Skip to content

Habari

Habari
Hifadhi

Risala na Barua

Matini
Hifadhi

Kumbukumbu na Simulizi

Kabla ya Mapinduzi
Baada ya Mapinduzi

Sauti na Taswira

Picha
Sauti
Video
Makamanda na Wafanyakazi wa Jeshi la Sepah Waonana na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Chapa
17/09/2013
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, leo asubuhi (Jumanne) ameonana na makamanda na maafisa wa ngazi za juu pamoja na maafisa wengine wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH na kuitaja rekodi inayong'ara ya SEPAH kuwa ni uthibitisho wa utambulisho wa kina, uzoefu wenye mafanikio na heshima kubwa ya taifa la Iran na huku akibainisha maana ya "ulinzi wa umma" inayokusudiwa na Mapinduzi ya Kiislamu (na kama lilivyochukua jina hilo jeshi la SEPAH), Ayatullah Udhma Khamenei amesisitiza kuwa: Ujumbe mkuu na wenye mvuto wa Mapinduzi ya Kiislamu ni kujizuia kufanya dhulma na kutokubali kudhululiwa na kwamba masuala yote ikiwemo mienendo, matendo na miamala ya mabeberu inabidi itafsiriwe na ichambuliwe kwa kuzingatia mivutano iliyopo baina ya madola hayo ya kibeberu na ujumbe huo wa Mapinduzi ya Kiislamu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu vile vile ametoa mkono wa baraka kwa mnasaba wa kuwadia sikukuu ya kukumbuka kuzaliwa kutukufu Imam Ali bin Musa ar Ridha Alayhis Salaam na kuongeza kuwa: Nafasi na cheo cha kimaanawi cha maimamu waongofu Alayhimus Salaam ni kikubwa mno kisichoweza kutasawarika katika akili, lakini pia maisha na sira za watukufu hao ni somo la kivitendo na la kudumu milele kwa wanadamu.
Aidha ameiashiria umri wa miaka 55 alioishi Imam wa Nane, Imam Ridha AS na miaka karibu 20 ya uimamu wake mtukufu na kuongeza kuwa: Imam Ali bin Musa ar Ridha Alayhis Salaam katika muda huo ambao takriban ni mfupi tena alioishi ndani ya kipindi kigumu cha mbinyo wa mfalme Harun ar Rashid, aliweza kutumia fursa hiyo kuweka misingi ya muda mrefu kwa namna ambayo aliweza kutangaza kwa kina uhakika wa Uislamu, fikra ya "Wilayat" na mafundisho ya chuo cha Ahlul Bayt wa Mtume Muhammad SAW na kuzifanya taasisi za kidhalimu za dikteta wa wakati huo zishindwe kukabiliana na jambo hilo na kuamua kubadilisha mbinu zao walizokuwa wamezipanga huko nyuma na hatimaye kuamua kumuua shahidi Imam huyo mtukufu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu pia amesema kuwa, ukiangalia namna Imam Ridha alivyouawa shahidi na namna alivyozikwa mtukufu huyo huko Mash-had kwa kweli utaona kwamba ulikuwa ni uhandisi na tadibiri ya Mwenyezi Mungu Mwenyewe. Ameongeza kuwa: Inabidi mambo na mipango yetu yote ya muda mrefu tuipange kwa kuzingatia malengo na mtazamo wa Imam huyo mtukufu.
Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesifu rekodi nzuri na inayong'ara ya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH na kusema kuwa: SEPAH imeingia kwenye medani ya jihadi na muqawama kwa imani thabiti na kwa itikadi yenye kina kirefu na mbali na kuleta makamanda wenye akili kubwa sana na madhubuti mno sambamba na kuwa na istrajitia bora za kijeshi, katika masuala yasiyo ya kijeshi pia, jeshi hilo limelea viongozi bora kabisa na wenye tadibiri na umakini wa hali ya juu na kuwatuma kwenye vyombo vya utawala.
Ayatullah Udhma Khamenei amezitaja sifa za kuishi kimapinduzi na kudumu kimapinduzi pamoja na kuwa imara kwamba ni katika sifa bora za Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH na kuongeza kuwa, jeshi hilo lililo imara sana hakuna wakati hata mmoja lilipowahi kutoka nje ya njia yake ya asili na sahihi licha ya kutokea mabadiliko mbali mbali duniani na udharura wa kuweko mabadiliko ndani ya jeshi hilo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria pia visingizio vinavyotumiwa na baadhi ya watu kwa ajili ya kuhalalalisha kusikitika na kujuta kwao na kuongeza kuwa: Kubadilika dunia kusiwe sababu ya kubadilisha malengo na shabaha zetu tukufu na wala kubadilisha njia sahihi tuliyoipita.
