Skip to content

Habari

Habari
Hifadhi

Risala na Barua

Matini
Hifadhi

Kumbukumbu na Simulizi

Kabla ya Mapinduzi
Baada ya Mapinduzi

Sauti na Taswira

Picha
Sauti
Video
Amirijeshi Mkuu wa Vikosi Vya Ulinzi vya Iran Ahudhuria Sherehe za Kuhitimu Maafisa wa Kijeshi Chapa
05/10/2013
Sherehe za Saba za pamoja za kuhitimu masomo, kula kiapo na kupewa vyeo wanachuo wa Vyuo Vikuu vya maafisa wa kijeshi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran vimefanyika asubuhi ya leo (Jumamosi) na kuhudhuriwa na Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ambaye pia ndiye amirijeshi mkuu wa vikosi vyote vya ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Sherehe hizo zimefanyika kwenye Chuo Kikuu cha mafunzo ya Jeshi la Anga cha Shahid Sattari.
Mwanzoni kabisa kwa kuingia kwenye eneo palipofanyika sherehe hizo, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amekwenda kwenye eneo la kumbukumbu za mashahidi wa jeshi na kuwasomea Faatiha pamoja na kuwaombea dua za kheri akimuomba Mwenyezi Mungu awapandishe daraja za juu za utukufu mashahidi hao.
Baada ya hapo Amirijeshi Mkuu wa vikosi vya Ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amekwenda kukagua paredi la vikosi vilivyokuwepo kwenye eneo hilo.
Ayatullah Udhma Khamenei amesema katika hotuba aliyoitoa kwenye sherehe hizo kwamba kuingia vijana wapya kwenye vikosi shujaa vya ulinzi na vyenye fakhari kubwa vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni ufakhari mkubwa kwa vijana hao na huku akiashiria wajibu wa kutiwa nguvu utayari na uimara wa kiulinzi vya vikosi hivyo vya ulinzi sambamba na kuimarishwa nguvu za ndani za mfumo wa Kiislamu na kutiwa nguvu mshikamano wa taifa amesema kuwa: Sisi tunaunga mkono harakati na hatua za kidiplomasia za serikali ikiwa ni pamoja na safari ya (Rais Rouhani) mjini New York (Marekani) kwani tuna imani na serikali yetu inayolitumikia taifa. Tuna mtazamo mzuri kuhusiana na serikali yetu, lakini baadhi ya mambo yaliyotokea kwenye safari ya New York hayakuwa ya mahala pake na sababu yake kubwa ni kuwa sisi hatuiamini hata chembe serikali ya Marekani hasa kwa vile Marekani inajiona bora kuliko watu wote, inafanya mambo kinyume na mantiki na haiheshimu ahadi zake.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Sisi tunawaamini viongozi wetu na tunawataka wafanya mambo yao kwa umakini wa hali ya juu na wachukue hatua kwa kuzingatia nukta zote za kadhia husika na kamwe wasisahau manufaa ya taifa.
Ayatullah Udhma Khamenei amesisitizia pia wajibu wa kuimarishwa nguvu za ndani ya mfumo wa Kiislamu na kuongeza kuwa: Watu wa asili yaani watu ambao tangu mwanzoni kabisa mwa Mapinduzi ya Kiislamu walikuwa mstari wa mbele katika kuyalinda mapinduzi haya ya Kiislamu na taifa la Iran na ambao ni kiini na chimbuko la maendeleo ya Iran, wakati wote walikuwa wakiyapa umuhimu mkubwa malengo makuu na matukufu ya Jamhuri ya Kiislamu na kuzingatia heshima ya taifa, hivyo viongozi wote na matabaka yote ya wananchi, nao pia wana jukumu la kulinda vilivyo heshima na utambulisho wa taifa.
Vile vile ameashiria namna Jamhuri ya Kiislamu isivyo na imani na isivyoisadiki hata kidogo Marekani na kusema kuwa serikali ya Marekani imedhibitiwa ndani ya makucha ya Wazayuni. Aidha amesema: Kwa kweli serikali ya Marekani inafanya mambo yake kwa ajili ya kulinda manufaa ya Wazayuni. Amesema, Marekani inazilazimisha nchi zote duniani kuipa nchini hiyo fidia na rushwa, lakini inapofika mbele ya utawala wa Kizayuni wa Israel, Marekani ndiyo inayotoa fidia kuupa utawala huo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aidha amesema kwa mara nyingine kuwa, taifa la Iran kamwe halijawahi kuwa tishio kwa nchi yoyote ile, lakini liko imara mbele ya maadui na kwamba uimara wa vikosi vyake vya ulinzi ndiyo sababu kuu ya kuweza kulindwa usalama wa Jamhuri ya Kiislamu.
