Skip to content

Habari

Habari
Hifadhi

Risala na Barua

Matini
Hifadhi

Kumbukumbu na Simulizi

Kabla ya Mapinduzi
Baada ya Mapinduzi

Sauti na Taswira

Picha
Sauti
Video
Hotuba ya Kiongozi Muadhamu Mbele ya Mabasiji na Wanaharakati wa Mpango wa Salihina Chapa
21/11/2012
Ifuatayo ni hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika mkutano na Mabasiji na wanaharakati wa mpango wa "Salihina", mwezi 6 Muharram 1434 Hijria.
Bismillahir Rahmanir Rahim
Tunamshukuru Mwenyezi Mungu kutokana na kujitokeza katika zama zetu mfano hai wa yale yaliyoshuhudiwa katika tukio kubwa la Ashura na yaliyosimuliwa kwetu; ni ya wanaume, wanawake na vijana ambao fikra zao zililenga kwenye lengo kuu na ambao walisamehe roho zao, mali zao na kila kitu cha maisha yao. Mfano huu tumeuona sisi kwa macho yetu katika kipindi cha Kujihami Kutakatifu na muendelezo wake pamoja na baraka zake tunaendelea kuushuhudia hii leo. Kusadifiana masiku haya na tukio adhimu la Ashura kunatupa funzo maalumu. Haifai hata kidogo kwa umma wa Kiislamu na jamii ya Kiislamu kujiweka mbali na tukio la Ashura, ambalo ni somo, ibra na bendera ya uongofu. Hakuna shaka yoyote kuwa Uislamu umebaki hai kutokana na Ashura na kutokana na Hussain Ibn Ali (alayhis salam). Kama alivyosema (Mtume) : وَ أَنَا مِنْ حُسَيْنٍ Na mimi ninatokana na Hussain; kwa mujibu wa maneno haya ni kwamba dini yangu, uendelezaji wa njia yangu utafanywa na Hussain (alayhis salam). Kama lisingekuwa tukio la Ashura, kama kujitolea mhanga huku kwenye adhama kusingefanyika katika historia ya Uislamu, umma wa Kiislamu usingepata tajiriba hii na somo hili la kivitendo, na bila ya shaka yoyote Uislamu ungepotoshwa kama zilivyopotoshwa dini za kabla ya Uislamu na kisingebakia chochote katika hakika ya Uislamu na nuru ya Uislamu. Adhama ya Ashura inatokana na jambo hili. Bila ya shaka msiba uliotokea siku ya Ashura ni mzito, hasara na maafa yake ni makubwa, kwani roho ya mtu kama Hussain Ibn Ali (alayhis salam) ni yenye thamani ya mbingu zote na ardhi; roho safi, njema na toharifu za masahaba wale, vijana wale na Ahlul Bayt haziwezi kulinganishwa na roho ya mtu mwengine yoyote; lakini watu hao walighariki kwenye dimbwi la damu, walijitolea mhanga, wakawa mhanga; watu azizi wa nyumba ya Mtume na Amirul Muuminin wakafanywa mateka; haya ni matukio mazito mno, machungu mno na magumu mno, lakini yale yaliyopatikana kwa kuvumilia matukio haya machungu na magumu ni makubwa, ni yenye adhama na ya kudumu kwa kadiri ya kuifanya iwe wepesi kwa mtu kama Hussain Ibn Ali (alayhis salam), masahaba zake na watu wa familia yake kuyavumilia matukio hayo magumu. Haya wameyapokea watu wakubwa; marehemu Al Haj Mirza Jawad Agha Maleki (ridhwanullah alayhi) anasisitiza katika kitabu cha Muraqibat - na maneno yake ni ushahidi na hoja - ya kwamba katika Siku ya Ashura kadiri masaibu yalivyozidi kuwa makubwa ndivyo uso wa Hussain Ibn Ali (alayhis salam) ulivyozidi kung'ara na athari za unawirifu zikawa zinazidi kudhihirika katika shakhsia ya mtukufu huyo. Hizi ni hakika zenye maana ya kina na zenye siri kubwa ambazo zinapasa ziendelee daima kuwa mbele ya macho yetu.
