Skip to content

Habari

Habari
Hifadhi

Risala na Barua

Matini
Hifadhi

Kumbukumbu na Simulizi

Kabla ya Mapinduzi
Baada ya Mapinduzi

Sauti na Taswira

Picha
Sauti
Video
Hotuba ya Kiongozi Muadhamu Mbele ya Wafanyakazi na Wadau wa Sekta ya Uzalishaji Chapa
27/04/2013

Ifuatayo ni hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika mkutano na wafanyakazi na wadau wa sekta ya uzalishaji nchini kwa mnasaba wa kukaribia Siku ya Wafanyakazi Duniani

Kwa jina la Allah Mwingi wa rehema Mwenye kurehemu

Ninakukaribisheni akina kaka na akina dada wapenzi, (ambao ni) rasilimali yenye thamani ya ustawi na maendeleo ya nchi, nyuso teule na aminifu za watu ambao mnabeba mzigo mzito wa kazi za moja ya sekta ngumu kabisa ya uendeshaji nchi na ya maendeleo ya nchi na katika njia ya saada ya taifa hili. Inshallah Mwenyezi Mungu authamini usumbufu wenu na jitihada zenu na inshallah nyote mpate jaza na malipo Yake Mola.
Katika mnasaba wa Siku ya Wafanyakazi ni kawaida kwa waandishi na wazungumzaji kuzungumzia sifa njema za tabaka la wafanyakazi; na bila ya shaka ni mahala pale kufanya hivyo.

