Skip to content

Habari

Habari
Hifadhi

Risala na Barua

Matini
Hifadhi

Kumbukumbu na Simulizi

Kabla ya Mapinduzi
Baada ya Mapinduzi

Sauti na Taswira

Picha
Sauti
Video
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Aonana na Wajumbe wa Baraza Kuu la Mapinduzi ya Kiutamadu Chapa
11/12/2013
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Aonana na Wajumbe wa Baraza Kuu la Mapinduzi ya KiutamaduAyatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu leo asubuhi (Jumanne) ameonana na wajumbe wa Baraza Kuu la Mapinduzi ya Kiutamaduni na sambamba na kubainisha umuhimu mkubwa mno wa suala la utamaduni na nafasi muhimu ya Baraza Kuu la Mapinduzi ya Kiutamaduni amebainisha masuala mbali mbali ikiwa ni pamoja na dhamana ya kutekeleza mambo yanayopasishwa na baraza hilo, majukumu ya kusimamia na kuongoza taasisi mbali mbali katika masuala ya utamaduni, udharura wa kuamiliana kwa hekima na masuala mbali mbali ya kiutamaduni, kuzidi kupiga hatua za kielimu katika Vyuo Vikuu, kutunga na kuandaa misingi ya mabadiliko ya kimapinduzi katika Sayansi ya Jamii na kulindwa uzuri na mvuto wa lugha ya Kifarsi.
Ayatullah Udhma Khamenei ameifanya nukta ya kwanza ya kuizungumzia kwenye hotuba yake hiyo muhimu kuwa ni suala la umuhimu na nafasi ya utamaduni katika jamii na huku akiashiria shakhsia na historia ya kazi za kiutamaduni za wakuu wa Mihimili Mitatu Mikuu ya dola (Bunge, Serikali na Mahakama) na vile vile historia ya masuala ya kiutamaduni ya wajumbe wengi wa Baraza Kuu la Mapinduzi ya Kiutamaduni wakiwa ni watu wenye uchungu na masuala ya kiutamaduni na kuongeza kuwa, ni kutokana na kuwa na wajumbe kama hao ndio maana kukawa kuna matarajio makubwa kwa baraza hilo kuongeza hima yake na kufanya juhudi kubwa zaidi kwa ajili ya kukuza na kutia nguvu masuala ya kiutamaduni katika jamii na kulifikisha suala hilo kwenye nafasi yake ya juu inayostahiki kuweko.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa, utamaduni na matukufu ya kiutamaduni ndio utambulisho wa roho ya taifa na kusisitiza kuwa, utamaduni si kitu cha pembeni au mkia wa masuala ya kiuchumi na kisiasa bali uchumi na siasa ndiyo mambo ya pembeni na mikia ya utamaduni.
Ayatullah Udhma Khamenei pia ameashiria mambo aliyokuwa akiyasisitizia huko nyuma kuhusu wajibu wa kuwepo mfungamano wa kiutamaduni katika masuala na kadhia zote muhimu kwenye nyuga tofauti na kuongeza kuwa, baadhi ya wakati inawezekana maamuzi na miswada inayopitishwa, ya kiuchumi, kisiasa, kijamii na hata ya kielimu, ikawa na matokeo mabaya ya kiutamaduni kwa jamii na sababu yake ni kukosekana mfungamano wa kiutamaduni katika maamuzi na miswada hiyo.
Vile vile amesisitiza kuwa, kuna udharura wa kuweka mipango makini ya kuendeshea harakati za kiutamaduni na haiwezekani kutarajia kuwa utamaduni wa nchi ujiratibu na ujiendeshe wenyewe bila ya kuwepo idili na jitihada za hali ya juu watu wa nchi hiyo ni sawa tu utamaduni huo uwe utamaduni wa umma, au utamaduni wa watu muhimu wenye vipaji na ushawishi katika jamii au utamaduni wa Vyuo Vikuu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu baada ya hapo ameingia kwenye nukta inayohusiana na wajibu wa kuweko usimamiaji na uendeshaji wa wa serikali katika masuala ya utamaduni na kuongeza kwamba, asasi mbali mbali nchini zina majukumu katika suala zima la utamaduni wa umma wa taifa.
