya kuelewa uhaba mkubwa tulionao katika suala hili; na kwa hivyo nitagusia juu ya suala hili la uhaba tulionao.
Ukweli ni kwamba maudhui ya Uhuru baina ya Wamagharibi, katika karne hizi tatu nne za karibu ya zama za Mvuvumko (Renaissance) na baada ya Mvuvumko imeshamiri na kustawi kwa kiwango kisicho na mfano. Iwe ni katika elimu ya falsafa au katika uwanja wa Sayansi ya Jamii, au katika uga wa Sanaa na Fasihi hakuna maudhui iliyojadiliwa zaidi huko Magharibi kama suala la Uhuru katika karne hizi tatu nne zilizopita. Suala hili lina sababu kuu na pia lina sababu za pembeni. Sababu kuu ni kwamba ili ipatikane harakati katika masuala ya msingi kama haya lazima kuwepo na tukio la kichocheo; yaani mara nyingi hutokea wimbi la kusukuma harakati za masuala ya msingi kama haya. Katika mazingira ya kawaida huwa haijitokezi mijadala ya changamoto za kina na muhimu kuhusiana na maudhui za msingi kama hizi; huwa lazima litokee kwanza tukio fulani ambalo litakuwa utangulizi wa kujiri kadhia hiyo. Tab'an kama nilivyoeleza, sambamba na kuashiria sababu hii kuu - na hapa ninaizungumzia sababu hiyo kuu - kuna sababu za pembeni pia. Tukio hilo kuu la kwanza lilikuwa ni la Mvuvumko (Renaissance) - Mvuvumko uliojiri katika majimui ya nchi za Ulaya; kuanzia Italia ambako ndiko lilikokuwa chimbuko lake, kisha Uingereza, Ufaransa na mahala kwengineko - baada ya lile la Mapinduzi ya Viwanda lililojitokeza nchini Uingereza mwishoni mwa karne ya kumi na saba na mwanzoni mwa karne ya kumi na nane. Mapinduzi yenyewe ya Viwanda lilikuwa tukio mithili ya mripuko linalowafanya watu wakae kulitafakari na linalowafanya wanafikra pia wakae kulitafakari. Kisha katika nusu ya karne ya kumi na nane yakajitokeza mazingira ya utangulizi wa kujiri Mapinduzi Makuu ya Ufaransa - ambayo yalikuwa mazingira ya kijamii ya kujiri mapinduzi makubwa - katika eneo ambalo halikuwa na mapinduzi ya aina hii. Bila ya shaka mapinduzi yanayofanana na hayo katika kipindi cha miaka mia moja hadi mia mbili kabla yake yalitokea kwa kipindi kifupi nchini Uingereza, lakini hayakuweza kulinganishwa na yale yaliyojiri katika Mapinduzi Makuu ya Ufaransa.
Utangulizi wa Mapinduzi ya Ufaransa ulikuwa ni ule utayarifu uliokuwemo ndani ya majimui; ni kile kitu kilichokuwa kikifukuta ndani ya jamii na ambacho wanafikra walikuwa wakikiona. Nikuelezeni tu kwamba, vile watu kama Montesquieu au Rousseau walivyofaidika kifikra kutokana na matukio ya ndani ya jamii ya Ufaransa matukio ya jamii ya Ufaransa hayakufaidika kwa kiwango kama hicho na fikra za watu hao. Mtu yeyote akiangalia ataweza kuliona hili. Mnajua kwamba Montesquieu mwenyewe alikuwa nje ya Ufaransa. Kulikuwepo na matukio kadhaa yaliyojiri. Kabla ya kujiri mripuko ule mkubwa wa mwaka 1789 - na kwa kweli ulikuwa mripuko mkubwa; kwani ulisababisha hasara kubwa, ulileta uharibifu mkubwa - kuna matukio mengi yaliyokuwa yakitokea ndani ya jamii, miji na nchi ambayo yalikuwa yakionyesha kuwa kuna kitu kinataka kujiri. Ama kuhusu maudhui ya Uhuru, wameielezea kuwa imetokana na fikra ya akili na mantiki. Lakini sio hivyo, mimi nitakuambieni; katika Mapinduzi Makuu ya Ufaransa inawezekana kwamba walikuwepo wanafikra wanne ambao walikuwa wakizungumza maneno ya namna moja, lakini katika medani ya utendaji kile ambacho hakikuwepo ni suala la akili na mantiki na mielekeo ya utumiaji akili. Hapana; ni suala la Uhuru tu ndilo lililokuwa likifikiriwa huko; na kwa sehemu kubwa ni uhuru wa kujivua na pingu za ufalme na utawala wa kidikteta uliokuwa umedhibiti kila kitu tokea karne kadhaa zilizopita; ni utawala wa Wabourboni waliokuwa wamedhibiti nguzo zote kuu za maisha ya watu. Na halikuwa tabaka la waliokuwa na mfungamano na utawala tu bali hata maashrafu wa Ufaransa nao pia kila mmoja alikuwa mfalme kwa upande wake. Kama mumesikia kuhusu Bastille na magereza ya Bastille haya hayakutokea katika kile kipindi kifupi; huenda karne kadhaa zilikuwa zimepita na Bastille ilikuwa ingali ileile. Yaani hali ilikuwa ni ya mchafukoge. Wakati watu wenye fikra kama vile Voltaire, Rousseau na Montesquieu walipokuwa wakiiona hali hiyo, kwa kuwa walikuwa na fikra na vipawa vya kufikiri waliweza kufikia natija fulani na kusema maneno fulani; lakini maneno yao hayakuwa yakizingatiwa na kupewa umuhimu asilani katika utendaji mambo ndani ya Ufaransa. Sasa angalieni hotuba zilizokuwa zikitolewa wakati ule na shakhsia waliokuwa na ufasaha wa kusema - Mirabeau na wengineo - hakuna yoyote kati ya hizo iliyokuwa ikiegemea kwenye maneno ya Montesquieu na maneno ya Voltaire na wengineo; zote hizo zililenga kwenye ufisadi wa vyombo vya utawala, udikteta wa vyombo vya utawala na mfano wa hayo. Huu ndio ukweli kuhusu mapinduzi ya Ufaransa.
Mapinduzi Makuu ya Ufaransa, yanaweza kuelezewa kuwa ni mapinduzi yaliyofeli. Si zaidi ya miaka kumi na moja hadi kumi na mbili baada ya mapinduzi, ukajitokeza utawala wa ufalme mkubwa na wenye nguvu wa Napoleone, yaani utawala mutlaki wa kifalme, yaani jinsi Napoleone alivyotawala kifalme hawakuwahi kutawala namna hiyo wafalme wote wa kabla ya Louis wa Kumi na Sita (XVI) aliyeuawa!
