Skip to content

Habari

Habari
Hifadhi

Risala na Barua

Matini
Hifadhi

Kumbukumbu na Simulizi

Kabla ya Mapinduzi
Baada ya Mapinduzi

Sauti na Taswira

Picha
Sauti
Video
Hotuba ya Kiongozi Muadhamu katika Maadhimnisho ya Kukumbuka Siku Aliyofariki Dunia Imam Khomeni MA Chapa
03/06/2012

Katika Haram Tukufu ya Imam Khomeini (Rahimahullah)
Karibu na maadhimisho ya siku ya kuzaliwa Amirul Muminin, Imam Ali AS

Bismillahir Rahmanir Rahim

Hamdu zote zinamstahikia Allah, Rabbi wa viumbe pia. Na rehema na amani ziwe juu ya Bwana wetu na Nabii wetu na kipenzi cha nyoyo zetu na tabibu wa nafsi zetu, Abil Qasim al Mustafa Muhammad na Aali zake wema na watoharifu na masahaba wake bora na wateule na kila anayewafuata kwa wema hadi siku ya Kiyama. Na rehema ziwe juu ya Baqiyyatullah (Imam Mahdi AS) katika ardhi ambaye kupitia kwake, Mwenyezi Mungu ataijaza ardhi usawa na uadilifu kama itakavyokuwa imejaa dhulma na uonevu.
Mwenyezi Mungu Mwingi wa hekima amesema katika Kitabu Chake:

بسم‌اللّه‌الرّحمن‌الرّحيم. وَتَوَكَّلْ عَلَى الْعَزِيزِ الرَّحِيمِ. الَّذِي يَرَاكَ حِينَ تَقُومُ. وَتَقَلُّبَكَ فِي السَّاجِدِينَ. إِنَّهُ هُوَ السَّمِيعُ الْعَلِيمُ.

Kwa jina la Allah Mwingi wa rehema Mwenye kurehemu. Na umtegemee Mtukufu Mwenye nguvu Mwenye kurehemu. Ambaye anakuona unaposimama, Na mageuko yako kati ya wanaosujudu. Hakika Yeye Ndiye Mwenye kusikia Mwenye kujua. (ash Shua'raa 26 : 217 - 220).
Ninamshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa kutupa fursa nyingine ya kuweko na kukutana tena katika Haram hii ya Imam, Kiongozi, nahodha na ‘murshidi' mkubwa wa taifa hili kwa ajili ya kutangaza kwa mara nyingine uaminifu na utiifu wetu kwa Imam wetu mtukufu, kusoma upya sira na darsa za Imam - ambazo ni darsa za Mapinduzi - na kwa ajili ya kuitia nuru na kuiweka wazi zaidi njia ya mustakbali wetu na kurekebisha penye makosa.
Siku hizi zinasadifiana pia na sikukuu za kukumbuka kuzaliwa kulikojaa baraka kwa Amirul Muminin (Imam Ali) AS ambaye ni baba wa umma. Wananchi wetu wameiita tarehe 13 Rajab kuwa ni "Siku ya Baba." Imam wetu mtukufu (Imam Khomeini) amelifanyia mambo mengi makubwa taifa hili na ana haki ya ubaba kwa taifa na kwa nchi hii. Baba wa umma maana yake ni dhihirisho la upole na huruma. Baba umma maana yake ni kigezo cha kusimama imara, nguvu, kuoneshga shakhsia bora, uimara wa shakhsia ya baba sambamba na mapenzi na huruma zake kwa wanawe. Fauka ya hayo yote, Imam (Khomeini) ni baba wa harakati ya Kiislamu ya leo hii katika ulimwengu wa Kiislamu. Moja ya njia kuu katika sira ya Imam na mienendo yake ambayo hapa leo tutaizungumzia na kuijadili kwa uchache sana tu, ni kupuliza roho ya heshima ya taifa katika mwili wa nchi yetu. Nimesema tutaijadili kwa uchache sana tu kwa sababu kujadili harakati adhimu ya Imam ya kupuliza roho ya heshima kwa nchi yetu na kwa taifa letu ni mjadala mpana wenye mashiko madhubuti katika matukio ya kweli kwenye jamii, si mjadala wa kidhahania tu. Nini maana ya heshima? Heshima maana yake ni muundo makini na madhubuti wa ndani ya mtu au ndani ya jamii, muundo ambao unamuwezesha mtu na jamii husika kukabiliana vilivyo na adui, na vikwazo vyote vinavyojitokeza mbele yake, kuwa na nguvu na kuweza kushinda changamoto zote.
Kwa kuanzia napenda kujadili kidogo mafundisho tunayoyapata katika Qur'ani Tukufu. Katika mantiki ya Qur'ani, heshima na utukufu wa kweli na wa ukamilifu ni wa Mwenyezi Mungu na ni wa kila mtu ambaye yumo katika kambi ya Mwenyezi Mungu. Katika Sura ya 35 ya Faatir kwenye sehemu ya kwanza ya aya ya 10, Qur'ani Tukufu inasema: Mwenye kutaka utukufu basi utukufu wote uko kwa Mwenyezi Mungu. Na katika sura ya 63 ya al Munafiqun kwenye sehemu ya mwisho ya aya ya 8, Qur'ani Tukufu inasema: Na Mwenyezi Mungu Ndiye Mwenye utukufu - Yeye, na Mtume Wake, na Waumini. Lakini wanaafiki hawajui. Huo ndio uhakika wenyewe kwamba heshima na utukufu wa kweli ni wa Mwenyezi Mungu na waumini hata kama wanafiki hawalidiriki hilo, na hawajui utukufu na heshima iko wapi, hawajui kitovu cha heshima na utukufu kiko wapi. Katika Suratun Nisaa Mwenyezi Mungu anazungumzia watu ambao wamejifungamanisha na vituo vya nguvu za kishetani kwa dhana kuwa wataweza kupata heshima, nguvu na utambulisho mzuri. Qur'ani Tukufu inasema: Wale ambao huwafanya makafiri kuwa ndio marafiki badala ya Waumini. Je! Wanataka wapate kwao utukufu? Basi hakika utukufu wote ni wa Mwenyezi Mungu. (an Nisaa, 4:139) Yaani hivi hawa watu hawa wanatafuta ufukufu na heshima kutoka kwa mahasimu na watu wanaompinga Mwenyezi Mungu, kutoka kwa maadui wa Mwenyezi Mungu ili wapate nguvu za kidunia? Basi wanapaswa kujua kuwa utukufu na heshima ya kweli iko kwa Mwenyezi Mungu. Katika Suratush Shu'araa Qur'ani Tukufu inatoa ripoti kuhusu majimui ya changamoto zilizowafika Manabii na Mitume wakubwa wa Mwenyezi Mungu - yaani Nabii Nuh, Nabii Ibrahim, Nabii Hud, Nabii Saleh, Nabii Shuaib, Nabii Musa - na kutoa ufafanuzi mpana kuhusu vikwazo na changamoto zilizowakumba Mitume na Manabii hao wakubwa wa Mwenyezi Mungu na kuwafunulia watu ripoti ya kiwahyi kutoka kwa Mola Mlezi. Wakati Mwenyezi Mungu alipotaka kuonesha ushindi wa kambi ya Manabii dhidi ya kambi ya makafiri, ametumia aya ndani ya Qur'ani Tukufu zinazosema: "Hakika katika haya zipo Ishara. Lakini wengi wao hawakuwa wenye kuamini. Na hakika Mola wako Mlezi Ndiye Yeye Mwenye nguvu Mwenye kurehemu." (ash Shu'araa, 26:8-9). Yaani licha ya kwamba kambi ya makafiri ina watu wengi, nguvu ziko mikononi mwao, wana fedha nyingi na wana silaha za kila namna lakini ushindi ni wa kambi ya tawhidi. Katika aya hii tukufu (ya 9) Mwenyezi Mungu anasema, Na hakika Mola wako Mlezi Ndiye Yeye Mwenye nguvu Mwenye kurehemu." Na baada ya Qur'ani Tukufu kutoa ripoti ya changamoto na ushindi mkubwa wa kambi ya tawhidi katika sura hiyo nzima, mwishoni mwa sura hiyo tukufu Mwenyezi Mungu anamwambia Mtume Wake: "Na mtegemee Mwenye nguvu, Mwenye kurehemu." Yaani, tawakkal na mtegemee Mwenyezi Mungu Ambaye Ndiye Yeye anayedhamini ushindi wa haki dhidi ya batili.