Ukiachilia mbali kwamba ni kwa kiasi gani kuzungumza na kuandika kuna thamani na umuhimu katika kupandisha na kuinua hadhi na nafasi ya mfanyakazi, sifa bora ya msingi na ya asili ya nguvukazi katika jamii ni kwamba kwa mwili wake, roho yake na ubongo wake, mfanyakazi anadhamini maendeleo ya nchi na ustawi wa watu. Ni sawa kwamba kuna vitu vingine pia vyenye taathira katika suala hili - kama rasilimali ya mtaji na rasilimali ya uongozi - na hayo pia yanapasa kuthaminiwa, lakini mfanyakazi anaifanya kazi hiyo kwa mwili wake na roho yake; hili lina thamani maradufu.
Kama katika nchi yoyote ile haitokuwepo rasilimaliwatu au ikawa dhaifu au ikawa haina umahiri au fikra yake na akili yake ikashughulishwa na mirengo mbalimbali ya kisiasa, nchi hiyo itapooza. Nyinyi majimui ya wafanyakazi nchini ni uti wa mgongo; na kwa kiwango kikubwa ni nyinyi ndio mnaozuia nchi isifikie hali ya kupooza; hili linapasa lijulikane na hili inapasa watu wote walifahamu na walijue. Katika kujenga utamaduni wa suala hili wananchi wanapaswa waijue thamani ya kazi; na vilevile katika uga wa utendaji pia watungaji sheria na watekelezaji wanapaswa muda wote wayazingatie mambo haya. Ikiwa tabaka la wafanyakazi katika nchi yoyote ile litakuwa linapata huduma nzuri za jamii, ikiwa litakuwa na moyo wa matumaini na litakuwa na usalama wa kazi, harakati ya nchi hiyo kuelekea kwenye maendeleo itakuwa nyepesi; huu ni uhakika wa mambo; hili ni jambo tunalopaswa kulielewa sote.
Mimi ninaamini kwamba katika nchi yetu umuhimu wa tabaka la wafanyakazi ni mkubwa hata zaidi ya huo. Haya yaliyoelezwa yanahusiana na kila mahala, na yanahusiana na nchi zote; lakini katika nchi yetu kuna suala la ziada nalo ni kwamba wafanyakazi, mbali na kutekeleza majukumu yao ya kikazi wametekeleza vizuri pia majukumu yao ya Mapinduzi na ya nchi. Tangu mwanzoni mwa Mapinduzi hadi ushindi wa Mapinduzi, harakati adhimu ya wafanyakazi ilikuwa moja ya funguo za ushindi - wafanyakazi wa shirika la mafuta na wengine na wengine - na pia katika wakati wa Vita vya Kulazimishwa. Katika medani ya vita, kila upande aliokuwa akiangalia mtu, kama kulikuwa na nafasi tupu basi ilijazwa na wafanyakazi vijana na wafanyakazi wa rika la makamo. Katika harakati mbalimbali za kisiasa pia wafanyakazi hawakutekwa na ghiliba za watu waliokuwa wakitaka kuitumia majimui ya wafanyakazi isimame dhidi ya Mapinduzi na dhidi ya Mfumo wa Kiislamu. Haya si mambo madogo. Tab'an kuna wengi sana ambao hawaujui ukweli huu; sisi tumeyashuhudia haya kwa karibu.
Katika siku zilezile za ushindi wa Mapinduzi, mimi binafsi nilikwenda kuonana na majimui moja ya wafanyakazi katika eneo la magharibi mwa Tehran; huko nikajionea ni mambo gani wanayafanya maadui wa Uislamu na maadui wa Mapinduzi; ni njama gani, ni mipango gani na ni mikakati gani walikuwa wakiipanga ili katika kipindi kilekile cha mwanzoni na katika wakati uleule wa awali wa kuanza kuchomoza miale ya mwanga wa Mapinduzi waweze kulitumia tabaka la wafanyakazi kwa ajili ya kuimarisha satua na ushawishi wao wa kisiasa uliokuwa na utegemezi kwa baadhi ya madola. Mimi nilijionea hili kwa karibu. Na katika kukabiliana na hilo nikaliona tabaka la wafanyakazi wetu waumini ambao kwa baraka za imani, kwa baraka za imani waliyokuwa nayo kwa Imamu Muadhamu (Khomeini) na kwa maulamaa, jinsi walivyosimama waziwazi na kwa ushujaa wa aina yake kukabiliana na watu hao; na hili limekaririwa tena katika kipindi cha miaka kadhaa. Leo miaka thelathini na nne imepita tokea siku zile. Kuna wengi ambao walitaka, walifanya jitihada na walitumia fedha ili waweze kulitumia tabaka la wafanyakazi kwa ajili ya kukabiliana na Mfumo wa Kiislamu; lakini tabaka la wafanyakazi limesimama imara; hili ni jambo muhimu sana. Haya ni mambo yanayotudhihirishia thamani ya majimui ya wafanyakazi wetu, thamani yao ya kiutu, thamani yao ya kimapinduzi na thamani yao ya ustaarabu; haya ni mambo yanayopasa kujengewa utamaduni; haya ni mambo wanayopaswa watu wote kuyajua na kuyafahamu; na nyinyi wafanyakazi mnapaswa kujivunia.
