Skip to content

Habari

Habari
Hifadhi

Risala na Barua

Matini
Hifadhi

Kumbukumbu na Simulizi

Kabla ya Mapinduzi
Baada ya Mapinduzi

Sauti na Taswira

Picha
Sauti
Video
Hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Alipoonana na Wananchi wa Azerbaijan Chapa
16/02/2013
Ifuatayo ni matini kamili ya hotuba ya Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aliyoitoa tarehe 16/02/2013 wakati alipoonana na mjumuiko mkubwa wa maelfu ya wananchi wa Tabriz (makao makuu ya mkoa wa Azerbaijan Mashariki wa kaskazini magharibi mwa Iran), kwa mnasaba wa kukaribia kumbukumbu ya harakati ya tarehe 29 Bahman mwaka 1356 Hijria Shamsia (mwafaka na Februari 18, 1978) ya wananchi wa Tabriz.

Kwa jina la Allah Mwingi wa rehma Mwenye kurehemu

Natumia fursa hii kukukaribisheni nyinyi nyote makaka wapendwa, madada azizi na vijana vipenzi; hususan familia zenye bongo za mashahidi azizi, wanachuo, maulama na maafisa ambao mumekata masafa marefu haya ya nchi hii na kuja hapa na zawadi na adia hii yenye thamani kubwa ya mahaba, mapenzi na risala ya istiqama na kusimama kidete ya wananchi azizi wa Azerbaijan kwa mnasaba wa kukumbuka siku hii adhimu. Nina matarajio, Inshallah Mwenyezi Mungu Mtukufu atakupeni na kukujaalieni nyinyi nyote huba kamili na mapenzi pamoja na rehma Zake. Nakusalimu nyinyi nyote makaka na madada azizi na wananchi wote wa Azerbaijan na Tabriz, wake kwa waume waumini; kwa hakika uwepo na mahudhurio ya Azerbaijan, Tabriz na miji mingine ya eneo hilo katika kipindi chetu chote cha huko nyuma, kuanzia miaka mia moja au mia moja na hamsini iliyopita hadi leo katika harakati ya taifa la Iran ni jambo lililokuwa na nafasi muhimu sana. Hii leo pia hali iko namna hii. Ni nyinyi ambao kwa hima yenu, kwa ghera yenu, kwa imani yenu na kwa azma thabiti mlionao mumeweza kuihifadhi izza (heshima) ya nchi na taifa hili mkabala na maadui. Kadiri siku zilivyosonga mbele, ndivyo dhihirisho la Azerbaijan katika medani na nyuga mbalimbali lilivyooongezeka. Kwa hakika inapita miaka 35 sasa tangu tukio lile la Azerbaijan lilipotokee tarehe 29 Bahman 1356 (mwafaka na Februari 18, 1978). Hii leo Azerbaijan kwa upande wa imani, kusimama kidete, muono wa mbali na istiqama iko mbele zaidi kuliko hata katika kipindi kile muhimu na nyeti cha uainishaji mambo. Njama zote hizi, huku kutakia mabaya kote huku kwa ajili ya kutenganisha hisia za baadhi na sehemu tofauti za nchi, athari yake (ya yote haya) imekuwa kinyume kabisa na matarajio ya maadui. Ni nyinyi ambao mliweza kuwa mstari wa mbele daima. Kwa hakika ni nyinyi ambao daima ndio nanga ya utulivu wa nchi na taifa hili la Kiislamu.
Kuna sifa moja maalumu ya wananchi azizi wa Azerbaijan ambayo mtu anaishuhudia kwa wadhiha kabisa. Kwa hakika sifa hii inapatikana katika maeneo mengine ya nchi, lakini huko Azerbaijan ni sifa ambayo inadhihirika wazi na bayana baina ya wananchi hao; nayo ni mapambano na harakati yenye ghera ya wananchi wa Azerbaijan katika duru mbalimbali (za historia ya taifa hili); katika kadhia ya Mashrutiyyat (ya kupigania kuwepo utawala wa kikatiba nchini), katika kadhia ya kukaliwa kimabavu kijeshi na katika kadhia mbalimbali - ambapo aghalabu ya kadhia hii walikuwa mstari wa mbele kuwashinda watu wengine - daima walikuwa pamoja na dini na imani ya kidini. Pamoja na kuwa, harakati ya kifikra ya mrengo wa kushoto na vile vile harakati ya kifikra iliyokuwa na mfungamano na Magharibi ilikuwa amilifu katika eneo la Azerbaijan - kuanzia katika masiku yale yale ya mwanzo ya kuingia fikra mbaya katika nchi yetu - na walikuwa wakifanya hima ili wawatenganishe watu na dini, na wakati huo huo kama nyinyi mtatazama harakati zilizoibuka huko Azerbaijan na nyingi kati ya harakati hizo zilikuwa ni za wananchi ambapo watu wa Azerbaijan walikuwa mbele ya wengine, mtaona kuwa, licha ya kuweko njama zile, harakati ya wananchi iliendelea kuwa mstari wa mbele sambamba na kufungamana kwake na masuala ya kidini na kuliweka wazi hilo kuliko (watu) wengine. Huko Tabriz, Sattarkhan alikuwa akisema: Fatuwa ya Maulama wa Najaf iko mfukoni mwangu. Yaani shakhsia huyu mkubwa na mwanamapambano shujaa alikuwa akifanya kazi na harakati zake kwa hidaya, miongozo na maelekezo ya maulama na Marajii wa Najaf al-Ashraf (Iraq); yaani hii ilikuwa kinyume kabisa na kile ambacho harakati za kifikra za Mashariki na Magharibi wakati huo zilikuwa zikitaka kulitwisha taifa hili. Daima hali ya mambo ilikuwa namna hii na hii leo pia hali iko namna hii na bila shaka kesho mambo mambo yataendelea kuwa hivi hivi, Inshallah.