Ameongeza kuwa, bila ya shaka yoyote SEPAH ina welewa mpana, kamili na wa kutosha kuhusu mabadiliko na harakati zote zinazofanyika kwenye medani tofauti ulimwenguni.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria pia mijadala ya kisiasa iliyopo hivi sasa nchini Iran na kusema kuwa: Hakuna udharura kwa SEPAH kujiingiza katika masuala ya siasa, lakini kazi ya kuyalinda Mapinduzi ya Kiislamu inataka kuwa na welewa wa kina na utambuzi wa hali ya juu kuhusu mambo mbali mbali yanayotokea, hivyo si jambo lililo sawa kwa taasisi muhimu na majimui kama hii ambayo ni kiungo muhimu sana cha kulinda Mapinduzi ya Kiislamu kufumbia macho mirengo mbali mbali potofu na hata isiyo potofu pamoja na mirengo tegemezi na mirengo mingineyo ya kisiasa.
Ayatullah Udhma Khamenei ameendelea kubainisha maana ya kina ya neno Ulinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa kujadili changamoto kuu na ya kimsingi yaliyo nayo Mapinduzi ya Kiislamu.
Amesisitiza kuwa, si sahihi kudharau na kufifiliza umuhimu wa kukabiliana na changamoto hiyo na wala kudharau changamoto hiyo kuu kwa sababu ya changamoto za kimirengo, mijadala ya kimakundi na kutokubaliana kimitazamo baina ya mtu na mtu. Ameongeza kuwa: Changamoto kuu iliyopo hivi sasa ni mapambano baina ya mfumo wa kibeberu na ujumbe wenye kutia hamasa wa Mapinduzi ya Kiislamu, yaani kujiepusha na kudhulumu na pia kutokubali kudhulumiwa.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria pia mfumo mpya ambao Mapinduzi ya Kiislamu yamemzawadia mwanadamu na kusema kuwa, mfumo wa kibeberu umeigawanya dunia katika pande mbili, moja ya madola yenye kudhulumu na nyingine ya mataifa yenye kudhulumiwa (yaani madola makubwa na madola machanga au madola ya kibeberu na madola ya mataifa yanayofanyiwa ubeberu). Hata hivyo amesema: Mapinduzi ya Kiislamu yamekuja na mantiki ya kupambana na dhulma ya aina yoyote ile pamoja na kujiepusha kudhulumu na mantiki hiyo imepelekea ujumbe wa Mapinduzi ya Kiislamu usibakie tu kwenye mipaka ya ardhi ya Iran bali yatoke nje ya mipaka hiyo na kupokewa vizuri mno na mataifa mengine duniani.
Amesema, madola ya kijabari na kibeberu, tawala tegemezi na za vibaraka wa mabeberu na kanali za waporaji za kimataifa ni miongoni mwa wapinzani wa ujumbe wa Mapinduzi ya taifa la Iran na kuongeza kuwa: Mfumo wa kibeberu na vibaraka wake wanatumia siasa tatu kuu, mosi ni kueneza vita duniani, pili kueneza umaskini ulimwenguni na tatu kueneza ufisadi, lakini dini tukufu ya Kiislamu inapinga siasa zote hizo na kupinga kwake huko ndiko kunakowafanya wapinzani wa Mapinduzi ya Kiislamu ya nchini Iran wasimame kidete kuyapinga mapinduzi hayo.
Ayatullah Udhma Khamenei amesisitiza kuwa, harakati na njama zote za maadui ambazo wamekuwa wakizozifanya dhidi ya Iran katika kipindi cha miaka 34 sasa, zinafanyika katika kalibu ya changamoto hiyo hiyo kuu na kuongeza kuwa: Hata kadhia ya nyuklia nayo inabidi itathminiwe katika mtazamo huo huo.
Ameongeza kuwa: Sisi tunaposema kuwa hatutaki silaha za nyuklia si kwa sababu ya kumuogopa Mmarekani na wala mtu mwingine yeyote asiye Mmarekani, bali ni kutokana na itikadi zetu za kidini ndio maana hatukubaliani na silaha za nyuklia na wakati tunaposema kuwa mtu yeyote yule duniani hapaswi kuwa na silaha za nyuklia huwa tuna maana ya kwanba hata na sisi nasi tunajiepusha na kumiliki silaha hizo, lakini wapinzani wa Iran wanasema mambo mengine kabisa kuhusu suala hilo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa, nchi hizo chache ambazo kimsingi hazitaki kuona zinapokonywa kuhodhi kwao teknolojia ya nyuklia, zinapiga makelele mengi wakati zinapoona nchi kama Iran inakuwa na teknolojia ya kisasa ya nyuklia lakini ukweli wa mambo ni kuwa wanapiga makelele hayo si kwa sababu ya kadhia ya nyuklia, bali ni kutokana na upinzani na uadui wao mkubwa walio nao kwa mfumo wa Kiislamu wa Iran ambao umekuja na fikra ya kutodhulumu na kutokubali kudhulumiwa.