Ayatullah Udhma Khamenei ameutaja uendeshaji na usimamiaji wa masuala ya utamaduni kuwa ni sawa na kutunza na kuchunga bustani iliyojaa maua mazuri ya kila namna na kuongeza kuwa, kupalilia na kuondoa magugu na majani ya ziada katika bustani hiyo huwa na maana ya kuruhusu maua yanawiri na yaweze kufaidika kimaumbile na maji na nuru.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, suala la utamaduni ni nyeti sana na ni wajibu wa serikali kupambana vilivyo na masuala yanayoharibu utamaduni wa taifa na kuongeza kuwa: Sisi sote tuna majukumu katika masuala ya kiutamaduni na ya utamaduni wa umma nchini, na jukumu letu hilo ni la kidini na ni la kisheria.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza pia kuwa, siku zote utamaduni unategemea kushirikishwa vilivyo wananchi na kuongeza kuwa: Kukabidhiwa wananchi masuala ya utamaduni hakufuti jukumu la serikali la kuendesha na kusimamia masuala ya utamaduni kama ambavyo pia kuwepo serikali na utawala katika masuala ya utamaduni hakuvui jukumu la wananchi katika masuala ya kiutamaduni.
Ayatullah Udhma Khamenei ameashiria pia baadhi ya matamshi yasiyo sahihi yanayotolewa na baadhi ya watu juu wa ulazima wa kuwepo uhuru usio na mipaka wa kiutamaduni kama ilivyo katika nchi za Magharibi na kuhoji kwa kusisitiza kwamba: Kwa nini Wamagharibi wao wawe wakaidi na washikilie mno masuala yao potofu na yasiyokubalika kiakili kama vile michanganyiko haramu ya wanawake na wanaume wakidai kuwa huo ni usawa baina ya watu au kung'ang'ania mtindo wao wa maisha wakidai kuwa hayo ndiyo maendelo, lakini sisi tushindwe kusimama kidete kulinda na kushikamana vilivyo na matukufu yetu aali na bora kabisa ya kiutamaduni?
Nafasi na umuhimu wa Baraza Kuu la Mapinduzi ya Kiutamaduni ni nukta ya pili iliyoashiriwa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika hotuba yake ya leo ambapo amesema: Baraza Kuu la Mapinduzi ya Kiutamaduni ni moja ya ubunifu uliojaa baraka wa Imam Khomeini (quddisa sirruh) na kwamba baraza hilo ndiyo asasi kubwa zaidi na bora zaidi ya kiutamaduni nchini Iran.
Ayatullah Udhma Khamenei amekutaja kuwemo viongozi wa ngazi za juu na vile vile sura zenye ushawishi wa kielimu na kiutamaduni ndani ya Baraza Kuu la Mapinduzi ya Kiutamaduni kuwa ni nukta muhimu sana inayolipambanua baraza hilo na asasi nyinginezo na kusisitiza kuwa: Sifa hiyo imelifanya suala la utamaduni nchini kutokuwa na kupanda na kushuka kunakoshuhudiwa katika masuala ya kisiasa na kwamba harakati ya kiutamaduni nchini sambamba na kuwa na utulivu wa siku zote na kutotetereka wala kupanda na kushuka, inapaswa daima ipige hatua za maendelo na itoke katika hali ya kuganda na kuwa na hali moja kila siku.
Ameongeza kuwa: Moja ya masuala muhimu ya Baraza Kuu la Mapinduzi ya Kiutamaduni ni kwa wajumbe wa baraza hilo kuelewa na kuwa na imani na ushawishi na nafasi muhimu sana ya baraza hilo ambalo ndicho kituo kikuu cha kutunga na kuweka sera za utamaduni nchini Iran.
Vile vile amesema ni jambo muhimu na la dharura mno kutoakhirishwa vikao vya baraza hilo na kuwepo wakati wote wajumbe wake akiongeza kuwa: Baraza Kuu la Mapinduzi ya Kiutamaduni linapaswa kushughulikia masuala ya kimsingi na muhimu kabisa na lijiepushe na kutekwa na masuala madogo madogo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameliteua suala la dhamana ya utekelezaji wa maamuzi ya Baraza Kuu la Mapinduzi ya Kiutamaduni kuwa nukta yake ya tatu ya kuizungumzia katika hotuba yake hiyo akisema kwa kugogoteza kwamba, ni lazima maamuzi yote ya baraza hilo yatekelezwe kivitendo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amekutaja kuwemo Mkuu wa Chombo cha Utekelezaji (Serikali), mkuu wa Chombo cha Kutunga Sheria (Bunge) na Mkuu wa Chombo