Skip to content

Habari

Habari
Hifadhi

Risala na Barua

Matini
Hifadhi

Kumbukumbu na Simulizi

Kabla ya Mapinduzi
Baada ya Mapinduzi

Sauti na Taswira

Picha
Sauti
Video
Hotuba ya Kiongozi Muadhamu katika Haram ya Imam Ridha AS Ulipoanza Mwaka 1392 Hijria Shamsia Chapa
21/03/2013
Kwa jina la Allah Mwingi wa rehma Mwenye kurehemu
 
Himidi zote zinamstahikia Allah, Mola Mlezi wa viumbe wote. Na rehma na amani zimshukie Bwana wetu na Mtume wetu, kipenzi cha nyoyo zetu Abul Qasim al Mustafa Muhammad na Aali zake wema, watoharifu na wateule hususan Baqiyyatullah (Imam wa Zama) ardhini. Amani ya Allah iwe juu ya Siddiqah Mtoharifu Fatima binti wa Mtume SAW. Amani iwe juu yake, juu ya baba yake, mumewe na wanawe.
Natoa salamu na pongezi za dhati kabisa kwa makaka na madada wote wapendwa waliohudhuria katika hafla hii iliyojaa hamasa; na ninamshukuru Allah kwa dhati kabisa na kwa moyo wangu wote kwakutokana na kunipa wasaa na tawfiki hii adhimu, ambapo kwa mara nyingine tena amenijaali na kwa mwaka mwingine tena amenipa tawfiki na kunifikisha katika Nairuzi nyingine na kunipa uwezo wa kuwa jirani na Haram Toharifu ya Mtukufu Abul Hassan Ali bin Mussa Ridha (Amani ya Mwenyezi Mungu iwe juu yake). Kwa hakika namshukuru Allah kwa kunipa fursa tena ya kuwa katika hadhara na mkusanyiko wenu huu nyinyi ndugu azizi wa Mash'had pamoja na waheshimiwa wafanyaziara (mliokuja kumzuru Imam Ali bin Mussa Ridha AS) ambao mumetoka katika nchi mbalimbali na kuwa hapa; na mimi kupata fursa ya kukutana na nyinyi ili niweze kuzungumza na nyinyi kuhusiana na masuala muhimu na yanayojiri ya nchi. Ninamuomba Allah aziongoze nyoyo zetu na ndimi zetu na akifanye kile ambacho anakiridhia kiwe ndio kinachopenya katika nyoyo zetu na kupita katika ndimi zetu. Amin. Kwa hakika hii nayo ni tawfiki kubwa ya kila mwaka katika sikukuu ya Nairuzi (sikukuu ya mwaka mpya wa Kiirani wa Hijria Shamsia) ambapo mbali na furaha na mambo mazuri yanaoambatana na sikukuu ya Nairuzi, hupata fursa sisi ya kuwa katika mkusanyiko wenu katika siku kama ya leo na hivyo kutathmini hali ya sasa ya nchi, ya huko nyuma pamoja na mustakbali. Katika siku hii (kawaida) tunaitumia kutupia jicho jumla kuhusiana na hali ya ndani na hali ya mambo ilivyokuwa katika kipindi cha mmoja mmoja uliopita (mwaka uliomalizika wa Kiirani) pamoja na kuchunguza na kutathmini masuala makubwa ya kitaifa hapa nchini; yaani tunatumia fursa hii kuihesabu nafsi kitaifa au kuihesabu nafsi (hali ya nchi) jumla jamala na kiujumla.
Kama ambavyo mtu anahitajika daima kutathmini na kuchunguza masuala yake binafsi na ya kila siku, kadhalika hali iko namna hiyo katika masuala yanayohusu nchi, yaani kuna haja ya kuweko tathmini ya kitafa na bila shaka hilo ni jambo muhimu mno kwani linatoa ibra na mazingatio na kuonyesha njia ya kufuata katika masuala yaliyopo sasa na yanayokuja baadaye. Aidha ni jambo la lazima kwetu kuihesabu nafsi katika masuala ya mtu binafsi - kama ilivyokuja katika hadithi: "Zihesabuni nafsi zenu kabla hamjahesabiwa". Hivyo kuna haja ya mtu kuihesabu nafsi yake yaani kufanya tathmini ya amani na matendo yake. Kuweko hali ya tathmini ya kitaifa nayo pia ni kazi muhimu na yenye thamani sana; tuzihesabu nafsi zetu na kuzifanyia tathmini; tujitazame; tukiweke tena mbele ya mambo yetu kile ambacho kimeshapita; tupate ibra na mazingatio kupitia hilo na tustafidi nalo kwa ajili ya mustakbali.
Makaka na madada wapendwa! Zingatieni kwamba sio sisi peke yetu tunayoyatazama masuala yetu na kuyachunguza na kuyafanyia tathmini; la hasha, bali kuna watu wengine ambao wanayatazama masuala na mambo yetu, wanayasoma mambo yetu na kuyatwalii; kuhusiana na kazi zetu, mambo yetu na wanatoa hukumu kuhusiana na hatua zetu na kutoa maoni kuhusiana na kazi zetu. Kuna mataifa ambayo yanastafidi na tajiriba zetu; kuna baadhi ya watu ambao wanafurahia maendeleo yetu na wanaonesha furaha kutokana na mafanikio tuliyoyapata; kama sisi tunapata ushindi, basi wao huhisi kwamba, wamepata ushindi; kama tutapata machungu (kukwama) katika kazi zetu basi nao wao pia hupatwa na uchungu. Kuna watu wengine duniani ambao wao wao wanazifuatilia kwa makini sana kazi zetu, wanazisoma na kuzitwalii kazi zetu, lakini kinyume na kundi la kwanza, wao hufurahi wanapoona tumeteleza mahala fulani na wanachukia pindi wanapoona tunapata mafanikio, wao ni watu wanaolitakia mabaya taifa la Iran; hawa nao wanazifuatilia na kuzitathmini kwa kina kazi zetu. Kikawaida hawa ni watu ambao katika kipindi cha miaka yote ya huko nyuma walikuwa na udhibiti wa kila kitu hapa nchini; walikuwa wakihodhi na kuwa na sauti na kila masuala ya nchi yetu; mapinduzi yakaja na kukata mikono yao; ni kwa msingi huo ndio maana hawayapendi mapinduzi, wanawachukia wananchi wanamapinduzi wa taifa hili, wana ubaya na utawala wa kimapinduzi hapa nchini na wana uadui na mfumo wa kimapinduzi hapa nchini. Kwa msingi huo basi, sisi tuko chini ya jicho kali la jamii kubwa ya mwanaadamu; wanatazama kazi yetu, wanaipima na kuifanyia tathmini.
Ni kwa msingi huo ndio maana tunapotazama utendaji wetu na mipango yetu ya huko nyuma na ya baadaye, mtazamo wetu unapaswa kuwa ni wa kuangalia mambo kwa uhakika na uhalisia wake; tathmini yetu nayo inapaswa kuwa ni tathmini sahihi kabisa. Baadhi ya wananchi wetu wakati wanapotazama hali ya mambo ya nchi hii, wao wanaona udhaifu na mapungufu tu; wanaona kuna ughali (wa maisha), wanaona kuna kupungua uzalishaji katika baadhi ya sekta za uzalishaji hapa nchini na wanaona kuna mashinikizo (ya kiuchumi) ya maadui. Kwa hakika mtazamo huu ni mtazamo wa nusu nusu. Mimi nina mtazamo tofauti. Mimi pindi ninapotazama hali ya mambo ya nchi na hali ya taifa letu, ninashuhudia medani kubwa na adhimu ambayo imejaa changamoto ambapo licha ya kuweko njama za maadui, taifa la Iran limeweza kuibuka na ushindi na kutembea kifua mbele katika medani hii.
Kuna udhaifu, mapungufu na matatizo; katika majimui ya matukio na mambo ya hapa nchini, kuna mambo machungu na matamu; lakini watu ambao wanamiliki nguvu za kimaada ulimwenguni, wamefanya kila wawezalo tena kwa nguvu zao zote ili kulikwamisha na kulifanya kilema taifa la Iran; jambo hili wamelisema kwa vinywa vyao. Yule mwanamke asiye na ustahiki (Hillary Clinton) ambaye alikuwa na jukumu la Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani alijitokeza wazi wazi tena kifua mbele na kusema kwamba, tunataka kuiwekea vikwazo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambavyo vitailemaza nchi hii! Alilisema hili wazi wazi pasina kificho. Sasa nitasema na kubainisha harakati na hatua zao zilikuwa zipi na matokeo yake yamekuwa nini.
