Skip to content

Habari

Habari
Hifadhi

Risala na Barua

Matini
Hifadhi

Kumbukumbu na Simulizi

Kabla ya Mapinduzi
Baada ya Mapinduzi

Sauti na Taswira

Picha
Sauti
Video
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ahutubia Mamilioni ya Watu katika Haram ya Imam Ridha AS Chapa
21/03/2014
Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu leo asubuhi (Ijumaa) ambayo imesadifiana na siku ya kwanza ya msimu wa machipuo na siku ya awali kabisa ya mwaka mpya wa Kiirani wa 1393 Hijria Shamsia ametoa hotuba muhimu sana mbele ya hadhara na mjumuiko mkubwa na uliojaa hamasa na shauku wa wafanya ziara na majirani wa Haram toharifu ya Imam Ridha AS mjini Mash'had, kaskazini mashariki mwa Iran. Sambamba na kutoa tena mkono wa baraka kwa mnasaba wa kuwadia mwaka mpya amebainisha pia vipengee tofauti vya ramani kuu ya njia kwa ajili ya Iran katika mwaka huu mpya yaani kaulimbiuo ya "Uchumi na Utamaduni wenye Azma ya Kitaifa na Uongozi wa Kijihadi." Aidha ametoa ufafanuzi kuhusu muundo, uwezo na mambo ya lazima ya kuweza kufanikisha uimarishaji wa uchumi na mambo ya wajibu yanayotakiwa na yasiyo ya wajibu yasiyotakiwa katika masuala ya utamaduni na kusisitiza kuwa: Tunapaswa kujiimarisha kwa namna ambayo mabeberu na waistikbari duniani hawataweza kudharau haki yoyote ile ya taifa hili.
Ayatullah Udhma Khamenei ametoa ufafanuzi kuhusu msimamo wake katika mwaka huu mpya yaani udharura wa kuwa imara na kuwa na nguvu zaidi taifa la Iran na nchi ya Iran na kuongezwa uwezo wa kitaifa, na ameashiria pia njama zinazofanywa na waistikbari na mabeberu wa dunia za kutaka kuyapora mataifa dhaifu haki zao na kuongeza kuwa: Maumbile ya dunia ambayo inaongozwa kwa fikra za kimaada ni kushuhudiwa ndani yake ubeberu na ukandamizaji wa madola yenye nguvu dhidi ya wanyonge, hivyo inabidi tuwe na nguvu na tuwe na maendeleo makubwa ili tuweze kukabiliana vizuri na hali hiyo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametoa ufafanuzi pia kuhusu sababu za kupewa mwaka huu mpya jina la "Uchumi na Utamaduni wenye Azma ya Kitaifa na Uongozi wa Kijihadi" ikiwa ndio muongozo na ramani ya njia kwa ajili ya mwaka huu wa 1393 (Hijria Shamsia) na pia ameashiria hatua kubwa na uzoefu wa hali ya juu wa taifa la Iran na suhula na uwezo mwingi uliomo nchini na kuongeza kuwa: Njia iliyojaa fakhari ya "Uwezo wa Kitaifa" itakwenda kwa haraka na kwa kasi kubwa zaidi iwapo viongozi na wananchi watakuwa makini katika utekelezaji wa kaulimbiu hiyo.
Vile vile amebainisha mambo makuu yanayolifanya taifa kuwa na nguvu na uwezo wa hali ya juu kwa kusema kwamba, kuwa na silaha za kisasa ni jambo la lazima, lakini hata hivyo ameongeza kuwa: Uchumi, utamaduni na elimu ni mambo makuu na muhimu sana ambayo yanalifanya taifa kuwa na nguvu ambapo kwa msaada wa Mwenyezi Mungu, katika kipindi cha miaka 12 iliyopita, Iran imeng'ara na imepiga hatua kubwa na nzuri sana katika upande wa elimu na maarifa.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu vile vile ameyataja masuala mengine mawili ya kulifanya taifa kuwa na nguvu, yaani uchumi na utamaduni kuwa ni mambo ya dharura na ya lazima ambapo katika sehemu ya kwanza ya hotuba yake amezingatia zaidi suala la uchumi akisema: Inabidi uchumi wa Iran uwe imara na uwe madhubuti na wenye nguvu kwa namna ambayo mtikisiko wa aina yoyote ile duniani au mtu yeyote yule katika sehemu yoyote ile awe Mmarekani au asiwe Mmarekani, asiweze kwa kuchukua uamuzi fulani au kufanya kikao na harakati fulani kuuathiri uchumi wa nchi na maisha ya watu wetu na huo ndio huo uchumi wa kimuqawama na wa kusimama kidete tunaouzungumzia.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria pia kuwasilishwa na kukabidhiwa siasa za uchumi wa kusimama kidete na namna siasa hizo zilivyopokewa vizuri na wakuu wa Mihimili Mitatu Mikuu ya dola la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran (Serikali, Bunge na Mahakama) na viongozi wengine nchni na hapo hapo akaauliza maswali matatu muhimu na baadaye ameanza kuyajibu maswali hayo moja baada ya jingine. Maswahili hayo ni:
1 - Sifa hasi na chanya za uchumi wa kusimama kidete ni zipi?
