Skip to content

Habari

Habari
Hifadhi

Risala na Barua

Matini
Hifadhi

Kumbukumbu na Simulizi

Kabla ya Mapinduzi
Baada ya Mapinduzi

Sauti na Taswira

Picha
Sauti
Video
Kikao cha Kubainisha Siasa za Uchumi wa Kusimama Kidete Chapa
11/03/2014
 Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, leo asubuhi (Jumanne) amebainisha muundo wa siasa za uchumi wa kimuqawama na wa kusimama kidete mbele ya mjumuiko ya mamia ya wakuu na maafisa wa vyombo mbali mbali, wanaharakati wa masuala ya kiuchumi, wakuu wa vituo vya kielimu, vyombo vya habari na taasisi za usimamizi. Amesema kuwa kuna kila sababu, nia na misukumo ya kweli iliyowafanya viongozi na maafisa husika waamue kutunga siasa hizo na mambo yake ya lazima na matumaini yaliyowekewa siasa hizo. Amesisitiza pia kuwa, nia ya kweli ya viongozi, kubadilika siasa hizo kuwa ratiba zenye muda maalumu wa kutekelezwa, usimamiaji wa kina, kuondoa vizuizi vinavyowakwamisha wanaharakati na wananchi kuingia katika medani ya uchumi, kufanywa suala hilo kuwa mjadala na mazungumzo ya watu wote nchini ni mambo ambayo yanatoa fursa ya kupatikana matunda matamu na ya wazi ya kigezo hicho cha kienyeji na kielimu katika wakati unaofaa kwenye maisha ya kila siku ya watu.
Mwanzoni mwa hotuba yake, Ayatullah Udhma Kkhamenei amelitaja lengo la kuitishwa kikao chenye muundo kama huo wa viongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni kuleta mazingira ya kufanya kazi kwa pamoja na kushirikiana kifikra katika utekelezaji wa siasa kuu za uchumi wa kusimama kidete, kutia kasi maendeleo ya Iran na kuchukua hatua muhimu katika jitihada za kufanikisha malengo makuu na matukufu ya mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu.
Aidha ameashiria suala la kuwasilishwa na kukabidhiwa siasa mbali mbali na za kila namna katika miaka ya huko nyuma na kukumbusha kuwa: Lengo la kuwasilishwa na kukabidhiwa siasa hizo lilikuwa ni kuonesha mwongozo na ramani ya njia katika kila sekta lakini kuhusu kadhia ya siasa kuu za uchumi wa kimuqawama, lengo la kuwasilishwa kwake si kuonesha muongozo na ramani ya njia tu, bali ni kuonesha pia vigezo na vielelezo sahihi vinavyotakiwa kwa ajili ya kuvitumia katika njia ya ufanikishaji wa siasa hizo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza pia kuwa: Majimui ya siasa kuu za uchumi wa kusimama kidete kwa hakika ni kigezo cha ndani ya nchi, cha jadi, cha kienyeji na cha kielimu ambacho ni matunda ya utamaduni wa kimapinduzi na Kiislamu ambao unakubaliana vizuri na hali ya hivi sasa na ya siku za usoni ya Iran.
Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa: Siasa za uchumi wa kimuqawama hazihusiana tu na hali ya hivi sasa bali ni tadibiri na ni mipango ya muda mrefu kwa ajili ya uchumi wa Iran kwa nia ya kufikia kwenye malengo makuu ya kiuchumi ya mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu.
