Skip to content

Habari

Habari
Hifadhi

Risala na Barua

Matini
Hifadhi

Kumbukumbu na Simulizi

Kabla ya Mapinduzi
Baada ya Mapinduzi

Sauti na Taswira

Picha
Sauti
Video
Maelfu ya wananchi wa Qum waonana na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Chapa
09/01/2014
Maelfu ya wananchi wa Qum waonana na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya KiislamuAyatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu leo asubuhi (Alkhamisi) ameonana na maelfu ya maulamaa, mafudhalaa, wanachuoni na matabaka mengine mbali mbali ya wananchi wa Qum na kusema kuwa moja ya vipengee muhimu vya tukio la tarehe 19 Dei 1356 (Mwaka wa Kiirani wa Hijria Shamsia sawa na Januari 19, 1978 Milaadia) ni kuchukuliwa hatua za kivitendo kwa kutegemea imani thabiti sambamba na kuwa na muono wa mbali tena katika mazingira magumu sana. Amesisitiza kuwa, somo muhimu zaidi linalopatikana katika tukio la tarehe 19 Dei la huko Qum ni kwamba, ili watu waweze kuvuuka kwenye matatizo, wanapaswa kuwa na imani thabiti na muono wa mbali kuhusu adui na kutomsahau adui wao na kutegemea uwezo na ubunifu wa ndani ya taifa pamoja na vipaji vya vijana wa taifa hilo na kutokuwa na tamaa na misaada kutoka nje.
Ayatullah Udhma Khamenei ambaye ametoa hotuba hiyo mbele ya maelfu ya watu wa Qum kwa mnasaba wa maadhimisho ya mwaka wa thelathini na sita wa kukumbuka harakati ya kihistoria ya tarehe 19 Dei 1356 (Januari 9, 1978) vile vile ameashiria moja ya aya za Surat Rum ya Qur'ani Tukufu ambapo Mwenyezi Mungu anaitaja nusra na kuwasaidia waumini wa kweli kuwa ni haki aliyoitolea ahadi kuitekeleza na kuongeza kuwa, ahadi ya Mwenyezi Mungu ambayo ni lazima hutimia inayotajwa katika aya hiyo inahusiana na mazingira ambayo waumini wa kweli wanakuwa wamefikia katika hali ambayo hawana matumaini tena katika kukabiliana na kambi kubwa ya maadui na kwamba siku hiyo (Dei 19, 1356) ambayo wananchi, vijana, matalaba (wanafunzi wa kidini) wa Qum walipomiminika mabarabarani kumuunga mkono Imam Khomeini (quddisa sirruh) na kunyanyua juu bendera ya kupambana na taghuti na kumwaga damu zao katika harakati hiyo adhimu, mtu yeyote hakuwa akitasawari kwamba harakati hiyo ingeliweza kuwa na taathira kubwa na baraka nyingi kiasi chote hiki. Amesisitiza kuwa, kama imani thabiti na ya kweli itakusanyika pamoja na busuri, muono wa mbali, kuchuliwa hatua za kibitendo, istikama na kusimama kidete, basi bila ya shaka yoyote nusra ya Mwenyezi Mungu nayo itapatikana.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa, kama hutokezea katika baadhi ya mambo, waumini wakakosa kupata nusra ya Mwenyezi Mungu, sababu yake ni udhaifu wa imani ya waumini hao, au imani yao si sahihi au imani yao huwa imekosa busuri na muono wa mbali, kwani imani inapokosa busuri huwa ni kama vile mtu amekosa macho na mtu asiye na macho hawezi kuongoza njia, bali hupotea.
Vile vile Ayatullah Udhma Khamenei amesema: Na hiyo ndiyo sababu inayonifanya niwe ninasisitiza sana suala la busuri na muono wa mbali kila ninapolizungumzia tukio la tarehe 19 Dei.
Amesema, sababu inayozifanya harakati na mapambano ya baadhi ya mataifa yasiweze kupata ushindi ni kutokana na harakati hizo kushindwa kutimiza masharti yanayotakiwa na ndio maana nusra ya Mwenyezi Mungu inakosekana kwenye harakati zao. Amesisitiza kuwa, taifa la Iran liliweza kupata nusra ya Mwenyezi Mungu baada ya kutimiza masharti yote kama vile imani ya kweli, busuri na uono wa mbali, kuchukkua hatua za kivitendo na kusimama imara bila ya kutetereka katika harakati yao na sababu yake ni kwamba taifa la Iran lilikuwa na kiongozi mkweli na mahiri kama Imam Khomeini (quddisa sirruh) ambaye alikuwa ni mwanachuoni mweledi wa masuala ya dunia, ambaye hakuwa kabisa na tamaa za masuala ya kidunia wala ubinafsi na alikuwa na welewa mkubwa wa Qur'ani na sunna za Bwana Mtume.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza pia juu ya wajibu wa kutaamali na kuyaangalia kwa mazingatio matukio ya huko nyuma na kupata funzo ndani yake kutokana na masuala na mambo mazuri na kupata ibra kutokana na mabaya yaliyowakumba waliotangulia na kuongeza kuwa, mtu yeyote hapaswi kujidanganya kuwa, maadui wa Mapinduzi ya Kiislamu sasa wameachana na uadui wao dhidi ya mapinduzi haya.
Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa: Tab'an inawezekana kila adui akalegeza kamba katika misimamo yake lakini si sahihi hata kidogo kumsahau adui na kughafilika na kambi ya adui kama ambavyo si sahihi pia kuziamini tabasamu na vicheko vya adui na wala kudanganywa na vicheko hivyo vya maadui.
Vile vile amesisitiza kuwa, si sahihi hata mara moja kusahau lengo kuu na kuongeza kuwa, lengo la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni kufikia kwenye malengo makuu matukufu ya Uislamu yaani maendeleo ya kimaada na kimaanawi ya mwanadamu na kwamba haiwezekani kulifikia lengo hilo takatifu isipokuwa kwa kuwa na imani thabiti na muono wa mbali kuhusu masuala yanayojiri kila leo na kutoghafilika wala kumsahau kabisa adui.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Sababu iliyonifanya niseme mara nyingi kuwa malengo ya mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran yako wazi ni kwamba wananchi wetu ni watu wenye imani, wenye busuri na muono wa mbali, wanaomtambua vizuri adui na wenye moyo mkubwa wa kufanya kazi na ubunifu.
Ayatullah Udhma Khamenei amesisitiza zaidi kwa kusema: Hivi kuna suala gani ambalo vijana wetu wanaingia ndani yake wakashindwa kulitatua? Kila sehemu walipoona miundombinu yake ipo, vijana wetu huingia na kufanikisha mambo na yote haya ni kutokana na baraka za vipaji na uwezo ambao Mwenyezi Mungu Mtukufu amelitukunuku taifa letu.
Ameongeza kuwa: Nasaha ninazopenda kutoa mara zote ni kuwa, inabidi tutegemee nguvu zetu za ndani na kutokuwa na tamaa kabisa na misaada kutokana nje katika kutatua matatizo ya nchi yetu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa, hakuna shaka hata kidogo kwamba ni jambo la wajibu kuwa amilifu na kufanya harakati katika nyuga za nje na za kimataifa na ameongeza kwa kusisitiza akisema: Amma ni lazima matumaini yetu yawe ni kupata msaada na auni kutoka kwa Mwenyezi Mungu na kutegemea nguvu ya ndani ya taifa letu na ni mtazamo huo ndio unaoipa kinga nchi yetu.
Ayatullah Udhma Khamenei ameendelea na hotuba yake hiyo muhimu kwa kuashiria kosa ambalo limekuwa likifanywa wakati wote na maadui la kutolitambua vyema taifa la Iran na kuongeza kuwa: Maadui wetu leo wanazungumza kwa namna ambayo kana kwamba taifa la Iran limesalimu amri na kunyanyua mikono juu kutokana na vikwazo wakati ambapo uhakika ni kuwa, maadui hao wanaendelea kufanya makosa yao ya kila siku kwani taifa hili si taifa ambalo linaweza kusalimu amri na kunyanyua mikono yake juu kuonesha limeshindwa.
Aidha amesisitiza kuwa, taifa la Iran halikusalimu amri katika mazingira na hali ngumu zaidi ya hii ya leo na kutoa mfano kwa kusema: Mfano wa wazi na usiokanushika ni uhakika kwamba, katika kipindi cha miaka minane ya kujihami kutakatifu (katika vita vilivyoanzishwa na utawala wa wakati huo wa Iraq dhidi ya Iran) ambapo madola yote ya kibeberu ya Mashariki na Magharibi ya wakati huo yalimsaidia Saddam muhalifu dhidi ya taifa na nchi ya Iran lakini kutokana na nia na imani ya kweli na msimamo usiotetereka wa taifa hili wa kuingia katika medani uwezo wake wa ndani, nusra ya Allah ililifikia taifa hili na mikwamo yote ikawa inakwamuka mmoja baada ya mwingine na kuufedhehesha kimataifa utawala wa Baath wa wakati huo wa Iraq na waungaji mkono wake na kuwalazimisha kurudi nyuma.
Ayatullah Udhma Khamenei amesisitiza kuwa: Leo hii pia matatizo yataweza kuondoka tu kwa kutumia mbinu zinazokwenda kinyume na matakwa ya maadui kupitia kusimama imara taifa na kutegemea uwezo wa ndani pamoja na kutawakali kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu.