Kwa hakika taifa la Iran katika majimui yake limeifanya imani ya kidini kuwa kigezo chake na muongozo wake. Sisi tumetoa mfano wa Azerbaijan, lakini katika kila pembe ya ardhi ya nchi hii na taifa hili wananchi wa taifa la Iran wako namna hii, isipokuwa wanaziadiana kwa viwango tu; yaani sehemu nyingine hali hii ni kubwa zaidi mathalani ikilinganishwa na sehemu nyingine ya nchi ambapo hali hii ni ya kiwango kidogo. La msingi ni kuwa harakati hii inafanyika kwa ghera, ushujaa na kuhisi kuwa na masuuliya (majukumu); lakini kwa muongozo wa dini, kwa kinga ya imani ya kidini; kwa hakika hili ni jambo lenye thamani sana. Ni kwa kuzingatia uhakika huu ndio maana mnaona kuwa, hatari ambazo kikawaida zinayaelekea mataifa mengine kutoka kwa madola ya kibeberu ulimwenguni na kuyatikisa mataifa hayo, hatari hizi hazijalitikisa hata kidogo wala kuliteteresha taifa la Iran. Sasa kuna kipindi fulani maadui walisema kuhusiana na suala la vikwazo na mashinikizo kwamba, wanataka kuliwekea vikwazo taifa la Iran ambavyo vitalidumaza; wakaandaa vikwazo hivyo. Siku mbili au tatu kabla ya tarehe 22 Bahmhindi wa mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran) waliingiza mahesabu ya vikwazo vipya katika marhala nyingine; miezi kadhaa iliyopita pia - katika mwezi Mordad mwaka huu huu - wakafanya tena kazi hii hii. Yaani kwa mujibu wa wanavyodhani wao ni kwamba, wameongeza mashinikizo kwa wananchi wa Iran katika masiku haya ya tarehe 22 Bahman. Kwa matumaini gani? kwa matumaini kwamba, watawakatisha tamaa wananchi. Jibu likawa nini? Jibu la wananchi wa Iran lilikuwa hili kwamba, maandamano ya maadhimisho ya tarehe 22 Bahman (siku ya kukumbuka ushindi wa mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran) yamefanyika kwa hamasa na shauku kubwa kuliko miaka ya huko nyuma. Watu wote walikuja na kujitokeza, walikuja kutoka kila sehemu tena wakiwa na ari na hamasa kubwa sambamba na nyuso zenye bashasha na tabasamu. Hili ndilo taifa la Iran. Kila mwaka katika siku ya tarehe 22 Bahman wananchi wa Iran hutoa pigo kwa maadui; tukio hili huwa kama kuangukiwa maadui na wapinzani na tufani kubwa. Mwaka huu pia tufani hii iliwaangukia maadui na watu wasiolitakia mema taifa hili. Kwa hakika mimi ninaona ni lazima kwangu mimi kulishukuru tena taifa la Iran - kwani hata kama tutashukuru mara mia moja na kukariri tena na tena, kushukuru huko kutakuwa sio kwingi - hivyo basi bado tutahitajika kuwashukuru tena na tena wananchi kwa moyo na muono wao wa mbali waliouonesha katika maandamano hayo.
Kwa hakika mtu anapaswa kuonesha heshima na taadhima mkabala na hisia hii na muono huu wa mbali (walio nao wananchi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran). Hili ndio taifa la Iran. Taifa la Iran liko namna hii. Kwa hakika mimi napenda kuwaambia kwamba, maadui wamekabiliwa na hali ya kushindwa kufanya chochote mkabala na hali hii. Kinyume na kile kinachotaka kuoneshwa kwamba, wao (maadui) wako amilifu, hapana, hali haiku namna hii; kwa hakika maadui wamekumbwa na hali ya kushindwa kufanya kitu mkabala na taifa la Iran. Taifa la Iran likiwa na azma thabiti, muono wa mbali na imani thabiti na imara linatambua na kufahamu vyema kwamba, linataka nini, litambua njia pia na wakati huo huo linastahamili na kuvumilia magumu likiwa na ushujaa kamili; silaha tofautzi tofauti za kisiasa, kijeshi, kiusalama na kiuchumi zimekumbwa na mwendo wa kinyonga (zimeshindwa kufanya kazi kama inavyotakiwa) katika kukabiliana naa taifa la Iran; hivyo basi adui sio amilifu katika hili kama inavyotaka kuoneshwa (mbele ya macho ya walimwengu). Kwa kuwa adui hayuko amilifu amekuwa akifanya harakati zisizo za kimantiki na zisizo na maana.