Aidha ameashiria nguvu na uwezo mkubwa wa siasa kuu za uchumi wa kusimama kidete na kuongeza kwamba: Siasa hizo zina uwezo wa kujikamilisha na kuoana na mazingira mbali mbali na kimsingi zitaufanya uchumi wa Iran uwe na hali ya kukubaliana na mazingira ya aina yoyote ile na kuondoa matatizo ya kiuchumi katika nyakati na mazingira tofauti.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa, sifa moja nyingine muhimu na ya kipekee ya siasa kuu za uchumi wa kusimama kidete ni mwafaka na makubaliano yaliyopo kati ya mihimili yote mikuu ya dola, (Serikali, Bunge na Mahakama) na taasisi nyinginezo nchini kuhusiana na siasa hizo, kwani kigezo hicho kimetungwa na kupasishwa kwa juhudi za pamoja na fikra zinazofanana za wasomi na wanafikra na kujadiliwa pia ndani ya Halmashauri ya Kuainisha Maslahi ya Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ambayo wakuu wa mihimili mitatu mikuu ya dola ni wajumbe ndani yake.
Ayatullah Udhma Khamenei amezitaja siasa kuu za uchumi wa kusimama kidete kuwa ni mkusanyiko makini kikamilifu na madhubuti kabisa na kuongeza kuwa, fikra ya kuwa na uchumi wa kimuqawama si jambo linaloihusu nchi ya Iran pekee, kwani katika miaka ya hivi karibuni na kutokana na kuzuka mgogoro wa kiuchumi duniani, nchi nyingine ulimwenguni nazo zimekuwa zikifanya jitihada za kutia nguvu na kusimamisha kidete uchumi wao kwa kutegemea muundo wa ndani wa nchi hizo.
Aidha amesema kwa kusisitiza kwamba: Tab'an nchi yetu inahitajia zaidi kuwa na uchumi wa kusimama kidete na wa kimuqawama kuliko nchi nyingine kwani kwa upande mmoja, nchi yetu kama zilivyo nchi nyingine zenye mfungamano na uchumi wa dunia na zenye nia ya kulinda na kudumisha uhusiano huo bila ya shaka yoyote itaathiriwa na masuala ya uchumi wa dunia na kwa upande wa pili mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu kutokana na kupigania kwake uhuru, heshima, kujitegemea na kusisitiza kwake kwamba haiko tayari kubebeshwa siasa za madola ya kibeberu duniani, inashambuliwa kutoka kila upande na maadui wenye nia mbaya na wanaotaka kuvuruga mambo ya Iran.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu vile vile amesema: Kwa mujibu wa misingi hiyo, na kwa mujibu wa hoja za kimantiki, tuna wajibu wa kuifanya misingi ya uchumi wa nchi yetu kuwa imara na isiyotetereka na tusiruhusu matukio na mitikisiko isiyoepukika na pia nia mbaya za madola ya kibeberu yanayofanya njama za kutuvuruga; ziathiri vibaya na kukwamisha maendeleo yetu ya kiuchumi.
Ayatullah Udhma Khamenei, baada ya kubainisha nafasi na umuhimu wa siasa kuu za uchumi wa kusimama kidete na vile vile hoja na usuli za kimantiki za kuimarisha misingi ya uchumi wa Iran, amebainisha pia sifa maalumu na vipengee kumi vilivyomo kpwenye uchumi wa kusimama kidete.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuhusu suala hilo kwamba: Vielelezo mbali mbali kama vile ustawi wa kiuchumi, uzalishaji wa ndani, uadilifu wa kijamii, nafasi za kazi, mfumuko wa bei na ustawi wa kijamii, ni mambo ambayo yatakuwa bora na kupelekea kushuhudiwa ustawi wa kiuchumi iwapo kutatekelezwa siasa kuu za uchumi wa kusimama kidete.
Aidha Ayatullah Udhma Khamenei amekumbushia nukta moja muhimu kuhusu kipengee hicho akisisitiza kuwa, uadilifu wa kijamii, ni kielelezo muhimu zaidi kati ya vielelezo vyote hivyo kwani mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu haukubaliani kabisa na ustawi wa kiuchumi usio na uadilifu wa kijamii na kwamba maendeleo yoyote yale ya kiuchumi ya Iran inabidi yayasaidie na yayanyanyue matabaka maskini kwa maana halisi ya neno.