Kwa muktadha huo, huo ni upande mmoja wa juhudi na harakati za adui, na upande wa pili ni mafanikio makubwa iliyolipata taifa la Iran katika medani na uwanja huu mkubwa wa changamoto na kukabiliana na adui. Kwa hakika jambo hili linaonesha na kudhihirisha nguvu, uwezo na werevu wa taifa hili kubwa. Kwa hakika katika medani na uwanja huo uliojaa changamoto, taifa hili la Iran limefanikiwa kubadilisha vitisho hivyo kuwa fursa nzuri kwake, kwa kutumia werevu wa hali ya juu na kwa nguvu zake nyingi, na mfano wa hilo ni kama mtu anayechukua ubingwa katika michezo, ambaye huibuka na ushindi baada ya kuvuka ushindani mkubwa na mkali ulioambatana na taabu na mashaka mengi na juhudi zisizochoka na hatimaye watu humpongeza na kumpa hongera kutokana na kuibuka na ushindi.
Mshindi wa medani hii kubwa na adhimu aliyeko mbele ya macho yetu ni taifa la Iran. Kila mtu ambaye ataliona hili kwa usahihi na kulitwalii kwa njia sahihi, bila shaka atalipongeza na kulipa hongera taifa la Iran; kama ambavyo leo sisi tunasikia sauti za pongezi na hongera kwa taifa la Iran kutoka katika nukta mbalimbali ulimwenguni ambapo katika nchi hizo hizo ambazo ni adui na zisizolitakia mema taifa la Iran, wanajitokeza watu wenye vipawa vya kisiasa, vipaji vya Vyuo Vikuu, watu walioona dunia (waliokula chumvi nyingi) na wazoefu ambao wanayafuatilia kwa karibu mambo yanayojiri hapa nchini ambao wamekuwa wakilipongeza na kulipa hongera taifa la Iran. Huu ni uwanja na medani ambayo iko mbele ya macho yetu.
Kwa msingi huo basi, kutazama mapungufu tu na kuyakazia macho si sahihi hata kidogo. Kuna ulazima wa kutazama majimui ya juhudi hizo katika kiwango cha nchi zinafanyika vipi na zinakuwa na natija gani. Wakati tunapotazama mambo kwa mtazamo na uoni huu ni lazima tutoe hongera kwa Iran na wananchi Waislamu wa Iran.
Tumesema kwamba, baadhi ya watu wanapatwa na huzuni na masononeko kutokana na maendeleo ya taifa la Iran. Hawa ni akina nani? Hili litalizungumzia baadaye. Maadui ambao hawataki kuliona taifa la Iran linapata ustawi, maendeleo na kukwea katika kila upande, wanafanya mambo mawili makuu katika ratiba na mipango yao:
Mosi, hufanya kila wawezalo kulikwamisha taifa la Iran ili lisiweze kufikia ustawi na maendeleo haya; kwa kutumia vikwazo, vitisho, kuwashughulisha wakurugenzi na viongozi na mambo ambayo ni ya daraja la pili na yasiyo ya kimsingi na kuzivuta hisia za wananchi wa taifa kubwa la Iran na watu wenye vipaji hapa nchini katika kazi na mambo ambayo hayako katika faharasa na orodha ya mambo na kazi zao ambazo ni za kimsingi; yaani kuweka vizuzi vya kivitendo.
Kazi ya pili ni kufanya propaganda kubwa za kukana maendeleo ya Iran. Hii leo kuna mtandao wa kanali za propaganda kubwa ambao una maelfu ya vyombo vya habari tofauti tofauti duniani ambao unajishughulisha na kazi ya kutaka kuthibitisha kwamba, hakuna maendeleo yanayopatikana katika nchi ya Iran; wakane ushindi linaoupata taifa la Iran; kama kuna nakisi, udhaifu na mapungufu basi wafanye njama za kuyakuza kupindukia (ili walimwengu wahisi kwamba, hakuna maendeleo yoyote ambayo taifa la Iran limeyapata).
Rais wa Marekani katika hotuba yake rasmi anazungumzia matatizo ya kiuchumi ya Iran; kama vile anazungumzia ushindi waliopata; kwamba, ndio, sarafu ya taifa nchini Iran imeanguka na kuna matatizo ya kiuchumi haya na yale. Hata hivyo, Rais wa Marekani hajaashiria nguvu ya taifa hili, hima na idili chanya na athirifu zinazofanyika hapa nchini na ushindi mkubwa uliolipata taifa la Iran na katu hawezi kuashiria hayo. Ni miaka thelathini sasa ambapo sisi tunakabiliwa na changamoto hizi - ambapo mimi katika kufanya tathmini ya miaka hii thelathini nitasema kitu hapo baadaye - lakini changamoto ambayo taifa la Iran inakabiliwa nayo na uadui ambao inaandamwa nao - katika vitendo na katika propaganda - wa kufanya njama za kutaka kuzuia kujitokeza na kudhihiri kunakoonekana taifa la Iran katika kivuli cha Uislamu na kuishi Kiislamu hakujakuwa na matunda, kwani hii leo hali hiyo ya taifa la Iran la kutaka kudhihiri chini ya kivuli cha Uislamu imeongezeka maradufu na inazidi kuimarika siku baada ya siku.
Mwaka uliomalizika wa 1391 Hijria Shamsia, ulikuwa ni mwaka wa kazi nyingi kwa madui (ikilinganishwa na miaka ya kabla yake) katika uwanja huu. Maadui walikuwa wakisema wazi kwamba, wanataka kuliwekea vikwazo taifa la Iran ambavyo vitalilemaza taifa hili. Kwa msingi huo basi, endapo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itakabiliana vilivyo na vikwazo vyote hivyo na kuendelea kuwa imara na madhubuti tena bila ya kutetereka bali na kuzidi kupata maendeleo katika nyuga tofauti, bila shaka jambo hilo kwa hakika litawaaibisha maadui hao; ndio maana kama wanaweza wazuie hilo na kama hawawezi basi kwa uchache wafanye propaganda na kupotosha uhakika na uhalisia wa mambo ulivyo. Hizi ni kazi mbili ambazo zinafanywa na maadui kwa nguvu kubwa; kwa kuweka vizuizi vya kivitendo - kwa vishinikizo, kwa vikwazo na mfano wa hayo - na vile vile kutumia propaganda kwa ajili ya kudogosha na kudunisha nukta yenye nguvu na kuikuza kupita kiasi nukta dhaifu. Kwa maana kwamba, maadui wanafanya propaganda za kuyadunisha maendeleo ya taifa la Iran na wakati huo huo mapungufu na udhaifu ambao upo wanaukuza kupindukia. Tumesema kuwa, hayo yanafanywa na maadui. Maadui hao ni akina nani? Liko wapi pango kuu la njama dhidi ya taifa la Iran? Jibu la maswali haya sio gumu. Hii leo ni miaka 34 ambapo kila mara neno "adui" limekuwa likitajwa ambapo mara tu linapotajwa, basi fikra za wananchi wa Iran huielekea serikali ya Marekani. Vizuri, viongozi wa Marekani wanapaswa kuzingatia nukta hii na wafahamu kwamba, katika kipindi hiki cha miaka thelathini na ushei, taifa la Iran limeona mambo na limepitia marhala na hatua tofauti mpaka limefikia kwamba, mara linapotajwa neno "adui" basi fikra na akili zao huielekea Marekani. Hili ni jambo muhimu sana kwa dola ambalo linataka kuishi kwa heshima duniani; jambo hili ni la kuzingatia na la kutilia maanani; kuna haja ya kulizingatia hili. Kituo cha njama ni hapa na msingi wa uadui uko hapa.
Tab'an, kuna maadui wengine ambao sisi hatuwahesabu na kuwaweka maadui hao katika faharasa na daraja la kwanza: Kuna adui Mzayuni, (utawala wa Kizayuni wa Israel) tab'an, utawala wa Kizayuni wa Israel hauko katika sifa na daraja ya kuwa katika safu ya maadui wa taifa la Iran. Kuna wakati mwingine, viongozi wa utawala haram wa Israel hututisha: Hutoa vitisho vya kutushambulia kijeshi; lakini kwa mtazamo wangu wao wenye wanafahamu na kama hawafahamu basi wanapaswa kutambua kwamba, kama watafanya kosa na kuthubutu kuishambulia kijeshi Iran, basi Jamhuri ya Kiislamu itasawazisha Tel Aviv na Haifa na udongo. Serikali khabithi ya Uingereza nayo inalifanyia uadui taifa la Iran; huyu naye ni miongoni mwa maadui wa jadi na wakongwe wa taifa la Iran; tab'an, Uingereza ni mkamilishaji tu wa njama na mipango ya Marekani katika medani hii. Yenyewe serikali ya Uingereza haina mamlaka hata mtu aifikie kuihesabnu kuwa ni adui wa kujitegemea; bali Uingereza imekuwa ikiifuata tu Marekani.
