Skip to content

Habari

Habari
Hifadhi

Risala na Barua

Matini
Hifadhi

Kumbukumbu na Simulizi

Kabla ya Mapinduzi
Baada ya Mapinduzi

Sauti na Taswira

Picha
Sauti
Video
Hotuba ya Kiongozi Muadhamu katika Mkutano na Washindi wa Medali katika Olimpiki na Paralimpiki Chapa
11/03/2013
Bismillahir Rahmanir Rahim
Nimefurahi sana kukutana na nyinyi wapendwa - mabingwa, wanamichezo manguli na waleta fahari (kwa nchi) - ambao alhamdulillah mumeweza kufikia kwenye vilele kutokana na hima, irada na azma thabiti. Kama ilivyo kwa hivi vilele vya milima ambavyo wapanda mlima, wapanda majabali na wapandaji mawe huvikwea na kufikia kileleni kwa tabu na mashaka makubwa na kuleta fahari na hali ya kujivunia, vilele vya kuleta fahari za kimaanawi na za kitaifa pia vinapofikiwa na vijana huwa kwa kweli vina thamani kubwa; na nyinyi mumeifanya kazi hii.
Kuna mambo mawili muhimu na yenye taathira kwa watu wanaotwaa ubingwa na inapasa kuyazingatia mambo mawili haya: Moja ni suala la mtu binafsi na jengine ni suala la wananchi na la kijamii. Katika suala la mtu binafsi vijana wanaoshinda na kutwaa ubingwa wanaonyesha na kuthibitisha kwamba wana sifa kubwa na maalumu; mathalani wana irada madhubuti. Kama mwanamichezo hatokuwa na irada madhubuti na azma thabiti bila ya shaka hawezi kufikia hatua ya kutwaa ubingwa; kama haitokuwepo irada hata michezo pia atakuwa hashiriki. Licha ya yote haya yanayosemwa kuhusu michezo - michezo ya kawaida, mazoezi ya viungo ya asubuhi - lakini baadhi ya watu hawako tayari hata kutumia dakika kumi, robo saa ya wakati wao kwa ajili ya jambo hili; huku ni kuwa na irada ndogo. Kwa hivyo wakati kijana anaposhiriki katika michezo, akavumilia tabu na machofu ya kimwili yanayotokana na michezo na akapiga hatua ya kukuza vipawa vyake vya kimwili kwa hamu na shauku, hii ni ishara ya kuwa na azma thabiti; hii ndiyo sifa maalumu ya mtu binafsi.
Sifa nyengine ni suala la uhodari. Hakuna bingwa yoyote wa michezo ambaye anaweza kutwaa ubingwa pasina kuwa na uhodari mkubwa. Wanamichezo wote wako hivi. Yaani si suala la mtu kuwa na nguvu tu na kuweza kufanya jambo hili kwa kutegemea nguvu; hapana, nguvu tu hazitoshi; uhodari pia una ulazima. Iwe ni katika michezo ya pamoja au michezo ya mtu mmoja mmoja, iwe ni katika mieleka, unyanyuaji vitu vizito, upandaji milima au michezo ya mapambano na mfano wa hayo ni kwamba kama mtu na mwanamichezo huyo hatokuwa hodari kwa kuwa na akili inayofanya kazi, yenye udadisi na elekevu haiwezekani kufikia hatua za juu. Kwa hivyo tunapomwangalia mtu ambaye ni bingwa tunaona kuwa yeye ni dhihirisho la uhodari, hima, irada uwezo wa kiwiliwili na sifa nyengine nyingi. Tab'an mtu ambaye ni nguli wa michezo huwa ana kiwango cha juu cha hali ya kujiamini; na hivi ndivyo anavyotakiwa awe, yaani asiwe na haja ya kufanya mambo wanayofanya watu wenye irada dhaifu; hana haja ya kujipendekeza na kujikomba, hana haja ya kusema uwongo na hana haja ya kufanya udanganyifu na kujifanya mtu mwenye nyuso mbili. Tab'an hatutaki kusema kwamba watu wote ambao ni wanamichezo hawana sifa hizi na wameepukana nazo; la, wanadamu huwa wanateleza; lakini hulka ya mwanamichezo nguli huwa anaweza kujiweka mbali na mwenendo huu wa kiakhlaqi na sifa hizi za kiakhlaqi. Kwa hivyo huu ni upande wa binafsi wa shakhsia ya wanamichezo mabingwa.