Katika zama zetu imeonekana mifano mbalimbali ya kujitolea huku mhanga, yale tuliyoyasoma katika historia, baadhi yao, baadhi ya mifano yao, ambao muhimu zaidi na dhihrisho kubwa zaidi kati yao ni huu mti mwema (shajaratun tayyibah) wa Basiji, ambao tumeuona mbele ya macho yetu kabla ya kuanza Vita vya Kulazimishwa, na pia wakati wa Vita vya Kulazimishwa hadi hii leo na ambayo ni tajiriba ngumu mno na nzito mno kwa nchi. Suala la Basiji, tajiriba ya Basiji imekuwa na baraka kubwa sana na inshallah baraka hizi lazima ziendelezwe na zitazidi kuendelezwa.
Nukta moja iliyopo ni kwamba katika kipindi cha Kujihami Kutakatifu yale yaliyokuwa yakionekana katika harakati ya Basiji, ya kipimo cha ikhlasi yalikuwa ya kiwango cha juu, na hili ni jambo tunalopaswa kuhakikisha linaendelea kuwepo leo hii katika harakati ya Basiji. Medani ya leo ni medani tata zaidi. Kwenda kwenye uwanja wa vita, mapigano na mapambano na kubeba jukumu la wadhifa fulani, kisha kufikia daraja ya kufa shahidi, au kuwa majeruhi wa vita au kurudi salama kutoka vitani ni mambo hatari kujitosa kwenye medani hizo, lakini hazina hali ya utata. Lakini kujitokeza kwenye medani hii leo ili kukabiliana na njama za adui, shambulio la adui na kukabiliana kwa safu mbili hizi na kambi mbili hizi kuu kuna utata mwingi; inawezekana zile hatari za moja kwa moja za wakati ule zisiwepo hii leo lakini utata wake ni mwingi zaidi. Kilichoshinda katika medani ile ni kwamba mtu aliyekuwa akienda huko alikuwa akionyesha waziwazi ikhlasi aliyokuwa nayo. Kujitosa kwenye medani ile, kulikuwa ni kuingia kwenye medani ya kufa na kupona; halikuwa jambo la mzaha: lilihitaji kuwa na ujasiri, lilihitaji mtu kuwa tayari kujitoa mhanga, lilihitaji imani na lilihitaji pia kutawakali kwa Mwenyezi Mungu; na watu wakienda huko na kufa shahidi. Leo katika medani mbalimbali inahitajika imani ileile na ujasiri uleule, lakini hata bila ya kuwa na sifa hizi inawezekana pia wakawepo watu watakaojitokeza katika vazi la Basiji; inapasa mlihadhari jambo hili. Tujichunge sisi wenyewe kwanza na baada ya hapo tuichunge anga ya Basiji; hii ni kazi ya mabasiji wote. Kiwango cha usafi wa moyo wa basiji ndani ya majimui ya Basiji, ikiwemo ndani ya majimui hii ya "Salihina" ambayo uongozi wake uko mikononi mwenu nyinyi na ndio mnaoiongoza kinapasa kipandishwe; tuhakikishe kunakuwepo moyo wa ikhlasi, na hili mhakikishe linakuwepo ndani ya majimui ya utendaji kazi. Hili ni gumu kwa kiwango fulani. Sababu moja ni kwamba jihadi katika medani ya kupambana na nafsi na masuala ya kimaanawi imepewa jina la "jihadi kubwa", na hili ndilo linaloifanya kazi hii iwe ngumu zaidi. Katika vita na adui - vita vya kijeshi - mtu anaweza kupima kirahisi kiwango cha ikhlasi yake na kiwango cha ikhlasi za watu wengine; huwa ni rahisi zaidi kuzipima, lakini hapa si hivyo; hapa mtu mwenyewe huweza kuteleza akafanya makosa na pia watu wengine hufanya makosa katika kumfahamu mtu.
Nukta nyengine ni kwamba tujitahidi sisi wenyewe kujiepusha na maradhi ya kinafsi. Maradhi ya ghururi, maradhi ya ria na kufanya mambo kwa kujionyesha ni maradhi yenye kuangamiza. Kama tutapata mafanikio tumshukuru Mwenyezi Mungu, tujue kuwa yametokana na Mwenyezi Mungu na tuombe msaada kwake ili mafanikio hayo yaendelee kupatikana; na hili ni suala la msingi kwamba tusije tukaingiwa na ghururi, tusije tukawa na hali ya kujiamini kupindukia, tusihisi kuwa kila kitu kinatokana na sisi wenyewe na tutawakali na kumtegemea Mwenyezi Mungu. Ukweli wa mambo hasa ndio huu; hakuna uwezo wala nguvu yoyote ghairi ya zile zilizoko kwenye mamlaka ya Muumba Dhuljalal; kila kitu kinatokana na Yeye; taufiki tunayopata, chaguo tunalofanya, uwezo tulionao, shauku tuliyonayo, imani na mapenzi yaliyomo ndani ya nyoyo zetu, yote hayo yanapatikana kutokana na Mola Muumba. Tulijue hili, tuwe washukurivu na tuombe tuzidishiwe na Yeye Mwenyezi Mungu Mtukufu. Kwa hivyo na hili pia ni suala jengine.
