Skip to content

Habari

Habari
Hifadhi

Risala na Barua

Matini
Hifadhi

Kumbukumbu na Simulizi

Kabla ya Mapinduzi
Baada ya Mapinduzi

Sauti na Taswira

Picha
Sauti
Video
Wajumbe wa Baraza la Wanavyuoni Wataalamu Waonana na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Chapa
06/03/2014
 Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu leo asubuhi (Alkhamisi) ameonana na mkuu na wajumbe wa Baraza la Wanavyuoni Wataalamu (linalomchagua na kusimamia kazi za Kiongozi Muadhamu) na kutoa hotuba muhimu. Amegusia baadhi ya matukio ya kimataifa na kuzungumza kwa ubainifu kuhusu majukumu waliyo nayo viongozi wa mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu katika wakati huu nyeti na tata. Aidha amesisitiza kuwa: "Kuangalia mambo katika uhalisia wake na kuziona nukta nyingi chanya pamoja na zile chache dhaifu," "kujivunia kizazi cha vijana waumini na wanamapinduzi," "kustafidi vizuri na uwezo usio na idadi wa ndani na wa taifa," "kutomsahau adui na maadui na kutoghafilika nao," "kuweka mipaka iliyo wazi na bayani na kambi ya kiistikbari," "kutofanya woga mbele ya adui," "kuwategemea wananchi na kutia nguvu harakati ya kijihadi," "kulinda na kutia nguvu umoja na mshikamano wa kitaifa," "kuzingatia na kuupa umuhimu mkubwa utamaduni wa kidini na kimapinduzi" na "kueneza utamaduni wa kuweko majadiliano katika masuala mbali mbali" ni mambo muhimu na kwamba hayo ni miongoni mwa majukumu hatari waliyo nayo viongozi wa Jamhuri ya Kiislamu katika sekta tofauti.
Mwanzoni mwa hotuba yake, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria nafasi maalumu na ya kipekee ya Baraza la Wanavyuoni Wataalamu katika majimui ya nguzo za mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu na kusema: Ijtimai na kujumuika pamoja maulamaa, watu wakubwa na mujtahidi wa taifa la Iran katika vikao vya Baraza la Wanavyuoni Wataalamu, daima kumekuwa na umuhimu mkubwa, lakini umuhimu huo katika baadhi ya mazingira na nyakati unakuwa mkubwa zaidi ambapo wakati uliopo hivi sasa ni miongoni mwa nyakati hizo zinazozifanya kazi za baraza hilo kuwa na umuhimu mkubwa zaidi.
Aidha Ayatullah Udhma Khamenei ameashiria matukio muhimu na tata yanayotokea leo hii duniani na katika eneo la Mashariki ya Kati na kulitaja suala la kujiangalia upya na kutathmini na kufanya jadidi majukumu, kuwa ni miongoni mwa dhima na wajibu wa wakati huu wa viongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kuongeza kuwa: Katika hali na mazingira kama haya, nguzo zote za mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu likiwemo Baraza la Wanavyuoni Wataalamu zinapaswa kuwa na mitazamo ya kiubunifu na ya kimsingi kuhusu matukio yanayojiri ulimwenguni.
Baada ya hapo, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amebainisha baadhi ya matukio yanayojiri leo hii katika kona mbali mbali za dunia na kusisitiza kuwa: Kuanza mabadiliko ya kimsingi duniani na katika eneo la Mashariki ya Kati na kujitokeza wazi dalili zake katika maeneo tofauti ikiwa ni pamoja na huko kaskazini mwa Afrika, Asia na Ulaya ni moja ya matukio ya hivi sasa ambayo inabidi dalili zake zionekane mapema na kufuatilia kwa karibu matukio hayo na pia kuyafanyia uchunguzi wa kina.
Kuvurugika na kuondoka utulivu wa kidhahiri wa kambi ya kibeberu na madola ambayo yanataka milele yawe madola makubwa duniani na yaendelee kuudhibiti ulimwengu ni tukio la pili ambalo Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameliashiria na kusema: Moja ya ishara na dalili za kukorogeka na kutibuka utulivu huo wa kidhahiri na wa kijuu juu wa madola hayo ni mgogoro wa kiuchumi ulioikumba Ulaya na Marekani ambapo dalili na alama za kufilisika uchumi wa nchi hizo zinazidi kujitokeza.