Upande wa wananchi na wa kijamii wa mtu bingwa ni kwamba kwa kuwa yeye anachukuliwa kuwa ni dhihirisho la uwezo wa taifa katika aina maalumu ya mchezo hulipa taifa hali ya kujiamini; yaani huipa majimui ya wananchi wote wa taifa zima moyo wa kujiamini; hiki ni kitu muhimu sana. Kwa upande mwengine mwanamichezo bingwa huwashajiisha watu wa jamii nzima wafuate njia hiyo. Yaani ukweli ni kwamba mchezo wenye mashindano ya ubingwa ni injini ya kuleta harakati kupitia michezo kwa watu wote na inawezekana kutumia mchezo wenye kiwango cha mashindano ya ubingwa ili kueneza utamaduni wa watu wote kujishughulisha na michezo. Michezo kwa wote nayo pia ni mojawapo ya mambo ya lazima kwa maisha; ni kama kula chakula, ni kama kuvuta hewa; inapasa nayo ipewe umuhimu. Na hii ni nukta nyengine ya mambo yanayoingia kwenye orodha ya athari za kijamii za michezo.
Suala jengine ni kwamba michezo ya mashindano ya ubingwa ambayo leo hii imezoeleka kuwa katika sura ya mashindano ya kimataifa ni dhihirisho la hamu, uwezo, vipawa, upambanuzi na utambulisho wa taifa fulani; na hili ni jambo muhimu sana. Wakati nyinyi mnapojitokeza katika uwanja wa michezo na akhlaqi za kiutu za kiungwana - na hivyo ndivyo mnavyojitokeza - kwa mtazamo wa watazamaji kimataifa waliopo na wanaokuoneni, ambapo leo hii kuna mamilioni ya watazamaji na wakati mwengine mabilioni, huwa mumebeba ujumbe wa hakika fulani kuhusu nchi yenu; hakika na ukweli ambao hauwezi kutangazwa kwa kutumia lugha na njia nyengine yoyote. Mwanamichezo bingwa huwa anafanya tablighi kwa uungwana wake na kwa kushikamana kwake na dini. Hili suala la wanamichezo wetu wanawake na wasichana ambao wanaingia uwanjani wakiwa na hijabu ni kitu muhimu sana. Mimi sijui kama watu wanaotaka kutathmini matukio ya nchi yetu wanalifanyia tathmini sahihi suala hili au la; hili ni suala lisilo la kawaida. Katika nchi moja miongoni mwa nchi za Ulaya wanajusuru kumpiga kisu na kumuua mwanamke kwa kosa la kuwa na hijabu; na tena linafanyika hili mbele ya mahakama na mbele ya macho ya hakimu! Hivi ndivyo hali ilivyo. Hawaoni aibu; kwa hukumu ya sheria walizojipangia, mwanamke mwenye hijabu huwa anaandamwa katika vyuo vikuu, viwanja vya michezo, kwenye bustani za mapumziko na mabarabarani. Kisha katika mazingira kama haya na ndani ya nchi hizi mwanamke mwenye hijabu aliyetwaa ubingwa anapanda juu ya jukwaa la utoaji medali kwa mabingwa na kuwafanya watu wote wampongeze na kumpa heshima. Ni jambo dogo hili? Hili ni jambo lenye adhama kubwa. Kwa kweli watu wote wanapaswa kutoa shukurani za dhati kwa wanamichezo wetu wa kike wanaojitokeza uwanjani wakiwa na hijabu, wakiwa na murua na wakiwa wamechunga staha na heshima zao. Au vilevile michezo ya watu wenye vilema na walemavu; kwa kweli ni hali ya kustaajabisha. Wakati watu wanapoangalia wanamwona