Skip to content

Habari

Habari
Hifadhi

Risala na Barua

Matini
Hifadhi

Kumbukumbu na Simulizi

Kabla ya Mapinduzi
Baada ya Mapinduzi

Sauti na Taswira

Picha
Sauti
Video
Wakuu wa Mihimili Mitatu Mikuu wa Dola la Iran Wafanya Kikao Kilichohudhuriwa na Kiongozi Muadhamu Chapa
25/02/2014
 Kufuatia kuwasilishwa na kukabidhiwa siasa kuu kuhusiana na uchumi wa kimuqawama na wa kusimama kidete, Kiongozi Mudhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu jana alishiriki katika kikao kilichohudhuriwa na wakuu wa mihimili mitatu mikuu ya dola ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran (Serikali, Bunge na Mahakama) na kuzungumza nao kuhusu namna na njia za kutekeleza kwa ufanisi siasa hizo.
Mwanzoni mwa kikao hicho Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei amewashukuru wakuu wa mihimili hiyo mitatu mikuu wa dola kwa kuweka ajenda za utekelezaji kwa ajili ya kufuatilia na kubuni haraka sana muongozo na ramani ya njia ya kutekeleza siasa za uchumi huo wa kimuqawama na wa kusimama kidete. Amesema: Siasa kuu za uchumi wa kimuqawama ni siasa pana zinazokusanya mambo mengi na kwamba kuna haja na udharura wa kuzingatiwa suala hilo kwa upana wa mambo yake mengi yaliyomo ndani yake katika kupanga sera za kuzitekeleza.
Ameyataja masuala ya kiuchumi na matatizo yanayotokana na masuala hayo kuwa ni suala muhimu sana kwa nchi na wananchi na kuongeza kuwa: Iwapo siasa kuu za uchumi wa kimuqawama zitafuatiliwa na kutekelezwa kwa uzito mkubwa na wa hali ya juu, basi kuna matumaini makubwa ya kustawi hali ya uchumi na kurekebishwa misingi ya uchumi wa nchi na kutatuliwa sehemu ya matatizo ya wananchi katika kipindi kifupi kijacho.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza pia kuwa, lengo la kufanyika kikao hicho kati yake na wakuu wa mihimili mitatu mikuu ya dola ni kujadili njia za kuweza kufanikisha utekelezaji wa kivitendo wa siasa kuu za uchumi wa kimuqawama na kuongeza kuwa: Baada ya kuwasilishwa na kukabidhiwa mihimnili hiyo mitatu mikuu siasa hizo, wananchi sasa wanasubiri kuona siasa hizo kuu zinatekelezwa na kupatikana taathira nzuri za siasa hizo za uchumni wa kusimama kidete, hivyo mihimili mitatu mikuu, Serikali, Bunge na Mahakama inapaswa kuanza kazi kwa uzito wa hali ya juu na kufuatilia na kufanikisha kwa kina kikubwa, majukumu yao katika kila sekta.
Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa: Inabidi mchakato wa utekelezaji wa siasa kuu za uchumi wa kimuqawama ziendelee kwa sura ya harakati ya kudumu na isiyosita hadi yatakapopatikana matunda yanayotakiwa na kila mhimili unapaswa kusimamia kwa kina mchakato wa kazi za kuweza kulifanya kwa ufanisi mkubwa jambo hilo.
Amesisitiza kuwa: Kama italazimu kuondoa baadhi ya sheria zinazokwamisha utekelezaji wa siasa kuu za uchumi wa kimuqawama, basi Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) ifanye uchunguzi kuhusu sheria hizo na kuziondoa. Vile vile iwapo utekelezaji wa siasa hizo utahitajia kufutwa baadhi ya njia na mbinu za utekelezaji na kuwekwa mikakati mipya, basi Serikali ifuatilie jambo hilo na kubuni njia mpya za kurahisisha utekelezaji wa siasa hizo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amekumbushia nukta moja nyingine kuhusu suala hilo akisema: Inabidi kuwa na hadhari ili sheria na mikakati mipya isitungwe na kubuniwa kwa namna ambayo itapelekea kuzuka mgongano wa kisheria.
Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa, kwa kufutwa na kuondolewa sheria na mbinu za utekelezaji zinazokinzana na siasa kuu za uchumi wa kimuqawama na baadhi ya wakati kupasisha sheria na kuweka mikakati mipya ya utekelezaji, kutaweza kurahisisha njia ya kutekeleza siasa hizo; jukumu ambalo kimsingi ni la Serikali.