cha Mahakama pamoja na mawaziri na viongozi wengine muhimu ndani ya baraza hilo kuwa kunatosha kuleta dhamana ya kutekelezwa maamuzi ya Baraza Kuu la Mapinduzi ya Kiutamaduni na kuongeza kuwa, kuna hati muhimu mno na nzuri kama vile ramani kuu ya kielimu ya nchi, hati ya mabadiliko ya kimsingi katika Wizara ya Elimu na Malezi, hati ya Chuo Kikuu cha Kiislamu na hati ya kiistratijia ya watu wenye vipaji ambazo zinapaswa zitekelezwe kivitendo na kwamba baraza lenyewe la mapinduzi ya kiutamaduni ndilo linalopaswa kusimamia namna ya utekelezaji wa hati hizo muhimu.
Uhakika unaojulikana kwa jina la mashambulizi ya kiutamaduni ni nukta ya nne ambayo Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameizingatia katika hotuba yake mbele ya wajumbe wa Baraza Kuu la Mapinduzi ya Kiutamaduni.
Ameashiria matamshi ya watu muhimu wa masuala ya kiutamaduni na kisiasa wa nchi mbali mbali duniani zikiwemo hata nchi za Ulaya kuhusu mashambulizi ya kiutamaduni yanayofanywa na Marekani dhidi ya tamaduni za mataifa mengine duniani na kuongeza kuwa: Leo hii inaonekana wazi wazi mifano isiyokanushika ya uhakika ambao kwa miaka mingi nimekuwa nikitahadharisha juu yake.
Baada ya hapo Ayatullah Udhma Khamenei ameashiria uhakika mwingine nao ni kuwa, kwa uchache kuna mamia ya vyombo vya habari vya sauti, picha, maandishi na Intaneti duniani ambavyo vyote lengo lao ni moja nalo ni kujaribu kuharibu akili na mienendo ya wananchi wa Iran.
Aidha amesema, baadhi ya michezo ya kompyuta na vidude vya kuchezea watoto vinavyotoka nje ni miongoni mwa mifano ya vitu ambavyo vinalenga kueneza tabia na mitindo ya maisha ya Kimagharibi katika akili za watoto wadogo, vijana wadogo na mabarobaro wa Iran.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aidha amelitaja suala la kufanya kazi kwa bidii kubwa na ubunifu wa hali ya juu kuwa ndio msingi wa kuweza kupambana kwa njia za hekima na suala la mashambulizi ya kiutamaduni na kusisitiza kuwa: Inabidi kufanyike juhudi za kiubunifu za kukabiliana na jambo hilo ambapo katika suala hilo, jukumu la Shirika la Sauti na Televisheni la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran (IRIB) na Wizara ya Utamaduni na Miongozo ya Kiislamu ni kubwa mno.
Ayatullah Udhma Khamenei ameipa nasaha Wizara ya Utamaduni na Miongozo ya Kiislamu akiisisitizia kwamba, utungaji na uzalishaji wa vitabu, kutarjumiwa vitabu vyenye faida, kuzalisha filamu zenye mfumo kwa kutegemea uwezo mkubwa ilio nao Iran katika uzalishaji filamu, kuzalisha michezo yenye faida ya kompyuta, kueneza michezo yenye harakati nyingi na kutengeneza vidude vya kuchezea vyenye maana na vya kuvutia ni mambo ambayo yanapaswa yapewe kipaumbele kikubwa na wizara hiyo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amelitaja suala la kufuatilia kwa karibuni na kuwa na welewa wa kina kuhusu mambo na mbinu mpya zinazotumika katika mashambulizi ya kiutamaduni kabla ya kuingia nchini Iran kuwa ni jambo la dharura na kuongeza kuwa, kuchelewa kufahamu na kuchelewa kuchukua hatua mara zote husababisha matatizo, hivyo inabidi kutambua haraka na kuchukua hatua za busara na za hekima katika wakati unaofaa.
Akifafanua zaidi kuhusiana na suala la kukabiliana na jambo hilo kwa hekima inayotakiwa amesema kuwa, baadhi ya wakati inabidi kuzuia moja kwa moja kupenya mashambulizi hayo, lakini kuna baadhi ya mambo yanaweza kupokewa, yakarekebishwa na kutumiwa vizuri.