kijana huyu aliyepatwa na masaibu ya kimwili lakini sio tu masaibu haya ya kimwili hayajamzuia kuishi maisha ya kawaida bali ameweza hata kuwa na hima, azma na irada madhubuti ya kumwezesha kuwa mwanamichezo na kufikia kwenye kiwango hiki katika michezo cha kuja kupanda juu ya jukwaa la ubingwa. Hii inaonyesha azma na irada ya taifa, hii inaonyesha heshima na utambulisho wa taifa. Hii mimi kutoa shukurani kwenu wakati mnapopata ushindi, pamoja na shukurani hizo kuna hisia za dhati na za moyoni ninazokuwa nazo ndani ya nafsi yangu; huwa ninahisi kwamba kwa kazi yenu hii, nyinyi mnaitumikia nchi yenu, taifa lenu na watu wenu. Nyinyi mnafikisha ujumbe ambao hauwezi kufikishwa kwa njia nyengine yoyote ile: ujumbe wa azma na irada, ujumbe wa kusimama imara, ujumbe wa imani. Baada ya kupata ushindi katika medani kama hizo na kushika nafasi za kwanza duniani, mwanamichezo wetu hutoa sha'ar za "Yaa Hussain"; au huporomoka chini kusujudu au huinua mikono yake juu kumshukuru Mwenyezi Mungu. Mnajua ni msisimko gani unapata umma wa Kiislamu na wananchi wa mataifa ya Kiislamu kutokana na harakati hizi mnazoonyesha? Wakati dunia inajaribu kuwaelekeza watu wote na hasa vijana kwenye mambo ya kuwavua imani, ya kutojali dini na kuyapa mgongo masuala ya umaanawi, kijana wetu hodari - sio kijana wa kawaida - anaonyesha namna hivi katika medani ya michezo jinsi anavyoyajali masuala ya umaanawi. Haya ni mambo muhimu na yenye taathira kubwa.
Mimi ninataka kusema kwamba muijue thamani yenu. Mambo makubwa sana yanafanyika katika medani za mashindano ya ubingwa. Bahati nzuri baada ya Mapinduzi kujia huku, Iran ya Kiislamu imepata maendeleo ya kustaajabisha katika suala hili. Leo nyinyi mnaongoza katika medani nyingi. Kuna wakati nyinyi mnacheza mieleka na kuwabwaga chini wapinzani wenu kutoka nchi zinazotajika duniani na kupanda juu ya jukwaa la ubingwa; hiki ni kitu kizuri sana na chenye umuhimu sana; lakini ukihesabu majimui ya kazi zote zinazofanywa ziko hivi pia. Chukulia mfano katika mashindano ya dunia - kama haya yaliyofanyika - nyinyi mathalani mnashiriki na wanamichezo 54 na mnanyakua medali 12; Marekani inashiriki na wanamichezo 530 na inabeba medali 110. Ikiwa Marekani itataka kunyakua medali kwa kiwango sawa na nyinyi itapaswa kubeba medali 120. Marekani inashiriki na wanamichezo ambao idadi yao ni mara kumi zaidi ya idadi yenu, hivyo inapasa inyakue idadi ya medali mara kumi ya medali zenu; inapaswa ibebe medali 120 lakini haipati idadi hiyo ya medali; maana yake ni kwamba iko nafasi ya chini zaidi kuliko nyinyi. Hii maana yake ni kwamba kama nyinyi mtashiriki katika michezo mbalimbali kwa kiwango hikihiki na kwa wanamichezo wenye vipaji hivihivi mtawashinda wote hao. Haya ni mambo yenye thamani. Hizi ni hakika zinazoonyesha fursa za uwezo tulizonazo.
