Skip to content

Habari

Habari
Hifadhi

Risala na Barua

Matini
Hifadhi

Kumbukumbu na Simulizi

Kabla ya Mapinduzi
Baada ya Mapinduzi

Sauti na Taswira

Picha
Sauti
Video
Kiongozi Muadhamu Aonana na Washiriki wa Kongamano la Saba la Taifa la Vijana wenye Vipaji Chapa
09/10/2013
Zaidi ya vijana elfu moja wenye vipaji bora kutoka Vyuo Vikuu mbali mbali vya Iran leo asubuhi wameonana kwa karibu na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei kwa muda wa masaa mawili, na kuelekezea mitazamo, fikra, mawazo na hata kutoa dukuduku zao. Vijana hao pia wamepata fursa ya kusikia mambo ya dharura, uwezo wa Iran katika suala zima la kuzidi kupiga hatua za haraka za kimaendeleo na kujizalishia yenyewe elimu likiwa ndilo jambo muhimu na la kimsingi la kuweza Iran kufikia vilele vya juu vya maendeleo, nguvu na ustawi.
Ayatullah Udhma Khamenei vile vile amekutaja kuonana kwake na vijana azizi wenye vipaji vya kila aina kuwa ni fursa nzuri sana kwake kama ilivyo siku zote na kwamba jambo hilo linatoa ilhamu nzuri na linaandaa uwanja wa kuchukuliwa hatua za kivitendo katika siasa na mipango ya nchi. Vile vile amesisitiza kuwa, vijana wenye vipawa nchini Iran ndio wabunifu na wahandisi wa maendeleo yajayo nchini.
Aidha amesisitiza kuwa, siasa za maendeleo ya kasi ya kisayansi ni siasa za kimsingi za mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu na kuongeza kuwa, wasomi na wanafikra wa Iran na wa Jamhuri ya Kiislamu wamebaini kwamba, kama suala la kuvuuka kwenye matatizo, kwenye hatari na kwenye misukosuko kunahitajia kuwa na nguzo kadhaa, basi moja ya nguzo hizo bila ya shaka yoyote ni maendeleo ya kielimu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu vile vile ameashiria namna Iran ilivyo na vipaji vingi na uwezo mkubwa wa kufanya mambo makubwa makubwa na kuongeza kuwa: Vijana wenye vipawa wanao uwezo wa kuifikisha nchi na taifa kwenye vilele vya maendeleo ya kila upande.
Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa: Vipaji vya watu wenye vipawa nchini Iran ni vya hali ya juu kiasi kwamba vinaweza kufikia shabaha yoyote ile ya kisayansi na kiteknolojia ambayo miundombinu yake imo nchini.
Amesema: Jambo lililolifanya suala la maendeleo ya kielimu kuwa ajenda kuu nchini Iran ni kwamba, maendeleo ya kweli hayawezi kufikiwa bila ya kuwa na maendeleo ya kisayansi na kiteknolojia.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Tab'an maendeleo hayo ya kisayansi nayo inabidi yawe na msingi wa ndani ya nchi, yazalishwe kwa kutumia vipaji vya ndani ya nchi, kwani harakati yoyote ile, au mapinduzi na ustawi wa kielimu unapotokana ndani ya nchi huandaa mazingira ya kupatikana heshima, itibari, hadhi na kutukuka nchi na taifa.
Ayatullah Udhma Khamenei amesisitiza pia kuwa, wakati chimbuko la maendeleo ya kielimu linapokuwa ni la ndani ya nchi, huiandalia uwezo nchi hiyo kuangaliwa kwa heshima na kwa usawa kisayansi na kiteknolojia na nchi nyinginezo na amesisitiza kuwa: Vijana wenye vipawa na viongozi wote nchini pamoja na wananchi wote wa Iran wanapaswa kujua kuwa, kambi iliyoelekeza mashambulizi yake kwa mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu inazingatia mno suala la kuizuia Iran isipate maendeleo ya kisayansi na kiteknolojia.