Kuna madola mengine duniani ambayo nayo yana uadui na taifa la Iran. Naona ni vyema nikatumia fursa kuwaambia viongozi wa serikali ya Ufaransa ambayo katika miaka ya hivi karibuni imefanya uadui wa wazi dhidi ya taifa la Iran; kwa hakika hii ni hatua isiyo ya busara ambayo ilifanywa na viongozi wa Ufaransa. Mtu mwenye akili (timamu) hususan wanasiasa wanaotumia akili, hawapaswi kuwa na msukumo huu kwamba, kiumbe ambaye siye adui yake wambadilishe na kumfanya kuwa adui yao. Kwa hakika sisi hatukuwa na mushikili na serikali ya Ufaransa na wala hatukuwa na tatizo na nchi ya Ufaransa; sio katika kipindi chote cha historia huko nyuma na hata katika zama za leo; lakini siasa ghalati (mbovu na mbaya) zilizoanza katika kipindi cha utawala wa Rais Nicolas Sarkozy - ambapo inasikitisha kwamba, serikali ya sasa ya Francois Hollande inaenda njia ile ile ya Sarkozy - zilipelekea kutokea uadui dhidi ya taifa la Iran. Kwa mtazamo wetu hiki ni kitendo ghalati, kazi isiyo na tadbiri wala utumiaji akili yaani ni kazi ambayo sio ya busara.
Wamarekani wakati wanapozungumza hutumia neno " jamii ya kimataifa". Neno jamii ya kimataifa wamelipatia nchi chache kadhaa; ambazo kinara wake ni Marekani ambapo nyuma yake kuna utawala wa Kizayuni wa Israel, serikali ya Uingereza na baadhi ya tawala nyingine chache! Katu jamii ya kimataifa haina uadui na Iran, Uirani na Iran ya Kiislamu.
Sasa kwa kuwa tunapaswa kutupia jicho (matukio ya) mwaka (uliokwisha) wa 1391 Hijria Shamsia yanipasa niseme kwamba, kuanzia mwanzoni mwa mwaka 1391, Wamarekani walianza kutekeleza ratiba na mipango yao mipya; licha ya kuwa vinywani na katika ndimi zao walionesha urafiki, na wakati mwingine kuonesha kuwa wana urafiki na sisi - katika barua, risala, ujumbe na mfano wa hayo - wakati mwingine walionyesha kuwa na urafiki na taifa la Iran katika vyombo vya habari, lakini kinyume na matamshi haya yasiyo na ukweli, katika vitendo walifanya kila wawezalo kuhakikisha kwamba, wanalifanyia taifa la Iran na wananchi wa Iran ugumu na kulikwamisha katika mambo yake; waliliwekea vikwazo shadidi (vikubwa) taifa la Iran kuanzia mwanzoni mwa mwaka uliopita wa Kiirani - vikwazo vya mafuta, vikwazo vya kibenki, mabadilishano na miamala ya kibenki na kifedha baina ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na nchi nyingine - wamefanya kazi na mambo mengi katika uwanja huu.
Hivi navyo ni miongoni visa vya ulimwenguni ambapo Wamarekani wanafanya uadui na wakati huo huo wanataka msijue kama wanakufanyieni uadui; wanaendesha upinzani, chuki na uadui kisha wanataraji kwamba, taifa la Iran lisifahamu kama wao ni maadui na kwamba, wanafanya uadui! Siasa hizi za kukabiliana na Iran zilianza kutekelezwa mwishoni mwa kipindi cha utawala wa Bush, na hii leo inasikitisha kwamba, siasa hizo hizo zingali zinaendelezwa na viongozi wa Marekani; Kwa hakika siasa hizo ni kuendelea na siasa zile zile za "kuficha makucha ndani ya glovu za mahameli" yaani siasa za kuuma na kupuliza. Miaka kadhaa iliyopita mimi niliwahi kusema tena hapa hapa jirani na haram tukufu ya Imam Ali bin Mussa Ridha (Alayihs Salaam) katika hotuba ya siku ya kwanza ya mwezi Farvardin (siku ya mwaka mpya) kwamba, kuweni makini hali yenu ya kuonesha mapenzi, matamshi yenu ya kujifanya ni marafiki na mwafaka wenu usiwe na maana ya kwamba, mmeficha makucha ndani ya glovu na mnajifanya tu kuonyesha mapenzi lakini katika batini na uhalisia wa mambo mnafanya uadui. Wamarekani wakiwa na lengo la kusimamisha uuzaji wa mafuta na kuhamisha fedha za Iran walimtuma mjumbe maalumu. Waliwatumia watu stadi, mahiri na maalumu ili wafanye mawasiliano na baadhi ya nchi na wasafiri katika nchi jirani; hata wafanye mazungumzo na mashirika ili mashirika hayo yasifuatilie suala la kuwa na mashirikiano na mahusiano ya kiuchumi katika uga wa mafuta na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran; na mashirika hayo yataadhibiwa kutokana na kuwa na uhusiano na mashirikiano ya kifedha na Jamhuri ya Kiislamu, uhusiano wa kipesa au kuwa na muamala wa kimafuta; mipango na mambo haya ya yalianza kutekelezwa mwanzoni mwa mwaka 1391 hususan kuanzia mwezi wa Mordad (mwezi wa tano) walianza kufanya haya kwa nguvu zaidi. Walikuwa na matarajio kwamba, Iran itasalimu amri mbele ya harakati hizi zilizopangiliwa vyema na walizokuwa wakizifuatilia kwa nguvu zao zote na hivyo iachane na ustawi wake wa kielimu na kusalimu amri mbele ya ubabe na utumiaji mabavu wa Marekani.
Tab'an, mimi napenda kusema hili - nalisema tena jambo hili ambalo miezi kadhaa iliyopita nililisema pia - ya kwamba, Wamarekani walionyesha furaha na wakasema kwamba, mtu fulani amekiri kwamba, vikwazo vimekuwa na taathira. Ndio, bila shaka vikwazo vimekuwa na taathira; wanataka kufurahia hili, sawa na wafurahi. Hatimaye vikwazo vimekuwa na taathira; huu nao ni mushkili wa kimsingi tulionao. Uchumi wetu umekumbwa na mushkili huu wa kufungamana na mafuta (kutegemea mafuta). Kwa hakika sisi tunapaswa kuutenganisha uchumi wetu na nishati ya mafuta; serikali zetu zinapaswa kulitia maanani hili katika mipango yao ya kimsingi. Nakumbuka miaka 17 au 18 iliyopita niliwaambia viongozi wa serikali iliyokuwa madarakani wakati huo kwamba, wafanye mambo ili sisi tufikie hatua kwamba, pindi tunapotaka tuweze kufunga visima vyetu vya mafuta. Watu wakatoa tabasamu la kukana wakisema, hivi hili linawezekana?! Ndio, linawezekana; ni lazima lifuatiliwe, ni lazima kuchukuliwe hatua na ni lazima kuweko na mipango na ratiba (kwa ajili ya hilo). Wakati mipango ya uchumi wa nchi inapokuwa imefungamana na nukta maalumu, maadui huja na kuizingatia na kuifanyia kazi ile nukta maalumu. Ndio, vikwazo vimekuwa na taathira, isipokuwa sio ile athari ambayo adui alikuwa akiitaka; na Inshallah nitalibainisha vyema suala hili. Hili ni kuhusiana na kazi ya kiuchumi. Katika uga wa kisiasa, vile vile maadui walifanya kila wawezalo katika kipindi chote cha mwaka uliomalizika (wa 1391 Hijria Shamsia), chambilecho wao, waitenge Jamhuri ya Kiislamu duniani; yaani wazifanye nchi ziwe na uhusiano wa kulegaleha na Jamhuri ya Kiislamu na wasiiruhusu Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itekeleze siasa zake katika Mashariki ya Kati, katika kiwango cha kimataifa na hata katika kiwango cha nchi. Kazi hiyo ilikabaliwa na hali ya kushindwa. Katika masuala ya kimataifa, Wamarekani (na maadui kwa Iran kwa ujumla) walikuwa wakitaka kukikifanya kikao kama cha Jumuiya ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote NAM ambacho kiliandaliwa na Iran kisiwe na mafanikio na kionekane kwamba, hakikufana; watu wote wasishiriki au kisiwe na ushiriki amilifu na wa hamasa. Lakini mambo yalikuwa kinyume kabisa na matarajio yao. Thuluthi mbili ya mataifa ulimwenguni ni wanachama wa Jumuiya ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote NAM. Viongozi wa nchi mbalimbali walishiriki kikao cha NAM mjini Tehran na viongozi wa ngazi za juu wa nchi mbalimbali walikuja hapa Tehran na kushiriki mkutano huo wa NAM. Watu wote wakaipongeza Iran na watu wote wakaonesha kushangazwa na maendeleo ya kielimu, kiteknolojia na ya kiuchumi ya Iran. Watu wote wakaisifu na kuipongeza Iran; hili ni jambo ambalo walitwambia sisi, wakalisema hilo katika mahojiano yao; na hata waliporejea katika nchi zao wakalisadikisha hilo. Yaani yaliyojiri ni kinyume kabisa na kile kilichokuwa kikitakiwa na maadui wa taifa la Iran; hawakuweza kuwa na taathira na mipango yao ya kuikwamisha Iran haikuwa na natija.