Wakati Napoleone alipotaka kuvishwa taji, walimleta Papa ili amvishe kichwani Napoleone taji la ufalme; lakini Napoleone hakumruhusu Papa amvishe; alimpokonya Papa mkononi na kujivisha kichwani mwenyewe! Nitoke kidogo nje ya mada. Katika kulinganisha na mapinduzi yetu si vibaya ikazingatiwa nukta ifuatayo: katika mapinduzi yetu, kitu ambacho hakikuruhusu matukio kama haya na maafa mbalimbali kutokea - angalau kwa sura fulani na hata kama mathalani ni kwa kiwango hafifu - ilikuwa ni kuwepo kwa Imam Khomeini. Yeye kiongozi aliyekuwa akikubalika, mwenye ushawishi na mwenye kutiiwa na wote, ndiye ambaye hakuruhusu hayo yatokee; vinginevyo nakuhakikishieni kwamba kama si matukio sawa na yale, basi yangejiri matukio yanayofanana na yale. Katika miaka ileile kumi hadi kumi na mbili ya baina ya mapinduzi hadi kudhihiri kwa Napoleone na kutwaa kwake madaraka, makundi matatu yalishika hatamu za madaraka; na kila kundi liliwaua na kuwaangamiza watu wa kundi la kabla yake na wao kushika hatamu za madaraka; kisha tena kundi lililofuatia liliwaua na kuwaangamiza watu wa kundi hili. Wananchi walikuwa wakiishi katika dhiki na masaibu ya kupindukia. Haya yalikuwa Mapinduzi Makuu ya Ufaransa. Nayo mapinduzi ya Oktoba ya Urusi yalikuwa hivyo pia kwa kiwango kikubwa - yaani yalifanana na Mapinduzi Makuu ya Ufaransa - isipokuwa kule Urusi kulikuwa na hali maalumu na sababu nyengine mbalimbali ambazo zilikuwa zikiwaongoza na kuwaelekeza wananchi kwa namna fulani. Haitokuwa vibaya kama nukta hizi zitazingatiwa. Katika duru mbalimbali ambazo nimekuwa na mawasiliano nazo - ziwe ni duru za kihistoria au duru za vyuo vikuu kama hizi - kwa masikitiko ni kwamba sizioni kuzipa umuhimu nukta zilizopo katika mapinduzi haya.
Bila ya shaka mnajua kwamba mapinduzi kadhaa yalitokea nchini Ufaransa. Haya mapinduzi yaliyotokea mwishoni mwa karne ya kumi na nane ndiyo Mapinduzi Makuu ya Ufaransa. Baada ya karibu miaka arubaini yalitokea mapinduzi mengine; karibu miaka mia mbili baada ya hapo yalitokea mapinduzi mengine; ni mapinduzi ya kikomunisti. Mapinduzi ya kwanza ya kikomunisti duniani yalitokea nchini Ufaransaa ambako walianzisha mfumo wa Ujima.
Kwa hivyo hizi ndizo sababu zilizokuza harakati hii ya kifikra: kwanza kabisa ni Mvuvumko Mkubwa wa Sanaa na Maarifa (Renaissance). Tab'an Mvuvumko halikuwa tukio la ghafla, lakini kuna matukio chungu nzima yaliyojiri katika kipindi cha miaka mia mbili ya kwanza ya Mvuvumko, mojawapo likiwa ni suala la Mapinduzi ya Viwanda, na jengine ni suala la Mapinduzi Makuu ya Ufaransa. Matukio haya, yenyewe yalizungumzia fikra ya Uhuru; kwa hivyo wakalifanyia kazi suala hilo. Wanafalsafa chungu nzima waliandika maelfu ya makala za uhakiki na vitabu. Katika nchi zote za Magharibi viliandikwa mamia ya vitabu kuhusu mada ya Uhuru. Baadaye fikra hii ilihamishiwa Marekani na huko pia wakaifanyia kazi.
Hadi kabla ya Mapinduzi ya Katiba (nchini Iran) sisi hatukuwahi kuwa katika mazingira yanayofanana na yale ya kuanzisha wimbi la kifikra la kutuelekeza kwenye maudhui kama ya Uhuru. Mapinduzi ya Katiba yalikuwa fursa nzuri sana. Mapinduzi ya Katiba yalikuwa tukio kubwa, na lilikuwa na uhusiano wa moja kwa moja na suala la Uhuru; kwa hivyo ilipasa ziwa letu hili lililotulia la fikra za kielimu lipate mtikiso, iwe ni katika medani za viongozi wa kidini au zisizokuwa za viongozi wa kidini; yaani lilihitajika wimbi la kuleta harakati, kama ambavyo ndivyo ilivyokuwa. Kwa hivyo zilizungumzwa fikra kuhusiana na Uhuru, lakini kulikuwepo na kasoro moja kubwa, na kasoro hiyo haikuturuhusu sisi kufuata njia sahihi katika fikra hii na kupiga hatua mbele katika njia hiyo; na kasoro yenyewe ni kwamba miaka kadhaa kabla ya Mapinduzi ya Katiba - huenda ikawa ni miongo miwili mitatu kabla ya Mapinduzi ya Katiba - fikra za Kimagharibi, kwa kupitia wafuasi wa kiashrafu, wana wafalme na wafuasi wa Ufalme, zilianza kufungua njia na kuanza kupenya taratibu ndani ya bongo za majimui moja ya wenyefikra angavu. Na tunaposema maashrafu, katika vipindi vile vya mwanzoni, maana ya mwenyefikra angavu ilikuwa ni uashrafu. Yaani sisi hatukuwa na mwenyefikra angavu asiyekuwa ashrafu. Wenyefikra angavu wetu wa daraja ya kwanza walikuwa watu walewale wa utawala na jamaa zao pamoja na watu wenye mfungamano na wao; na tokea hapo mwanzo watu hao walikuwa na uelewa wa fikra za Kimagharibi katika suala la Uhuru. Kwa hivyo wakati mnapoingia kwenye maudhui ya Uhuru katika zama za Mapinduzi ya Katiba - ambayo ni maudhui yenye kuzusha makelele na zogo kubwa - mtaona kuwa mielekeo ileile ya kupinga Kanisa huko Magharibi ambayo ilikuwa ndiyo kigezo muhimu cha kupigania Uhuru ilionekana hapa pia kwa sura ya kupinga Msikiti, kuwapinga mashekhe na kupinga dini. Lakini mawili hayo yalikuwa na hali zisizofanana. Asili ya muelekeo wa Mvuvumko (Renaissance) ilikuwa ni dhidi ya dini na dhidi ya Kanisa; kwa sababu hiyo ikaweka msingi wa mielekeo ya Kuupa Kipaumbele Utashi wa Mwanadamu (Humanism) na upendeleo wa fikra za watu. Baada ya hapo pia harakati zote za Kimagharibi zilijengeka juu ya msingi wa Kuupa Kipaumbele Utashi wa Mwanadamu na hivyo ndivyo ilivyo hadi hii leo. Licha ya tofauti zote zilizojitokeza, msingi wake mkuu ni ule ule wa Kuupa Kipaumbele Utashi wa Mwanadamu; yaani msingi wa ukafiri, msingi wa shirki - ikiwa fursa itaruhusu nitaliashiria hili hapo baadaye - na sawa kabisa na hayo yakaletwa hapa. Mnawaona waandishi wa makala wenyefikra angavu, wanasiasa wenyefikra angavu na hata mashekhe waliofungamana na wenyefikra angavu wakati wanapoandika kitabu na makala kuhusu Mapinduzi ya Katiba, nao pia wanakariri maneno yaleyale ya Wamagharibi; si kitu kingine zaidi ya hicho. Na ni kwa sababu hiyo hakuna kitu kinachozalishwa.