2 - Je, lengo hilo linafanikishika au ni matumani na ndoto tu zisizotimia?
3 - Kama linafanikishika, mambo yake ya lazima ni yepi?
Akijibu swali la kwanza yaani sifa za "uchumi wa kimuqawama na wa kusimama kidete" amesema: Uchumi wa kusimama kidete ni kigezo cha kielimu kinachokubaliana na mahitaji ya nchi na ambacho tab'an nchi nyingi duniani zimeamua kuwa na uchumi wa aina hiyo unaokubaliana na mazingira maalumu ya nchi zao katika jitihada zao za kupunguza athari mbaya zinazozikumba chumi zao kutokana na mitikisiko ya kijamii na kiuchumi duniani.
Kutegemea uwezo wa ndani na kuegemea kwenye suhula na tani za ndani ya nchi sambamba na kufuatilia kwa karibu na kuamiliana kwa njia sahihi na chumi za nchi nyinginezo duniani, ni sifa ya pili malumu ya uchumi wa kusimama kidete kama alivyobainisha Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu.
Ameongeza kuwa: Inasikitisha kuona kuna baadhi ya waandishi na wazungumzaji wanafanya njama za kuzusha shaka na wasiwasi usio na msingi kama vile kudai kuwa uchumi huo utaufanya uchumi wa Iran ubanwe na uzingirwe na lengo lao ni kuwa kulifungia njia taifa la Iran katika jitihada zake za kuimarisha uchumi wake na kujiletea ustawi wakati ambapo uchumi wa kimuqawama na wa kusimama kidete ni uchumi wa kuamiliana vizuri na kwa njia sahihi na jamii ya kimataifa.
Ayatullah Udhma Khamenei amebainisha sifa ya tatu maalumu ya uchumi wa kimuqawama na wa kusimama kidete kwa kusema kuwa, uchumi huo si uchumi wa kiserikali bali ni uchumi wenye misingi ya wananchi. Tab'an viongozi wa nchi nao wana jukumu la kuandaa mazingira na kuongoza na kusaidia katika kuwafanya wananchi washiriki vilivyo kwenye uchumi huo na kuvutia uwekezaji wa wananchi.
Uchumi unaotokana na uzalishaji wa elimu za kimsingi sambamba na kustafidi vizuri na uzoefu na ustadi na utaalamu wa magwiji wa masuala ya viwanda na kilimo, ni ufafanuzi mwingine uliotolewa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika kuongeza welewa wa umma kuhusu sifa maalumu za uchumi wa kusimama kidete.
Wajibu wa kupewa umuhimu mkubwa uadilifu wa kiuchumi na kijamii sambamba na kuzingatiwa vielelezo maarufu vya kiuchumi duniani kama vile ustawi wa taifa, uzalishaji usio ghafi wa taifa na taathira nzuri za uchumi wa kusimama kidete katika mazingira na nyakati zote iwe ni wakati wa vikwazo au wakati usio na vikwazo, ni sifa ya mwisho maalumu ambayo Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameitaja katika kujibu swali la kwanza linalohusiana na sifa chanya na hasi za uchumi wa kusimama kidete.