Niwaambie kwamba: Viongozi wa Marekani ni watu wasio na mantiki; maneno yao sio ya kimantiki, vitendo vyao sio vya kimantiki, bali matamshi na vitendo vyao ni vya utumiaji mabavu na ubabe; wana matarajio kwamba, watu wengine wasalimu amri mkabala na vitendo vyao vya kibabe, utumiaji mabavu na visivyo vya kimantiki; vizuri, kuna baadhi ya watu ambao wamekuwa wakisalimu amri; baadhi ya madola, baadhi ya watu wenye vipawa vya kisiasa katika baadhi ya nchi wamekuwa wakisalimu amri mkabala na ubabe na utumiaji mabavu huu wa viongozi wa Marekani; lakini taifa la Iran na Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu si wenye kusalimu amri (si mbele ya Marekani wala mbele ya waitifaki wake). Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu una maneno, una mantiki, una uwezo na una nguvu; na ndio maana hauko tayari kusalimu amri mbele ya maneno na matamshi yasiyo ya kimantiki na kazi isiyo ya kimantiki. Vipi wao sio watu wa mantiki? Ishara na dalili za kwamba, wao sio watu wa (kutumia) mantiki ni huu huu mgongano wao ambao unashuhudiwa baina ya maneno na vitendo pamoja na muamala wao; wanasema kitu fulani lakini wanafanya kitu kingine. Vizuri, je kuna dalili wadhiha na bayana ya kwamba, wao sio watu wa (kutumia) mantiki zaidi ya hii? Mtu ambaye ni (wa kutumia ) mantiki huzungumza maneno ya kukinaisha (ya maana) na kisha baadaye hufanya harakati kwa ajili ya kutekeleza kivitendo maneno na matamshi aliyoyazungumza. Hawa mabwana - viongozi wa Marekani na (viongozi) wengine wanaowafuata wa Kimagharibi - wao hawako namna hii; husema jambo, hudai jaambo lakini katika amali na vitendo hufanya mambo kinyume kabisa na madai yao. Sasa hapa mimi nitataja mifano kadhaa: Wanadai kwamba, sisi tunafungamana na suala la haki za binaadamu. Ndio, Wamarekani wamenyanyua juu bendera ya haki za binaadamu, wanasema sisi tunafungamana na suala la haki za binaadamu; tena sio katika nchi yao tu - yaani ndani ya Marekani - bali duniani kote. Vizuri, haya ni maneno na ni madai, (hebu tuje sasa na tutazame je) katika amali na katika vitendo hali ikoje? Tukirejea katika vitendo (vya viongozi hao wanaodai kuwa wanafungamana na suala la haki za binaadamu) tunaona kuwa, wao wamekuwa wakiukaji wakubwa zaidi wa haki za binadamu ulimwenguni; wamekuwa watu wanaovunjia heshima zaidi haki za binaadamu katika nchi mbalimbali na kwa wananchi wa mataifa tofauti ulimwenguni. Magereza yao ya siri katika pembe na maeneo mbalimbali duniani, gereza lao la Guantanamo, gereza lao huko Iraq - Abu Ghuraib -, hujuma na mashambulio yao dhidi ya raia nchini Afghanistan, Pakistan na katika maeneo mbalimbali ulimwenguni; hii ni mifano tu (ya wazi kabisa) ya (kuheshimu na kufungamana na suala la) haki za binaadamu zinazodaiwa na Wamarekani! Ndege zao zisizo na rubani hufanya ujasusi na wakati huo huo huwashinikiza watu; ambapo kila siku habari za ndege hizo mumekuwa mukizisikia kutoka Afghanistan na Pakistan. Hizi hizi ndege zao zisizo na rubani kama alivyoandika hivi karibuni mwandishi wa jarida moja la Marekani ni kuwa, katika mustakbali zitaitia matatani Marekani na viongozi wake.
Viongozi wa Marekani wanadai kwamba, wanafungamana na suala la kutozalisha silaha za atomiki. Hata kisingizio cha kuishambulia kijeshi Iraq miaka kumi na moja iliyopita kilikuwa hiki hiki. Walidai kwamba, nchini Iraq utawala wa dikteta Saddam Hussain unatengeneza silaha za nyuklia. Tab'an, walikwenda na kutopata silaha hizo na hivyo ikafahamika kwamba, madai yao yalikuwa urongo mtupu (na walikuwa na malengo mengine katika kuishambulia kijeshi Iraq). Wanasema kwamba, sisi tunafungamana na suala la kutozalishwa silaha za nyuklia; wakati huo huo wanauunga mkono na kuusaidia utawala wa shari ambao una silaha za nyuklia na ambao umekuwa ukitishia kutumia silaha hizo hatari (na za maangamizi) yaani utawala wa Kizayuni wa Israel. Sasa tazameni yale ndio maneno yao na hivi ndivyo vitendo vyao. Tazameni wamesema na kutoa madai gani na kile wanachokifanya kwa sasa ni kipi.
Vizuri, wanadai kwamba, wao wanafungamana na suala la kuenea demokrasia duniani - sasa sisi hatuna kazi na kwamba, demokrasia ya Marekani yenyewe ni demokrasia ya aina gani; hatufanyi mjadala katika uwanja huu - kwa madai haya Marekani imekuwa ikipingana na kukabiliana na nchi kama Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambayo ina demokrasia ya wazi kabisa ya wananchi kuwa na nafasi katika maamuzi ya nchi katika Mashariki ya Kati; Marekani hiyo hiyo ambayo inapingana na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, inasimama nyuma na kuzitetea baadhi ya nchi katika Mashariki ya Kati ambazo wananchi wake hawajawahi kunusa harufu ya demokrasia na wala wananchi wake hawajawahi kushiriki katika uchaguzi hata mara moja kwa ajili ya kuwachagua viongozi wao. Hhivyo basi, huku ndiko kufungamana kwa viongozi wa Marekani na kadhia ya demokrasia! Tazameni kuna pengo (tofauti kubwa) kiasi gani baina ya maneno na vitendo vyao.
Wanadai kwamba, tunataka kutatua masuala yetu na Iran. Haya ni maneno tu ambayo wameyasema mara kadhaa, hivi karibuni sasa wamekuwa wakiyasema na kuyakariri zaidi. Wanasema, tunataka kufanya mazungumzo na kutatua mambo yetu na Iran - haya ndio maneno na madai yao - lakini katika amali na vitendo wamekuwa wakifungamana na vikwazo, propaganda na maneno yasiyofaa. Wamekuwa wakieneza mambo ambaayo ni kinyume kabisa na uhakika wa mambo kuhusiana na Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu na taifa la Iran.
Siku chache zilizopita, Rais wa Marekani alizungumzia suala la nishati ya nyuklia ya Iran kwa namna ambayo utadhani hitialfu baina ya Iran na Marekani ni kuwa, Iran inataka kutengeneza silaha za nyuklia. Alisema kuwa, sisi tutajitahidi kadiri tunavyoweza ili tusiruhusu Iran itengeneze silaha za nyuklia! Vizuri, kama sisi tungekuwa tunataka kutengeneza silaha za nyuklia, vipi nyinyi mngeweza kutuzuia? Kama Iran ingeazimia kutengeneza silaha za nyuklia, katu Marekani isingekuwa na ubavu wa kuizuia Iran kufanya hivyo.