Basi muone, hivi ndivyo ilivyo sifa ya fikra ya uigaji. Wakati nyinyi mnapochukua nuskha na kopi ya mtu kwa lengo la kuisoma na kuitekeleza nuskha na kopi hiyo hakuna maana tena ya kuzalisha kitu kipya. Kama utakuwa umechukua elimu, nadharia au fikra kutoka kwake, hapo unaweza wewe mwenyewe kuanzisha harakati na kupatikana uzalishaji wa kitu kipya. Lakini hili halikutokea; kwa hivyo baadaye hakuna kitu kilichozalishwa; na kwa hivyo katika uga unaohusiana na Uhuru hakuna fikra mpya, nadharia mpya wala mfumo mpya wa kifikra uliopangika - kama mifumo ya kifikra waliyonayo Wamagharibi - uliozalishwa. Wengi miongoni mwa hawa wanafikra huko Magharibi wana mfumo wa kifikra uliopangika kuhusu Uhuru. Huu ukosoaji mbalimbali uliofanywa kwa Uliberali wa zamani na pia ukosoaji mbalimbali uliokuja kufanywa baadaye kwa nadharia mpya za Uliberali na Demokrasia ya Kiliberali na zile fikra zilizoibuka baada ya Ulibereali wa mathalani karne ya kumi na saba au kumi na sita, kila moja kati ya hizo ina mfumo wa kifikra uliopangika; ule wa kwanza unao, wa mwisho pia unao, na majibu ya masuali chungu nzima pia inayo. Sisi hatukuweza kuleta hata chembe moja ya hizo katika nchi yetu; licha ya kuwa na vyanzo na marejeo mengi, sisi hatuna uhaba wa marejeo - kama walivyoashiria jamaa hapa - yaani kwa kweli tunao uwezo wa kubuni majimui ya kifikra iliyopangika, mfumo kamili wa kifikra uliopangika kuhusu Uhuru - ambao utatoa majibu kwa masuali yote madogo na makubwa kuhusu Uhuru. Bila ya shaka kazi hii inahitajia hima; si kazi rahisi. Sisi bado hatujaifanya kazi hii. Sisi licha ya kuwa na vyanzo na marejeo lakini tumefuata mfumo uleule wao wa kifikra; kilichofanyika ni kutegemea na kila mtu alipoweza kupata na kufikia; mmoja alikuwa na mawasiliano na mahusiano na Austria kwa kufuata kile kilichosemwa na mtaalamu wa Kiaustria; mwengine alikuwa akijua Kifaransa, akafuata kile kilichosemwa na kuzungumzwa Ufaransa; mmoja mwengine alikuwa na mafungamano na Uingereza na Ujerumani na kwa hivyo akaiga na kufuata yale yaliyozungumzwa kwa lugha ya Kiingereza au Kijerumani; ikawa ni uigaji tu. Wapinzani pia, ambao walikuwa wakionekana kama wapinzani wa Uhuru, nao pia walitokana na mfumo huohuo wa kifikra - yaani makundi yote mawili yalitokana na uigaji wa mfumo mmoja - na wao pia walipoona maneno na fikra hizo zinapingana na dini na zinapingana na Mungu wakaamua kukabiliana nazo.
Leo sisi tuna uhaba, sisi tuna mapengo mengi matupu na kuna mipasuko mingi ya uwazi; na licha ya kuwa na vyanzo na marejeo lakini hatuna mfumo wa kifikra uliopangika. Katika mjumuiko wa leo janabi Dakta Barzegyar - kama nitakuwa sijakosea - kwa maoni yangu alikuwa ndiye mtu pekee aliyebainisha fikra ya mfumo uliopangika. Inawezekana nyinyi mkahisi mfumo wake huo una kasoro na pengine ukawa kweli una kasoro; hilo si tatizo. Inatupasa tuelekee kwenye ubunifu wa mfumo wa fikra uliopangika; yaani tufanye kazi ya kuipanga kila kete ya dama hili mahala pake, tutengeneze mfumo uliokamilika; hili ndilo tunalohitaji kufanya. Na hii si kazi ya udoho udoho; si kazi ya kikao kimoja au vikao viwili; ni kazi ya pamoja inayohitaji kuwa na uwezo kamili wa kutabahari; kutabahari kwenye marejeo ya Kiislamu na pia kutabahari kwenye marejeo ya Magharibi; na nitaeleza kuhusu hili.
Sasa nieleze mimi kuna nukta mbili tatu. Suala moja ni kuhusu kubainisha maudhui. Kama mlivyoona, jamaa hapa wameashiria kuhusu Uhuru wa Kimaanawi. Uhuru wa Kimaanawi kwa ile maana iliyoashiriwa katika baadhi ya riwaya na hadithi zetu na walizoziashiria baadhi ya wanafikra wetu kama marehemu shahidi Mutahari, ambayo ni daraja ya juu kabisa katika aina za fadhila za mtu. Hili halina shaka yoyote, lakini hii sio mada ya mjadala wetu. Kimsingi mjadala wetu si kuhusu Uhuru wa Kimaanawi kwa maana ya kukwea daraja za kuelekea kwa Mwenyezi Mungu, kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu na kupiga hatua mbele katika uga wa tauhidi walioogolea watu kama Mulla Husseinquli Hamedani au marehemu janabi Qadhi au marehemeu Tabatabai; mazungumzo yetu ni kuhusu uhuru wa kijamii na kisiasa; uhuru wa mtu binafsi na wa kijamii; suala linalojadiliwa leo hii duniani. Ni sawa kwamba inawezekana sisi tukawa na masuala mengine mia moja ambayo asilani Magharibi hawajui chochote kuhusu masuala hayo - ni kama hili la kukwea daraja za kimaanawi na mfano wake - hayo tuyajadili na kuyazungumzia katika mahala pake. Tunachokifuatilia sisi kwa sasa ni mjadala wa Uhuru kwa maana hii maarufu na iliyozoeleka katika duru za vyuo vikuu, za kisiasa na za wenyefikra angavu wa leo duniani, ambao wanajadili na kuzungumza kuhusu Uhuru. Sisi tunataka kulijadili suala hili. Uhuru wa kimaanawi kwa maana ile ya kukwea daraja za kuelekea kwa Mwenyezi Mungu, kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu, kumuelekea