Ayatullah Udhma Khampenei ameendeleza hotuba yake mbele ya mkusanyiko adhimu wa wafanya ziara na majirani wa Haram tukufu ya Imam Ridha AS kwa kujibu swali la pili ambalo linasema: Je, uchumi wa kimuqawama na wa kusimama kidete ni ndoto tu zisizo na ukweli wowote? Amejibu swali hilo kwa ufasaha kabisa na kwa kutegemea ushahidi wa taarifa zilizofanyiwa utafiti na uchunguzi wa kina.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema: Uwezo mkubwa wa nguvu kazi ikiwemo idadi kubwa sana ya vijana, wanafunzi milioni kumi waliohitimu masomo ya Vyuo Vikuu, zaidi ya wanafunzi milioni nne wanaoendelea na masomo katika Vyuo Vikuu na mamilioni ya nguvu kazi imara na yenye nguvu na uzoefu katika sekta za viwanda na zisizo za viwanda sambamba na maliasili nyingi za kimaumbile na zenye thamani kubwa sana, nafasi muhimu ya kijiografia na isiyo na kifani na miundombinu mbali mbali ya teknolojia za kisasa ni mambo ambayo yanaonesha kuwa hakuna shaka yoyote katika suala la kufanikishwa uchumi wa kimuqawama na wa kusimama kidete.
Ameongeza kuwa: Tab'an inawezekana mtu akasema kuwa mazingira ya vikwazo hayaruhusu kustafidi na suhula na uwezo huo mkubwa sana lakini swali linalojitokeza hapa ni kuwa kwani sisi hatukupata maendeleo ya kustaajabisha na ya kipekee ya kielimu na kiulinzi kama vile maendeleo ya tekonoloji za nano, nyuklia, seli shina, viwanda vya kiulinzi na makombora ya kisasa katika mazingira haya hayaya mashinikizo na vikwazo?
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza pia kuwa: Kwa kuzingatia uhakika huo tutaona kwamba kama tutakuwa na hima na azma ya kweli, na kama tutashirikiana vilivyo na kufanya kazi bega kwa bega na kutokusubiri kuondolewa vikwazo na maadui hasa kwa vile imethibiti kuwa kamwe maadui hawataacha uadui wao dhidi ya Iran, basi tutaweza katika nyuga nyinginezo pia zikiwemo za kiuchumi, kuwa na nguvu kubwa za kitaifa.
Mambo ya lazima na ya dharura ya kuweza kufanikisha uchumi wa kusimama kidete lilikuwa ni swali la tatu ambalo kutokana na umuhimu wake mkubwa, Ayatullah Udhma Khamenei ameaumua kuliingiza katika hotuba yake ya siku ya kwanza kabisa ya mwaka mpya (wa 1393 Hijria Shamsia).
Katika kujibu swali hiyo, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amezingatia zaidi mambo manne: 1 - Uungaji mkono wa pande zote wa viongozi nchini kwa uzalishaji wa ndani ikiwa ni sehemu muhimu na ya kimsingi ya maendeleo ya nchi. 2 - Wajibu wa wawekezaji na wazalishaji kulipa umuhimu mkubwa suala la uzalishaji bora wa ndani. 3 - Wajibu wa wawekezaji kuelekeza nguvu zao katika nyuga za uzalishaji badala ya kuganda kwenye sekta zisizo za uzalishaji na 4 - Kuhakikisha kuwa wananchi wanapenda na wanashikamana kitaifa na matumizi ya bidhaa zinazozalishwa nchini.
Katika kuitolea ufafanuza nukta ya nne amesema: Sitaki kusema kuwa kununua bidhaa za nje ni haramu bali ninalotaka kusema kwa kusisitiza ni kuwa, kujenga tabia ya kutumia bidhaa za ndani ni jambo muhimu na la dharura mno katika kuimarisha uchumi na maendeleo ya nchi yetu na ni jambo ambalo lina taathira katika masuala yote yakiwemo ya nafasi za kazi na kuongezeka ubora wa uzalishaji wa ndani na tab'an viongozi nchini wao wana jukumu kubwa zaidi katika suala hilo.
Baada ya kutoa muhtasari wa maelezo yake kuhusu masuala hayo na kusisitiza juu ya wajibu wa kuweko ushirikiano mkubwa baina ya wananchi na viongozi katika jitihada za kuimarisha misingi ya uchumi nchini Iran, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameanza kuzungumzia suala la utamaduni akisema: Suala hilo ni muhimu zaidi kuliko hata suala la uchumi.
Ayatullah Udhma Khamenei ametoa ufafanuzi kuhusu sababu zinazolifanya suala la utamaduni kuwa muhimu zaidi kuliko hata suala la uchumi akisema: Utamaduni ni mithili ya hewa ambayo tutake tusitake lazima tuivute. Hivyo kama hewa itachanganyika na uchafu basi athari zake mbaya zitayakumba masuala yote ya jamii yetu.