Sisi hatutaki kutengeneza silaha za nyuklia; sio kwamba, kwa sababu kufanya hivyo kunaiudhi Marekani; la hasha, bali hatufanyi hivyo kwa mujibu wa imani na itikadi yetu. Sisi tunaamini kwamba, silaha za nyuklia ni jinai dhidi ya binaadamu hivyo haipasi (si sahihi) kuzalisha silaha hizi; na silaha za nyuklia ambazo tayari zipo duniani zinapaswa kutokomezwa na kuangamizwa; hii ndio itikadi yetu na wala haikuhusuni nyinyi. Hata hivyo (tambueni kwamba) kama sisi tusingekuwa na itikadi hii na kuchukua uamuzi wa kutengeneza silaha za nyuklia basi hakuna nguvu yoyote ambayo ingeweza kutuzuia kufikia hilo; kama ambavyo hawajaweza kuzuia hilo katika maeneo mengine duniani: hawakuweza kulizuia hilo nchini India, hawakuweza kulizuia hilo nchini Pakistan na hawakuweza kukwamisha hilo huko Korea ya Kaskazini. Wamarekani walikuwa wanapinga, lakini nchi hizo ziliweza kutengeneza silaha za nyuklia (na zinamiliki silaha hizo hadi sasa).
Hii kwamba, wanasema "sisi haturuhusu Iran kutengeneza silaha za nyuklia" ni kughushi katika kuzungumza. Kwani suala ni silaha za nyuklia? Katika kadhia ya nyuklia ya Iran, suala sio silaha za nyuklia; suala hapa ni kwamba, nyinyi (Marekani na waitifaki wenu) mnataka kuizuia haki kamili na ya wazi ya taifa la Iran - ambayo ni kurutubisha madini ya urani na kustafidi na nishati ya nyuklia kwa matumini ya amani tena kwa kutumia wataalamu wa hapa hapa ndani - huu ndio uhakika wa mambo. Tab'an, hili pia hamuwezi kulifanya kwani taifa la Iran (limesimama kidete) na litafanya kile ambacho ni haki yake (na wala msidhani kwamba, litalegeza kamba na kufumbia macho haki yake hii ya kimsingi na ya wazi kabisa).
Viongozi wa Marekani wanazungumza bila ya (kutumia) mantiki. Kwa hakika mtu hawezi kukaa na kuzungumza kwa mantiki na mtu ambaye hazungumzi kwa kutumia mantiki; kwa sababu mtu huyo sio wa kutumia mantiki. Kutokuwa na mantiki maana yake ni mtu kutumia mabavu katika mazungumzo na kuzungumza mambo yasio na maana. Huu ni ukweli na uhakika ambao tumeupata katika kipindi chote hiki cha miaka thelathini cha kuamiliana na kadhia mbalimbali ulimwenguni. Kwa hakika sisi tunafahamu vyema kwamba, tunakabiliana na nani na ni namna gani tunapaswa kuzungumza pamoja na kuamiliana mtu huyo.
Kuna nukta kadhaa nimezinakili na nitatumia fursa hii kukubainishieni nyinyi makaka na madada wapendwa na taifa la Iran kwa ujumla kuhusiana na masuala mbalimbali. Tab'an, maneno haya ni kwa ajili ya taifa la Iran.
Wale ambao wanasema, Rais wa Marekani ambaye anasema, washirika na waitifaki wake kutoka katika serikali ya Marekani lengo lao ni kwa ajili ya kuzihadaa fikra za waliowengi; sasa iwe ni fikra za waliowengi ulimwenguni au fikra za waliowengi katika mataifa ya Mashariki ya Kati; au kama wataweza wazihadae fikra za wananchi wa taifa letu. Kwa sasa sisi hatuna kazi na fikra za waliowengi ulimwenguni. Kanali zinazofungamana na Wazayuni - Wamarekani hawaakisi maneno yetu kama ilivyo (yaani wanapotosha); au hawaakisi kabisa, au wanaakisi nusu nusu au wanaakisi kinyume kabisa na ukweli wa mambo ulivyo. Mimi ninazungumza kwa ajili ya wananchi wa taifa letu na kuhusiana na wananchi wetu. Uwezo na nguvu za Jamhuri ya Kiislamu hazihusiani na fikra za waliowengi ulimwenguni. Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haikupata nguvu zake, uwezo wake, izza yake na heshima yake kutoka kwa fikra za waliowengi ulimwenguni; bali imepata yote haya kutoka kwa wananchi hawa. Lile jengo imara na madhubuti ambalo taifa la Iran imelijenga na hii leo linaeneza ujumbe wake mfululizo kwa walimwengu wote linaegemea na kuwategemea wananchi wenyewe. Mimi ninazungumza kwa ajili ya wananchi wetu na kuhusiana na wananchi wetu, sina kazi na watu wengine; wasikilize au wasisikilize shauri yao; wakitaka waliakise au wasiliakisi, hilo ni juu yao; lakini la msingi ni kuwa hili ni jambo ambalo wananchi wetu azizi wanapaswa kulifahamu. Hivyo basi nukta ya kwanza ni hii kwamba, watu hawa sio wa (wa kutumia) mantiki, wanazungumza mambo bila ya kuwa na itikadi nayo na maneno yao na vitendo vyao katu havilingani au kwenda sambamba, bali kuna tofauti baina ya maneno na vitendo vyao.
Nukta ya pili: Wamekuja (Wamarekani) na suala la mazungumzo kwamba, Iran njoo tukae chini na tuzungumze. Katika wito wao huu huu wa kutaka kufanya mazungumzo na Iran kuna vitendo na muamala usio wa (kutumia) kimantiki ambao unashuhudiwa. Lengo lao sio kutatua matatizo (kama wanavyodai) - ambapo baadaye mimi nitatoa ufafanuzi wa hili - bali lengo lao ni (kuendesha) propaganda. Wanataka kuyaonyesha mataifa ya Kiislamu kwamba, tazameni huu mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu pamoja na ungangari wake na kusimama kwake kidete, umelazimika kuja katika meza ya mapatano na mazungumzo na sisi. Wakati taifa la Iran liko namna hii nyinyi mnasema nini? Haya ni mambo ambayo maadui hawa wanahitajia kwa ajili ya kuzima wimbi na kuyakatisha tamaa mataifa ya Kiislamu ambapo leo katika akthari ya nchi za Kiislamu kunashuhudiwa upepo na vuguvugu la mwamko. Wananchi wa mataifa ya Kiislamu hii leo wanahisi kuwa na izza kutokana na Uislamu. Kwa hakika tangu mwanzoni mwa mapinduzi, hili ndilo lililokuwa moja ya malengo (makuu) ya maadui. Kuanzia katika kipindi cha miaka ya mwanzo ya mapinduzi, moja ya malengo ya maadui lilikuwa ni kuifanya Iran ikae na wao katika meza ya mapatano na hivyo kujadiliana kwamba, Iran itoe nini ili ipate nini; hivyo basi propaganda zao za leo ni kutaka kusema kwamba, si mnao Iran ambayo ilikuwa ikidai kwamba, inajitawala, imesimama kidete, iko ngangari haiogopi na ni shujaa, sasa imelazimika kuja na kukaa katika meza ya mazungumzo (na Marekani). Hii leo leo wanafuatilia lengo hili hili. Hili ni jambo muhimu. Wakati lengo la mazungumzo linapokuwa ni lengo lisilohusiana na masuala ya kimsingi, bali lengo lake ni propaganda, bila shaka inaeleweka wazi kwamba, upande wa pili ambao ni Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haujala na sio kipofu, bali unafahamu lengo lenu ni lipi; hivyo basi unakupeni jibu kulingana na nia yenu mliyonayo.