Katika uga wa siasa za ndani, lengo la vikwazo vyao hivi lilikuwa ni kuwafanya wananchi wa Iran waingiwe na shaka katika njia yao; walete utengano baina ya wananchi wa Iran na Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu (unaotawala hapa nchini); na wawakatishe tamaa wananchi. Katika siku ya tarehe 22 Bahman (siku ya kuadhimisha kumbukumbu ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu) taifa la Iran lilihudhuria kwa wingi katika maandamano ya siku hiyo, likiwa na hamasa na shauku kubwa sambamba na kuonyesha hisia (nzuri walionao) kuhusiana na Uislamu, mapinduzi ya Kiislamu na Mfumo wa Kiislamu na hivyo kutoa kipigo kikali kwa maadui. Katika uwanja wa masuala ya kiusalama vile vile walifanya njama za kuvuruga usalama wa nchi - ambapo kwa undani zaidi kuhusiana na hayo, yamebainishwa na viongozi katika mahojiano na mazungumzo yao na wananchi - lakini hawakufanikiwa pia katika hilo. Katika uwanja wa masuala ya kisiasa katika eneo la Mashariki ya Kati na satwa pamoja na ushawishi wa Jamhuri ya Kiislamu kwa mara nyingine tena wamepata tajiriba. Katika masuala ya Mashariki ya Kati, hali imefikia kuwa, wanakiri na kusema bayana kwamba, bila ya Iran, bila ya kuishirikisha Iran na bila ya kuweko maoni na mtazamo wa Iran haiwezekani kuutatua mushkili wowote ule katika Mashariki ya Kati. Katika kadhia ya utawaka wa Kizayuni wa Israel ya kuishambulia kijeshi Gaza, uwepo wenye nguvu wa Iran nyuma ya pazia ulipelekea kama walivyokiri wenyewe kushindwa Israel katika kukabiliana na wapiganaji wanamuqawama wa Kipalestina; ni wao waliosema - sisi hatukusema, wao walisema na kusisitiza juu ya hilo - kwamba, kama kusingekuweko na mahudhurio kama haya yenye nguvu ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kama kusingekuweko na uonyeshaji nguvu huu wa Jamhuri ya Kiislamu, wanamapambano wa Kipalestina wasingeweza kusimama kidete mbele ya utawala wa Kizayuni wa Israel, seuze kuipigisha magoti Israel; ambapo katika vita vya siku nane, Wapalestina waliweza kuipigisha magoti Israel na jambo hilo lilikuwa la kwanza katika historia ya utawala huo bandia na ghasibu wa Kizayuni. Tumesema kuwa, juhudi na njama za maadui sio kwamba hazikuwa na taathira, ndio zimekuwa na taathira, lakini pembeni ya taathira hasi kulijitokeza taathira chanya kubwa ambayo ilikuwa ikitarajiwa na sisi; yaani vikwazo vimeifanya nguvu ya ndani na uwezo mkubwa wa taifa la Iran kuwa amilifu, vipaji kuchomoza na kudhihirika na kupelekea kufanyika kazi kubwa; ambapo kama vikwazo visingekuweko, kazi hizi zisingefanyika. Kwa hakika kwa baraka ya vikwazo, sisi tumeweza kufanya mambo makubwa; vijana wetu wameweza kuliletea mafanikio taifa hili ambapo kama vikwazo hivi visingelikuweko kwa yakini sisi tusingeweza kuyafikia haya. Katika uwanja wa kazi za kimsingi (miundo mbinu) - ambapo nitalizungumzia hili baadaye - katika mwaka uliokwisha wa 1391 Hijria Shamsia kumepatikana maendeleo na mwaka uliopita ukilinganishwa na miaka iliyotangulia tunaona kuwa, mwaka huo ulikuwa ni mwaka muhimu. Kazi nyingi za kimsingi zimefanyika; katika uwanja wa barabara, katika uga wa nishati, katika uwanja wa kugundua vyanzo (visima) vipya vya mafuta, katika uga wa kugundua vyanzo vipya vya madini ya Urani, katika masuala ya kuanzisha na kupanua vituo na viwanda kuna makumi ya kazi yamefanyika; ambapo haya yote ni misingi ya uchumi wa baadaye wa nchi hii. Kama sisi tungekuwa tumeandaa misingi hii tangu hapo kabla, basi hiki hiki kiwango cha taathira hasi cha vikwazo vya adui ambacho kimekuweko, bila shaka kisingekuweko. Sisi tumefanya kazi hizi na tumeweza kusonga mbele bega kwa bega na uadui pamoja na mashinikizo ya maadui.
Kuna kazi kubwa zimefanyika; kuna mrundikano wa maendeleo makubwa ya kielimu yaliyopatikana katika kipindi chote cha mwaka 1391 Hijria Shamsiya. Katika uwanja wa elimu na teknolojia kuna kazi ambazo zimefanyika ambazo kwa hakika zinamfurahisha na kumburudisha kila mtu mwenye kuwa na itikadi na mustakabali wa nchi. Yaani huu huu mwaka ambao maadui walitaka kulibinya taifa la Iran, vijana wetu azizi na wataalamu wetu wakapeleka angani satalaiti ya Nahid, wakapeleka angani satalaiti ya Kavoshgar iliyopiga hatua ikiwa na kiumbe hai; na wakatengeneza ndege za kivita za kisasa. Thamani na umuhimu wa kila moja kati ya haya ni mkubwa kiasi kwamba, ni mahala pake taifa kuonyesha furaha kwa moja kati ya haya, atunge wimbo kuhusu hilo na aandae tamasha. Kazi ni nyingi lakini hazitangazwi kama inavyotakiwa na hakuchukuliwi hatua sahihi za kuzitambulisha (kwa watu). Wakati kiumbe huyu hai alipopelekwa angani na kurejea salama salimini, jambo hili lilikuwa la kushangaza mno kwa wasomi na wataalamu wa dunia na wasimamizi wa masuala ya kimataifa kiasi kwamba, mwanzoni walilikana hili; lakini baadaye wakaona kuwa, hakuna budi kwani wameshuhudia uhakika na ishara sahihi za ukweli wa mambo, hivyo wakalazimika kulikubali hili. Katika uwanja wa masuala ya afya na uhandisi wa kitiba kuna kazi kubwa mno ambazo zimefanyika ambazo zinahusiana na afya na uzima wa watu. Katika uga wa bioteknolojia sisi tumekuwa wa kwanza katika Mashariki ya Kati. Kuna kazi za kitaalamu na muhimu zimefanyika katika uwanja huu na kumezalishwa bidhaa nyingi za madawa kwa msingi huu. Huu ndio ule mwaka ambao (maadui) walilibinya taifa la Iran ili walinyime maisha na matunda ya mambo yote ambayo yanatokana na kipaji cha mwanaadamu. Ni katika mwaka huu katika uwanja wa teknolojia ya nano - ambayo ni mapinduzi makubwa katika uwanja wa teknolojia na viwanda - tulifanikiwa kushika nafasi ya kwanza katika Mashariki ya Kati. Katika mwaka huu huu (1391) vituo kadhaa muhimu vya kielimu vilishika nafasi ya kwanza ya uzalishaji elimu katika Mashariki ya Kati. Katika rekodi za kielimu, uzalishaji elimu, katika kutoa na kueneza makala za kielimu, katika kasi ya ustawi na maendeleo ya kielimu, tulishuhudia maendeleo katika hisa ya nchi ya kuchangia uzalishaji elimu ulimwenguni kote. Katika mashindano ya kielimu ya kiteknolojia ya wanachuo, nchi yetu ilipiga hatua mwaka jana na kupata ongezeko la asilimia 31 ikilinganishwa na mwaka wa kabla yake. Katika mwaka 1391, idadi ya wanachuo iliongezeka kwa namna ambayo ni mara 25 ikilinganishwa na mwanzoni mwa mapinduzi. Wanachuo wanaojishughulisha na masomo hapa nchini hii leo idadi yao ni mara 25 ya wanachuo wa mwanzoni mwa mapinduzi. Haya ni maendeleo makubwa ya taifa la Iran. Katika uwanja wa maji, katika uga wa mazingira, katika masuala ya seli mama, katika teknolojia ya Nano, katika madawa ya mimea na katika teknolojia ya nyuklia, nchi hii imeweza kupiga hatua kubwa mno. Haya yote ni mambo yaliyotokea katika ule mwaka ambao maadui wa taifa la Iran walifanya kila wawezalo na kukusanya nguvu zao zote ni kulikwamisha taifa la Iran.