Aidha ameutaja uwezo wa kusimama kidete mbele ya mambo yanayozusha vitisho kuwa ni sifa nyingine ya pili ya kipekee ya siasa kuu za uchumi wa kimuqawama na kuongeza kuwa: Mitikisiko ya kiuchumi duniani, mabalaa ya kimaumbile na mitikisiko itokanayo na chuki na uhasama kama vile vikwazo, ni miongoni mwa mambo yanayozaa vitisho.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amebainisha kipengee cha tatu cha siasa kuu za uchumi wa kusimama kidete kuwa ni uwezo wa ndani ya taifa na kuongeza kwamba: Uwezo huo mwingi unajumuisha pia uwezo mkubwa wa kielimu, kibinadamu, kimaumbile, kifedha, kijiografia na kieneo ambapo inabidi itegemewe katika utekelezaji wa siasa hizo.
Ayatullah Udhma Khamenei pia ameashiria nukta nyingine muhimu akisema: Kutegemea uwezo mkubwa wa ndani hakuna maana ya kudharau na kufumbia macho suhula na uwezo wa nchi nyingine duniani, bali mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu sambamba na kutegemea suhula za ndani utatumia pia suhula na uwezo wa nchi nyingine duniani kadiri inavyowezekana.
Aidha ameendelea na hotuba yake kwa kubainisha kipengee cha nne kwa kugusia fikra ya kijihadi na kuongeza kuwa: Utekelezaji wa siasa hizo hauwezekani kwa harakati za kawaida tena ambazo baadhi ya wakati zinakuwa za ulegevu na kusinzia sinzia bila ya kuwa na hisia kali zinazotakiwa, bali utekelezaji wa siasa hizo unahitajia harakati ya kielimu, hima na uendeshaji wa kijihadi wa mambo.
Kuwapa kipaumbele kikuu wananchi ni kipengee cha tano ambacho Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei amekiashiria katika hotuba yake hiyo na kusema: Kwa mujibu wa mafundisho ya Kiislamu na kidini na vile vile kwa mujibu wa tajiriba na uzoefu wa miaka 35 iliyopita, katika medani yoyote ambayo wananchi wanaingia ndani yake hufuatana na rehema na msaada wa Mwenyezi Mungu na kufanikisha mambo.
Amekumbusha kuwa: Hadi hivi sasa wananchi na suhula zilizopo zimetumiwa kidogo katika nyuga za kiuchumi, na wananchi hawajapewa fursa na nafasi inayotakiwa, wakati ambapo inabidi kubuniwe uwanja wa kutumiwa vizuri uwezo na nguvu zisizo na kikomo za wananchi, iwe wananchi hao ni wanaharakati wa kiuchumi au wajasiriamali, au wabunifu, au wawekezaji na watu wenye utaalamu wa fani mbali mbali na waungwe mkono watu hao na kwamba jukumu kuu la kufanya hivyo liko mabegani mwa Serikali.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amelitaja lengo la kukabidhiwa na kuwasilishwa siasa kuu za kifungu cha 44 cha Katiba ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran miaka michache iliyopita kuwa ni kutumia uwezo na suhula za wananchi katika uchumi wa nchi na kusema kuwa, inasikitisha kuona kuwa siasa hizo hazikupewa haki yake.
Ayatullah Udhma Khamenei vile vile amelitaja suala la kudhaminiwa bidhaa za kiistratijia na za kimsingi hususan chakula na madawa na kujitosheleza katika bidhaa hizo kuwa ni kipengee cha sita cha uchuni wa kusimama kidete na kuhusu kipengee cha saba amesema: Kupunguza kutegemea fedha zitokanazo na kuuza mafuta ni moja ya sifa kuu za siasa hizo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amelitaja suala la kurekebishwa kigezo cha matumizi kuwa ni kipengee cha nane cha siasa kuu za uchumi wa kusimama kidete na kuongeza kwa kusema: Ninaowalenga zaidi mimi katika mazungumzo yangu hapa kuhusu suala hili ni viongozi ambapo wao wanapaswa kuwa mstari wa mbele katika kujiepusha na israfu na ufujaji wa mali ya umma wanapokuwa wametumwa kufanya kazi fulani katika hatua ya kwanza na katika hatua ya pili, wao wenyewe pia wanapaswa katika maisha yao binafsi ya kila siku kuchunga vilivyo jambo hilo.