Vile vile amesisitiza kuwa: Unapoyachambua masuala na matukio yote ya kisiasa, kiuchumi, kieneo na kimataifa unapaswa kuwa na mtazamo huu mkubwa na mpana kwamba, kuna kambi yenye nguvu duniani ambayo haipendi kuiona Iran ya Kiislamu inakuwa ni nchi na taifa lenye nguvu katika nyuga tofauti hususan katika uga wa maendeleo ya kisayansi na kiteknolojia.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria pia makala zilizoandikwa na baadhi ya wasomi na wanafikra wakubwa wa Marekani na Magharibi mwanzoni mwa ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu na kuongeza kuwa, ndani ya makala hizo, taasisi za kisiasa za Magharibi zinaonywa kwamba Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran hayana maana ya kubadilika timu fulani tu ya watawala, bali ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu una maana ya kujitokeza nguvu mpya katika eneo la magharibi mwa Asia ambayo yanaweza kulitoa eneo hilo nyeti na tajiri mikononi mwa udhibiti wa Magharibi au kuteteresha udhibiti wa Magharibi wa eneo hilo na ni nguvu ambayo inaweza kuuteteresha ulimwengu wa Magharibi katika upande wa maendeleo ya sayansi na teknolojia.
Amesisitiza kuwa, hivi sasa na baada ya kupita zaidi ya miongo mitatu, Wamagharibi na Wamarekani wamekumbana na jinamizi walilokuwa wakiliogopa, kujitokeza nguvu kubwa ya kitaifa na kieneo ambayo imeweza kusimama imara na bila ya kutetereka mbele ya mashinikizo ya kila nui ya kisiasa, kiuchumi, kiusalama na kipropaganda. Si hayo tu, lakini nguvu hiyo kubwa pia imeandaa uwanja wa kutoa athari nzuri kwa watu wa mataifa mengine ya eneo hili na kuwarejeshea Waislamu utambulisho wao.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria pia matukio muhimu mno yaliyotokea katika eneo la Mashariki ya Kati na kaskazini mwa Afrika katika kipindi cha miaka miwili iliyopita na radiamali iliyooneshwa na Marekani na nchi za Magharibi kuhusu matukio hayo na kusisitiza kuwa: Kuamka wananchi wa mataifa hayo na kusimama imara licha ya kutokuwa na kitu mkononi na wakapambana na udhalilishaji wanaofanyiwa na Magharibi na Marekani ni tukio kubwa sana ambalo licha ya kwamba Wamagharibi wanadhani kuwa limezima, lakini bado halijazima na wala halijaisha.
Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa: Matukio hayo yalikuwa ni sehemu ya matukio ya kihistoria ambayo eneo hili limepitia ndani yake, na bado hayajamalizika, na ni wazi kuwa Wamagharibi wana hofu na wasi wasi na matukio hayo.
Ameongeza kuwa: Matukio hayo muhimu yametokea kwa baraka za Mapinduzi ya Kiislamu ambayo tangu kupata kwake ushindi nchini Iran yalitoa bishara njema za kujitokeza nguvu ya kitaifa, nguvu kubwa, nguvu ya watu wenye imani thabiti, nguvu isiyotetereka na nguvu ya watu vipaji vya kila namna na ambavyo siku zote inazidi kunawiri na kuimarika.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu pia amesema kuwa, miongoni mwa sababu zilizoifanya nguvu huyo ya kitaifa kubakia imara ni kulindwa na kuhifadhiwa kasi ya maeneo ya kielimu nchini Iran na kwamba hilo ni jambo la dharura kabisa na la kimsingi sana. Ameongeza kuwa, ili ujumbe wa kihistoria wa Mapinduzi ya Kiislamu uweze kufanikishwa, inabidi kuwe na harakati yenye kasi ya kielimu nchini Iran na kusiwe na kusitasita, wala kukwama wala kutaradadi na wala kufanya uvivu wa aina yoyote hilo katika jambo hilo.