Nukta ya tatu ni hii kwamba, mazungumzo katika ada na mazoea ya Wamarekani na madola ya kibeberu maana yake ni kwamba, njooni tukae na tuzungumze ili mkubali maneno yetu - hili ndilo lengo la mazungumzo - njooni tukae na tuzungumze ili natija ya mazungumzo hayo iwe hii kwamba, hatimaye yale mambo ambayo huko nyuma mlikuwa hamyakubali sasa muyakubali. Kuanzia hivi sasa katika propaganda zilizoanzishwa na Wamarekani kuhusiana na mazungumzo - ambapo ni muda sasa wameanza kupiga makelele haya bila shaka mumeyasikia - na wamekuwa wakisema tunataka mazungumzo ya moja kwa moja na Iran, tufanye hivi na vile, katika maneno haya haya maana hii tuliyoisema inashuhudiwa kikamilifu: yaani njooni tukae ili tuikinaishe Iran iache kurutubisha madini ya urani; iachane na nishati ya nyuklia. Hili ndilo lengo. Hawasemi kwamba, njooni tukae na tufanye mazungumzo ili Iran ibainishe hoja zake na sisi tuache kuishinikiza kuhusiana na suala la nishati ya nyuklia, tuache kuiwekea vikwazo, tuache kuingilia masuala yake ya ndani ya kiusalama, kisiasa na kadhalika; bali wanasema, njooni tukae na kufanya mazungumzo ili Iran ikubaliane na kile tunachotaka sisi!
Vizuri, mazungumzo ya namna hii hayana faida wala maana yoyote; mazungumzo kama haya hayawezi kufikia popote. Tujaalie kwamba, serikali ya Iran imekubali na ikaenda kisha ikakaa nao na kufanya mazungumzo na Wamarekani. Wakati lengo linapokuwa ni hili, mazungumzo haya yatakuwa ni mazungumzo gani?, vizuri, bila shaka inaeleweka wazi kwamba, Iran katu haiwezi kufumbia macho haki zake. Pindi wahusika wakati wa mazungumzo wanapoona kwamba, upande wa pili unazungumza maneno ya (kutumia) mantiki na wao wanapwaya mkabala na Iran, hukatisha mazungumzo hapo hapo; kisha hudai kwamba, Iran haiko tayari kuzungumza! Kanali za habari na duru za kisiasa nazo ziko pamoja na wao; zinafanya propaganda. Hili ni jambo ambalo sisi tuna tajiriba nalo. Katika kipindi hiki cha miaka kumi au kumi na tano iliyopita, imetokea mara mbili au mara tatu ambapo Wamarekani waliwatumia ujumbe viongozi wetu wa nchi kuhusiana na jambo fulani, wakasisitiza na kung'ang'ania kwamba, ni jambo muhimu, la dharura na la haraka mno hivyo njooni tukae na tuzungumze. Vizuri, maafisa wa serikali wakaenda na kukaa sehemu fulani na kuzungumza nao; baada ya maafisa hao kubainisha maneno yao ya kimantiki, upande wa pili haukuwa na jibu, wakakatisha mazungumzo kwa upande mmoja! Tab'an, walistafidi kipropaganda na jambo hilo. Hii ni tajiriba tuliyonayo.
Nukta ya nne: Katika propaganda wanataka kuonesha kwamba, kama Iran itakaa katika meza moja ya mazungumzo na Marekani, vikwazo vitaondolewa. Huu nao ni urongo mtupu. Lengo lao ni kuwa, kwa kutumia ahadi za kuiondolea vikwazo Iran, ilishajiishe taifa hili na suala la kufanya mazungumzo na Marekani. Wao wanadhani kwamba, taifa la Iran limeshachoshwa na vikwazo na kila kitu kimevurugika; hivyo sisi tuseme, vizuri sana, njooni basi tufanye mazungumzo ili mtuondolee vikwazo.
Maneno haya pia ni miongoni mwa yale maneno yasiyo ya kimantiki na ambayo yanaambatana na hila, makri na mafamba na unatumiwa kama wenzo wa utumiaji mabavu. Kwanza - kama tulivyosema - hii kwamba, wanasema, njooni tufanye mazungumzo, lengo lao la mazungumzo, kwa hakika sio mazungumzo ya kiadilifu na kimantiki; mazungumzo wanayoyakusudia maana yake ni njooni mkubali mambo yetu, matakwa yetu na msalimu amri ili sisi tukuondoleeni vikwazo. Vizuri, kama taifa la Iran lilikuwa linataka kusalimu amri, basi kwa nini limefanya mapinduzi? Marekani ilikuwa ikidhibiti mambo nchini Iran na ilikuwa ikifanya kila inachotaka. Taifa la Iran limefanya mapinduzi ili liondokane na gogoo na mkatale wa Marekani; sasa waje na kisha wakae na kusalimu amri tena? Hili ni tatizo (ishkali) la kwanza.