Nukta moja ya msingi ambayo kwa bahati nzuri nimeona imezingatiwa na waheshimiwa waliozungumza hapa ni kuzingatiwa ubora na umakini wa kina katika kazi za majimui zinazounda jengo la Basiji na misingi mikuu ya Basiji. Mambo yanayosababisha madhara na kupata pigo lenye madhara ni kuwa na uoni wa kijuujuu katika itikadi, ufahamu na uchaguzi wa mantiki na misingi ya mambo. Uoni wa kijuujuu unasababisha madhara; ni sawa na kifurushi cha mzigo wa ziada kinachowekwa juu ya majimui ya mizigo lakini kinapopigwa na upepo mkali au mtingisiko mkubwa huanguka. Lazima ufanyaji mambo uwe wa umakini wa kina, lazima misingi ya itikadi ikite mizizi; haya ni mambo ambayo Alhamdulillah mnayazingatia. Asili ya kuundwa majimui za "Salihina" ilitokana na mtazamo huu wa kuijenga kwa kina fikra na moyo wa vijana wetu wa Basiji katika vitengo mbalimbali kwa upande wa kimaanawi, kwa upande wa maandalizi na kwa upande wa mafunzo.
Tunapoiangalia majmui yenyewe tunabaini kuwa kuwepo kwa Basiji ni moja ya miujiza ya Mapinduzi. Ubunifu huu wa Imam wetu muadhamu (Khomeini), unaonyesha uelewa wake, hekima yake na mfungamano wa moyo wake wenye nuru, na irada na hekima ya Mwenyezi Mungu. Kwa hivyo Basiji ikawa moja ya nguzo imara kwa Mapinduzi. Leo Basiji iko amilifu na inachapa kazi mno katika uga wa elimu, katika uga wa tajiriba, katika uga wa teknolojia, katika nyanja za kimaanawi, katika uga wa huduma za jamii, katika ubunifu wa nadharia katika pande tofauti za maisha ya kijamii, katika uga wa masomo na katika uga wa malezi na maandalizi. Kama kuna siku itatokea tajiriba yoyote na wananchi wakalazimika kubeba silaha na kujihami kijeshi ili kukabiliana na adui, ni majimui hiihii ya vijana, ni Basiji hiihii na ni vijana hawa hawa mashujaa wa taifa letu azizi ndio watakaomuonyesha adui ujasiri wa taifa la Iran, ungangari wa taifa la Iran, nguvu za taifa la Iran na kutoshindika kwa taifa la Iran. Majimui nyenginezo na nchi nyenginezo pia ambazo zimetaka kupiga hatua au zimeshapiga hatua katika njia hii ing'arayo ya Uislamu, zitafuata tajiriba na uzoefu huu. Tajiriba hii ni tajiriba iliyofanikiwa. Sisi tunapaswa kuonyesha utendaji mzuri. Muongozo huu wa kivitendo wa Basiji utathibiti kuwa mfano hai katika Ulimwengu wa Kiislamu wa muongozo wa kivitendo unaoweza kuigwa na kufuatwa na nchi za Kiislamu na mataifa ya Kiislamu, na leo hii hali hii imetokea na imejiri kwa kiwango kikubwa. Kwa hivyo kuimarisha Basiji, kuwafanya mabasiji watu wenye ikhlasi zaidi na wenye umaanawi zaidi na kupanua harakati za Basiji katika nyanja zote za maisha ni miongoni mwa kazi za msingi zinazopasa kufuatiliwa na majimui ya watendaji katika Basiji, watu wenye mafungamano na Basiji na wanaharakati waliomo ndani ya Basiji.