Kwa hakika matukio ya mwaka 91 ni darsa na mafunzo makubwa kwetu; somo na darsa hilo ni kuwa, taifa ambalo liko hai katu haliwezi kupiga magoti na kusalimu amri mbele ya vitisho, mashinikizo na hatua za mbinyo za adui. Imeeleweka wazi kwetu sisi na kwa watu wote ambao wanafuatilia masuala ya Iran kwamba, kile ambacho ni muhimu kwa taifa ni kutegemea nguvu za ndani, kutawakkali (kumtegemea) kwa Mwenyezi Mungu, kujiamini na kutowategemea maadui; hili ndilo jambo linaloweza kulifanya taifa likasonga mbele. Kwa hakika mwaka uliopita wa 1391 ulikuwa ni uwanja wa mtihani na majaribu na ulikuwa ni uwanja wa mazoezi. Kwa hakika sisi tukiwa taifa la Iran hatujapata ulemavu kutokana na upofu wa adui, tumeweza katika medani na uwanja huu wa majaribio na mazoezi kuonyesha ustadi na umahiri wetu. Tab'an,tumeweza pia kufahamu mapungufu na udhaifu wetu; hii ndio sifa ya mazoezi na majaribio. Katika mafunzo na mazoezi ya upiganaji, katika majarabio na mazoezi ya majimui ya wapiganaji, wahusika na washiriki huweza kufahamu nguvu zao na halikadhalika udhaifu na mapungufu yao na kuyatafutia ufumbuzi mapungufu hayo. Kwa hakika sisi tumefahamu na kutambua udhaifu na mapungufu yetu. Udhaifu wetu katika uchumi ambao umeishia katika ugumu wa maisha kwa matabaka fulani ya wananchi ni kufungamana kwenu na mafuta - kama ambavyo nimesema huu ni moja ya udhaifu wetu - kupuuza sera kuu za kiuchumi na siasa pamoja na sera na maamuzi mtawalia ya kila siku. Maafisa na viongozi wa nchi - maafisa na viongozi wa leo, hususan maafisa wa baadaye watakaoingia madarakani baada ya uchaguzi wa mwaka huu - wanapaswa kuzingatia nukta hii; nchi inapaswa kuwa na sera kuu za kiuchumi za wazi, zilizoandikwa na ambazo zimepangwa na kuratibiwa; matukio tofauti yasiweze kuleta mabadiliko yoyote katika sera hizo.
Somo jingine kubwa tulilopata lilikuwa ni kwamba, nchi imeimarisha msingi wake. Wakati msingi unapokuwa imara na madhubuti taathira za chuki na mipango pamoja na njama za maadui huwa na matunda madogo. Endapo viongozi watayakubali majukumu na masuuliya ya nchi hii kubwa wakiwa na msingi huu imara kisha wakafanya kazi kwa tadbiri, na wakurugenzi lao likawa moja na wakafanya kazi kwa pamoja - hizi ni nasaha ambazo sisi daima tumekuwa tukiwausia maafisa na wakurugenzi wa nchi - wafanye kazi kwa azma na tadbiri, wakati tunaweza kutumia kila kitu na kukibadilisha na kukifanya kuwa ni fursa; Kama ambavyo katika katika mwaka 1391 tulitengeneza fursa kutoka katika vitisho vya maadui na tukaweza kupiga hatua kuelekea mbele. Kile ambacho kimefanywa na viongozi na wananchi wetu azizi katika mwaka 1391, Inshallah kinapaswa kuwa na taathira katika maisha ya wananchi, katika mustakbali wa nchi na kudhihirika na kuonekana katika miaka ijayo.
Tab'an, suala muhimu la uchumi ni jambo ambalo mimi katika miaka ya hivi karibuni na mwaka baada ya mwaka nimekuwa nikilitilia mkazo na kulisisitiza, hata hivyo suala muhimu sio kadhia ya uchumi tu; suala la usalama wa nchi ni muhimu, afya na uzima wa nchi ni muhimu, maendeleo ya nchi ni muhimu na msingi wa kazi ni kazi za kimsingi (miundo mbinu) - ambapo kama katika nchi kutakuwa na maendeleo kama haya, kazi nyingine zote zitakazofuata zitakuwa nyepesi na sahali kuzifanya - istiklali na mamlaka ya kujitawala, izza (heshima) ya kitaifa ni muhimu kwa nchi, taifa fulani kutokuwa chini ya udhibiti na kutokuwa na bwana ni jambo muhimu, satwa, ushawishi pamoja na nguvu za kieneo kwa ajili ya nchi pamoja na himaya ya mamlaka ya kujitawala na usalama wa nchi ni jambo muhimu pia kwa nchi. Kwa hakika sisi tumepiga hatua katika mambo yote haya; katika uwanja wa usalama na vile vile katika uga wa afya na uzima. Aidha tumepiga hatua katika suala la satwa na ushawishi wa kimataifa na katika uwanja wa udhibiti kuhusiana na matukio mbalimbali ambayo yanatokea hapa nchini na katika eneo (Mashariki ya Kati).
Kwa maendeleo liliyoyapata, taifa letu limethibitisha kwamba, kutoishi chini ya kivuli cha Marekani hakuna maana ya kubakia nyuma kimaendeleo; hii ni nukta muhimu. Madola yenye nguvu duniani, wakoloni - katika kipindi ambacho kulikuweko na ukoloni wa moja kwa moja - na leo Marekani yanataka kuyathibitishia mataifa mengine duniani kwamba, kama yanataka kuwa na maisha mazuri na kuwa na maendeleo, ni lazima yawe chini ya kivuli chao. Taifa la Iran limethibitisha kwamba, maneno haya ni urongo mtupu. Taifa letu limethibitisha kwamba, kutofungamana na kutoitegemea Marekani na madola makubwa (ya kibeberu) duniani sio tu sio kubakia nyuma kimaendeleo, bali hupelekea kupatikana maendeleo; sababu ya hilo iko wazi kabisa nayo ni kuwa, nyinyi ilinganisheni Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ya miaka thelathini na miaka thethani ya baadhi ya nchi ambazo ziliishi chini ya kivuli cha Marekani, wamezifurahisha nyoyo zao kwa msaada wa mwaka wa dola bilioni mbili au tatu za Marekani na kusalimu amri mbele ya dola hilo la kibeberu; zitazameni nchi hizo ziko wapi na mtutazame sisi muone tuko wapi? Kuna nchi ambazo zimeufunga mkia wao kwa Marekani na hivyo kuifuata Marekani kila inapokwenda. Mbele yetu kuna tajiriba ya miaka thelathini. Tazameni Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imepitisha vipi miaka hii na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na taifa la Iran limetokea wapi na sasa liko wapi, kisha mzitazame zile nchi ambazo zilikuwa ni kibaraka wa Marekani ziko katika hali gani sasa hivi. Kila mtu ambaye atayatwalii haya atafahamu kwamba, kutofungamana na madola makubwa ni fursa kwa nchi husika na sio tishio; na fursa hii Alhamdulilahi taifa la Iran limeweza kujiletea kwa nguvu zake, ushujaa wake na kwa busara na utumiaji akili wake.
Kuna mambo mawili muhimu hapa ambayo ni lazima niyaseme na mambo haya yanahusiana na mustakbali: Jambo la kwanza ni kwamba, kwanza sisi tunapaswa kuwa mbele ya adui daima katika ratiba na mipango. Taifa linapaswa kuwa amilifu na kutolegalega mkabala na harakati za adui. Kuna haja ya kutumia akili na kukisia mipango ya adui kwa busara na kisha kuiainisha na hivyo kufanya harakati mbele ya adui. Katika moja ya mambo sisi tumefanya hivi na kuona mafanikio yake; mfano mmoja katika hilo ni hili hili suala la kujidhaminia fueli kutoka katika urani iliyorutubishwa kwa asilimia 20 ambayo ni hitajio kwa ajili ya tanuri nyuklia ya utafiti ya Tehran ambapo Radioactive muhimu ambazo ni mahitajio ya nchi zinazalishwa hapo. Tanuru nyuklia hii ya Tehran ilikuwa kikihitajia fueli kutoka katika urani iliyorutubishwa kwa asilimia 20, ambapo sisi hatukuwa tukizalisha asilimia 20 na daima tulikuwa tukiagizia kutoka nje. Maadui wetu wakaona kamba, watumie fursa hii na kuzuia hiyo fueli na hitajio hilo la kitaifa ili waishinikize Jamhuri ya Kiislamu ikubali amri na kutwishwa mambo sambamba na kutaka kuifanya ikubali matakwa yao kupitia hili. Vijana wetu na wasomi wetu wakaweza kuandaa fueli kutoka katika urani iliyorutubishwa kwa asilimia 20 hata kabla mashinikizo y adui hajafikia katika hatua nyeti na kisha kuibadilisha na kuwa mafuta kwa ajili ya kituo hicho cha utafiti.