Mwaka uliopita tulisema kuwa ni mwaka wa "Kutoa Msukumo kwa Kazi na Rasilimali za Kiirani". Suala hili haliishii katika mwaka mmoja tu. Hivi sasa jamaa na wakuu husika wanatoa ripoti kuwa kazi hizi zimefanyika; ni vizuri sana na Mwenyezi Mungu aitie baraka kila kazi inayofanywa kwa nia sahihi; lakini kazi inapasa iendelezwe kwa uzito mkubwa na kwa sura ya msingi mkuu; hili ni jukumu la watu wote. Huu ujengaji utamaduni wa suala hili tulioueleza sehemu yake moja muhimu iko hapa.
Tulisema: Uzalishaji wa Ndani; Kazi za Kiirani, Rasilimali za Kiirani. Hii maana yake ni kwamba marembo na mapambo ya majina (ya bidhaa) za kigeni yasivutie na kuteka macho ya watu. Watu wote wajue kwamba bidhaa hii wanayonunua inaweza kumneemesha mfanyakazi wa kiwandani wa Kiirani; na inaweza kumkosesha na kumneemesha mfanyakazi wa kiwandani wa kigeni. Hakuna shaka kuwa sisi tunawapenda wanadamu wote, lakini mfanyakazi wa kiwandani wa Kiirani yeye anafanya juhudi kwa ajili ya kuiletea heshima nchi hii; ni kiungo kimoja azizi na chenye thamani cha mwili wa taifa hili; kwa hivyo inapasa kumuunga mkono na inapasa kumtia nguvu. Baadhi ya watu hawalifahamu na hawalielewi hili au kwao wao hakuna tofauti kati ya nembo ya bidhaa inayozalishwa Iran na ile ya kigeni; au hata kinyume chake, badala ya kutafuta bidhaa yenye nembo ya Kiirani wanatafuta zile zenye nembo za kigeni; huku ni kwenda pogo, hili ni kosa. Maneno haya yanawahusu watu wote.
Mimi ninasisitiza na ninatilia mkazo kwa kuwaomba wananchi wote wa taifa la Iran: elekeeni kwenye upande wa matumizi ya bidhaa zinazozalishwa ndani; hili si jambo dogo, hili si jambo lenye umuhimu mdogo; hili ni jambo lenye umuhimu mkubwa. Bila ya shaka vyombo vya utawala na vya serikali - serikali kwa maana yake pana - vina jukumu maradufu katika suala hili. Wakati wizara fulani, shirika fulani na idara fulani zinapotaka kukidhi mahitaji yake ya ndani zisitumie bidhaa ya nje asilani; ziende kutumia bidhaa zinazozalishwa ndani. Bila ya shaka katika upande huu pia wazalishaji wa ndani - iwe ni yule mudiri, yule mfanyakazi wa kiwandani au yule mwekezaji - wanatakiwa na wanasisitizwa kuzalisha bidhaa safi, nzima na iliyokamilika. Yote hayo mawili yameashiriwa na Uislamu na kuamrishwa na dini yetu tukufu. Kufanya kazi kwa umakini tumetakiwa kufanya hivyo na Mwenyezi Mungu, kumheshimu mfanyakazi tumetakiwa kufanya hivyo na Mwenyezi Mungu; kumdhaminia mfanyakazi usalama wa maisha na kazi yake tumetakiwa kufanya hivyo na Mwenyezi Mungu na kudhamini usalama wa mtaji wa uwekezaji pia tumetakiwa kufanya hivyo na Mwenyezi Mungu.