Kuanza kufanya mambo kwa kujiangalia mtu mwenyewe kwanza ni miongoni mwa maamrisho tuliyopewa na Uislamu; sisi sote na katika ngazi zote tunapaswa kuanza kwanza kujangalia sisi wenyewe. مَنْ نَصَبَ نَفْسَهُ لِلنَّاسِ إِمَاماً فَلْيَبْدَأْ بِتَعْلِيمِ نَفْسِهِ قَبْلَ تَعْلِيمِ غَيْرِهِ Anayeifanya nafsi yake kiongozi kwa watu aanze kwanza kuifunza nafsi yake kabla ya kuwafunza wengine. Hivi ndivyo ilivyo katika ngazi zote. Tunapaswa tuanzie kwenye nafsi zetu sisi wenyewe; tulianzishe suala hili ndani ya Basiji.
Huu mtindo wa maisha na utaratibu wa maisha kulingana na mtazamo wa Uislamu unaweza kufanywa ndani ya Basiji kuwa kipimo cha mtu kujitambua nafsi yake. Suala si kwamba vyombo vikuu na vya juu zaidi vije kutupima viwango vyetu na kuelewa vikoje, suala ni kwamba sisi wenyewe tufanye kazi ya kujipima viwango vyetu. Mwenendo wetu katika sehemu ya kazi ukoje? Mwenendo wetu kwa wake zetu na watoto wetu ukoje? Mwenendo wetu katika mazingira ya kimaisha na mazingira ya kijamii ukoje? Mwenendo wetu na walio chini yetu ukoje? Tabia zetu zikoje tunapoamiliana na mtu wa juu yetu? Mwenendo wetu na rafiki ukoje? Na adui pia ukoje? Haya yote ni mambo yenye vipimo na vigezo katika Uislamu. Tujipime sisi wenyewe. Hiki kitakuwa kipimo cha kupima ubora wetu sisi wenyewe na kujielewa barabara sisi wenyewe. Kama tutaanzia hapa, msingi wa maisha yetu na msingi wa kazi zetu katika sehemu zote na hasa ndani ya Basiji, ambayo ndiyo tunayoizungumzia hivi sasa, utakuwa imara.
Alaa kulli hal nchi yetu, taifa letu, Mapinduzi yetu na historia yetu inahitajia Basiji, na Basiji inahitaji kujiimarisha zaidi kwa ubora siku baada ya siku na kazi hii mnayoifanya nyinyi akina kaka na akina dada wapenzi ni sehemu ya suala linalohusiana na "Salihina", na hizi silisili za "Salihina" ni miongoni mwa kazi nzuri sana na inshallah izidi kukamilika zaidi kupitia mpango huu wa ukamilishaji wa Basiji. Viwango vya ubora vipandishwe juu; bila ya shaka ubora unafadhilishwa kuliko wingi, lakini wingi wenye ubora una umuhimu pia; yaani kuongeza kiwango cha wingi sambamba na hali ya ubora. Leo Ulimwengu wa Kiislamu unahitajia harakati hii ya Basiji.
Huu unyama na ushenzi uliofanywa katika wiki hii huko Gaza ambao kwa kweli unamfanya mtu apigwe na butwaa kutokana na ukubwa wa unyama na ushenzi wa viongozi wa utawala wa Kizayuni, unapasa kuzipa mtikiso dhamiri na hisia za Ulimwengu wa Kiislamu na kuipa nguvu mpya harakati hii adhimu ya wananchi katika Ulimwengu wa Kiislamu. Adui hajakaa tu, na harakati hii (ya Wazayuni) ina hali kadhaa: Kwanza ni kubainisha ushenzi wa viongozi wa utawala wa Kizayuni. Ni wanyama na washenzi wa kiwango gani!, ni kwa kiwango gani wako mbali na dhamiri na hisia za utu!; kuwashambulia namna hii watu wasio na hatia na watu ambao ni raia wa kawaida! Kwa kweli mtu anashangaa, anaduwaa; hawa hawaijui hata harufu ya utu. Hawa wanakabiliana na Ulimwengu wa Kiislamu, wanakabiliana na Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu, hawa ni watu wanaopingana na Jamhuri ya Kiislamu katika duru za ulimwengu; hawa hawaijui hata harufu ya utu. Hii ni hali moja ya suala hili na ambayo ni muhimu sana.