Wapinzani wetu hawakuwa hata wakifikiria kwamba, sisi tunaweza kulifanya hili; lakini maafisa wa serikali walipohisi hitajio hili basi walifanya mambo kwa wakati; wakavigundua vipaji vya Kiirani na kisha kazi hii ikafanyika kwa mafanikio makubwa. Katika hali ambayo maadui walikuwa wakitaraj kuiona Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ikiwabembeleza na kuwanyenyekea ili ipatiwe fueli kutoka katika urani iliyorutubishwa kwa asilimia 20, Iran ikatangaza kwamba, inajidhaminia mafuta hayo ya asilimia 20 hapa hapa ndani ya nchi na haihitajii tena kuagiza kutoka nje. Kama wasomi wetu, watu wetu wa masuala ya kielimu na vijana wetu wasingefanya kazi hii, basi hii leo sisi ingekuwa ni lazima tunyenyekee, tuombe na kujiendekeza tena kwa kugharamika sana mbele ya watu ambao sio marafiki zetu kwa ajili ya kuomba hilo.
Maafisa na viongozi wa serikali walitabiri na kulifahamu hilo kwa wakati unaofaa; na kukifanya kile ambacho kilikuwa ni lazima kufanywa; na ndio maana tukashinda na kupata ushindi. Hili ni jambo ambalo linahitajia ratiba na mipango kwa ajili ya masuala yote ya kimsingi hapa nchini pamoja na mahitaji yote ya nchi.
Serikali, watu wa masuala ya viwanda, wakulima, wenye mitaji, wajasiriamali, watafiti wa masuala ya kielimu, wapangaji wa masuala ya kielimu na kiviwanda wote wanapaswa kujiandaa kwa ajili ya jukumu hili kubwa la kiakhlaqi na wadhifa huu wa kiakili kabla ya hitajio na kufanya harakati hatua mbele moja mkabala na harakati na mipango ya adui.
Wakurugenzi wa masuala ya uchumi, wahadhiri wa Vyuo Vikuu, jumuiya za kielimu na vituo vya kielimu na kiteknolojia vyote hivi vinapaswa kwa pamoja kushiriki kwa hima na juhudi kubwa katika kazi za kielimu; makala za kielimu zinazoandikwa zinapaswa kuwa na muelekeo huu au zinapaswa kulenga huku, utafiti wa elimu unaofanyika unapaswa kuwa katika upande huu; kazi za kiviwanda zinazofanyika zinapaswa kuwa katika muelekeo huu; wakurugenzi wa serikali, wakurugenzi wa Vyuo Vikuu, wakurugenzi wa masuala ya kielimu na wananchi wanapaswa kufanya harakati katika upande huu. Jukumu letu sote linapaswa kuwa ni kufanya juhudi na hima kwa ajili ya kuimarisha nchi ili isiweze kupenyeka, isiweze kuathiriwa na adui, tuilinde na kuihifadhi; haya ni mambo ya lazima kwa ajili ya uchumi wa kimuqawama ambao sisi tumeuzungumzia. Katika uchumi wa kimuqawama, moja ya nguzo muhimu na ya kimsingi ni kuwa imara uchumi. Uchumi unapaswa kuwa imara. Hii ni nukta ya kwanza ambayo ilikuwa ni lazima niizungumzie.
Jambo la pili: Wamarekani wakitumia njia mbalimbali kututumia ujumbe sisi kila mara kwamba, njooni tufanye mazungumzo ya nyuklia; wamekuwa wakitutumia ujumbe na wamekuwa wakilipigia debe hilo katika propaganda zao duniani. Viongozi wa ngazi za juu na viongozi wa kati wa Marekani mara chungu nzima wanasema kuwa, njooni tukae na tufanye mazungumzo kando ya mazungumzo ya 5+1 kuhusiana na nyuklia.
Yaani Marekani na Iran zikae pamoja yaani mazungumzo ya pande mbili tu na kisha zitajadili kadhia ya nishati ya nyuklia ya Iran. Kwa hakika mimi sina mtazamo mzuri kuhusiana na mazungumzo haya. Kwa nini? Kwa sababu tajiriba na uzoefu wa huko nyuma unaonesha kuwa, katika mantiki ya Marekani mazungumzo hayana maana ya kuja tukae na kutafuta njia ya kimantiki ya ufumbuzi - makusudio yao kuhusiana na suala la mazungumzo sio hili - bali madhumuni na malengo yao kuhusiana na mazungumzo ni tukae na tuzungumze ili nyinyi (yaani Iran) mkubali mitazamo yetu (Marekani)! Lengo la mazungumzo hayo limetangazwa tangu awali; ni lazima kuukubali mtazamo wa upande wa pili. Ndio maana sisi daima tumekuwa tukitangaza kuwa, mazungumzo ya namna hii sio mazungumzo; huku ni kutwisha mambo na Iran katu haikubali kunyongeshwa au kutwishwa mambo. Mimi sina matumaini wala mtazamo mzuri na matamshi haya, lakini hata hivyo sipingi hili. Kuhusiana na hili kuna mambo kadhaa ambayo yanapaswa kuwekwa wazi:
Jambo la kwanza ni kwamba, daima Wamarekani wamekuwa wakituma ujumbe - wakati mwingine wanaandika, baadhi ya wakati wanatuma ujumbe - ya kwamba, hawana nia ya kubadilisha mfumo wa Kiislamu (unaotawala hapa nchini), wanatwambia sisi hivi. Jibu ni hili kwamba, sisi hatuna wasi wasi kwamba, nyinyi mna nia au hamna nia ya kubadilisha mfumo unaotawala hapa nchini, sasa mmeng'ang'ania na mmekuwa mkisisitiza daima ooo sisi hatuna nia ya kubadilisha mfumo unaotawala nchini Iran. Siku ambayo nyinyi mlikuwa na nia ya kutaka kubadilisha mfumo unaotawala hapa nchini na kulitangaza hilo wazi, hamkuweza kufanya chochote na baada ya hapa pia hamtoweza kufanya chochote.
Nukta ya pili: Wamarekani daima wamekuwa wakituma ujumbe kwamba, wana mapendekezo ya nia njema kabisa kuhusiana na suala la mazungumzo; wanadai kwamba, wanatutaka tufanye mazungumzo nao wakiwa na nia njema na ya dhati kabisa na mazungumzo hayo yawe ya kimantiki; yaani yasiwe mazungumzo ya kutwishana mambo.
Mimi ninasema katika kuwajibu ya kwamba: Sisi tumekwambieni mara chungu nzima ya kuwa, hatufanyi juhudi za kuwa na silaha za nyuklia, nyinyi mnasema, hamuamini; kwa nini sisi ni lazima tuyaamini maneno yenu?! Wakati nyinyi hamko tayari kukubali maneno ya kimantiki na yenye nia ya dhati na ya kweli, kwa nini sisi tukubali maneno yenu ambayo mara kadhaa yamethibiti kinyume chake? Tunachokifahamu sisi ni kuwa, pendekezo la mazungumzo linatolewa na Marekani ni mbinu ya Marekani ya kuzihadaa fikra za waliowengi; fikra za waliowengi duniani na fikra za waliowengi za wananchi wetu. Mnapaswa kuthibitisha kwamba, sivyo. Mnaweza kuthibitisha hili? Kama mnaweza basi lithibitisheni.
Natumia fursa hii hapa kusema kwamba, miongoni mwa mbinu za kipropaganda za Marekani ni kueneza uvumi kwamba, wamefanya mazungumzo na watu ambao walitumwa na Kiongozi Muadhamu; hii nayo ni moja ya mbinu nyingine za kipropaganda na ni uongo mtupu. Hakuna mtu ambaye alitumwa na Kiongozi Muadhamu ambaye amefanya nao mazungumzo. Katika mambo kadhaa katika kipindi cha miaka iliyopita, katika serikali mbalimbali kuna watu walifanya nao mazungumzo kuhusiana na maudhui fulani na sisi hatukupinga hilo; lakini hilo ni jambo linalohusiana na serikali. Tab'an, hao pia waliokwenda kufanya mazungumzo na Marekani walitakiwa kuchunga mistari myekundu ya Kiongozi Muadhamu; hii leo pia wanapaswa kufanya hivyo na ni lazima wachunge hilo.
