Skip to content

Habari

Habari
Hifadhi

Risala na Barua

Matini
Hifadhi

Kumbukumbu na Simulizi

Kabla ya Mapinduzi
Baada ya Mapinduzi

Sauti na Taswira

Picha
Sauti
Video
Ujumbe wa Nairuzi wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu wa Mwaka 1392 Hijria Shamsia Chapa
20/03/2013

بسم الله الرحمن الرحیم
یا مقلّب القلوب و الابصار، یا مدبّر اللّیل و النّهار، یا محوّل الحول و الاحوال، حوّل حالنا الی احسن الحال
Kwa jina la Allah Mwingi wa rehema Mwenye kurehemu
Ewe Mgeuzaji wa nyoyo na basari! Ewe Mpangiliaji wa Usiku na Mchana!
Ewe Mbadilishaji wa mwaka na hali! Badilisha hali zetu kuwa bora ya hali.

Ewe Mola wangu, mminie rehema kipenzi chako, Bibi bora kuliko wanawake wote ulimwenguni, Faatima binti Muhammad (rehema za Allah ziwe juu yake na Aali zake). Mola wangu mmiminie rehema yeye na baba yake na mumewe na wanawe. Mola wangu, kuwa; kwa ajili ya walii Wako na hujja Wako, mwana wa Hasan (Imam Mahdi AS), rehema ziwe juu yake na wazazi wake, katika saa hii na katika kila saa; (kuwa) Walii wake, na Mlinzi wake, na Kiongozi wake na Mwenye kumnusuru na Mwonyesha njia na jicho lake hadi utakapomfikisha kwenye ardhi Yako akiwa mtiifu kikamilifu Kwako na umneemeshe na umstareheshe humo milele. Ewe Mwenyezi Mungu nakuomba umpe katika nafsi yake mambo yanayotuliza jicho na kufurahisha nafsi, na kizazi chake, na wafuasi wake, na watu anaowaongoza, na watu wake maalumu, na watu wake wote kiujumla na adui yake na binaadamu wote.
Ninatoa mkono wa baraka na fanaka kwa mnasaba wa kuwadia sikukuu ya Nairuzi na kwa kuanza mwaka mpya. Mkono wangu wa baraka uwaendee wananchi wenzangu wote azizi nchini, na Wairani wote walioko katika kila kona ya dunia na kwa mataifa yote yanayoadhimisha sikukuu ya Nairuzi. Mkono wangu wa baraka hasa hasa nautuma kwa familia azizi za mashahidi, majeruhi wa vita, aila zao, watu wote wanaojitolea katika njia ya haki, na watu wote wanaofanya kazi kwa bidii na idili kubwa katika nyuga tofauti. Ninamuomba Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa matumaini makubwa, aujaalie mwanzo huu wa mwaka (na siku ya leo) kuwa siku iliyojaa furaha, nishati na ustawi kwa taifa la Iran na Waislamu wote duniani na atuwafikishe na atupe nguvu za kutekeleza vilivyo majukumu yetu. Ninapenda kuwaeleza wananchi wenzangu kuwa wakumbuke na wazingatie kwamba siku za "Fatimiyyah" ziko katikati ya siku za sikukuu ya Nairuzi na ni wajibu kwetu sisi sote kuzitukuza na kuzipa heshima yake siku hizo.
Saa ya kubadilika mwaka na zile sekunde za kuingia mwaka mpya; hicho kwa hakika huwa ni kipindi cha baina ya mwisho wa kitu na mwanzo wa kitu kingine; ni kipindi cha kumalizika mwaka uliopita na kuanza mwaka mpya, tab'an jicho letu zaidi linapaswa kukita upande wa mbele, yaani upande wa mwaka mpya, na tujiandae kwa ajili ya mwaka huo, tuuwekee mipango inayotakiwa lakini tujue pia kuwa, kuangalia nyuma na kuona njia tuliyoipita pia kuna faida kwetu, kwani kufanya hivyo kutatuwezesha kuona tulichokifanya hadi hivi sasa na vipi tuendelee na safari na tutaona matunda ya kazi zetu za huko nyuma na kwa njia hiyo tutaweza kupata funzo, uzoefu na tajiriba kutokana na matukio yaliyopita.
Mwaka wa 1391 ((Hijria Shamsia) kama ilivyokuwa miaka mingine ya kabla yake, ulikuwa ni mwaka wenye vitu vingi, ulikuwa na rangi tofauti na ramani mbali mbali, ulikuwa na mambo matamu kama ambavyo pia ulikuwa na mambo machungu. Ulikuwa na ushindi kama ulivyokuwa pia na kudorora na kubaki nyuma na hivi ndivyo yalivyo maisha ya wanadamu katika kipindi chote cha maisha yao. Shida na raha siku zote zinakuwepo katika maisha yaliyojaa kupanda na kushuka ya mwanadamu. Kilicho muhimu ni kuhakikisha tunajiondoa mabondeni na chini milimani na kujiweka juu vileleni.