Hali nyengine ya kadhia ni kwamba viongozi wa mfumo wa Uistikbari wanaamiliana na kadhia hii bila ya kuona haya kwa namna inayomstaajabisha mtu; yaani sio tu hawakunji uso kuonyesha kuchukizwa wala hawauzuii utawala huu wenye moyo katili na wa kinyama kufanya unayoyafanya bali unauimarisha na kuupa nguvu, unaushajiisha na unauunga mkono! Marekani imeuunga mkono waziwazi, Uingereza imeunga mkono na Ufaransa pia imeunga mkono. Hawa ni viongozi wa ulimwengu wa Uistikbari. Hawa ni watu walewale ambao mataifa ya Waislamu leo hii hayana adui katili zaidi na anayechukiza zaidi ndani ya nyoyo zao kama watu hawa. Wote hawa wameunga mkono waziwazi. Kutokana na tukio hili mtu anaweza kufahamu uzito wa muelekeo wa kushikamana na akhlaqi na umaanawi ulivyo katika ulimwengu wa Uistikbari. Ni kwa kiwango gani watu hawa wako mbali na utu! Lakini kama wanaunga mkono kisiasa kwa sababu ya malengo yao maovu ya kisiasa, kwa nini tena watu hawa wanadai kuzungumzia haki za binadamu?! Ikiwa Marekani sio tu haichukui hatua yoyote ya msimamo kukabiliana na harakati hii ya kikatili na ya kishenzi bali inaiunga mkono pia, itakuwa na haki tena ya kuzungumzia haki za binadamu? Ina haki ya kujifanya mtoaji hukumu dhidi ya mataifa na nchi nyengine kuhusiana na haki za binadamu? Na huu ni ufidhuli maradufu. Ufaransa pia ni hivyohivyo, Uingereza pia ni hivyohivyo. Rekodi ya mwenendo wa watu hawa katika Ulimwengu wa Kiislamu, jinai mbalimbali walizofanya, mauaji waliyofanya na mashinikizo na mbinyo waliotoa kwa wananchi Waislamu katika nchi mbalimbali, na hayo bado hayajafutika kwenye kumbukumbu za wananchi wa mataifa ya Kiislamu, leo pia wanauunga mkono utawala wa kinyama na wa kishenzi kama utawala wa Kizayuni, na wanatetea mambo unayofanya. Huu pia ni upande mmoja wa kadhia hii.
Upande mwengine wa kadhia ni mwenendo wa nchi za Kiarabu na za Kiislamu ambao haukuwa mwenendo wa sawa. Baadhi yao wametosheka na kusema tu, baadhi yao hata hawakusema kitu; hata hawakulaani pia! Wale watu wanaodai kuzungumzia Uislamu wanaodai kutoa wito wa umoja baina ya Waislamu, wanaodai kuongoza Ulimwengu wa Kiislamu, ilipasa wajitokeze katika mazingira kama haya. Katika kadhia mbalimbali zinazokidhi malengo yao ya kisiasa, hujitokeza bila kusitasita, lakini kwa kuwa upande unaohusika hapa ni Marekani, kwa kuwa upande unaohusika ni Uingereza hawako tayari hata kulaani kisawasawa. Au wanatosheka na kuunga mkono kwa maneno matupu tu ambako hakuna thamani yoyote; ni hatua yenye taathira ndogo. Leo Ulimwengu wa Kiislamu na hasa majimui ya nchi za Kiarabu zinapaswa kupeana mkono wa umoja, kuwatetea wananchi hawa, kuondoa mzingiro na kujaribu kuwasaidia wananchi hawa madhulumu wa Gaza.