Tatizo (ishkali) jingine ni kwamba, vikwazo hivi havitoondolewa kwa mazungumzo; hili ni jambo ambalo ninawaambia. Lengo la vikwazo ni kitu kingine. Lengo la vikwazo ni kuwachosha wananchi wa Iran na kuwatenganisha wananchi na Mfumo wa Kiislamu. Endapo mazungumzo yatafanyika, endapo taifa la Iran litaendelea kubakia uwanjani na kung'ang'ania haki zake, hapana shaka kuwa, vikwazo hivi vitaendelea kuweko. Taifa la Iran linafanya nini mkabala na fikra hii ghalati na potofu ya adui?
Tizameni, katika fikra na akili za pande ambazo zinakabiliana na sisi kuna hali ya kuzingatia mambo ambayo tunapaswa kuifungua na kuichambua. Wao wanasema kuwa, Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu unategemea nguvu ya wananchi na kwamba, kama tutaweza kuwatenganisha wananchi na Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu basi nguvu ya kusimama kidete mfumo huu wa Kiislamu itaondoka. Hii ni fikra mbayo wanayo watu wanaokabiliana na sisi. Vizuri, fikra hii ina makole mawili; kole la kwanza ni upande ambao wameufahamu sahihi na kole la pili ni upande ambao wameufahamu kimakosa. Upande ambao wameufahamu sahihi ni huu kwamba, mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu umeegemea nguvu ya wananchi; hakuna kinga (imara na madhubuti) ya mfumo wa Kiislamu kama majimui adhimu ya wananchi wa taifa la Iran; ngao na tegemeo la nchi hii na mfumo huu (Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu unaotawala hapa nchini) ni hawa wananchi. Amma kile ambacho wamekifahamu kimakosa (ghalati) ni hiki kwamba, wanadhani kuwa, kwa mashinikizo ya vikwazo, kwa kutumia mabavu katika masuala ya kimataifa, masoko, uzalishaji na kadhalika, wataweza kulifanya taifa la Iran lipige magoti na lishindwe kufanya kitu. Kama wanadhani kwamba, wataweza kuipokonya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hii kinga na ngome (yaani himaya na uungaji mkono wa wananchi), kwa hakika wanakosea.
Ndio, taifa la Iran litafanya tadbiri mkabala na kile ambacho adui anataka kukifanya. Taifa la Iran linafuatilia kuchanua uchumi, ustawi wa kiuchumi na ustawi kamili; lakini taifa la Iran halitaki kulipata hili kupitia njia ya kudhiliwa (madhila) mkabala na adui; bali linataka kulifikia hili kwa nguvu yake, azma yake, irada yake, ushujaa wake, usongaji mbele wake na kwa nguvu zake; na sio kinyume chake. Ndio, vikwazo ni mashinikizo, na maudhi - hakuna shaka katika hilo - lakini kuna njia mbili katika kukabiliana na mashinikizo na maudhi haya. Kwa mataifa dhaifu pindi adui anapotoa mashinikizo huwenda na kusalimu amri mbele ya adui, hunyenyea na kutubu mbele ya adui huyo. Lakini kwa mataifa ambayo ni shujaa kama Iran, pindi linapoona adui anatoa mashinikizo, hufanya hima ya kuifanya nguvu yake ya ndani kuwa amilifu na kukusanya nguvu na hivyo kufanikiwa kupita eneo la hatari kwa nguvu na ushujaa; na kwa hakika hii ni kazi ambayo itafanywa na wananchi wa Iran. Hii ni tajiriba na uzoefu wetu (tulioupata) wa miaka thelathini.
Kuna nchi katika eneo letu hili hili ambazo zilikuwa katika udhibiti wa Marekani kwa miaka thelathini na ushei, serikali zao zilikuwa vibaraka, vikaragosi ambavyo vilikuwa vikitii kila amri ya Marekani; ziko wapi nchi hizo? Taifa la Iran pia kwa miaka thelathini na ushei limesimama kidete mbele ya Marekani; taifa la Iran liko wapi sasa? Katika kipindi hiki hiki cha miaka thelathini ya mashinikizo ya Marekani, taifa la Iran limepiga hatua kwa upande wa maendeleo ya kielimu, ustawi wa kiuchumi, maendeleo ya kiutamaduni, heshima katika uga wa kimataifa, satua na ushawishi pamoja na nguvu za kisiasa kiasi kwamba, katika kipindi cha tawala za Kifalme za Kipahlavi na Kiqajar haya ni mambo ambayo hayakuwa hata yakifikiriwa ndotoni, si wananchi wala viongozi. Sisi tuna tajiriba na tumefanya majaribio katika uwanja huu. Sisi tumesimama kidete kwa muda wa miaka thelathini mkabala na mashinikizo ya Marekani, na tumefikia hapa tulipo; kuna mataifa ambayo pia yamesalimu amri mbele ya Marekani kwa miaka thelathini na hivi sasa yako nyuma kwa marhala na hatua kadhaa. Kwa hakika sisi hatujaona baya katika kusimama kidete na katika kufanya muqawama (na kutokubali kunyongeshwa). Kwa hakika muqawama unahuisha nguvu ya ndani ya taifa na kuifikisha katika hatua amilifu. Hivi hivi vikwazo wanavyoweka vitalisaidia taifa la Iran na kwa idhini ya Mwenyezi Mungu na tawfiki yake, Inshallah taifa hili litafikia ustawi na maendeleo. Hii ni nukta muhimu.
Vizuri, mwaka huu mumeona wananchi wamefanya nini katika maandamano ya tarehe 22 Bahman (siku ya kukumbuka ushindi wa mapinduzi ya Kiislamu). Haiwezekani kusema kwamba, wananchi hawana malalamiko na manung'uniko kutokana na matatizo ya ughali wa maisha; kwani ni kweli kwamba, kuna ughali wa maisha na kuna matatizo ya kiuchumi na wananchi wamekuwa wakilihisi hilo - hususan tabaka la chini - lakini jambo hili halijapelekea wananchi kujitenga na Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu (unaotawala hapa nchini). Wananchi wanafahamu kwamba, nguvu inayoweza kutatua matatizo ni Mfumo wa Kiislamu; ni Uislamu azizi na Uislamu wenye nguvu na wenye kutambua majukumu ambao wao wameshikamana nao; haya ndio mambo ambayo yanaweza kutatua matatizo haya. Kusalimu amri mkabala na maadui ni jambo ambalo haliwezi kutatua matatizo.