Ameitaja jamii iliyo imara na yenye uchangamfu mkubwa ya watu wenye vipaji, Wizara ya Sayansi, Utafiti na Teknolojia, Wizara ya Afya, Matibabu na Elimu ya Tiba na Kitengo cha Sayansi cha Ofisi ya Rais kuwa ni nguzo nne muhimu na endelevu katika harakati ya kielimu yenye kasi kubwa nchini Iran na kuongeza kuwa, kitengo na taasisi hiyo ya watu wenye vipaji ina majukumu nyeti na makubwa sana katika suala zima la maendeleo ya kisayansi ya Iran.
Ayatullah Udhma Khamenei ameashiria pia kazi zilizofanywa na Bw. Waizadeh na Bi Sultankhoh, wakuu waliopita wa kitengo hicho na pia kuteuliwa Bw. Sattari kuongoza kitengo hicho cha sayansi na kuongeza kuwa: Viongozi wapya wa kitengo hicho wasianze sifuri katika kazi zao bali wategemee kazi zilizofanywa na viongozi waliowatangaulia na watie nguvu nukta na mambo mazuri yaliyofanywa na wenzao waliowatangulia na kuondoa mapungufu na kujaza mapengo yaliyopo na nakisi zinazojitokeza.
Ayatullah Udhma Khamenei ameitaka taasisi ya watu wenye vipaji iendelee na kazi zake kwa bidii kubwa na kutayarisha mazingira ya kuzidi kujitokeza hamasa katika masuala ya kielimu na kuongeza kwamba: Iwapo lengo hilo litafikiwa, basi wataalamu na watu wenye vipawa wa ndani ya nje ya nchi watapata hamu kubwa zaidi ya kuwepo nchini Iran na kutoa michango yao katika jitihada za kuliletea taifa maendeleo ya kielimu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu vile vile amesema kuwa, ubunifu katika masuala ya elimu ni jambo muhimu na lenye athari kubwa na nzuri katika kuzidisha kasi ya ustawi na maendeleo nchini na kuongeza kuwa: Viongozi wa wizara za sayansi na afya na tiba na kitengo cha sayansi cha Ofisi ya Rais wote wanapaswa kuelekeza hima na jitihada zao katika kupanua wigo wa ubunifu wa kielimu nchini Iran.
Aidha amelitaja suala la kufuatilia kwa karibu na kwa kila siku harakati ya kielimu nchini kwa nia ya kuwa na welewa wa kina juu ya mikwamo na matatizo yaliyopo na yanayojitokeza na kufanya juhudi za kuondoa mikwamo na matatizo hayo kuwa ni jambo ambalo litaandaa uwanja wa kuongezeka kasi katika harakati ya ubunifu wa kielimu na kuongeza kuwa: Taasisi zote husikz katika daraja tofauti za kiasasi, kielimu na kiutendaji, zinapaswa zifanye kazi kwa pamoja na ziwe na uratibu mzuri katika utekelezaji wa majukumu yao.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu vile vile amezitaka taasisi husika ziandae mashindano ya kweli, makubwa na ya kina kuhusiana na ubunifu wa kisayansi na kiteknolojia na kuongeza kuwa: Inabidi katika tasnifu za shahada za uzamivu za Vyuo Vikuu suala la ubunifu nalo lipewe umuhimu mkubwa na liwe ni kipimo cha kutathmini watahiniwa na kuwapa alama zao kwa kuzingatia ubunifu wao.
Kutokinaishwa na kutotosheka na maendeleo ya kielimu yaliyopo nchini Iran ni nasaha nyingine zilizotolewa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika mkutano huo wa leo.
Ameongeza kuwa, ukuaji na kasi ya maendeleo ya kielimu ya Iran ni nzuri sana ikilinganishwa na kasi ya maendeleo hayo katika eneo la Mashariki ya Kati na duniani kiujumla, lakini pamoja na hayo hilo halina maana kuwa tumefika kwenye malengo tuliyokusudia au hata kuyakaribia malengo hayo kwani huko nyuma tulikuwa tumebakia nyuma sana katika maendeleo ya kisayansi na vile vile ni kwamba leo hii nchi nyingine kila siku zinazidi kupiga hatua mpya mbele za kielimu, hivyo tunatakiwa tusiridhike na maendeleo tuliyo nayo.
Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa: Tunapaswa tuongeze kasi ya kujiletea maendeleo ya kielimu ili tuweze kuwa kwenye mistari ya mbele ya kielimu duniani na ili kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu na kwa hima ya vijana na watu wetu wenye vipaji vya kila namna na walio amilifu katika kazi zao, tuweze kuwa marejeo ya kielimu duniani katika kipindi cha miongo minne au mitano ijayo.
Ameongeza kuwa: Tufikirie mustakbali unaong'ara na ambao bila ya shaka utapatikana yaani mustakbali wa Iran wa kuwa jabali la kielimu duniani na kila mtu atakayetaka kupata utaalamu na elimu mpya na za kisasa alazimike kujifunza lugha ya Kifarsi ili apate elimu hizo.
Katika sehemu mnyingine ya hotuba yake, Ayatullah Udhma Khamenei amekosoa namna ilivyoshindikana kufanikishwa kikamilifu suala la kuzioanisha kikamilifu elimu za sayansi na za ufundi na kuongeza kuwa: Licha ya jambo hilo muhimu kuhitajika sana, na licha ya kwamba Vyuo Vikuu na vituo vya elimu za kiufundi kuhitajia mno jambo hilo, lakini bado hakuna uhusiano na wala ushirikiano kamili na wa kimantiki baina ya vituo vya utafiti na vya sayansi kwa upande mmoja na viwanda na taasisi za uzalishaji bidhaa kwa upande wa pili.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa, ni jambo la dharura kuweko maelewano na mashirikiano zaidi baina ya mashirika, viwanda na vituo vya kielimu na Vyuo Vikuu na kuongeza kwamba: Kama kila mwaka tutashuhudia Vyuo Vikuu vyetu vinafanya mamia ya miradi ya utafiti ya ndani yanayohitajiwa na viwanda vyetu basi wakati huo tutasema kwamba sasa ukuwaji wa kweli wa kisayansi na kiteknolojia utafanikiwa.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amefafanua zaidi jambo hilo kwa kuashiria udhaifu mkubwa uliopo yaani udhaifu unaoonekana katika utekelezaji wa miradi inayohitajiwa na vituo vya nje katika baadhi vya Vyuo Vikuu na kuongeza kuwa: Sisi hatupingi kufanyika kazi za kielimu ambazo zitaweza kudhamini mahitaji ya watu wa nje lakini kipaji cha kweli kinaonekana pale panapofanyika kazi ya kielimu na kiutafiti inayoweza kutatua matatizo ya ndani na kudhamini mahitaji yetu ya ndani.
Mwishoni mwa hotuba yake, Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei amewausia watu wenye vipaji na vipawa mbali mbali nchini wajiidilishe katika taqwa na uchaji Mungu na kuzitia nguvu nafsi zao kimaanawi. Ameongeza kuwa: Usafi wa nyoyo na nuru katika nafsi za vijana wenye vipaji huandaa uwanja wa kupatikana rehema za Mwenyezi Mungu na kusahilika njia ya maendeleo na kustawi na kunawiri elimu.
Mwanzoni mwa mkutano huo, mabwana:
- Muhammad Hussein Noraniyan - kijana mwenye medali ya fedha katika mashindano ya Olympiad ambaye hivi sasa anasomea shahada ya uzamivu katika masuala ya umeme kwenye Chuo Kikuu cha Khojeh Naseer;
- Muhammad Hussein Dehqani Firoozabadi - mwanafunzi bora wa mitihani ya kuainisha wanafunzi wenye sifa za kuingia Chuo Kikuu mwaka 2002;
- Hamid Reza Lurk Agha - Aliyeteuliwa kushiriki katika mashindano ya Olympiad ya wanafunzi wa shule za msingi na ambaye hivi sasa ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu anayesomea uhandisi wa anga za juu;
- Hussein Pir Hussein Luw - mwanafunzi bora katika mtihani wa uchunguzi wa kuingia Chuo Kikuu mwaka 2009 ambaye hivi sasa ni mwanachuo wa fani ya uhanidisi wa umeme katika Chuo Kikuu cha Sharif;
- Ali Rajab Luw - anayesomea shahada ya uzamivu katika fani ya mekanika katika Chuo Kikuu cha Tehran;
