Skip to content

Habari

Habari
Hifadhi

Risala na Barua

Matini
Hifadhi

Kumbukumbu na Simulizi

Kabla ya Mapinduzi
Baada ya Mapinduzi

Sauti na Taswira

Picha
Sauti
Video
Hotuba ya Kiongozi Muadhamu Mbele ya Tume ya Maandalizi ya Kongamano la Kumuenzi Mirza Kuchak Chapa
19/11/2012

Ifuatayo ni hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika mkutano na wajumbe wa tume ya maandalizi ya kongamano la kumuenzi Mirza Kuchak Khan Jangali

 Bismillahir Rahamnir Rahim

Kadhia ya marehemu Mirza Kuchak Jangali ni kadhia ya aina yake; japokuwa katika kipindi kile maalumu - yaani kipindi cha baina ya zama za Mapinduzi ya Katiba na kuja madarakani Reza Khan - yalitokea matukio mbalimbali nchini, na wakati mmoja na Harakati ya Msitu yalijiri matukio mengine kadhaa pia katika pembe hii au ile ya nchi - kama lile lililoongozwa na marehemu Sheikh Muhammad Kheyabani kule Tabriz, au lile lililoongozwa na kanali Muhammad Taqi Khan Pasyan kule Mashhad - na yote hayo yalijiri takribani katika wakati mmoja, lakini kadhia ya Msitu ni kadhia ya kipekee. Sote tunazijua vizuri kadhia za matukio ya Tabrizi na kujitokeza kwa marehemu Sheikh Muhammad Kheyabani na wengineo; hayo yameandikwa katika maandishi ya historia na pia tunajua mambo mengi na masuala ya ndani kuhusiana na matukio hayo, lakini ile hali ya kupendwa na watu na usafi iliyonayo harakati ya marehemu Mirza Kuchak Khan Jangali haifanani na yoyote kati ya hizi harakati mbili tatu nyengine ambazo zilitokea katika kila pembe ya Iran wakati mmoja katika zama zile. Mirza Kuchak - kama mlivyoashiria - ni shekhe na mwanafunzi wa chuo cha kidini. Tab'an mimi niliwahi kusikia, na hili tulisimuliwa miaka mingi nyuma kwamba yeye alimwahi marehemu Mirza Shirazi, lakini hili si la kuaminika sana. Habari hii alisimuliwa marehemu baba yangu na marehemu janabi Sayyid Ali Akbar Mar'ashi - ambaye alikuwa mume wa dada wa baba yetu aliyekuwa ameoa nyumba moja na marehemu Sheikh Muhammad Kheyabani - ambaye alikuwa mmoja wa maulamaa wakubwa na aliyetengwa mjini Tehran; yeye alisema kwamba Mirza Kuchak aliwahi kuhudhuria darsa za marehemu Mirza Shirazi; amma kuhusu yeye (Mirza Kuchak) kuwa mwanafunzi wa kidini na kwamba alikuwa shekhe hili halina shaka yoyote; katika hawza (chuo cha kidini) yenyewe ya Rasht atakuwa aliweza kunufaika na elimu ya maulamaa wakubwa wa zama zile, na hakuna shaka yoyote juu ya hili. Kwa hivyo chimbuko la harakati ya Mirza Kuchak Khan kwa asilimia mia moja ni chimbuko la kidini na la kiitikadi.

Mwenendo wake pia ni mwenendo wa kidini na wa kiitikadi, yaani mtu anashuhudia kuwa japokuwa alikuwa na wapinzani ndani ya harakati yake, na baadhi ya matabaka tofauti ya watu wenye kutajika pia walikuwa wakimpinga, lakini katika kuamiliana na watu hao, marehemu Mirza Kuchak alikuwa akizingatia kikamilifu mipaka ya sharia za dini na hakuwa mtu wa kukwaruzana na watu wake wa ndani. Kwa mfano walikuwepo watu ambao walikuwa wakipingana naye kiitikadi; wale waliokuwa pamoja naye - yaani wenye misimamo ya kufurutu mpaka - walikuwa wakisema, tuwapige hawa tuwakandamize! Lakini Mirza Kuchak hakuwaruhusu, alikataza na kuwazuia watu hao kufanya hivyo; yaani mwenendo wake pia ulikuwa mwenendo wa kidini.
Nayo harakati, ilikuwa kwa asilimia mia moja harakati ya Kiislamu na ya Kiirani. Wakati ule - kama mnavyojua - makelele ya harakati ya Kimaksi na ya kuundwa kwa Urusi yalikuwa yamepamba moto duniani, na kwa sababu ya mvuto iliotoa kwa baadhi ya mataifa, bila ya shaka iliwateka pia baadhi ya watu na waliokuwa wamemzunguka (Mirza Kuchak) ambao walimsaliti kwa njia hiyo; lakini kutokana na kushikamana kwake na Uislamu mtu huyo hakuvutwa na kutekwa na nadharia ya Kimaksi; bali aliipinga vikali na waziwazi nadharia hiyo - japokuwa baadhi ya watu wake wa karibu waliokuwa pamoja naye tangu mwanzo walifuata mielekeo hiyo; na tab'an watu hao waliondoka duniani wakiwa wameharibikiwa, kwani hakuna yeyote kati yao aliyepata heri yoyote katika maisha haya wala kushuhudia heri wala mlahaka wowote wa kiungwana katika harakati ile ya Kibolsheviki - na alikuwa mpinzani pia kwanza wa ajnabi; yaani kwa kuwa siasa hizo zilikuwa zinatokana na wageni, hata kama wageni hao walikuwa wakikabiliana na vyombo vilivyokuwa vikitawala kama Waingereza na Warusi wa Kiqazaqi na mfano wa hao, lakini hakuvutiwa na mrengo huo; yaani aliendelea kuwa na msimamo wa kujitegemea. Mirza Kuchak Khan ni kigezo na mfano mkubwa sana wa aina yake; inshallah Mwenyezi Mungu amuinue daraja yake.
Kazi yenu pia, kutokana na haya malengo mliyoyataja na muundo mliouelezea, ni kazi nzuri sana. Bila ya shaka vitabu vingi vimeandikwa kuhusu Mirza Kuchak. Kinyume na watu wengine ambao walijitosa kwenye hizi njia za mapambano na harakati mfano wa hizo na kutegemewa majina yao yatajwe midomoni mwa watu na kujulikana na watu wote, katika hali ambayo wengi wa watu hawa niliowaashiria watu hawawajui asilani na baadhi yao hata majina yao hawajawahi kuyasikia, bahati nzuri ikhlasi ya mtu huyu imekuwa sababu ya yeye kujulikana na watu na kuandikwa vitabu pia kumzungumzia yeye. Juhudi zifanyike za kufanya kazi iliyokamilika na yenye nukta kuu za msingi kuhusu maisha yake ili inshallah shakhsia yake izidi kufahamika na watu wetu na vijana wetu.
Yeye alianzisha sampuli ya Mfumo wa Kiislamu na Jamhuri ya Kiislamu kule Rasht na katika mipaka maalumu ya eneo alilokuwepo la Gilani. Ninatoa shukurani zangu kwenu nyinyi mnaoifanya kazi hii na ninawataka wahusika serikalini na viongozi wa masuala ya tablighi na uenezi na mfano wao washirikiane na nyinyi na kutoa msaada ili kazi hii ikamilike kwa ufanisi bora inshallah.
Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

 
< Nyuma   Mbele >

^