Wakati haya yanapozingatiwa kwa pamoja hapajitokezi tena hali hii ya kufurutu mpaka inayoletwa kwa kutumia majina mbalimbali, iwe ni katika eneo la harakati za uchumi wa Uhuria (Uliberali) au kama wanavyodai wenyewe soko huru - huru kwa ajili ya bepari, lakini ni kifungo, mahabusu na mbinyo kwa tabaka la wanaodhulumiwa na mafakiri; hali ambayo radiamali yake na misuguano yake mnaiona leo hii huko Ulaya - au katika uga wa Usoshalisti. Hoja kubwa zaidi ya kuonyesha kuwa uchumi unaoitwa eti wa Uhuria ni mbovu ni haya matukio yanayojiri leo hii Ulaya na yanayoanza kujitokeza Marekani. Katika medani ya utendaji na uga wa tajiriba, uchumi wa kibepari umeonyesha kuwa ni mbovu na umefeli; hauna faida na tijara hata kwa yale matabaka ambayo uchumi huu ulikuja kwa lengo la kuyanufaisha. Tabaka la wafanyakazi za vibarua linajulikana kwamba kwa miaka mingi lilikuwa likikandamizwa huko, lakini hauna faida hata kwa mabepari wenyewe, wenye mabenki na wamiliki wa mashirika na makampuni makubwa makubwa; na huu ni mwanzo tu, baada ya hapa hali itakuwa mbaya zaidi. Wanatoa ahadi tu kwamba tutarekebisha, tutarekebisha; hawatoweza kuirekebisha. Njia hii ni njia ya maporomoko ya mtelezo; wamo wanaelekea chini, na hii ni sehemu moja ya kuyumba kwa ustaarabu mbovu na wa kimaada wa Magharibi; upande wao wa kikhlaqi, kiitikadi, kinadharia na kifikra una hesabu yake mbali. Mambo haya ni funzo na tajiriba kwetu. Kwa upande wa uga wa Usoshalisti nao pia tangu miaka na miaka nyuma ulionyesha jinsi ulivyoshindwa na ulivyofeli.
Uislamu una mtazamo wa wastani, wa kumzingatia mtu na wa kuzingatia uadilifu katika nyuga zote ukiwemo uga huu; ni wa kuzingatia upande huu na pia wa kuzingatia upande ule; ni wa utangamano baina ya mawili haya ni si kugongana; na yote yanazingatia kutekeleza wajibu wa kidini na kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu ni Mwenye kuoa na Mwenye kushuhudia. Haya yanapasa yawe ni utamaduni wa maisha yetu na ndivyo uwe utendaji wetu.
Tumesema "Hamasa ya Kisiasa" na "Hamasa ya Kiuchumi". Hamasa ya kiuchumi haiko mikononi mwa serikali peke yake; bila ya shaka mipango inayoratibiwa na serikali ina taathira. Hamasa maana yake ni tukio linalotekelezwa kwa sura ya kijihadi na kwa msisimko wa ukakamavu; hili linapasa lizingatiwe na wananchi wa Iran na viongozi nchini; wafidie udhaifu na kujaza uwazi uliopo; na kwanza wautambue. Katika mipango yote inayoratibiwa inapasa yazingatiwe maisha na hali ya matabaka dhaifu; kisha ziandaliwe ratiba kwa ajili yao. Hii itakuwa ni hamasa. Wananchi wote, iwe ni katika matumizi yao au katika uzalishaji wao; sekta za uzalishaji kwa namna moja, upande wa wanunuzi na watumiaji kwa namna nyengine na sekta za utoaji huduma pia kwa namna yao; wote hao wajue kwamba kwa ajili ya maendeleo ya nchi kuna ulazima wa kuwa na harakati ya hatua kubwa mbele, kuna ulazima wa kutekeleza hamasa; hapo ndipo nchi itapiga hatua mbele na itaweza kuwa na uthabiti. Hamasa ya Kisiasa na Hamasa ya Kiuchumi ni vitu viwili vinavyotangamana; kila kimoja kinakitia nguvu kingine, kinakilinda na kukidumisha.
Wakati mwanzoni mwa mwaka tulipozungumzia Hamasa ya Kisiasa na Kiuchumi tulielewa tulichokuwa tukikisema; adui pia alifahamu ni nini tunachokisema. Kwa vikwazo na mashinikizo mbalimbali ya kiuchumi, adui alijaribu kuwatoa wananchi nje ya medani. Eti wanasema 'sisi hatuna uadui na wananchi'. Wanasema uwongo; bila ya hofu na bila ya kuona haya! Mashinikizo zaidi wanayotoa ni kwa lengo la kutaka wananchi waudhike, kuwaweka wananchi kwenye hali ya dhiki na kuwaweka wananchi kwenye mashinikizo ili labda kwa njia hiyo waweze kuleta mpasuko baina ya wananchi na Mfumo wa Kiislamu. Lengo ni kuwaweka wananchi kwenye mashinikizo. Ikiwa harakati hii adhimu ya kiuchumi, huu mwendo wa hatua ya mpigo kuelekea mbele na huu upangaji sahihi wa ratiba, iwe ni katika upande wa utungaji sheria, katika upande wa utekelezaji au katika ngazi tofauti utazingatiwa na kupewa umuhimu mashinikizo yote haya yatazimwa. Wananchi wa Iran na viongozi nchini wanatakiwa wawe na azma thabiti ya kumkatisha tamaa adui.