وَتَوَكَّلْ عَلَى الْعَزِيزِ الرَّحِيمِ. الَّذِي يَرَاكَ حِينَ تَقُومُ. وَتَقَلُّبَكَ فِي السَّاجِدِينَ. إِنَّهُ هُوَ السَّمِيعُ الْعَلِيمُ.

Na umtegemee Mtukufu Mwenye nguvu Mwenye kurehemu. Ambaye anakuona unaposimama, Na mageuko yako kati ya wanaosujudu. Hakika Yeye ndiye Mwenye kusikia Mwenye kujua. (ash Shu'araa, 26 : 217 - 220).
Anamwambia Mtume Wake: Yeye Mwenyezi Mungu Ndiye msimamiaji wa mambo yake, anamuona wakati wote na anasimamia mambo yake yote kwani إِنَّهُ هُوَ السَّمِيعُ الْعَلِيمُ Hakika Yeye ndiye Mwenye kusikia Mwenye kujua. Hivyo basi mantiki ya Qur'ani ni kuwa heshima, nguvu na utukufu inabidi mtu autafute kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwani utukufu na heshima na nguvu zote ni Zake Yeye tu Mwenyezi Mungu.
Wakati mtu au jamii inapopata fadhila za kuwa na utukufu na heshima hiyo, basi huwa ni kama vile imepata kigingi na ngao madhubuti na inakuwa vigumu kwa maadui kumvunja nguvu mtu na jamii hiyo. Fadhila hizo anapokuwa nazo mtu, humlinda mtu huyo mbele ya ushawishi wa adui. Na kadiri heshima na utukufu huo unapokuwa na tabaka nyingi na nzito ndivyo mtu na jamii hiyo inavyozidi kushuhudia umakini na uimara na kumzuia kabisa adui kupenya ndani yake na hufika mahala ikawa mtu kama ambavyo huhifadhika na ushawishi wa kiuchumi wa adui, huweza pia kushinda ushawishi wa adui mkubwa na wa asili yaani shetani. Wale watu ambao wana heshima za juu juu tu, huwa hawana ule utukufu wa ndani ya nyoyo, wala heshima za dhati na wala tabaka nzito na madhubuti za ndani ya nafsi zao hivyo huwa hawana kinga mbele ya adui ni inakuwa rahisi kwa adui kupenya ndani ya watu hao.
Kuna kisa mashuhuri ambacho kinasema, wakati Alexander Macedonian alipokuwa akipita njiani wakati fulani, watu wote waliacha kazi zao na kuanza kuonyesha heshima zao kwa kumuinamia na kumnyanyukia. Mtu mmoja muumini mwenye taqwa akawa yeye amekaa pembeni hakumsimamia wala hakumnyenyekea wala kumuonyesha heshima zilizokuwa zinaonyeshwa na watu wengine. Alexander alistaajabu na kutoa amri kwa walinzi wake apelekwe mtu huyo mbele yake. Wakampeleka. Akamwambia: Kwa nini hukunisimamia, wala hukuninyenyekea na kunionyesha heshima walizonionyesha watu wengine? Akamjibu akisema: Kwa sababu wewe ni mmoja wa maghulamu na watumishi wangu. Hivyo vipi nikusimamie na kukunyenyekea? Akamuuliza: Kivipi? Akamjibu: Kwa sababu wewe ni mtumwa wa hawaa na ghadhabu za nafsi yako; na hawaa na ghadhabu ni watumwa wangu, mimi ninazidhibiti sifa hizo, mimi nimezishinda sifa hizo.
Hivyo iwapo heshima na utukufu wa nafsi unapokuwa umejengeka matabaka kwa matabaka na kujizatiti vizuri ndani ya nafsi ya mtu, huwa si rahisi kwa shetani kuweza kupenya na kuacha athari zake, wala hawaa za nafsi huwa hazina nafasi ndani ya mtu huyo na wala mtu huyo hawezi kuchezewa na pepesi za ghadhabu za kishetani.
Sisi tumemjua hivi Imam (Khomeini - quddisa sirruh). Katika maisha yake, iwe ni katika Hawza na wakati wa usomeshaji, au ndani ya mapambano mazito au ndani ya masuala ya maongozi ya nchi na taifa - wakati ule alipochukua uongozi wa taifa na kuongoza jamii - wakati wote Imam (Khomeini) alikuwa ni ushahidi na dhihirisho la kweli la aya ya Mwenyezi Mungu inayosema وَتَوَكَّلْ عَلَى الْعَزِيزِ الرَّحِيمِ. Yaani: "Na umtegemee Mtukufu Mwenye nguvu Mwenye kurehemu." (ash Shu'araa, 26:217). Na ni kwa sababu hiyo ndio maana aliweza kufanya mambo makubwa ambayo watu wote walisema mambo hayo yaliwezekana kwa kuja kwake Imam (Khomeini - quddisa sirruh). Sambamba na kwamba yeye alikuwa ni dhihirisho la heshima ya nafsi na nguvu za kimaanawi, alilihuisha na kulifufua pia taifa. Hiyo ndiyo kazi kubwa iliyofanywa na Imam wetu mtukufu; ambapo nami hapa narejea tena kutoa ufafanuzi kuhusu nukta hii. Taifa letu limeweza kujitambua kutokana na masomo liliyopata kutoka kwa Mapinduzi ya Kiislamu na kutoka katika chuo cha Imam. Taifa letu limeweza kujielewa na kugundua dhati yake sambamba na kumaizi na kung'amua uwezo wake. Hivyo ndivyo ilivyojiri na ni kwa sababu hiyo ndio maana sisi tumeweza kushuhudia kutimia ahadi nyingi za Mwenyezi Mungu katika miongo kadhaa iliyopita vitu ambavyo tulikuwa tukivisoma tu katika tarikh na historia na tukiviuona tu kwenye vitabu, lakini sasa tumevishuhudia kwa macho yetu, yaani ushindi wa wanyonge mbele ya mabeberu na waistikbari na udhaifu mkubwa wa makasri ya waistikbari ambayo kwa nje yanaonekana imara sana. Tumeshuhudia mambo mengi sana yanayoonyesha kutimia ahadi za Mwenyezi Mungu katika miongo hii ya hivi karibuni.
Hapa ninapenda kutilia mkazo hili suala la heshima na utukufu wa taifa ili niweze kufikia nukta moja maalumu niliyoikusudia. Leo ni siku kubwa sana. Ni siku ya kukumbuka alipofariki dunia mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Leo hii kumbukumbu za Imam wetu mtukufu ziko hai zaidi kuliko wakati mwingine wowote uliopita. Watu wote wanashuhudia kwa macho yao urithi uliojaa baraka aliotuachia humu nchini na katika ulimwengu mzima wa Kiislamu. Hebu natuangalie baadhi ya vipengee vya uwepo wa harakati hii.
Heshima ya Kitaifa. Sisi Wairani tumeshuhudia hali tofauti katika suala la heshima ya taifa katika kipindi chote cha historia yetu ndefu na katika nyakati tofauti. Kuna wakati tuliwahi kuwa na heshima ya taifa na kuna wakati mwingine tulikuwa na udhalili. Hata hivyo katika kipindi hiki kirefu cha miaka mia mbili iliyomalizikia kwenye ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, kipindi chote hicho kilikuwa kigumu mno katika udhalili lilioushuhudia taifa letu. Kuna wajibu wa kuisoma kwa umakini wa hali ya juu historia na kuzama sana katika matukio ya kihistoria. Inabidi kupata funzo kutoka katika historia. Kwa kweli sisi tumekipitisha kipindi hiki cha miaka 200 ya hivi karibuni kwa madhila kwani kipindi hicho kwetu kilikuwa kimejaa kiza. Ushahidi wa uduni na udhalili huo ni mwingi. Sisi katika kipindi chote hicho tulikuwa ni taifa lililotengwa katika upande wa kisiasa katika masuala yote ya eneo letu hili - hatusemi tena katika masuala ya kimataifa - na hatukuwa na taathira yoyote ile. Katika kipindi hicho cha miaka mia mbili, kulitokezea kitu kinachoitwa ukoloni. Madola ya kikoloni