Suala tunalozungumzia leo ni la michezo, lakini hali hii haiko kwenye michezo tu; bahati nzuri katika uwanja wa elimu pia ni hivyohivyo. Katika nyanja za utafiti na kupanua ufanyaji uhakiki na tafakuri ya kina kuhusiana na masuala mbalimbali iwe ni katika uga wa uchumi, uga wa siasa, uga wa masuala ya uongozi, uga wa masuala ya kimataifa na mahala popote pale panapohitajia kuonyesha vipawa vya Kiirani tumeshuhudia mote humo ishara za maendeleo. Huu ndio uwezo wetu na hii ndio nchi yetu. Kwa sababu hii pia historia yetu imeng'ara kiasi hiki na kufikia kwenye kilele. Ibn Sinaa na Farabi, Muhammad Zakariyya Razi, Sa'adi, Hafez na mfano wa hao hawakuzaliwa katika jamii ya kiwango cha chini; hii inaonyesha kuwepo vipawa vilivyorundikana katika eneo hili la dunia. Lakini vipawa hivi vilikuwa vimezorota kutokana na athari za udhibiti wa tawala kandamizi na za kidikteta zilizokuwepo, kujitenga kwao na wananchi na kutokuwa na sifa za kimaanawi, za kiutu na za kielimu. Bahati nzuri leo Mapinduzi yamefanya kazi ambayo imepelekea kuibuka kwa vipawa hivi kila mahala na hasahasa katika uga wa michezo.
Kwa hivyo hizi ndizo sifa zenu njema ndugu wapenzi ambazo nimezieleza, kwamba nyinyi ni vilele. Nyinyi wenyewe mnahesabiwa kuwa ni vilele na pia kazi mnayofanya kwa kweli ni harakati kuelekea kileleni na harakati ya kuielekeza jamii ya watu kuelekea kileleni; na haya ni mambo yenye thamani kubwa. Nimesema kwamba nyinyi ni mabalozi wa Iran, utambulisho na heshima ya Kiirani; endeleeni kuzitunza sifa hizi. Hii hali ya nyinyi kwenda kulitangaza taifa lenu kuwa ni taifa lenye irada, lenye azma thabiti, lenye imani, lenye kushikamana na dini, lenye vipawa na lenye sifa za kipekee ni kitu chenye thamani kubwa; inapasa muitunze na kuidumisha hali hii; msiruhusu iingie doa.
Vijana nchini wanakutazameni nyinyi. Nyinyi mnaitangaza michezo kivitendo; mimi nasema itangazeni michezo kwa ndimi zenu pia. Yaani katika mazungumzo na maelezo yenu mnayotoa kwa wananchi, katika jamii na vyombo vya habari, katika mahojiano, kwenye televisheni na mfano wa hayo wahamasisheni vijana nchini; zungumzieni tajiriba na uzoefu wenu katika michezo ili vijana waingiwe na hamu na shauku. Sisi tunahitaji watu wote nchini washiriki kwenye michezo; hili kwa kweli ni hitajio la nchi. Rasilimaliwatu yenye afya ina umuhimu wa daraja la kwanza kwa nchi; kwa sababu maendeleo ya kila nchi yanategemea rasilimaliwatu. Maliasili, madini, utajiri wa chini ya ardhi na utajiri wa kimaumbile ni vitu vizuri sana; lakini kama hakutowekupo rasilimaliwatu, kama havitokuwepo vipawa katika nchi hiyo, itakuwa hali ileile mnayoishuhudia leo hii katika baadhi ya nchi zenye maliasili hizi; wanakuja watu wengine kuzitumia na kuwaelekeza zaidi watu wa nchi hizo kwenye hali ya kujipweteka na kupenda raha. Vipawa vya watu vinapasa kukuzwa ili utajiri wa kimaumbile uweze kweli kutumika kwa ajili ya jamii. Kwa hivyo rasilimaliwatu ndio kitu muhimu zaidi.
Rasilimaliwatu inapasa iwe na elimu, iwe na hima, iwe imeshika dini na iwe na afya njema. Uzima wa kiwiliwili ndilo sharti kuu. Kujishughulisha wananchi na michezo kunatatua matatizo na masaibu mengi ya kijamii na kiakhlaqi; kama suala la uraibu wa mihadarati, suala la mizozo ya kifamilia, ya ndani, matatizo ya ajira, msongo wa mawazo na mengineyo na mengineyo. Ikiwa michezo litakuwa suala lililokubalika kwa watu wote nchini - na tab'an hali ya leo ni bora kuliko ya nyuma, lakini tungali tunahitaji kufikia kwenye hali hii - matatizo mengi sana yatatatuka. Nyinyi mnaweza kuwa na taathira katika suala hili; yaani muwe waenezaji wa akhlaqi na mila za Kiirani.