Ni hivihivi pia kwa upande wa Hamasa ya Kisiasa. Hamasa ya Kisiasa maana yake ni kujitokeza wananchi kwa uelewa kamili katika uga wa siasa za nchi na katika uendeshaji nchi; mfano wake hai kabisa ni hili tukio la uchaguzi, ambalo muda mfupi ujao inshallah kwa taufiki ya Mola na kwa wakati uliopangwa, utafanyika kwa ushiriki na mahudhurio yenye msisimko mkubwa ya wananchi. Kwa kuwa (maadui) wamefahamu ni nini lengo la Hamasa ya Kisiasa na Hamasa ya Kiuchumi, tokea hivi sasa, na kwa dhana zao wameshaanza kufanya hujuma. Leo kuna anuai na kila namna za propaganda zenye lengo la kuwakatisha tamaa na kuwavunja moyo wananchi katika uga wa uchumi na kupunguza nguvu ya moyo wa wananchi wa kujitokeza kwenye medani ya siasa na hasa katika medani ya uchaguzi. Wao hawajawatambua wananchi wa Iran. Harakati hii adhimu ya wananchi wa Iran katika nyuga tofauti haijaweza kuwazindua na kuwatoa kwenye mghafala na ujinga walionao wapangaji na waandaaji sera nyuma ya pazia wa Uistikbari; hawajui wanayekabiliana naye ni nani. Katika muda wote huu wa miaka thelathini na ushei, taifa hili limesimama imara licha ya kukabiliwa na upinzani wote huu pamoja na uadui wote huu. Ikiwa viongozi wameweza kusimama imara katika wakati fulani ilikuwa ni kutokana na msukumo wa wananchi na uungaji mkono wa wananchi. Heko ya kwanza ni ya wananchi, pongezi kubwa wanastahiki wananchi; ni wao ndio waliokuwa wakiwapa moyo viongozi na kutoa msukumo kwao wa kuweza kusimama imara kukabiliana na ubabe, mashinikizo na uchu wa maadui na Waistikbari pale waliposimama imara kukabiliana nao. Leo hii pia ni vivyo hivyo, na katika mustakabali pia, kwa taufiki ya Mwenyezi Mungu, ndivyo itakavyokuwa.
Suala la uchaguzi ni suala muhimu. Uga wa uchaguzi ni uga wa kudhihiri nguvu za taifa katika nchi yoyote. Taifa (hili) lililoko hai, lina uchangamko, linategemea irada ya Mwenyezi Mungu, lina uhakika wa kupata msaada wa Mwenyezi Mungu, na ni taifa litakalopata ushindi katika nyuga zote; na katika uga huu pia ndivyo itakavyokuwa.
Tumesema kwamba watu wenye utashi wa aina tofauti (kisiasa) na kila mtu anayehisi kuwa anao uwezo basi na aje ajitose uwanjani; nao umma wa wananchi na umati adhimu wa makumi ya mamilioni ya watu inshallah watajitosa katika medani (kuwachagua); lakini katika kupanga mahesabu, wale watu wanaotaka kuwa wagombea wasije wakafanya makosa; wajue ni nini maana ya uongozi wa kuendesha nchi. Wasifanye makosa katika kutathmini hitajio la nchi kwa mtu mwenye uwezo wa utendaji na wala wasifanye makosa katika kutathmini uwezo wao wenyewe walionao. Kama watakuwa wamefanya tathmini sahihi basi na wajitokeze uwanjani, wananchi nao watawaangalia na kuwachagua.
Kanuni na taratibu za uchaguzi katika nchi yetu ni kanuni na taratibu madhubuti. Kwamba baadhi ya watu wanakaa huku na kule kulalamika, kwa kweli (malalamiko hayo) hayana mantiki; (ni malalamiko) ambayo kwa kweli si ya mahala pake. Kuwepo Baraza la Walinzi wa Katiba - na Imam (Khomeini) alikuwa akilisisitiza hilo mara kwa mara - kwa kweli ni uwepo wenye baraka. Utambuzi wa Baraza la Walinzi wa Katiba ni utambuzi wa jopo la watu waadilifu, wasio na upendeleo na wenye uono mpana kuhusiana na kuwachunguza watu wenye sifa; hili ni jambo lenye baraka kwetu na kwa wananchi wote. Kisha baada ya hapo kati ya watu waliotambulika kuwa wanafaa, wananchi wanazunguka, wanafanya uhakiki, wanawauliza watu, wanawauliza wale wanaowaamini, wanaangalia rekodi za wagombea, wanaangalia sha'ar zao na wanaangalia maneno na kauli zao kisha wanachukua uamuzi.