Ayatullah Udhma Khamenei amebainisha ukubwa na kina kirefu cha uadui wa waistikbari kwa Mapinduzi ya Kiislamu na kusisitiza kwamba: Imam Khomeini (quddisa sirruh) alikuwa na utukufu mkubwa kama mwanaadamu kiasi kwamba hata maadui zake walikuwa wanamheshimu, lakini kutokana na uadui mkubwa walio nao maadu kwa Mapinduzi ya Kiislamu, hakuna mtu anayechukiza zaidi mbele ya maadui hao kama Imam Khomeini (quddisa sirruh), na sababu yake ni kuwa, Imam alisimama imara na bila ya kutetereka mbele ya maadui akiwa na busuri na mtazamo wa mbali na kudiriki vizuri malengo ya kiuadui ya maadui hao na alisimama imara mbele yao mithili ya kigingi madhubuti kisichovuukika.
Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa: Hivi sasa pia hali ni hiyo hiyo, na mtu yeyote anapokuwa ameshikamana na ujumbe wa asili na mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu na kuzitathmini njama na mienendo ya maadui katika kalibu ya mivutano iliyopo baina ya mfumo wa kibeberu na Mapinduzi ya Kiislamu, huchukiza zaidi na kukasirikiwa zaidi na mabeberu kuliko watu wengine.
Vile vile ameashiria jinsi ulimwengu wa kidiplomasia ulivyo tata na kuongeza kuwa: Uwanja wa kidiplomasia ni uwanja wa kuoneshana tabasamu na kuonesha kuwa watu wanataka mazungumzo lakini mienendo yote hiyo inabidi itathiniwe kwa kuzingatia changamoto kuu na ya asili iliyopo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameelezea kukubaliana kwake na harakati sahihi na za kimantiki katika siasa za nje na ndani ya Iran na kuongeza kwamba: Mimi ninakubaliana na suala ambalo miaka mingi nyuma nililiita kwa jina la "ulaini wa kishujaa" kwani harakati hiyo katika baadhi ya sehemu ni nzuri sana bali kuna wakati huwa ni lazima kuwa na harakati za namna hiyo lakini bila ya kusahau kushikamana na sharti moja kuu.
Amekutaja kuutambua vyema upande wa pili na kuwa na welewa sahihi kuhusiana na malengo ya upande huo kuwa ndilo sharti kuu la kutumia mbinu ya ulaini wa kishujaa na kuongeza kuwa: Mpiganaji mieleka bingwa naye baadhi ya wakati huonesha ulaini ikiwa ni katika mbinu yake ya kupambana lakini kamwe hamsahau mpinzani wake na anaendelea kutilia maanani vilivyo malengo ya mpinzani wake. Katika sehemu nyingine ya miongozo yake, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameunga mkono matamshi ya Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH kuhusiana na majukumu ya jeshi hilo na kuwahutubu maafisa wa jeshi hilo akisema kuwa: Simameni imara, msitetereke na endeleeni na utekelezaji wa majukumu hayo kwa kutegemea welewa sahihi wa suala ambalo mumechukua jukumu la kuilinda.
Vile vile amewasisitizia sana maafisa wa SEPAH suala la kujiimarisha kimaanawi na kuongeza kuwa: Tab'an kujiimarisha kimaanawi hakupingani kivyovyote vile na suala la kushughulikia msingi wa kimaada wa kufanya kazi na kuwa na mpangilio mzuri katika jambo hilo.
Sehemu ya mwisho ya hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu imesisitiza kwenye mustakbali unaong'ara wa Mapinduzi ya Kiislamu.
