Skip to content

Habari

Habari
Hifadhi

Risala na Barua

Matini
Hifadhi

Kumbukumbu na Simulizi

Kabla ya Mapinduzi
Baada ya Mapinduzi

Sauti na Taswira

Picha
Sauti
Video
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Aonana na Meya na Wajumbe wa Baraza la Kiislamu la Tehran Chapa
13/01/2014

 Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, leo (Jumatatu) ameonana na mkuu na wajumbe wa Baraza la Kiislamu, meya wa Tehran, manaibu wake, na wakuu wa wilaya tofauti za Tehran na huku akiashiria juu ya ulazima wa kupewa umuhimu maalumu na wa kipekee usanifu majengo wa jiji la Tehran kwa lengo la kuleta mtindo wa Kiislamu wa maisha amesisitiza kuwa: Kuendesha jiji kubwa kama la Tehran na miji mingine mikubwa nchini kunataka moyo na kujitolea na kuwatumikia wananchi kwa nia ya kutafuta radhi za Mwenyezi Mungu na kwa kutumia elimu na mikakati mizuri kwa moyo ule ule wa kijihadi ili kwa njia hiyo iwezekane kutatuliwa matatizo yanayojitokeza na kupiga hatua mbele za maendeleo.
Vile vile ametoa mkono wa baraka kwa wajumbe wa duru mpya ya Baraza la Kiislamu la mji wa Tehran na kwa meya wa jiji hilo kutokana na kupata fursa ya kuwatumikia wananchi na kuongeza kuwa, umuhimu wa jiji la Tehran ni mkubwa zaidi ya kuangaliwa katika sura ya jiji kubwa tu.
Amesema, kwa upande mmoja, Tehran ni nembo ya ustawi, ubora, ufanisi na mtindo wa maisha nchini na kwa upande mwingine ni kigezo na ni muonyeshaji njia kwa miji mingine mikubwa kote nchini Iran.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesifu kazi zilizofanywa na ofisi ya meya wa jiji la Tehran katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni na kuongeza kuwa, pamoja na kuwepo baadhi ya matatizo kama vile uchafuzi wa hali ya hewa, usafirishaji na msongamano wa watu mjini Tehran, lakini hatua zilizochukuliwa na ofisi ya meya wa Tehran katika nyuga tofauti kama vile usafi wa mji, sehemu za mabustani na kijani kibichi, kujenga mabarabara makubwa na madaraja ya kisasa, kupanua reli ya chini ya ardhi (metro) na kuandaa maeneo mengi ya michezo ni miongoni mwa mambo muhimu sana yaliyofanywa na ofisi hiyo.
Ayatullah Udhma Khamenei ameitaja siri ya mafanikio hayo kuwa ni kuweko uongozi na usimamiaji wa kijihadi katika kazi hizo na kusisitiza kuwa, wakati unapokuwepo uongozi na usimamiaji wa kijihadi yaani kufanya kazi na kufanya jitihada kwa ajili ya kutafuta radhi za Mwenyezi Mungu na kutumia elimu na mikakati mizuri, matatizo ya nchi ya kipindi hiki cha mashinikizo ya kikhabithi ya madola makubwa na katika mazingira mingine yanaweza kutatuliwa na kuifanya nchi izidi kupiga hatua mbele za kimaendeleo.
Aidha ameashiria kuwepo fikra na mitazamo tofauti ya kisiasa katika Baraza la Kiislamu la jiji la Tehran na kusema kuwa, madhali nia ya wajumbe wote wa baraza hilo itaendelea kuwa ni kuwahudumiwa wananchi; kuwa na mitazamo tofauti wajumbe wa baraza hilo katika kufikia malengo aali na matukufu, hakuwezi kuharibu jambo lolote.