Nukta ya mwisho: Kinyume na wao sisi ni watu wa mantiki. Maafisa na viongozi wetu ni watu wa kimantiki na wananchi wetu ni watu wa kimantiki. Sisi tunayakubali maneno ya kimantiki na kazi ya kimantiki. Wamarekani waonyeshe kwamba, hawana ubabe (hawasemi kwa ubabe na kutaka mambo yao tu yatejelezwe), waonyeshe kwamba, hawataki ushari, waonyeshe kwamba, hawazungumzi wala kufanya mambo yasiyo ya kimantiki, waonyeshe kwamba, wanaheshimu haki za taifa la Iran, waonyeshe kwamba, hawachochei mambo katika Mashariki ya Kati, waonyeshe kwamba, hawaingilii masuala ya ndani ya Iran; waache kuingilia mambo kama walivyofanya katika fitina ya mwaka 1388 (Juni 2009), wasitoe himaya na uungaji mkono kwa wafanya fitina, kwa mitandao na kanali za kijamii ambazo zinahudumia wafanya fitina - kuna mtandao na kanali ambayo katika kipindi hicho ilitaka kufungwa kwa ajili ya matengenezo, wakasema msiifunge; ili iweze kuwa na taathira katika fitina na kuwasha moto wa fitina! - waache kufanya mambo haya, wataona kwamba, Jamhuri ya Kiislamu ni mfumo unaotaka kheri; na wananchi wake ni wananchi wa kutumia mantiki. Njia ya kuamiliana na Jamhuri ya Kiislamu ni hizi njia nilizozitaja na sio ghairi ya hizi; kupitia njia hii wanaweza kuamiliana na Jamhuri ya Kiislamu. Wamarekani wanapaswa kuthibitisha kama kweli wana nia njema; waonyeshe kwamba, hawataki kutumia mabavu. Kama wataonyesha hayo, wakati huo wataona taifa la Iran litatoa jibu gani. Kusiweko na ushari, kusiweko na hali ya kuingilia mambo, kusiweko na utumiaji mabavu, kuweko na hali ya kutambuliwa haki za taifa la Iran, wakati huo Iran itatoa jibu mwafaka.
Niseme pia nukta nyingine hapa kuhusiana na masuala ya ndani ya nchi yetu ambapo suala hili nalo ni muhimu. Kumejitokeza jambo katika Bunge; kwa hakika kadhia hiyo ilikuwa mbaya na wala haikuwa kadhia inayofaa hata kidogo; wananchi wamechukizwa na jambo hilo na hata wenye vipawa hapa nchini hawajapendezwa hata kidogo na jambo hilo. Kwa upande wangu mimi nimechukia katika pande mbili: binafsi nimehisi kuathirika mno na kadhia hii; na nimechukia kutokana na wananchi kuchukia na kuhuzunika kutokana na kadhia hii. Vizuri, tuhuma dhidi ya mmoja wa wakuu wa Mihimili Mitatu Mikuu ya Dola (Serikali, Bunge na Mahakama) hazikuthibitika kupitia ushahidi fulani na jambo hilo halikupelekwa mahakamani, nguzo mbili za dola zinatuhumiana; hiki kilikuwa kitendo kibaya na kisichofaa hata kidogo; vitendo kama hivyo ni kinyume cha sharia na kinakinzana kabisa na kanuni na vile vile kinakwenda kinyume na maadili na wakati huo huo ni kukanyaga haki za kimsingi za wananchi.
Moja ya haki muhimu za kimsingi za wananchi ni kwamba, waishi katika mazingira tulivu kifikra na wawe na amani ya kifikra na kisaikolojia; nchini usalama wa kimaadili utawale. Kama kuna mtu anatuhumiwa kwa kufanya ufisadi, haifai kuwatuhumu watu wengine kwa sababu ya mtu huyo; hata kama itathibiti, seuze kama tuhuma zenyewe bado hazijathibitishwa, kesi haijapelekwa mahakamani na wala hukumu haijatolewa. Kwa sababu ya kumtuhumu mtu mmoja, mtu aje na kuwatuhumu watu wengine, alituhumu Bunge na kukituhumu Chombo cha Mahakama; kwa kweli hiki sio kitendo sahihi, hiki ni kitendo ghalati na kisicho sahihi hata kidogo.
Binafsi kwa sasa natumia fursa hii kutoa nasaha tu. Kitendo hiki sio kitendo kinachofaa kwa Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu. Upande ule wa kadhia nao, asili ya usaili Bunge ambao umefanyika haukuwa sahihi. Usaili (kuitwa waziri na kusailiwa Bungeni) unapaswa kuwa na faida. Kufanya usaili na kumuita waziri Bungeni na kumsaili ikiwa imebakia miezi michache tu kabla ya muda wa serikali kumalizika tena kwa dalili na sababu ambayo haihusiani na waziri husika, kuna maana gani? kwa nini? Hili nalo lilikuwa kosa. Mambo yote haya ni mambo ambayo hayanasibiani na Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu; sio kule kutoa tuhuma, sio kule jinsi watu walivyoamiliana na jambo hilo na wala sio usaili; yote haya yalikuwa ni makosa na mambo ambayo kwa hakika hayanasibiani na Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu. Utetezi pia ambao ulifanywa na Spika wa Bunge kwa ajili ya kujitetea nao kwa namna fulani ulivuka mipaka; hakukuwa na haja ya kufanya hivyo.