Ameongeza kuwa: Taifa la Iran linavihesabu vikosi vyake vya ulinzi, likiwemo Jeshi, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH, Basiji na jeshi la Polisi, kuwa ni ngao kubwa na madhubuti sana ya kukabiliana na maadui.
Amirijeshi Mkuu wa vikosi vya ulinzi vya Iran aidha ameashiria vitisho vinavyochefua moyo vinavyotolewa mara kwa mara na maadui wa taifa la Iran dhidi ya Iran ya Kiislamu na kusisitiza kuwa: Watu wote waliozoea kutoa vitisho dhidi ya Iran watambue kuwa majibu yatu kwa ushari wa aina yoyote ile dhidi ya taifa la Iran yatakuwa majibu makali mno.
Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa: Taifa la Iran pia limeonesha msimamo wake madhubuti katika njia ya kulinda malengo yake matukufu na manufaa yake kama ambavyo pia limeonesha pia hamu na shauku yake kubwa ya kuishi na mataifa mengine kwa amani na utulivu kwani mambo hayo siku zote lazima yawepo pamoja.
Mwishoni mwa miongozo yake, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amelishukuru jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hasa Jeshi la Anga kwa ushujaa na kujitolea kwake muhanga katika kulilinda taifa la Iran kwenye miaka yote minane ya vita vya kujihami kutakatifu (vilivyoanzishwa na utawala wa zamani wa Saddam Hussein wa Iraq dhidi ya Iran) kama ambavyo pia amewakumbuka kwa wema mashahidi watukufu wa vita hivyo vya kujihami kutakatifu wakiwemo mashahidi Babai na Sattari.
Baada ya hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Brigedia Jenerali Shah Safi, Kamanda wa Jeshi la Anga la Jamhuri ya Kiislamu amesisitiza kuwa, katika Vyuo Vikuu vya maafisa wa kijeshi vya Jamhuri ya Kiislamu, sambamba na kutolewa mafunzo ya elimu mpya na za kisasa, mafundisho ya kidini na kiitikadi nayo ni katika ratiba kuu na za asili za vyuo vikuu hivyo. Vile vile ameashiria mikakati ya ndani ya Iran ya kubuni na kujitengenezea wenyewe zana za kisasa katika Jeshi la Anga la Iran kulingana na mazingira yake na hali yake ya ndani na kusisitiza kuwa, Jeshi la Anga la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran limeimarisha sana uwezo wake wa kiulinzi na kuepusha kutokea mashambulizi dhidi ya Iran na liko tayari wake wote kwa ajili ya kulinda mipaka ya anga ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Naye Brigedia Jenerali Bakhshande, Kamanda wa Chuo Kikuu cha Masuala ya Anga cha Shahid Sattari ametoa ripoti kuhusu ratiba za mafunzo na utafiti katika Chuo Kikuu cha Jeshi la Anga cha Shahid Sattari hususan mipango ya kuzidi kuimarisha utengenezaji na utumiaji wa ndege za kijeshi zisizo na rubani na ndege nyinginezo za kisasa.
Katika sherehe hizo, makamanda, wahadhiri wa Vyuo Vikuu, marubani na wanafunzi wa Vyuo Vikuu vya maafisa wa kijeshi pamoja na watu kadhaa wa famiia za mashahidi, wamepewa zawadi za Qur'ani Tukufu na zawadi nyinginezo. Vile vile wawakilishi wa wanachuo wapya na waliohitimu masomo yao, wamepandishwa cheo na Amirijeshi Mkuu wa vikosi vya ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei.
Katika sherehe hizo pia, wanafunzi wa Vyuo Vikuu vya maafisa wa kijeshi nchini Iran waliendesha ratiba mbali mbali za kijeshi katika sherehe hizo.
Mwisho mwa sherehe hizo, vikosi vilivyokuwepo kwenye eneo hilo vilipita kwa gwaride mbele ya jukwaa kubwa alipokuwepo Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu sambamba na kufanya mazoezi ya aina mbali mbali ya kuonyesha uwezo wao wa kijeshi.
 
< Nyuma   Mbele >

^