yalikuja katika eneo hili kutoka maeneo ya mbali ya dunia, yakaziteka nchi zetu na kuwafanya mateka watu wake pamoja na kupora utajiri wa mataifa haya. Katika kipindi hiki cha miaka mia mbili, dola na taifa la Iran lililkuwa limelala na kughafilika kabisa pengine baadhi ya wakati lilipokuwa linaangalia mambo lilikuwa linashindwa kujua hata kitu gani kinaendelea, hatusemi tena liwe na nafasi na taathira kwenye matukio hayo. Katika upande wa kiuchumi pia, hali yetu ilikuwa inaporomoka siku baada ya siku. Kwenye uga wa elimu na teknolojia pia tulikuwa tumebakia nyuma kikamilifu na hatukuwa na maendeleo yoyote ya kielimu ambayo yangelipasa kuonyeshwa kwa walimwengu na kuwa na maana katika harakati kubwa na adhimu ya kielimu duniani. Katika suala la siasa zetu za humu ndani pia hatukuwa na kitu bali siasa zetu ziliathiriwa kikamilifu na siasa za wageni. Wakoloni na madola yaliyoidhibiti dunia yalikuwa yanazidhibiti kikamilifu siasa zetu za ndani na kuwaburuza viongozi wa wakati huo wa nchi yetu upande wowote waliopenda, walikuwa wakiwabebesha matakwa yao, walikuwa wakiwatumia wanavyopenda, serikali na tawala zetu nazo, wafalme wetu, taasisi zetu kuu zote zilikuwa zinashindwa kufanya chochote ambacho mtu anaweza kujivunia na kujifakharisha nacho. Hata katika ulinzi wa umoja wa ardhi ya Iran pia, tunaona kulikuwa na udhaifu mkubwa katika kipindi hicho cha miaka mia mbili ya ukoloni humu nchini ambao mtu unaona haya hata kuusema. Ni katika kipindi hicho cha miaka mia mbili ndipo yalipofikiwa makubaliano yaliyojaa madhila yaliyojulikana kwa jina la Makubaliano ya Torkamanchay (Torkanachay ni moja ya miji ya Iran uko kwenye mkoa wa Azerbaijan Mashariki na "Makubaliano ya Torkamanchay" yalifikiwa Februari 21, 1828 Milaadia kati ya Iran na Urusi huko Caucasia Kusini. Kwa mujibu wa makubaliano hayo, Iran ilipoteza ardhi zake nyingi kwa Urusi ambayo kwa upande wake ilitoa ahadi tu za kumuunga mkono mrithi wa kiti cha ufalme wa Iran Abas Mirza. Iran pia ililazimishwa kuipa fedha nyingi Urusi katika makubaliano hayo) na kabla ya hapo (kulitiwa saini) makubaliano mengine ya Golestan na kupelekea Iran ipoteze mikoa yake 18 ya Caucasia. Ilikuwa ni katika kipindi hicho cha miaka mia mbili ndipo walipokuja kuiteka na kuikalia kwa mabavu Bushehr yetu tena bila ya kupata upinzani wowote ule kutoka kwa serikali na viongozi wa wakati huo wa Iran. Ni katika kipindi hicho pia ndipo serikali moja ya wageni ilikuja Iran ikaweka kambi yake ya kijeshi huko Qazvin na kuitishia serikali kuu ya Tehran kwamba lazima ifanye jambo fulani na lazima iache kufanya jambo fulani, imfukuze fulani, ifanye hivi na vile, vinginevyo Tehran itashambuliwa. Yaani waliingia ndani ya ardhi ya Iran na kufika hadi Qazvin na kutoa vitisho dhidi ya Tehran na kuitikisa serikali ya wakati huo ya Tehran. Laiti watu nadra wasingelijitokeza kwenye matukio hayo basi watawala wa Tehran mwisho wake wangelisalimu amri tu mbele ya wanajeshi hao wa kigeni. Ilikuwa ni katika kipindi hicho pia ndipo walipokuja Waingereza na kuweka serikali waitakayo ya wafalme wa Kipahlavi nchini Iran, wakamteua Reza Khan, wakampandisha juu katika kituo kimoja cha Firdousi na kumpa ufalme na kuutangaza ufalme wake kuwa ni sheria kwa Iran nzima na kumkabidhi yeye mambo yote na yeye naye katika kulipa fadhila akawakabidhi Waingereza mambo yote na akawa kibaraka wao kikamilifu. Ni katika kipindi hicho pia ndipo mkataba mbaya wa 1299 - 1919 Milaadia ulipotiwa saini ambapo kwa mujibu wa mkataba huo, uchumi wa Iran uliingia mikononi mwa mabeberu kutoka nje na masuala ya akisiasa na kiuchumi ya Iran yakaingizwa mara moja mikononi mwa maadui wa Iran. Ni katika kipindi hicho pia ndipo Marais wa nchi tatu za nje walipokuja Tehran wakaitisha kikao bila ya hata kupata ruhusu kutoka kwa serikali kuu na bila ya hata kujali angalau kidogo kwamba Tehran palikuwa na serikali. Marais hao walikuwa ni wa nchi waitifaki katika vita (vya pili vya dunia). Yaani Roosevelt, Churchill na Stalin walijileta wenyewe tu mjini Tehran bila ya kujali utawala wa Iran, wakafanya kikao chao mjini Tehran bila ya idhini ya mtu yeyote. Waliingia nchini Iran bila ya hata kuonesha pasi ya kusafiria. Viongozi hao wa nchi tatu hawakumjali Muhammad Reza ambaye alikuwa mfalme wa wakati huo wa Iran, bali hata hawakuwa na wakati wa kwenda kuonana naye, bali yeye ndiye aliyelazimika kuwafuata huko walikofikia na alipoingia walimuonesha madharau makubwa! Yaani hata hawakusimama kumkaribisha! Huu ndio udhalili na uduni waliokuwa nao viongozi wa wakati huo wa Iran waliowafanya wananchi nao wadhalilishwe. Hayo ndiyo masuala yetu ya miaka mia mbili. Sasa unapolinganisha wakati huo na Iran ya hivi sasa utaona kuwa kuna tofauti kubwa sana. Wapi na wapi Iran ya leo yenye heshima na Iran ya wakati huo. Udhalili na uduni ulikuweko kwenye kipindi hicho cha miaka mia mbili, lakini si leo tena (ambapo taifa la Iran limeamka na limeimarika kila upande).
Tab'an katika kipindi hicho cha miaka mia mbili kulikuwa na mambo yaliyokuwa na sifa nyingine tofauti na hiyo. Mathalan ilijitokeza harakati ya miaka mitatu ya Amir Kabir. Na kwa fatwa ya Mirza Mkubwa Shirazi akalipa sura nzuri suala la tumbaku. Vile vile maulamaa waliingilia suala la mfumo wa sheria na bunge, katika kipindi fulani aidha kulikuwa pia na harakati ya kuyafanya mafuta ya Iran kuwa mali ya taifa, lakini mambo yote hayo yalikuwa ya muda mfupi, yalikuwa ni ya kupita na baadhi yake hayakufanikiwa kabisa. Lakini unapoangalia muundo jumla, harakati jumla, utaona kwamba ilikuwa ni kutwishwa na kubebeshwa uduni na udhalili taifa hili kubwa, ilikuwa ni kulidhalilisha tu taifa hili lenye kujenga historia, taifa hili lenye turathi nyingi adhimu za kihistoria.
Yalipokuja Mapinduzi Makubwa ya Kiislamu yalibadilisha kila kitu, yaliugeuza kabisa ukurasa huo. Hima ya Imam - ambaye ndiye kiongozi wa Mapinduzi haya na mkuu wa Mapinduzi yetu haya na kigezo cha Mapinduzi yetu matukufu - ilikita katika suala hili kwamba moyo wa heshima ya taifa uhuishwe kati ya wananchi wa taifa hili, heshima na hadhi yao irejee. Imam mtukufu aliingiza kwenye midomo ya wananchi wa taifa hili, utamaduni wa "sisi tunaweza" na kuufanya ukite katika nyoyo zao. Huo ndio ule ule utamaduni wa Qur'ani Tukufu ambayo inasema:
«و لا تهنوا و لا تحزنوا و انتم الاعلون ان كنتم مؤمنين».
Wala msilegee, wala msihuzunike, kwani nyinyi ndio wa juu mkiwa ni waumini. (Aal Imran, 3:139).
Yaani kuwa na imani kwenyewe basi kunaleta utukufu na kumfanya mtu kuwa wa juu. Kuwa na imani ni njia ya kupata utukufu wa kimaada, lakini si hayo tu, bali imani yenyewe inamfanya mtu kuwa wa juu, imani yenyewe inampa heshima mtu, inaliongoza na kulipa utukufu taifa. Imam mwenyewe alikuwa mbele, akaongoza, hapo ndipo nia na msukumo ukaamka ndani ya nyoyo za wananchi, wananchi wakaingia hima, vipaji vikanawiri na kazi za wananchi zikaimarika na kujitokeza wananchi katika medani kukaongezeka na hivyo kukaandaa uwanja wa kupatikana rehema za Mwenyezi Mungu. Hii ni nukta adhimu sana. Rehema za Mwenyezi Mungu ni pana sana, lakini kama mwanadamu mwenyewe hakujiandaa kupokea rehema hiyo basi mvua ya rehema hiyo kubwa ya Mwenyezi Mungu haiwezi kumnyeshea. Taifa letu lilijitokeza katika medani, likajiweka katikati ya medani, hapo ndipo likaweza kuandaa uwanja wa kumiminikiwa na rehema za Mwenyezi Mungu, na baraka za Mwenyezi Mungu; na uongofu wa Mwenyezi Mungu ukalifikia taifa hili, rehema za Mwenyezi Mungu zikalishukia taifa hili, harakati isiyo na mkwamo ikaanza, harakati kuelekea kwenye heshima, harakati ya kuelekea mbele, harakati yenye kuleta heshima, tab'an baadhi ya wakati kasi ya harakati hiyo inaweza kuonekana imepungua na baadhi yake kasi yake ni kubwa, lakini hakuna mkwamo wala kusimimama kabisa katika harakati hii.
Wakati unapoiangalia fasihi ya mapinduzi ya Imam utaona kuwa imejikita zaidi katika kulijenga ndani kwa ndani taifa, kuhuisha moyo wa heshima tab'an usio na majivuno, usio na ghururi, usio na kujiona, bali kujiimarisha ndani kwa ndani. Jambo ambalo tunapaswa kulizingatia ni kuwa kazi hiyo si ya kupita na wala si ya muda mfupi, bali ni kazi ya kuendelea, ni kazi ya kila siku. Taifa linapaswa kupambana na sababu zote za kuzorotesha na kukwamisha harakati hiyo. Kuna baadhi ya mambo humzuia mtu kusonga mbele, hukwamisha maendeleo ya taifa, baadhi ya mambo hayo yamo ndani yetu wenyewe na baadhi ya mambo hayo yanasababishwa na adui. Kama tunataka tusikumbwe na mkwamo, tusidhalilike na kuwa duni, tusibaki nyuma, na tusikumbwe na ile hali ya jahanamu ya huko nyuma, basi tunapaswa kuhakikisha kuwa harakati yetu haisimami na haikwami. Ni hapa ndipo inapojitokeza istilahi inayojulikana kwa jina la "maendeleo." Tunapaswa tupige hatua za maendeleo wakati wote. Muongo huu (wa Mapinduzi ya Kiislamu) umepewa jina la "muongo wa maendeleo na uadilifu." Uadilifu nao umo ndani ya dhati ya maendeleo. Maana ya maendeleo haiishii tu katika masuala ya dhahiri ya kimaada, bali yamo katika vipengee vyote vya maisha ya mwanadamu. Umo ndani yake uhuru, umo ndani yake uadilifu, kumo ndani yake kujiimarisha kimaadili na kimaanawi; haya yote yanajumuisha maana ya maendeleo. Tab'an yamo pia ndani yake maendeleo ya kimaada, maendeleo ya mambo ya dhahiri ya maisha na maendeleo ya kielimu. Kwa harakati yake ile, Imam alituweka kwenye jia pana na kubwa ambalo inabidi wakati wote tupige hatua za kusonga mbele kwenye jia hili. Kukwama na kusita kwa namna yoyote ile kutatubakisha nyuma katika harakati hii. Taifa ambalo limejua maana halisi ya heshima na utukufu na ambalo liko katika barabara pana ya maendeleo, (linapaswa kuwa macho wakati wote) na kama litaikufuru neema hiyo basi lijue kuwa litathibitikiwa na aya ya Mwenyezi Mungu inayosema:
أ لم تر الى الّذين بدّلوا نعمت اللّه كفرا و احلّوا قومهم دار البوار. جهنّم يصلونها و بئس القرار
Je hukuwaona wale waliobadilisha neema ya Mwenyezi Mungu kuwa kufuru, na wakawafikisha watu wao kwenye nyumba ya maangamizo? Nayo ni Jahannam! Maovu yaliyoje makazi hayo! (Surat Ibrahim, 14: 28-29).
Kama litaikufuru neema hiyo basi dunia itakuwa tena jahanamu kwake na maisha yatakuwa machungu tena kwa taifa hili. Kama mataifa hayatasimama kidete, na kama hayatapiga hatua mbele, basi yatakumbwa na matatizao na yatadumu kwenye kipindi kile kile kigumu cha uduni na udhalili yaliokuwa nao.
Sisi hivi sasa tuna kigezo maalumu hai katika suala la heshima ya taifa na maendeleo yanayotokana na heshima hiyo. Nimesema kwamba mjadala wetu hauhusiana na masuala ya dhihinia tu. Tuna kigezo hai (cha uadilifu na maendeleo) nacho ni hili taifa lenyewe na jamii yenyewe ya Iran. Taifa hili lina modeli iliyofanyiwa majaribio na kupasi mtihani. Taifa la Iran limeingia katika medani likiwa na kigezo hicho. Hapa nitatoa mifano ya maendeleo ya taifa la Iran. Kila moja ya maendeleo hayo lina ufafanuzi wa kina na ushahidi mwingi wa wazi.
Moja ya mifano ya maendeleo ya taifa la Iran ni kushinda changamoto zote za kisiasa, kijeshi, kiusalama na kiuchumi katika kipindi chote hiki cha miaka 33 (ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu). Lengo la maadui katika changamoto hizo ni kuangamiza kabisa uwepo wa mfumo huu wa Kiislamu. Lakini taifa la Iran limeshinda changamoto zote hizo. Wakati dunia hii ilipokuwa na kambi mbili za Mashariki na Magharibi, taifa la Iran lilijitokeza na (kitu kipya yaani kaulimbiu mpya ya si Mashariki wala Magharibi, bali ni Jamhuri ya Kiislamu na kufanikiwa) kuzishinda (kambi hizo mbili za) Mashariki na Magharibi. Hivi sasa hali inavyoonekana juu juu ni kuwa dunia iko mikononi mwa ulimwengu wa Magharibi, lakini taifa la Iran limefanikiwa kuishinda Magharibi hiyo iliyopotoka.