Aidha amezungumzia athari za kipekee za utamaduni katika kubadilisha mitazamo ya wananchi kuhusu masuala kama vile uzalishaji wa ndani, kuheshimu sheria pamoja na masuala ya familia na kuongeza kuwa: Mienendo na miamala yote ya kila siku, ada na desturi za watu na "mtazamo wa kiuchumi kijamii na kisiasa" wa wananchi unapata ilhamu kutoka katika utamaduni wa watu hao, hivyo itikadi za kiutamaduni ni muhimu na zina taathira kubwa katika masuala na nyuga zote nyingine.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, hatua ya maadui ya kulenga zaidi mashambulizi yao katika masuala ya utamaduni inatokana na umuhimu mkubwa wa suala hilo na kusisitiza kuwa: Maafisa wa masuala ya kiutamaduni wanapaswa kuwa macho na kuwa na hisia kali mbele ya uwezekano wa kujipenyeza mambo ya hatari kabisa katika utamaduni wa taifa na wanapaswa kutekeleza vizuri majukumu yao katika kupambana na mashambulizi ya kiutamaduni ya maadui.
Ayatullah Udhma Khamenei ameashiria pia taathira mbaya za kudharau mambo, kutowajibika na kutokuwa na mipangilio mizuri ya ndani kuhusu utamaduni wa umma na kusisisiza kwamba: Si kwamba matatizo yote ya kiutamaduni yanatokana na mashambulizi ya maadui lakini vile vile hatuwezi kukanusha wala kufumbia macho mashambulizi haribifu ya maadui katika utamaduni wa taifa letu kwenye kipindi chote hiki cha miaka 35 iliyopita.
Vile vile amesema kuwa, suala la "uhuru" ni nara na kaiulimbiu kuu na ya kimsingi ya Mapinduzi ya Kiislamu na ni katika misingi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kuongeza kuwa: Hisia kali za viongozi nchini kuhusiana na mashambulizi na upotoshaji wa kiutamaduni hazina ukinzani wowote ule na suala la uhuru kwani uhuru ambao ni katika neema kubwa za Mwenyezi Mungu kwa waja Wake ni kitu kimoja, na tabia ya kutojali mambo, kupuuza mambo na kuacha mambo yafanyike ovyo ovyo ni kitu kingine mbali.
Aidha Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, uhuru usio na mipaka hauna maana na hapo hapo ameashiria namna madola ya Magharibi yanavyong'ang'ania mistari yao myekundu licha ya kudai kuwa ni viranja wa kupigania uhuru wa mambo mbali mbali na kuongeza kuwa: Huko barani Ulaya mtu hadhubutu hata kutilia shaka tu suala la holocaust ambalo hata halijulikani ukweli wake, lakini hao hao Wamagharibi wanatutaka sisi tusijali na tudharau mistari myekundu ya dini yetu tukufu ya Uislamu na mistari myekundu ya Mapinduzi yetu ya Kiislamu.
Ayatullah Udhma Khamenei ameashiria pia masuala mengine mbalimbali akisema: Kama atatokezea mtu na kushambulia roho ya uhuru wa taifa na kuchochea fikra za watu kuwa vibaraka ajue kuwa amesaliti misingi ya kimaadili na kidini ya jamii yetu. Kama mtu huyo atashambulia nara na kaulimbiu kuu za Mapinduzi ya Kiislamu na kudharau lugha ya Kifarsi na mila na desturi za taifa na akawa anaeneza vitendo viovu na vichafu na ikawa anailenga moja kwa moja roho ya heshimu ya taifa kijana la Iran, je, tutapaswa kumwangalia tu na kutochukua hatua yoyote dhidi ya mtu kama huyo?
Aidha ameashiria namna Wamagharibi wanavyoshindwa kuvumilia masuala kama ya Hijabu na kujisitiri vizuri wanawake wa Kiislamu katika nchi zao na namna Waislamu hao wanavyoshambuliwa na kunyanyaswa kiuadui kutokana na taasubu zilizotanda kwenye nyoyo za baadhi ya watu wa nchi hizo za Magharibi na kuongeza kuwa: Hii ni baadhi ya mifano tu inayoshudhudiwa huko Magharibi; mambo ambayo kuna baadhi ya watu wanafanya njama za kulifanya taifa lililostaarabika na lenye historia kongwe la Iran lifuate mambo kama hayo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiisamu amewakhutubu maafisa husika katika asasi na taasisi za utamaduni na tablighi nchini ambao kwa njia ya moja na isiyo ya moja kwa moja wanahusika pia na serikali akisisitiza kuwa, makeke na makelele yanayopigwa na vyombo vya habari vya kibeberu au vyombo vinavyotumia lugha za mabeberu yasikutisheni, bali pangilieni vizuri mambo yenu ili muweze kukabiliana vilivyo na propaganda za vyombo hivyo.