Ayatullah Udhma Khamenei amezungumzia nukta ya mwisho kuhusu suala la mashambulizi ya kiutamaduni kwa kusema kuwa ni pupa na ni kusubiri mambo yatokee na kuanza kujitetea tu mbele ya utamaduni unaoshambulia na kulitaja jambo hilo kuwa ndilo chaguo baya mno na ni lenye madhara makubwa. Amesema, baadhi ya wakati kuwa na misimamo ya kushambulia huwa ni jambo la lazima katika baadhi ya mambo lakini kwa hali yoyote ile, busara inahitajika katika hali zote, na inabidi kufanywe mambo kwa tafakuri na umakini wa hali ya juu.
Baada ya hapo Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amezungumzia nukta ya tano katika hotuba yake mbele ya mkuu na wajumbe wa Baraza Kuu la Mapinduzi ya Kiutamadunia kwa kusisitizia wajibu wa kuzingatiwa kikamilifu udharura wa kuendelea na hatua za maendeleo ya kielimu katika Vyuo Vikuu na vituo vya utafiti nchini.
Ameitaja kasi ya hali ya juu ya maendeleo ya kielimu ya Iran na maendeleo makubwa ya kielimu liliyopata taifa la Iran katika kipindi cha muongo mmoja uliopita na kuutaja uhakika huo kuwa ni jambo lililojaa baraka ambalo hata wapinzani wa Iran nao wanashindwa kulikanusha.
Ayatullah Udhma Khamenei amekumbushia matamshi ya Rais wa Iran kuhusu suala hilo na kutumia fursa hiyo kuwataka viongozi wote nchini na hasa Mawaziri wa Elimu ya Juu, Afya na Tiba kufanya jitihada zao zote kuhakikisha kuwa gurudumu la maendeleo ya kielimu nchini linaendelea kwa kasi na halipungui kasi yake bali kila leo liwe linazidi kunawiri na kuongezeka kasi hiyo.
Ameongeza kuwa, uhakika unaojulikana kwa jina la "sisi tunaweza" unafukuta ndani ya nyoyo za vijana wa Iran na kwamba mawimbi hayo yanayozaa hamasa yanapaswa yatiwe nguvu ili kwa msaada wa Mwenyezi Mungu yaweze kufanikisha kufika nchi kwenye vilele vya juu vya kilimu na hatimaye Iran kuwa marejeo ya kielimu kama ambavyo mawimbi ya hamasa hizo yaimarishwe vilivyo ili yaweze kusaidia kuundwa ustaarabu mpya wa Kiislamu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu vile vile ametoa nasaha nyingine muhimu sana akisema: Vyuo Vikuu havipaswi kutekwa na mrengo wowote ule wa kisiasa katika hali yoyote ile kwani jambo hilo litazuia ustawi na kasi ya maendeleo ya kielimu nchini.
Vile vile amesisitiza kwamba: Kama ilivyokuwa huko nyuma, bado tunaamini kuwa, vijana na hasa vijana wa Vyuo Vikuu ndio injini ya mabadiliko ya kisiasa na kijamii lakini suala hilo litakuwa kinyume kabisa iwapo Vyuo Vikuu vitabadilika kuwa paredi na uwanja wa kutunishiana misuli mirengo ya kisiasa.
Nukta ya sita iliyokuwemo kwenye hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu wakati alipoonana na wajumbe wa Baraza Kuu la Mapinduzi ya Kiutamaduni ni wasiwasi na hofu yake kuu yaani wasiwasi wake mkubwa kuhusu kudharauliwa na kutozingatiwa inavyopaswa lugha ya Kifarsi na mshambulizi yanayofanywa dhidi ya lugha hiyo.
Amekosoa vikali kutumiwa maneno ya kigeni wakati maneno ya Kifarsi yapo na kuongeza kuwa: Ni jambo la kusikitisha kuona hali imekuwa mbaya kiasi kwamba kuna baadhi ya watu wanaona aibu kutumia istilahi za asili na badala yake wanatumia majina na maneno ya kigeni katika masuala tofauti na hata katika masuala yanayohusiana na watoto wadogo na vijana mabarobaro, na inasikitisha zaidi kuona jambo hilo linakuwa kwa kasi.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa: Baraza Kuu la Mapinduzi ya Kiutamaduni linapaswa sambamba na kukabiliana kwa busara na jaribio lolote la kuidhoofisha na kuidharau lugha ya Kifarsi yenye kina kirefu, yenye utajiri mkubwa wa msamiati na mvuto wa hali ya juu wa maneno, lifanye jitihada kubwa pia na zenye kuonekana katika kustawisha, kukuza na kuimarisha lugha ya Kifarsi katika nyuga zote.