Ayatullah Udhma Khamenei amesisitizia wajibu wa viongozi kushikamana na suala la kujiepusha na israfu kwani iwapo viongozi nchini watalipa uzito wa hali ya juu suala la kujiepusha na israfu na kufuja mali, basi utamaduni huo utaenea kwa watu katika jamii na kuongeza kuwa, makusudio ya kurekebisha kigezo cha matumizi, si kuleta tabu na wala kuwabana watu bali lengo lake ni kutumia vitu kulingana na kigezo cha kimantiki, kilichopangiliwa vizuri, kigezo sahihi cha matumizi kinachokubaliwa na dini tukufu ya Kiislamu.
Vile vile amezungumzia namna baadhi ya watu wanavyoufananisha uchumi wa kusimama kidete na baadhi ya mifumo mingine ya uchumi na kusema, tofauti kabisa na mifumo hiyo ya kiuchumi, uchumi wa kimuqawama na wa kusimama kidete utapelekea kustawi maisha ya watu wote hususan watu wa matabaka dhaifu.
Kupambana na ufisadi ni kipengee cha tisa kilichoashiriwa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kuhusu siasa kuu za uchumi wa kusimama kidete na kusisitiza kwamba, usalama ni jambo la lazima katika kufanya jitihada na amali salama zilizojaa harakati na kwamba kupambana na wafanya ufisadi wa kiuchumi na watu wanaokwepa kutekeleza sheria ni jambo la lazima katika kudhamini usalama wa kiuchumi.
Ayatullah Udhma Khamenei amelitaja suala la kuweka wazi mambo kuwa ni sharti kuu la kupambana na ufisadi wa kiuchumi na kuongeza kuwa, inabidi kuandaliwe mazingira ya kujitokeza anga ya ushindani wa kudumu wa kiuchumi kwani ni katika anga hiyo salama, ndipo mwanaharakati wa masuala kiuchumi atakapohisi kuwa na usalama sambamba na kwamba ni katika mazingira kama hayo ndipo panapopatikana utafutaji sahihi wa utajiri kwa kutumia ubunifu na uchapa kazi unaokubaliwa na mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu.
Vile vile ameashiria jinsi wakuu wa mihimili mitatu mikuu ya dola walivyotangaza kuweko kwao tayari kupambana vilivyo na ufisadi wa kiuchumi na kusisitiza kuwa: Katika suala hilo haitoshi kusema kwa maneno na kutangaza msimamo tu, bali maafisa wote wa mihimili hiyo mitatu, Serikali, Bunge na Mahakama wana jukumu la kutekeleza kivitendo vipengee vyote vya suala hilo.
Kufanywa elimu kuwa mhimili ni kipengee cha kumi na cha mwisho kilichoashiriwa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika kubainisha siasa kuu za uchumi wa kusimama kidete.
Amesema, leo hii hali ya Iran katika upande wa maendeleo ya kielimu iko kwa namna ambavyo, tunaweza kuwa na matumaini makubwa sana ya kulifanya kuwa katika malengo yetu suala la kuwa na uchumi uliosimama juu ya elimu za kimsingi.
Ayatullah Udhma Khamenei amefafanua zaidi suala hilo akisema, uchumi unaotegemea elimu za kimsingi ni miongoni mwa miundombinu muhimu mno ya kiuchumi kwa kila nchi na iwapo suala hilo litapewa uzito unaotakiwa, basi bila ya shaka yoyote mchakato wa kuibadilisha elimu kuwa chanzo cha utajiri, utakamilika.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameianza sehemu ya pili ya hotuba yake hiyo kwa kuiuliza jamii swali lifuatalo: Je, siasa za uchumi wa kusimama kidete ni za muda mfupi ambazo zimetungwa kutokana na mashinikizo iliyowekewa Iran? Jibu la wazi na lisilotetereka la Kiongozi Muadhamu kwa swali hilo ni kamwe na hapana si hivyo.