Hii hatua iliyochukuliwa na baadhi ya vijana wetu katika uwanja wa mashindano, ya kukataa kwenda kushindana na upande wa Kizayuni ni jambo lenye thamani kubwa; na ndiyo maana imewakasirisha mno Waistikbari wa dunia. Kadhia hii imetokea mara kadhaa, na wao wameonyesha radiamali kali. Hatua inayochukuliwa na vijana wetu hawa ni hatua muhimu sana. Yaani kwa kweli hii ni moja ya juhudi muhimu na nyeti mno za kidiplomasia ya kukabiliana na utawala wa Kizayuni. Hatua hii waliyochukua ilikuwa hatua yenye thamani kubwa.
Suala jengine moja ninalotaka kulitilia mkazo juu ya hili ni suala la akhlaqi katika michezo. Jamaa wamelieleza, na mimi pia ninazo taarifa na ninakubaliana nalo. Bahati nzuri kwa upande wa akhlaqi, jamii yetu ya michezo ni jamii safi na salama; lakini inapasa uwekwe mkazo mkubwa juu ya suala hili. Mambo ya kutelezesha yapo. Wakati kijana wetu mwanamichezo anapoandamwa na mawimbi ya propaganda, kimataifa na fikra za waliowengi hukabiliwa na hatari ya kiakhlaqi. Sisi tunapaswa kujihifadhi na hatari hii ya kiakhlaqi. Kwanza kabisa nyinyi ambao ni wanamichezo, kisha viongozi wa michezo na watu wenye nyadhifa mbalimbali za uendeshaji ambao wanayapa umuhimu masuala haya, na masuala haya yana uhusiano na wao, wanapaswa kulipa umuhimu suala la akhlaqi katika michezo. Suala la akhlaqi katika michezo ni muhimu sana. Kutoingiwa na ghururi, kubaki kuwa mtu wa watu, kubaki kuwa na uungwana, kuwa pamoja na watu na moyo wako kuungulika kwa ajili ya watu ni mambo muhimu sana. Kupatikana kwa sifa hizi ndani ya nafsi ya mtu ni suala moja, na kuendelea kubaki sifa hizi ndani ya nafsi yake mtu ni suala gumu zaidi; mtu anapaswa kuyadumisha mambo haya.
Kwa maoni yangu baadhi ya watu wanahiharibu anga ya michezo; ni kutokana na upakaji matope, uzushaji tuhuma, kusema uwongo na kuchochea ugomvi baina ya majimui za michezo. Kwa masikitiko nafasi ya vyombo vya habari za michezo pia katika mwenendo huu usio sahihi si ndogo. Inalazimu hapa nitoe tanabahisho na onyo. Vyombo vya habari vya michezo vinaanzisha kitu kidogo dhidi ya mtu, dhidi ya harakati ya michezo, dhidi ya timu, dhidi ya shirikisho fulani na dhidi ya mwanamichezo fulani na kukifanya kuwa wenzo wa kumchonganisha huyu na yule, na kumchonganisha yule na huyu; ili wagombane. Kisha ni kuwaingiza watu kwenye mahojiano. Na kadiri yule mtu anayehojiwa atakavyotoa maneno makali zaidi, kadiri atakavyomsema mtu vibaya zaidi na kadiri atakavyotoa maneno machafu na ya kufedhehesha zaidi chombo hicho cha habari hufurahi zaidi! Hiki ni kitu kibaya. Vyombo hivi vinapaswa kufuata muelekeo ulio mkabala dhidi ya huu, utendaji wao unapasa uwe kinyume na huu.