Kitu tulichoshuhudia katika kipindi kizima cha mwaka uliopita wa 1391 katika upande wa mapambano yetu na ulimwengu wa kiistikbari na kibeberu ni kuongezeka kwa mashinikizo ya maadui dhidi ya taifa la Iran na dhidi ya mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu. Tab'an kijuu juu na katika dhahiri ya jambo hilo yaliyonekana mashinikizo ya adui lakini utaona kwamba katika batini yake, jambo hilo lilikuwa ni fursa ya kuzidi kupata uzoefu na kuimarika taifa la Iran na kuzidi kupata ushindi taifa hilo katika medani tofauti. Kitu ambacho maadui wetu walifanya shabaha yao kilikuwa ni kulilenga taifa letu katika nyuga na nyanja tofauti na zaidi kutufanyia uadui katika uwanja wa kiuchumi na kisiasa. Katika upande wa uchumi walisema waziwazi na bila ya kificho kuwa, wana nia ya kulifanya kilema taifa la Iran kupitia vikwazo vyao lakini wameshindwa kulifanya taifa la Iran kuwa kilema, bali sisi tumepata mafanikio makubwa katika medani tofauti za kiuchumi kwa taufiki na msaada wa Mwenyezi Mungu Mtukufu. Ufafanuzi wa jambo hilo wataelezwa wananchi wetu azizi na mimi katika hotuba yangu ya tarehe Mosi Farvardin (siku ya mwanzo ya mwaka mwa Kiirani wa Hijria Shamsia) kwa majaaliwa ya Mwenyezi Mungu nitalitolea ufafanuzi jumla suala hilo.
Tab'an wananchi walipata mashinikizo katika upande wa maisha, na matatizo ya kiuchumi yalikuwepo (katika mwaka ulioisha) hasa kwa vile tatizo lilikuwa pia linatokea ndani ya nchi, kuna baadhi ya uzembe na kutowajibika kulishuhudiwa humu nchini na hivyo kusaidia njama za maadui, lakini kiujumla ni kuwa, harakati jumla ya mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu na harakati jumla ya wananchi, ilikuwa ni harakati ya kupiga hatua mbele na Inshaallah matunda mazuri ya uimara na uzoefu huo yataonekana katika siku za usoni.
Katika upande wa kisiasa, hima kuu ya maadui ilikuwa ni kulifanya taifa la Iran litengwe duniani na katika upande mwingine kuwafanya wananchi wa Iran wachanganyikiwe na wasijue la kufanya na kudhoofisha nguvu na hima yao ya kujiletea maendeleo. Lakini matokeo yake yamekuwa kinyume na matarajio ya maadui, naam, kwa hakika hali imekuwa kinyume kabisa na walivyotarajia. Katika suala la kutaka taifa la Iran litengwe kimataifa, si tu maadui wameshindwa kupunguza siasa zetu za kimataifa na kieneo, lakini hata kuna baadhi ya mambo kama vile Kikao cha Harakati ya Nchi Zizisofungamana na Siasa za Upande Wowote NAM kilifanyika mjini Tehran mwaka jana na kuhudhuriwa na idadi kubwa ya viongozi na wakuu wa nchi nyingi duniani kiasi kwamba kikao hicho kilivunja rekodi, tofauti kabisa na walivyotaka maadui wetu. Kikao hicho kilithibitisha (kivitendo) kuwa Jamhuri ya Kiislamu si tu haijatengwa, lakini pia dunia inaiangalia kwa jicho la heshima na mapenzi Jamhuri ya Kiislamu na Iran ya Kiislamu na taifa letu azizi.
Katika upande wa masuala ya ndani ya nchi, wananchi wetu azizi kadiri walivyopata fursa ya kuonyesha hisia zao - hususan tarehe 22 Bahman 1391 (siku zilipofikia kileleni sherehe za Mapinduzi ya Kiislamu ya nchini Iran) walitumia vizuri fursa hiyo kuonesha hamasa na hisia zao na walijitokeza katika medani kwa hamasa kubwa zaidi na kwa wingi mkubwa zaidi kuliko miaka iliyotangulia. Mfano mwingine wa wazi ni jinsi wananchi wa Khorasan Kaskazini walivyojitokeza (kwa wingi mno kumpokea Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika safari yake ya kuutembelea mkoa huo) tena katika ule wakati wa ambapo vikwazo (vya maadui dhidi ya taifa la Iran) vilikuwa vimeshamiri, na huo uolikuwa ni mfano mwingine wa hali ya mapenzi ya moyoni ya wananchi wa Iran kwa mfumo wao wa Kiislamu na kwa viongozi wao wanaolitumikia taifa. Alhamdulillah kazi nyingine nyingi kubwa zilifanyika katika kipindi chote cha mwaka huo; kulifanyika jitihada kubwa za kielimu, kazi za ujenzi, harakati nyingi za viongozi na wananchi, kuliandaliwa nyanja pana za kupiga hatua za maendeleo na Inshaallah mazingira ya mabadiliko makubwa yameshaandaliwa iwe ni katika upande wa kiuchumi na pia katika upande wa kisiasa na katika nyuga nyingine zote za maisha.