Bila ya shaka Mwenyezi Mungu amewapa taufiki wananchi wa Gaza ya kuonyesha muqawama na kusimama imara kukabiliana na adui huyu katili na mwenye silka za kinyama, nao wamepata tija ya kusimama kwao imara ambayo ni ile izza ya watu wa Gaza; wameonyesha kuwa, kwa kusimama imara, kwa kuonyesha muqawama na kwa kuvumilia tabu inawezekana kuwa na idadi ndogo na kuishinda idadi kubwa, tata, iliyojizatiti kwa silaha na inayoungwa mkono na madola makubwa. Leo Wazayuni wanaoitawala Palestina inayokaliwa kwa mabavu wanahaha zaidi kutaka kusitisha vita kuliko watu wa Gaza na viongozi wa Gaza. Ni wao ndio waliotenda jinai, ni wao ndio waliofanya maovu, ni wao ndio waliofanya unyama, lakini wao ndio wanaoendelea kupata kipigo zaidi kutokana na kusimama imara idadi ndogo ya Waislamu ya watu wa Gaza na vijana wa Gaza. Na hakuna njia nyengine ghairi ya hii; huu ni ujumbe kwa Ulimwengu wa Kiislamu: ikiwa Ulimwengu wa Kiislamu unataka ubaki kuwa na uwezo wa kutodhoofishwa na mashambulio ya maadui, uovu wa maadui, njama za maadui, unyama wa maadui na ubaya wa maadui unalazimika kujihami kwa nguvu zake. Inapasa ujenge nguvu kutoka ndani yake wenyewe; nguvu za kimaanawi ambazo ni nguvu za kiimani na azma ya irada, na pia nguvu za kimaada. Maendeleo ya kielimu ni nguvu za kimaada; tajiriba na teknolojia ni nguvu za kimaada; uwezo wa kutengeneza zana za maisha zikiwemo silaha na zisizokuwa silaha ni nguvu za kimaada. Haya ni mambo ambayo Ulimwengu wa Kiislamu na jamii za Kiislamu zinapaswa kujiandalia. Majimui moja yenye udogo kama wa Gaza inavumilia tabu na inatoa mhanga mashahidi lakini inamkabili adui kwa namna ambayo, kama tulivyosema, leo adui anahahaha zaidi kutaka kusitisha vita huko Gaza kuliko viongozi wenyewe wa Gaza na watu wa Gaza. Hili ni somo kwa Ulimwengu wa Kiislamu na tab'an sisi tulijifunza somo hili kutokana na kipindi cha Kujihami Kutakatifu. Alhamdulillah watu wetu, vijana wetu, wataalamu wetu na watu wetu wenye tajiriba walipiga hatua kimaendeleo katika suala hili. Kwa upande wa kielimu tulipiga hatua, kwa upande wa tajiriba tulipiga hatua; tuliielewa hakika hii kwamba tunapaswa kujitegemea sisi wenyewe. Hii pia ni moja ya sababu za kuweza kusimama imara.
Na suala la umoja; umoja. Hili suala la umoja na kalima ya umoja kati ya Waislamu na umma wa Kiislamu kwa mtazamo mmoja; na baina ya wananchi Waislamu ndani ya kila nchi, umoja kati ya watu wa nchi moja na baina ya matabaka mbalimbali ya wanachi hao ni jambo muhimu; kuhusiana na sisi pia ni hivyohivyo. Hii kwamba sisi tunarudia mara kwa mara kuiambia mirengo ya kisiasa na viongozi waheshimiwa kuhusu kudumisha umoja, kwa watu wanaotumia viriri vya kuzungumza; yawe ni magazeti, mitandao ya intaneti au vipaza sauti mbalimbali za vyombo vya serikali na visivyo vya serikali, ambapo nasaha zetu daima kwa jamaa, akina kaka, viongozi, waandishi na wazungumzaji ni kuhusu suala la umoja, ni kwa sababu umoja ni jambo adhimu. Na nchi yetu, kwa bahati nzuri kutokana na umoja lilionao taifa - na bahati nzuri hizi hitilafu mbalimbali zimeshindwa kuligawa taifa - limeweza kudumnisha mshikamano wake kwa kiwango cha juu. Viongozi nao wanatafautiana kiutashi, lakini hitilafu hizi huwa hazina tatizo kama hazitoishia kwenye kukabana koo. Ni umoja huu na kuwa kitu kimoja ndiko kulikowezesha kuilinda nchi na kuifanya ionekane mbele ya macho ya maadui kuwa ni majimui yenye nguvu na nchi yenye nguvu. Hivi sasa pia ni vivyo hivyo. Kitambo kidogo nyuma nilitoa agizo juu ya mshikamano na umoja; bahati nzuri waheshimiwa viongozi wa mihimili mikuu ya dola wameliitika agizo hilo; ni jambo la thamani kubwa. Inabidi kutoa shukurani kwao; viongozi wa mihimili ya dola, wakuu wa mihimili mitatu wameitika, wametangaza na wamesisitiza kwamba wataendelea kuwa na umoja kati yao katika nyanja mbalimbali licha ya hitilafu za utashi na hitilafu za mitazamo zilizopo baina yao. Na sisi kwa upande wetu tunalikubali hili kutoka kwa hawa akina kaka wapenzi na waheshimiwa viongozi kwa kulichukulia kuwa ni harakati chanya, na tunaamini kwa dhati kuwa hatua hii ya jamaa ilikuwa harakati nzuri na kwa hivyo sasa wanapaswa wachunge maneno na matamshi yao.