Mwenyezi Mungu, kuwa na huba na mapenzi ya Mwenyezi Mungu na mfano wa hayo, hiyo ni maudhui nyengine na ina mahala pake. Kwa maana moja kuna aina nyengine ya Uhuru ambao unaweza kuitwa Uhuru wa Kimaanawi, na huo ni Uhuru wa kujivua na kujikomboa na vitu vya ndani ya nafsi ambavyo vinatuzuia sisi kufanya jambo la uhuru katika jamii, au vinavyotuzuia sisi kuwa na uhuru wa kufikiri katika jamii; kama hofu ya kifo, hofu ya njaa, hofu ya ufakiri. Hofu hizi zimeashiriwa ndani ya Qur'ani: فلا تخشوا النّاس و اخشون Basi msiwaogope watu bali niogopeni Mimi (Al - Maidah 5:44), فلا تخافوهم و خافون ان كنتم مؤمنينBasi msiwaogope na niogopeni Mimi, ikiwa nyinyi ni waumini (Al - Imran 3:175) Imemhutubu Mtume kwa kumwambia: و تخشى النّاس و اللّه احقّ ان تخشاه Na ukachelea watu na hali Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye haki zaidi ya kumchelea (Al - Ahzab 33:37). Au kuwa na hofu ya kupoteza fursa za upendeleo. Chukulia mfano sisi tunapata fursa za upendeleo katika taasisi fulani; kama tutasema maneno haya, kama tutaamua kuitumia sifa ya kuwa huru, kama tutaamrisha mema tutaanguka na kupoteza fursa hizo. Au tamaa ya kitu. Tamaa huweza kunifanya mimi nisikueleze aibu yako, nisiamiliane na wewe kwa uhuru - wewe ambaye ni mtu kwenye madaraka - kwa sababu ya kuwa na tamaa ya kitu kwako wewe. Au husuda, ambayo hutokana na taasubi zisizo na msingi na potofu au fikra mgando; haya pia ni aina fulani za vizuizi vya ndani ya nafsi ambapo mtu anapokomboka navyo na kuwa huru tunaweza kuuita huo Uhuru wa Kimaanawi. Kwa hivyo sisi tuna istilahi mbili katika Uhuru wa Kimaanawi: Istilahi moja ni ile ya kwanza ambayo ni kupaa kimaanawi kuelekea kwa Mwenyezi Mungu, kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu, kuwa na mapenzi ya kweli ya Mwenyezi Mungu na masuala kama hayo. Hayo hayaingii asilani katika mazungumzo yetu, hiyo ni maudhui nyengine kabisa. Nyengine ni istilahi ya Uhuru wa Kimaanawi kwa maana ya kujivua na pingu na minyororo ya ndani ya nafsi ambayo inanizuia mimi nisiende kwenye Jihadi, ambayo hairuhusu mimi kuingia kwenye mapambano, ambayo hainiruhusu mimi kusema maneno kwa uwazi kabisa, ambayo hainiruhusu mimi kubainisha waziwazi misimamo yangu, inayonifanya mimi niwe na unafiki na kuwa na hali ya nyuso mbili. Suala hili linaweza kujadiliwa katika maudhui ya kupambana na vizuizi vya Uhuru.
Nukta inayofuatia ni kwamba sisi tunataka kuelewa mtazamo wa Uislamu juu ya suala hili. Tunapaswa kuwa wawazi katika suala hili. Ikiwa sisi tunataka kufuata nadharia ghairi ya Uislamu - ya kila kile kinachotupitikia na kubuniwa na akili zetu - tutasibiwa na hali zile zile za mkanganyo unaowapata wanafikra wa Kimagharibi katika nyanja mbalimbali; ya kuwa na nadharia na rai tofauti zenye kugongana ambazo aghalabu yao hazina uendeleaji wa kiutekelezaji. Sisi hatuyataki hayo, tunataka kujua Uislamu una mtazamo gani.
Kwa hivyo katika mjadala wa Uhuru, tunaamua kujiwekea mpaka wa kwanza kwa ajili yetu sisi wenyewe. Mpaka huo ni upi? Mpaka wenyewe ni kwamba sisi tunautaka mtazamo wa Uislamu; tunajiwekea mpaka sisi wenyewe kulingana na mtazamo wa Uislamu na katika fremu na kalibu ya Uislamu. Huu ni mpaka wa kwanza. Tusiogope kuwepo mpaka katika mjadala juu ya Uhuru. Kwa sababu wakati inaposemwa kuhusu Uhuru, uhuru katika maana yake ya kwanza - ambayo inafahamika kwa kuzingatia dhati yake ya asili - ina maana ya kukomboka na kuwa huru. Mtu anayetaka kuzungumza kuhusu Uhuru ni kana kwamba anahisi uzito wa kila kitu kinachokinzana walau kidogo tu na kuwa huru; yaani anatafuta kila kilicho nje ya hali hiyo ya mkinzano. Kaida na kanuni yake ni kuwa huru mutlaki. Yeye huwa anatafuta kile "kinachotoka nje ya kaida hiyo kwa hoja"ajue ni kipi ili aseme, katika nyuga hizi Uhuru 'hapana' na katika nyuga zile uhuru 'hapana', lakini baada ya kuvuka nyuga hizi Uhuru huwa 'sawa'. Hili ni kosa ambalo mtu anaweza kulifanya katika kuzungumzia mada ya Uhuru. Mimi ninasema kwamba suala hili haliko hivyo. Tangu mwanzo wake hakuna dhana ya kuchukulia kwamba Uhuru ni kitu mutlaki - na hapa nitaeleza kwamba Uhuru katika Uislamu asili na chimbuko lake ni nini hasa - tokea mwanzo wake sisi hatuna nadharia tete ya kuchukulia kwamba Uhuru mutlaki ni haki ya mwanadamu, ni milki yake mtu na ni kitu chenye sura ya thamani kwa mtu. Hebu sasa na turudi kuangalia hizo hali zinazotoka nje ya kaida ni zipi, "zilizotoka nje ya kaida kwa hoja" ni zipi. Kadhia haiko hivyo asilani. Sisi tusiogope kuwepo mpaka. Kama nilivyoeleza, mpaka wa kwanza tunaozungumzia kuhusu mijadala juu ya Uhuru katika Uislamu ni kwamba sisi tunasema, katika "Uislamu"; yaani kuanzia mwanzo tunaanza kuweka kalibu na fremu maalumu; tokea mwanzo tunautengenezea Uhuru mpaka. Uhuru katika Uislamu una maana gani? Huu wenyewe ni mpaka. Na hapa ndipo hasa ulipo mjadala wetu.