Ayatullah Udhma Khamenei amekutaja kuporomoka na kufeli katika upande wa kimaadili na kukanyagwa misingi ya kibinadamu na kuzidi kufichuka sura na utambulisho halisi wa utamaduni wa Magharibi uliojengeka juu ya misingi ya "Humanism" (fikra na aidiliojia ya ‘ubinaadamu' inayompa kipaumbele kwanza binadamu na mahitaji yake kuliko misingi ya dini, mapote yanayoegemea humanism na falsafa iliyozaliwa kutokana na fikra hizo za humanism ya Magharibi na kwa mujibu wa fikra hiyo, mwanadamu yuko huru kufanya analopenda bila ya kujali mipaka iliyowekwa na dini) kuwa ni miongoni mwa dalili na ishara za kuburugika na kuzidi kuvurugika utulivu huo wa kijuu juu wa kambi ya kibeberu na kusisitiza kuwa: Mauaji, uporaji, utumiaji mabavu, ufisadi, uasherati, mahusiano machafu ya kijinsia kama vile kuenea ndoa za watu wa jinsia moja, kuunga mkono wazi wazi ugaidi, machafuko na vitendo vya kinyama na kihayawani katika eneo hili na kuvunjia heshima wazi wazi matukufu na watu watukufu wa kidini, ni mifano ya wazi kabisa ya kuporomoka utamaduni wa Magharibi katika masuala ya kimaadili.
Vile vile amekutaja kuporomoka vibaya misingi ya kielimua na kiutambulisho ya utamaduni wa Magharibi mmoja baada ya mwingine na kuzidi walimwengu kuichukia Marekani na madola mengine ya kiistikbari na kuzidi kufedheheka kimataifa madola hayo ya kibeberu kuwa ni ishara na dalili nyingine za kuporomoka utamaduni wa Magharibi zinazoshuhudiwa katika matukio yanayotokea hivi sasa duniani.
Ameongeza kuwa: Kuamka mataifa ya dunia hususan mwamko unaoshuhudiwa katika ulimwengu wa Kiislamu na kuzidi kuimarika istikama ya Kiislamu ni tukio jingine katika matukio muhimu ya leo hii duniani.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria pia misimamo inayochukuliwa na baadhi ya watu katika kuzungumzia istilahi ya "Mwamko wa Kiislamu" na kusisitiza kuwa: Hivi sasa imebainika wazi kwamba mwamko huo ulikuwa unahusiana kikamilifu na Uislamu ijapokuwa katika dhahiri yake inaonekana kuwa wameuzima lakini moyo ya kujiamini na kujitambulisha kwa utambulisho wa Kiislamu si jambo ambalo linaweza kuondoka wakati wowote ule na hivi sasa pia mwamko huo haujazimwa na haujaondoka.
Pia Ayatullah Udhma Khamenei amekutaja kuzidi kuimarika na kusimama kidete na kuzidi kupata nguvu heshima ya Kiislamu ya taifa la Iran na moyo wa kupenda kuwa huru na kujitegemea taifa la Iran licha ya kupita miaka 35 ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu kuwa ni miongoni mwa matukio muhimu yanayoshuhudiwa duniani leo na kuongeza kuwa, moyo wa kimapinduzi bado uko hai ndani ya taifa la Iran na kile kilichoshuhudiwa katika maandamano ya mwaka huu ya Bahman 22 (zilipofikia kileleni sherehe za Mapinduzi ya Kiislamu ya nchini Iran) lilikuwa ni tukio la kipekee na la aina yake linalozidi kutilia nguvu suala hilo.
Baada ya kubainisha baadhi ya matukio muhimu yanayoshuhudiwa duniani leo, Ayatullah Udhma Khamenei amebainisha majukumu ya viongozi wa mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu katika kipindi na wakati huu nyeti sana.
Kuhusu suala hilo Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametaja majukumu 12 ya viongozi wa mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu.
Kuangalia mambo katika uhalisia wake na kuziona nukta nyingi chanya pembeni mwa baadhi ya nukta dhaifu, ni jukumu la kwanza ambalo Ayatullah Udhma Khamenei ameliashiria na kusema: Ukweli wa mambo ni kuwa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran tofauti na mapinduzi mengine ya kawaida duniani, licha ya kupita zaidi ya miongo minne ya tangu kupata kwake ushindi (Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran) bado yako hai kabisa na yako imara na yamesimama imara kupigania Uislamu, uhuru, kusimama imara kitaifa na kujistawisha kwa kutumia nguvu za ndani na kusimamisha uadilifu na wakati wote (mapinduzi hayo) yanafanya juhudi za kufikia malengo hayo makubwa.
Kujivunia kizazi cha vijana kilichoshikamana na dini na chenye fikra za kimapinduzi na kujua thamani ya vijana hao, ni jukumu jingine ambalo Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amewakumbusha viongozi wa Jamhuri ya Kiislamu.