Amesisitiza kuwa, uchumi wa kimuqawama na wa kusimama kidete kamwe si siasa za muda mfupi bali ni mkakati na ni tadibiri ya kiistrajitia ambayo ni muhimu wakati wote iwe ni wakati wa vikwazo au wakati visipokuwepo vikwazo. Siasa hizo ni mwongozo muhimu wa kuonyesha njia sahihi ya kufanikisha mambo.
Ayatullah Udhma Khamenei ametoa ufafanuzi kuhusu sababu na shabaha za kuwasilishwa siasa za uchumi wa kusimama kidete kwa kutaja sababu nne kuu akisema: Uwezo mkubwa na mwingi wa kimaada na kimaanawi wa Iran, kutatua matatizo sugu na ya muda mrefu wa kiuchumi, kupambana na vikwazo na kupunguza kikamilifu kuathiriwa uchumi wa nchi na migogoro ya kiuchumi ni katika sababu zilizopelekea kubuniwa na kuwasilishwa siasa hizo.
Amma kuhusu nukta hiyo ya kwanza amesema: Uwezo mkubwa wa nguvu kazi, utajiri wa mali asili kama vile madini, utajiri wa kimaumbile na viwanda, na vile vile kuwepo Iran katika eneo bora kabisa la kijiografia ulikuwa msukumo mkuu uliopelekea kubuniwa kigezo hicho muhimu sana cha kiuchumi yaani uchumi wa kusimama kidete.
Ayatullah Udhma Khamenei ametoa ufafanuzi kuhusu msukumo na shabaha ya pili ya kutungwa na kuwasilishwa siasa kuu za uchumi wa kusimama kidete kuwa ni kuzingatia udharura wa kutatuliwa matatizo yaliyopo ya kiuchumi.
Ameongeza kuwa, matatizo sugu na ya muda mrefu ya kiuchumi kama vile mfumuko wa bei, ukosefu wa kazi, kutegemea pato litokanalo na kuuza mafuta, kuingiza bidhaa nchini kutoka nje bila ya mpangilio, kuwa na matatizo baadhi ya miundo ya kiuchumi, kuwa chini kiwango cha matumizi mazuri ya na kigezo kisicho sahihi cha matumizi ni mambo ambayo ni muhali kuweza kupambana nayo bila ya kuwa na mkakati uliopangiliwa vizuri sana wa kuuimarisha na kuuwekea misingi imara uchumi wa nchi.
Kiongozi Muadhamu ameutaja udharura wa kukabiliana vilivyo na vita vya pande zote vya kiuchumi vya maadui, kuwa ni jambo jingine lililopelekea kubuniwa na kuwasilishwa siasa za uchumi wa kimuqawama na kuongeza kwamba: Vikwazo dhidi ya Iran vilikuwepo hata kabla ya kuzuka suala la nishati ya nyuklia na hata kama mazungumzo Inshaallah yatafikia natija ya kutatuliwa suala hilo, vikwazo hivyo havitaondoka, vitaendelea kuwepo kwani suala la nishati ya nyuklia, haki za binadamu na masuala mengineyo yanatumiwa kama kisingizio tu na mabeberu wa dunia ambao wanaiogopa misimamo ya Iran ya kupigania ukombozi na kugeuka taifa hili kuwa kigezo kizuri kwa mataifa mengine.
Ameongeza kuwa, kama tunataka kupambana vilivyo na mashinikizo ya kiuchumi ya maadui, tunapaswa kuutia nguvu na kuuimarisha uchumi wetu kwa namna ambayo maadui watakata tamaa katika njama zao za kuharibu uchumi wetu na kwamba lengo hilo linaweza kufikiwa kwa kutekelezwa siasa zilizowasilishwa za uchumi wa kusimama kidete.