Ayatullah Udhma Khamenei amewakhutubu wajumbe wa Baraza la nne la jiji la Tehran na kuwasisitizia jambo kwa kuwaambia: Fanyeni jitihada kubwa na hima na kuchapa kazi kwa bidii na kulihudumia vizuri taifa ili muweze kuweka kumbukumbu ya uzoefu mzuri wa kazi zenu.
Akiendelea na hotuba yake, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amegusia mambo kadhaa yanayohusiana na ofisi ya meya wa Tehran.
Ushirikiano wa pande mbili baina ya ofisi ya Meya wa Tehran na Serikali, ni maudhui ya kwanza iliyoashiriwa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu.
Ayatullah Udhma Khamenei amesema: Suala hilo ndilo ambalo nimekuwa nikilisisitizia sana na kwa bahati mbaya katika baadhi ya vipindi, nasaha zangu hazikufanyiwa kazi na matokeo yake ikawa ni kupelekea kuzuka matatizo. Kiujumla ni kwamba, inabidi ofisi ya Meya wa Tehran ifanye jitihada zake zote kuhakikisha kwamba inakuwa na muamala mzuri na Serikali na tab'an Serikali nayo nimeshaipa nasaha zangu za kushirikiana vizuri na ofisi ya Meya na Baraza la Kiislamu la jiji la Tehran.
Vile vile ameashiria matamshi ya mkuu wa Baraza la Jiji la Tehran yaliyohusu kuhudhuria mawaziri katika vikao vya baraza hilo na kuongeza kuwa, mwenendo huo wa kushirikiana na kufanya kazi kwa pamoja inabidi uendelee.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislalmu ameashiria pia suala la usanifu majengo na ujenzi wa vitu mbalimbali jijini Tehran na kusema kuwa: Ni ukweli usiopingika kuwa, usanifu majengo na mandhari ya jiji la Tehran si mandhari ya mji wa Kiislamu na kwamba ofisi ya Meya na Baraza la Mji zinapaswa kulifanya suala hilo kuwa ni kadhia inayostahiki kupewa uzito na kipaumbele cha juu kabisa.
Ayatullah Udhma Khamenei ameashiria pia namna usanifu majengo na mandhari ya ujenzi inavyoathiri mtindo wa maisha wa watu wanaoshi katika mji huo na kuongeza kuwa: Inabidi kufanyike jitihada kadiri inavyowezekana kuhakikisha kuwa ufanikishaji wa mtindo wa maisha ya Kiislamu unakuwa rahisi na unasahilishiwa njia.
Vituo vya kiutamaduni vya mji na ulazima wa kulipa uzito mkubwa zaidi suala hilo na vitu vilivyomo kwenye vituo hivyo vya kiutamaduni, ni maudhui nyingine iliyozungumziwa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika miongozo yake hiyo.
Ayatullah Udhma Khamenei amesema: Kazi na hatua za kiutamaduni ni mithili ya upanga wa nchi mbili, kwa maana ya kwamba kama yaliyomo ndani yake yatakuwa mambo mazuri, jamii nayo hutengenea na kufaidika vizuri na kama yaliyomo ndani yake hayatakuwa mambo yanayofaa, hali ya jamii husika nayo huharibika, hupotoka na hukumbwa na matatizo mengi.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amehimiza sana suala la kutumiwa mambo mazuri na yenye athari nyingi katika masuala ya utamaduni na kuongeza kuwa: Katika vituo vya kiutamaduni pia, inabidi watu wenye weledi mkubwa wa masuala ya kiutamaduni watumiwe vizuri; watu ambao wameshikamana vilivyo na dini na wanamapidunzi wenye itikadi thabiti na Uislamu wa kisiasa na mfumo wa demokrasia ya kidini.