Katika aya maarufu ya sura tukufu ya al Aaraf, Mwenyezi Mungu anasema:

الَّذِينَ يَتَّبِعُونَ الرَّسُولَ النَّبِيَّ الأُمِّيَّ الَّذِي يَجِدُونَهُ مَكْتُوبًا عِندَهُمْ فِي التَّوْرَاةِ وَالإِنجِيلِ يَأْمُرُهُم بِالْمَعْرُوفِ وَيَنْهَاهُمْ عَنِ الْمُنكَرِ وَيُحِلُّ لَهُمُ الطَّيِّبَاتِ وَيُحَرِّمُ عَلَيْهِمُ الْخَبَائِثَ وَيَضَعُ عَنْهُمْ إِصْرَهُمْ وَالأَغْلالَ الَّتِي كَانَتْ عَلَيْهِمْ

Ambao kwamba wanamfuata huyo Mtume, Nabii, asiye soma wala kuandika, wanaye mkuta kaandikwa kwao katika Taurati na Injili, anaye waamrisha mema na anawakanya maovu, na anawahalalishia vizuri, na ana waharimishia viovu, na anawaondolea mizigo yao na minyororo iliyo kuwa juu yao. (Al Aaraf 7:157). Hii ni aya katika Qur'ani inayobainisha kwa uwazi kabisa suala la Uhuru, yaani uondoaji wa اصر(mizigo)". اصر ni zile kamba zinazofungwa kwenye vigingi vya hema vinavyolizuia lisichukuliwe na upepo; yaani vinalishikiza na ardhi. وَلَكِنَّهُ أَخْلَدَ إِلَى الأَرْضِ lakini yeye akaushikilia ulimwengu (Al Aaraf: 7:176). Na huku ni kuushikilia ulimwengu." اواصر" zetu ni vile vitu vinavyotugandisha sisi na ardhi na kutuzuia tusiweze kuruka kimaanawi. "" غلni mnyororo kama tunavyojua ambapo Mtume alikuja ili kuiondoa minyororo hiyo. Katika aya hiihii kabla ya kusema يَضَعُ عَنْهُمْ إِصْرَهُمْ وَالأَغْلالَ الَّتِي كَانَتْ عَلَيْهِمْ anawaondolea mizigo yao na minyororo iliyo kuwa juu yao, inasema وَيُحِلُّ لَهُمُ الطَّيِّبَاتِ وَيُحَرِّمُ عَلَيْهِمُ الْخَبَائِثَ na anawahalalishia vizuri, na anawaharimishia viovu. Nini maana ya halali na haramu? Maana ya halali na haramu ni kuweka mpaka, ni kuzuia; kunakoambatana na kupiga marufuku. Kwa hivyo tusihisi tabu asilani ndani ya akili zetu wakati tunapozungumzia Uhuru kwa sababu ya kuwepo mpaka na katazo.
Baadhi ya majanabi wamesema kuna tofauti za katika asili na kiini baina ya mtazamo juu ya Uhuru na nadharia ya Uhuru katika Uislamu na katika Ulimwengu wa Magharibi; na kwa upande wa Magharibi hasa wameuzungumzia Uhuria; na tab'an kuna nadharia nyengine pia lakini zote hizo zina mtazamo mmoja katika suala hilo. Ni kweli na sawa kabisa; hizi tofauti walizoeleza majanabi ziko kweli; lakini tofauti muhimu zaidi ni kwamba: katika Uhuria asili ya Uhuru, ikiwa ni haki au thamani, maana yake imesimama juu ya fikra ya kumfanya mtu kuwa asili ya kila kitu - Humanism (Kuupa Kipaumbele Utashi wa Mwanadamu) - kwa sababu mhimili mkuu wa ulimwengu wa uwepo na mhimili mkuu katika ulimwengu huu wa viumbe ni "Mwanadamu"; na bila ya kuwa na hiyari na uhuru, kuwepo kwake huwa hakuna maana yoyote; kwa hivyo lazima awe na hiyari na uhuru. Tab'an hiyari hii siyo ile hiyari ya "Lazima na Hiyari". Baadhi ya majanabi wameizungumzia ‘Lazima na Hiyari'. Hiyari tunayoizungumzia katika mjadala wa ‘Lazima na Hiyari' ni kwamba mtu "ana uwezo wa kuchagua" - ana uwezo wa dhati na wa kimaumbile - lakini tunapozungumza hapa tunasema "haki ya kuchagua". Lakini hakuna mfungamano wa lazima baina ya uwezo wa kuchagua haki na haki ya kuchagua. Bila ya shaka inawezekana mtu akajaalia kuwepo mfungamano baina yao lakini hakuna uhakika kwamba ujaaliaji huo unaweza kuwa na hoja za kuridhisha. Kwa hivyo wanachosema wao ni kwamba mwanadamu ndiyo asili na mhimili mkuu wa kila kitu; yaani mwanadamu ndiye mungu wa ulimwengu wa viumbe, na yeye hawezi kuwepo pasina kuwa na uwezo wa kuchagua na bila ya kuwa na irada ya kuamua. Yaani bila ya kuwa na irada ya kutekeleza atakacho - ambayo ni maana nyengine ya Uhuru - haiwezekani sisi kujaalia na kumchukulia mwanadamu kuwa ndiye mwenye mamlaka ya kila kitu katika ulimwengu wa ujudi wa viumbe. Huu ndio msingi mkuu wa mjadala kuhusu Uhuru. Huu ndio msingi wa fikra ya Kuupa Kipaumbele Utashi wa Mwanadamu (Humanism) kuhusu Uhuru.
Katika Uislamu, suala hili lina hali na sura tofauti kabisa na hii. Katika Uislamu msingi mkuu wa Uhuru wa mtu ni tauhidi. Tab'an jamaa hapa wametaja na mambo mengine pia - na hayo pia ni sahihi - lakini kiini na msingi mkuu ni tauhidi. Maana ya tauhidi si kumwamini Mwenyezi Mungu tu; maana ya tauhidi ni kumwamini Mwenyezi Mungu na kumkana taghuti; kumwabudu Mwenyezi Mungu na kukataa kumwabudu mwengine ghairi ya Mwenyezi Mungu;

 تَعَالَوْا إِلَى كَلِمَةٍ سَوَاء بَيْنَنَا وَبَيْنَكُمْ أَلاَّ نَعْبُدَ إِلاَّ اللَّهَ وَلاَ نُشْرِكَ بِهِ شَيْئًا

Njooni kwenye neno lilio sawa baina yetu na nyinyi: Ya kwamba tusimuabudu yeyote ila Mwenyezi Mungu, wala tusimshirikishe na chochote. (Al - Imran 3:64) Haisemi لا نشرك به احدا yaani tusimshirikishe na yeyote - na tab'an kuna mahala inaelezwa kuwa na احدا yaani na yeyote, lakini hapa imezungumzwa kwa upana zaidi - inasema: وَلاَ نُشْرِكَ بِهِ شَيْئًا yaani na wala tusimshirikishe na chochote. Yaani msikifanye kitu chochote mshirika wa Mwenyezi Mungu. Yaani kama nyinyi mnafuata mambo kimazoea bila ya hoja, hilo linakinzana na tauhidi; ikiwa mnawafuata watu, ni vivyo hivyo pia, ikiwa mnafuata mifumo ya kijamii, ni hivyo hivyo pia - yale yote ambayo hayaishii kwenye kukidhi irada ya Mwenyezi Mungu - yote hayo ni kumshirikisha Mwenyezi Mungu, na tauhidi maana yake ni kujiepusha na shirki hizo. فَمَنْ يَكْفُرْ بِالطَّاغُوتِ وَيُؤْمِن بِاللَّهِ فَقَدِ اسْتَمْسَكَ بِالْعُرْوَةِ الْوُثْقَىَ لاَ انفِصَامَ لَهَا Basi anaye mkataa Shet'ani na akamuamini Mwenyezi Mungu bila ya shaka amekamata kishikio madhubuti, kisicho vunjika. (Al Baqarah 2:256). Hapa kuna kumkana taghuti kisha baadaye inafuatia imani juu ya Mwenyezi Mungu. Na hii ndiyo maana ya Uhuru. Yaani wewe unakuwa huru na vifungo na vizuizi vyote vinavyokuzuia kumwabudu Mwenyezi Mungu.