Mfano mwingine wa maendeleo ya taifa la Iran ni kuwa sisi taifa la Iran leo hii tuna nguvu kubwa zaidi katika upande wa nguvu za kisiasa, katika upande wa uwezo wa kutoa taathira kwenye matukio ya dunia na kuwa na taathira pia katika masuala ya eneo hili letu bali pia katika maeneo mengine ya dunia. Hivi sasa tuko imara zaidi na tuna nguvu kubwa zaidi katika masuala hayo ikilinganishwa na awali ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu. Jambo hilo lina mifano yake, lina ushahidi wake na ni maadui ndio wanaokiri mambo hayo. Mmoja wa marais wa utawala pandikizi wa Kizayuni ambao unahesabiwa kuwa ni adui nambari moja wa taifa la Iran na Mapinduzi ya Iran amekiri jambo hilo akisema - na haya ni maneno yake mwenyewe kama alivyosema - leo hii kuna nuru yenye nguvu inayokwenda kinyume na malengo yetu na Iran ndiyo inayoongoza nguvu hiyo. Mwanasiasa huyo (Mzayuni) aliyeemewa na kuchanganyikiwa anakiri akisema kuwa: Leo hii Khomeini amepiga kambi nje ya mipaka yetu! Mwanasiasa mwingine mkongwe na maarufu wa Marekani ambaye tunazijua vizuri sifa zake katika moja ya vikao anaweka mlingano baina ya Marekani ya mwaka 2001 na Marekani ya mwaka 2011 na anasema - na maneno haya yote ni ya hii miezi miwili mitatu iliyopita - (anasema kwamba) mwendawazimu gani ameibadilisha Marekani iliyokuwa dola lenye nguvu mwanzoni mwa milenia na kuwa Marekani dhaifu kiasi chote hiki katika mwaka 2011 - mwaka jana Milaadia? Baadaye anasema: Haya ndiyo masuala yaliyotokea na kuyafikisha mambo hapa yalipofika na nchi iliyochochea mabadiliko hayo ni Iran. Maana ya maneno hayo ni kuwa, leo hii taifa la Iran limefanikiwa kwa uwepo wake makini, kwa istikama yake, kwa heshima yake, kwa ungangari wake, kutoa taathira kubwa sana kwa matukio muhimu duniani na matukio muhimu ya eneo hili. Hii nayo ni moja ya sifa za maendeleo ambayo nimetangulia kusema kuwa mifano yake iko wazi mbele ya macho yetu.
Mfano mwingine wa wazi ni kiwango cha kazi za ujenzi na ustawi zinazofanyika katika nchi hii kubwa na pana. Leo hii unapoangalia kila upande na kila kona ya nchi hii unashuhudia kunafanyika kazi kubwa za ujenzi, kazi kubwa za ustawi, kazi kubwa za maendeleo kwa maana halisi ya neno na kazi hizo zinaongezeka mwaka baada ya mwaka. Hii ni miongoni mwa sifa maalumu za maendeleo ya taifa. Miongoni mwa sifa za maendeleo ni kuona kuwa, miradi tata na migumu sana, zana tata na za kisasa kabisa za viwandani, miradi mikubwa mikubwa inayohitajia uhandisi wa hali ya juu, viwanda vikubwa vya chuma cha pua, vinu vya kila namna na kazi nyingine kubwa kubwa, zote zinafanywa kikamilifu na wataalamu wenyewe wa Iran na vijana wanaojulikana kwa jina la vijana wa Mapinduzi ya Kiislamu. Sisi hivi sasa katika kazi nyingi muhimu zinazofanyika humu nchini, hatuna haja na msaada wowote wa wataalamu wa nchi za kigeni. Hii ndiyo ile nchi ambayo hapo zamani wakati ilipokuwa inataka kutia lami tu, au kujenga daraja barabarani ililazimika iende nje ya nchi kuchukua wataalamu na kuwaleta humu nchini waifanyie kazi hiyo. Lakini leo kazi kubwa kubwa, majengo makubwa yanayohitajia uhandisi wsa hali ya juu na kazi nyingine nzito nzito zinafanyika humu humu ndani kwa kutumia wataalamu wenyewe wa Iran. Wanaofanya kazi zote hizi ni hawa hawa vijana ambao wamelelewa na kukuwa katika mazingira ya Mapinduzi ya Kiislamu. Ni vijana hawa hawa waliochipukia na kukulia kwenye kipindi hiki cha Mapinduzi na kusimama kubeba kazi hizo nzito muhimu.
Mfano mwingine ulio wazi ni kasi ya kielimu nchini Iran - ambapo mara nyingi jambo hilo limekuwa likikaririwa na kusemwa mara kwa mara - bidhaa zinazozalishwa, daraja ya elimu ya Iran mwaka 2011, yote hayo ni maendeleo ya kujivunia yaliyopatikana humu nchini. Na haya si maneno yetu sisi, takwimu hizi hatuzitoi sisi, bali zinatolewa na vituo rasmi vya kielimu duniani, wao ndio wanaosema hayo. Wanasema, ukuwaji wa elimu nchini Iran ni mara 11 ya wastani wa ukuaji wa elimu duniani na mwaka 2011 kiwango hicho kiliongezeka kwa asilimia 20 ilinganishwa na mwaka wa kabla yake. Wao ndio wanaosema hayo. Katika baadhi ya nyanja kama vile uwanja wa nyuklia, uwanja wa teknolojia ya Nano, uga wa seli shina, uwanja wa anga za juu, uwanja wa masuala ya kibiolojia, hali yetu inang'ara katika masuala yote hayo. Kazi zinazofanyika hivi sasa pia ni kubwa na muhimu ambapo ni mara chache unashuhudiwa mfano wake duniani. Kati ya nchi zote hizi duniani - nchi zinazodaiwa kuendelea na zile zilizopewa jina la nchi zisizoendelea - utaona kwamba baadhi ya kazi zinazofanywa humu nchini zinashuhudiwa katika nchi tano, au kumi au kumi na tano tu zilizoendelea duniani. Na maendeleo haya tumeyapata huku wakiwa hawajatusaidia kwa hali yoyote ile. Wamewafungia milango wanachuo wetu wasiingie kwenye Vyuo Vikuu vyao na vituo vyao vya kielimu. Lakini vipaji vya vijana wetu vimechomoza vyenyewe na kuliletea taifa maendeleo yote haya. Tab'an ni vyema pembeni mwa yote haya niseme kuwa vikwazo hivi vilivyowekwa dhidi yetu vimetusaidia sana katika jambo hilo.
Moja ya madhihirisho, mifano na vielelezo vya maendeleo ni demokrasia ya kidini ambapo inabidi mambo hayo nayo yazingatiwe kwa pamoja kwani ni muhimu sana. Sisi tumekuwa na chaguzi zenye hamasa kubwa humu nchini. Chaguzi za Rais katika vipindi mbali mbali ambapo uchaguzi wa duru ya kumi uliofanyika miaka mitatu iliyopita ulikuwa wa hamasa kubwa zaidi. Vile vile chaguzi za Majlis (Bunge) hadi sasa tumeshashuhudia duru tisa za baraza hilo la kutunga sheria ambapo duru zote tisa zimefanyika tarehe ile ile moja yaani tarehe saba Khordad (kwa mwaka wa Kiirani wa Hijria Shamsia) bila ya kuakhirishwakwa hata siku moja. Je hilo ni jambo dogo? Katika kipindi chote hiki cha miaka 33, kumefanyika duru tisa za uchaguzi wa Bunge na kwamba Majlis 9 za ushauri wa Kiislamu zimeundwa humu nchini bila ya kuakhirishwa hata kwa simu moja, hakuna tukio lolote la kisiasa au tukio la kiusalama au tukio la kiuchumi au vitisho vya adui vilivyoweza kuakhrisha kutendeka jambo hilo hata kwa siku moja. Duru zote za Majlisi zimefanyika siku moja, tarehe saba Khordad, siku ya kuundwa Bunge jipya nchini Iran.
Suala jingine ni misukumo, nia na kaulimbiu za kimapinduzi za wananchi. Hebu angalieni katika sherehe za maadhimisho ya mapinduzi mengine duniani zinavyofanyika. Utaona kunafanyika sherehe rasmi, baadhi ya watu wanakusanyika sehemu moja, baadhi ya wakati maafisa wa vikosi vya ulinzi wanapiga paredi na kuadhimisha mapinduzi hayo. Lakini nchini Iran, maadhimisho ya ushindi wa Mapinduzi - yaani Bahman ishirini na mbili - hufanywa na mamilioni ya wananchi katika kila kona ya nchi, kwa shauku na hamasa kubwa na kila mwaka sherehe hizo zinafana zaidi kuliko za kabla yake. Maadhimisho hayo yanakuwa muhimu zaidi na makubwa zaidi kila mwaka, jambo ambalo linaonesha kuwa hai taifa la Iran na kuzidi kupiga hatua za maendeleo taifa hili chini ya mwavuli wa malengo ya kimapinduzi.