Ayatullah Udhma Khamenei ametaja sababu ya tatu iliyopelekea kubuniwa siasa za uchumi wa kusimama kidete nchini Iran kuwa ni udharura wa kupunguzwa kuathirika uchumi wa nchi kutokana na migogoro ya kimataifa na kuongeza kuwa, sababu hizo nne zimepelekea suala la kubuni na kutunga kigezo cha uchumi wa kusimama kidete kuwa ajenda ya mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu.
Sehemu ya tatu ya hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu mbele ya mamia ya viongozi na maafisa wa mihimili mitatu mikuu ya dola, na mbele ya wanaharakati wa kiuchumi, kijamii na vyombo vya habari, imehusiana na kubainisha mambo ya lazima na matarajio yaliyopo.
Ameitaja nia ya kweli na isiyotetereka ya viongozi nchini hususan wale wa mihimili mitatu mikuu ya dola na hasa hasa serikali kuwa sababu muhimu mno ya jitihada hizo kubwa za kuimarisha uchumi na kuongeza kuwa, kutolewa tu siasa hizo za uchumi wa kimuqawama na wa kusimama kidete hakuwezi kutatua jambo lolote, bali nia na jitihada za viongozi na maafisa wa sekta zote husika katika utekelezaji wa kivitendo wa siasa hizo ndiko kutakakofanikisha malengo yaliyokusudiwa.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amelitaja suala la kuingia kwenye medani ya vitendo kuwa ni mategemeo na matarajio yake ya pili kutoka kwa viongozi nchini na kusisitiza kuwa, mpango na siasa hizo kuu inabidi zitekelezwe kwa kutumia mipango na ratiba mbali mbali za utekelezaji ili kwa njia hiyo iwezekane kushuhudiwa hamasa ya kweli ya kiuchumi.
Ayatullah Udhma Khamenei ameashiria hatua ya kutangazwa mwaka huu (wa Kiirani wa 1392 Hijria Shamsia) kuwa mwaka wa Hamasa ya Kisiasa na Hamasa ya Kiuchumi na kuongeza kuwa: Kwa bahati nzuri hamasa ya kisiasa imefanikishwa lakini inasikitisha kuona kuwa hamasa ya kiuchumi imechelewa kutokea na ni matumaini yangu kuwa jambo hilo litafuatiliwa kwa uzito mkubwa katika mwaka ujao wa 1393 (Hijria Shamsia) chini ya kivuli cha siasa zilizowasilishwa za uchumi wa kusimama kidete.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amelitaja suala la kutungwa mipango ya utekelezaji yenye makataa maalumu kuwa ni jambo la tatu la dharura katika suala hilo na kusisitiza kuwa: Inabidi nafasi ya kila mhimili wa dola na vile vile nafasi ya kila asasi katika utekelezaji wa siasa za uchumi wa kusimama kidete ziainishwe wazi na kwa umakini na usahihi wa hali ya juu.
Ameongeza kuwa: Kuna ulazima wa kuandaliwa ratiba zilizo wazi za utekelezaji zenye vielelezo vya wakati maalumu ili kwa njia hiyo iwezekane kufuatilia vizuri na kwa karibu namna kazi inavyoendelea.
Kuchukua hatua za kivitendo wakuu wa mihimili mitatu mikuu ya dola (Serikali, Bunge na Mahakama) na kuandaa mipango ya kuweko uratibu wa pamoja kati ya asasi na vyombo husika pamoja na kusimamia na kuangalia kwa karibu utekelezaji wa kila hatua, ni mambo ya nne na tano ya dharura yaliyosisitizwa na Kiongozi Muadhamu.
Ameongeza kuwa: Halmashauri ya Kuainisha Maslahi ya Mfumo wa Jamhuri ya Kiisamu nayo ina wajibu wa kutekeleza kikamilifu jukumu ililopewa la usimamizi.