Miaka kadhaa nyuma mimi nilizungumzia mada hii ya Uhuru katika hotuba kumi au kumi na moja katika Sala ya Ijumaa ya Tehran. Kule niliashiria suala moja na kueleza kwamba sisi katika Uislamu tunajihesabu kuwa ni watumwa wa Mwenyezi Mungu; lakini katika baadhi ya dini watu huwa wanajihesabu wao wenyewe kuwa ni wana wa Mungu. Nikasema huu ni utani; wanajifanya wana wa Mungu lakini wanakuwa watumwa wa maelfu ya watu, watumwa wa maelfu ya vitu na watu! Hivi ndivyo unavyosema Uislamu; unasema, wewe kuwa mwana wa mtu yeyote unayetaka; lakini unapaswa kuwa mtumwa wa Mwenyezi Mungu tu, usiwe mtumwa wa asiyekuwa Mwenyezi Mungu. Mafundisho mengi ya Kiislamu yanayohusiana na suala la Uhuru yanatilia mkazo nukta hii.
Kuna hadithi hii maarufu iliyopokewa kutoka kwa Amirul Muuminin, na inavyoonekana imepokewa pia kutoka kwa Imam Sajjad, kwa ninavyokumbuka imepokewa vilevile kutoka kwa Imam Hadi (alayhi ssalam) ambayo inasema:
أَلَا حُرٌّ يَدَعُ هَذِهِ اللُّمَاظَةَ لِأَهْلِهَا Aliye huru hasa ni yule anayekiacha kitu hiki duni kisicho na thamani kwa mwenyewe - huku ndiko kuwa huru - yaani je aliye huru hasa si yule anayemtupia mwenyewe mbele yake bidhaa hii duni - lamadha, yaani Kamasi au mate ya mnyama duni. Mpaka hapa hatuwezi kufahamu chochote. Kinachofahamika ni kwamba mtu huru ni mwenye kukitupa kitu hiki mbele ya mwenyewe, asiende kukifuata kitu hicho. Kisha inasema: فليس لأنفسكم ثمن الّا الجنّة فلا تبيعوها بغيرها Hazina nafsi zenu thamani ya kitu kingine ila Pepo basi msije mkaziuza kwa kingine ghairi ya hicho. Thamani yenu nyinyi ni Pepo tu. Kwa hivyo inabainika hapa kuwa walitaka kuzipa thamani zile kamasi na vicheuo; yaani walikuwa wakiitoa hii nafsi kwa ajili ya ile لماظه (vicheuo) yaani kuutoa ujudi huu, dhati hii na shakhsia hii; kilichofanyika hapa ni muamala, na kwa hivyo hadithi inakataza muamala huo. Yaani kama ni kufanya muamala, kwa nini mnazitoa nafsi zenu kwa ajili ya hii لماظه (kicheuo)? Zitoeni kwa ajili ya Pepo na kumwabudu Mwenyezi Mungu tu. Kwa hivyo nukta kuu ya msingi ni hii. Tab'an kuna nukta nyengine kuu ya msingi pia ambayo ni ile heshima ya utu ambayo inaonyeshwa na hii ibara ya فليس لأنفسكم ثمن الّا الجنّة Hazina nafsi zenu thamani ya kitu kingine ila Pepo; lakini hatutoingia kwenye mjadala huu kwa sasa.
Nukta nyengine ni kwamba katika kushikamana kwetu na marejeo ya Kiislamu - kama walivyoashiria baadhi ya majanabi, kwamba kuna marejeo chungu nzima ya Qur'ani na yasiyo ya Qur'ani na Hadithi; ambapo mimi nilipata wasaa na fursa ya kuyatafuta na kuyapata baadhi yao na kisha kuyasoma na kuyabainisha katika mfululizo wa hotuba za wakati ule za Ijumaa - tusitosheke kufuatilia suala moja tu la kuthibitisha kwamba mjadala juu ya Uhuru si hidaya ya Magharibi na tuzo tuliyozawadiwa sisi na Wazungu wa Ulaya. Kwa sababu baadhi ya wakati tunalitumia suala hili kusema kwamba ‘kwa nini bwana baadhi ya wenye kasumba za Magharibi wanasema kuwa masuala haya wametufunza Wazungu wa Ulaya; hapana, karne kadhaa kabla ya kuibuka mijadala hii huko Ulaya, shakhsia wakubwa wa Uislamu walikuwa wameshaizungumzia.' Vizuri sana, hii ni faida mojawapo; lakini suala zima sio hili tu. Sisi tunapaswa kurudi kwenye vyanzo na marejeo ili tuweze kupata kutoka kwenye majimui ya vyanzo hivyo ule mfumo uliopangika wa kifikra kuhusiana na Uhuru. Nukta nyengine ni kwamba sisi tunaweza kuuzungumzia Uhuru katika mitazamo minne: mmoja ni mtazamo wa haki, kulingana na istilahi ya Kiqur'ani na si istilahi ya fiqhi na sheria; na nitalieleza hili kwa muhtasari. Moja ya mtazamo wa haki ni wa istilahi ya fiqhi na sheria; haki, miliki na mtazamo wa haki kuhusiana na milki. Mtazamo mwengine ni wa wajibu. Mwengine pia ni mtazamo kwa uoni wa kitu cha thamani, cha mfumo wa kithamani. Kwa maoni yangu, muhimu zaidi ya yote hayo ni ule mtazamo wa kwanza ambao ni sisi kuuzungumzia Uhuru kwa mtazamo wa haki kulingana na istilahi ya Kiqur'ani. Haki katika istilahi ya Qur'ani - na nadhani neno "haki" limekaririwa zaidi ya mara mia mbili ndani ya Qur'ani; ni kitu cha kustaajabisha sana - ina maana pana na ya kina; lakini tunachoweza kueleza kwa muhtasari na kwa ufupi katika maneno mawili na kwa maana yake ya kijuujuu ni mfumo wenye nidhamu na lengo maalumu. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema katika aya kadhaa za Qur'ani ya kwamba: ulimwengu mzima wa viumbe umeumbwa kwa haki; مَا خَلَقْنَاهُمَا إِلاَّ بِالْحَقِّ Hatukuviumba hivyo ila kwa Haki (Addukhan: 44:39), وَخَلَقَ اللَّهُ السَّمَاوَاتِ وَالأَرْضَ بِالْحَقِّ Na Mwenyezi Mungu ameziumba mbingu na ardhi kwa haki (Al - Jaathiyah: 45:22); yaani mfumo huu wa ulimwengu wa viumbe na wa uumbaji - ikiwemo uumbwaji wa kimaumbile wa mwanadamu, ukiondoa suala la irada na hiyari ya ndani ya nafsi ya mtu - ni mfumo wa vitu vilivyotengenezwa na kuumbwa vikiwa na mfungamano, mshikamano na mahusiano ya pamoja baina yao na pia una nidhamu na lengo maalumu. Kisha baada ya hapo suala hili hili linabainishwa pia katika mfumo wa hukumu na sheria. Nimeashiria baadhi ya aya kuhusiana na mfumo wa uumbaji. Kuhusu mfumo wa hukumu na sheria Qur'ani inasema: نَزَّلَ الْكِتَابَ بِالْحَقِّ Ameteremsha Kitabu kwa haki (Al Baqara: 2:176), أَرْسَلْنَاكَ بِالْحَقِّ بَشِيرًا وَنَذِيرًا Tumekutuma kwa Haki uwe mbashiri, na mwonyaji. (Al Baqara: 2: 119), لَقَدْ جَاءَتْ رُسُلُ رَبِّنَا بِالْحَقِّ Hakika Mitume wa Mola wetu Mlezi walileta Haki. (Al A'raaf: 7:43). Haki hii ndio haki ileile; ni ile katika ulimwengu wa uumbaji, na ndiyo hii katika ulimwengu wa hukumu na sheria. Maana ya maneno haya ni