Hali ni hiyo hiyo katika kuilea na kuitakasa roho. Baadhi ya watu wanapoona mambo fulani, wanapoona baadhi chache ya vijana wa kiume na baadhi ya wanawake au wanaume wachache tu wanafanya mambo ya uhalifu, utawaona wanakimbilia moja kwa moja kuwajumuisha watu wote na mambo hayo. Hilo ni kosa. Wananchi wetu wanayapa umuhimu sana masuala ya kimaanawi na kidini. Siku chache zijazo nendeni kwenye misikiti ya Vyuo Vikuu vyetu mtaona wenyewe jinsi watu wanavyojazana misikitini katika siku za itikafu. Kuanzia kesho vijana wetu wataanza kumiminika misikitini kwa ajili ya itikafu. Sehemu zinazoshirikisha watu wengi zaidi, kwa sahauku na hamasa kubwa zaidi katika ibada hiyo ni misikiti ya vyuo Vikuu vyetu, na hapo hatujaitia misikiti mikubwa iliyoenea kila mahala, huko kote utawaona watu wanajazana kwenye misikiti kwa ajili ya itikafu. Ni kwa mambo kama haya ndipo tutakapoweza kuhukumu mambo na kutoa tathimini nzuri. Tunapaswa kuhukumu kuwa nchi yetu hivi sasa, taifa letu, limo katika kupiga hatua za kimaendeleo. Nchi yetu inapiga hatua za kimaendeleo katika mambo yote. Na yote hayo yanafanyika chini ya bendera ya Uislamu, chini ya kivuli cha mwito wa Mwenyezi Mungu kwa watu hawa wakubwa, watu hawa bora, naibu huyu wa haki wa Mtume na mawalii wa Mwenyezi Mungu. Watu hawa wakubwa wamelifungulia njia taifa letu.
Duru za kisiasa na vyombo vya habari duniani vinaeneza propaganda za kuonesha kuwa Iran ya nyuklia ni hatari, yaani vinadai kuwa Iran yenye nyuklia ni hatari! Lakini mimi nasema kuwa watu hao na vyombo vyao vya habari wanasema uongo. Wanawadangaya walimwengu. Wanachoogopa wao na ambacho lazima wakiogope si Iran yenye nyuklia, bali ni Iran ya Kiislamu. Ni Iran ya Kiislamu ndiyo iliyoteteresha nguzo zenye nguvu za mabeberu duniani. Wananchi wa Iran wamethibitisha kuwa taifa linaweza kujitegemea na kuwa na mafanikio makubwa ya kisiasa bila ya kuitegemea Marekani na bila ya kutegemea madola makubwa yenye majigambo mengi bali hata kwa kushirikiana na maadui wa Marekani na wa madola makubwa yenye majigambo mengi. Taifa la Iran limewathibitishia walimwengu kuwa inawezekana kupata maendeleo bila ya msaada wa Marekani na bila ya kuwa chini ya ushawishi wa Marekani. Taifa la Iran limethibitisha kuwa mafanikio hayo yanaweza kupatikana si bila ya Marekani tu, bali hata pamoja na maadui wa Marekani. Hilo ni somo kubwa linalotolewa na taifa la Iran kwa walimwengu na ni jambo hilo ndilo linaloyaogopesha madola ya kibeberu (si suala la nyuklia kama yanavyodai).
Naam, sasa umefika wakati wa mimi kusema maneno yangu ya mwisho leo hii kuhusu kadhia hii. Wapendwa wangu, vijana azizi, wananchi waumini! Naam, ni kweli kabisa kwamba sisi tumevunja rekodi, tumepiga hatua kubwa za maendeleo, lakini kama nyoyo zetu zitapumbazika na hiki ambacho tumeweza kukifikia hadi hivi sasa, Basi bila ya shaka yoyote tutafeli katika mambo yetu. Iwapo tutaishia hapa tulipofikia, basi bila ya shaka tutavurumishwa nyuma, iwapo tutakumbwa na ghururi na majivuno, iwapo tutaanza kujistaajabia wenyewe na kuona lo, tumefika mbali sana, bila ya shaka tutaanguka na tutakula mweleka. Kama sisi viongozi - na hili linatuhusu sisi hasa viongozi - tutakumbwa na ugonjwa wa kila mmoja wetu kujivutia upande wake, kiburi na majivuno, basi bila ya shaka yoyote tutapata pigo kubwa sana. Hivi ndivyo dunia ilivyo. Hiyo ndiyo sunna ya Mwenyezi Mungu. Tujiepushe na ugonjwa wa kutafuta umaarufu, tujiepushe na kukumbwa na ugonjwa wa kupenda anasa za dunia, tujiepushe na ugonjwa wa kupenda makuu, maisha ya fakhari na ya gharama kubwa. Sisi ni viongozi, tunapaswa kuchunga sana mambo tunayoyatenda, tunapaswa kujidhibiti kama alivyofanya mtu huyu mkubwa (Imam Khomeini quddisa sirruh). Iwapo sisi tutafanya makosa hapa tulipofikia basi tutakuwa mfano wa wazi wa ile aya ya Mwenyezi Mungu inayosema:
«و احلّوا قومهم دار البوار. جهنّم يصلونها و بئس القرار».
...na wakawafikisha watu wao kwenye nyumba ya maangamizo. Nayo ni Jahannam! Maovu yalioje makaazi hayo! (Surat Ibrahim, 14: 27-28).
Ni marufuku kusita japo kidogo katika njia ya mendeleo. Ni marufuku kujistaajabia sisi wenyewe. Ni marufuku kuruhusu nyoyo zetu zikumbwe na mghafala. Ni marufuku kuishi maisha ya fakhari na ya gharama kubwa. Ni marufuku kupenda anasa. Tujue kuwa hivi sasa tumo katika safari ya kupita katikati ya milima. Bado hatujafika kileleni. Bado tuna safari ndefu. Siku ambapo taifa la Iran litafika kileleni, uadui wote nao utamalizika. Siku ambapo taifa la Iran litafika kileleni upinzani uliojaa ukhabithi utamalizika. Sisi bado tuna safari ndefu ya kufikia huko. Tunapaswa tuendelee na safari yetu bila ya kusimama hata kidogo. Ninapenda kuwaeleza vijana, viongozi, wanafunzi wa Vyuo Vikuu, maulamaa watukufu na watu wote wenye ushawishi katika jamii na wenye uwezo wa kuzungumza na wananchi kwamba tunapaswa kuendelea na safari hii ya kuelekea kwenye maendeleo bila ya kusita hata kidogo, iwe ni katika uwanja wa siasa, au uwanja wa elimu na teknolojia na hasa hasa katika upande wa maadili na umaanawi. Tuzisafishe nafsi zetu na sisi wenyewe tuwe waja wema. Tujue aibu zetu na tufanye idili za kuziondoa. Iwapo tutafanya hivyo, basi vizuizi vyote ambavyo adui anatuwekea mbele yetu havitakuwa na athari yoyote. Vikwazo havitakuwa na athari. Vikwazo haviwezi kulizuia taifa la Iran kuendelea mbele na harakati yake. Athari pekee ambayo vikwazo hivyo vya upande mmoja na pande kadhaa vinaweza kulipatia taifa la Iran ni kuwa, chuki na hasira za wananchi wa Iran dhidi ya uadui wa nchi za Magharibi zitazidi kuongezeka na kuwa kubwa zaidi.