Kuondoa vizuizi vya kikanuni, vya kiutendaji na vya kisheria na mahakama katika juhudi za kutekeleza siasa hizo za uchumi wa kusimama kidete ni jukumu la sita ambalo Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema inabidi viongozi wa mihimili mitatu mikuu ya dola walitekeleze.
Vile vile amesisitiza kuwa, inabidi viondolewa vizuri vyote vinavyosumbua sumbua na kukwamisha mambo ili wanaharakati wa masuala ya kiuchumi, wajasiriamali, wabunifu, wasomi na wataalamu wa mambo waweze kuingia na kufanya kazi zao kwa utulivu ndani ya medani hiyo na wahisi kuwa hakuna vizuizi vyovyote visivyo vya lazima na visivyo vya kimantiki vinavyokwamisha kazi zao.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amelitaja suala la kugeuzwa kadhia ya uchumi wa kusimama kidete kuwa mjadala na mazungumzo ya watu wote na kutolewa taswira sahihi kuhusu uchumi wa aina hiyo kuwa ni jukumu la Shirika la Sauti na Televisheni la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran (IRIB), vyombo vingine vya habari, viongozi, watu wenye uchungu na nchi na wasomi na wanafikra na kuongeza kuwa, vyombo vya kipropaganda vinavyopiga vita maendeleo ya Iran vinafanya njama za kuingiza utata, kukatisha watu tamaa na kukwamisha mambo na kuonesha kuwa siasa hizo zilizowasilishwa za uchumi wa kusimama kidete hazina umuhimu wowote lakini kama itaoneshwa taswira halisi na sahihi kuhusiana na harakati hii kubwa, na kama kigezo hiki bora kitageuzwa kuwa mjadala na mazungumzo ya kila siku ya watu wote, basi wananchi wataliitakidi jambo hilo na watakuwa na imani thabiti na suala hilo na hatimaye watawataka viongozi nchini watekeleze kivitendo siasa hizo na kwa njia hiyo kazi zitafanyika vizuri na malengo yaliyokusudiwa yatafikiwa.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amebainisha matarajio yake ya mwisho kutoka kwa viongozi na maafisa husika kwa kuzungumzia suala la ufuatiliaji na kufikishiwa wananchi habari za suala hilo kwa njia sahihi na ya kina.
Ameongeza kuwa, inabidi kuweko kituo chenye nguvu na makini cha kuweza kufuatilia na kuangalia kwa kina kazi zinavyofanyika.
Kukusanya na kusambaza taarifa, kuzalisha na kuainisha vielelezo kwa ajili ya kila sekta na kuwafikishia wananchi taarifa zake ni miongoni mwa majukumu ambayo ameyaainisha kuhusu kituo hicho.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amemalizia hotua yake hiyo kwa maneno yafuatayo: Inshaallah kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu kazi kubwa iliyoanza kutekeleza, inaendelea kwa kasi nzuri na kwa kutawakali kwa Mwenyezi Mungu, na wananchi watapata matunda yake matamu katika serikali hii hii ya hivi sasa.
Mbali na Mawaziri na viongozi waandamizi wa asasi mbali mbali za utendaji na za kiserikali, mkutano huo umehudhuriwa pia na maafisa wa ngazi za juu wa Mahakama na Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran), wanaharakati wa masuala ya kiuchumi, vyama vya ushirika, wakuu wa taasisi na vituo mbali mbali vinavyoshughulikia masuala ya kiuchumi, taasisi za usimamiaji na za masuala ya kielimu, wakuu wa mikoa, wawakilishi wa Fakihi Mtawala (Waliyyul Faqih) mikoani, wakuu wa Hawza (Chuo Kikuu cha Kidini), wakuu na wakurugenzi wa Shirika la Sauti na Televisheni la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran (IRIB) na kutoka katika baadhi ya vyombo vingine vya habari, makamanda wa polisi na jeshi pamoja na wakuu wa miji.
 
< Nyuma   Mbele >

^