kwamba kwa hekima ya Mwenyezi Mungu, ulimwengu wa hukumu na sheria unawiyana na kutangamana kwa asilimia mia moja na ulimwengu wa uumbaji. Irada ya mwanadamu inaweza kuharibu na kuvuruga baadhi ya sehemu za utangamano huo. Lakini kwa kuwa unawiyana na kutengamana na ulimwengu wa uumbaji, na kwa kuwa muelekeo wake ni muelekeo wa haki - yaani kile kinachopasa kuwepo kimekadiriwa kuwepo kwa hekima ya Mwenyezi Mungu - kwa hivyo mwishowe ile harakati kuu na ya muelekeo mkuu ndiyo inayoshinda na kutawala juu ya harakati zote hizi ndogo ndogo zinazohalifu, kukinzana na kukengeuka njia hii kuu; kwa hivyo ukinzani na ukengeukaji unaweza kufanyika. Huu ni ulimwengu wa uumbaji na huu ndio ulimwengu wa hukumu na sheria. Sasa moja ya vitu vya ulimwengu huu ni irada ya mwanadamu; moja ya vitu vya upangaji hukumu na sheria ni uhuru wa mwanadamu; kwa hivyo hii ni haki. Tuliangalie suala la Uhuru kwa mtazamo huu, kwamba Uhuru ni haki mkabala na batili. Mtazamo mwengine wa haki ni wa istilahi ya kisheria ambapo tumesema kwamba hii inampa mtu uwezo wa kudai na kutaka - yaani kuwa na sifa ya kumwezesha mtu kudai na kutaka kitu - lakini hii inatafautiana na lile suala la hiyari katika haki ya kuchagua katika mtazamo wa ‘Lazima na Hiyari'.
Jengine ni suala la jukumu, yaani tunapaswa kuuangalia Uhuru kwa mtazamo wa kuwa ni jukumu. Isiwe hivi, kwamba tuseme kuwa Uhuru ni kitu kizuri lakini mimi sikitaki kitu hiki kizuri. Hapana, haiwezekani hivyo, inapasa mtu aupiganie Uhuru; kwanza Uhuru wake mwenyewe na vilevile Uhuru wa watu wengine; asiruhusu mtu yeyote abakie katika hali ya kunyongeshwa, kudhalilishwa na kutawaliwa. Amirul Muuminin (alayhi ssalam) amesema:" لا تكن عبد غيرك و قد جعلك اللّه حرّا"Usiwe mtumwa wa mwengine na ilhali Mwenyezi Mungu amekufanya huru". Qur'ani nayo imesema:" مَا لَكُمْ لاَ تُقَاتِلُونَ فِي سَبِيلِ اللَّهِ وَالْمُسْتَضْعَفِينَ Mna nini msipigane katika Njia ya Mwenyezi Mungu na ya wale wanaoonewa (An - Nisaa: 4:75), yaani nyinyi mna wajibu wa kudhamini Uhuru wa wengine pia hata kama ni kwa vita; na hili lina mijadala yake mbalimbali.
Nukta ya nne ni mtazamo wa kithamani pia; na hili katika mfumo wa thamani za Kiislamu ni katika masuala ya daraja la kwanza; na tab'an ni ule uhuru tuliouzungumzia.
Katika sehemu ya mwisho ya mazungumzo yangu niseme kwamba ikiwa sisi tunataka kujadili suala la Uhuru, kulifanyia uhakiki na utafiti na kwenda mbele zaidi ya hapo mtazamo wetu kuhusiana na mitazamo ya Kimagharibi unapasa uweje? Hii ni nukta moja ya msingi. Hoja na maelezo mbalimbali waliyotoa majanabi na masiti, yote yameonyesha kuwa kuna ufa mkubwa kati ya mtazamo na uoni wa Uislamu na uoni na mtazamo wa Magharibi; na hilo ni sawa kabisa ndivyo ilivyo. Chanzo halisi cha hali hiyo - kama tulivyokwisha eleza - ni kwamba kipimo na kigezo cha Uhuru huko ni kumfanya mtu mhimili mkuu wa kila kitu, wakati hapa mhimili mkuu wa kila kitu ni Mwenyezi Mungu, kumwabudu Mwenyezi Mungu na tauhidi; hili liko palepale. Wakati sisi tunapoangalia nadharia na mitazamo ya Kimagharibi tutaona kuwa mitazamo hiyo haikuwa na mafanikio mazuri; huu ndio ukweli wa mambo. Wanafikra wao wote hawa wakubwa na wenye kutajika - Kant na wengineo - wamezungumzia suala la Uhuru na kulitolea maelezo mbalimbali; nini matokeo yake? Ni mahala gani katika ulimwengu wa Magharibi ambako kwa mtazamo wa matendo mwenendo wao unaafikiana na yale waliyoyasema na waliyoyataka wanafikra hao? Haiko ile mipaka waliyoizingatia na kuichunga. Kama tutaichukulia ile hali halisi tunayoishuhudia leo hii huko Magharibi kuwa ndiyo tafsiri halisi ya utekelezaji wa fikra zao basi wao walikuwa na hali mbaya sana; kwa sababu leo hali ya Magharibi kwa mtazamo wa Uhuru ni hali mbaya na ya kusikitisha mno; yaani haiwezi kutetewa kwa namna yoyote ile.
Leo huko Magharibi Uhuru wa kiuchumi uko katika ile hali waliyoiashiria majanabi hapa. Katika uga wa uchumi: kumiliki na kuhodhi fursa za kiuchumi kuko mikononi mwa watu wachache. Kama mtu ameweza kujifikisha kwenye klabu ya wenye uwezo wa kiuchumi kwa ujanja au kwa udanganyifu au kwa namna nyengineyo, kila kitu huwa milki yake yeye. Tab'an huko Marekani hawaangalii rekodi ya uashrafu wa mtu; kinyume na Ulaya na mila za Ulaya ambako kwa kiwango fulani walikuwa wakiyapa umuhimu masuala haya; huko nyuma ilikuwa sana na hivi sasa kwa kiwango kidogo. Huko Marekani hakuna masuala ya rekodi za kiashrafu, za kifamilia na za mambo kama hayo. Huko kila mtu - hata kama ni mpagazi, mchukuzi - kama ataweza kuitumia fursa atakayoipata walau mara moja na kuweza kufika kwenye ile nukta ya juu ya Ubepari, ataingia kwenye safu ya hao mabepari na ataweza kupata fursa na upendeleo wanaopata mabepari hao. Kwenye ile Hati waliyotayarisha Wamarekani, mmoja wa wakubwa, viongozi na waasisi wa Marekani ya leo - ambayo ni ya miaka mia mbili iliyopita na wala sikumbuki hivi sasa ni yupi kati yao; ilikuwa ni katika kipindi cha karibu sana na kabla ya kutokea Mapinduzi Makuu ya Ufaransa, ambapo matukio yale yalijiri na kuasisiwa utawala wa Marekani - anasema uendeshaji nchi lazima uwe mikononi mwa wale watu ambao utajiri wa nchi ya Marekani uko mikononi mwao wao. Hii ni kanuni kuu, na wala hawaionei aibu yoyote. Utajiri wa nchi uko mikononi mwa wachache hao, na ni wao ndio inapasa waendeshe na kuongoza nchi; ni kinyume kabisa na yale anayotaka kufanya ndugu yetu mpenzi hapa ya kuanzisha kwa njia ya muawana na watu wa Ushirika, ya wao pia kuwa na haki ya uongozi wa uendeshaji walau kwa kuwa na hisa moja. Kwa hivyo huu ndio Uhuru wao wa kiuchumi.