Katika kubainisha suala hili kwamba mustakbali unaong'ara wa Mapinduzi ya Kiislamu ni jambo la uhakika na wala si suala la kujifurahisha moyo bila ya ushahidi wowote, ushahidi wa kwanza wa suala hilo ni uzoefu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria tofauti ya kustaajabisha iliyopo hivi sasa nchini Iran katika upande wa maendeleo ya kielimu, kijeshi, kiuongozi na kiuchumi na katika nyuga nyinginezo ikilinganishwa na hali ilivyokuwa nchini Iran mwanzoni mwa ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu na kuongeza kwamba: Maendeleo yote haya yamepitakana nchini Iran licha ya kuwa taifa hili limo kwenye mashinikizo na njama nyingi za maadui na kwamba uzoefu huu wenye thamani kubwa, unathibitisha kwamba hakuna kitu chochote kinachoweza kulizuia taifa hili la waumini, lililo makini, lililo madhubuti na lisilotetereka lisindelee na njia yake ya kujiletea maendeleo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Hasara uliobebeshwa Uislamu katika matukio ya hivi karibuni ya eneo la Mashariki ya Kati linatokana na ukweli kwamba baadhi ya watu hawakuzijua njia sahihi na hadi hivi sasa baadhi yao hawajazijua, lakini ni jambo lililo bayana kwamba hali haitabakia kuwa hivi milele na mwamko wa Kiislamu uliojitokeza kwa nguvu za aina yake katika ulimwengu wa Kiislamu, utarekebisha mambo.
Ushahidi wa pili uliotolewa na Kiongozi Muadhamu kuthibitisha kuwa mustakbali wa Mapinduzi ya Kiislamu ni mustakbali unaong'ara ni namna taifa hili linavyofanya mambo yake kielimu na mahesabu ya kimantiki.
Amesema, taifa la Iran linasonga mbele kwa mantiki na mahesabu ya kielimu na wakati huo huo adui anazidi kudhoofika na kurudi nyuma kutokana na kujijengea lenyewe mambo yanayogongana na kukinzana na ijapokuwa adui huyo halisemi waziwazi jambo hilo, lakini hivi sasa anazidi kurudi nyuma na bila ya shaka yoyote ushindi katika mapambano ya maadui na Mapinduzi ya Kiislamu, ni wa upande ambao unafanya mambo yake kimantiki na mahesabu mazuri ya kielimu.
Amma nukta za mwisho zilizotiliwa mkazo na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika mkutano huo ni kuutia nguvu na kuufanya imara muundo wa ndani wa Jamhuri ya Kiislamu, kuendelea na jitihada za kujiletea maendedleo ya kielimu, kunyanyua uzalishaji wa bidhaa za ndani na kutegemea sana vipaji vya ndani ya nchi.
Amesisitiza kwamba, mustakbali unaong'ara wa Mapinduzi ya Kiislamu ni jambo lisiloepukika lakini kutimia jambo hilo kwa haraka au kwa kuchelewa kunategemea namna wananchi na viongozi nchini Iran watakavyofanya kazi zao. Amesema iwapo tutakuwa wamoja, na iwapo tutakuwa imara na tutakuwa ni watu wenye misimamo isiyotetereka, mustakbali huo unang'aa utashuhudiwa mapema na iwapo tutafanya uvivu, tutakuwa na ubinafsi na kama tutakuwa na matatizo mengine, basi mustakbali huo utachelewa kutufikia.
Mwanzoni mwa mkutano huo Hujjatul Islam Walmuslimin Saidi, Mwakilishi wa Fakihi Mtawala (Waliyyul Faqih) katika Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH ametoa ripoti kuhusu kazi muhimu zaidi za chuo cha kidini zinazofanywa na ofisi ya Fakihi Mtawala katika SEPAH.
Kwa upande wake, Meja Jenerali Jaafari, Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH, ametoa ripoti kuhusu matunda na mafanikio makubwa yaliyopatikana kwenye jeshi la SEPAH katika upande wa masuala ya kijeshi na kiutamaduni na kusisitiza kuwa: Leo hii jeshi la SEPAH linatumia vizuri uzoefu wa Mapinduzi ya Kiislamu na lina uwezo wa kuingia kwa nguvu kubwa katika changamoto zote zinazoyakabili Mapinduzi ya Kiislamu na kusonga mbele katika njia ya ufanikishaji wa malengo matukufu ya Mapinduzi ya Kiislamu kwa heshima na fakhari kubwa.
Meja Jenerali Jaafari vile vile ameashiria kiapo lilichokula jeshi la SEPAH cha kuyalinda kwa kila hali malengo matukufu ya Jamhuri ya Kiislamu, njia ya Imam Khomeini (quddisa sirruh) na ya mashahidi wa Mapinduzi ya Kiislamu na kuongeza kuwa: Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH lina nguvu za kila upande za kuepusha mashambulizi na kwamba limeelekeza nguvu zake za mashambulizi katika masuala ya kujiimarisha kulinganana na hali ilivyo katika kila zama na kujiweka tayari wakati wote kwa ajili ya kutekeleza majukumu yake ya kuyalinda Mapinduzi ya Kiislamu.
 
< Nyuma   Mbele >

^