Aidha ametoa nasaha maalumu kwa Serikali akiiambia: Undeni timu ya kufuatilia na kutekeleza sisa kuu za uchumi wa kimuqawama yenye watu ambao wana misukumo na malengo ya kimapinduzi na wenye imani ya kutosha ya wananchi ili waweze kutekeleza vizuri siasa hizo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amelitaja suala la kuweko uratibu wa pamoja baina ya mihimili mitatu mikuu ya dola katika utekelezaji wa siasa kuu za uchumi wa kimuqawama kuwa ni jambo la dharura sana na kusisitiza kuwa: Inabidi kujiepusha kikamilifu na kuunda taasisi nyingi mpya mpya na kufanya kazi kipeke yake peke yake.
Aytullah Udhma Khamanei amelitaja suala la kuandaa mazingira ya kujengeka utamaduni wa watu wote wa kutekeleza siasa kuu za uchumi wa kimuqawama kuwa nalo ni jambo la dharura na kuongeza kuwa: Inabidi wananchi waelezwe na kupewa hoja kwa njia sahihi na za kimantiki kuhusu vipengee vikuu vya siasa hizo ili pole pole vipengee vya siasa hizo viweze kupenya na kukita mizizi katika jamii na kuzifanya siasa hizo kuwa mahitajio ya umma na ya watu wote.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Kuitisha mijadala kuhusu uchumi wa kusimama kidete na wa kimuqawama na kufanya jambo hilo kuwa mijadala na mazungumzo ya watu wote ni suala ambalo linaweza kuondoa matatizo mengi na kurahisisha kazi ya utekelezaji wa siasa hizo.
Vile vile ametaja moja ya mihimili mikuu ya siasa hizo kuu za uchumi wa kimuqawama kuwa ni kushirikishwa wananchi na namna ya kuufanya uchumi kuwa mikononi mwa wananchi na kuongeza kuwa: Katika kipindi chote hiki cha miaka 35 hususan katika kile kipindi cha ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu na kile kipindi cha miaka minane ya vita vya kujihami kutakatifu (vilivyoanzishwa na utawala wa zamani wa Iraq dhidi ya utawala mchanga wa Jamhuri ya Kiislamu nchini Iran), nchi ya Iran imepata faida kubwa kutokana na kushirikishwa wananchi katika masuala mbali mbali, na kwamba katika suala la kiuchumi pia, bila ya shaka yoyote iwapo uwekezaji na rasilimali ndogo ndogo za wananchi zitaongozwa upande wa uchumi wa umma na watu wote, jambo hilo litaweza kutoa athari kubwa nzuri na kusahilisha mno mambo.
Kiongozi Muadhamu wa mapinduzi ya Kiislamu amesema: Kwa kutumiwa uwezo na nafasi ya wananchi, inawezekana kabisa kufanya kazi ambazo yumkini hata haziwezekani kufanywa na wizara kadhaa.
Ayatullah Udhma Khamenei amelitaja suala la kupunguza uingizaji bidhaa kutoka nje na kudhamini usalama wa chakula na akiba ya kiistratijia, kuwa ni mhimili mwingine mkuu wa siasa kuu za uchumi wa kusimama kidete na kusisitiza kuwa: Ukitoa masuala hayo, inabidi kuzuiwe kabisa kuingiza nchini kiholela bidhaa nyinginezo kutoka nje.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema mwishoni mwa miongozo yake hiyo muhimu kwamba: Hivi sasa mazingira mazuri yameandaliwa kwa ajili ya kuanza utekelezaji wa kivitendo wa siasa kuu za uchumi wa kimuqawama na kwamba kama mihimili yote mikuu ya dola pamoja na taasisi nyinginezo zitatia hima na kufanya jitihada zinazotakiwa, basi kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu jambo hilo litaweza kutendeka kwa ufanisi mkubwa na kwa sura nzuri kabisa.
Katika kikao hicho, Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameashiria hatua yake ya hivi karibuni ya kumhimiza Makamu wa Kwanza wa Rais na kuipa jukumu kamati ya uratibu wa kiuchumi ya Serikali la kuweka mipango maalumu ya kufanyika katika wakati maalumu wa utekelezaji sambamba na umuhimu wa kubuniwa mikakati madhubuti ya utekelezaji wa siasa kuu za uchumi wa kimuqawama na kuongeza kuwa: Serikali yake yote ina imani ya dhati kuhusiana na siasa hizo na watumishi serikali nao wana nia ya kweli ya kuzitekeleza kiufanisi siasa hizo kwani Serikali inaamini kuwa kama itaweza kufanikisha inavyotakiwa utekelezaji wa siasa kuu za uchumi wa kimuqawama basi jambo hilo litaleta mapinduzi na mabadiliko makubwa katika uchumi wa nchi.
Bw. Rouhani aidha ameashiria zoezi linalotarajiwa kufanywa hivi karibuni na serikali la kuanza kutekeleza awamu ya pili ya mpango wa kutoa ruzuku kwa malengo maalumu na kuongeza kuwa: Kama ilivyosisitizwa katika siasa zilizowasilishwa, Serikali itatumia fursa ya mpango wa kutoa ruzuku kwa malengo maalumu kuyapa kipaumbele maalumu masuala ya uzalishaji wa ndani ya nchi, kubuni nafasi za kazi na kudumisha uadilifu katika jamii.