Akiendelea na hotuba yake, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amekumbushia majukumu ya Baraza Kuu la Mapinduzi ya Kiutamaduni katika fani za Sayansi ya Jamii na kuongeza kuwa: Baraza Kuu la Mapinduzi ya Kiutamaduni linapaswa kufanya kazi yake ya kimsingi ya kutunga na kuweka usuli na misingi ya kielimu na kifalsafa ya mapinduzi na mabadiliko makubwa katika masomo ya Sayansi ya Jamii.
Katika nukta yake ya mwisho, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitizia udharura wa kuzingatiwa madhara ya kijamii na sababu zake za kiutamaduni na kuongeza kuwa, kutafuta chanzo na kuchunguza njia za kutatua masuala kama vile talaka, ufisadi wa kifedha na vitendo vya uhalifu ni mambo ambayo nayo yanapaswa kuzingatiwa na kupewa umuhimu mkubwa na baraza hilo.
Amma katika upande wa masuala ya kijamii, amesema kuwa, kupanda umri wa jamii ya Iran ni hatari kubwa kwa Iran na kuongeza kuwa: viongozi nchini wanapaswa kulipa uzito wa hali ya juu suala la kukabiliana vilivyo na kupungua idadi ya vijana nchini na wanapaswa kutafuta utatuzi wa kweli wa jambo hilo.
Vile vile katika mkutano huo, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amemkumbuka kwa wema marhum Dk Hasan Habibi aliyekuwa mmoja wa wajumbe muhimu sana katika Baraza Kuu la Mapinduzi ya Kiutamaduni kabla ya kufariki kwake dunia.
Kabla ya hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Hujjatul Islam Walmuslimin Rouhani, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu amelitaja Baraza Kuu la Mapinduzi ya Kiutamaduni kuwa ndicho chombo kikuu zaidi cha kuweka sera za kiutamaduni nchini Iran na kusema kuwa: Wakati serikali inapohitajia washauri bora kabisa wa masuala ya kiutamaduni haiwezi kupata washauri bora kuliko wajumbe wa Baraza Kuu la Mapinduzi ya Kiutamaduni.
Rais Rouhani ameashiria pia maamuzi muhimu sana ya baraza hilo hususan kuhusu suala la uzalishaji elimu na teknolojia na kusisitiza kuwa: Serikali ina azma ya kweli ya kuchukua hatua za maana na za kivitendo za kukamilisha mchakato wa elimu na teknolojia nchini na kuzalisha utajiri kwa kutumia elimu na kuongeza nguvu za taifa.
Rais Rouhani vile vile amesisitizia azma ya serikali yake ya kutekeleza vilivyo maamuzi yanayofikiwa katika Baraza Kuu la Mapinduzi ya Kiutamaduni na kuongeza kuwa: Miongoni mwa hati za baraza hilo ni hati inayohusiana na watu wenye ushawishi na wenye vipaji ambapo Serikali imeazimia kuchukua hatua maalumu za kutekeleza hati hiyo kupitia kusaidia mashirika ya Elimu Msingi.
Hujjatul Islam Walmuslimin Rouhani amesema kuwa, moja ya misimamo ya Serikali ni kuandaa mfungamano wa kiutamaduni kwa ajili ya masuala ya utendaji, masuala ya kiuchumi na masuala ya kisiasa na kijamii na huku akiashiria namna serikali yake inavyolipa umuhimu mkubwa suala la kulindwa itikadi za kidini na kimaadili ameongeza kuwa: Sisi tunaamini kuwa, itikadi na imani za kidini inabidi zichungwe na zidumishwe kimantiki na kwa misimamo ya wastani na ziepushwe na misimamo ya kufurutu ada na upotoshaji na ziepushwe pia na kutegemea tu shaari na kaulimbiu zisizo na utekelezaji.
Rais Rouhani pia ameashiria nafasi ya wananchi katika masuala ya kiutamaduni na pia jukumu la usimamiaji la Baraza Kuu la Mapinduzi ya Kiutamaduni na kulitaja masuala ya familia na elimu na malezi kuwa yana umuhimu mkubwa na wa hali ya juu na kusisitiza ikuwa: Kurekebisha na kusahihisha utamaduni wa umma katika jamii ni jambo linalowezekana kwa kutumia kutengeneza utamaduni katika familia, elimu na malezi mshuleni.
 
< Nyuma   Mbele >

^