Skip to content

Habari

Habari
Hifadhi

Risala na Barua

Matini
Hifadhi

Kumbukumbu na Simulizi

Kabla ya Mapinduzi
Baada ya Mapinduzi

Sauti na Taswira

Picha
Sauti
Video
Kiongozi Muadhamu Aonana na Maafisa wa Misafara Inayotembelea Maeneo ya Vita vya Kujihami Kutakatifu Chapa
17/03/2014
 Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, leo asubuhi (Jumatatu) ameonana na viongozi na maafisa wa kambi za misafara inayotembelea maeneo vilipotokea vita vya miaka minane vya kujihami kutakatifu (vilivyoanzishwa na utawala wa zamani wa Iraq dhidi ya utawala mchanga wakati huo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran) na kusisitiza kuwa, ubunifu uliofanyika wa kutembelea maeneo ya operesheni za kijeshi za wakati wa vita vya kujihami kutakatifu, ni ubunifu unaomridhisha Mwenyezi Mungu na ni ubunifu wa kimapinduzi ambao ulistahiki kabisa kubuniwa kwa ajili ya kukielewesha kizazi chipukizi mambo mazuri ya tukio hilo kubwa la kihistoria la kujihami kutakatifu.
Ameongeza kuwa, kusahauliwa na kupotoshwa ukweli ni hatari mbili kubwa ambazo zinalinyemelea kila tukio kubwa la kihistoria na kwamba watu wenye vipaji, watu wenye ushawishi, watu wenye busara na maafisa wanaoshughulikia masuala ya tukio hilo kubwa la kujihami kutakatifu wana jukumu la kuwaelimisha watu kwa njia sahihi na ya kina mambo yanayohusiana na akiba na hazina hiyo kubwa ya kiutamaduni na wasiruhusu hamasa hiyo isahauliwe au ipotoshwe.
Ayatullah Udhma Khamenei pia ameashiria athari nyingi za uandishi na za sanaa zilizotolewa hadi hivi sasa kuhusiana na kadhia hiyo ya kujihami kutakatifu na kuongeza kuwa, vita vya kujihamu kutakatifu ni mithili ya bango kubwa lililotukuka ambapo kadiri mtazamaji anapokaribia kwenye asili ya tukio hilo na kuzama kwenye vipengee vyake, ndivyo anavyizidi kuona kina kikubwa zaidi na cha kustaajabisha zaidi cha tukio hilo.
Ameongeza kuwa, msingi wa usia wa Imam Khomeini (quddisa sirruh) kwa wananchi na viongozi wote nchini kuhusu udharura wa kuzisoma kwa kina barua na nasaha za mashujaa wa vita vya kujihami kutakatifu unatokana na jambo hilo hilo na ameongeza kuwa: Nasaha zilizotolewa na mashahidi hao ni mlango wa kufahamu hali ya kimaanawi iliyokuwa imetawala katika dhati za wanamapambano hao wa Kiislamu hali ambayo iliwawezesha kufanya mambo makubwa na kupata ushindi katika medani ambazo kwa kama kutatumika mahesabu ya kawaida ya kimaada na kijeshi yaliyozoeleka duniani, basi itaonekana kuwa mambo hayo yasingeliwezekana kabisa.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameendelea kutoa ufafanuzi kuhusu hatari mbili kubwa zinazolikabili kila tukio kubwa duniani kwa kuashiria hatari ya kusahauliwa tukio kubwa kutokana na kutojikariri na kutotokea tena mambo yaliyolifanya tukio hilo liwe kubwa.
Katika ufafanuzi wake wa suala hilo, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria kadhia ya Palestina na kusema kuwa, hivi sasa mfumo wa kiistikbari na kibeberu duniani unafanya njama kwa kutumia mbinu hiyo hiyo ili kulisahaulishwa na kufifiliza pole pole umuhimu wa tukio kubwa na zito kama hilo la kuwafukuza wenyeji wa Palestina kwenye miji na vijiji vya nchi yao.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza pia kuwa, kadhia ya Palestina imebakia hai na haikusahauliwa katika kipindi cha miaka yote hii licha ya kuweko njama za kila namna za kambi ya mabeberu, kutokana na jitihada za Mapinduzi ya Kiislamu na sauti ya juu iliyotolewa kwa ikhlasi kamili na Imam Khomeini (quddisa sirruh) ya kulitetea taifa la Palestina. Ameongeza kuwa: Haipasi kuruhusu kusahauliwa tukio adhimu la vita vya kujihami kutakatifu.