Wakati sisi sote ni ndugu na wakati huo huo tuna adui wa pamoja ambaye yuko mbele yetu na wakati tunaona kuna njama, tunapaswa kufanya nini? Hadi leo maafisa na viongozi wamesimama kidete tena kwa pamoja katika kukabiliana na njama za adui, sasa hivi pia tunapaswa kuwa namna hii na ni lazima tuwe namna hii. Mimi daima nimekuwa nikiwaunga mkono wakuu wa Mihimili Mitatu Mikuu ya Dola pamoja na maafisa na viongozi wa serikali; na vile vile nitaendelea kumuunga mkono mtu yeyote ambaye atachukua jukumu la kuiongoza nchi na nitamsaidia; lakini sipendi mambo haya; mambo haya na vitendo hivi havinasibiani kabisa na viapo vilivyotolewa. Kwa hakika taifa hili adhimu na wananchi hawa hawastahiki mambo kama haya. Hii leo maafisa na viongozi wa serikali wanapaswa kufanya kila wawezalo kutatua matatizo ya kiuchumi na kuyapatia ufumbuzi mambo haya.
Miaka mitatu au minne iliyopita, nilisema wazi na bayana katika mazungumzo na hotuba yangu ya mwanzo wa mwaka kwa kuwaambia maafisa na viongozi wa serikali kwamba, mkakati wa maadui wa taifa la Iran kuanzia sasa na kuendelea ni katika uga wa kiuchumi. Vizuri, mnaona mambo yamekuwa kama nilivyosema. Serikali, Bunge na nguvu zake zote, wote hawa wanapaswa kukita nguvu zao katika (kuboresha) sera sahihi za kiuchumi. Miaka kadhaa iliyopita niliwaandikia barua Wakuu wa Mihimili Mitatu Mikuu ya Dola kuhusiana na suala la ufisadi wa kiuchumi. Kwa hakika mambo hayamaliziki kwa kusema maneno matupu tu; pigeni vita ufisadi wa kiuchumi kivitendo. Sio tuseme tu, tupambane na ufisadi wa kiuchumi. Vizuri, vita dhidi ya ufisadi viko wapi? Kivitendo hali ikoje? Mumefanya nini? Haya ndio mambo ambayo yanamuathiri sana mtu. Matarajio yangu kutoka kwa maafisa na viongozi kwamba, hivi sasa ambao muamala wa adui umeshika kasi, ni nyinyi kuongeza urafiki na udugu na kuweni pamoja zaidi. Taqwa, taqwa, taqwa, subira, kutoruhusu mambo yasiyofaa, kuzingatia maslahi ya nchi na kutumia nguvu zote kwa ajili ya kutatua matatizo ya nchi na ya wananchi; haya ndio matarajio yetu (kutoka kwa maafisa na viongozi wa serikali). Tuna matarajio kwamba, Inshallah nasaha hizi za kutaka kheri zitazingatiwa na waheshimiwa viongozi wa nchi hususan viongozi wa ngazi za juu; wafungamane na suala hili.
Napenda kusema hapa pia kwamba, maneno haya ambayo mimi nimeyazungumza leo na kuonyesha manung'uniko yangu niliyonayo kwa baadhi ya maafisa na viongozi wa nchini, yasipelekee watu fulani kuwaandama wengine na waanze kupiga nara dhidi ya huyu na yule; hapana, mimi ninapinga mambo haya. Hii kwamba, nyinyi mumuainishe mtu mmoja na kumpa jina la dhidi ya Wilaya, dhidi ya muono wa mbali, dhidi sijui ya kitu gani; halafu kikundi fulani cha watu kije na kuanza kupiga nara dhidi yake na hivyo kulivuruga Bunge, mimi ninapinga mambo haya; hili ni jambo ambalo mimi ninalisema wazi kabisa. Mambo yaliyotokea mjini Qum ni mambo ambayo mimi ninayapinga kabisa. Mambo yaliyotokea katika Haram ya Imam Khomeini (Radhiallahu an'hu) ni mambo ambayo mimi sikubaliani nayo.
Nimewakumbusha mara chungu nzima maafisa na viongozi wa serikali ambao wanaweza kuzuia kutokea mambo kama haya. Watu ambao wanafanya mambo haya, kwa hakika kama ni waumini na wafuasi wakweli wa Mwenyezi Mungu, vizuri, waache kufanya haya. Bila shaka mumeona kuwa, maamuzi yetu kwamba, mambo haya ni kwa madhara ya nchi ni ya kweli kabisa; haya ni mambo ambayo hayana maslahi na nchi. Watoke huku na kule na wapige nara kwa hisia zao dhidi ya huyu na yule; kwa hakika kupiga nara huku hakupeleki mbele mambo. Hizi ghadhabu na hizi hisia ziwekeni kwa ajili ya sehemu nyingine ya lazima.
Katika kipindi cha kujitetea kutakatifu kama Mabasiji wangetaka kwenda sehemu fulani hivi hivi na kwenda kushambulia mahala kwa shauku na matamanio yao, bila shaka wangepata shida. Nidhamu ni jambo la lazima na kufanya mambo kwa mipango ni jambo la dharura. Hivyo kuna haja ya kuzingatia mambo. Kama kuna watu ambao hawazingatii maneno haya, hawa hesabu yao iko kando; lakini watu ambao wanazingatia maneno haya na wanafungamana nayo wasifanye harakati kinyume na uwiano wa kisheria, bali wanapaswa kujichunga na wasifanye mambo haya.
Tab'an, taifa la Iran kwa huba na mapenzi ya Mwenyezi Mungu na kwa hidaya Yake ni taifa ambalo lina muono wa mbali. Napenda kuwaambia vijana kwamba, kipindi ambacho sisi hatutakuweko na nyinyi mtakuweko, tambueni kwamba, siku hiyo hali ya taifa la Iran, muelekeo wake na maisha yake ya kimaada na kimaanawi yatakuwa bora zaidi ikilinganishwa na leo. Harakati ya taifa la Iran ni kuelekea upande unaong'ara na mielekeo ni yenye kung'ara. Kwa hakika sisi kwa namna fulani tunapaswa kujichunga.
Kwa hakika sisi tunapaswa kumuomba Mwenyezi Mungu Mtukufu atusaidie; tunapaswa kuomba msaada kwa roho takasifu za mashahidi na roho takatifu ya Imam wetu wa shani (Imam Khomeini MA). Inshallah sisi na nyinyi tutajumuishwa pamoja katika dua za Mtukufu Baqiyatullah al-A'adham (Imam Mahdi roho zetu ziwe fidia kwake).
Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

 
< Nyuma   Mbele >

^