Nukta nyengine ambayo nimeshaieleza mara kadhaa - na hili linawahusu viongozi wa michezo - ni kwamba zingatieni vipaumbele katika aina za michezo. Kuna baadhi ya michezo ambayo hapa nchini ina historia ndefu, tunayo uwezo nayo na pia tuna tajiriba na uzoefu nayo - yaani uwezo wa namna mbalimbali - hii ni michezo inayotuletea ubingwa. Katika miaka ile niliwahi kutaja majina ya baadhi ya michezo hii. Lakini katika mchezo fulani sisi hatushiki nafasi yoyote duniani, wala hakuna uwezekano wa kupata bahati hiyo; yaani hatuna bahati ya kushika nafasi - na tab'an kuna sababu zake - lakini katika baadhi ya michezo sisi tunashika nafasi za juu duniani. Leo nyinyi mnapanda kwenye jukwaa la ubingwa duniani - mathalani katika mieleka au katika unyanyuaji vitu vizito au katika baadhi ya michezo mingine - hili ni jambo muhimu sana. Miaka kadhaa nyuma - sikumbuki ulikuwa mwaka gani - ambapo walikuja hapa jamaa hawahawa wa michezo kwa ajili ya mkutano, nilitaja kwa mfano mchezo wa "Chugan". Chugan ni mchezo wetu sisi Wairani, ni wetu sisi; na ni mchezo mzuri pia, mchezo wa kuburudisha na wa kufurahisha pia. Vipaji vya mchezo huu viko hapa nchini Iran; kama visingekuwepo mchezo huu usingekuwepo. Katika muda wote wa historia mchezo wa Chugan ulikuwa kitu maarufu nchini Iran. Au mathalani kuna baadhi ya michezo ya jadi ambayo baadaye ilifanyiwa kazi na kuna juhudi mbalimbali zilizofanywa kuihuisha. Hizi ni kazi nzuri na za kuvutia ambazo zinafanyika. Alaa kulli hal muangalie vipaumbele na shughulikieni zaidi michezo ambayo ina chimbuko na historia; na hasa yenye uwezo na vipaji; hususan yenye makocha wa ndani.
Mmoja wa ndugu zetu amesema watumike makocha kutoka nje; mimi sina pingamizi yoyote. Isije ikadhaniwa kwamba ninapinga kutumiwa kocha mzuri anayefaa kutoka nje; lakini wakati nyinyi mnapomtumia kocha wa ndani kwa ajili mpira wa miguua au mpira wa kikapu au mpira wa wavu au mieleka au mchezo mwengine wowote mimi hufurahi na kuona fahari. Hili ni jambo zuri sana kwamba kocha wa watoto na vijana wetu kuwa mtu anayetokana na sisi wenyewe; ambaye amelelewa hapa na amekulia hapa. Bila ya shaka baadhi ya makocha wa kigeni ni wazuri na baadhi yao si wazuri; wanachukua pesa nyingi pia na wana matarajio makubwa pia, na baadhi ya wakati hawana kazi wanayofanya; watu wa aina hii pia wako. Kwa hivyo kama kuna wakati limezungumziwa suala la kocha wa kigeni, maneno yangu mimi yanazingatia nukta hizi.
Jamaa wamezungumza kuhusu kuipa michezo sura ya taaluma; hili ni sawa kabisa; haya ni miongoni mwa maneno yangu ambayo nimeyasema mara kadhaa. Katika fani za michezo - kwa ile michezo ambayo ina kaida za kielimu - wahusika wazifanyie utafiti wa kina wa kielimu; wafanye kazi za ziada za uhakiki wa kielimu. Chukulia mfano kuna kitu ambacho kimegunduliwa leo hii duniani katika mchezo fulani na kinafanyiwa kazi, lakini ugunduzi huu sio wa mwisho - ni kama zilivyo kazi nyengine za kielimu - inawezekana kutoa fikra nyengine za kuongezea juu ya msingi wa ugunduzi huo ambazo zinaweza kuboresha au ku hata kubatilisha msingi huo. Kwa hivyo kazi hizi zifanyike hapa Iran. Sisi tumeweza kupata maendeleo yote haya katika nyanja ngumu za kisayansi kutokana na vijana hawahawa. Tumefanya mambo mbalimbali ambayo hayakuwapitikia kamwe maadui zetu akilini mwao kwamba Muirani ataweza kuyafanya. Kwa hivyo na hili pia lifanyeni.