Baada ya kubainisha majukumu mazito waliyo nayo maafisa wa taasisi za kiutamaduni nchini Iran, Ayatullah Udhma Khamenei amesema: Nukta iliyo muhimu zaidi katika maneno yangu hapa kuhusiana na kadhia ya utamaduni ni kuwa maneno yangu hayo yanawalenga vijana wenye imani thabiti za kidini na kimapinduzi ambao wamejitolea kufanya kazi za ubunifu za kiutamaduni katika kona mbali mbali nchini ambao kwa hakika wamefanya kazi nzuri.
Vile vile amewasisitizia vijana nchini Iran akiwaambia: Wapendwa wangu endeleeni na kazi zenu za kiutamaduni kwa uzito wa hali ya juu kadiri mnavyoweza kwani kazi zenu za kiutamaduni tangu awali ya Mapinduzi zimekuwa na nafasi muhimu sana katika kusimama kidete na kupiga hatua za kimaendeleo nchi yetu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amewakhutubu pia watu muhimu na wenye ushawishi katika masuala ya kiutamaduni kama vile maulamaa, wahadhiri wa vyuo vikuu, wasomi wenye fikra za kimapinduzi na wasanii wenye maadili mazuri na kuwapa nasaha akiwaambia: Endeleeni kuwa na mtazamo na msimamo huo huo wa kukosoa kila mnapoona panakwenda kombo katika masuala ya kiutamaduni na tumieni mantiki na hoja zenye nguvu na kuwabainishaji mambo ya lazima kwa ufasaha na kwa uwazi maafisa wanaohusika na masuala ya utamaduni nchini.
Wakati huo huo lakini amesema kwa kusisitiza kuwa: Inabidi watu wajiepushe kutoa tuhuma zisizo na msingi katika suala hilo na wajiepushe kikamilifu na kuzusha fujo na makelele pamoja na kuwatoa watu katika dini na kwamba majimui ya watu wenye fikra za kimapinduzi nchini iwe ni vijana wenye imani thabiti ya dini au watu wakubwa na watu wenye vipawa na ushawishi, wote wanapaswa kutumia mantiki na hoja zenye nguvu katika kukosoa mambo na kutubainishia sisi viongozi nukta dhaifu na sehemu palipokwenda kombo na kwamba jambo hilo ndilo hilo tunalosema kwamba ni kuwa na hima na azma ya kitaifa na uongozi wa kijihadi katika uwanja wa utamaduni.
Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria uamuzi wa kupewa jina la "Hamasa ya Kisiasa na Hamasa ya Kiuchumi" mwaka uliopita wa 1392 (Hijria Shamsia) na kuongeza kuwa: Katika kadhia ya hamasa ya kisiasa, wananchi wameonesha hamasa hiyo kwa kiwango ambacho kilitarajiwa na kwa kupitia harakati zao mbili kubwa, yaani mosi, uchaguzi wa 11 wa rais wa Jamhuri ya Kiislamu, na pili, maandamano adhimu ya nchi nzima ya Bahman 22 (zilipofikia kileleni sherehe za mwaka wa 35 wa ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran) wananchi wa Iran walifanikiwa vizuri kuonesha hamasa iliyokusudiwa ya kisiasa.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduizi ya Kiislamu ameyataja matukio mawili makuu yaani uchaguzi wa 11 wa rais wa Jamhuri ya Kiislamu na maandamano ya Bahman 22 kuwa ni sawa na vyombo vya habari vya mawasiliano vinavyowafikia watu wengi vilivyofikisha na kutangaza vizuri sana uhakika wa Iran na wa taifa la Iran kwa walimwengu na kukabiliana ipasavyo na propaganda za vyombo vya habari vya maadui wa taifa la Iran.