Ameongeza kuwa, wakati adui anapokumbana na taifa lenye misimamo imara isiyotetereka huwa hana njia nyingine isipokuwa kulegeza misimamo na kurudi nyuma na kwamba kudhani kuwa taifa la Iran limekwenda kwenye meza ya mazungumzo kutokana na mashinikizo na vikwazo ni kujidanganya na ni kosa lililo wazi kabisa na bila ya shaka yoyote taifa la Iran litalivuruga kosa hilo la maadui.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Sisi tangu zamani tuliwahi kusema kuwa, mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran unaweza kufanya mazungumzo na shetani huyu katika baadhi ya mambo maalumu kwa ajili ya kuondoa shari za shetani huyo na kutatua suala fulani.
Ayatullah Udhma Khamenei amesisitiza pia kwamba, moja ya baraka na faida za mazungumzo ya hivi karibuni ni kuzidi kudhihirika wazi uadui wa viongozi wa Marekani dhidi ya Iran na Wairani na dhidi ya Uislamu na Waislamu.
Ameongeza kuwa, jambo hilo limeonekana wazi katika lugha na misamiati iliyotumiwa na viongozi wa Marekani katika wiki za hivi karibuni na watu wote wameona.
Ameongeza kusema: Kama Wamarekani wanaonekana hawachukui hatua dhidi ya jambo fulani, sababu yake ni kuwa wameshindwa kuchukua hatua hizo na si kwa sababu wameacha uadui wao dhidi ya taifa la Iran.
Amesema: Wamarekani wamesema wazi kuwa, kama tungeliweza tungeliangamiza kila nukta ya miradi ya nyuklia ya Iran, lakini hatuwezi. Naam, hawawezi kwani irada ya taifa la Iran ni imara, kwani taifa la Iran limesimama thabiti juu ya miguu yake na limeingiza katika medani ubunifu na uwezo wake.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa: Mazungumzo ya hivi karibuni yameonesha uadui wa Marekani kama ambavyo pia yamefichua uwezo wao.
Ayatullah Udhma Khamenei ameashiria namna viongozi na duru mbali mbali za kisiasa na vyombo vya habari vya Marekani vinavyoendelea kutoa matamshi ya chuki dhidi ya mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu na dhidi ya taifa la Iran ikiwa ni pamoja na madai ya Wamarekani hao kuhusu suala la haki za binaadamu na kuongeza kuwa: Hata kama kila mtu ana haki za kuzungumzia haki za binaadamu, lakini Wamarekani hawana haki za kuzungumzia suala hilo, kwani serikali ya Marekani ndiye mvunjaji mkuu wa haki za binadamu duniani.
Aidha ameashiria uungaji mkono wa kila upande na wa kudumu wa Marekani kwa utawala ghasibu wa Kizayuni na dhulma na jinai zinazofanywa na utawala huo dhidi ya wananchi madhlumu wa Palestina wakiwemo wananchi madhlumu wa Ukanda wa Ghaza na kuwazuia Wapalestina hao kupata hata mahitaji ya awali kabisa ya chakula na tiba na kuhoji kwa kusema: Je, mambo hayo ni ushahidi wa wazi wa dhulma na kukanyaga haki za binadamu? Je, watu hao hawaoni haya kutamka na jina la haki binadamu na kuzungumzia jambo hilo wakati hivi ndivyo wanavyozifanya haki za binadamu?
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria pia ahadi alizotoa Rais wa Marekani wakati wa kampeni za uchaguzi alipoahidi kuifunga jela ya Guantanamo na kushindwa kutimiza ahadi zake hizo baada ya kupita miaka mitano tangu aingie madarakani na kuongeza kwamba: Mashambulizi yanayofanywa na ndege zisizo na rubani za Marekani dhidi ya wananchi wa Pakistan na Afghanistan na maelfu ya jinai nyingine pamoja na mbinu nyingine zisizojulikana za jinai zinazofanywa na Wamarekani kote ulimwenguni ni mambo ambayo yanazidi kubainisha sura hali ya Marekani ya kutoheshimu hata chembe haki za binadamu.
Vile vile Ayatullah Udhma Khamenei amesisitiza kwa kusema: Sisi tuna malalamiko mengi kuhusu vitendo vya Marekani na vya serikali nyingi za nchi za Magharibi kuhusiana na kuvunja kwao haki za binadamu nasi tunawachukua mbele ya mahakama ya fikra za walimwengu ili watoe majibu kuhusu jinai wanazotenda.
Amekumbusha pia kuwa: Taifa la Iran linamtegemea Mwenyezi Mungu Mtukufu na litafanikiwa kuvuuka salama katika vizuizi vyote na kufikia kwenye malengo yake aali na matukufu.
Pia katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amezungumzia nafasi ya wananchi wa Qum katika vipindi mbali mbali vya baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu hususan katika vipindi nyeti na kusema kuwa, nafasi ya wananchi hao ni kubwa na bora kabisa na kusisitiza kuwa: Qum ni kituo kikuu cha wanavyuoni na masomo ya kidini ya Kishia na Kiislamu na ni nembo ya uadhama wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
 
< Nyuma   Mbele >

^