Mgombea wa uchaguzi, kwanza anapaswa awe na itikadi na imani ya Mwenyezi Mungu, kwa Mapinduzi, kwa katiba na kwa wananchi; pili awe na moyo wa muqawama. Taifa hili lina malengo makubwa, lina kazi kubwa za kufanya, hakuna kusalimu amri, hakuna mtu anayeweza kuzungumza na taifa hili kwa lugha ya ubabe. Watu wanaokuwa katika nafasi za juu kabisa za utendaji wanapaswa wawe watu ngangari na wenye muqawama wa kukabili mashinikizo ya maadui; wasiwe watu wa kuingiwa na hofu haraka, wasitoke nje ya medani haraka; hili ni moja ya masharti ya lazima. Tatu, wawe ni watu wenye tadbiri na wenye hekima. Katika siasa za nje, sisi tumesema"Izza, Hekima na Maslahi"; katika uendeshaji nchi pia ni vivyo hivyo, katika masuala ya ndani pia ni hivyohivyo, katika uchumi pia ni hivyohivyo; inapasa wajitose uwanjani wakiwa na ratiba maalumu, wakiwa na hekima, wakiwa na tadbiri, wakiwa na mtazamo wa muda mrefu na wa pande zote, na wa kuangalia mambo kwa mahesabu na mikakati sahihi.
Kufikiria masuala ya uchumi kwa mahesabu ya kila siku tu kuna madhara; kubadilisha sera za kiuchumi kila mara kuna madhara - na hili ni katika sekta zote na hasa ya uchumi - kutegemea mawazo yasiyo ya kitaalamu kuna madhara; kutegemea mbinu za utiaji jeki za chumi za uburuzaji za Mashariki na Magharibi kuna madhara. Sera za uchumi zinapasa ziwe sera za "Uchumi wa Muqawama". Uchumi wa muqawama unapasa uwe uchumi ulio madhubuti katika muundo wake wa ndani, uweze kusimama imara; usiyumbe kutokana na mabadiliko mbalimbali yanayojiri katika pembe hii ya dunia na pembe ile ya dunia; hivi ni vitu vya lazima. Rais anayetaka kuongoza nchi hii kubwa na kukata masafa ya njia hii ya kujivunia kwa msaada wa wananchi na kwa ajili ya wananchi, anapaswa kuwa na sifa hizi maalumu. Nne, anapaswa awe amejitakasa kikhlaqi, kwa kutoshughulika na mambo yasiyo na msingi. Haya ni mambo ya lazima. Huu umekuwa ndio wasia wangu wa kila mara kwa serikali zote. Mnajua kwamba daima mimi nimekuwa nikizihami serikali na marais katika kipindi cha miaka yote hii; nimekuwa nikiziasa, na katika mara nyingi nimekuwa nikitaka maelezo kwao pia. Mkazo zaidi umekuwa ni kwamba wasiwabebeshe gharama wananchi, wasiwaletee matatizo, wasiwatie tafrani, wasiwatie wananchi wasiwasi na tashwishi; na tab'an wasiwape ahadi zisizo na sababu wala zisizo na msingi, wasifungue mlango pia wa utoaji ahadi zisizo za kimantiki; waipeleke mbele harakati kimantiki, kibusara, kulingana na hali halisi na kwa kutawakali kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu; inapasa katika mustakabali inshallah iwe hivi pia.
Tulichofahamu kutokana na tajiriba ya miaka mingi ya Mapinduzi ni kwamba kwa fadhila zake Mwenyezi Mungu Mtukufu na kwa mwongozo wake, taifa hili litawashinda maadui zake wote; wao wenyewe maadui watasadikisha - kama ambavyo leo hii pia wanasadikisha - na mtu yoyote yule atakayepambana na taifa hili, na harakati hii adhimu liliyoanzisha, na moyo huu wa imani ya kina iliyokita ndani ya taifa hili, bila ya shaka atashindwa tu.
Tunamwomba Mwenyezi Mungu Mtukufu aujaalie mustakabali wa taifa hili azizi na nchi hii uzidi kuwa bora siku baada ya siku zaidi ya ilivyokuwa huko nyuma, na kukupeni ushindi wa mtawalia nyinyi wananchi wapenzi. Inshallah fahari ambazo tabaka la wafanyakazi na majimui adhimu za wafanyakazi zimeweza kuleta hadi hii leo, ziweze kuleta fahari maradufu katika mustakabali, na inshallah sura ing'arayo ya rasilimali ya kazi na mfanyakazi izidi kudhihirika zaidi mbele ya wananchi wetu.
Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabaraakatuh.

 
< Nyuma   Mbele >

^