Kutokana na mipango ya maendeleo yenye kutia matumaini ambayo kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu na kwa hima ya wananchi Waislamu wa Iran tumeandaliwa hivi sasa, mwaka huu wa 1392 utakuwa mwaka wa maendeleo, mwaka wa harakati na kuzidi kuwa imara taifa la Iran, tab'an si kwa maana ya kuwa uadui wa maadui utapungua, bali kwa maana ya kwamba, utayari wa taifa la Iran utakuwa mkubwa zaidi na uwepo wake utakuwa na taathira kubwa zaidi na ujenzi wa mustakbali wa taifa hili - kwa mikono yake yenyewe na kwa hima na kujitosheleza lenyewe - utakuwa mkubwa na bora zaidi Inshaallah.
Tab'an kitu ambacho tunakitabiri sisi katika mwaka huu wa 1392 (Hijria Shamsia) ni kuweko jukumu kubwa ambalo zaidi litakuwa katika uwanja muhimu wa kiuchumi na kisiasa. Katika upande wa kiuchumi, inabidi suala la uzalishaji wa ndani na uzalishaji wa taifa lipewe umuhimu mkubwa kama ilivyokuwa kaulimbiu ya mwaka uliopita. Tab'an kazi zimeanza kufanyika katika suala hilo, lakini kueneza fikra na utamaduini wa "Uzalishaji wa Taifa, Kuunga Mkono Kazi na Rasilimali za Iran" ni suala linalohitajia muda na miaka mingi kufanikishwa, na si jambo la kuweza kufanikishwa katika kipindi cha mwaka mmoja. Kwa bahati nzuri, katika nusu ya pili ya mwaka 91 (Hijria Shamsia), kulipitishwa siasa za uzalishaji wa taifa na kukabidhiwa kwa wahusika - yaani reli ya safari za treni ya kazi hiyo tayari imeshawekwa - na sasa (vyombo viwili vikuu) Bunge na Serikali vinaweza kuweka mipango ya kuanzisha safari vizuri na Inshaallah jambo hilo litafanyika kwa hima ya hali ya juu na uchapaji kazi usiojua kuchoka.
Katika upande wa kazi za kisiasa pia, kazi kubwa tuliyo nayo mbele yetu mwaka huu wa 1392 ni uchaguzi wa Rais ambao kwa hakika unapanga na kukadiria kazi za utekelezaji na za kisiasa na kwa ufupi kazi zote za umma nchini kwa ajili ya miaka minne inayokuja. Inshaallah kushiriki kwa wingi wananchi katika medani hiyo, kwa kweli kutaweza kutoa bishara ya mustakbali mwema kwao wao wananchi na kwa nchi nzima. Tab'an ni jambo la lazima kwa wananchi kushiriki kijihadi katika masuala ya kiuchumi na katika uwanja wa kisiasa. Inabidi kuingia katika medani hizo kwa hamasa na shauku kubwa, kwa hima ya hali ya juu na kwa mtazamo wa matumaini na kwa moyo uliojaa rajua na matarajio mema na uliojaa hamasa na shauku kubwa. Ni kwa kuwa na sifa hizo ndipo tutaweza kufikia malengo yetu.
Aidha ni kwa kuzingatia yote hayo ndio maana mwaka huu wa 1392 tunaupa jina la "Mwaka wa Hamasa ya Kisiasa na Hamasa ya Kiuchumi," na tunataraji kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu, kutashuhudiwa hamasa ya kiuchumi na hamasa ya kisaisa katika mwaka huu kutoka kwa wananchi wetu azizi na kwa viongozi wenye uchungu na nchi.
Tunamuomba Mwenyezi Mungu azidi kutuangalia kwa jicho la rehema na tunataraji dua ya Baqiyyatullah (Imam Mahdi - Arwahuna Fadaahu) itatujumuisha na sisi na tunamuomba Mwenyezi Mungu aipandishe daraja za juu roho toharifu ya Imam wetu mtukufu na mashahidi wetu azizi.
Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

 
< Nyuma   Mbele >

^