Amesisitiza kwamba: Nukta iliyo muhumi kuhusu chaguzi katika mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni kwamba tangu awali kabisa ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini hadi leo hii, rekodi na kiwango kikubwa cha ushiriki wa wananchi katika chaguzi hizo kimekuwa kikijikariri mara kwa mara, hakuna wakati kimepungua na kwamba katika uchaguzi wa 11 wa rais pia, asilimia 72 ya wananchi waliotimiza masharti ya kupiga kura walishiriki kwenye uchaguzi huo na hii ni rekodi ya aina yake kabisa.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Maana ya kushirikia mtawalia wananchi katika nyuga mbali mbali ni kuwa, misingi ya demokrasia ya kidini imekita mizizi katika mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu na kwamba kuna udharura na kuna haja ya kujua thamani ya neema hiyo. Hata hivyo amesema ni jambo la kusikitisha kuona kuwa katika uchaguzi wa rais wa mwaka 2009 kuna baadhi ya watu hawakuthamini neema hiyo kubwa.
Baada ya hapo amezungumzia namna wananchi walivyoshiriki kwa wingi zaidi na kwa hamasa kubwa zaidi katika maandamano ya Bahman 22 mwaka 1392 (Februari 11, 2014) na kusema kuwa, sababu zilizopelekea kushuhudiwa tukio hilo adhimu ni siasa za kambi ya kibeberu za kukabiliana na wananchi wa Iran na lugha za jeuri na zisizo za heshima za Wamarekani kuhusiana na taifa la Iran.
Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa: Hata wakati ambapo mazungumzo ya nyuklia yalikuwa yanaendelea, wanasiasa wa Marekani walitumia maneno yasiyo na heshima ili kujaribu kuonesha kuwa wananchi wa Iran wameachana na maneno na misingi yao mikuu lakini taifa la Iran lina ghera na hisia kali kuhusu mambo yake na sifa hiyo ndiyo iliyotoa msukumo mkubwa uliopelekea wananchi wajitokeze kwa wingi na kwa shauku kubwa zaidi katika maandamano hayo na kuthibitisha kwamba wamesimama kidete kuilinda Jamhuri ya Kiislamu na bendera ya Uislamu iliyonyanyuliwa juu nchini Iran pamoja na mfumo wa Kiislamu unaotawala nchini Iran.
Mwishoni mwa hotuba yake, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria namna Marekani ilivyoshindwa katika maeneo tofauti duniani ikiwa ni pamoja na Palestina, Syria, Iraq, Afghanistan na Pakistana na kuongeza kuwa: Matukio yanayoendelea kutokea hivi sasa duniani hayaendani na matakwa ya Marekani.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Katika nchi azizi ya Iran pia, Wamarekani wameshindwa kufikia maleno yako licha ya kufanya njama za kila namna katika kipindi chote hiki cha miaka 35 ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu kutokana na kusimama kidete taifa la Iran na kuwa imara wakati wote wananchi wa Iran katika medani mbali mbali.
Vile vile amekumbusha kuwa, watu wenye ushawishi katika serikali ya Marekani wanasema wazi wazi na bila ya kificho kwamba wameongeza na kushadidisha mashinikizo dhidi ya Iran ili kuwafanya wananchi wasimame kuupinga mfumo wa Kiislamu unaotawala nchini Iran na wawamiminike katika barabara za Iran ili kuyavunja Mapinduzi ya Kiislamu, lakini kujitokeza wingi na kwa hamasa kubwa na kwa welewa wa hali ya juu wananchi wa Iran katika maandamano ya kuunga mkono Mapinduzi ya Kiislamu na mfumo wao wa utawala wa Kiislamu, kumefelisha njama hizo za Wamarekani.
Mwishoni kabisa mwa hotuba yake, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema: Kwa taufiki ya Mwenyezi Mungu, mustakbali mwema ni wa vijana wa ardhi hii azizi na kwamba njama za maadui zitaendelea kushindwa moja baada ya nyingine na siku baadhi ya siku.
Kabla ya hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Waiz Tabasi, Mwakilishi wa Fakihi Mtawala katika mkoa wa Khorasan Razavi ambaye pia ni mdhamini wa Haram Tukufu ya Imam Ridha AS ametoa hotuba fupi na huku akiashiria namna taifa la Iran lilivyoshikamana vilivyo na njia yake iliyojaa fakhari ya uhuru na heshima ya taifa amesema: Kaulimbiuo ya "Uchumi na Utamaduni wenye Azma ya Kitaifa na Uongozi wa Kijihadi" itafanikishwa kwa ushirikiano na hima ya pamoja ya wananchi na viongozi wao nchini Iran.
 
< Nyuma   Mbele >

^