- Hujjatul Islam Walmuslimin Jamalzade - aliyeshika nafasi ya kwanza katika mashindano ya Olympiad ya wanafunzi wa Vyuo Vikuu ambaye hivi sasa ni mwanachuo katika masomo ya sayansi na hadhithi katika Chuo Kikuu cha Elimu za Kiislamu cha Razavi;
- Muhammad Masoud Endalib - aliyeshika nafasi ya kwanza katika mitihani ya nchi nzima ya Iran mwaka 2013 na ambayo anasomea shahada ya uzamivu katika elimu ya tiba kwenye Chuo Kikuu cha Elimu ya Tiba cha Tehran;
Na mabibi:
- Madineh Karami - aliyeshika nafasi ya kwanza katika mashindano ya Olympiad ya wanafunzi wa Vyuo Vikuu ambaye hivi sasa anasomea shahada ya uzamili katika fani ya lugha na fasihi ya Kifarsi katika Chuo Kikuu cha Shiraz;
- Farahnaz Fahimi Pur - mwanachuo wa shahada ya uzamivu wa fani ya matibabu ya meno katika Chuo Kikuu cha Elimu ya Tiba cha Tehran; wamepata fursa ya kuzungumza na wametumia fursa hiyo kutoa mitazamo yao mbali mbali katika nyuga za kielimu na Vyuo Vikuu.
Miongoni mwa nukta muhimu zilizozungumziwa na vijana hao wenye vipaji mbali mbali ni pamoja na:
- Ulazima wa kuangaliwa upya muundo wa taasisi zinazohusiana na masuala ya utafiti;
- Kufanyiwa wepesi na kusahilishiwa mambo vituo vya utafiti;
- Umuhimu wa kuangaliwa katika uhakika wake na kwa mtazamo sahihi suala la utafiti na mashirika ya elimu msingi;
- Haja ya kuweko kituo na marejeo makuu ya data kwa ajili ya watu wenye vipaji na kwa ajili ya marudio yao ya utafiti;
- Kukosolewa upokeaji wa kupindukia wa wanachuo katika hatua mbali mbali za masomo ya ukamilishaji;
- Kuanzishwa vituo vya utafiti wa kiutamaduni na kisanaa vyenye itibari kwa ajili ya kufanya utafiti kwa kuzingatia mahitaji ya jamii;
- Udharura wa kuweko mabadiliko katika mitazamo ya hivi sasa ya Vyuo Vikuu kuhusu lugha na sarufi ya Kifarsi
- Kuondolewa vizuizi na matatizo ya kiidara na yasiyo ya kiidara kwa ajili ya kutoa mwanya wa kurejea nchini idadi kubwa zaidi ya wanafunzi wanaomaliza masomo yao nje ya nchi;
- Kukosolewa kutokuwepo uratibu wa pamoja kati ya watu wenye vipaji kutokana na udhaifu wa kukosekana ufanyaji kazi wa pamoja;
- Pendekezo la kuundwa mabaraza ya wataalamu chini ya usimamiaji wa Taasisi ya Taifa ya Watu wenye Vipaji kwa lengo la kuleta mawasiliano baina ya watu wenye vipawa;
- Umuhimu wa kuboreshwa anga ya utendaji na utafutaji kazi na kueneza utamaduni wa kuzalisha utajiri kwa kutumia elimu;
- Pendekezo la kuundwa kanali ya kukuza mawasiliano baina ya vijana wenye vipaji na ulimwengu wa Kiislamu;
- Kuelelezea wasiwasi kuhusu kupanda kwa miaka ya watu ya kufanya kazi;
- Haja ya kuanza kujifunza kazi wakati wanafunzi wanapokuwa kwenye elimu za sekondari kwa ajili ya kurekebisha na kusahihisha utamaduni wa kazi;
- Haja ya kupunguzwa idadi ya masomo yasiyo na faida na kuongezwa masomo yenye manufaa;
- Ulazima wa kutekelezwa kikamilifu sheria za mashirika ya elimu msingi;
- Kupewa kipaumbele harakati za kielimu kwa kuzingatia nafasi ya jamii ya kielimu nchini;
- Kulalamikia uongozi wa wahandisi katika taasisi za masomo ya Sayansi ya Jamii;
- Matokeo mabaya ya kuhama elimu kutoka elimu za msingi na za uhandisi na kuhamia kwenye elimu za Sayansi ya Jamii;
- Wasiwasi wa kujitokeza jambo lisilo zuri la kuingizwa siasa katika masuala ya elimu ya Sayansi ya Jamii;
- Kukosolewa suala la kuhodhiwa na baadhi ya watu na kutokuwa na faida baadhi ya taasisi za Serikali;
- Na ulazima wa kuweko uwazi katika mfumo wa afya na tiba na kudumu kazi za maafisa na watendaji wa sekta mbali mbali za Serikali.
 
< Nyuma   Mbele >

^