Hii kazi inayofanywa hivi sasa katika Majlisi tukufu ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge) nayo pia ni moja ya yale masuala ambayo ndani yake yana hali ya kusifiwa na kupongezwa. Nilieleze hili; na mzingatie nyinyi akina kaka na akina dada wapenzi na wananchi wetu wapenzi; huku kuwauliza masuali viongozi wa nchi awe ni Rais au viongozi wengine wa serikali ni jambo zuri na chanya katika hali mbili: ya kwanza ni kwamba inaonyesha wawakilishi wa wananchi bungeni wanahisi kuwa wana jukumu kuhusiana na masuala ya nchi; hili ni jambo chanya. Hali nyengine ni kwamba viongozi wa nchi, kwa kujiamini na kwa ushujaa unaostahiki pongezi wanasema wako tayari kwenda kutoa maelezo kuhusu masuali hayo; hili pia ni jambo chanya. Viongozi wetu wa bunge wanatekeleza wajibu wao na pia viongozi wetu wa serikali wanaonyesha kuwa wana uhakika na wanajiamini kuhusu ukweli na usahihi wa kazi zao. Mtu anataka nini tena, bora zaidi ya yote ni hili. Na jambo hili limetokea, yaani bunge linasema linataka kuuliza, huku ni kuwajibika; serikali nayo inasema inataka kutoa jibu kwa kujiamini na inaonyesha kuwa inao uwezo wa kujibu - na hili wametueleza sisi pia - hili pia ni jambo la kupongezwa; nukta zote mbili ni nzuri, lakini mimi ninaitakidi kwamba nukta hizi ni chanya hadi kufikia hapa, lakini baada ya hapa zisiendelezwe tena. Wayahatimishe hapahapa; walimalize suala hili hapahapa. Bunge limefanya mtihani wake vizuri, na viongozi wa serikali nao wamefanya mtihani wao vizuri; mtihani huu ulikuwa mtihani mzuri. Wananchi nao kutokana na uono wa mbali walionao wanafahamu na wanaelewa. Kuendeleza suala hili ndicho kitu wanachokitaka maadui; wanapenda kuigonganisha vichwa mihimili hii miwili ya dola; kisha baadhi ya watu watekwe na upande huu na baadhi ya watu watekwe na kuathiriwa na upande ule na kisha baadhi ya waandishi na vyombo vya propaganda katika magazeti, mitandao ya intaneti na vinginevyo viingie kazini na kuanzisha zogo. Hapana, nchi inahitaji utulivu. Viongozi wote, wawe wa bunge, wa mahakama au wa serikali, ili waweze kuendelea kufanya kazi zao wanahitaji utulivu, na wananchi pia wanapenda utulivu. Ule ambao ulikuwa wajibu wa bunge umetekelezwa; serikali nayo imeonyesha kuwa inajiamini kuhusiana na kile kilichokuwa wajibu wa bunge; hili n jambo la kufurahisha kutoka pande zote mbili. Kuanzia sasa ninawaomba wale akina kaka na majimui ya watu kumi katika bunge walioanzisha suala hili walihitimishe na kuonyesha kivitendo kwamba viongozi wa serikali, viongozi wa bunge na pia viongozi wa mahakama wanaheshimu umoja wa taifa hili na utulivu wa nchi kuliko kitu chochote.
Ninawashukuru akina kaka na akina dada wote wanaoshughulika kwenye kitengo cha ufanyaji kazi cha Basiji. Inshallah Mwenyezi Mungu Mtukufu akupeni taufiki nyote. Ninawashukuru pia akina kaka na akina dada wote waliozungumza. Ni matumaini yangu kuwa inshallah Mwenyezi Mungu atawapa wote jaza ya kheri. Ninamshukuru pia huyu ndugu mpenzi aliyenitunukia medali yake hii. Na mimi nimeikubali medali hii kutoka kwake lakini pamoja na hayo ninairejesha na kumtunukia yeye mwenyewe; na hivi ndivyo bora kwamba ibakie mikononi mwake na kuwa kumbukumbu ya ubingwa wake na pia kumbukumbu yangu mimi kwake. Inshallah mpate mafanikio.
Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.
 
< Nyuma   Mbele >

^