Vile vile amesisitiza juu ya wajibu wa kujiepusha na israfu na ubadhirifu katika ofisi ya Meya na kutiwa nguvu moyo wa kufanya kazi kwa bidii na kwa njia sahihi na uaminifu. Amma kuhusu uhusiano baina ya Baraza la Mji na ofisi ya Meya amesema: Baraza la Mji la Kiislamu linapaswa sambamba na kusimamia kazi za ofisi ya Meya, linapaswa pia kuisaidia na kuunga mkono kazi za ofisi hiyo na kuhakikisha kuwa kazi zinafanyika kwa maelewano, kiudugu na kwa kila mmoja kuhisi wajibu wa kutekeleza vizuri majukumu yake.
Ayatullah Udhma Khamenei vile vile amesisitiza juu ya wajibu wa kujua thamani ya mabustani na miti iliyoko katika kila kona ya Tehran kama ambavyo amesisitizia pia wajibu wa kulindwa utajiri huo wa taifa na aidha amezungumzia ujenzi katika maeneo ya juu ya Tehran na wajibu wa kuzuia kubadilishwa vyanzo vya kimaumbile kuwa majengo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu vile vile ameshukuru jitihada na kazi za utumishi zilizofanywa na wajumbe wa Baraza la Tatu la Kiislamu la Jiji la Tehran na amemshukuru pia Muhandisi Chamran, mkuu wa baraza hilo la tatu.
Mwanzoni mwa mkutano huo, meya wa jiji la Tehran, Bw. Mohammad Baqer Qalibaf ametoa ripoti fupi kuhusu kazi za ofisi ya meya ya jiji la Tehran na kutaja baadhi ya malengo na mikakati ya ofisi hiyo kuwa ni pamoja na kufanya kazi kwa kuzingatia uadilifu, kupungua mwanya wa matabaka ya watu katika jiji, kuimarisha moyo wa kijihadi na utamaduni kwa kuchapa kazi na kufanya jitihada mbalimbali, kusisitizia na kutia nguvu kazi za kielimu, za utafiti na za hekima na kuimarisha busara za kijamii, kushirikishwa wananchi na watu wenye vipaji mbali mbali katika uendeshaji wa jiji, kupambana vilivyo na ufisadi wa kiofisi na kifedha, kuipa kipaumbele misikiti, husainia na Hawza (vyuo vikuu vya kidini), kuweko uwazi na kuheshimu sheria, kuwepo uratibu wa pamoja na kusisitizia ushirikiano wa kiudugu baina ya ofisi ya meya na wajumbe wa Baraza la Jiji.
Vile vile ametoa ripoti kuhusu hatua na kazi zilizofanywa na ofisi ya Meya ya jiji la Tehran katika kipindi cha miaka minane iliyopita ikiwa ni pamoja na kilomita 235 za barabara kubwa, madaraja 330, kuongeza njia za reli ya chini ya ardhi (metro) kwa urefu wa kilomita 162, kujenga viti elfu kumi vya sinema na kujenga bustani ya kumbukumbu za vita vya kujihami kutakatifu na bustani ya Kitabu pamoja na maeneo mengi ya kielimu na kimichezo.
Naye Bw. Masjid Jamei, Mkuu wa Baraza la Kiislamu la Jiji la Tehran ametoa ripoti fupi kuhusu kazi za baraza hilo ikiwa ni pamoja na kuundwa tume tatu maalumu ile ya usimamiaji, ile ya usalama wa kiafya na ile ya kusimamia ujenzi wa majengo na ujenzi wa mji, katika baraza hilo kwa lengo la kuchunguza na kutatua matatizo yanayojitokeza.
Vile vile ameashiria uzoefu, utaalamu na historia ya kujitolea ya wajumbe wa Baraza la Jiji la Tehran na kusema kuwa, kuna ushirikiano mzuri na wa kiurafiki na kidugu baina ya baraza hilo na Serikali na Majilisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran). Ameongeza kuwa, ushirikiano na msaada wa wajumbe wa baraza hilo ni jambo muhimu na lenye thamani kubwa na kwamba jambo hilo linaweza kusaidia sana katika utatuzi wa mambo mengi.
 
< Nyuma   Mbele >

^