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameashiria pia kipengee kinachozungumzia suala la usalama wa chakula na masuala ya afya kilichomo katika siasa kuu za uchumi wa kimuqawama na kusema: Usalama wa chakula na usalama wa kiafya wa wananchi ni masuala mawili muhimu sana ambapo Serikali tangu awali kabisa ya kuingia kwake madarakani imetoa hima na kipaumbele maalumu juu ya maudhui hizo mbili na kwamba katika awamu wa pili ya utekelezaji wa mpango wa kutoa ruzuku kwa malengo maalumu, suala la kuongeza usalama wa kiafya wa wananchi litakuwa moja ya mihimili mikuu ya utendaji wa Serikali.
Dk Rouhani ameashiria pia suala la mafuta, gesi na petrokemikali ambayo ni moja ya mihimili ya siasa kuu za uchumi wa kimuqawama na wa kusimama kidete akisisitiza kwamba: Serikali ina nia ya kuongeza kiwango cha uzalishaji wa mafuta na gesi ili kwa njia hiyo iweze kuliweka katika ajenda zake muhimu suala la kustawisha uzalishaji wa sekta ya petrokemikali.
Kuweka mikakati na mipango ya kuweza kustafidi vilivyo na kwa njia sahihi na uwezo na fursa za maeneo huru hususan ya kiuchumi na hasa hasa katika sekta ya utalii wa masuala ya kiafya na vile vile kutoa msukumo kwa sekta ya usafirishaji nje bidhaa, kutilia mkazo suala la kuleta mabadiliko katika nguvu kazi na uchumi utokanao na elimu za kimsingi kuwa ni moja ya masuala ambayo Rais Rouhani ameyazungumzia kuhusiana na siasa kuu za uchumi wa kimuqawama.
Kwa upande wake, Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu yaani Bunge la Iran, Dk Ali Larijani amesisitiza katika kikao hicho juu ya namna wabunge wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu wanavyolitilia hima na kulipa umuhimu mkubwa suala la kuandaliwa uwanja mzuri wa kutekelezwa siasa kuu za uchumi wa kimuqawama na kusema kuwa, nia na azma ya mihimili mitatu mikuu ya dola ni muhimu mno katika utekelezaji wa siasa hizo.
Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu vile vile amelitaja suala la kuipa kipaumbele na mazingatio maalumu sekta ya uzalishaji bidhaa ndani ya nchi na kuwatumia vizuri wataalamu wa ndani pamoja na sekta binafsi na kuzuia kuingiza ovyo bidhaa kutoka nje ya nchi kuwa ni moja ya nyuga za dharura za kuendeshea siasa kuu za uchumi wa kimuqawama.
Ameongeza kuwa: Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) imetunga na kupasisha sheria nzuri za kusahilisha na kuleta wepesi katika masuala ya kutafuta rizki na kufanya kazi na hivi sasa hakuna tatizo lolote la kisheria kwa uwekezaji na kazi za sekta binafsi.
Bw. Ali Larijani vile vile amesisitizia udharura wa vyombo vya habari kuyapa mazingatio maalumu masuala na vipaumbele vya kiuchumi na kujiepushe na masuala ya pembeni na yasiyo na tija, ya kisiasa.
Naye Ayatullah Amoli Larijani, Mkuu wa Chombo cha Mahakama cha Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameashiria katika kikao hicho juu ya kifungu cha 19 cha siasa kuu za uchumi wa kimuqawama kinachohusiana na udharura wa kuweko uwazi na wajibu wa kufanyika jitihada na harakati salama za kiuchumi na kuzuia kujitokeza nyuga za ufisadi akisisitiza kwamba: Chombo cha Mahakama kitaendelea kwa nguvu zake zote kutekeleza vilivyo majukumu yake ya kupambana na ufisadi wa kiuchumi, na wakati huo huo kitaendelea kuunga mkono jitihada na harakati salama za kiuchumi.
Vile vile mkuu wa chombo cha mahakama cha Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amelitaja suala la kueneza katika jamii fikra za uchumi wa kimuqawama na wa kusimama kidete kuwa ni jambo la dharura na kusisitiza kuwa: Moja ya mambo ya lazima na ya dharura kwa ajili ya kufanikisha siasa kuu za uchumi wa kimuqawama ni kulipa mazingatio maalumu suala la utamaduni wa kuchapa kazi katika jamii.
 
< Nyuma   Mbele >

^