Fueli ya tanurinyuklia la utafiti la Tehran ilikuwa inakaribia kwisha, wakatuambia lazima msafirishe urani yenu iliyorutubishwa kwa kiwango cha asilimia 3.5 kupeleka nchi fulani ili iibadilishe kwa kiwango cha asilimia 20; baadaye nchi hiyo iipe nchi fulani iibadilishe katika sura ya fueli; kisha baadaye kwa ruhusa ya mabwana wa dunia fueli hiyo iletwe hapa nchini! Yaani ipitie kwa mabwana kadhaa na ambao bila ya shaka yoyote wasingeruhusu. Kama sisi tungetaka kununua kutoka kwao wao fueli ya nyuklia kwa ajili ya hili tanurinyuklia la utafiti tulilonalo hapa, wasingetupa hata chembe ya fueli hiyo kabla ya kulidunisha na kulidhalilisha taifa la Iran. Kuna wakati niliwahi kusema kuwa kama haya mafuta tuliyonayo sisi leo hii yangekuwa mali ya Wazungu wa Ulaya na ikabidi sisi tununue mafuta au petroli kutoka kwao wao wangetuuzia kila chupa moja kwa bei ya juu kabisa. Hivi ndivyo walivyo. Kwa hivyo wao walikuwa wakidhani kwamba sisi tutalazimika na tutawaridhia wao katika suala la kununua fueli iliyorutubishwa kwa kiwango cha asilimia 20; kwa hivyo wakaweka vizuizi hivi. Lakini vijana wetu wakaja wakafanya kazi ya utafiti na kuweza kutengeneza wao wenyewe fueli ya asilimia 20. Kisha wao wakawa wanadhani kwamba sisi hatuwezi kutengeneza loho za fueli na nondo za fueli; lakini vijana wetu wakaitengeneza na kuiwezesha kufanya kazi. Sasa wamebaki wameemewa kutokana na kazi iliyofanywa na taifa la Iran! Kazi tata kama hizi na zenye ukubwa kama huu zinaendelea kufanywa; kuna tatizo gani la kuzuia kufanyika kazi kubwa pia katika uga wa michezo? Kanuni zilizopo leo hii duniani kuhusiana na michezo, iwe ni michezo ya mtu mmoja mmoja kama mieleka na unyanyuaji vitu vizito au michezo ya kitimu zifanyiwe utafiti wa kina wa kielimu, nyengine ziongezwe juu ya hizo na baadhi yao zifanyiwe marekebisho.
Iendelezeni michezo katika kuifanya kuwa na sura ya kitaaluma. Hii ni kuhusu ile michezo ambayo imeekewa kanuni za kimichezo na za kielimu ulimwenguni na ambayo imezoeleka. Kuna baadhi ya michezo yetu pia ambayo haina kanuni za kielimu; hii inapasa tuiwekee kanuni za kielimu - na inawezekana kuiwekea - kama hii michezo ya jadi waliyoizungumzia jamaa. Baadhi ya michezo ya jadi ni michezo ya kuvutia sana; mfano huu mchezo wa kushika nondo ambao Wamashhad wanauita Gawarageh; huu ni mchezo mzuri sana na wa kuvutia mno. Kuna tatizo gani kama zitaandaliwa kanuni kwa ajili ya mchezo huu na ukaja kujumuishwa kwenye idadi ya michezo ya wote? Au mathalani mchezo wa mzunguko. Au kama hii michezo mingine iliyomo kwenye michezo yetu ya jadi.
Alaa kulli hal ni matumaini yetu kuwa inshallah Mwenyezi Mungu Mtukufu atakujaalieni nyote mpate mafanikio. Ninakushukuruni kwa dhati nyinyi nyote na wale wapendwa wote kutokana na harakati mbalimbali walizoonyesha vijana wetu katika medani za mashindano, kama kuadhini kwenye vilele virefu kabisa vya milima, au kusujudu ndani ya ulingo wa mashindano, au kuinua mikono juu na kuomba dua, au kulitaja jina la mmoja wa Maimamu au kuchunga murua wa kidini. Inshallah Mwenyezi Mungu atakujaalieni nyote mpate mafanikio. Nyinyi ni nuru ya mboni ya jicho la taifa la Iran na inshallah muwe hivyo.
Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.
 
< Nyuma   Mbele >

^