Ameongeza kuwa: Hadhi na umuhimu wa kizazi cha vijana cha hivi sasa cha Mapinduzi ya Kiislamu ni umuhimu wa juu zaidi kuliko hata wa vijana wa mwanzoni mwa Mapinduzi ya Kiislamu kwani vijana wa leo pamoja na kwamba hawakuwepo na hawakuuona ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu na masuala yaliyoambatana na ushindi huo na licha ya kwamba wanakabiliwa na anuwai kwa anuwai ya mashambulizi yanayotokana na upotoshaji wa vyombo vya mawasiliano ya umma vinavyotumia satalaiti pamoja na Intaneti, lakini wameendelea kushikamana na dini na kusimama imara juu ya misingi ya Mapinduzi ya Kiislamu.
Ayatullah Udhma Khamenei aidha amelitaja suala la kuzingatia na kuupa umuhimu mkubwa uwezo mbali mbali usio na idadi wa kitaifa na wa ndani ya Iran na kustafidi nao vizuri, kuwa ni jukumu jingine la viongozi wa Jamhuri ya Kiislamu na kuongeza kwamba: Kwa bahati nzuri, viongozi nchini Iran wakiwemo viongozi wa serikali mpya, wote wanaujua uwezo usio na idadi wa ndani ya nchi na wanaamini kuwa inabidi uwezo huo utumiwe vizuri kadiri inavyowezekana.
Ameongeza kuwa: Ni uwezo huo mkubwa wa ndani ndio uliowafanya baadhi ya viongozi wa mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu kupata fikra ya kuwa na uchumi wa kimuqawama na wa kusimama kidete.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza pia juu ya wajibu ya kutoghafilika na kutomsahau hata chembe adui na maadui akisema kuwa hilo ni jukumu jingine muhimu la viongozi wa Jamhuri ya Kiislamu.
Ameongeza kuwa: Madhali mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu na taifa la Iran litaendelea kushikamana na usuli na misingi ya Uislamu, Mapinduzi ya Kiislamu na kuendelea kuwa huru, basi adui naye ataendelea na uadui wake dhidi ya taifa hili, hivyo si sahihi hata kidogo kughafilika na kumsahau adui hata mara moja.
Ayatullah Udhma Khamenei amesisitiza kwamba, kambi ya kibeberu ina uadui mkubwa sana na taifa la Iran na leo hii watu wote wanauona ukubwa wa chuki, bugudha, fihi, uhasidi na ushari wa maadui hao katika matamshi yao.
Vile vile amelitaja suala la kutekeleza kivitendo siasa za uchumi wa kimuqawama na wa kusimama kidete kuwa ni jukumu jingine walilo nalo viongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Ameongeza kuwa, pamoja na kwamba adui ana chuki na husda kubwa dhidi ya taifa la Iran, lakini ameshindwa kukabiliana na mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu na taifa la Iran na ni kwa sababu ya kushindwa kwake huko ndio maana ameamua kuliwekea vikwazo taifa hili wakati hata wenyewe hao maadui wanatambua kuwa, vikwazo vimefeli na havina faida tangu awali kabisa ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu hadi hivi sasa.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amekitaja kitendo cha viongozi wa Marekani cha kutoa vitisho vya maneno vya kutumia nguvu za kijeshi dhidi ya Iran kuwa ni ushahidi wa kutokuwa na faida vikwazo vya maadui hao dhidi ya taifa la Iran na kuongeza kwamba: Umoja na mshikamano uliopo baina ya wakuu wa mihimili mitatu mikuu ya dola (Serikali, Bunge na Mahakama) na viongozi wote wa serikali iwe ni mheshimiwa Rais au mawaziri wake kuhusu wajibu wa kutekeleza kivitendo siasa za uchumi wa kimuqawama na wa kusimama kidete ni bishara njema kwamba, kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu, uchumi wa kimuqawama utavishinda vikwazo na njama zote za maadui.