Kwa upande wa uga wa kisiasa pia mnauona huu mchezo wa ghasia za vyama viwili vilivyohodhi ulingo wa siasa, na bila ya shaka wale watu wenye mfungamano na vyama hivi, kiwango na idadi yao ni ndogo na ya chini mno ya asilimia moja. Kimsingi hasa vyama hivyo havina mtandao halisi na wa kweli wa kuenea hadi mashinani katika jamii; kwa kweli hizo ni klabu za kukusanya pamoja idadi fulani ya watu. Wale wanaojiunga nao hupiga kura, au hudanganyika na sha'ar zao au huathiriwa na udhibiti wa vyombo vya habari ambavyo vina utajiri na vimepiga hatua katika hali isiyo ya kawaida huko Magharibi; na hasa Marekani ambako kwa kweli umbali wa hatua iliyopiga kulinganisha na sisi ni ya baina ya mbingu na ardhi kwa upande wa uwezo walionao katika propaganda na kupindua ukweli halisi wa mambo - cheusi wanakionyesha kuwa cheupe na cheupe wanakionyesha kuwa cheusi - wamepata ufanisi na kupiga hatua isiyo ya kawaida katika nyanja hizi. Ni kwa kutumia njia hizi wanawateka na kuwavuta watu.
Katika uga wa masuala ya kiakhlaqi pia hili suala la watu wa jinsia moja wanaoingiliana kimwili ambalo huyu dada yetu mpenzi alikuja kulieleza; ni haya mambo ya ufuska yaliyopo. Bila ya shaka baadhi ya mambo yangali yameekewa mpaka. Lakini mtu anaweza kukisia kwamba baada ya muda si mrefu mipaka hiyo pia itaondoka; yaani kwa kuwepo ndoa za watu maharimu, zina na watu maharimu; kwa sababu kimantiki haipasi kuwepo marufuku yoyote juu ya masuala hayo. Kwa sababu kama tunachukulia kwamba hamu na utashi wa mtu ndio kipimo na ruhusa ya maingiliano ya kimwili ya watu wa jinsia moja na watu kuishi maisha ya pamoja bila kuoana, basi anaweza kutokezea mtu akawa na hamu mathalani ya kutaka kufanya uovu kama huu na maharimu wake; kuna sababu gani ya kuwepo marufuku? Yaani kimantiki hakuna sababu. Kwa hivyo kimantiki marufuku za haya pia zitaondoka, marufuku za mambo hayo pia zitaondolewa.
Kwa hivyo hali halisi ya jamii ya Magharibi ni mbaya, chungu, chafu na baadhi ya wakati ya kuchukiza na kukirihisha; si uadilifu uko huko si kitu kingine kiko huko; ubaguzi uko huko, uonevu na utumiaji mabavu uko huko; katika uga wa masuala ya kimataifa kuna ushupaliaji wa kuwasha moto wa vita. Ili viwanda vyao vya uundaji silaha viweze kupata fedha na ustawi wanachochea vita kati ya mataifa mawili kwa kutaka viwanda hivyo visije vikafilisika! Wanakuja kuzitia hofu nchi za Ghuba ya Uajemi juu ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ili waweze kuziuzia Fantom, waweze kuziuzia Mirage! Mambo haya yanafanyika kwa hali ya mtawalia.
Wanayafanyia miamala ya kibaguzi masuala ya thamani - suala kama haki za binadamu, suala kama utawala wa wananchi - wanayafanyia masuala hayo miamala mibaya sana na isiyo ya kiakhlaqi. Kwa hivyo hali ya mazingira halisi ya hivi sasa ya maisha huko Magharibi, Magharibi ambayo wanafalsafa wake walizungumza mambo chungu nzima kuhusu maudhui ya Uhuru, hali yake kwa kweli ni mbaya hasa.
Mtu kuziangalia na kuzihakiki nadharia hizi kisha akaamua kuzirudi na kuzipinga hiyo ni aina moja ya mtazamo. Mimi ninaitakidi kuwa mtazamo huo usiwe wa mutlaki. Ni sawa kabisa kwamba matukio haya kwa kiwango kikubwa yanaonyesha kuwa wanafikra hao, ambao walijiweka mbali na Mungu na wao wenyewe wakajihisi wana ukwasi wa kutohitajia mwongozo wa Mwenyezi Mungu na kuzitegemea nafsi zao wenyewe tu, walitumbukia kwenye upotofu; walizipotoa nafasi zao wenyewe na wakawapotosha na watu wao pia; wao wenyewe wakajielekeza kwenye jahanamu na watu wao pia wakawaelekeza kwenye jahanamu; hakuna shaka yoyote juu ya hili. Lakini mimi ninahisi kuwa kuzipitia na kuzitalii nadharia za wanafikra wa Magharibi pamoja na migongano yao ya kifikra, uzoefu wao mkongwe katika uga huu wa ubunifu wa fikra, ubunifu wa mfumo wa fikra uliopangika na uratibu na uunganishaji wa pamoja wa maudhui utakuwa na faida kwa wanafikra wetu kwa sharti moja; na sharti hilo ni kuacha kuiga na kufuata tu; kwa sababu kuiga kutupu kunapingana na Uhuru; isiwe ni kuiga tu; lakini aina ya kazi yao waliyofanya inaweza kukusaidieni.
Kuna mambo mengine ya kuzungumza ambayo nilikuwa nimeyaandika hapa, lakini muda umepita mno; na hasa kwangu mimi ambaye saa hizi kwa ilivyo nisiwe macho na kikawaida huwa siko macho. Lakini kuwepo kwa majanabi waheshimiwa na akina dada na ndugu wapenzi kunampa mtu uchangamfu kiasi cha kuurusha usingizi. Wanasema: "Utaweza kumfikia muhibu (Mwenyezi Mungu) wakati utakapouacha usingizi na kula". Usingizi kwa usiku wa leo umechelewa hivi, lakini katika dhifa ya ulaji tutakuwa pamoja na majanabi inshallah!
Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

 
< Nyuma   Mbele >

^