Nukta ya tatu: Kwa mujibu wa tajiriba na kutazama uwanja (uwanja wa mambo) kwa umakini na udadisi tufikia natija hii kwamba, Marekani haina nia ya kumalizika mazungumzo ya nyuklia. Wamarekani hawataki kuona mazungumzo ya nyuklia yanafikia tamati na kadhia ya nyuklia kupatiwa ufumbuzi; kwani kama kweli wangekuwa wanataka kuona mazungumzo haya yanamalizika na kadhia ya nyuklia inapatiwa ufumbuzi njia ya hilo iko karibu ni nyepesi na sahali sana. Katika suala la nyuklia, inachotaka Iran ni kuona kuwa haki yake ya kurutubisha madini ya urani - ambayo ni haki yake ya kimsingi - inatambuliwa na dunia; viongozi wa nchi zenye kutoa madai wakiri kwamba, taifa la Iran lina haki ya kurutubisha madini ya Urani kwa ajili ya matumizi ya amani katika nchi yake na ilifanye hili yenyewe; je haya ni matarajio makubwa? Hiki ndicho kile kitu ambacho tumekisema daima; wao (Marekani na waitifaki wake) hawalitaki hili.
Wao (Marekani na washirikia wake) wanasema kuwa, wana wasi wasi Iran isije ikaenda upande wa kuzalisha na kutengeneza silaha za nyuklia - nchi kadhaa tena chache tu, wanakuja na kuzipa jina la "Jamii ya Kimataifa"! - kisha wanadai kwamba, jamii ya kimataifa ina wasi wasi. Hapana, jamii ya kimataifa haina wasi wasi wowote ule. Akthari ya nchi duniani zipo upande wa Jamhuri ya Kiislamu na wanaunga mkono matakwa ya Iran; kwa sababu takwa la Iran ni takwa la haki. Kama Wamarekani wanataka kadhia hii ipatiwe ufumbuzi njia ya hili ni nyepesi na sahali sana; Wamarekani wangeweza kuitambua rasmi haki ya kurutubisha madini ya urani ya Iran na huu ungekuwa ufumbuzi mwepesi wa kadhia ya nyuklia ya Iran; ili kuondoa wasi wasi wangeweza kuheshimu sheria za wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Nyuklia IAEA; tangu awali sisi hatukuwa tukipinga sheria za Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Nyuklia IAEA.
Kila mara tunapokaribia njia ya kupatia ufumbuzi kadhia hii Wamarekani hujitokeza na kuweka kizingiti na kizuizi katika njia ya kuelekea kupatikana natija katika mazungumzo hayo. Kwa uoni na mtazamo wangu ni kuwa, lengo la Marekani ni kutaka kuona kadhia hii inaendelea kubakia hivi hivi, ili kuweko na kisingizio cha mashinikizo; ambapo mashinikizo hayo - kama walivyosema wenyewe - ni kwa ajili ya kulifanya kilema taifa la Iran. Tab'ani, taifa la Iran katu haliwezi kulemazwa na vikwazo hivyo vya maadui.
Nukta ya nne na ya mwisho katika kadhia hii ni kwamba, kama kweli Wamarekani wanataka kwa nia ya dhati kabisa na ya kweli hii kadhia ifikie mwisho na kupatiwa ufumbuzi wa kudumu mimi ninapendekeza njia za kufikia hilo: Ni kuacha Wamarekani uadui wao dhidi ya taifa la Iran, kwa maneno na kwa matendo. Pendekezo la mazungumzo sio maneno ya kimantiki, madhubuti na ya hoja; haya ndio maneno sasa. Kama wanataka matatizo haya yaliyopo yaondoke na kupatiwa ufumbuzi - ambapo wamekuwa wakisema, "sisi tunataka kusiweko mushkili baina yetu na Iran - basi waache kulifanyia uadui taifa hili (la Kiislamu). Ni miaka 34 sasa ambapo serikali na tawala mbalimbali za Marekani zimepanga na kuweka mikakati ya kulifanyia uadui mbalimbali taifa la Iran kutokana na kuwa na ufahamu ghalati na usio sahihi kuhusiana na Iran na Uirani. Kuanzia mwaka wa kwanza wa ushindi wa mapinduzi na kuundwa mfumo wa Kiislamu, watu hawa (Wamarekani) walitufanyia uadui; katika uwanja wa usalama walipanga mipango na mikakati dhidi ya usalama wetu; walifanya miamala na harakati za chuki na kiadui; walichukua hatua za kiadui dhidi ya ardhi yote ya nchi yetu; daima Wamarekani waliwaunga mkono maadui zetu wadogo na wakubwa katika kipindi cha miaka yote hii; walifanya mambo ambayo yako dhidi ya uchumi wetu wa taifa; walitumia kila nyenzo na suhula dhidi ya taifa la Iran; na Alhamdulilahi, walishindwa katika yote haya; na baada ya hapa kama watataka kuendeleza uadui dhidi ya taifa la Iran watashindwa kama walivyoshindwa huko nyuma. Kwa muktadha huo, ninawapa muongozo viongozi wa Marekani kama wanatafuta njia ya kiakili, basi njia ya kiakili ni hii kwamba, wajirekebishe; warekebishe na kusahihisha matendo na mienendo yao na kuacha kulifanyia uadui taifa la Iran. Hili limekwisha.
Nina jambo jingine ambalo napaswa kulizungumzia jumla jamala nalo ni suala muhimu mno la uchaguzi. Uchaguzi katika nchi yetu ni dhihirisho la Hamasa ya Kisiasa. Kile nilichokisema na ambacho ni wadhifa na jukumu letu na jukumu la matabaka mbalimbali ya wananchi na ambacho tunapaswa kukifanya ni dhihirisho la "Hamasa ya Kisiasa" dhirisho la nguvu ya Kiislamu; na ni dhihirisho la heshima ya mfumo (wa Jamhuri ya Kiislamu unaotawala hapa nchini). Heshima ya Jamhuri ya Kiislamu ina mfungamano na uchaguzi na suala la kujitokeza wananchi katika masanduku ya kupigia kura na jambo hilo lina taathira ya kila mwananchi katika kuwachagua viongozi wa nchi. Uchaguzi ni dhihirisho la irada ya kitaifa na ni nembo ya Demokrasia ya Kidini. Sisi tumezungumzia suala la Demokrasia ya Kidini mkabala na Demokrasia ya Kiliberali ya Magharibi, dhihirisho la demokrasia ya kidini ni haya mahudhurio ya wananchi katika uchaguzi.
Ndio maana kutokana na umuhimu ulionao uchaguzi, maadui wa taifa la Iran daima wamekuwa wakiwaza na kuwazua na kufanya njama za kuhakikisha kwamba, uchaguzi unaofanyika hapa nchini hauwi wa hamasa na wenye mahudhurio makubwa; wamekuwa wakiweka mikakati kuhakikisha kwamba wananchi hawajitokezi katika masanduku ya kupigia kura; na wawakatishe tamaa wananchi. Sisi tumekuwa tukifanya chaguzi mbalimbai katika kipindi chote cha miaka hii - iwe ni uchaguzi wa Bunge au au uchaguzi huo uwe makhususi kwa ajili ya kumchagua Rais wa nchi - daima maadui wetu wamekuwa wakifanya njama za kuukwamisha uchaguzi huu; hii ni kutokana na umuhimu wa uchaguzi katika nchi. Hapa nitataja nukta kadhaa kuhusiana na uchaguzi. Tab'an, bado kuna fursa ya miezi miwili na ushei hadi kufanyika kwa uchaguzi huo; kama Allah atanijaalia umri, Inshallah nitazungumzia masuala yanayohusiana na uchaguzi katika fursa nyingine; kwa sasa nitataja nukta kadhaa tu.
Nukta ya kwanza ni hii kwamba, katika hatua ya awali kuna haja ya kuandaa mazingira na uwanja mzuri wa ushiriki na mahudhuriomakubwa ya wananchi katika uchaguzi. Hili ni jambo lenye umuhimu mkubwa sana. Hamasa ya uchaguzi na mahudhurio ya wananchi katika masanduku ya kupigia kura ni jambo lenye umuhimu. Kushiriki kwa wingi na kwa hamasa kubwa wananchi katika uchaguzi huo sambamba na kudhamini usalama wa nchi, kutapelekea pia kutokuwa na athari vitisho vya maadui na kutawakatisha tamaa kabisa maadui wa taifa hili. Wananchi wetu wote azizi walioko katika kila kona ya nchi hii wanapaswa kulitambua hili; mahudhurio yao makubwa katika masanduku ya kupigia kura ni jambo ambalo lina taathira kwa mustakbali wa nchi; katika usalama, katika mamlaka ya kujitawala, katika utajiri wa kitaifa, katika uchumi na katika masuala yote muhimu ya nchi, jambo hili lina taathira kubwa. Hii ni nukta ya kwanza; ambapo uchaguzi unapaswa kufanyika kwa tawfiki ya Mwenyezi Mungu, kwa auni na msaada Wake Mola Mlezi na kwa hima ya taifa la Iran na ushiriki mkubwa wa wananchi wa taifa hili.