Aidha Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, kupotoshwa na kubadilishwa muundo halisi wa tukio ni hatari ya pili inayoyakabili matukio makubwa.
Ayatullah Udhma Khamenei ameitaja asili ya Mapinduzi ya Kiislamu na kujihami kutakatifu kuwa nayo inakabiliwa na hatari ya kupotoshwa na kubadilishwa uhalisia wake.
Ameongeza kuwa: Hakuna maana kwa baadhi ya watu kuona kuwa athari za kiutamaduni na kisanii zinazotengenezwa kuhusu suala la kujihami kutakatifu au makongamano yanayofanyika kuzungumzia tukio hilo muhimu, kwamba ni mambo yanayokinzana na muundo na uhalisia wa harakati hiyo adhimu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aidha amezitaja kambi za misafara inayokwenda kutembelea maeneo zilikofanyika operesheni za kijeshi za wakati wa vita vya kujihami kutakatifu kuwa ni sunna nzuri yenye shabaha ya kuzuia hatari mbili za kusahaulishwa na kupotoshwa jambo hilo zisilifikie tukio hilo adhimu na wakati huo huo ametahadharisha kuwa, inabidi jitihada zifanyike kuhakikisha kuwa baadhi ya matukio yanayotokea kwenye kambi hizo hayatokei tena na pia matukio hayo yasifanywe sababu ya kuitilia shaka na kuiweka chini ya alama ya kuuliza harakati hiyo kubwa yenye faida nyingi.
Amefafanua zaidi kwa kusema: Nukta kuu na ya asili katika kambi hizo za misafara ya kutembelea maeneo vilipotokea vita vya miaka minane vya kujihami kutakatifu ni kuandaa uwanja wa kufanyika ziara za kujifunza mambo mengi kutokana na operesheni zilizofanyika kwenye vita hivyo.
Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa: Moja ya njia za kuandaa uwanja wa kufanyika ziara za kuongeza elimu na maarifa ni kuzalishwa vijitabu vya kutambulisha maeneo ya vita na operesheni za kujihami kutakatifu na kuongeza kuwa: Kuna vitabu vizuri sana vimeandikwa hadi hivi sasa kuhusu vita vya kujihami kutakatifu na vitabu hivyo vina uwezo wa kubadilishwa kuwa filamu zenye mvuto mkubwa (na zenye watazamaji wengi) kama ambavyo pia maeneo yote kulikopiganwa vita hivyo na kila operesheni ya vita vya kujihami kutakatifu inaweza kuwa marejeo mazuri ya kuzalishia athari za maana na zenye faida kubwa.
Udharura wa kuyafanya kuwa amilifu wakati wote majimui na vikundi mbali mbali vya watu, kuendelea kuandaliwa safari za pamoja za watu wengi na kuteuliwa watu weledi wa mambo wa kutoa ufafanuzi na kuhadhithia matukio hayo ambao walikuwepo na waliyashuhudia kwa karibu matukio ya siku nyeti na muhimu mno za kipindi cha vita vya kujihami kutakatifu, ni miongoni mwa nasaha nyingine zilizotolewa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa maafisa na wasimamiaji wa kambi za misafara ya kutembelea maeneo zilikofanyika operesheni za vita vya kujihami kutakatifu vilivyoanzishwa na utawala wa zamani wa Iraq dhidi ya utawala wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambao wakati huo ulikuwa ndio kwanza umeasisiwa.
Mwanzoni mwa mkutano huo, Kamanda Karegar, mkuu wa kamati kuu ya misafara ya kutembelea maeneo ya vita vya kujihami kutakatifu ametoa ripoti fupi kuhusiana na kazi, hatua zilizochukuliwa na ratiba za kamati yake hiyo.
 
< Nyuma   Mbele >

^