Naam, jambo lililo muhimu hapa ni kulindwa heshima ya taifa. Unapoangalia harakati na mapinduzi haya yanayoendelea hivi sasa katika eneo hili (la Mashariki ya Kati na kaskazini mwa Afrika) utaona kuwa yote yanahusiana na heshima ya taifa. Unapoangalia harakati hizo kutoka Yemen hadi Bahrain na kutoka Misri hadi Libya na Tunisia pamoja na nchi ambazo moto wa harakati za mapinduzi hayo unafukuta chini kwa chini utaona kuwa msukumo wa harakati zote hizo ni kutaka wananchi wa mataifa hayo kurejesha heshima za mataifa yao, uadilifu wa kijamii na uhuru na zote zinafanyika chini ya kivuli cha kupigania Uislamu. Inaposemwa kuwa ni mwamko wa Kiislamu kwa kweli maneno hayo yana msingi mkubwa, naam msingi wa maneno hayo ni madhubuti. Mataifa ya Kiislamu yanataka uadilifu, yanataka uhuru, yanataka demokrasia, yanataka kulindwa na kuheshimu utu na ubinaadamu wao. Wananchi hao Waislamu katikanchi hizo wanaona mafundisho ya dini yao yanasema hivyo na hayaonekani hayo katika aidiolojia nyinginezo isipokuwa aidiolojia ya Kiislamu tu kwani aidiolojia hizo zisizo za Kiislamu zimejaribisha na zimeshindwa kumpa mwanadamu mambo hayo matukufu. Misingi hiyo ya kifikra iliyosimama juu ya msingi wa imani na itikadi za mataifa ya eneo hilo inatokana na Uislamu na mwamko wa Kiislamu. Hii ndiyo dhati na sura halisi ya harakati hizo.
Wamagharibi na tawala za vibaraka wa Magharibi katika eneo hili zinataka kupotosha ukweli wa mambo na zinataka kuwaonyesha walimwengu sura isiyo ya kweli, lakini juhudi zao hizo hazitasaidia kitu. Shakhsia wenye ushawishi katika mataifa ya Kiislamu wanapaswa kuwa macho, wasije wakaenda pogo. Wananchi nao wanapaswa kuwa macho, wasije wakadanganywa. Wananchi wa mataifa ya eneo hili wamefanya kazi kubwa. Wameweza kuleta mabadiliko makubwa na ya kimsingi katika anga ya kisiasa na kijamii ya eneo hili na huu ndio wakati wake. Wanaoyachukia haya na wakae na ndoto zao hizo hizo kuwa wataweza kuzuia harakati hizi lakini wajue kuwa huu ni mwanzo tu. Katika hatua hizi hizi za mwanzo tu za harakati hii tayari anga ya kisiasa ya eneo hili imebadilika; mfano wa wazi ni kuwa wakati mapambano ya wananchi yalipopamba moto huko nchini Misri Wamagharibi walio wengi na tawala nyingi za kidikteta za eneo hili zilijitahidi sana kumlinda na kumtetea Mubarak ili ikiwezekana wamuokoe na wazuie utawala wake wa kidikteta usipinduliwe, lakini baada ya kuona wananchi wa Misri wamepata nguvu na wameshinda sasa yanasikika hayo hayo madola ya kibeberu, na madikteta wakubwa zaidi na madhalimu wakubwa zaidi na watu wanaojidunisha kupindukia mbele ya Wamagharibi wameanza kuzungumzia haki za binaadamu, wanapiga domo la demokrasia! Maana ya jambo hilo ni kuwa, hivi sasa suala la demokrasia limekuwa ni sarafu iliyoenea katika eneo hili zima na hata wale watu ambao zamani walikuwa hawataki hata kusikia tu neno la demokrasia na haki ya wananchi ya kujiamulia mambo yao, leo hii wamelazimika kukubali jambo hilo, na hawana njia nyingine isipokuwa hiyo kwani wanataka kuwavutia wananchi, unawasikia wanapiga domo la demokrasia, wanazungumzia bila kupenda suala la haki za wananchi.
Mapinduzi haya kwa kweli ni muhimu mno. Mimi hapa napenda kuzungumzia zaidi suala la Misri. Misri ni nchi kubwa, Misri ni taifa kongwe, Misri ni eneo muhimu sana katika ulimwengu wa Kiislamu, hata hivyo watawala fasidi, vibaraka, dhalili na duni wamelifanya taifa la Misri lidhalilike, wameifanya Misri kuwa hazina ya kiistratijia ya utawala wa Kizayuni na haya si maneno yangu, bali wakuu wenyewe wa utawala wa Kizayuni wanalisema wazi jambo hilo. Nchi ya Misri, taifa la Misri, taifa adhimu na lenye historia kongwe, walikuwa wameligeuza kuwa hazina ya utawala pandikizi na vamizi wa Kizayuni. Je kuna udhalili na uduni mkubwa kuliko huu? Sasa lakini hazina hiyo imeanguka. Sasa hazina hiyo imetoka mikononi mwa maghasibu wa nchi ya Palestina. Utawala wa Mubarak uliidhaminia Israel usalama wake kwa muda wa miaka 30. Hata ulikuwa tayari kuwaweka kwenye jela kubwa watu milioni moja na nusu huko Ghaza (waliozingirwa kila upande). Watu milioni moja na nusu huko Ghaza walikuwa wanashambuliwa kinyama na Wazayuni makhabithi, na wakati huo huo utawala wa Mubarak ukawa umewafungia njia zote wananchi wa Ghaza wasivuuke mpaka kuingia Misri ambayo ilikuwa njia yao pekee iliyokuwa imesalia kwa ajili ya kubakia hai; jinai hizi kwa kweli historia haiwezi kuzisahau.
Wakati ule wa vita vya siku ishirini na mbili, mwanamapambano mmoja wa Kipalestina alisema katika mahojiano aliyofanyiwa kuwa leo - yaani siku alipokuwa anafanyiwa mahojiano hayo - ni siku ya kumi na tisa inapita tangu vita hivi vianze, lakini hadi sasa tumeshindwa kuingiza (katika Ukanda wa Ghaza) hata kilo 19 tu za ngano na unga kutoka Misri! Njia ya kuwaletea chakula watu, madawa na mahitaji mengine yaani kivuko cha Rafah ilikuwa imefungwa na utawala wa Misri. Yaani waliwaweka kifungoni watu milioni moja na nusu wakiwanyima chakula na mahitaji yote muhimu huko Ghaza ili tu kuufurahisha utawala wa Kizayuni (ambao haukutosheka na hayo, lakini pia ulikuwa unawashambulia kikatili wananchi wa eneo hilo baada ya kuwafungia njia zote za kuingia na kutoka kwa miaka kadhaa). Lakini hivi sasa utawala wa Kizayuni unajiona umevuliwa nguo na uko mtupu, umechanganyikiwa na haujui la kufanya. Haya makelele mnayosikia yakinukuliwa kupigwa na viongozi wa utawala wa Kizayuni na kupiga kwao domo la kuchukua hatua za kijeshi na kushambulia kijeshi, yote haya yanaonesha jinsi walivyoishiwa na jinsi woga na hofu ilivyozikumba nyoyo zao na namna walivyochanganyikiwa na hawajui la kufanya. Wanajua kwamba hivi sasa wako katika mazingira ya kula hasara zaidi kuliko wakati mwingine wowote. Wanaelewa vyema kuwa, wakichukua hatua yoyote ile pogo, au hatua yoyote ile ya kiuanagenzi, basi watakumbwa na kipigo kikubwa mithili ya radi.
Wamagharibi na Wamarekani ambao siku zote wamekuwa wakiuunga mkono kwa kila namna utawala ghasibu wa Kizayuni hivi sasa nao wamekumbwa na matatizo mengi sana kuliko wakati mwingine wowote. Nchi za Magharibi zinaonja matatizo yaliyosababishwa na wenyewe Wamagharibi. Hivi sasa nchi hizo zimezongwa vibaya na matatizo ya mali, matatizo ya kifedha, matatizo ya kiuchumi na matatizo ya kijamii na wakati huo huo hawajui wakabiliane vipi na hasira za wananchi wao. Tawala kadhaa zilizokuwa zinaiunga mkono Marekani zimeanguka barani Ulaya. Kwa kweli wananchi wa Ulaya wanapopata mwanya tu wa kuonyesha hasira zao wanatumia nguvu zao kuonesha hasira zao dhidi ya ubeberu wa Marekani. Hii ndiyo hali iliyowakumba Wamagharibi hivi sasa. Marekani yenyewe nayo hali yake ni mbaya zaidi ya hiyo. Mataifa ya dunia yanachukizwa sana na siasa za kibeberu za Marekani. Marekani hivi sasa imekumbwa na mgogoro. Tab'an wanataka kuuhamishia barani Asia mgogoro wao huo, wanataka kuuhamishia Afrika na Mashariki ya Kati. Wanataka kuficha matatizo yao kwa kuzusha migogoro katika nchi nyingine dhaifu za maeneo mengine duniani. Miongoni mwa mambo waliyokusudia kuyafanya ni ya hapa katika eneo letu yaani kujaribu kuyafanya mapinduzi ya wananchi wa eneo hili yawatumbukie nyongo wananchi wa nchi za eneo hili. Wamekusudia kuzusha fitna za kikabila, mifarakano ya kimadhehebu na hitilafu za kitaifa kati ya watu wa eneo hili. Kwa kweli tunapaswa kuwa macho mbele ya njama hizo.