Nukta ya pili: Uchaguzi hauwahusu watu wa mrengo mmoja na wa fikra moja tu, bali ni jukumu na ni haki ya watu wote wenye uchungu na nchi na wanaojali manufaa ya taifa na uhuru wa nchi yao. Uchaguzi ni mali ya watu wote ambao wanaitakidi mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu, wenye kuwa na imani na mamlaka ya kujitawala nchi na ambao wanatilia umuhimu mustakbali wa nchi na ambao wana uchungu na maslahi ya kitaifa; hawa wanapaswa kushiriki katika uchaguzi. Kuupa mgongo uchaguzi ni jambo linalofanywa na watu ambao wanaupinga mfumo wa Kiislamu.
Nukta ya tatu, hatimaye kura za wananchi ndizo zenye kuainisha mambo. Kile ambacho kina umuhimu ni chaguo lenu na kura zenu. Kwa hakika, uamuzi wa wananchi juu ya nani bora zaidi kati ya wagombea ni jambo muhimu na wananchi wanapaswa kufanya uchunguzi wa kina kuhusu wagombea ili waweze kupata utulivu wa moyo kuhusu mtu anayefaa zaidi kwa ajili ya kumpa dhamana ya kubeba jukumu hilo. Kiongozi Muadhamu hana kura zaidi ya moja. Mimi mja dhaifu kama walivyo wananchi wengine, nina kura moja; na kabla ya kura hiyo kutiwa katika sanduku la kupigia kura, hakuna mtu atakayejua kwamba amempigia nani kura. Yamkini watu wanaoshughulikia masanduku ya kupigia kura, baada ya zoezi la upigaji kura yaani wakati wa kuhesabu kura wakafungua masanduku hayo na kufahamu hati yangu na hivyo kuelewa nimempigia nani kura; lakini kabla ya kupigwa kura, hakuna mtu atakayefahamu nitampigia nani au ninataka kumpigia na kumpa kura yangu nani. Matamshi na maoni yoyote yale kuhusiana na kwamba Kiongozi Muadhamu anamuunga mkono mgombea fulani kuliko wagombea wengine, kwa kweli ni maneno ambayo hayana ukweli wowote. Tab'an, siku hizi kuna suhula na vyombo vya upashaji habari vya ajabu - kama njia hii ya kutuma ujumbe mfupi kwa njia ya simu na mfano wa hayo -, inasikitisha kwamba, kuna mengi ambayo yamekuwa yakisemwa na kuenezwa habari zinazonasibishwa na watu na mambo fulani.
Wakati mwingine mtu hutuma jumbe fupi elfu moja. Nimepatiwa ripoti kwamba, yamkini katika masiku ya uchaguzi yamkini siku moja watu wakatuma na kupokea jumbe milioni kadhaa. Kuweni macho yasije masuala ya pembeni yakakuathirini katika kuchagua mtu anayefaa zaidi na msije mkatekwa na matamshi yanayotolewa kwenye vyombo mbali mbali vya habari ikiwa ni pamoja na wimbi kubwa la ujumbe mfupi uliojaa katika zama hizi. Tab'an, kila mtu au mwanaharakati wa kisiasa anaweza kuwashawishi watu wengine ili wakubaliane na maoni yake - hili halina tatizo - lakini kutoka kwangu mtu hatosikia kitu.
Katika hali ya hivi sasa wananchi wanaweza kuzungumza baina yao kuhusiana na suala la uchaguzi, wausiane, wabadilishane mawazo, wakinaishane, wajadiliane na wasaidiane kwa ajili ya kumtambua mgombea bora zaidi. Ala Kulli haal, kile ambacho ni kigezo cha amali ni kura za wananchi.
Nukta ya nne: Katika suala la uchaguzi na lisilo la uchaguzi, watu wote wanapaswa kusalimu amri mbele ya sheria; na kuheshimu sheria. Yale matukio yaliyotokea mwaka 1388 Hijria Shamsia (2009 ) - na ambayo yalikuwa na madhara kwa nchi - yote hayo chimbuko lake lilikuwa ni kuweko watu waliokataa kuheshimu sheria na hawakuwa tayari kuheshimu kura na maamuzi ya wananchi. Yamkini kura za wananchi zikawa kinyume na kile kitu ninachotaka mimi; lakini ni lazima niheshimu uamuzi huo wa wananchi. Ni lazima watu waheshimu uamuzi wa wengi, na kile ambacho akthari ya wananchi wamekiamua; watu wote wanapaswa kuheshimu hilo.
Kwa bahati nzuri kuna utatuzi wa kisheria kwa ajili ya kuondoa mushkili, kosa na shubha (utata) iliyopo; wahusika watumie fursa na utatuzi huu wa kisheria. Hii kwamba, baada ya matokeo (ya uchaguzi) kuwa kinyume na matarajio yetu tuamue kuwachochea wananchi na kuwataka wajitokeze mabarabarani - ambapo jambo hili lilitokea mwaka 1388 Hijria Shamsia mwafaka na 2009 nadhani) - ni moja ya makosa yasiyoweza kufidika. Jambo hili limekuwa funzo na tajiriba kwa taifa letu na bila shaka wananchi wa taifa hili daima watasimama kukabiliana na matukio kama haya.
Nukta ya mwisho: Watu wote wanapaswa kutambua kwamba, rais ajaye ambaye tunamtaka sisi ni yule ambaye sambamba na kuwa na sifa za Rais aliyemtangulia awe mbali pia na udhaifu aliokuwa nao Rais aliyekuwa kabla yake. Bila shaka kila mtu ana nukta zenye nguvu na ana nukta pungufu yaani ana madhaifu pia. Marais wa nchi - iwe ni Rais wa sasa au Rais wa baadaye - ana nukta zenye nguvu na nukta dhaifu. Sote tuko namna hii; yaani tuna nukta zenye nguvu na tuna mapungufu pia. Kile ambacho leo kinahesabiwa kuwa ni nukta yenye nguvu kwa serikali na Rais wa sasa wa nchi ni mambo ambayo anapaswa kuwa nayo Rais ajaye na anapaswa kuwa na mambo haya; amma yale ambayo leo yanahesabiwa kuwa ni mapungufu ya Rais na serikali ya sasa - ambapo yamkini nyinyi mkasema na kuyataja hayo mapungufu, mimi nikayasema na mwingine akaja na kuyasema - Rais ajaye pamoja na serikali yake wanapaswa kujitenga mbali kabisa na mambo haya. Yaani mlolongo wa serikali zinazokuja na kuingia madarakani hapa nchini zinapaswa kusonga mbele na kuwa kamili zaidi kuliko serikali zilizopita na hivyo hatua kwa hatua tunapaswa kuwachagua watu ambao ni bora zaidi. Yaani inabidi chaguo la wananchi katika uchaguzi ujao wa Rais lioneshe kuweko maendeleo na kukamilika zaidi na liwe chaguo bora zaidi kuliko machaguo yote bora yaliyotangulia na hilo linatakikana katika kila kipindi cha uchaguzi.
Watu wanaoingia kwenye kinyang'ayiro cha uchaguzi wa Rais wanapaswa kuwa ni wenye kushikamana na Mapinduzi ya Kiislamu na matukufu ya Jamhuri ya Kiislamu, wawe ni wenye kufungamana na manufaa ya taifa na wawe ni watu ambao wanaamini wajibu wa kuendeshwa nchi kimantiki, kushirikishwa watu wote, tadbiri na kwa umakini wa hali ya juu. Nchi inapaswa kuongozwa namna hii. Nchi hii ni nchi kubwa; wananchi nao ni wananchi wenye adhama na kuna masuala mengi ya kushajiisha na ambayo ni bishara njema, kuna matatizo katika njia ya kila taifa ikiwemo njia ya la Iran. Watu ambao wanajiandaa kwa ajili ya kuingia katika njia hii wanapaswa kuwa wakamilifu wa nguvu, watawakkali na kumtegemea Mwenyezi Mungu na wasonge mbele wakiwa na imani na uwezo wa taifa hili.
Ewe Mwenyezi Mungu! Tunakuomba ulijaalie taifa hili kile ambacho ni cha kheri na chenye manufaa na maslahi na nchi hii. Ewe Mwenyezi Mungu! Ujaalie moyo mtakatifu wa Waliul Asr uwe na furaha. Ewe Mwenyezi Mungu! Tunakuomba uifanye roho ya Imam (Imam Khomeini RA) pamoja na roho za mashahidi wetu azizi ziwe zenye kuturidhia. Kile ambacho tumekisema kikubali na ukifanye kuwa kiwe katika njia Yako.
Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.
 
< Nyuma   Mbele >

^