Ayatullah Udhma Khamenei amelitaja suala la kuwategemea wananchi na kufanya harakati kijihadi kuwa ni jukumu jingine muhimu la viongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kuongeza kuwa: Tangu awali ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu hadi hivi sasa, imethibitika kwamba kila wakati wananchi walipoingizwa katikati ya medani na kuanza harakati ya kijihadi kwa jina la Mwenyezi Mungu, mara zote wananchi hao ndio walioshinda ambapo mfano wa wazi kabisa wa jambo hilo ni ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu (uliong'oa mzadarakani mfalme Shah) na ushindi lilioupata taifa la Iran katika vita vya miaka minane vya kujihami kutakatifu (vilivyoanzishwa na utawala wa wakati huo wa Iraq dhidi ya utawala mchanga wa wakati huo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran).
Aidha amelitaja suala la wajibu wa viongozi nchini Iran kuwa macho wakati wote na kupima hali ya hivi sasa na uwezo mbali mbali uliopo leo na mazingira yaliyokuwepo katika miaka ya huko nyuma kuwa ni jukumu jingine la viongozi wa Jamhuri ya Kiislamu na amma kuhusu jukumu la viongozi nchini Iran ametoa ufafanuzi zaidi akisema kuwa: Viongozi nchini wanapaswa kuweka mipaka iliyo wazi kati yao na maadui hususan katika kipindi na wakati wa hivi sasa.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kwamba: Kuna baadhi ya watu wanafanya makosa wanapojaribu kuonesha kwamba kuweka mipaka na adui kuna maana ya kukata uhusiano na dunia wakati ambapo kuweka mipaka iliyo wazi na kambi ya adui ni sawa na kuweka mipaka ya kijiografia ambayo itatupambanua sisi na adui.
Ayatullah Udhma Khamenei amewakosoa pia watu ambao wanafanya juhudi za kutumia kisingizio cha utandawazi kufifiliza na kupunguza nguvu za suala la kuwa huru na kutokuwa tegemezi na kuongeza kwamba: Kuwa huru ni miongoni mwa mipaka tunayopaswa kuiweka kati yetu na adui na kwamba watu ambao wanajaribu kufifiliza na kufubaza rangi ya mipaka ya kidini, kiitikadi na mipaka ya kisiasa au kuifuta kabisa mipaka hiyo wajue kuwa kufanya kwao huko ni kwa madhara ya nchi na wananchi wa Iran.
Ameongeza kuwa: Hakuna mtu anayepinga suala la kuwa na uhusiano na nchi nyingine duniani lakini inabidi ibainike wazi kwamba tunapaswa kuwa na uhusiano na nchi gani na uhusiano huo uwe wa namna gani.
Vile vile Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amewakosoa watu ambao wanatumia baadhi ya matatizo yaliyopo nchini kuwalaumu watu waliosimama kidete na kuongeza kuwa: Baadhi ya watu wasifikirie kuwa kama sisi tutawapigia magoti magodi maadui na kujisalimisha kwa maadui hao, basi matatizo yaliyopo yataondoka.
Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa: Mimi kusema kweli ninawashukuru sana viongozi wa nchi ambao wanachukua misimamo iliyo wazi mbele ya adui na kutangaza wazi kuwa taifa la Iran na Mapinduzi ya Kiislamu hayatetereki na kwamba kuwa na misimamo ya aina hiyo mbele ya adui kunapaswa kuenee kwa watu wote nchini.
Aidha ametaja jukumu jingine la viongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuwa ni kutokuwa na woga mbele ya adui na watawakali na kumtegemea Mwenyezi Mungu katika mambo yao yote. Amesisitiza kuwa: Leo hii maadui wa taifa la Iran ni miongoni mwa madola yenye jina baya kabisa. Hivi sasa Marekani inatambulika kimataifa kuwa dola la kibeberu linalopenda kutumia mabavu, kufanya jinai na ni mkiukaji mkubwa wa haki wanadamu na hata ndani ya Marekani kwenyewe utawala wa nchi hiyo unaonekana kuwa ni utawala pandikizi unaosema uongo kiasi kwamba leo hii kiwango cha imani ya wananchi wa Marekani kwa serikali yao kiko chini kabisa.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kusema: Hivyo si sahihi kujitia woga mbele ya utawala wa namna hiyo usio na hadhi na iwapo tutakuwa pamoja na Allah na kufanya mambo yetu yote kwa ajili ya kutafuta radhi Zake tu, bila ya shaka yoyote Mwenyezi Mungu atakuwa pamoja nasi na atatusaidia.