Hivi sasa Wamarekani wanatumia uzoefu wa Waingereza katika kuzusha mizozo ya kimadhehebu baina ya Waislamu wa Kishia na Kisuni. Waingereza ni mabingwa wa kuzusha uadui kati ya makundi tofauti ikiwa ni pamoja na baina ya Waislamu wa Kisuni na Kishia katika ulimwengu wa Kiislamu na wamekuwa wakitumia mbinu hiyo kwa mamia kadhaa ya miaka sasa. Sasa Wamarekani nao wameamua kutumia uzoefu huo mchungu dhidi ya Waislamu. Kila linapotokezea tukio katika ulimwengu wa Kiislamu, inapozuka kadhia ya Palestina, linapojitokeza suala la Misri kwa mfano, ghafla moja utawaona wanatumia hila na ujanja kwa namna ambayo lazima hila zao hizo zitaishia kwenye suala la kimadhehebu ili kuvuruga harakati hiyo ya wananchi. Waislamu wote wanapaswa kuamka, Waislamu wa Kisuni wanapaswa kuwa macho, Waislamu wa Kishia wanapaswa kuwa macho, kila aalim wa madhehebu yote ya Kiislamu anapaswa kuwa macho, watu muhimu na wenye ushawishi katika jamii nao wanapaswa kuamka na kuwa macho, matabaka mbali mbali ya wananachi pia, kila mmoja anapaswa awe macho, wote wanapaswa kutambua adui anafanya nini, waelewe kuwa adui anafanya njama kubwa, wanapaswa wazitambue njama za adui ili wasije wakamsaidia adui kufanikisha uadui wake dhidi ya Waislamu. Kueneza mizozo kati ya Waislamu ndizo njama zinazofanywa sasa hivi na maadui.
Tab'an Wamagharibi wakiwemo Wamarekani, wanafanya pia mambo ya kipunguwani. Wanalikuza kupindukia suala la nyuklia ili kufunika na kuficha matatizo yao mbele ya walimwengu. Wanaifanya kadhia ya nyuklia ya Iran kuwa suala muhimu kuliko yote duniani wakati ambapo ukweli wa mambo ni kinyume na hivyo. Wanatumia uongo kuhusiana na silaha za nyuklia na wanalikuza kupindukia suala la nyuklia la Iran ili kuwadanganya walimwengu kuhusu kadhia hiyo lengo lao likiwa ni kutaka walimwengu washughulishwe na mambo mengine na wasishughulikie masuala yanayotokea Marekani na yanayoendelea kutokea katika bara la Ulaya kwenyewe. Tab'an, hawatafanikiwa katika njama zao hizo.
Mtazamo wetu sisi kuhusu eneo hili ni mtazamo wa matumaini. Hivi sasa nchi ya Misri inashughulishwa na masuala yake ya ndani na matukio yanayoshuhudiwa hivi sasa Misri ni mambo ya kawaida wakati mapinduzi yanapotokea kwenye nchi fulani. Lazima matukio kama haya yatatokea na hakuna njia nyingine ila kutatua matatizo hayo ambayo yamewashughulisha wananchi. Wananchi wanahisi kuna mwanya ulio wazi na imekuwa ni fursa kwa baadhi ya nchi kujiingiza kwenye masuala ya eneo hili, uingiliaji wa kuzifurahisha nchi za Magharibi, wa kuifurahisha Marekani. Ni uingiliaji unaofanyika kwa niaba ya Marekani na kwa kutumia fedha nyingi, naam, ni harakati zinazofanyika kwa niaba ya Marekani, kwenda huku na huko kuingilia masuala ya ndani ya nchi hiyo. Lakini Inshaallah nchi ambazo wananchi wamefanya mapinduzi hususan nchi kubwa ya Misri zitapata utulivu na amani na zitaweza kushinda matatizo na njama zote zinazozikumba nchi hizo. Utawala wa kidikteta umeangushwa, mabaki ya utawala huo nao wataangushwa kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu na mataifa yataweza kuchukua nafasi yao wanayostahiki kuwa nayo.
Tab'an inabidi hapa niseme wazi kuwa kati ya matukio ya eneo hili, suala la harakati ya wananchi wa Bahrain limekumbwa na dhulma kubwa zaidi. Kwa hakika wananchi wa Bahrain wananyongeshwa kila upande. Wananchi wa nchi hiyo wanaongozwa na utawala kandamizi wa kidikteta na wanakandamizwa bila ya sababu yoyote, malalamiko yao yanakandamizwa kwa njia ya kikatili kabisa wakati ambapo wananchi hao hawataki isipokuwa haki yao. Wanachotaka wao ni haki za awali na za kimsingi kabisa wanazopaswa kuwa nazo watu wote, yaani demokrasia na uhuru wa kujichagulia viongozi wao si zaidi ya hapo. Lakini utaona maadui wanazusha suala la Ushia na Usuni katika kadhia hiyo wakisema, Bwana we, hawa ni Mashia hawa. Lakini ukweli wa mambo kuhusu kadhia ya Bahrain si ugomvi baina ya Masuni na Mashia, ni harakati ya wananchi dhidi ya watawala wa kidikteta. Tofauti ya Bahrain na nchi nyingine ni kuwa asilimia 70 ya wananchi wa nchi hiyo ni Waislamu wa Kishia. Lakini hata kama asilimia hiyo sabiini ingelikuwa na madhehebu nyingine, msimamo wetu sisi ungelikuwa ni huo huo usingelikuwa na tofauti yoyote. Bahrain ni taifa ambalo watu wake wengi ni wa madhehebu mamoja, yaani madhehebu ya Kishia ya wafuasi wa Ahlul Bayt AS ambao wanapambana na utawala wa kiimla na kidikteta. Wala mapambano hayo hayafanyiki kwa sababu eti watawala wa Bahrain ni wa madhehebu mengine, hapana. Taifa la Iran lilikuwa linatawaliwa na utawala wa Shah ambao nao ulikuwa ukijifanya ni wa Waislamu, na tena walikuwa ni Mashia, na walikuwa wakienda kufanya ziara kwenye Haram ya Imam Ridha AS, lakini wananchi wa Iran walisimama na kuupindua utawala huo. Hivyo suala la Bahrain halina uhusiano wowote na Ushia na Usuni. Ila maadui wanajaribu kuuhusisha mgogoro wa nchi hiyo na hitilafu za kimadhehebu ili kwa njia hiyo wawanyime wananchi wa nchi hiyo haki zao. Lakini Inshaallah jitihada zote zinazofanywa na wananchi hao zitazaa matunda. Tunapaswa kuwa macho usije moto wa mizozo ya kikabila, kitaifa na kimakundi ukapamba moto; haya ndiyo tunayoyataka sisi, hizi ndizo nasaha zetu kwa wahusika wote wa kadhia hizo.
Ni matumaini yetu Inshaallah Mwenyezi Mungu Mtukufu ataleta msaada Wake, na kwa yakini ataleta nusra Yake. Bila ya shaka yoyote mustakbali wa mataifa ya Waislamu na kwa ajili ya Uislamu na Waislamu na kwa ajili ya taifa la Iran utakuwa bora zaidi kuliko kabla yake.
Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

 
< Nyuma   Mbele >

^