"Kulinda na kutia nguvu umoja na mshikamano wa kitaifa" iwe ni mshikamano wa kidini na kimadhebu au mshikamano wa kaumu na makabila mbali mbali nchini, ni jukumu jingine ambalo Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei amewabainishia viongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Ameutaja wajibu wa kuzingatia utamaduni wa kidini na kimapinduzi kuwa moja ya majukumu hatari waliyo nayo viongozi wa Jamhuri ya Kiislamu na huku akiashiria namna wajumbe wa Baraza la Wanazuoni Wataalamu walivyo na wasi wasi kuhusu masuala ya kiutamaduni nchini amesisitiza kwamba: Mimi pia nina wasi wasi na masuala ya utamaduni na niko pamoja na waheshimiwa wajumbe wa Baraza la Wanazuoni Wataalamu katika wasi wasi huo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Serikali inapaswa kulizingatia mno suala hilo na kwamba maafisa wanaohusika na masuala ya utamaduni nao wanapaswa kuzingatia kila wanachokifanya kwani haiwezekani kunyamazia kimya masuala ya utamaduni.
Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa: Suala la utamaduni ni muhimu sana kwani msingi wa kusimama kidete na msingi wa harakati ya mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu umesimama juu ya kulinda utamaduni wa Kiislamu na kimapinduzi na kutia nguvu utamaduni uliosimama juu ya misingi ya imani thabiti ya kidini na kimapinduzi.
Amesema, kwa hakika watu wote wanapaswa kujua thamani ya kuwa na vijana walio imara katika imani ya kidini na kimapinduzi kwani ni vijana hao ndio ambao wanaokuwa mstari wa mbele kulinda dini, taifa na nchi yao.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu pia ameashiria ongezeko la vijana wenye imani thabiti ya kidini na kimapinduzi katika masuala ya utamaduni na katika nyuga nyinginezo na kusisitiza kuwa: Watu ambao wanawaangalia vijana hao kwa jicho baya na wanajaribu kuwatenga na kuwaweka pembeni wajue kuwa kufanya kwao hivyo si kwa faida wala manufaa ya Mapinduzi ya Kiislamu na nchi.
Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa: Tab'an ni wazi kuwa vijana hao wenye imani thabiti ya kidini na kimapinduzi, kamwe hawawezi kutengwa na kuwekwa pembeni.
Jukumu la mwisho ambalo Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amewaeleza viongozi wa mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ni wajibu wa kufanywa mambo muhimu nchini Iran kuwa mjadala na mazungumzo ya watu wote.
Ayatullah Udhma Khamenei amesema: Inabidi kuhakikisha kwamba masuala yaliyozungumzwa yanakuwa mjadala na mazungumzo ya watu wote nchini na iwe ndiyo imani ya wote na kwamba ili jambo hilo liwezekane na litimie inabidi mambo hayo wabainishiwe vizuri wananchi kimantiki na kiutaalamu na kujiepusha na kuongeza chumvi kwa namna yoyote ile na yabainishwe kwa lugha nzuri iliyojaa mvuto.
Mwanzoni mwa mkutano huo, Ayatullah Mahdavi Kani, Mkuu wa Baraza la Wanazuoni Wataalamu wanaomchagua na kusimamia kazi za Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria kufanyika kwa muda wa siku mbili kikao cha kumi na tano cha baraza hilo na kutoa shukrani zake kutokana na kushiriki karibu wajumbe wote wa baraza hilo kwenye kikao hicho cha siku mbili kama ambavyo amezungumzia pia kwa muhtasari masuala yaliyojadiliwa kwenye kikao hicho.
Naye Ayatullah Yazdi, Naibu wa Mkuu wa Baraza la Wanazuoni Wataalamu ametoa ripoti fupi kuhusu kikao hicho cha siku mbili cha baraza hilo.
Kuchunguza na kujadili mchakato wa mazungumzo ya nyuklia (kati ya Iran na kundi la 5+1) na kusisitiza juu ya wajibu wa kulindwa na kuhifadhiwa haki za nyuklia za Iran, kubainishwa masuala ya kiuchumi na ulazima wa kuzingatiwa mfumo wa benki usio na riba, sisitizo juu ya umuhimu wa kutekelezwa kivitendo siasa na sera za uchumi wa kimuqawama na wa kusimama kidete na kujiepusha na kuleweshwa na nara na kaulimbiu tu bila vitendo kuhusu suala hilo, kuisaidia na kuiunga mkono Serikali na wasi wasi wa wajumbe wa baraza hilo kuhusiana na masuala ya utamaduni ni miongoni mwa nukta ambazo Naibu wa Mkuu wa Baraza la Wanazuoni Wataalamu ameziashiria katika ripoti yake hiyo zikiwa ndizo mada kuu zilizokuwemo kwenye mijadala, matamshi na mazungumzo ya wajumbe wa baraza hilo katika kikao chao hicho cha siku mbili.
 
< Nyuma   Mbele >

^